Make your own free website on Tripod.com

LIGI YA NANE BORA

Moro United kumenyana na Simba Jumapili

Na Tom Chilala

VINARA wa Kigi Kuu ya Tanzania Bara, Timu ya Soka ya Moro United, Jumapili hii inashuka tena dimbani kupambana na timu ya Simba katika mfululizo wa michuano ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hatua ya "Nane Bora".

Mchezo huo utakaofanyika katika uwanja wa Jamhuri

mjini Morogoro, unavuta hisia za wapenzi wengi wa soka kutokana na timu hizo mbili kupishana kwa pointi moja kila moja.

Mechi hiyo ni moja ya mechi muhimu kwa kila timu kwani Simba itahakikisha kuwa inarudisha heshima kwa wapenzi wao kutokana na Moro United kuifunga Simba mabao 2-1 katika mzunguko wa kwanza katika mchezo uliofanyika Kirumba Mwanza.

Moro United hadi sasa imeshatia kibindoni pointi 18. imeshinda michezo mitano, kutoka sare 3 na haijapoteza hata mchezo mmoja.

inayo magoli 10 ya kufunga na imefungwa magoli 5.

Simba imeshajinyakulia pointi 17 baada ya kucheza mechi 8. Imeshinda michezo mitano, imetoka sare 2 na imepoteza mechi moja. Ina magoli 15 ya kufunga na imekwishafungwa magoli 6.

Kufuatia mechi hiyo ya Jumapili, Uongozi wa Simba umeandaa mabasi madogo 100 aina ya Coaster kwa ajili ya kuwasafirisha mashabiki watakaokwenda Morogoro kuishangilia timu hiyo.

Katibu Mkuu wa Simba Kasssim Dewji, amesema kuwa mabasi hayo yataanza safari ya kwenda Morogoro saa mbili asubuhi toka makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Msimbazi Dar-Es-Salaam, na kurejea baada ya mchezo kumalizika.

Yanga tawi la Tandale kuchagua viongozi Sept. 16

l Asilia mabingwa mchezo wa bao Kinondoni

Na Maneno Nguru

UCHAGUZI wa viongozi Tawi la Yanga Tandale kwa Tumbo Jijini Dar-Es-Salaam, unatazamiwa kufanyika Septemba 16, mwaka huu, katika shule ya msingi Tandale, kuanzia saa nne asubuhi.

Mwenyekiti wa muda wa tawi hilo, Hamisi Ally Makenyangiro maarufu kama Hamisi Kibonge amezitaja nafasi mbalimbali zinazogombewa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi, Mweka Hazina, na Wajumbe wanne.

Kibonge amesema kwamba wanamichezo wanaowania nafasi za uongozi wameanza kujiorodhesha tokea Agosti 30, mwaka huu.Aidha, alisema kwamba mwisho wa kujiorodhesha ni Septemba 10, mwaka huu.

Wakati huo huo: Klabu ya mchezo wa bao ijulikananyo kama Asilia, yenye maskani yake maeneo ya Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam, hivi karibuni ilijunyakulia ubingwa wa mchezo huo katika Wilaya ya Konondoni katika mashindano ya kumtafuta Bingwa wa Bao wilayani humo yaliyofanyika katika shule ya Msingi Karume, iliyopo Magomeni Mwembe chai.

Katika Mashindnao hayo, timu ya Asilia ilijipatia zawadi ya Redio wakati mshindi wa pili, Klabu ya Minazini ya Mwananyamala A, ilijipatia zawadi ya saa ya ukutani.

Nayo klabu ya Mchakamchaka ya Tandale kwa Tumbo, iliiibuka mshindi wa tatu na iliambulia zawadi ya miche minne ya sabuni ya kufulia.

Mashindano hayo yalianza Agosti 25, mwaka huu na kumalizika Septemba 2. Yalizishirikisha timu 12 wilayani humo.Vilabu hivyo ni Elephant ya Kawemzimuni, Jahazu ya Mwananyamala kwa Kopa, Asilia ya Magomeni Kagera, Kizota ya Mburahati na Mchakamchaka ya Tandale kwa Tumbo.

Vilabu vingine ni Mtamboni ya Magomeni Mzimuni, Mbezi ya Mbezi Luisi, Minazini ya Mwananyamala A, Makuti ya Magomeni Makuti, Uyagauyaga ya Mwananyamala B, Na Yellow Star ya Ukwamani, Kawe.

Timu 24 kushiriki Ligi ya Yosso Ilala

Na Jenifa Benedicto, DSJ

TIMU 24 za soka zinatarajiwa kushiriki katika mechi mbalimbali za Ligi ya Yosso katika Manispa ya Ilala kuanzia Septemba 10, mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar-Es-salaam, Katibu wa Chama cha Michezo ya Watoto IDYOSA, Hemedi Bosso, alisema kuwa michuano hiyo itafanyika katika viwanja vya Karume jijini.

