Make your own free website on Tripod.com

Michezo

Simba B kujitupa uwanjani na Everet

l TEFA yaifungia timu ya Kiburugwa kushiriki kwenye mashindano

Na Vick Peter

TIMU ya Soka ya Simba kikosi B ya Dar-Es-Salaam, leo inategemewa kupambana na timu ya soka ya Everet ya Temeke katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika katika viwanja vya Tandika Mabatini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu Mkuu wa Chama cha soka wilayani Temeke (TEFA) Abdallah Kitumbi alisema kuwa mchezo huo utakuwa na lengo la kupimana nguvu na kuinua viwango vya wachezaji.

Aidha, alisema pambano hilo litakuwa na kiingilio kidogo ambacho hakukitaja na kiasi cha pesa kitakachopatikana kitakuwa ni kwa ajili ya kuendeleza mchezo katika wilaya ya Temeke.TEFA yazuia Kiburugwa kucheza popote

Wakati huo huo: Chama cha Soka Wilayani Temeke (TEFA), kimeisimamisha timu ya soka Kiburugwa kushiriki mashindano yoyote ndani na nje ya wilaya hiyo kwa kosa la kumpiga mwamuzi, Said Ndyamkama kwenye fainali za Ligi Daraja la Nne wilayani humo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu Mkuu wa TEFA Abdallah Kitumbi, alisema tukio hilo lilitokea Januari 7 mwaka huu wakati timu hiyo ilipokuwa ikipambana na timu ya Soka ya Ujamaa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Antoni.

Alisema sababu ya kupigwa kwa mwamuzi huyo ni kuingia kwa goli la pili lililofungwa na timu ya Ujamaa na hivyo, kuifanya timu ya Kiburugwa kubaki nyuma kwa goli moja jambo ambalo halikuwafurahisha wachezaji wa timu hiyo walioamua kumshambulia mwamuzi huyo kwa madai kuwa anapendelea.

Katika mchezo huo, hadi kipindi cha kwanza kunamalizika, timu ya Kiburugwa ilikuwa inaongoza kwa goli moja. Kipindi cha pili, vijana wa Ujamaa walichachamaa na kurudisha goli hilo na kisha kuongeza goli la pili lililofungwa dakika za mwisho za kipindi cha pili.

Kutokana na tukio hilo Katibu wa Chama cha Soka Wilayani Temeke, ameiagiza Kamati ya Ufundi ya Chama hicho kukutana kuzungumzia suala hilo ili kupata uamuzi haraka iwezekanavyo.

Ligi Daraja la Tatu, Nne Ilala kuanza Juni

Na Getrude Madembwe

LIGI Soka Daraja la Tatu na Nne katika Manispaa ya Ilala, inatarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu.

Akizungumza na KIONGOZI katika ofisi za Chama cha Mpira wa Miguu katika Manispaa ya Ilala katikati ya juma, Afisa Mtendaji wa chama hicho, Daud Kanuti, alisema kuwa Ligi Daraja la Tatu itaanza Juni 5 na Daraja la Nne, itaanza Juni 19, mwaka huu.

Alisema kuwa katika Ligi Daraja la Tatu, takriban timu 38 zinatarajiwa kushiriki na wakati za daraja la Nne, zinatarajiwa kuwa kati ya 45 na 50.

Kanuti alisema kuwa katika michezo hiyo, timu 3 kutoka Daraja la Tatu, zitapanda hadi kufikia Ligi ya Kanda na timu 6 kutoka ligi hiyo, zitashushwa Daraja la Nne na timu nyingine 6 kutoka Daraja la Nne zitapanda hadi Daraja la Tatu.

Aidha, Kanuti alisema kuwa wataanza kutoa taarifa kwa vilabu husika ili waanze usajili wa timu hizo.

Alivitaja viwanja vitakavyotumika katika michezo hiyo kuwa ni pamoja na uwanja wa Magereza, Airwing, Chuo cha Magereza na Uwanja wa Karume endapo utakuwa haujaanza kukarabatiwa.

Juu ya gharama za ushiriki mashindano, Kanuti alisema, "Mwaka jana ada ilikuwa shilingi 21,000 kwa Ligi Daraja la Nne na shilingi 31,000 kwa Ligi Daraja la Tatu ikiwa ni pamoja na kadi pamoja na ada ya ushiriki sasa bado hatujapanga kama ada hiyo itapanda kupungua au kubakia hapo hapo."

Wakatoliki Dar kufanya Tamasha la Pentekoste

l KKKT walenga kukusanya milioni 2/=

Na Dalphina Rubyema

PAROKIA ya Ukonga katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, imeandaa Tamasha la Kwaya litakalofanyika Juni 3, Mwaka huu na kuzishirikisha kwaya zaidi ya 30 toka jimboni.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni, Katibu wa Kamati ya Matangazo ya Tamasha hilo linalojulikana kama Tamasha la Pentekoste, Aldo Mfide, alisema lengo la tamasha hilo, ni kuitukuza Siku Kuu ya Pentekoste.

"Tunatarajia kuwa na kwaya zaidi ya 30 walau kwaya moja moja kutoka kila parokia na mgeni rasmi, tunatarajia atakuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Saalaam au Msaidizi wake," alisema Mfinde.

Alisema, mbali na kulenga kuitukuza Siku Kuu ya Pentekoste, pia michango mbalimbali itakayopatikana wakati wa tamasha hilo, itatumika kununua vifaa mbalimbali vya kwaya za parokia hiyo ya Ukonga ambazo ni Kwaya ya Bikira Maria, Kristo Mfalame na Kwaya ya Mtakatifu Sesilia.

