Make your own free website on Tripod.com

Riwaya

Jeraha Lisilopona (5)

NILIPOFIKA nyumbani, nilijifungia chumbani na kuanza kulia. Muda si mrefu, nilisikia kana kwamba kulikuwa na mtu anabisha hodi. Kabla ya kutoka, nilijifuta machozi. Nilipofungua, nilimkuta jirani. Endelea...

Nilipofika nyumbani nilijifungia chumbani na kuanza kulia.

Baadaye nilisikia mtu anabisha hodi nilijifuta machozi na kutoka nje. alikuwa ni yule jirani niliyemwachia mtoto. Kwa mshangao, akaniuliza kulikoni ? Nikamwambia aniache kwanza nitamweleza baadaye. Nikampokea mtoto ambaye alikuwa amesinzia na kwenda kumlaza kitandani.

Baada ya hapo, nilianza kutafakari kuanzia tulipokutana na Emma kwa mara ya kwanza hadi nikafikia kujutia uamuzi wangu wa kutoroka nyumbani na kumfuata.

Nilijuta kwa kitendo changu cha kukaidi ushauri na nia yao njema ya wazazi waliyokuwa wameiweka kwangu pasipo mimi kujua kwa wakati huo.

"Au ndiyo laana yenyewe?" niliwaza. Baadaye nilichukuliwa na usingizi, nikalala.

Baada ya fumanizi lile lisilo rasmi ilipita wiki nzima mume wangu hajarudi nyumbani.

Nikajikuta napatwa na wasiwasi sana. Ikanibidi niende kwa ndugu zake niwaelezee kuhusu visa na ushenzi wa ndugu yao na juu ya kutoweka kwake. Ndugu zake waliniahidi watamtafuta na kumshauri.

Ilikuwa ni Jumapili jioni nikiwa nimejikalia sebuleni kwenye kochi huku nimesongwa na lindi la mawazo. Jioni hiyo nikasikia mlango ukigongwa. Wakati huo mwanangu aliyekuwa amelala, alianza kutamka maneno.

Nilinyanyuka nikaenda kufunga mlango. Macho yangu yakamshuhudia Emma akiwa mlangoni. Sote tulibaki kimya. Hakuna aliyemwamkia wala kumsemesha mwenzake.

Alipitiliza moja kwa moja hadi chumbani. Alipotoka alikuwa ameshikilia briefcase kubwa yenye rangi nyeusi. Mara nyingi alikuwa akiitumia briefcase hiyo anapokuwa na safari muhimu.

Aliponifikia pale sebuleni nilipokaa, alitamka, "Sikiliza Imelda. Nimegundua kuwa nilifanya kosa kubwa kukuoa. Sasa najua kuwa sikupendi nampenda Suzane si wewe, na hakuna anayeweza kututenganisha na kwa wewe, labda umfuate Andrew pengine bado anakupenda na huyo mtoto nakuachia kama zawadi bila shaka zawadi hiyo utaipenda?" Emma aliyasema maneno hayo huku akiniangalia kwa dharau na kisirani na kisha, akaondoka.

Maneno hayo yalinipenya moyoni kama moto wa radi. Nilihisi kama ardhi imeondoka chini ya miguu yangu na kuniacha naelea hewani, utupu na mauzauza vilinizunguka. Nilipotafuta mahali pa kujificha, sikupaona. Kizunguzungu kilinipata, nikashikwa na woga na mfadhaiko. Nikaona thamani ya maisha na uhai vimetoweka. Naam, nikatamani kufa.

Pembeni yangu, kulikuwa na TV. Nikanyoosha mkono wangu na kuchomoa ule waya wake wa umeme. Kwa taratibu huku nusu ninajitambua na nusu sijitambui,na kama kwamba ninaota, nikaanza kutengeneza kitanzi.

Nilipomaliza kukitengeneza, nikatumia dakika kadhaa kuikiangalia bila woga. Nikajikuta natabasamu. Nikakivalisha kitanzi kile shingoni pangu. Nikazidi kutabasamu. Sasa nilihisi maisha yangu yakielekea ulipo ukomo wake.

Usaliti wa Emma kwa penzi langu kwake, ulikuwa umevunjavunja imani na matumaini yangu yote na kuniachia jereha baya lisiloweza kupona. Kwani nani awezae kuutibu moyo uliopondwa na mtu yule uliyempenda, ukamwamini, ukamkabidhi uhai na matumaini yako yote kwake; na kisha akusaliti? Ni dhahiri uchungu huo unakuwa haukadiriki, maumivu yatabaki kumbukumbu isiyotoweka damuni. Ni kidonda kinachovuja daima.

Ningewezaje kuhimili hayo!

Nilichukua stuli nikaipeleka chumbani. Taratibu nikapanda juu ya ile stuli na kuanza kufunga darini kile kitanzi nilichokuwa nimejivalisha shingoni.

Nikamaliza kufunga kile kitanzi sawasawa na sasa najiandaa kusukumia ile stuli pembeni ili nibaki naning’inizwa na kile kitanzi bila kuegemezwa na chochote.Sitaki tena kubaki naelea hapa duniani kama mpumbavu. Kwani waliokufa wao ni wajinga?

