Michezo

Mtibwa Sugar itatamba Ethiopia Jumapili?

Na Mwandishi Wetu

WASHABIKI wa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar na wengine nchini, wako tumbo joto wakihaha kusubiri timu hiyo kuibuka na ushindi katika pambano lake na EELPA ya Ethiopia

Timu ya Mtibwa Sugar, mwishoni mwa juma lililopita, iliondoka kwenda nchini Ethiopia kwa ajili ya pambano la marudiano katika Kombe la CAF ambapo Jumapili hii inapambana na klabu hiyo wenyeji.

Timu hiyo imesema licha ya kutokuwa na michezo kadha ya majaribio, lakini bado inatarajia kupata ushindi na hivyo mashabiki wake wasi hofu kitu

Hata hivyo, alipokuwa akizungumza jijini Dar-Es-Salaam, Mratibu wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro, Jamal Bayser alisema timu yake haikupenda kuwahi kwenda nchini Ethiopia kwani ingeweza kufanyiwa hujuma mbalimbali.

Aliongeza kuwa sababu nyingine ya kutowahi zaidi ilikuwa walimu kukamilisha ufundishaji wa timu.

Katika mchezo wa hivi karibuni baina ya vilabu hivyo uliofanyika hivi karibuni mjini Morogoro, Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mtibwa inahitaji kutoka sare au kuibuka na ushindi ili isonge mbele.

Habari za kuaminika zilizopatikana jijini jana, zilisema viongozi walio katika safari ya Ethiopia pamoja na timu yao ni pamoja na makocha wa timu; Roul Shungu na John Simkoko.

The Daban yaandaa pambano la ngumi

Na Dalphina Rubyema

THE Daban Camp Promotion ya jijini Dar-Es-Salaam imeandaa pambano la ngumi litakalofanyika Aprili 16 mwaka huu katika ukumbi wa Friends Corner jijini Dar-Es-Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya maandalizi wa pambano hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa vile siyo msemaji, mabondia wanaopigana uzito mbalimbali watapambanishwa.

Aliwataja mabondia hao kuwa ni Ramadhani Ally (Miyeyusho) atakaye pambana na Kassim Kapala katika uzito wa Buntam utakaochukua raundi 8.

Pambano hilo litatanguliwa na lile la utangulizi kati ya Shabani Mohamed (Star Boy) anayezipiga na Godfrey Mawa katika uzito wa Super Fly litakalo chukua raundi 6.

Wengine ni Chivan Bruno atakayetwangana na Hamis Mkwele katika uzito wa Super Fly wakati Almasi Zubery atazipiga na Charles Mashauri katika uzito wa Light Fly.

Katika uzito wa Paper Fly, bondia Sunday Elias ataingia ulingoni na bondia Kurwa Kinondoni. Kwa mujibu wa mjumbe huyo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkurugenzi wa Daban Nassoro Ndosa na Mkurugenzi wa Dynamite Promotion, Shomari

'Mzungu Four' asisitiza Tanzania kuna vibwetere wengi kuliko Uganda

Na Josephs Sabinus

MWINJILISTI kwa njia ya nyimbo, Jossey Mzungu, maarufu kwa jina la "Mzungu Four", amesisitiza kauli yake kuwa Tanzania kuna watu wengi wenye ukatili wa kiroho kuliko hata Joseph Kibwetere aliyeua zaidi ya waamini 500 wa Madhehebu ya Kurejesha Amri Kumi za Mungu.

Katika mauaji hayo yaliyofanyika Kanungu nchini Uganda Machi 17, mwaka jana, Kibwetere aliwafungia waamini hao ndani ya hekalu na kisha kuchoma hekalu.

Jossey Mzungu anayesema kuwa jina Mzungu Four limetokana na ukoo wao kutumia jina la ukoo; Mzungu, na yeye kuwa wa nne katika familia yao kutumia jina hilo, alisema mwanzoni mwa juma alipozungumza na mwandishi wa habari hizi katika Mkutano wa Injili kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka ulioandaliwa na "Peace makers Church" na kufanyika katika viwanja vya WAPO Mission Center Kurasini jijijini.

Alikuwa akizungumza juu ya kanda yake mpya aliyoizindua Desemba 15, mwaka jana iitwayo KIBWETERE iliyorekodiwa katika FM Studio. Gazeti la Kiongozi lilitaka ufafanuzi wa maneno yaliyopo katika wimbo unaobeba jina la kanda hiyo.

Walioshiriki kuandaa kanda hiyo kwa mujibu wa Mzungu Four, ni yeye mwenyewe akiwa mtunzi na mwimbaji, John Merry Madunga na Edward David Twinning, waliohusika katika upigaji wa kinanda huku gitaa likichezwa pia na Edward D. Twinning.

Mwinjilisti huyo ambaye ni muumini wa kanisa la Evangelism Assemblies of God Tanzania(EAGT), alisema, "Nilitunga huu wimbo ili jamii ya Watanzania ielewe kuwa roho ya ukibwetere sio tu kwamba ni roho ya Uganda tu, bali hata hapa Tanzania wapo viongozi wengi wa kiroho wanaotumia ubabe wa kiroho na hao wananguvu, ushawishi na masharti mengi kwa wafuasi wao. Hao, Watanzania wajihadhari nao."

