Make your own free website on Tripod.com

Jeraha Lisilopona (3)

Siku hiyo niliwadanganya kuwa naenda kwa rafiki yangu Janeth ambaye hata wao walikuwa wanamfahamu. Hawakunizuia. Nikajiandaa harakaharaka na kuondoka mpaka Kirumba kwa kaka Emma. Sasa Endelea

Nilimkuta Emma na kaka yake wamejipumzisha sebuleni wakiangalia mpira kati ya Manchester United na Arsenal kwenye Luninga. Waliponiona walionesha nyuso za furaha na faraja fulani.

"Karibu Imelda...karibu sana," Emma alinichangamkia.

"Ahsante habari za hapa nyumbani?"

Nzuri sana! Huko ulikotoka hawajambo?"

"Wazima! Shemeji shikamoo," nilimwamkia kakaye Emma aliyekuwa kimya akituangalia.

"Marahaba Imelda, hujambo?"

"Sijambo! Sijui wewe?"

"Sisi wazima tu hofu yetu ilikuwa juu yako wewe, uliyekuwa kimya mpaka tukaogopa!"

"Aa wapi; kama mliogopa, mbona hamjaja kunitazama?" nikauliza kwa hali ya utaniutani.

"Huku kwenu tutapitia wapi ili tukutane wakati hakuingiliki?" kaka yake aliuliza kwa mzaha.

"Jamani mimi sina muda mwingi nimeaga naenda kwa rafiki yangu hivyo, nategemewa niwahi kurudi; nimepita kidogo tu, kuwaona".

"Haya! Ngoja niwapishe muongee," alisema kakaye Emma huku akinyanyuka.

"Mbona unaonekana kama una wasiwasi kuna nini Imelda?" aliniuliza Emma huku akinisogelea.

"Ni kwamba kule nyumbani wazee wamekuwa ni "ngangari" kwelikweli hawataki niolewe hadi nimalize chuo kama unataka kunisomesha, wanadai unisomeshee palepale nyumbani halafu ndio ndoa ifuate baadaye na si vinginevyo!. Nimekuja nikueleze ili nipate msimamo wako".

"Mimi Imelda ukweli ni kwamba ninakupenda sana na sitakubali nikupoteze mpenzi. Tangu siku ile, nilipofika kwenu sina raha kabisa kwani naona wazazi wako ni kama wanaweka vizingiti ili nisikuoe. Ila nimejadiliana na "bradha", akanishauri tutumie "short cut" la sivyo, hapa hakieleweki.

Hivyo basi, nilikuwa nakusubiri nikueleze. Kwa kweli sitaruhusu chochote kitutenganishe mimi na wewe isipokuwa, Mungu peke yake ndio hapo kipingamizi", Emma alinieleza huku akinitazama kwa makini.

"Na hiyo short cut ndiyo ipi, Emma?" nilimuuliza. "Nilikuwa nashauri tutoroke Imelda tuondoke wote, hakuna haja ya kuendelea kusubiri, kama ni kusoma, utasoma tu Imelda usiwe na wasiwasi."

Nilimuamini Emma. Sina pingamizi lolote Emma nakusikiliza wewe tu; ila tu ninachoshauri ni kwamba, uniachie hela ya nauli halafu wewe utangulie mimi nitakuja peke yangu; ili ‘deal’ mpango yetu isije ikashtukiwa".

"Sawa Imelda nimekuelewa naomba kesho tukutane Tilapia Hotel tuzungumze zaidi na kupanga mipango yetu vizuri.

Baada ya mazungumzo yetu tuliagana na kuahidiana ili kesho yake, tukutane.

Siku iliyofuata tulikutana Tilapia Hotel kujadili tena mipango yetu na kupanga kila kitu.

Kesho yake, Emma akaondoka kuelekea Dar. akaniacha mimi najiandaa kutoroka ili tukaishi sote kama mke na mume.

Baada ya Emma kuondoka wazazi wangu walianza kusema, "Unaona sasa, yule kijana alikuwa tapeli tu, alitaka kutuharibia tu; binti yetu. Mbona hakurudi tena!"

Mimi nilibakia kimya bila kuchangia lolote kwani nilijua kilichokuwa kinaendelea.

Usiku wa kuamkia siku yangu ya kuondoka, niliandika barua ndefu na kuiweka sebuleni ili wakiamka tu, waione. Siku hiyo niliamka asubuhi, nikavaa nguo harakaharaka tayari kwa safari. Niliwaacha wadogo zangu wawili wamelala wakiwa hawana habari na hila yangu hiyo.

xxxxxxxxxxxxx

Miezi miwili ilikuwa imepita tangu tuwe pamoja na Emma. Maisha yetu yalikuwa mazuri sana na yenye kujaa furaha. Kila jioni, tulikuwa tunatoka pamoja na mume wangu kwa ajili ya matembezi na kwenda kwenye "kanywaji" kupata moja baridi, na moja moto.

