Make your own free website on Tripod.com

Kweli kosa ni langu

"NAKIRI kwa kinywa changu; kweli kosa ni langu maana, nimekosa mimi, nimekosa sana," anasikika akijisemea peke yake hali Natasha akizidi kuuloanisha kwa machozi, mto ule aliokuwa ameuegemezea kichwa chake pale kitandani.

Natasha mtoto wa watu, hakuwa anajua ni nani kati ya wote aliowakosea, atakaye kuwa tayari kumsamehe. Aliirudisha nyuma kumbukmbu ya maisha yake kwa takriban miaka mitano iliyopita.

Aliufungua ule mkoba wake mdogo wa rangi ya kijivu na kukitoa kile kitambaa alichokitumia kufuta machozi yaliyokuwa yamejenga mitaro katika mashavu yake.

Mara tena, anasikika akijisemea, "Natasha! Kweli kosa ni langu. Nimekosa mimi, nimekosa sana."

Anaikumbuka siku moja kabla ya kifo cha mpendwa mama yake mzazi. Ni siku hiyo Natasha alipofuatwa shuleni kwake katika sekondari ya Nguru. Siku ambayo sasa wanafunzi wa kidato cha nne, walikuwa wakihesabu saa ndani ya siku tano kama walivyozoea kuziita, "days left" yaani, siku zilizobaki ili waanze mitihani yao ya mwisho.

Licha ya kwamba kutoka nyumbani kwao Natasha maeneo ya kijiji cha Nkongore, hadi ilipo shule hiyo si umbali mkubwa unaohitaji nauli, ni kwa kujua umuhimu na uzito wa mitihani hiyo, ndiyo maana hawakutaka kumjulisha Natasha juu ya ugonjwa ulioanza mapema kumsibu mama yake.

Walifanya hivyo kwa makusudi mazima ya kutomvuruga akili hasa wakati huo muhimu kwa ajili ya maandalizi yake kimasomo.

Hata hivyo, suala lenyewe lilikuwa nyeti kwa mama yake kwani lilitokana na mimba aliyoipata huku mumewe akiwa masomoni katika chuo kimoja cha uandishi wa habari huko jijini Dar-Es-salaam.

Natasha ambaye wazazi wake waliujua na kuuzingatia sana uzazi wa mpango, ambao siku hizi nasikia unaitwa NYOTA YA KIJANI, alikuwa ndiye msichna mkubwa katika familia yao ya watoto watatu; wote wa kike waliopishana kwa miaka sitasita.

Alifika na kumkuta mama yake mzazi akiwa kitandani hoi bin taabani.

Ghafla mgonjwa yule alipata nguvu za ajabu, sijui niziite nguvu za miujiza au vipi hata ninashindwa nisemeje.

Mgonjwa aliamka akamnyooshea mikono Natasha. Nae Natasha alipomsogelea, mgonjwa alimkumbatia kwa nguvu zilizowashangaza waliokuwapo. Kisha, akawapungia mkono watu waliokuwapo ishara ya kuwataka waondoke na kuwapisha wawili kwa mazungumzo ya faragha. Ikawa hivyo.

"Mwanangu mkubwa Natasha! Sikupenda nikutoe masomoni na kukuvurugia ratiba yako lakini, imenibidi kwani niliyonayo ya kukupa, asingepatikana mwingine wa kumsemea zaidi yako," akasema mama yule huku akinyanyua macho yake na kumtazama Natasha aliyekuwa kasimama kando ya kile kitanda huku ametia kiganja cha mkono wake wa kushoto katika shavu naye, akimsikiliza mama yake kwa makini."

"Mwanangu, kweli kosa ni langu nimemkosea Mungu, nimemkosea mume wangu, na pia nimewakosea ninyi wananangu na jamii nzima wanaonifahamu vema.

Hata mimi sikupenda niwaache katika hali hii mkiwa hamjui hata mahali pa kuchota maji ya kunywa; eti mtunzwe na mama wa kambo; lakini, tamaa imenilazimisha kuwafikisha huko nisikokutaka," akasema mama-natasha kwa huzuni.

"maskini sijui mume wangu ataambiwa vipi juu yangu! Tulipendana na kuheshimiana sana na tangu nifunge naye pingu za maisha, tofauti na wanaume wengine niwaonao, sikupata kusikia hata majirani wakinong’ona wala kupiga majungu juu ya mienendo mibaya ya mume wangu kuhujumu ndoa yetu.

Sina shaka kuwa ni kwa kuwa alijua kuwa hali hiyo inayo madhara mengi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana na janga la UKIMWI"

"Sasa, sijui iweje leo mume wangu huyohuyo aliyekuwa mstari wa mbele kunihimiza juu ya uaminifu katika ndoa, ajue kuwa ndimi mimi huyo msaliti wa ndoa yetu. Usaliti wangu sasa umewaponza hata nyie wanangu; viumbe msio na hatia. Hivi ni nani kati yenu atakaye nisamehe mimi ninayejuta namna hii?

Niliye mdhambi kuliko wadhambi wote duniani? Hakika kweli nimekosa mimi, nimekosa sana," anatulia kidogo kumeza mate na kabla hajaendelea zaidi, Natasha akadakiza,

"Mama mbona sikuelewi?" "Nilijua hutanielewa kwa kuwa bado mtoto mdogo; hata akili yako haijajua misemo. Sasa Natasha sogea; utege masikio na kunisikiliza kwa makini ninanchokunong’oneza, unielewe vizuri na wala usimwambie mtu."

Natasha akasogeza sikio lake huku ameinama kumuelekea mama yake. "Usifikiri eti ninavyosema eti nini ukadhani ni kweli; la hasha! Nakuibia siri hii na liwe fundisho kwako. Kamwe usifanye kosa kama nililofanya mimi kwa kuwa sasa unajua madhara yake.

Ogopa kabisa tamaa ya mapenzi. Ukane na kuusuta moyo wako unaokuelekeza huko; moyo wa tamaa; umewaponza na kuwaliza wengi nikiwa miongoni mwao.

Tamaa niliyokuwa nayo hadi kufanya mapenzi na yule rafiki wa baba yenu, ndiyo inayonirudi na kuniumbua namna hii na hata kuwa bei ya mauti yangu,"

Natasha akadakiza bila simile, "Hivi mama unataka kufa!?" "Mhh!!" Mama yule akaguna na kuendelea, "Lilikuwa ni kosa la siku moja lakini sasa majuto na madhara yake, yanakuwa ya milele. Hivi unadhani bila kutoa hiyo mimba, ningemweleza nini baba yako?" Mama akatulia kidogo, akakohoa kusafisha koo na kumeza mate. Kisha akaendelea,

"Au basi kama unavyojua, wanadamu hawalazi jambo, midomo yao ni kama zege, unadhani mpaka sasa hawajampigia simu au kumwandikia barua juu ya kisa hiki? Ndiyo maana nimeona ili kupunguza ngebe, ni heri nitangulie kule ahera au hata kama ni kuzimu, niende tu, litakalo kuwa na liwe."

"Tena msihangaike wala kujaribu kuniokoa kwani licha ya hiyo ‘tiketi’ yangu niliyotumia kusafiria toka duniani hadi ahera, bado mimba hiyo nimeitoa kwa matatizo makubwa.

Nakusihi wewe pia usijefanya vitendo hivi ambavyo ni chukizo kwa wanadamu na kwa Mungu pia," akasema Mama-Natasha huku akinyoosha kidole kumuonesha Natasha chupa ya sumu ya panya aliyokunywa muda mfupi kabla Natasha hajaingia mle ndani.

"Na hii barua, usisahau kumpa baba yako au yeyote atakayepaswa kupewa. Kwa heri Nata...Nata... Natasha, Kwa heri Natasha! Kwa heri mume wangu mpenzi; baba-Natsha, na kwa heri walimwengu. Simlaumu mtu, bali najilaumu mwenyewe. Kwa heri na buriani Natasha."

