Make your own free website on Tripod.com

KUFUATIA KUIBUKA BINGWA WA LIGI KUU TANZANIA BARA

Timu ya Simba yazidi kutumiwa pongezi

Na Omary Mngindo, Kibaha

WANACHAMA wa timu ya soka ya Simba tawi la Kibaha kwa Mfipa, wametuma salamu za pongezi kwa Simba makao makuu kufuatia timu hiyo kuibuka Bingwa Mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akitoa Salaam hizo kwa niaba ya wanachama wake, Katibu wa tawi hilo, Mshindo Kitike kusema mshikamano ulioonyeshwa na Wanasimba kwa kushirikiana na uongozi ndiyo umesaidia timu yao kufanya vizuri tokea msimu huu uanze.

" Msimu huu tulianza vizuri tangu katika kombe la Tusker ambalo lipo mikononi mwetu, na pia tuliweza kuonyesha uhai kwenye Kombe la Washindi pale tulipoweza kuwachachafya Wamisri," alisema Kitike

Naye Mweka Hazina wa tawi hilo la Kihaba kwa Mfipa, Fahim Mohamed, ametoa pongezi kwa timu ya Ruvu JKT kwa kupanda hadi Ligi Daraja la Kwanza Tanzania, msimu ujao.

Mohamed ambaye alizungumza na gazeti hili kwenye ofisi yake,alisema kuwa, hii ni hatua ya kujivunia kwa wilaya ya Kibaha na mkoa wa Pwani kwa jumla.

Aidha amewaomba washikadau wa michezo wilaya na mkoa kwa pamoja wakutane mapema na kupanga mikakati ya ubingwa wa ligi hiyo ili kombe hilo litue mkoa wa Pwani.

Timu 12 kushindania ubingwa Temeke

Na Mariam Salum

Jumla ya timu 12 za soka wilayani Temeke, zinatarajia kushiriki katika Mashindano ya kutafuta bingwa wa wilaya hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Michezo ya Watoto Wilayani humo (TEDIYOSA), Adam Mkami, alisema michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 10, itafanyika katika viwanja vya Tandika Mabatini na Uwanja wa Taifa.

Alisema lengo la michuano hiyo ni kutafuta timu nne ambazo zitashiriki katika ligi ya mkoa wa Dar es Salaam.

Adam alisema, timu hizo zimegawanyika katika makundi mawili ya A na B. Alizitaja timu za kundi A kuwa ni: Jitegemee, Mchangani, Mtakuja, Mzamba, Kiguluvenja na Manchester.

Timu zinazounda kundi B kama zilivyotajwa na Makamu Mwenyekiti huyo wa TEDIYOSA ni Kiembe Samaki, Miembeni, Nuru ya Kiini, Temeke Kidizini, Palama Kidizi na Big Fish.

Alisema washindi wa michuano hiyo wanatarajiwa kuzawadiwa ambapo mshindi wa kwanza atapata mipira mitatu, wa pili mipira miwili na watatu na nne watapata mpira mmoja kila mmoja.

Mbali na ti zitakazoshindwa kuzawadiwa,vile vile mchezaji bora wa kwanza na wa pili watapata ofa ya kupanda daladala kwa muda wa mwezi mmoja ambapo alizitaja Daladala hizo ni, Alijinunu na Kitendawili.

Ukata wasababisha Rebecca asipeleke muziki wa Injili mikoani

Na Dalphina Rubyema

MFUKO wa Udhamini wa Wanawake Wakristo (Christian Business Women Foundation Trust Fund), umesema ukosefu wa pesa ndio uliosababisha ushindwe kumpeleka mikoani mwana muziki wa nyimbo za Injili, kutoka nchini Afrika ya Kusini, Rebecca Malope.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-es-Salaam katikati ya juma, Mlezi wa mfuko huo ulioandaa ziara ya mwanamuziki huyo wa Injili, Mchungaji Nathanael Kigwild, alisema licha ya kutambua umuhimu wa kuupeleka ujumbe wa Rebecca katika mikoa mingine pia, Mfuko huo meshindwa kufanya hivyo kutokana na gharama kuwa kubwa.

Maelezo ya Mchungaji Kigwild yametokana na gazeti hili kutaka kujua sababu za mwanamuziki huyo kuishia jijini Dar-ss-Salaam pekee, huku hata walio katika mikoa mingine wanahitaji Injili ili iwanusuru katika maangamizi ya kiroho na kimwili kutokana na ugonjwa wa UKIMWI na vita ya koo na koo.

"Ni kweli kulikuwa na umuhimu mkubwa sana wa kumpeleka mwanamuziki huyo mikoani lakini sababu kubwa ni ukosefu wa pesa. Gharama za kufanya hivyo ni kubwa na hivyo, tumeona afanye maonesho yake hapa Dar-es-Salaam na watu wa mikoani watapata ujumbe wake kupitia vyombo vya habari na watu watakao bahatika kumwona," alisema.

Aliongeza, "Hata Yesu hakufika dunia nzima kuwaeleza watu juu ya wokovu, alifika katika baadhi ya maeneo lakini ujumbe wake ukasambaa dunia nzima".

Mwanamuziki huyo na ujumbe wake waliwasili nchini mwishoni mwa juma kwa ajili ya maonesho mawili ya nyimbo za Injili katika ukumbi wa Diamond Jubilei kwa siku za Ijumaa na Jumamosi.

Ziara yake ina lenga kuchangia watoto walioathirika na ugonjwa wa UKIMWI.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili jijini Dar-es-Salaam, mwanamuziki huyo alisema amekuwa akifanya kampeni dhidi ya UKIMWI hata akiwa nchini kwake Afrika ya Kusini, akichangia watoto walioathirika na ugonjwa huo kupitia muziki wake.

Alisema kutokana na muziki kuutumia muziki wake wa Injili katika kampeni dhidi ya UKIMWI, Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandela, aliwahi kumpa tuzo na kula naye chakula.

TEFA yaandaa Michuano ya Ukimwi

Na Meryna Chilonji

Chama cha Mpira wa Miguu WilayaniTemeke (TEFA), kinaadaa michuano ya Ligi Daraja la Tatu kwa ajili ya tamasha la siku ya UKIMWI duniani inayoadhimishwa Desemba Mosi mwaka huu.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan Mpanjira, ameliambia KIONGOZI katikati ya juma kuwa, tamasha hilo limeandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Health Scope Tanzania.

Kwa mujibu wa Mpanjila, tamasha hilo litajumuisha michezo ya aina mbalimbali ukiwemo mpira wa miguu.

Aidha Mpanjira alisema, mpaka sasa jumla ya timu nane zimeishateuliwa kwa ajili ya michuano hiyo.

Alizitaja Timu hizo kuwa ni Hevarest, Yombo Stars, Mbagala Market, Kiburugwa, Panama, Mwanga All Stars, Shababi na Mzizima.

" Timu zilizoteuliwa zitachuana ili kupata timu moja ambayo itapata zawadi toka Health Scope Tanzania," alisema Mpanjira.

Alisema timu zitazofungua dimba hapo Desemba 6 mwaka huu ni Evarest na Yombo Stars kwenye uwanja wa Tandika Mabatini ambapo Desemba 7 mwaka huu katika uwanja wa Mbagala,timu ya Mbagala Market na Kiburugwa zitatoana jasho.

Desemba 13, timu za Panama na Mwanga All Stars zitawasha moto katika uwanja wa Tandika Mabatini ambapo mchezo wa mwisho utakuwa ni kati ya Shababi na Mzizima, ambao utachezwa katika uwanja wa shule ya Msingi Kigamboni.