Make your own free website on Tripod.com

BAADA YA KUFANYA BIASHARA...

TEFA yalia 'kuumia'

Na Leocardia Moswery

CHAMA cha Mpira wa Miguu wilayani Temeke katika Mkoa wa Dar-Es-Salaam(TEFA), kimepata hasara ya zaidi ya shilingi 90,000/= baada ya kuikaribisha bendi ya Muziki ya OTTU kutumbuiza ili kutunisha mfuko wa chama hicho.

Katibu Msaidizi wa TEFA, Hassan Mpanjilla, aliliambia KIONGOZI hivi karibuni ofisini kwake kuwa, licha ya kuwalipa OTTU shilingi 200,000/= wakati wa burudani, walikusanya shilingi 140,000/= kama kiingilio.

Alisema kwa hesabu ya haraka, hiyo ni hasara kwani bado walikuwa wanadaiwa pesa waliyokodi jenereta, kiasi cha shilingi 20,000/=.

Alisema hasara nyingine waliyopata ni kushindwa kupata pesa ya kulipia viti walivyokodi kwa shilingi 10,000.

Katika onesho la bendi hiyo ya OTTU lililofanyika Jumamosi iliyopita katika ukumbi wa ofisi hiyo uliopo eneo la Tandika-Mabatini, jijini Dar-Es-Salaam, kiingilio kilikuwa shilingi 1000.

Gharama nyingine ambayo hakutaja kiasi chake, ni kumlipa mlinzi.

Alisema lengo la kufanya onesho hilo lilikuwa kutunisha mfuko wao ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya wajumbe watakao kwenda Zanzibar kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

Safari hiyo inatarajiwa kuwashirikisha karibu viongozi 1000 toka Tanzania Bara.

Alidokeza kuwa, kwa mwaka huu safari hiyo imeandaliwa na wenyeji wa Zanzibar na kwa kawaida, hulenga katika kubadilishana mawazo na uzoefu ili kuendeleza mchezo wa soka nchini.

Alisema ziara hiyo inatarajiwa kufanyika Aprili 12 hadi 17.

Wakati huo huo: Katibu huyo Msaidizi wa TEFA, amevihimiza vilabu mbalimbali katika eneo lake, kushiriki mashindano ya Ligi ya Kanda yanayoendelea katika viwanja mbalimbali wilayani Temeke.

Amevitaja baadhi ya viwanja hivyo kuwa ni pamoja na Tandika-Mabatini na Mbagala.

Mashindano ya Wavu Sekondari Dar Kuanza Aprili 25

Na Getrude Madembwe

MASHINADANO ya Mpira wa Wavu katika shule za sekondari mkoani Dar-Es-Salaam, yanatarajiwa kufanyika Aprili 25 hadi Mei Mosi mwaka huu katika viwanja vya Taasisi ya Teknolojia Dar-Es-salaam(DIT).

Kwa mujibu wa Mratibu wa Mashindano hayo yajulikanayo kama May Day, Mwalimu Flowin Sapula, lengo la mshindano hayo mwaka huu ni kuimarisha mpira wa wavu kwa wanafunzi wa sekondari mkoani Dar-Es-Salaam.

Akizungumza katika ofisi za gazeti la hili katikati ya juma lililopita, Mwalimu Sapula alisema lengo lingine ni kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi maarufu kama Mei Mosi, pamoja na kutoa sheria mpya za mpira wa wavu.

"Pamoja na kusherehekea Mei Dei, lengo lingine la mashindano haya ni kuuendeleza mchezo huu na kutoa sheria mpya za mchezo," alisema Sapula.

Alisema watatumia nafasi hiyo kuitangaza sheria mpya ya mpira wa wavu kwa kuwa hadi sasa wachezaji waliopo katika shule za sekondari hawaijui tofauti na ilivyo kwa vyuo vikuu.

Alisema shule zote za sekondari katika mkoa wa Dar-Es-Salaam, zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika katika viwanja vya DIT.

