Hivi Alikuwa Bado Yu Hai ?

Na. Josephs Sabinus

"HIVI bado yu hai, mbona hakuna shida inatokea?" Mmiliki wa hoteli hiyo alisikika kwa mbali akihoji kwa sauti ya kusubiri matokeo.

Sikujua lengo la swali hilo wakati nikitokea kwenye "chumba cha kujificha" na masikio yangu kunasa yasiyotarajiwa toka chumba kile. Nilirudi hadi pale kitini nilipokuwa nimeketi na kuacha kinywaji changu kwenye glasi iliyokuwa juu ya meza.

Kwa kuwa ulikuwa sasa muda mrefu nilikuwa nimeagiza kinywaji changu baada ya kuona ile chupa yangu ya konyagi ikielekea "kuzubaa", nilitua juu ya kiti na kutupa macho pale kaunta ili niwatazame kwa mshangao ni jinsi gani huduma ya baa hiyo ilivyo duni.

Fema nilipigwa na butwaa, sioni yeyote tofauti na wateja wengine waliokuwa wakiendelea kutumia pesa zao huku wengine wakijisindikiza kwa supu na nyama choma ya mbuzi sambamba na ndizi za kuchoma.

Wapo wengine ambao waliendelea kushusha kiama kwa kile walichoita, "chemsha" mimi siijui, naendelea na kilicho changu.

Mara msichana yule aliyekuwa akiendelea kuosha vyombo kwa ajili ya huduma za jikoni, akaja huku akiwa amebeba chupa ya konyagi na ile glasi ndogo kwa ajili ya kinywaji hicho kisicho cha kuendea kasi.

Kama ulivyo ukarimu wa hudumu wa baa na hoteli, akanimiminia kwenye glasi huku akiwa katika mwelekeo wa kunitazama.

" Kaka tafadhali usinywe pombe hii. Usinywe tafadhali," akasema kwa sauti ya chini mno lakini iliyonifikia sawia huku akinimimia kinywaji kwenye glasi. Hakuna aliyegundua hilo.

"Usipuuze tafadahali nakuomba,". Alipomaliza na kunyanyuka, akasema kwa sauti kubwa ya makusudi, "Na mimi nipate bia moja?" tayari akili yangu alijua kuwa yote hayo anayasema kwa lengo maalumu na hivyo yanahitaji umakini usio na hata chembe moja ya mzaha.

Sigara aina ya Embassy nilizokuwa nazo kwenye pakiti ziliongeza kasi ya kumalizika kwa kuwa akili yangu ilikuwa njia panda. Sikujua kulikoni mwanamke huyo nisiyemjua kwa jina wala sura, afikie hatua ya kunitahadharisha namna hiyo.

Yote hayo yalikuwa ni mgogoro kwangu kimawazo lakini, kila aliyeniona, ninaamini hakuna aliyeweza kugundua tofauti yoyote kwangu kwani namna nilivyoingia, ndivyo nilivyokuwa hadi wakati ule.

xxxxxxxxxxxxxxxxxx

Katika nchi hii ya Ughaibuni, mkoa wa Kati liliishi kundi kubwa la watu wenye asili ya Kihindi waliokuwa maarufu kwa biashara mbalimbali ikiwamo ya magendo.

Mauaji ya makusudi na ya kinyama kwa baadhi ya askari na wandishi wa habari waliofanya jaribio la kufichua vitendo hivyo, yalikuwa ni miongoni mwa maovu na hujuma zilizoendeshwa nchini sambamba na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Fema katika utundu wa kipaji alionao katika fani ya uandishi wa habari, alishani dodosa tangu matandu na sasa alikuwa njiani kukamilisha makoko ya ukweli kuwa kundi hilo lililoangamiza hata uchumi wa nchi, pia liliwahusisha baadhi ya vigogo serikalini wakiwamo matajiri wengine.

Alikuwa tayari amekwishapata baadhi ya takwimu muhimu za ushahidi. Kwa kuwa tayari alishaapa kuwa mwaminifu katika taaluma yake na taifa lake kwa jumla, tayari alishafichua baadhi ya "vigongo" na "vigogo" vya siri kubwa za hujuma hizo na "wachawi" wenyewe ni akina nani.

Wengine waliokuwa watumishi wa wafanyabiashara hao haramu, tayari walishakamatwa na mali zao kushikiliwa mikononi mwa serikali.

Sasa zilibakia siku mbili mahakama ya wilaya, isikilize kesi hiyo huku Bw. Fema akiwa shahidi namba mbili upande wa mashitaka.