Sehemu ya wimbo huo wa KIBWETERE katika kanda hiyo inasema hivi:

"...Karibu viongozi wote wa dini hizo ni wasemaji wazuri, walaghai na wana mvuto mkubwa kwa wafuasi wao lakini, wana moyo wa ukatili. Wakisha wanasa wafuasi, huwa wanadai wafuasi wajitolee mali zao kama vito, dhahabu na fedha na kuwakabidhi viongozi hao.

Pili, wana vitisho kwa yeyote atakayetaka kujaribu kuacha dini hiyo. Na ukatili wao mkubwa ni kuwaangamiza wafuasi wao mambo yao yanapoelekea ukingoni.

Waathirika wakubwa wa madhehebu haya ni akinamama. Wengine wanaamini wakifuata dhehebu hilo, matatizo yao katika maisha yatapungua kumbe wanajiangamiza; katika vinywa vya chatu; wanajipeleka wenyewe.

Hapa kwetu Tanzania, vibwetere pia wapo wengi isipokuwa, mbinu za utendaji ni tofauti. Wakati Kibwetere yule wa Kanungu, Uganda ametuima moto wa kiberiti kuteketeza waamini 500, vibwetere hawa wa Tanzania hawatumii moto wa kiberiti, bali wanatumia ubabe yaani "spritual bounce" na madaraka yao kuwafanyia waamini udikteta wa kiroho kuwakandamiza na kuwanyima haki zao za kiroho.

Pia, wapo tayari muumini afe kiroho lakini dini zao zisife au zisiaibike lakini roho ya muumini ipotelee kwa mbali. Kwa hiyo, wao hulinda sana dini zao kuliko roho ya muumini.

Vibwetere wa aina hii ni wengi sana hapa Tanzania na ni wabaya mno kuliko hata wale vibwetere ambao tumewataja.

Hivyo, ndugu yangu nakusihi ujihadhari na roho ya ukibwetere. Mwamini sasa Bwana Wetu Yesu Kristo. Yeye alikuja kuziokoa roho wala hakuja kuziangamiza kamwe. Jihadhari na kibwetere. Nakuonya ndugu jihadhari na kibwetere."

Hatuna ugomvu na DRFA lakini hatukubali kuburuzwa - KIFA

Na Benjamin Mwakibinga

UONGOZI wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani Kinondoni(KIFA), umesema hauna uhasama wowote na Chama cha Soka mkoani Dar-Es-Salaam(DRFA) kama inavyoelezwa na baadhi ya viongozi wa DRFA.

Wakizungumza jijini, Katibu Mkuu wa KIFA, Ramadhani Kampira na Makamo wake, Frank Mchaki, walisema hawaendeshi shughuli za soka kinyume na kanuni.

Walisema wanafuata sheria na kujali maslahi ya wilaya ya Kinondoni kwa kuwa wamepewa dhamana hiyo na wanasoka wa Kinondoni.

Katika mahojiano yaliyofanyika katika ofisi za KIFA zilizopo Magomeni jijini, Kampira alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa hawaelewi anachokisema kuhusu DRFA na matokeo yake, wamekuwa wakimtafsiri kwa makosa.

Aliyasema gazeti hili lilipotaka ufafanuzi juu ya madai yaliyo ripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba kama timu ya Abajalo ingeshindwa katika pambano lake na IPP, mashindano hayo yasingeendelea.

Pambano la hivi karibuni kati ya IPP SC na Abajalo FC lililofanyika katika uwanja wa Karume jijini, halikumalizika baada ya Abajalo kushindwa kuendelea na mchezo kwa madai kuwa mwamuzi alikuwa akiwabeba IPP.

Kampira alisema kuwa kwa kosa hilo, timu ya Abajalo ya Sinza ilipigwa faini ya shilingi 100,000/= "Hili hatulishangai sana kwa vile DRFA ina mazoea ya kuzikandamiza timu za wilaya ya Kinondoni," alisema Kampira.

Alisema hata siku moja, kama viongozi hawatakubali kuendesha KIFA kwa kuinyenyekea DRFA na badala yake, wataendelea kuiheshimu na maamuzi yake halali kwa kuwa ni ngazi ya juu.

Alisisitiza kuwa jukumu lao sio tu, kukubali kila jambo hata kama halina manufaa kwa wanamichezo wa kinondoni.

Wakati huo huo: Katika kukuza mchezo wa soka wilayani humo, KIFA wanampango wa kuandaa darasa maalumu la waamuzi na tayari wamekwiwasiliana na Chama cha Waamuzi Kinondoni (KIFRA).

Wamesema wamefanya mawasiliano hayo ili kuomba msaada juu ya suala hilo kwa vile mpaka sasa waamuzi waliopo katika wilaya hiyo, ni wachache.

"Tutawataka watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 na wenye afya nzuri kujiunga na mafunzo hayo," alisema katibu huyo na kuongeza kuwa, washiriki watatakiwa kulipa gharama kidogo.

Ligi ya Daraja la Tatu ngazi ya Wilaya ya Kinondoni inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili na kwamba, timu zipatazo 34 zimekwisha thibitisha kushiriki.

Katika tukio jingine: Timu nne zilizoshuka daraja wilayani Kinondoni zimetajwa kuwa ni Kinondoni FC, Nanga FC, AFC OPEC na Sinza Boys.