Lakini kabla sijatekeleza kitendo hicho, mara nikasikia sauti ya mwanangu ikisema kwa sauti na lafudhi ya kitoto, "Mama! Mama afanya nini apo?" Moyo ulinilipuka "paa". Pumzi zikanipaa. Nikafumba macho na kutulia tuli. Kisha, taratibu nikaipeleka mikono yangu nikakishika kile kitanzi na kukivua shingoni kwangu. Nikageuka nikaanglia pale kitandani nikamkuta mwanangu ameamka amekaa kitandani nikaangalia kwa mshangao.

Mara nikajawa huruma na aibu nikatambua ni kwa kiasi gani nilikuwa nimekuwa mbinafsi kwa kutaka kujiua; Nikajiona nimemkosea Mungu kwa kosa la mauaji. hata serikali ikijua huyo...! Muda wote ule halikuwa limenijia wazo juu ya mwanangu. Nilikuwa nimejifikiria mimi tu; kama ningejua nani angemlea mwanangu; na kama mwanangu angekuwa mkubwa na kubaini ukweli na kwamba baba yake alimtelekeza akiwa bado mdogo na mama akajiua na kumwacha bila msaada wowote, ni kiasi gani ukweli huo ungemjeruhi na kumuumiza moyo mwanangu.

"Ee Mungu nisaidie;Ee Mungu wangu nisamehe!" Nilijuta kwa sala hiyo fupi.

Kisha baada ya hapo, nguvu kidogo zikanirejea. Nikashuka pale juu ya stuli na kumwendea mwanangu nikamkumbatia na kuanza kulia; mpaka leo ninalia na huenda nitalia maisha yangu yote, kwani jeraha aliloniachia Emma; ni JERAHA LISILOPONA

........Mwisho..........

Wimbo niupendao

Tuyapige Vita Matendo Maovu

Na Getrude Madembwe

WIMBO wa Tuyapige Vita Matendo Maovu, ni kati ya nyimbo zilizoimbwa wakati wa Maadhimisho ya Kongamano la Walei ambao lilifanyika kitaifa Msimbazi Centre katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Ni miongoni mwa nyimbo zilizowahamisha waamini juu ya kongamano hilo na pia kutoa elimu kwa watu wa rika zote zote.

Akiongea na gazeti hili katikati ya juma Mwenyekiti wa Kwaya ya Watakatifu Wote iliyopo katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Bw. Dismas Sambala alisema kuwa wimbo huo ulitungwa na Damian Chanya, una maudhui ya kuwaasa vijana waache matendo maovu .

"Vijana sasa hivi wameharibikiwa. Wengine kwa uvutaji wa bangi, dawa za kulevya pamoja na mambo mengine maovu ambayo kamwe, hayampendezi Mungu.

Aidha alisema kuwa kanda hiyo, ni toleo la pili kwa kwaya hiyo ambayo ilirekodiwa katika studio za Baraza hilo la Maaskofu lililoko Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Mbali na kuwausia vijana waachane na vitendo viovu vikiwamo vya uzinzi na uasherati vinavyoweza kuwaangamiza hasa kutokana na gonjwa hatari la UKIMWI, pia ina lengo la kuwatahadharisha watu wajiepushe na vitendo vya rushwa ambayo imekithiri karibu ulimwengu mzima.

Viongozi wa Kwaya hii ni Bw. Dismas Sambala ambaye ni Mwenyekiti, na Makamu wake ni Sista Flora Chuma. Katibu wa Kwaya ni Bradha James Msungu wakati Msaidizi wake ni Mathias.

Mweka Hazina ni Teddy Mlavila wakati Kiongozi wa Nyimbo ni Bw. Steven Msowoya.

Nyimbo zingine zilizoko katika kanda hiyo ni Enyi Watu uliotungwa na E. Zunda, Tuyapige Vita, Bwana Amejaa Huruma, Inguluvi(kwa Kihehe una Mungu), Njooni Kwangu ambazo zilitungwa na D. Chonya.

Nyingine ni Kanisa la Kitume uliotungwa na J. Mgandu, Mbingu na Nchi,uliotungwa na A.Msigwa, Muhume Mlave(Mtoke muwahi), Walei Simama ambao ndio wimbo uliobeba jina la kanda yaani Nanyi Mtakuwa Mashahidi Wangu na Tunaiombea Amani hizi ni nyimbo zilizotungwa na Bategeleza, Umtumaini Bwana umetungwa na R. Kawite.

Wimbo wenyewe ni:-

Tuyapige vita matendo mabaya hasa kwa kizazi cha sasa, Walei twendeni kwa pamoja pande zote za Tanzania tuungane naye Baba Mtakatifu na (....) wenzetu wa Roma na Msimbazi.

1. Ni jambo la kusikitisha UKIMWI unatumaliza Walei tutafakari kwa uchungu.

2. Na Rushwa imekuwa kero inawatawala walei hata michango mingine kupotea.

3. Imani imeshapungua wengine wanahama dini Kanisa linasikitika kwa uchungu.