Mshindi Simba, Yanga atavuna nini Jumapili?

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya timu ya Simba ya Msimbazi jijini Dar-es-Salaam, kuwa bingwa wa Tanzania Bara baada ya miaka sita na Yanga kuvuliwa ubingwa wa Muungano, kuna wasiwasi kuwa, huenda mechi ya Jumapili ikapoa.

Kwa matokeo ya mechi baina ya Simba na Mtibwa iliyofanyika katika Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza Alhamisi iliyopita, Simba sasa imefikisha pointi 30 ambazo haziwezi kufikiwa na mpinzani wake wa karibu ambaye ni Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Katika pambano hilo, Timu ya Simba iliirarua Mtibwa kwa mabao 2-1 na hivyo, Mtibwa kujikuta imevuliwa ubingwa ambao imedumu nao kwa miaka miwili.

Jumapili hii, pia timu ya Mtibwa itamenyana na maafande wa 977KJ.

Timu za Simba,Mtibwa, na Moro United, tayari zimefuzu kucheza Ligi Kuu ya Muungano.

Wasiwasi huo unatokana na ukweli kwamba mechi hiyo haitabadilisha msimamo wala washiriki wa Ligi Kuu ya Muungano zaidi ya kukamilisha ratiba tu. Pia, tayari Simba imekwishatwaa ubingwa huo wakati bado ligi hiyo inaendelea na bado Simba ina mchezo mmoja dhidi ya Yanga.

Licha ya kupooza kwa mchezo huo, pia wasiwasi mwingine unatokaana na hofu kwamba huenda watazamaji wachache tu, wakajitokeza na hivyo, kuathiri mapato ya mechi.

Timu zinazoshiriki Ligi Kuu kwa sasa sana sana zinategemea mapato ya mechi baada ya mdhamini wa siku nyingi wa ligi hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kujitoa kudhamini ligi hiyo, kutokana na Chama cha Soka nchini(FAT), kuvuruga mfumo wa ligi kwa kuongeza timu bora kutoka 6 hadi 8.

Hata hivyo, mashabiki wengine hawana wasiwasi kuwa mechi hiyo itakuwa na msisimko kama kawaida kutokana na upinzani wa kijadi uliopo kati ya timu hizo mbili za Dar-es-Salaam.

Timu itakayoshinda mechi ya Jumapili itapata tu heshima na kuthibitisha umwamba wake dhidi ya mwenzake lakini, ushindi hautabadili sura katika ligi.

Katika mchezo wa Mtibwa na Simba, bao la kwanza la Simba ilifungwa na Boniface Pawasa katika dakika ya 45.

Kunako dakika ya 63, Amri Saidi alimkwatua Kassim Issa katika eneo lao la hatari na ivyo, Mwamuzi Hussein Kantabula, kutoa adhabu ya penalti dhidi ya Simba iliyopigwa na Dua Saidi. Bao la pili la Simba lilifungwa na Emmanuel Gabriel.

Liverpool, Owen watiliana saini

l Atalipwa milioni 1 kwa siku?

LONDON, Uingereza

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya soka ya Liverpool ya Uingereza, amesaini mkataba mpya kuichezea klabu hiyo kwa miaka minne.

Hivi sasa Owen ni majeruhi kutokana na kuumia Jumamosi iliyopita wakati wa pambano baina ya Liverpool na Tottenham Hotspurs, katika Ligi Kuu ya England.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Liverpool, Gerard Houllier, Owen atakuwa akilipwa Paundi 10,000 (Sawa na shilingi 1,000,000) kwa siku.

Akizungumzia hatua hiyo ya kusaini upya, Michael Owen alisema mkataba huo ni wa nne katika kuichezea timu ya Liverpool.

"Sijawahi kuwa na wazo la kuchezea timu nyingine mbali na Liverpool," alisema Owen mwenye miaka 21.

Aliongeza kuwa, uaminifu wa timu hiyo kwake, umechangia uamuzi wake wa kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo kwani uongozi wake umekuwa wazi katika kuufanyia marekebisho mkataba wake.

