Make your own free website on Tripod.com

Nitalipeleka soka la Tanzania nje ya nchi - Mgombea FAT

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA mmoja wa nafsi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Nchini (FAT), amesema endapio atachaguliwa kushika nafasi hiyo, atahakikisha soka la Tanzania linafahamika hadi nje ya nchi kwa ubora wake.

Ramadhani Ahungu ambaye ni mgombea wa sita katika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu wa FAT, alisema alipokabidhiwa fomu ya kugombea na Ofisa wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Julian Matagi kuwa, lengo la kuwania nafasi hiyo nyeti ni kulinusuru soka la Tanzania.

Alisema soka la nchini limekuwa likidorarora kila mwaka na hivyo, anakusudia kuiondoa hali hiyo.

Ramadhani Ahungu aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Muda ya FAT baada ya aliyekuwa Waziri wa Michezo na Utamadauni Profesa Juma Kapuya, kumteua kutokana na aliyekuwa Mwenyekiti Muhidin Ndolanga kusimamisha uchaguzi wa FAT mahakamani akipinga kufutwa jina lake.

Kwa sasa nafasi ya Katibu Mkuu wa FAT inashikiliwa na Ismail Aden Rage, tangu alipochaguliwa mwaka 1996.

Hadi tunakwenda mitamboni, nafasi hiyo ilikuwa ikigombewa na Ally Hassan Mwanakatwe, Azim Dewji, Kadata S. Kadata, Machael Wambura na Ismail Aden Rage mwenyewe.

Hadi Alhamisi iliyopita, wagombea 63 walikuwa wamekwisha jitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho.

Uchaguzi wa FAT unatarajiwa kufanyika Desemba 31, mwaka huu mjini Arusha ambapo mwisho wa kurudisha fomu ni Desemba 24 na usaili utafanyika Desemba 27. Majina yatatangazwa Desemba 28, mwaka huu.

Ngumi baina ya Tyson, Lewis mashakani

NEW-YORK, Marekani

BAADA ya Bondia Mike Tyson kumtwanga makonde bondia wa zamani, Mitchell Rose, pambano la ndondi baina yake na Lennox Lewis, liko mashakani kutokana na bondia huyo kuchunguzwa na polisi.

Pambano hilo la ngumi za uzito wa juu, lilipangwa kufanyika Aprili mwaka ujao.

Kuna madai kuwa Desemba 16, mwaka huu, Tyson ambaye ni binwa wa zamani wa uzito wa juu duniani alimchapa ngumi hadi kumuangusha chini bondia wa zamani, Mitchell Rose wakiwa nje ya klabu ya usiku Mjini Newyork. Kuna habari kuwa polsi wanayafanyia uchunguzi madai hayo.

Mmoja wa wanasheria wa Tyson, Darrow Soll, amethibitisha kuzungumza na wapelezi wa polisi.

"Tumefanya kazi na maofisa wa polisi, tumefanya mahojiano na mashahidi na tuhuma hizo haziungwi mkono kabisa," alisema Soll wakati akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

Bondia Mike Tyson ambaye yuko katika pilikapilika za kutafuta kibali cha Jimbo la Nevada ili kupigana na Lewis Aprili mwakani, hana leseni ya kupigana nchini Marekani.

Kuna habari kuwa Tyson anakabiliwa pia na kikwazo kingine katika kupigana na Lewis kwani uwezo wa Promota Don King ambaye anadaiwa kumshawishi Tyson kwa dili la Paundi Milioni 60 kwa mapambano sita iwapo Tyson atakaubali kuanza kupigana na bingwa wa Chama cha cha Ngumi Duniani (WBA) John Ruiz.

Dk. Remmy awakandia wanamuziki wa Tanzania

lAsema miziki yao ni ya kitoto

Na Dalphina Rubyema

MUZIKI inayopigwa na baadhi ya wanamuziki wa hapa nchini imeelezwa kuwa ni ya kitotona isiyokuwa na ujumbe wowote katika kuielimisha jamii.

Kauli hiyo imetolewa na mwanamuziki mkongwe nchini, Dk. Remmy Ongala, wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake eneo la Sinza jijini Dar es Salaam.

Remmy alisema kuwa muziki inayopigwa ni ya kitoto na haina ujumbe wowote hali inayofanya chati ya muziki hapa nchini kushuka.

"Mwanamuziki unatuimbia nyimbo zenye maneno ya kitoto, unakuta watoto wanacheza na wewe unakariri maneno kuja kutuimbia sasa hapo unajenga nini!" Remmy aliuliza kwa mshangao.

Alitoa wito kwa wanamuziki wote nchini kutunga na kuimba nyimbo zinazotoa mafunzo kwa jamii badala ya kukalia kile alicho kiita utoto.

Hata hivyo mwana muziki huyo mkongwe ambaye kwa hivi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi, aliwasifia baadhi ya wanamuziki ambao alisema kidogo wanajitahidi kufikisha ujumbe unaotakiwa kwa jamii.

"Siyo kwamba wana muziki wote ni mambumbumbu, kuna wengine wanajitahidi kwa kiasi fulani kufikisha ujumbe mzuri kwa jamii," alisema Remmy bila kutaja majina na bendi za wanamuziki hao.

KALLY ONGALA: Sina mpango kucheza soka nchini

Na Anthony Ngonyani

ALIYEKUWA mshambuliaji hatari wa klabu ya soka Yanga, Kalimangonga(Kally) Ongala, amesema hana mpango wa kucheza soka hapa nchini na kwamba amewasili kwa ajili ya mapumziko.

Akizungumza jijini Dar-es-Salaam muda mfupi baada ya kuwasili nchini hivi karibuni Kally alisema tayari ameanza majaribio katika timu ya Portsmouth ya England ambayo iko daraja la kwanza.

Alisema kutokana na hali hiyo, hana mpango wowote wa kucheza soka hapa nchini.

Na kwamba amekuja kwa ajili ya mapumziko na familia yake na kisha atarejea England.

Kally aliongeza kuwa, tayari ameishaanza majaribio katika timu hiyo ya England inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

Alidokeza kuwa, kwa kuwa timu hiyo ndiyo inamgharimia kwa mambo yote yakiwamo malazi, chakula na huduma za afya, hayupo tayari kujisajili na timu nyingine zikiwamo za hapa nchini.

Mshambuliaji huyo aliyechipukia katika timu ya Daraja la Tatu, ya Abajalo ya jijini Dar es Salaam.

Wakati akifanya majaribio katika timu ya Bradford City, Kally alibahatika kuichezea timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Manchester City, Sheffield, Wednesday na Newcastle United.

Kally aliongeza kuwa, wakati akiichea Bradford city aliumia kifundo cha mguu na akalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Kally alisema sasa amepona na yupo katika hali nzuri ya kucheza soka.

Imbeni nyimbo zinazoeleweka - Askofu

Na Mwandishi Wetu, Rulenge

KANISA Katoliki katika Jimbo la Rulenge, limevitaka vikundi vya kwaya makanisani kuimba nyimbo zinazoeleweka kwa waamini ili waende sambamba na ibada.

Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Severine NiweMugizi, alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati wa Ibada ya Jumapili ya Pili ya Majilio iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili, Mhashamu NiweMugizi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alitoa rai hiyo baada ya waimbaji katika misa hiyo kuimba nyimbo ambazo waamini wengine hawakuzielewa na hivyo, kuifanya misa kupoteza sehemu ya uhai.

Akinukuu Mtaguso wa Pili wa Vatikano katika Hati ya Litururujia juu ya Neno la Mungu (Sacrosanctum Concilium) namba 30, inayoongelea kushiriki kikamilifu kwa waamini.

Mhashamu NiweMugizi alisema kwaya hazina budi kuhakikisha kuwa zinaimba nyimbo zinazofahamika kwa waamini ili waende sambamba na ibada.

Alisema, juhudi za makusudi pia hazina budi kufanyika ili kuwafundisha waamii nyimbo mpya kabla ya kuziimba kanisani ili waamini washiriki ibada kikamilifu.

"Kwaya kwa ajili ya kuboresha ibada na kuwafanya waamini waweze kusali mara mbili. Si lengo la Kanisa kuruhusu kwaya kanisani ili zifanye maonesho na kuwafanya waamini kuwa watazamaji au wasikilizaji tu," alisema.

Alisisitiza kuwa ni lazima waamini waimbe katika ibada na kwamba, kwaya hiyo ipo ili iwaongoze waamini kuimba na si vinginevyo.