Kila nilichokihitaji nilikipata; niseme nini wakati huo halafu kikosekane; eti nisipewe na mume wangu mpenzi! Kila alipokuwa kazini, Emma hakukosa kupiga simu nyumbani ili kunijulia hali.

Tayari nilikuwa na ujauzito wa miezi mitatu. Mume wangu alifurahi sana baada ya kujua kuwa niko katika hali hiyo.

Tuliendelea kulea mimba yetu bila wasiwasi. Miezi sita tangu nipate ujauzito, nikapata taarifa kuwa baba mdogo amefariki. Mume wangu aliniomba niende peke yangu kwani yeye, hakupewa ruhusa kazini.

Tulikubaliana, akanikatia tiketi haraka haraka nikaondoka kuelekea Mwanza kwenye msiba.

Nilimaliza wiki moja tu huko Mwanza kisha nikarudi Dar. Siku ya kurudi, tuliahidiana na mume wangu Emma aje kunipokea kwenye kituo cha mabasi, Ubungo. Lakini nilipofika, Emma hakuwepo kituoni.

Hata hivyo, sikuwa na mawazo mabaya bali nilijua pengine ni kazi tu, zilizokuwa zimemzidia. Nilikodi taksi kunipeleka nyumbani. Kwa kuwa nilikuwa na funguo wangu, sikuhitaji kumsubiria Emma.

Niliingia ndani na kuendelea na taratibu za nyumabni kama kawaida.

Nilipumzika kidogo halafu nikaingia kuoga. Kisha nikaamua kujipumzisha kitandani kwani nilijisikia kuchoka sana.

Nilifunga mlango na kujilaza pale kitandani na baada kitambo kidogo, usingizi ukanizoa.

Nilishtuka toka usingizini kama saa kumi na mbili hivi. Jioni hiyo ilimaanisha kuwa niliuchapa usingizi kwa takribani saa nne.

Nilinyanyuka pale kitandani na kutoka nje. Mume wangu alikuwa bado hajarudi.

Ilipotimia kama saa tano hivi usiku, Emma akawasili nyumbani huku akiwa amelewa chakari. kiasi alichokuwa amelewa siku hiyo, hakika sikuwahi kumuona hata siku moja.

Nilipigwa na butwaa kwani kabla sijaondoka kwenda Mwanza, haikuwa kawaida kwa mume wangu huyo kuchelewa kurudi nyumbani na hata akaraudi usiku akiwa amelewa namna hiyo. Hayo, yalikuwa mageni.

Kwa kweli nilishindwa na kukosa hata neno moja la kusema. Nikabaki nikimwangalia huku nikijiuliza kuwa, kama wiki moja niliyosafiri, imembadili namna hiyo mume wangu, je, ningekaa mwaka!

Huku akipepesuka kwa ulevi aliniamkia, "Vipi da...da...darling... ume... umer... umerudi saa ngapi?" Mimi sikujibu wala kuongea lolote".

Alijitupa pale kitandani kama gunia la mchanga na kuanza kukoroma. Siyo siri, nilijawa na hasira na kutokana na vitendo vyake, nikatoka nje.

Nilikaa nje kama nusu saa hivi halafu nikarudi ndani. Nikamkuta ameshapitiwa na usingizi. Nilijisikia vibaya kwani nilikuwa na hamu ya kuongea na kufurahi pamoja na mume wangu baada ya kutengana kwa juma zima lakini, sasa haitakuwa hivyo.

Kwa kweli niliwaza sana pasipo kupata suluhisho la mashaka yangu hatimaye, nilichoka nikajilalia.

Nilijua fika hata kama ningemwamsha wakati ule ule, kwa jinsi alivyokuwa amelewa, tusingeweza kuelewana hata kidogo.

Aliamka asubuhi na mapema. Pombe tayari zilikuwa zimetoka. Akaniomba nimsamehe kwa yote yaliyokuwa yametokea jana yake nami nikamsamehe; yakaisha kabisa bila kinyongo chochote kwa mume wangu.

Siku zilizidi kupita na mimba ikaendelea kukua lakini, tabia ya mume wangu ilizidi kubadilika.

Alikuwa mlevi zaidi akawa anapenda kususa na kuwa na kinyongo kila tunapokosana.

Kunipiga sasa ikawa ni kawaida yake. nilijitahidi kutafuta chanzo cha tabia hii ngeni ya mume wangu.

Hata hivyo, zoezi la kubaini kilichombadili namna hiyo lilikuwa gumu kwani sikufanikiwa kubaini chanzo cha tatizo.

Ndipo siku moja nikiwa naongea na majirani zangu kuhusu tabia na karaha za waume zetu, mara mmojawapo akanizibua masikio, "Shoga na wewe mwenzetu, usipoangalia, ndoa yako itabomoka sasa hivi".

Kauli ile ilinishitua sana nikamuuliza, "Hee kwanini useme hivyo Grace?"

