BAADA YA TARIMBA KUPIGWA CHUPA...

Yanga sasa kulipiza kisasi?

Na Mwandishi Wetu

KUFUATIA Mwenyekiti wa Yanga kupigwa chupa usoni, baadhi ya washabiki wa timu hiyo wamesema watalipiza kisasi kwa kuwa wanaamini kitendo hichi kimefanywa na mashabiki wa klabu ya soka ya Simba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar-Es-Salaam mwishoni mwa juma, baadhi ya mashabiki wa Yanga walisema wanaamini kupigwa chupa kwa Tarimba kulikomsababishia jeraha na kupelekwa hospitali, ni njama ya washabiki wa Simba.

"Tunajua chuki za simba wamezihamishia kwa yanga baada ya kufungwa na Toto Afrika," alisema shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Gweso Mkami, mkazi wa Temeke.

Tukio la kupigwa kwa Tarimba lilitokea Jumatano katika Uwanja wa Taifa jijini Dar-Es-salaam, baada ya mchezo baina ya klabu ya Simba ya Dar. na Toto Afrika ya jijini Mwanza.

Shabiki mwingine wa kike aliyejitambulisha kwa jina la Stumai, mkazi wa magomeni jijini, alisema anashangaa badala ya kukasirikia timu iliyowafunga Simba(Toto Afrika), washabiki wa Simba wanaanza kurusha chupa ambazo licha ya kumpiga Tarimba, hazifuti mabao waliyofungwa.

" Hivi wanafikiri kumpiga Tarimba ndilo dawa la timu yao kucheza vizuri! Sasa kila timu ikitaka kulipiza kisasi tutafika wapi?" alihoji kwa mshangao.

Mmoja wa mashabiki ambaye alizungumza bila kujua kuwa kuna mwandishi wa habari na kisha kukataa kuzungumza na mwandishi maeneo ya Shule ya Uhuru, alisikika akisema kuwa lazima washabiki wa yanga nao walipize kisasi dhidi ya Simba.

Tarimba alipigwa na chupa usoni wakati akitoka katika Uwanja wa taifa kupitia lango kuu la jukwaa kuu uwanjani hapo. Ilikuwa baada ya kumaliza mechi baina ya klabu za Simba na Toto Afrika katika Ligi Kuu ya Safari lager.

Hata hivyo, washabiki wengi wa sokajijini dar-Es-salaam, wameiponda mikakati ya kulipiza visasi kwa washabiki na wachezaji wakidai vitendo hivyo ni vya kipuuzi na havisaidii kwa lolote, soka la Tanzania.

Wanawake wajitokeza kugombea CHANEta

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Netiboli katika wilaya ya Kinondoni (CHANETA), kimesema tayari baadhi ya wanawake wamejitokeza kuchukua fomu ili kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Habari zilizopatikana jijini Dar-Es-Salaam, mwishoni mwa juma, zilisema wanawake wapatao 20, tayari walikuwa wamekwisha chukua fomu hizo hadi Ijumaa.

Zilisema hadi siku hiyo fomu kumi zilikuwa tayari zimekwisha rejeshwa.

Kwa mujibu wa habari hizo, waliorudisha fomu hizo ni ni Rehema Kisandu anayewania nafasi ya Mwenyekiti, Elizabeth Majori anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mjumbe, pamoja na Halima Kombo anayesaka nafasi za Ukatibu Msaidizi na Ujumbe.

Wengine ni Victor Roma anayetaka kuwania nafasi ya Mweka Hazina, Janeth Raymond na Ujumbe. Wengine katika nafasi hiyo ni Grace Kitunda, Judith Wilbert, Efelo Mfuni, Azama Bilali na Corona Shilinde.

Habari hizo zimewataja ambao hadi Ijumaa walikuwa hawajarudisha fomu kuwa ni

ni Shida Ngweho, Nyaso Mzee, Getrude Kachenje, Mariam Masebo, Pili Abdallah na Getrude Madembwe.

Wengine waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho na hawajarudisha fomu ni Helen Kantange, Mary Kinyonya, Zetty Kisatu, G. Biyabatu na Laura Komba.

Kamati ya FAT kusambaza rasimu mikoani

Na. Pelagia Gasper

KAMATI ya Mseto ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), imesema rasimu ya katiba mpya ya FAT itakamilika mwishoni mwa mwezi huu na kusambazwa katika vyama mbalimbali vya soka mikoani.

Katibu Mkuu wa kamati hiyo, Ismail Aden Rage, alisema ofisini kwake mwishoni mwa juma katika mazungumzo na mwandishi wa habari kuwa, bado wanafanya uchambuzi wa katiba za nchi nyingine tano zilizo Kusini mwa Tanzania na kwamba zoezi hilo linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

"Mwishoni mwa mwezi huu, tunatarajia kuwa tumekamilisha rasimu na Julai, itaanza kusambazwa kwa wajumbe wote nchini na kwa vyombo husika vya soka ili navyo, vitoe maoni ya nyongeza na kubaini mapungufu," alisema.

Alizitaja nchi ambazo FAT inapitia katiba zao kuwa ni Malawi, Botswana, Zimbabwe, Zambia na Namibia.

Alisema chama hicho kitakachoundwa, kitawajibika kwa mujibu wa sheria za nchi, kuheshimu sheria zote zinazopitishwa na Bunge na kuzingatia kanuni za FIFA katika maswala mbalimbali ya soka.

Wakati huo huo: Raundi ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa ya Taifa ya Mpira wa Wavu inatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Dar-Es-Salaam kutoka tarehe itakayopangwa siku za baadaye.

Katika mchezo wa mwisho juma lililopita, Jitegemee iliinyuka Ruaha kwa seti 3-0 na J.K.T Wanaume, ilichalaza Jitegemee kwa seti 3-0.

Katika awamu ya kwanza, timu za Jeshi Stars, Jitegemee na J.K.T, zote za Wanawake na Wanaume, zilitia fora huku wenyeji Ruaha Wanawake na Wanaume Mgololo na K.K.K.T zikisuasua.

Timu zilizoshiriki awamu hiyo ya kwanza kwa upande wa wanaume ni mabingwa, Jeshi Stars, Ruaha, J.K.T, K.K.K.T ya Moshi, Mgololo na Jitegemee na kwa upande wa wanawake, ni mabingwa Jeshi Stars, J.K.T, Jitegemee na Ruaha.