Make your own free website on Tripod.com

Yanga yasema haina mpango wa kumsajili Malima

l Yadai ana maringo na dharau nyingi

l Yakiri kuwa beki mzuri

Na Gerald Kamia

KLABU ya Soka ya Yanga ya jijini Dar-Es-Salaam, imesema kuwa haina mpango wa kumsajili beki Bakari Malima kwa ajili ya ligi msimu huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkoani Morogoro wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Isack Shekiondo alisema kuwa klabu yake haiwezi kumsajili mchezaji huyo kufuatia vitendo vyake vya utovu wa nidhamu.

Shekiondo amesema kuwa Bakari ambaye alikuwa akisakata ndinga nje ya nchi,pamoja na uchezaji wake kuwa mzuri na wa kuridhisha , tatizo lake kubwa maringo ambapo amedai kuwa vitendo kama hivyo klabu yake haiwezi kuivumilia.

"Malima kweli ni beki mzuri na anacheza kwa nguvu , lakini tatizo kubwa la Malima ni dharau pamoja na kujiamulia mambo kwani anaweza kuondoka nje ya nchi bila ya ruhusa kutoka kwa viongozi wa klabu" alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo ameongeza kusema kuwa kutokana na kukamilika kwa kikosi cha timu hiyo msimu huu ,haoni sababu ya kuongeza mchezaji mwingine kwani kufanya hivyo ni kujiongezea mzigo.

Aidha Shekiondo amesema kuwa licha ya kufungiwa kwa beki wake Abubakari Kombo lakini klabu yake itamleta beki huyo na kumpa mahitaji kama wachezaji wengine wa klabu hiyo.

Mashindano ya Kombe la Parokia ya manzese kuanza Machi 12

Na Dalphina Rubyema

MASHINDANO ya kuwania Kombe la Parokia ya Manzese "Parokia ya Manzese Cup" yanatarajiwa kuanza Machi 12 mwaka huu ambapo timu mbalimbali za mpira wa mikono zinatarajiwa kushiriki.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye parokia hiyo ya Manzese iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar- Es -Salaam ,mashindano hayo yatafanyika kwenye viwanja vya parokia hiyo.

Lengo la mashindano hayo ni kuleta uelewano kati ya vijana wanaopenda michezo . "Tutafuata sheria za Netball zile zinazotambulika na CHANETA" inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyo sainiwa na katibu wa mashindano hayo, Azam Basil.

Taarifa hiyo inazidi kueleza kuwa kila timu itakayoshiriki michuano hiyo inatakiwa kutoa shilingi 5,000 kama ada ya ushiriki.

Moro United, Reli nani kuibuka Mkali?

Na Gerald Kamia, Morogoro

UWANJA wa Jamhuri uliopo mkoani Morogoro ,Jumapili hii utawaka moto pale wapinzani wa jadi timu za Moro United na timu ya Reli zitakapoumana vikali katika mfululizo wa michuano ya Ligi Kuu ya Safari Lager.

Mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na timu hizo mbili kukamuana vikali pindi zinapokutana na kufanya mashabiki wa soka mkoani hapa kushindwa kutabiri na nani ataibuka na ushindi katika mpambano huo.

Licha ya kufanya vibaya katika michezo yake miwili iliyopita ,timu ya Reli imesema kuwa haitafanya makosa tena katika mechi hiyo ya Jumapili.

Kocha wa timu hiyo, Joseph Sehaba amesema kuwa amesharekebisha makosa yote yaliyojitokeza katika mechi zilizopita na kuwataka mashabiki wa timu ya Reli mkoani hapa kutokuwa na wasiwasi wowote juu ya mechi hiyo.

Naye Kocha Mkuu wa timu ya Moro United inayojulikana kama ‘zaragosa’ Muhamed Msomali amesema kuwa ushindi kwa timu yake siku hiyo ya Jumapili ni lazima kwani haoni kipingamizi chochote cha kuizuia timu hiyo isitoke na ushindi.

"Tunatarajia kushusha kikosi cha mauaji ambacho tutahakikisha tunatwaa pointi tatu kama tulivyotwaa katika timu nyingine ,vijana wamejiandaa vizuri na wameahidi kutoka na ushindi mnono siku ya Jumapili’ alisema Msomali.

Mkataba wa TPBC, ISPM wakwama

Na Josephat Kiboga

KUSAINI kwa mkataba wa mamilioni ya fedha kwa mabondia wawili wa kulipwa nchini ambao ulikuwa ufanyike wiki ijayo umekwama kufuatia kujiuzulu kwa Rais wa Tume ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBC) Onesmo Ngowi ambaye alitarajiwa awe mgeni rasmi.

Mkataba huo ni kati ya Kampuni mpya ya International Promotions Management (ISPM) ya jijini na mabondia Magoma Shabani wa uzito wa Jr Bantam Weight, na Bingwa wa Afrika IBF katika uzito wa Super Welter Weight Maneno Oswald.

Habari kutoka ndani ya TPBC ambazo zimethibitishwa na kiongozi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini zinasema kuwa kujiuzulu kwa Ngowi kumekwamisha zoezi hilo la kusaini mkataba kwani itabadili TPBC ikae na kupendekeza upya jina la mgeni rasmi.

Mikataba hiyo ya miaka mitatu itamuwezesha kila bondia kujipatia zaidi ya shilingi milioni 20 kwa mwaka.

Sherehe za kusaini mkataba huo zilitarajiwa kufanyika katika hoteli ya Sheraton iliyopo jijini Dar -Es -Salaam.