"Aaa! Basi. Mi’ sitaki kutenganisha ndoa za watu, ila mdogo wangu mwenzako nakupenda na tena nakuhurumia. Kwa kweli sipendi uharibikiwe mdogo wangu," alisema Grace.

Ghafla nilijawa na wasiwasi kutokana na maneno yale ya Grace. Ni kuharibikiwa gani alikokuwa amekulenga? Nini alichokuwa anakijua kuhusu mume wangu, nilitamani sana Grace awe wazi zaidi.

"Dada Grace, mwenzio sijakuelewa una maana gani," nikazidi kusisitiza.

"Kama unataka kujua, tafuta muda mzuri uje nikueleze A mpaka Z. Kuna 'mdudu' ameingilia ndoa yako".

"Mdudu!" nilijiuliza kwa mshangao.

"Aa! Wewe nawe! Unakuwa kama mtoto!" Grace akanikatisha.

Sikutaka kuendelea kumsumbua Grace kwa maswali zaidi hasa nilipozingatia kuwa, alikuwa ameahidi kuniambia siku nyingine kwa muda muafaka zaidi.

basi nililazimika kuvuta subira, hata hivyo siku hiyo sikubaki na raha mawazo mengi mabaya yalitalii ubongoni mwangu ‘Grace alikuwa na maana gani’ swali liliendelea kunijia tena na tena fikrani..

Muda wa kujifungua ulikuwa umekaribia. mimba ilikuwa imefikisha miezi minane. siku hiyo nilikuwa nimechoka vilivyo.

Saa zilikuwa zimeenda na mme wangu alikuwa hajarudi; kuchelewa kwa mume wangu ni wazi sasa ilikuwa imekuwa ni mazoea, nilikereka sana moyoni kwa tabia yake hiyo au siku hizi mume wangu ana mwanamke mwingine huku nje" niliwaza jinsi nilivyozidi kuwazia jambo hilo ndivyo nilivyozidi kulisadiki; hata nikafikiria kuwa pengine hao ndio yule mdudu aliyekuwa ameongelea Grace.

wivu na hasira vikanikalia na kujenga chuki dhidi ya mume wangu;.

Ili kupunguza hasira na kupitisha muda nikaamua nitafute angalau kazi kidogo ya kufanya. Nikaanza kupiga nguo pasi baadaye nikazipanga vizuri kabatini kisha nikaanza kupanga vitabu vya mme wangu kwenye ‘shelf’ kabla sijamaliza kazi hiyo nikaona bahasha iko chini ya kitabu kimoja nikanyanyua kile kitabu nikaichukua ile bahasha kwa jina na anwani ya mume wangu Emma katika hati ya kike.

Ile hati ya kike ilichochea shauku ya kutaka kujua kilicho ndani ya ile bahasha; na kwa kuwa ilikuwa imeshafunguliwa niliingiza mkono na kuchomoa karatasi iliyokuwemo ndani ilikuwa ni bora.

Nilipoisoma ile barua sikuyaamini macho yangu niliyafikicha kana kwamba hayaoni vizuri, lakini wapi! hayo hayo niliyokuwa nimeyaona na kuyasoma ndiyo hayo hayo niliyoyaona na kuyasoma tena ndani ya barua ile;

Barua yenyewe ilikuwa inatoka kwa Suzana, mpenzi wa Zamani wa Emma, na ilionyesha kuwa haikuwa ya muda mrefu uliopita na kilichonistua zaidi ni pale nilipogundua kuwa kumbe Emma alikuwa anamsomesha kadri ya maelezo ya ile barua, kwani Suzana akiomba Emma amtumie hela ya ada huku akilalamika kuwa pesa aliyomtumia mara ya kwanza ilikuwa haikutosha!.

Nilipogundua moja kwa moja jibu nilipata hoja mbili. nilibaini kwamba Emma hakuwa na penzi la dhati kwangu nilihisi kusalitiwa na kudhalilishwa.

niliona uchungu kwamba Emma anaweza kunighilibu na kunichezea kiasi kile, kwa nini anitendee hivi lakini?

Alipokuwa ananipa mimba ina maana alikuwa hamuoni huyo Suzana? Ananidanganya kuwa tuzae kwanza mtoto mmoja ndipo nikasome kumbe anawasomesha malaya zake. Haiwezekani..! mawazo ya uchungu na hasira yalinikalia mara machozi yalianza kububujika halafu nikaanza kulia kwa uchungu.

XXXXXXXXXX

Mlango wa chumbani ulifunguliwa na mume wangu akaingia.

‘Vipi Imelda mbona macho mekundu unaumwa?",alisema huku akinishika begani mie sikumjibu kwani nilihisi alikuwa ananiongezea maumivu moyoni. nikaanza kulia kwa sauti na kwikwi huku akibaki ameshangaa na kujawa na wasiwasi.

"Vipi Imelda unataka kuzaa nini?.... sema kama unahisi uchungu nikachukue gari twende hospitali!