Msimamo wa Ligi ya Soka ya Mabingwa wa Ulaya

KUNDI A

TIMU P W D L F A Pts

Real Madrid 3 3 0 0 10 2 9

AS Roma 3 1 1 1 3 3 4

Anderlecht 3 0 2 1 2 5 2

Lokomotiv 3 0 1 2 2 7 1

KUNDI B

TIMU P W D L F A Pts

Boavista 3 2 1 0 6 3 7

Liverpool 3 1 2 0 2 1 5

Borussia 3 0 2 1 3 4 2

Dynamo 3 0 1 2 3 6 1

KUNDI C

TIMU P W D L F A Pts

Panathinaikos 3 3 0 0 5 0 9

Real Mallorca 3 2 0 1 2 2 6

Arsenal 3 0 0 3 2 6 0

KUNDI D

TIMU P W D L F A Pts

PSV 3 2 0 1 5 5 6

Galatasaray 3 2 0 1 3 3 6

Nantes 3 2 0 1 7 3 6

Lazio 3 0 0 3 1 5 0

Msimamo huu ni kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana hadi tunakwenda mitamboni.

 

Mengi afunga mashindano ya Bonite Jumamosi

Na Modest Msangi

MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi, Jumamosi hii anafunga Mashindano ya 14 ya Wazi ya Kimataifa ya Kombe la Bonite ambayo yamekuwa yakifanyika katika viwanja vya Hindu Mandal mjini Moshi, yakizishirikisha timu 40 kutoka Kenya, Uganda, Malawi na Tanzania.

Akifungua Mashindano hayo wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hilda Ngowi, aliwataka wanamichezo kujenga uhusiano kwa kushindana katika michezo bila ugomvi ili kuimarisha ujirani baina ya nchi zao.

Mratibu wa Mashindano ambaye pia ni Meneja masoko wa Bonite, Gilbert Uwisso, amesema kuwa, Mengi atakabidhi kombe kwa washindi wanaume na wanawake pamoja na shilingi 300,000 na 100,000 kwa washindi wa kwanza na wa pili na wachezaji bora.

Timu za Tanzania zimekuwa wasindikizaji katika mashindano hayo ya kila mwaka ya Mpira wa Wavu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya timu za kutumainiwa Jeshi Stars na Metro za Dar-es-Salaam kwa kuanza kufanya vibaya.

Timu ya Jeshi Stars ilianza vibaya katika mchezo wa ufunguzi baada ya kuchapwa seti 3-1 na Halmashauri ya Jiji la Nairobi (NCC) wakati mabingwa watetezi wa kombe hilo kwa wanaume, General Motors (GM) waliwazabua viziwi wa mji wa zamani wa Kampala (OKD) kwa seti 3-1.

Timu nyingine ya Metro ilishindwa kufurukuta mbele ya Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuchapwa seti 3 bila majibu huku GM ikiiadhibu timu ngeni katika mashindano hayo, Shangani ya Zanzibar kwa seti 3-0 hivyo, GM kujihakikishia utetezi wa kombe kwa mwaka wa nne mfululizo.

Jeshi Stars ilizinduka na kuichapa Halmashauri ya Jiji la Kampala (KCC) kwa seti 3-0.

Hadi tunakwenda mitamboni, Jeshi Stars ndiyo pekee ilifanikiwa kuingia robo fainali. Mabingwa watetezi kwa wanawake, NCC, ilianza vema kutetea kombe baada ya kuichapa timu ya Jitegemee kwa seti 3-0.

Timu nyingine za Tanzania ni pamoja na JKT Mbweni, Dar Mchanganyiko, Morogoro Mchanganyiko, Ruaha, Tanga Mchanganyiko na timu sita za mkoa wa Kilimanjaro zote hizo tangu michezo hiyo kushirikisha timu za Afrika Mashariki na Kati zimekuwa wasindikizaji.

Wakati huo huo: Chama cha Mpira wa Wavu nchini (TAVA), kinakutana Jumapili hii kujadili maendeleo yake kwa mwaka uliopita.

Katibu Mkuu wa TAVA, Adam Gwao, alisema mkutano huo ni wa kawaida kila mwaka baada ya kumalizika mashindano hayo yanayoendeshwa na kudhaminiwa na Bonite.