Ni dhahii Fema alikuwa akiwindwa kwa kila hatua aliyokuwa akikanyaga ili walau waone linalowezekana kumkatisha kilimilimi; aidha kwa kunyonga, au kumchinja mardi tu, aende; afe.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Fema niliwaza na kuwazua haraka. Nikaacha vitu vyangu mezani na kuelekea jikoni, niliigeuzageuza makusudi nyama ya mbuzi iliyokuwa imening’inizwa pale ili kuwavutia wateja. Nikamuonesha mhudumu sehemu niliyotaka ili anichomee.

Huku nikilenga kila mmoja aone ninafanya nini, nikatoa shilingi 2000 na kulipia. Kisha nikamulekeza nilipokaa. Nikarudi mezani kwangu.

Wakati ninakaa, ambaye hakuona kilichoendelea, shauri zake mimi sijui ila ninachojua, meza iligongwa kwa goti langu, atakayesema ni makusudi sawa na atakayesema bahati mbaya naye, aseme mradi tu, kufikiri ndio uhuru pekee uliokamilika alionao mwandamu.

Tena huo ni uhuru wa asilimia 100. Uhuru mwingine una mipaka, kusema au kutenda kuna mipaka; ukivuka, sheria inakuwa juu yako.

Chupa na glasi nyingi zilianguka na kuvunjika hata ile glasi iliyokuwa na kinywaji, ikapata ufa kidogo huku ikibakia tupu. Bado hali ya wahudumu wale wa kawaida baani kuzidi kutokuonekana zaidi, ilizidi kunichanganya na kunipa nafsi ya kupata zaidi ya kupata nyeti.

"Waliweka sumu," mwanamke yule ambaye kwa wakati huo nilimtambua kama Lydia, akasema huku akikusanya vipande vya glasi na chupa zilizopasuka.

Niliaga kutoka kidogo huku nikisisitiza wahudumu waniandalie vizuri oda yangu ya nyamachoma ya mbuzi.

Nikapiga simu kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa ule wa Kati. Hakuchelewa kunitambua ninayeongea. Nikaelezea mintarafu tukio zima. Hata hivyo, nikamsihi atumie ufundi ambao utawawezesha askari wake kufanya kazi bila kutoa mazingira ya kumjengea uadui Lydia kwani endapo angegundulika kuwa ndiye aliyevujisha siri hiyo na kuninusuru, yeye angebeba "msalaba wangu".

Haukupita muda mrefu, nikawa nimerudi pale na Land Rover 110 ya polisi ikaingia huku imesheheni maafande. Waliponitupia macho, niliwaminyia macho ishara ya kuwaonesha msichana Lydia wamfahamu.

Watumishi mbalimbali wakiwamo viongozi wa juu wa baa hiyo, wakachukuliwa ili kutoa maelezo na kusaidia uchunguzi. Walivyochunguza hatujui lakini, baada ya muda, majibu toka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, yakaoenesha kuwa katika glasi ile niliyopewa, kulikuwa na aina kali ya sumu.

Na hata hivyo kwa kadiri ya mafunzo waliyopewa, askari wakawabaini na kuwashikilia wote waliopanga "niko" hiyo ya kuniua wakiwamo viongozi wa baa ile ambao walianza kutupiana jukumu hata wakafikia hatua ya kumkabidhi Lydia jukumu hilo wakidhani wakati wanapanga mpango huo pale mapokezi, hakuwasia.

Sheria ikawa juu yao na ingawa kama njia ya kujitetea apunguziwe adhabu, Mkurugenzi wa Hotel hiyo ambaye hata mimi sikumjua kuwa ni kaka wa mmoja anayeshilikiwa na polisi kutokana na ufichuaji wangu, akasema anaomba msamaha kwa kuwa naye ameshtuka kuona bado ni ngali hai. Akazirai baada ya kusikia kuwa amehukumiwa kifo ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kukatili maisha ya wenzao.

Yakaisha, ikapita miaka na miaka kila mmoja anajua Patel, Mkurugenzi yawa Hoteli hiyo maarufu ya SUGAR VIEW, kesha nyongwa kama malipo ya uovu wake.

Amini usiamini, kama hali haitabadilishwa katika nchi hiyo ya Ughaibuni, mambo yatazidi kuharibika kila kukicha. Kumbe ndio tabia inayowafanya hata viongozi wa serikali au watumishi wakifanya kosa katika mkoa huu na hata likabainika wazi, adhabu yake inakuwa kuhamishwa wilaya au mkoa mwingine.

