Make your own free website on Tripod.com

Sikutarajia Yawe Haya (2)

Katika toleo lililopita, tuliona namna kijana Bahati alivyoiokota ile bahasha iliyoangushwa na Nafsa ikiwa na vitu kadhaa ikiwa ni pamoja na fedha na picha ya binti huyo maridhawa na tena mantashau.

Akaamua kujitafutia mtumba wa kulipumzisha lile shati lake ambalo yeye, analiita "chanika nikushone" au "kauka nikuvae". Lakini je, Bahati atabahatisha nguo hiyo kama alivyokusudia,? Ungana na Mtunzi wetu Mahili Emanuel Boniface ujue yaliyomsibu Bahati.

Ile nimekaribia mitumba tu, macho yangu yanagonga juu ya sura maridhawa ya Nafsa.

Ninaona kiwingu; ninaamua kubadili uelekeo harakaharaka na kuhamia eneo lingine.

Kwa mara nyingine tena, kabla sijainama kuchagua mitumba, nataharuki kumuona Nafsa akiwa kando yangu hali akiendelea kupekua pekua zile tisheti nzuri za mitumba.

Anaipata moja inayomvutia na baada ya kuambiwa bei, anaitupia mahali pake na kujiondokea.

Kwa kuwa hali yangu ni ya chini ukilinganisha na yake, ukizingatia na tabia yake niliyoijua tangu zamani kuwa ni ya maringo na nyodo tele, ninashangaa safari hii Nafsa anauelekeza uso wake kwangu, ukiwa umechanua tabasamu la nguvu nao mdomo wake ukiwa na dalili za kicheko.

"Bahati mambo!" akanisalimia.

"Poa, Sijui wewe?"

"Safi!" anajibu.

Kama ungekuwa ni wewe, ungejishuku vipi? maana kama siku nyingine tulikuwa hatusalimiani, vipi na iweje leo atokee kunichangamkia ghafla vile?

Basi, ikanibidi nijisalimishe kwa Nafsa baada ya kujuliana naye hali.

"Umepoteza nini dada?" nilijikuta nikiuliza kwa hali ya kuwa mweupe; yaani, niliyeishiwa pointi.

"Aka! Mi sijapoteza kitu!" Nafsa akamaka kwa upole huku akipandisha mabega yake juu, ishara ya kukataa, "Kwani vipi Bahati?" anauliza baada ya kuona ninababaika. Nikazidi kushangaa alijuaje jina langu.

Hali hiyo inaniongezea wasiwasi kwa kufikiria kuwa huenda alinifanyia mtego kwa kuniundia njama ili nipekuliwe na kuadhiriwa kwa tuhuma za wizi. Nikaona ni vema nimtaimu kwa kujifichua mwenyewe.

"Huu mzigo si wako?" Nikauliza kwa kujikakamua. "Haa! Jamani umetoa wapi hii picha?" akaniuliza huku akionesha kuwa mwenye furaha.

Nikamweleza jinsi nilivyoipata picha ile na namna nilivyojitahidi, eti kumtafuta nimpe.

Uso wa Nafsa ukaonesha kuridhishwa na huo uaminifu wangu. Akanimwagia sifa na shukrani nyingi.

"Bahati haiji mara mbili," nikajiwazia, sikutaka kupoteza fursa ile. Nilizikusanya na kuvuta pumzi zangu kwa pamoja na kumtamkia haja yangu huku nikijifanya "mtakatifu" kadri inavyowezekana.

Ghafla, nikaanza kujisikia mwepesi na mwenye furaha. Kijasho chembemba kikinitoka.

Kwa mara nyingine tena, nikasahau na kukiuka wosia na nasaha za wazazi wangu walionionya kujiepusha na anasa na uasherati, kwani waliyajua madhara yake kuwa ni mengi hasa kwa mtu ambaye nilikuwa sijaoa wala kujenga hata nyumba ya maboksi.

Walijua tabia hiyo ina madhara mengi kimwili na hata kiroho hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na majanga mengi likiwamo hili la UKIMWI.

Hata tukiacha hayo, waliniasa wakijua dhahiri kuwa huko duniani niendako, huko Pwani, nitakutana na wengi wakiwa na mengi. Tena ya aina nyingi hata mengi mabaya yanayokuja kwa sura nzuri.