Aliongeza kuwa, watu binafsi watakaotaka kujumuika na wanakwaya hao wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, watatakiwa kununua kadi zinazouzwa kwa bei ya shilingi 10,000 na kwamba zinapatikana kwenye Duka la Vitabu la Jimbo Kuu lililopo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, parokiani Chang’ombe na duka la WAWATA parokiani Ukonga.

Pia, kutakuwepo na mnada wa vitu mbalimbali vilivyoandaliwa na parokia.

Aliwataka wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kununua kadi hizo kwani pamoja na kufaidika kimichezo, watapata huduma ya chakula na vinywaji.

Vile vile alizitaka kwaya mbalimbali kuthibitisha kushiriki tamasha hilo kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Naye Gabriel Mduma anaripoti kuwa; Umoja wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) Tanzania, Usharika wa Mburahati katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, umeandaa tamasha la ukusanyaji fedha kwa ajili ya kununulia vyombo vya muziki.

Katibu Mkuu wa Umoja huo, Joseph Mghamba alisema tamasha hilo la Mei 27, litafanyika usharikani hapo na kuzishirikisha kwaya 6 na wageni waalikwa zaidi ya 1500.

Alizitaja kwaya hizo za KKKT kuwa ni Kawe, Sayuni ya Kinondoni, Makongo, Magomeni, Mburahati na kwaya moja ya Kanisa la Anglikani la Mabibo.

Alisema Tamasha hilo la aina yake limekadiriwa kukusanya shilingi milioni 2 zikiwa ni mchanganyiko wa fedha taslimu na ahadi.

"Lengo letu ni kuburudisha katika ibada zetu kanisani, raha ya ibada itachangamshwa pindi tutakapofanikisha lengo letu hili,’ alisema Katibu huyona kuwataka waamini kujitokeza kwa wingi kulifanikisha.

Mghamba alisema karibu kwaya zote zimethibitisha kushiriki na kuwa barua maalumu za kuwaalika wageni mbalimbali zimesambazwa ambapo wageni kama Mawaziri na Wabunge nao pia wamealikwa.

Masista wawazawadia waimbaji sabuni

Na Vick Peter

KWAYA ya Mtakatifu Fransico Xaveri ya parokiani Chang’ombe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, mwanzoni mwa wiki iliyopita, imezawadiwa vitu mbalimbali mbalimbali zikiwemo sabuni kwa ajili ya kufulia sare.

Zawadi hizo zilifuatia kwaya hiyo kujitokeza kuwaburidisha kwa nyimbo, wagonjwa pamoja na wazee katika sikukuu yao iliyofanyika hivi karibuni parokani hapo.

Wakikabidhi zawadi hizo, masista wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli, walisema kuwa wameamua kufanya hivyo kama shukrani kwa kwaya hiyo kwa kuwa hawakutegemea na hivyo, kuwataka wanakwaya hao kuendelea na moyo huo wa kujitolea.

Masista hao walisema hawakuwa na kikubwa zaidi cha kuwapa zaidi ya zawadi hiyo waliyotoa kwao ambapo kila mwanakwaya alipewa mchi mmoja wa sabuni pamoja na kwaya kwa ujumla kupewa sabuni kwa ajili ya kufulia sare za kwaya hiyo.

Katika siku hiyo iliyohudhuriwa na wagonjwa pamoja na wazee kutoka katika dini na madhehebu mbalimbali, wagonjwa na wazee hao walionekana kufurahi na kupiga vigelegele kila kwaya hiyo ilipokuwa ikiimba na wao kuimba kwa kupaza sauti walipoona wimbo unaeleweka kwao.

Nyimbo zilizowafurahisha ni pamoja na wimbo usemao, "Tazama Tazama" ulioimbwa na Kwaya ya Mtakatifu Stephano, Chang’onbe na Bwana Alikuwa Tegemeo Langu ulioimbwa na kwaya ya Bugando Mwanza.

Wasanii wa TAUSI wakonga nyoyo za washabiki Dar

Na Joyce Joliga, TIME

WASANII wa kikundi cha Tausi cha Kenya ambao wapo hapa nchini kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Watoto Yatima wa mjini Arusha, Jumapili iliyopita walikonga mioyo ya mashabiki kutokana na umahiri wao wawapo jukwaani.

Baadhi ya mamia ya mashabiki waliofurika katika ukumbi huo wa Msimbazi Centre uliopo jijini Dar-Es-Salaam Jumapili iliyopita, wamewapongeza wasanii hao wa Kenya kwa umahiri wao waliouonesha wakati wakitoa burudani.

"Tumefurahishwa sana na waigizaji hao wa Kenya ingawa michezo yao ilikuwa ni mifupi mifupi lakini siyo siri, wametuburudisha sana na tunawakaribisha tena Tanzania watakapopata nafasi," walisema mashabiki hao.

Akizungumza jijini Dar-Es-Salaam, Mwenyeji wa wasanii hao Bw. Oddo Ndonde, alisema kuwa wasanii hao wapo nchini kwa ajili ya kuchangia mfuko wa watoto yatima wa mjini Arusha.

Pamoja na hayo Bw. Ndonde aliwaomba radhi mamia ya mashabiki hao waliofika ukumbini hapo kwa kuoneshwa michezo mifupi mifupi" alisema.

Wasanii hao wa kikundi cha Tausi wamewashukuru Watanzania kwa kujitokeza kwao kwa wingi na kwa ukarimu waliowaonesha. Wamewaasa Watanzania kuwapenda watoto yatima na kuwasaidia pale wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.