Alizitaja baadhi ya shule za sekondari zilizokwisha thibitisha ushiriki wake katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na Jitegemee, Makongo, Vituka, Air Wing, Kigamboni na Taasisis ya Teknolojia Dar-Es-Salaam.

Sapula alibainisha kuwa shule shiriki, zitatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 40,000 kila moja kwa ajili ya malipo ya wataalamu wa mchezo huo na hivyo, kuepuka wababaishaji wa mitaani.

Sapula alisema zawadi kadhaa zitatolewa kwa washindi watatu wa kwanza; wavulana na wasichana.

Wengine watakaozawadiwa ni wachezaji bora wa kwanza hadi wa sita.

Mapromota wa ndondi watakiwa kuheshimu Sheria

Na Dalphina Rubyema

MAPROMOTA wa masumbwi nchini waliosajiliwa na umoja wa ngumi unaojulikana kama Pugilistic Syndicate (PST) wametakiwa kuheshimu sheria na kanunu za michezo ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na kaimu Rais wa PST Ally Bakari ‘Champion’ wakati akizungumza na gazeti hili jijini Dar es salaam.

Bakari alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuendeleza mchezo wa masumbwi ikiwa ni pamoja na kuwalidna mabondia na mapromota wenyewe.

Makamu huyo wa Rais wa PST vile vile amewakumbusha mapromota hao kuzingatia sheria muhimu za PST.

Alizitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni pamoja na kila promota kulipa shilingi 20,000 kwa ajili ya pambano analotaka lipate uratibu wa PST (Sanction fee).

Sheria nyingine ya PST kama ilivyotajwa na Bakari ni kwamba promota anatakiwa kutiliana mikataba na mabondia kwenye fomu ya mikataba zilizotengenezwana kuidhinishwa na wakili wa PST.

Pamoja na sheria nyingine za PST Bakari amesisitiza mapromota wasisahau ile sheria ya promota ambayo anataka pambano lifanyike na kuweka usafiri tayari kwa ajili ya kumkimbiza hospitalini bondia yeyote ambaye ataumia.

Chuo cha Ualimu chawafundisha Wasalvatoriani 3-2

l DSJ yawazamisha DSA 1-0

Na Eric Samba, Morogoro

TIMU ya Soka ya Mchanganyiko ya wanafunzi toka mashirika mbalimbali ya kimisionari wanaosoma Chuo Kikuu cha Salvatoriani cha mjini hapa, Jumanne ilishindwa kutamba mbele ya ile ya Chuo cha Ualimu Morogoro baada ya kuchapwa mabao 3-2.

Katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Salvatoriani na ulikuwa na upinzani mkali ambapo kila timu ilijitahidi kupata bao la kuongoza.

Ni Salvatoriani waolipata bao katika kipindi cha kwanza lililofungwa na Frateri Thomas Marwa.

Hadi kipindi cha pili, wenyeji; Salvatoriani walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku wenyeji wakitaka kuongeza bao na wageni wakitaka kusawazisha na kuongeza bao la ushindi.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Salvatoriani walipata pigo kubwa baada ya golikipa wao wa kutumainiwa Frateri Magnus Tegete, kuumia katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake.

Ndipo alipogongana na mshambuliaji Deo Mhagama wa Morogoro TTC na kuumia hata hivyo, mshambuliaji huyo alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kusawazisha.

Salvatoriani walimwingiza golikipa wa akiba Frateri Emannuel Chuwa, kuziba pengo lililoachwa na mlinda mlango nambari moja aliyeumia.

Baada ya bao hilo, Salvatoriani walifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Morogoro TTC ambapo mshambuliaji wake hatari Frateri Nelson Lupogo.

Hata hivyo vijana wa morogoro TTC ambao walicheza mpira wa kasi na kuelewana huku wakionyesha kutokuchoka haraka walifanya shambulizi moja la nguvu langoni mwa Salvatoriani na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji yule yule Deo Mhagama ambaye mara kadhaa aliisumbua sana ngome ya Salvatoriani.