Wakakumbuka kile kisa cha bustani ya Edeni? Lile tunda lilikuwa zuri kwa chakula... lenye kutamanika kwa macho! Lakini matokeo yake ilikuwa nini? Mauti.

Lakini, binadamu hatujaweza kujifunza. Jamani tupewe somo gani zuri zaidi ya hilo!

Dunia sasa iko katika kilele cha mapambano kati ya wema na uovu; kati ya uasi na utii; kati ya haki na ubatili; kati ya ukweli na uongo; kati ya upendo na chuki;

Silaha za hatari na vivutio vyenye majaribu makubwa.

Dunia imejaa hatari; kuna mbwa mwitu wakali, majoka meusi na mekundu ya kutisha; shetani yuko "bize" akiwajeruhi wanadamu na kuzivua roho dhaifu toka zizini kwa Bwana.

Naye Yesu bila kuchoka, anaziokoa roho hizo dhaifu. Anazitibu majeraha na kuzirudisha zizini.

Binadamu tuko katikati ya mapambano haya na mitego ya shetani ni ya hila sana.

Si imeandikwa kwamba Roho waovu hujigeuza "malaika wa nuru" ili kutupotosha binadamu! Nasi dhaifu kiasi hiki tutashinda?

XXXXXXXXX

Hata hivyo; mbele ya mtoto Nafsa ni mwanaume gani, rijali aliyekamilika kama mimi ambaye angeyatilia maanani maneno yote hayo!

Basi, nami nikayapuuza, nikaanza kumwaga "sera" nyingine za ukweli na baadhi za uongo mithili ya wanasiasa na vitimbi vyao, na midomo yao kama tarumbeta wanapokuwa wanafanya kampeni za kugombea madaraka katika nchi au tapeli anayetafuta mkopo toka benki.

Hii yote, ni kwa sababu tayari "nilishamzimia" yule kimwana ashrafu.

Ndipo nami nilipojihisi kama kushukiwa na malakika aliyenitoa katika jehanamu ya mateso na kunipeleka katika kisiwa kile cha maraha.

Nikajiona ni kijogoo kinachowika wakati wote.

Hakika, ilikuwa ni furaha ilioje pale Nafsa alipokiri kuielea roho yangu kimapenzi.

Moyo wangu ukasuuzika na kufarijika sana.

Wahenga walisema; Msema kweli ni mpenzi wa Mungu na mungwana hubaki na uadilifu wake hata kwenye umaskini; nami kwa hili nitakuwa mkweli.

Mimi nilikuwa tofauti kabisa na wanaume wengi ambao mara tu, wanapokutana na vimwana warembo na mantashau kama Nafsa, huanza kujipamba sifa zingine ambazo hata hawana na kutunisha misuli yao ya kipesa.

Hali hiyo huwafanya hata wafikie hatua ya kuuza sufuria za nyumbani na kuweka amana baa na mahotelini, zile saa zao za "Seiko Five" walizovaa mikononi na hata pengine kuvuliwa viatu, mimi nilimueleza wazi kimwana Nafsa kuhusu hali yangu duni kipesa na kimaisha kwa jumla.

Ilinibidi nijiwahi haraka kabla chombo hicho hakijaanza zile tabia za wanawake wa mjini, tabia ambazo huwa ni kero kwa wengi na zenye kumshushia mtu hadhi yake.

Ni tabia zile ambazo mara tu unapomsalimia mwanamke, kabla hata hajageuka, kumuona anayemsalimia ni nani ili aiitikie, ghafla yeye huanza "Nina njaa! Ninunulie chips au Soda, basi!" na akishaitikia salamu huanza tena, huku akitafuna chips mayai au hata kavu, huanza huku akiendelea kushusha kiama, "Naomba hela nikachukulie nguo yangu kwa fundi!" Hee hivi hii ni fasheni kwa wote; mbona haitofautiani?!

Sasa hiyo huwa ni rasharasha, masika huwa bado nyuma inakuja polepole maana ole wao mbuzi wanaofuata nyayo za fisi.

Japo ilikuwa ni muda mfupi, muda huo mfupi ulikuwa na historia yake; ni vema niseme hivyo maana tuliongea mengi mazuri na matamu. Hata ule mzunguko wa masaa uliokuwa unalikaribisha giza ulionekana kwenda kasi na tukauona ni ule wenye kutukatili kwa makusudi.