"Hivi hawajui kuwa unaambukiza ugonjwa katika eneo kubwa! Hata kama ni kulindana, basi kulindana kuwe na misingi ya kujenga sio kulindana ili kuzidi kuangamiza."

"Hivi kwanini nyoka aue watu katika kijiji hiki badala ya kumuua na kumkomesha asidhuru wengine, anahamishiwa kijiji kingine . Ili iweje, akawaue na kuwaangamiza wa huko au...?" nikajisemea siku moja kimoyomoyo.

Ni siku tuliyopata habari kuwa Balozi mmoja wa nchi yetu ya Ughaibuni kafariki dunia. Kama ilivyokuwa ada, wote wenye mapenzi mema na nchi tulifurika kutoa heshima zetu kwa marehemu balozi wetu huku tumevalia mavazi meusi ya kuomboleza.

" Hivi alikuwa bado yu hai?" " Hivi ni huyu?" "Hivi hakunyongwa ... huyu ni balozi au ni muuaji?" Vilio vya maneno ya namna hiyo vikageuka na kutawala msiba. Wageni wa kutoka mataifa mengine wakapigwa na butwaa wasijue la kufanya.

Hata mapaparazi wa nje ya nchi wasio laza jambo, wakaanza kudodosa zaidi. Kesho yake Serikali ya nchi ikalazimika kufafanua kwa kutoa nusu ukweli.

"Katika kusherehekea taifa kutimiza miaka 10 ya uhuru, Mtukufu Rais aliwapa msamaha baadhi ya wafungwa na waharifu waliokuwa wakitumikia adhabu mbalimbali.

Miongoni mwao alikuwamo marehemu ambaye baadaye aliteuliwa kuwa..." inasema sehemu ya taarifa ya serikali.

"Ama kweli kama Rais alifanya hivyo, alishauriwa vibaya na watu wanaokula meza moja na wahalifu nchini, HIVI KWELI ALIKUWA BADO YU HAI? Siamini."

Nilidhani nimepata kumbe...3

Na. Modest Msangi

Lulu akaketi kama alivyotakiwa. "Habari za siku nyingi!" "Nzuri," Lulu akaitikia salamu hiyo. "Ujumbe wangu umeupata?" akauliza Salali.

"Sijaupata" akavuta meza na kuanza kusoma kimya kimya. Baada ya muda, akavunja ukimya ule, "Umemwambia nini Mona?" "Si umesema hujaupata. Ati mdogo wake amemwambia kuwa jamaa yule ni bwana yake."

"Mdogo wako amekudanganya," Lulu akasisitiza.

Salali akamhadithia jinsi ilivyokuwa. Lulu akabaki kimya kama kondoo aliyenyeshewa; bila kusema neno.

Baada ya muda, akasimama na kuaga. "Haya nisalimie," Salali akaitikia huku akiendelea kusoma pale mezani.

Lulu aliona kitendo cha siku hiyo kutosindikizwa na salali, kilikuwa kama ndoto ya mchana.

Kwa chuki aliyokuwa nayo, Salali alionekana anayetaka kutapika. Si kwa sababu ya kula kitu kisicho kizuri la hasha, bali kutokana na alichonitendea huku akijua akiamini kuwa Lulu alijua namna Salali alivyompenda.

Alimpa kila alichohitaji kwake. "Ngoja aniulize nimtapikie," Salali akamsubiri kwa usongo lakini, kama aliyejua, Lulu hakuuliza lolote kama ilivyo kawaida.

Akaondoka.

Siku iliyofuata,mambo yakawa yaleyale. Baada ya salamu, ukimya mkubwa ukatawala. Akatamani kusemeshana kitu lakini haikuwa hivyo. Akainuka na kuaga kuondoka. Salali akamuitikia kwa unyonge.

Lulu alitoka chumbani akionekana kana kwamba kamwagiwa maji ya barafu. Kwa aliye wajua awali, alijua dhahiri kuwa uhusiano wao umeguswa na baka.

Siku moja Salali alikuwa akisikiliza radio. Kipindi kilichokuwa hewani kilikuwa kikijadili kituo kimoja cha maelezo ya afya kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hicho hutoa huduma ya ushauri nasaha kwa wagonjwa na waathirika wa UKIMWI ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kujipima kujua afya yako.

Kwa kuwa ni siri kati ya mgonjwa na kituo, Salali naye akahamasika. Akaamua kwenda ili naye ajue moja. Haikuwa rahisi kujipeleka mwenyewe kutabiri atakufa lini. Lakini ilikuwa hivyo.

Terehe ya kurudi ilipofika, alitoka nyumbani akiwa na mawazo mengi. Hakujua kama nae anao, au la. Lakini, akajikaza kiume. "Mtu huvuna alichopanda . Kama ninao basi. Pia ninamshukuru Mungu,na kama ..." alijisemea kimoyomoyo.

Aliomba aambiwe ukweli pasi kufichwa lolote kama ni "mashariki, au magharibi". Alitaka ajue moja ili apange vema maisha yake.

"Usiwe na wasiwasi huna dalili zozote za UKIMWI lakini, usipokuwa makini, unaweza kuupata wakati wowote kuanzia sasa," Mshauri wa masuala ya UKIMWI, akamdokeza Salali siri ya mafanikio.

Miezi mingi ilipita tangu Salali ageuke bubu kwa Lulu. Siku moja alipata bahati ya kuhudhuria semina ya kiroho kwa vijana. Katika semina hiyo, yalifundishwa mambo mengi lakini yeye akakumbuka moja, jinsi ya kupata mchumba wa kike au wa kiume; na jinsi ya kuomba kwa Mungu.

Mada ilimvutia akawa makini zaidi. Mshauri akasema, "Vijana wengi wanaangalia sura na uwezo wa kifedha kwa huyo anaetamani awe mweza katika maisha tena wengine, wanamlazimisha Mungu kutaka vile wanavyotaka wao".

Hakika alifafanua mpaka hata Salali aliye mgumu wa kuelewa, akaelewa.

Yakamgusa. Akakumbuka namna alivyoomba kumpata mke mwenye umbo la nane, mrefu na mzuri wa kupendeza, eti aje aipambe nyumba yake ili asiwe na macho ya nje tena.

Mtoa mada akasema, "Ukiomba kichefuchefu, Mungu atakupa." Akagundua kuwa aliomba vibaya. "Nilidhani nimepata kumbe nimepatikana," akajisemea.

Akiwa kwenye mpango mpya, siku moja Lulu akaja nyumbani kwake. Akakuta Salali amebadilisha kitasa cha mlango wa nje na hivyo, akashindwa kuingia.

Akaacha maagizo kwa majirani ili Salali amauachie funguo mpya. Labda hakujua kuwa kubadili kitasa ilikuwa ni moja ya hatua zilizoashiria kumchoka na hata salali kutomtaka kabisa Lulu nyumbani kwake.

Siku nyingine tena, Lulu akamkuta Salali. Alipoingia ndani tu, alianza kufoka, "Mbona hukuniachia funguo! Ulijua mimi nipite wapi?" "Ufunguo wako" Salali alimjibu kwa "jibu swali" kumkata kilimilimi.

Akaongeza kwa hasira, "Samahani sana mkataba na wewe ulikwisha zamani. Naomba usizidi kunifuatafuata mimi, mfuate..."

Lulu alifanya jaribio la kuibuka mbogo, "Umenipotezea muda wangu halafu leo unasema hunitaki?" kahoji kwa hasira iliyochanganyika na huzuni.

"Wewe ndiye umenipotezea muda wangu na mipango yangu imeharibika kwa kukosa uaminifu. Nenda kwa huyo jamaa atakuoa. Huyo ndiye amekupotezea muda. Mimi niko mbioni kufunga ndoa na tayari kadi za harusi zilishaandaliwa; tena hizi hapa." Salali akasema huku akionesha kadi zile.

Lulu alilia huku akiomba msamaha lakini, muda ulikuwa umekwisha maana msamaha angeomba siku alipooneshwa kosa lake lakini, iweje sasa akae mwaka mzima!

"Wewe ni mla kunde umesahau, lakini mimi mtupa maganda, siwezi kusahau," MIMI NILIDHANI NIMEPATA: KUMBE NI MIMI NILIYEPATIKANA!!" Salali akasema kwa uchungu huku Lulu akimtazama macho ya huruma.

"Mungu wangu! Nilidhani hawezi kuniacha kwa namna alivyoonekana kunipenda na kuniheshimu kumbe maskini nilikuwa nachezea shilingi kwenye tundu la choo! Sasa nifanye nini mie nimekosa mwana kwa maji ya moto!" Lulu akjisemea akilia na kujutia matendo yake akaondoka naye akijisemea, "NILIDHANI NIMEPATA, KUMBE NIMEPATIKANA"