Baada ya kuingia bao hilo na kufanya matokeo kuwa sawa, vijana wa Morogoro TTC waliendelea na mchezo wa kasi na kutawala mchezo huku Salvatoriani wakionekana kuchoka na kuzidi kuelemewa.

Hali hiyo ilipelekea Salvatoriani kufanya faulo nyingi dhidi ya vijana wa Morogoro TTC. Katika dakika za majeruhi, beki mshambuliaji wa Morogoro TTC aliyekuwa anakata mbuga kwenda kufunga ndipo mwamuzi aliamua upigwe mpira wa adhabu uliopigwa na mchezaji Raphael Mkumbara kwa shuti la moja kwa moja na kuifungia Morogoro TTC Goli la Tatu na la ushindi.

Pamoja na kufanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili, Salvatoriani walishindwa kuwadhibiti washambuliaji wa Morogoro TTC walipozidiwa mbio na hivyo, kuchezeshwa mchakamchaka na walimu wa Morogoro TTC.

Hadi mwisho wa mchezo, walimu wa Morogoro TTC walitoka kifua mbele kwa magoli matatu dhidi ya mawili ya watawa wa Salvatoriani.

Kiongozi wa timu ya Salvatoriani Frateri Thomas Wambura, alisema timu yake ilichoka katika kipindi cha pili kwa sababu ya kukosa mazoezi muda mrefu.

Wakati huo huo: Timu ya mpira wa kikapu ya Chuo cha Ualimu Morogoro, imeinyuka timu ya Watawa wa Salcatoriani kwa vikapu 30-23. Mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Seminari Kuu ya Mt. Gaspari.

Michezo hiyo ya kirafiki ilikuwa ni kwa ajili ya kudumisa ujirani mwema kati yao na kujiweka sawa kimchezo.

Naye Leonard Magumba anaripoti kuwa timu ya soka ya Chuo cha Uandishi wa Habari Dar-Es-Salaam (DSJ) kwa mara nyingine tena imefanikiwa kuifunga timu ya Chuo cha Uhasibu (DSA) bao 1-0 katika mchezo uliofanyika hivi karibuni kwenye uwanja wa DSA jijini Dar-Es-Salaam.

Vyuo mbalimbali nchini vimekuwa na mfumo wa kuendeleza michezo kama sehemu ya kukuza ushirikiano na katika mechi hiyo iliyoandaliwa na DSA,ilikuwa na lengo la kuwapongeza viongozi wapya wa DSJ na kuwaaga wale wa zamani.

Timu nane kushiriki michuano ya Pasaka

Dalphina Rubyema na Getrude Madembwe

JUMLA ya timu nane za soka za jijini Dar-Es-Salaam, zinatarajiwa kushiriki michuano ya Pasaka kwa vijana walio na umri wa miaka 17 kwenda chini ,pambano litakalofanyika wiki ijayo kwenye uwanja wa Taifa.

Kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi wa michuano hiyo inayojulikana kama Easter Youth Tournament ,Ronny Mintjens ,washiriki wa michuano hiyo wametakiwa kuzingatia sheria na masharti ya michuano hiyo.

"Wachezaji wote wanatakiwa wawe wamezaliwa mwaka 1984 au baada ya mwaka huo na kila mchezaji anatakiwa kuleta kwenye kamati ya maandalizi cheti chake cha kuzaliwa" alisema Mintjens.

Mjumbe huyo alizitaja timu hizo nane kuwa ni Kambarage FC, Temeke Kids, Wakati ujao, Shule ya Sekondari Tegeta ,Kunduchi Stars, Dar Youth Onlympic Centre na timu ya Yanga.

Hata hivyo mjumbe huyo alisema zawadi kwa timu zitakazo ibuka washindi bado zinaandaliwa

"Bado kamati inaandaa na nina imani itakuwa nzuri na kuwapa motisha vijana kupenda kushiriki michezo mbalimbali" alisema Mintjens.