Mama-Natasha akatetemeka kwa takriban dakika mbili hivi. Kisha akapunga mkono ishara ya mwisho ya kuaga. Akabadili jina na cheo toka Mama-Natasha, hadi Marehemu Mama-Natasha.

Natasha akabaki amemtumbulia macho pasi kujua aseme au afanye nini. Alipigwa butwaa lisilomithilika na ghafla akazinduka toka katika butwaa hilo.

Akaangua kilio huku amejitwisha mikono kichwani akiwa tayari ameitupa chini ile barua aliyokabidhiwa na mama yake kabla ya kifo.

Haupiti muda mrefu, umati wa watu ukawa umejaa pale chumbani. Wakaupa hifadhi inayoustahili mwili wa marehemu huku taratibu za kawaida za msiba na mazishi, zikiendelea.

Ni asubuhi ya siku iliyofuata. Wazee wa kijijini walikwisha fika huku wengine wamshikilia fimbo zao za kizee.

Nao wengine wamekaa kando kidogo mwa yule ng’ombe aliyechinjwa kwa ajili ya msiba wakihakikisha kuwa taratibu za kimila, hazikiukwi.

Kila mtu sasa alikuwa akielezea wema wa marehemu. Hata wale maadui zake ambao hadi jana kabla ya mauti yake walikuwa hawasalimiani, nao sasa wanasikika wakimsifia marehemu eti alikuwa mtu mzuri.

Walikuwapo pia miongoni mwao waliosubiri muda wa kuanza kutoa lawama msibani; Oooo! Mimi sikupewa nyama kubwa, ooo! Mimi sikula nishibe, Hee! Hivi hawajui hapo ni msibani au pamegeuka harusi?

Basi fasheni ikawa hiyo mradi tu, kinachosikika ni sifa za wema wa marehemu. Si hata wewe unajua mtu akifa anavyokuwa mwema midomoni pa watu?

Anakuwa mzuri kuliko hata ng’ombe ambaye kinyesi chake ni kizuri kwa mbolea,, akifa ni mzuri kwa matumizi ya binadamu(nyama), ngozi yake ni nzuri kwa uzalishaji wa bidhaa kama viatu na mikanda, meno na mifupa, ni mizuri hasa kwa uzalishaji wa chaki kwa matumizi ya shule na hata pembe na kwato ni nzuri sana kwa uzalishaji wa gundi. Na mengine nisiyoyajua wala kuyafikiria kama hayo.

Mara mzee mmoja maarufu pale kijijini Nkongore, Mang’era, anagonganisha viganja vya mikono yake akiasharia watu wanyamaze kidogo. Kimya kile kilichovamia ghafla, kinavunjwa na sauti ya mzee huyo aliyeshikilia kipande cha karatasi kilichookotwa jana chumbani mwa marehemu. Anaeleza namna alivyokipata na kuanza kuwasomea waliokuwapo.

"Mpendwa Mume wangu Baba-Natasha, natumaini haujambo japokuwa utausoma ujumbe huu kwa majonzi huku umeshika tama na machozi yakikutoka. Au hata lolote linaloweza kukutokea.

Awali ya yote, nakutakia maisha mema katika dunia hii niliyokuachia bila ridhaa yako wala ridhaa ya Mungu.

Nakuachia ulimwengu huu ulio kigeugeu namna hii. Pili, ni kwa huzuni na soni kuu ninapokujulisha kwa mkono wangu kuwa nimetangulia kutafuta makao kule ahera hata kabla ya kuitwa na Mungu ili aniweke anapotaka yeye.

Hata mimi sifurahii kukujulisha hivyo kwani ni kutokana na shinikizo la tamaa lililonifanya niisaliti ndoa yetu.

Hata hivyo, mengi watakusimulia walimwengu ila, ninakuomba unitunzie vema wanangu maana nawaacha wakiwa bado wadogo wanaohitaji msaada na mapenzi ya wazazi na walezi wao.

Sio siri ninakiri kuwa kosa ni langu maana, nimekosa mimi, nimekosa sana.