Make your own free website on Tripod.com

Michezo

Tamaa za viongozi zimechangia kuzorotesha soka-Lazaro

Na Sebastian Mafwele

UKOSEFU wa fedha na tamaa za viongozi wa timu zilizoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara,imeelezwa kuwa ni moja ya sababu zinazopelekea baadhi ya timu za mikoani kushindwa kufanya vizuri kwenye ligi hiyo.

Maelezo hayo yalitolewa katikati ya juma jijini Dar-es Salaam na Kocha Msaidizi wa timu ya Coastal Union ya Tanga ,Joseph Lazaro wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili.

Lazaro alisema kuwa baadhi ya timu za mikoani zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa fedha hali inayosababisha timu hizo zijiendeshe katika mazingira magumu.

Alisema timu nyingi hazitoi mishahara kwa wachezaji na hata kwa makocha bali kinachotolewa ni posho tu ambayo hutolewa mara baada ya mechi kama siyo wakati wa safari ya kwenda nje ya mikoa.

Lazaro ambaye aliwahi kuichezea timu ya Yanga ya jijini Dae es Salaam na Coastol Union yenyewe,alisema kwa mara zote posho zinazotolewa huwa hazitoshelezi mahitaji kwani mara nyingi huwa haizidi sana sh.3,000.

Alisema hali hiyo hupelekea baadhi ya viongozi na wachezaji kuuza mechi na hasa wanapokutana na timu zenye uwezo kifedha.

"Timu za mikoani ni nzuri na zina wachezaji wazuri kuliko hizi za hapa Dar es Salaam bali hukatishwa tamaa kutokana na hali ya kifedha ambayo hupelekea kukosa huduma muhimu hata wachezaji wanapokuwa kambini"alisema Lazaro.

Kwa hali hii alisema kuwa ushindani wa timu kwenye Ligi Kuu huwa ni mkubwa na hivyo kutoleta msisimko na hatimaye kiwango cha soka kutelemka.

KKKT yaandaa mashindano ya Kwaya Kuu

Na Neema Dawson

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Daiyosisi ya Mashariki na Pwani imeandaa Mashindano ya kwaya yatakayofanyika Novemba 18 mwaka huu katika viwanja vya KKKT,Usharika wa Kijitonyama.

Mashindano hayo yatazihusisha Kwaya Kuu za Majimbo sita ya Daiyosisi hiyo ambapo kila jimbo litawakilishwa na kwaya tatu.

Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na Mkuu wa Jimbo la Kinondoni, Mchungaji Ajuaye Kinghomela ,zinasema kuwa kwaya zitakazowakilisha jimbo hilo la Kinondoni,tayari zimekwisha patikana ambapo zilitajwa kuwa ni Kimara Lutheran, Sinza Lutherani, na Kwaya ya Kunduchi Lutherani ambazo zote ni kwaya kuu.

Mchungaji Kinghomela alisema kuwa lengo la mashindano hayo ni kudumisha mahusiano, mawasiliano na ujirani kati ya kwaya moja na nyingine, pamoja na kuwaelimisha wakristo kuimba nyimbo ambazo ziko katika kitabu cha nyimbo cha Mwimbieni Bwana.

"Kila kwaya itaimba wimbo mmoja kutoka katika kitabu cha nyimbo cha Mwimbieni Bwana na wimbo mmoja wa kiasili wenye maudhui ya kumtukuza Mungu"alisema.

Aidha alisema kuwa katika mashindano hayo Mgeni rasmi atakuwa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jerry Mngwamba na wanatarajia kupata washindi watatu kutoka kwaya 18 zitakazoshiriki.

"Matokeo yatatangazwa na waamuzi ambao watakuwa wamechaguliwa kufanya kazi hiyo na washindi watapata tuzo na vikombe kwa ajili ya kumtangaza na kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji"alisema .

Tanzania yajiandaa kushiriki mashindano ya dansi

Na Meryna Chillonji

TANZANIA inajiandaa kushiriki katika mashindano ya muziki wa dansi yanayotazamiwa kufanyika mwakani nchini Singapore chini ya usimamaizi wa World Playnet Dance.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam, Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania(TDMA), Samwel Semkuruto, alisema kuwa, awali mashindano hayo yalipangwa yafanyike Oktoba 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, mashindano hayo yatafanyika kuanzia mwezi Desemba mwaka huu hadi Januari Mosi mwakani dhumuni ya kumtafuta mshindi mmoja atakayewakilisha katika mashindano ya dunia.

Amesema kwamba mashindano hayo yatakayofanyika kwa awamu , yataanzia Dar-es-Salaam wakati wa sikukuu ya Krisimasi na Iddi , Arusha na mwisho yatafanyika mjini Mwanza wakati wa mwaka mpya.

Katibu huyo amesema mpaka sasa wameshapeleka barua katika makampuni kadhaa kwa nia ya kuomba udhamini wa mashindano hayo ikiwemo kampuni ya simu za mkononi ya Voda Com na kampuni ya bia nchini(TBL).

MALUMBANO KATI YA makatibu FAT NA FRAT

Nkamia amtaka Rage kuwa mvumilivu

Na Anthony Ngonyani

KATIBU Mwenezi wa timu ya Simba, Juma Nkamia amemtaka Katibu wa Chama cha Soka nchini (FAT)Ismail Aden Rage kuwa mvumilivu na kupunguza hasira na malumbano dhidi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi wa Soka nchini (FRAT).

Rage alitoa kauli hiyo wakati alipohojiwa na gazeti hili juu ya malumbano yanayoendelea kati ya Katibu huyo wa FAT na Katibu Mkuu wa FRAT,Hussein Mchatta.

Alipendekeza Rage kuwa mvumilivu na kuzingatia kuwa hilo suala ni moja ya majukumu yake kwani FRAT ni sehemu ya FAT angeweza kumaliza kabisa suala hilo bila vyombo vya habari kupata kitu .

Alisema kinachotakiwa katika kutatua suala hili ni uvumilivu na busara kitu ambacho ni muhimu kwa FRAT,ikizingatiwa kuwa kila chama lazima kiwe na mkutano mkuu wa mwaka katika kuimarisha utendaji.

Vile vile Katibu huyo Mwenezi wa Simba amekilaani kitendo cha Rage kwenda ofisi za FRAT kwa nia ya kumtafuta Machatta ambapo alisema si cha kiungwana.

Malumbano hayo yanatokana na kile kilichodaiwa kuwa Machatta anamutuhumu Rage kama Katibu Mkuu wa FAT,kuwa ni kikwazo kikubwa katika kuidhinisha FRAT ipewe msaada wa fedha za kufanyia mkutano mkuu.