Mtibwa Sugar kuchapwa na Simba leo?

Na Mwandishi Wetu

Jumamosi hii katika Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro kutakuwa na kitendawili kitakachojibiwa baada ya kumalizika mchezo baina ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Soka ya Safari Lager , Mtibwa Sugar na Vigogo wa katika Kundi B la ligi hiyo, Simba.

Tayari klabu ya Simba imekwisha tamba kuwa inayo nafasi kubwa ya kuwanyuka hao wapinzani wao katika mchezo wa leo.

Wakati Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo amesema kuwa timu yake haitasita kugawa dozi nyingine itakazokutana nazo uso kwa uso, Mweka Hazina wake ametamba kuwa jijini Dar-Es-Salaam kuwa, bila kujali timu yake itacheza na klabu ipi ya soka ikiwamo Mtibwa Sugar, Simba inaendelea na mazoezi kama ilivyo ada.

"Sisi tunaendelea na mazoezi kama kawaida na Mtibwa tunaiona kama timu nyingine tu; kwa hiyo wala hatutabadili mfumo. Hivi sasa ushindi ni jadi yetu tu," alisema Mweka Hazina huyo, Jossiah Jackson.

Alisema ingawa Mtibwa walikataa kucheza katika uwanja wa Jamhuri kama walivyoombwa na Simba ili mapato, (simba) wamekubali kucheza katika uwanja wa Manungu.

Hata hivyo Jamhuri Kihwelo, aliisifia timu yake ya Simba kuwa inacheza kwa kuzingatia maagizo ya Kocha wake Mkuu, James Siang’a, raia wa Kenya.

Kutokuona hakuzuii kupiga muziki - Seven Blind Beats

Na Leocardia Moswery

MWENYEKITI wa bendi ya wasioona ya Seven Blind Beats ya jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Boniface Kinyese, amesema badala ya kuwashangaa, jamii iwasaidie kufanya mema wanayoyaona ya kuwasaidia katika fani yao ya muziki.

Bw. Kinyese alisema hayo jijini Dar-Es-salaam, katikati ya juma wakati akizungumza na KIONGOZI.

Alisema jamii haipaswi kukaa na kuwashangaa kwa kupiga muziki huku wakiwa hawaoni kwani kutokuona hakuzuii kupiga muziki.

Amesema ili kudhihirisha ukweli huo, watu wamekuwa wakipendezwa na muziki wanaoupiga licha ya hali yao ya kutokuona na kuongeza kuwa muziki wao unazingatia mandhari ya Kiafrika hususan Tanzania.

Bw. Kinyese alisema kulingana na mazingira ya Kitanzania katika upigaji muziki ili kuendesha shughuli zao, hupiga muziki kwa mtindo wa SIKUNGOZE, wenye maana kuwa, "sio vizuri kudharau ngoma zetu".

Bendi hiyo inayojiendesha kutokana na kukodishwa kupiga muziki katika shughuli mbalimbali, inao wanamuziki kumi, wawili kati yao, wakiwa wasichana.

Kati ya wana muziki hao kumi, watatu wanaona kidogo, na wanaobaki hawaoni kabisa.

Wanamuziki katika bendi hiyo ni pamoja na katibu wa Bendi, Bw. Robert Yohana, , Mark Kilumba, Raphael Noah na Kassim Juma.

Wengine ni Amir Abdalahman, ambaye anapiga dramu, Mbaraka Yusufu, Severina Elias na Alecksina Masesa; wanaopiga solo.

Mwenyekiti huyo wa bendi amewaomba wafadhili kuichangia bendi hiyo na kuisaidia kwa kuwa hivi sasa inakabiliwa na uhaba wa vifaa kama kipaza sauti, dramu, spika, miksa, mashine kubwa ya besi nakinanda.

Kwaya ya WAKIDA yaanza kuchapa kazi

Na Vick Peter

KWAYA ya Waimbaji wa Kilatini Dar-Es-Salaam, (WAKIDA), imeanza rasmi kazi yake ya kuwakumbusha waamini wake lugha hiyo kwa njia ya nyimbo.

Jumapili iliyopita, WAKIDA walianza kazi yao katika parokia ya Ubungo Msewe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Kwaya hiyo iliundwa mapema mwaka huu kwa nia ya kuhakikisha kwamba lugha ya Kilatini, inaendelea kutumika kama lugha ya Kanisa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na uongozi wa kwaya hiyo, kila mwaka WAKIDA itakuwa inazitembelea parokia nne na kuongoza ibada kama njia mojawapo ya kuwakumbusha waamini lugha hiyo.

Kabla ya kuundwa kwa kwaya hiyo, mmoja wa wahamasishaji wa uimbaji wa nyimbo za Kilatini, Peter Kapungu alimwomba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardianal Pengo, kusali pamoja na waimbaji pamoja na wapenzi wa lugha hiyo katika kila tarehe 26 ya Mwezi Desemba yaani, siku ya pili ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu. Lugha ya Kilatini ilikuwa ikitumika kama lugha Kuu ya Kanisa miaka ya nyuma hadi baada ya Mtaguzo Mkuu wa Pili wa Veterani lugha iliyopendekezwa kutumika kama lugha ya Kanisa ili kupanua uelewa wa waamini juu ya Neno la Mungu katika miaka ya 1960.

Ziara ya pili ya kwaya hiyo, inategemewa kufanyika Jumapili ya Kwanza baada ya Sikukuu ya Pasaka ya mwaka huu.

Nitamtoa Mbotswana raundi ya pili tu - Maneno

Na Mwandishi Wetu

BINGWA wa Ngumi wa Uzito wa Superwelter Afrika, anayetambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF), katika kanda ya Afrika, Maneno Oswald, amesema anajiandaa vikali kumtwanga MbotswanaThuso Khubamang, katika raundi ya pili itakayokuwa mwisho wake.

"Ninajua hata fika raundi ya pili na ikitokea akafika, asitegemee kuvuka hapo maana hivi sasa ninafanya mazoezi ya nguvu," alisema Maneno.

Maneno ambaye hivi sasa amepiga kambi na mabondia wengine akiwamo Abdallah Mohamed, Chaulembo Palasa, Rashid Ally na ramadhani miyeyusho wanaojiandaa kwa mapambano mbalimbali ndani na nje ya nchi, anatarajiwa kuwa na pambano na Khubamang wa Botswana, Machi 31, mwaka huu huko Gaborrone , Botswana.

Maneno alisema jijini kuwa ingawa hamjui mpinzani wake, lakini anaamini kabisa kuwa mtindo wa mchezo anaoutumia katika mchezo wake wa ndondi, utamsumbua sana.

Februari 4, Mwaka huu, bondia Maneno Oswald alimchapa rashid matumla ambaye ni Bingwa wa wa dunia anayetambulika na Umoja wa Ngumi Duniani(WBU).