KIFA yaipigia magoti ofisi ya Meya

Na Getrude Madembwe

CHAMA cha Mpira wa Miguu Wilayani Kinondoni (KIFA) kimemwandikia barua Meya wa Manispaa hiyo kuomba msaada wa pesa wa kusaidia timu ya Kumbukumbu ambayo imepangiwa kucheza Ligi Daraja la Kwanza mkoa wa Kigoma.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma ,Katibu Mkuu wa chama hicho , Ramadhani Kampira alisema kuwa wameamua kuomba msaada huo baada ya kuona kuwa timu hiyo inahitaji kiasi kikubwa cha pesa na chama hicho hakina uwezo wa kuzipata.

"Timu hii ipo katika Manispaa yetu ingawa ni timu binafsi (Private), hivyo basi tumeamua kuitafutia pesa ili iweze kufika Kigoma kushiriki katika Ligi Daraja la Kwanza.

Katibu Mkuu huyo alikitaja kiasi cha fedha kinachohitaji kuwa ni shilingi 780,000 ambazo ni gharama za kwenda na kurudi katika mashindano hayo.

Wakati huo huo: Chama hicho kimeomba kumiliki uwanja wa mpira wa miguu wa Mburahati uliopo katika Manispaa hiyo.

Kwa sasa uwanja huo unamilikiwa na Baraza la Michezo la wilaya ya Kinondoni.

Kampira aliiambia Kiongozi ofisini kwake kuwa iwapo watapewa uwanja huo itasaidia kupunguza wimbi la kuomba misaada kwa watu wengine kwani watakuwa wanapata pesa kutokana na uwanja huo utakaokuwa ukikodishwa na timu mbalimbali.

"Tukipewa uwanja huo utatusaidia sana na hata hivyo tumewapata wafadhili kutoka Japani ambao wametuahidi tuwapelekee hati na ramani ili watusaidie kuukarabati pia waweze kuingiza katika bajeti yao itakayoanza mwishoni mwa mwezi Juni" alisema.

Kupigwa kwa waamuzi ni kutojua sheria - Mkufunzi

Getrude Madembwe na Bilhah Massaro

MKUFUNZI wa Waamuzi wa Mpira wa Miguu mkoani Dar-Es-Salaam ,Omari Kasinde amesema kuwa suala la waamuzi kupigwa uwanjani linatokana na wachezaji na mashabiki wa mchezo huo kutofahamu sheria .

Kashinde aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili jijini Dar-Es-Salaam

Aliwataka wachezaji watambue kuwa wanapokuwa uwanjani hawatakiwi kushikana mashati na wakifanya hivyo wanakuwa wamefanya kosa hivyo ni haki ya Mwamuzi kupiga filimbi ama kutoa adhabu.

"Mwamuzi akitoa adhabu,mashabiki na wachezaji huanza kutoa maneno machafu au kumsonga na kumpiga"alisema.

Aliongeza"Bado wachezaji na mashabiki hawafahamu kuwa hata kama timu fulani ikifunga goli kwa stahili ya kutatanisha ni lazima Mwamuzi alikatae goli hilo".

Vile vile Mkufunzi huyo alikishauri chama cha Mpira wa Miguu nchini (FAT) kuzingatia umuhimu wa kuwapeleka Makamisaa ambao wanazifahamu sheria za mpira Alisema kuwa iwapo atapelekwa mtu ambaye hazijui sheria anaweza akaboronga mechi.

Vile vile alisema kuwa viongozi hao wa FAT wanatakiwa kuwapeleka masomoni au hata kuwasaidia watendaji wake ikiwa ni pamoja na kuwasomesha.

Wakati huo huo: Kamati ya Mpira wa Miguu Manispaa ya Ilala (IDFA) itakuna Jumamosi hii kujadili usaili na kupanga tarehe kwa vilabu kuchukua fomu za usaili huo.

Akizungumza na gazeti hili katika ofisi za chama hicho ,Afisa Mtendaji wa Chama hicho ,Daudi Kanuti alisema kuwa pamoja na kupanga tarehe pia watajadili ada itakayohitajika.

Kiburugwa yapigwa faini kwa kufanya vurugu

l Kinyang'anyiro cha Kombe la Yagga kuanza leo

Na Vick Peter

CHAMA cha Mpira wa Miguu wilayani Temeke (TEFA) kimeipiga faini timu ya Kiburugwa inayoshiriki Ligi Daraja la Nne wilayani humo kwa kosa la kufanya vurugu wakati ilipopambana na timu ya Ujamaa hivi karibuni.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi za TEFA, Katibu Msaidizi wa TEFA, Hassan Mpanjila alisema uamuzi huo ulitolewa katika kikao cha Waamuzi wa TEFA kilichofanyika Jumatano wiki hii ili iwe fundisho kwa timu zenye tabia kama hiyo ya kuwapiga waamuzi.

Alisema mbali na kulipa faini hiyo ya sh.50,000,vile vile timu hiyo imetakiwa kulipa vifaa vya Mwamuzi wa mechi hiyo vilivyopotea kutokana na vurugu hizo.

Aidha alisema kuwa endapo timu hiyo itashindwa kutekeleza amri hiyo hadi kufikia Mei 30 mwaka huu itaondolewa kabisa kwenye fainali hizo.

Wakati huo huo: Mashindano ya kugombea kombe la Yagga wilayani humo (Yagga Cup) yanategemewa kuanza Jumamosi hii katika viwanja vya Tandika Mabatini.

Mpanjila alisema kuwa mashindano hayo yanashirikisha timu zote za wilaya hiyo zilizopo Daraja la III na la IV.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza atapewa jezi 14 za juu na 14 za chini wa pili jezi 14 za juu ambapo mshindi wa tatu atajinyakulia mipira miwili na mshindi wa nne atazawadiwa mpira mmoja.

Maandalizi ya tamasha la pentekoste yazidi kupamba moto

Na. Dalphina Rubyema

MAANDALIZI ya Tamasha la Kwaya la Pentekoste Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam ambayo yanayoandaliwa na parokia ya Ukonga yanazidi kupamba moto ambapo kwaya za parokia mbalimbali zimethibitisha kushiriki.

Taarifa kutoka kwa Katibu wa Kamati ya Matangazo ya Tamasha hilo ,Aldo Mfinde zinasema kuwa hadi hivi sasa zaidi ya kwaya kumi zimekwisha rudisha majibu ya kukubali kushiriki tamasha hilo.

Alisema mbali na kwaya hizo ambazo hata hivyo hakuwa tayari kuzitaja kwa majina, watu binafsi nao pia wameanza kujitokeza kununua kadi ambazo zinauzwa katika parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Hata hivyo pamoja na maandalizi ya tamasha hilo kuonekana kupata mafanikio , Katibu huyo amewakumbusha waamini na wale wenye mapenzi mema kujitokeza zaidi kununua kadi hizo zinazouzwa kwa shilingi 10,000.

Aliyataja maeneo ambayo kadi ya hizo zinauzwa kuwa ni kwenye duka la Mtakatifu Yosefu ,parokiani Msimbazi, Chang’ombe, Yombo,Makuburi, Mwenge na kwenye parokia ya Ukonga yenyewe kwenye duka la WAWATA.

Mfinde vile vile alivikumbusha vikundi mbalimbali vya kwaya ambazo hazijarudisha fomu za kushiriki vifanye hivyo na tarehe ya mwisho ya kurudisha fomu hizo imesogezwa mbele badala ya Mei 15 mwaka huu itakuwa Mei 25 mwaka huu.