Alisema, timu zitakazoshiriki ligi hiyo ni zile zilizokamilisha utaratibu wote usajili wa ligi hiyo ikiwa ni pamoja na ulipaji ada na urudishaji wa fomu za usajili.

Hemedi alisema kuwa, timu hizo zimegawanyika katika makundi mawili; A na B.Alizitaja timu za kundi A kuwa ni; Ikweta, King African, Wonder Boys, Tabata United, Super Control, Wizard, Simba Kids, African Star, Madawa, Sahara, Chura Dume na Kisukuru.

Aidha, timu za kundi B ni Manchester United, Small Tiger, Mogo, Gett, Gonga, Sitaki Shari, City Republic, Goold Villah, Yanga Kids, Reli, Ndanda Kids na Dar-Es-Salaam Newala.

Michuano hiyo ilizinduliwa Septemba 3, mwaka huu, na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Abuu Bin Juma; aliyekuwa mgeni rasmi.Timu zitakazocheza septemba 10 ni Ikweta na King African, watacheza saa tisa na saa kumi Manchester itapambana na Small Tiger.

Wakati huo huo: Kamati ya IDYOSA, ilisema kuwa hawana wadhamini wa kuendesha mechi hizo hivyo uendesha kibahati bahati tu.

Hata hivyo, kamati hiyo imetoa ombi kuwa, kama kuna mtu au shirika linaloweza kuwadhamini, liwasiliane na chama hicho au kilabu chochote kilichosajiliwa

Lister, Bajiu kupiga ngumi Sept. 16

Na Mwandishi Wetu

BINGWA wa taifa wa ngumi za kulipwa wa uzani wa Super Middle, Georg Lister Sabuni, atapanda ulingoni Septemba 16 katika pambano lisilo la kuwania ubingwa dhidi ya Ernest Bujiu.

Akizungumza na KIONGOZI jijini mwishoni mwa juma, Mweka Hazina wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Tutus Kadyanji alisema kuwa pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Annex, uliopo Keko jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema pambano hilo ni katika maandilizi ya bondia huyo kuwania mojawapo ya mataji ya kimataifa.

Sabuni ambaye kwa hivi sasa anajulikana kama "Simba Mzee", alisema kuwa ana nia ya kuwania Taji la Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBF), kama ilivyo kwa baadhi ya mabondia wa Tanzania.

MICHUANO YA KOMBE LA CASTLE:

Tanzania Kuvuna nini?

Na Mwandishi Wetu

MICHUANO ya kuwania ubingwa wa Kombe la Castle, ambayo itashirikisha nchi nne inatarajiwa kufanyika mwezi ujao kwenye uwanja wa Sheikh Amir Abeid, mjini Arusha.

Nchi zitakazoshiriki michano hiyo ni tatu za Afrika Mashariki pamoja na moja iliyoalikwa ambayo ni Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC)

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyopangwa katika halfa fupi iliyofanyika Hoteli ya Sea Cliff, jijini Dar es salaam, hivi karibuni michuano hiyo itaanza Oktoba 24, kwa kuzikutanisha timu za taifa za The Cranes ya Uganda na Harambee Stars ya Kenya.

Pia, siku hiyo Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itajitupa uwanjani kuivaa timu ya Taifa ya DRC.

Licha ya ratiba hiyo kupangwa, wasiwasi mkubwa wa Watanzania wengi ni juu ya timu yao ya Taifa ambayo mpaka sasa haijaanza maandalizi yoyote licha ya kutangazwa.

Wasiwasi huo unatokana na Tanzania kuonekana kuwa na kiwango cha chini katika soka licha ya kukosa maandalizi mwafaka ikilinganishwa na washiriki wengine.

Kwa mujibu wa Chama cha Soka Nchini (FAT), Taifa Stars itaingia kambini mwezi ujao chini ya makocha watatu ambao ni Mshindo Msola, Syller Said Mziray na Charles Boniphace Mkwassa, siku chache kabla ya michuano kuanza.

Mwakilishi wa Kampuni ya Bia ya Afrika Kusini, Ponga Liwewe ambayo ndio wadhamini wa michuano hiyo kupitia bia yake ya Castle, alizitaja zawadi za michano hiyo kuwa ni shs. milioni 12 kwa mshindi wa pili, sh. milioni 10 kwa mshindi wa tatu na timu itakayoshika mkia itaambulia shs. milioni 8.

Pia kila mchezaji bora wa kila mchezo atakuwa akijinyakulia kikombe kidogo kama zawadi.

Bingwa mtetezi wa michauno ya Kombe la Castle ni The Cranes ya Uganda iliyonyakua taji hilo kwa kuichapa Harambee Sars ya Kenya, nafasi ya tatu ilichukuliwa na Taifa Stars ambapo Black Stars ya Ghana, ilishika mkia katika michuano hiyo iliyofanyika uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi.