Vyama vya michezo havizuii BMT, BMZ kufanya kazi - Msajili

Na Dalphina Rubyema

MSAJILI wa Vyama vya Michezo nchini, Leonard Thadeo, amesema kuwa utaratibu unaowekwa na vyama vya Michezo hauizuii Baraza la Michezo Tanzania(BMT) na Baraza la Michezo Zanzibar(BMZ) kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

Msajili ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya wapenzi wa michezo kudai kuwa utaratibu wa kuchukua fomu za kugombea uongozi wa kamati ya Olympic Tanzania (TOC), umekiuka taratibu za BMT na BMZ.

Katika utaratibu wake, TOC ilitoa ufafanuzi mzima wa namna ya kuchukuwa fomu na kuzirudisha na jinsi wao(TOC) watakavyoziwasilisha BMT na BMZ.

"Kimsingi vyama vyote vya michezo havizuiliwi kujiwekea utaratibu huo kama ilivyofanyika TOC lakini, pia hatua hiyo haizuii BMT na BMZ kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni za sheria zilizopo," alisema katika mzungumzo na Kiongozi jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni.

Aliongeza, "Vyama vya michezo vinaweza kuweka utaratibu wake ili mradi havikiuki kanuni na sheria zilizopo nchini".

Hata hivyo Leonard alisema kuwa tayari TOC imekwisha pewa maelekezo yanayohusu marekebisho ya katiba yao na kwamba, uchunguzi wake utafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo na si vinginevyo.

Kwa mujibu wa TOC, uchaguzi huo utafanyika Februari 25 mwaka huu mjini Morogoro.

Timu 16 kushiriki Nje Cup

lZimo pia za Kenya na Uganda

Na Dalphina Rubyema

JUMLA ya timu 16 zikiwemo mbili kutoka Kenya na Uganda, zinatarajiwa kushiriki michezo ya Nje Cup itakayoanza Machi 10-16, mwaka huu katika Uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake katikati ya wiki, Katibu wa michuano hiyo inayoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ramadhani Sakulu, alisema kuwa tayari ofisini yake imekwisha tuma barua za mwaliko wa timu hizo.

Alizitaja timu hizo zinazotarajiwa kuwa ni TELCOM ya Kenya, NIC ya Uganda, Chipukizi ya Zanzibar na Polisi ya Dar-Es-Salaam.

Nyingine ni Bandari, Jeshi Star, JKT Mbweni, Polisi(Ruvuma), Polisi(Arusha), JKU (Zanzibar), Bandari, Zanzibar Mapinduzi(Dodoma), Reli(Morogoro), Jitegemee, Ulinzi na Jeshi la Zanzibar.

Alisema kuwa hadi hivi sasa timu za Polisi Ruvuma, Jeshi Star ya Dar-Es-Salaam, na JKU ya Zanzibar, ndizo zimekwishathibitisha kushiriki michuano hiyo.

Timu ambazo hazijathibitisha kushiriki kwake zimekumbushwa kufanya hivyo mapema ili kufanikisha maandalizi ya michuano hiyo.

"Mwisho wa kudhibitisha ni Machi 1,2001. kwa wale wote walioandikiwa barua za mialiko, wathibitishe mapema kwa maandishi ili tukamilishe maandalizi yetu kwani kuchelewa kuthibitisha, kunachelewesha maandalizi," alisema.

Mbali na mshindi wa kwanza hadi wa tatu katika michuano hiyo kupewa zawadi ya vikombe, pia kutakuwa na zawadi nyingine ambazo bado hazijafahamika vizuri.

Mwaka jana michuano hiyo iliyofanyika Zanzibar na timu ya NIC ya Uganda iliibuka bingwa.

Kwaya ya Watakatifu Wote yapata Nahodha wapya

Na Mwandishi Wetu

KIKUNDI cha kwaya ya Watakatifu Wote ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kimepata nahodha wapya, watakaoongoza kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Katika Uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEC, eneo la Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, na kusimamiwa na Bradha Andrew Chimesella, na Padre Elias Msemwa, Bw. Dismas Samballa, aliibuka mshindi na kushika nafasi ya uenyekiti.

Meneja wa kituo cha TEC, maarufu kama Senta, Sista Flora Chuma, alishika nafasi ya makamu Mwenyekiti wakati Bradha jacob Msungu anakuwa katibu wa kwaya hiyo akisaidiwa na Bw. Mathias. Mtunza hazina ni Bi. Teddy Mlavilla.

Padre Msemwa ambaye ni 'Paroko' wa TEC, alitoa wito kwa viongozi hao wapya kutoa na kupokea ushirikiano toka kwa wanakwaya wao, ili kutumia kipaji chao cha uimbaji kwa kuburudisha na kuinjilisha jamii.

Naye Vick Peter anaripoti kuwa, Kwaya za Kikatoliki zimetakiwa kutafuta njia rahisi ya kujipatia pesa na kuacha kutegemea misaada kutoka kwa wahisani.

Akizungumza na wanakwaya mbalimbali katika tamasha lililofanyika Jumapili iliyopita katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar-Es-Salaam, Paroko wa Parokia ya Ukonga katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Stephano Nyilawila, alisema wanakwaya hawanabudi kutambua kuwa hata kama watajaribu, si rahisi wahisani wakasaidia kwa kila analohitaji mtu(kwaya).

Padre Nyilawila aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, alisema kuwa mhisani anaangalia kwanza juhudi zako ndipo ajue atakusaidia vipi kwani hawezi kukusaidia huku akijua una uwezo wa kujisaidia mwenyewe.

Aliendelea kuwa, njia za kujipatia pesa kwa vikundi vya kwaya ni nyingi ikiwemo kuandaa matamasha kwa ajili ya kuchangishana wenyewe kwa wenyewe.

"kwaya zetu za Kikatoliki zitaendelea kuwa za kimaskini endapo sisi wenyewe hatutajishughulisha," alisema.

Tamasha hilo lilikuwa ni kwa ajili ya kuchangia mfuko wa kwaya ya Mtakatifu Stephano, iliyopo katika parokia ya Chang’ombe.

Lewis kutetea mikanda Afrika Kusini

LONDON,Uingereza

BINGWA mtetezi wa WBC na IBF, mwanandondi Lewis, ana kitendawili kikubwa cha kama atafanikiwa kutetea mikanda yake katika uzito wa juu katika pambano lake na Hasim Rahman, linalotarajiwa kufanyika, Johannesburg, Afrika Kusini.

Meneja wa Lewis, Frank Maloney, amethibitisha kufanyika kwa pambano hilo Aprili 21, mwaka huu huko Johannesburg na wala si Las Vegas.

Hali hiyo inampa Lewis, upinzani toka kwa Promota wa mchezo huu wa ngumi, Panos Eliades, anayetaka kulipwa fidia ya Dola milioni 2.5 toka kwa Lewis.

Lewis amekwisha ilalamikia hatua hiyo katika Bodi ya Ngumi ya Uingereza.

Meloney alisema pambano hilo la ndani litafanyika nyakati za asubuhi ili kuviwezesha vituo vya televisheni vya Marekani kulionesha moja kwa moja.

Rais wa HBO Sports, Ross Greenburg, alisema mjini NewYork kuwa, "Iwapo pambano hilo litafanyika Afrika Kusini kama lilivyopangwa, litaoneshwa moja kwa moja.

Greenburg aliyekuwa Afrika Kusini hivi karibuni kwa ajili ya maandalizi, aliongeza, "pambano hilo litafanyika nje kidogo ya Johannesburg, Carnival City." alisema tatizo kubwa litakalolikumba pambano hilo, ni kufanyika futi 1000 toka usawa wa bahari.

Tumieni ritungu, zeze kuimarisha koo- Dc

Na Chistopher Gamaina, Tarime

MKUU wa Wilaya ya Tarime Bw. Paschal K. Mabiti, ameyahimiza mabaraza ya jadi wilayani hapa, kutumia michezo ya asili kama ngoma, ritungu na zeze, kuimarisha mahusiano baina ya koo na koo za Wakurya.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika semina ya siku moja ya walinzi na mabaraza ya jadi katika tarafa ya Inchungu. Semina hiyo iliyofanyika katika shule ya msingi Sirari.

Alisema jamii haina budi kuzingatia umuhimu wa kushiriki michezo mbalimbali ikiwamo ya kijadi kama zeze na ritungu ili kuimarisha urafiki na kuchochea ushirikiano katika kutatua matatizo baina ya koo za Kikurya.

Alisema hali ya kushiriki michezo baada ya kazi, pia itachangia kuwaondolea vijana, muda na mawazo ya kufikiri na hata kujihusisha katika michezo mibaya ikiwamo kamali na "karata tatu" na pia, kushiriki vitendo vya uhalifu kama wizi.

"Muwe na ushirikiano katika shughuli za michezo na burudani. Hii itasaidia sana umoja kati yenu na kujenga urafiki kati ya ukoo huu na huu," alisema.

Licha ya kuimarisha urafiki na mahusiano, michezo mbalimbali ikiwamo ya asili, mpira, riadha na mitupo, huweka mwili katika hali ya ukakamavu, kulinda afya pamoja na kuongeza kipato.