Usajili Yanga utakuwa bora mwaka huu - Shungu

Na Leonard Magumba

TIMU ya Soka ya Yanga ya jijini Dar-Es-Salaam, imepania zaidi kuboresha usajili wa wachezaji wake msimu huu, baada ya kusajili wachezaji wake kibao toka Simba pamoja na mmoja toka Express ya Uganda.

Kwa mujibu wa mkuu wa klabu hiyo Roul Shungu kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, klabu hiyo imepania kuwa na usajili mzuri zaidi msimu huu wa Ligi Kuu hapa nchini.

"Tunataka kuwa na kikosi safi kipindi hiki cha Ligi Kuu ya Mwaka 2001 kama ilivyo kawaida ya Yanga na bado ninaangalia baadhi ya wachezaji wazuri," alisema.

Klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani, ina mipango ya kumsajili kiungo toka klabu ya soka ya Express ya Uganda, Yembe Serge, ambaye hivi karibuni amekuwa akionekana katika mazoezi ya timu hiyo na majuzi kuonesha kiwango cha juu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Kipanga.

Baadhi ya wachezaji wanaotegemewa kusajiliwa na timu hiyo na majuzi walionekana katika mechi dhidi ya Kipanga na kuonesha mchezo mzuri ni Peter Mbuta, Doyi Monke, Shauri Idd, Khalid Ngome, Haruna Moshi, Mwanamtwa Kiwelo pamoja na Bashiru Husseni, nduguye Mohamed Hussein (Mmachinga).

"Huyu Yembe Senge, ni mchezaji safi na bado namfanyia practice (mazoezi) ili niweze kufahamu vizuri kiwango chake maana ana muda wa wiki tatu sasa toka aje toka Uganda," alisema Shungu.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara inategemea kuanza mwezi Februari mwaka huu na inategemewa kuwa ya kusisimua kutokana na timu zinazoshiriki kujitayarisha vilivyo katika zoezi la usajili.

Maradona kurudi Napoli?

ROME,Italia

GIORGIO Corbelli, anayemiliki timu ya soka ya Napoli, ya Italia, amesema anataka kumrejesha Mchezaji nyota katika ulimwengu wa soka nchini Argentina, Diego Maradona katika klabu hiyo iliyompatia umaarufu miaka ya nyuma.

Alisema uvumi kuwa Maradona atapewa nafasi ya kuwa Meneja Mkuu wa klabu ya Napoli, hauna maana kwa kuwa hawezi kuiweka timu hiyo kuwa chini ya uangalizi wa mtu ambaye hana uzoefu huo.

Katika msimu uliopita, Corbelli alinunua hisa nyingi katika klabu ya Napoli. Pia ni mshirika wa Corrado Ferlaino.

Katika kipindi cha mwezi uliopita, Corbelli amezungumza na Maradona juu ya mkataba huo mpya.

Alisema ana matumaini ya kukutana na Maradona Jumamosi hii.

Mwanasoka, Maradona mwenye umri wa miaka arobaini, aliondoka Napoli mwaka 1991 baada ya kushindwa kuelewana na uongozi wa kalbu hiyo.

Maradona bado ni kipenzi cha wanasoka mashabiki wa klabu ya Napoli, licha ya mapambano yake na matumizi ya madawa ya kulevya aina ya cocaine.

Wapenzi wa Netiboli watakiwa kuufufua

Na Leocardia Moswery

WAPENZI wa mchezo wa pete (Netball), wameombwa kuchangia kwa hali na mali ili kufufua mchezo huo ambao umefifia kiasi cha kutisha kutokana na mashirika wafadhili kushindwa kumudu gharama za wachezaji.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na mjumbe wa kamati ya netiboli wilayani Temeke

Hassan Mpanjilla, alipozungumza na gazeti hili.

Mpanjila ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani Temeke(TEFA), alisema, "mpira wa pete uliokuwapo siku za nyuma na tena, wapenzi wake walikuwa wengi mno, haswa ikiwepo timu ya Bandari ambayo ndiyo ilikuwa kivutio sana kwa jamii. Hali hiyo ni tofauti na ilivyo sasa. Mchezo huu umedorora kupita kiasi".

Mpanjilla alisema kuwa sababu ya kudorora kwa mchezo huo, ni mashirika mengi yanayofadhili mchezo huo ambapo sasa hivi yameshindwa kumudu gharama.

"Mpira wa pete umedorora sana kwa sababu ya mashirika kushindwa kumudu gharama za wachezaji," alisema.

Amesema kuwa mpira huo utakapotiliwa mkazo, utawasaidia washiriki katika kuweka vizuri afya zao kwa kuepuka kupata magonjwa ovyo, kuimarisha mahusiano na kuongeza vipato vyao.

FRAD yawasimamisha waamuzi wanne

Na Getrude Madembwe

CHAMA Cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Dar-Es-Salaam (FRAD), kimewafungia kwa muda usiojulikana, waamuzi wanne wilayani Kinondoni kwa kosa la kuchezesha mchezo wa Lucky Rangers Club.

Kwa mujibu wa barua ya FRAD ya Januari 3, mwaka huu kwa waamuzi waliosimamishwa, waamuzi hao walikiuka agizo la chama hicho la kuwataka waamuzi wa mkoa huu (Dar-Es-Salaam), kutochezesha michezo hiyo.

"Kikao cha dharura cha kamati ya Utendaji ya Mkoa FRAD, kilichofanyika tarehe 02/01/2001, kimeagiza ufanye yafuatayo, utoe maelezo kwanini wewe binafsi ulipinga agizo la chama cha waamuzi mkoa FRAD, ambacho Kilisisitiza kuwa waamuzi wa mkoa huu wa Dar-Es-Salaam, kutochesha michezo hiyo ya Lucky Rangers Sports Club" inasema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na kaimu Katibu Mkuu wa FRAD, Ruvu Kiwanga.

Barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa Makatibu Wakuu wa DRFA, KIFRA, KIFA na Lucky Rangers Sports Club, imeataka waliosimamishwa kujieleza ndani ya siku saba hadi Januari 10, mwaka huu.

Waamuzi waliosimamishwa ni Christopher E. Kapera, wa Daraja la Kwanza, Michael J. Malama wa daraja la pili, China Kabala na Ambwene Mwekizega, wote wa daraja la tatu

Wakati huohuo: Chama hicho wilaya ya Kinondoni, Jumapili hii kinatarajia kupitia katiba yake.

Katibu wa Chama hicho, Bw. Beni Mtura, wanahitaji kupitia katiba hiyo kwa pamoja na wajumbe wengine na kumshirikisha kiongozi mmoja wa KIFA ili kuona uwezekanao wa kukisajili chama hicho rasmi.