Make your own free website on Tripod.com

Tuache kiburi, upumbavu amani ya kweli ipatikane

KILIO kikuu katika ulimwengu mzima siku hizi kimekuwa AMANI - AMANI - AMANI. Hakuna binadamu asiyetambua umuhimu wa amani katika jamii tukianzia kwa mtu binafsi, mazingira na watu anaoishi nao, jamii na taifa zima.

Je, Amani ni nini? Mtakatifu Augustino Askofu, anasema kuwa ‘Amani ni utulivu wa utaratibu. Hali ya amani kwa kawaida ni utulivu, ni yenye kuwa na utaratibu.Ni kuishi kufuatana na sheria za kimaumbile, sheria na taratibu za mahali, sheria za uraia, sheria za kijamii, sheria za nchi na sheria za nchi na za kidini.

Siku zote amani hutoweka kwa sababu baadhi ya watu hawataki kufuata taratibu zilizopo katika jamii.

Ni jukumu la wanajamii kutambua na kuzingatia ukweli kuwa, hali ya kutoweki, ni lazima zipo baadhi ya haki na taratibu ambazo hazikulindwa wala kuthaminiwa.

Inapotokea hali hiyo, ni wajibu wa kila mmoja kujiuliza na kutafiti ni haki na taratibu gani zimekiukwa na kwanini.

Tunasema hivi tukiamini ukweli kuwa ni silika ya kila mwanadamu kutafuta haki yake kwa utaratibu aliowekewa na Mungu. Ikiwa mtu atasogeza kijiti kwenye pua ya mwenzake, ni dhahiri kuwa huo ni mwanzo wa kuvunjika kwa amani.

Kwa maneno mengine, kuvunjika kwa amani ni kuvunja utaratibu unaoleta na kuendeleza utulivu katika maisha ya watu.

Ni dhahiri na sisi tunaamini kuwa, kuvunjika kwa amani kunatokea kutokana na kuingiliana katika suala la haki za binadamu. Migogoro mingi hutokea kwa kuwa watu wanaingiliana katika haki mbalimbali ukiwamo umiliki wa mali, kuthaminiwa kwa utu wa mtu na hata uhuru wa wengine.

Katika Zaburi ya 85 tunasoma hivi: "Nasikia anayosema Mungu, Mwenyezi Mungu: anaahidi kuwapa watu wake waaminifu amani, ikiwa hawatarudia upumbavu wao..."

Mtu anayeharibu utaratibu mahali popote, ni mpumbavu. Hivyo, tukumbuke kuwa kuvunjika kwa amani kwa kiasi kikubwa, hutokana na upumbavu wa watu kwa kuwanyang’anya wengine haki zao na kuharibu utaratibu unaotakiwa katika kuishi na watu wengine.

Sisi tunamini kuwa hata watoto wadogo wanajua madhara ya ukosefu wa amani katika jamii yoyote. Ni dhahiri yanapotokea machafuko mahali popote, huambatana na uharibifu wa mali, uharibifu wa ardhi na kikubwa zaidi, uharibifu wa maisha ya watu.

Ni muhimu kwa watu wasiojua hasara za ukosefu wa amani na ubaya wa kuwapo kwa machafuko, wakafanya tafiti mbalimbali kabla ya kufanya majaribio ya kipumbavu ambayo huleta vilio na maangamizo ya kutisha katika jamii.

Tunasema hivi kwani tunajua dhahiri penye machafuko, waathirika wengi ni watoto, wazee, walemavu na wanawake ambao hawana hatia.

Ni wakati huo ambao watu hao na wengine hata kama walikuwa wataalamu, utaalamu wao hufia mgongoni kwa machafuko hayo. Biahara huathirika na hali ya afya kwa jamii huharibika kutokana na adha ya mwendo mkubwa na prukshani za ukimbizi.Shughuli za kibiashara na nyingine za uchumi, zinasimama na kuharibika; nini matokeo yake na faida iko wapi?

Inasikitisha kuona kuwa hata katika jamii zinazoutambua ukweli na uhalali wa uwepo wa Mungu, bado wapo wanaojiona kuwa na haki zaidi ya wengine.

Hali hiyo ni hatari kimwili na kiroho na ni upumbavu kwani ni kinyume na mapenzi ya jamii na kikubwa zaidi, ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Ipo dosari kubwa pia kwa baadhi ya nchi kwani licha ya kuwa na mipaka yake, serikali yake, na mali zake za asili, bado wapo wanaopenda kuingilia taratibu za nchi na kupora mali za wengine.

Ni dhahiri kuwa watu, kikundi, au yeyote anayefanya hivyo, huzua fujo na hivyo, kusababisha amani kutoweka.

Kwa maneno mengine, wapo watu ambao wamefanya jambo la upumbavu wa kuingilia taratibu za watu wengine na hivyo katika kutetea haki zao hizo, kukazuka kuvunjika amani ya kweli.

Tunapozungumzia amani ya kweli katika ulimwengu huu, ni lazima tuzungumzie pia kuhusu ushikaji wa sheria zinazotawala na kuongoza maisha ya binadamu.

Kila mmoja ni lazima atambue na kuziheshimu haki za mwenzake na kuzingatia wajibu wake kwa Mungu , kanisa na jamii kwa jumla.

Ni wajibu wa wanajamii wote wenye mapenzi mema, kuishi chini ya taratibu zinazozingatia sheria za Mungu na za nchi; kila mahali tunapokuwa. Ni vema pia kila mmoja kwa nafasi yake, akasali na kuwa mstari wa mbele kimatendo ili amani ya kweli ipatikane ulimwenguni.

Tunapotafuta amani tujiulize ni kwa nini amani hutoweka? Jibu lake litakuwa ni kutokana hasa na uvunjaji wa sheria na unyag’a nyi wa haki za wengine.

Tunatoa rai kwa wananchi wote kuwa tunahitaji kweli utulivu katika taifa letu, lakini inatupasa kabisa kuondokana na tabia ya uvunjaji wa taratibu na sheria katika jamii yetu. Tunapenda pia kuiambia jamii ya kimataifa kuwa, ikiwa inataka taka amani ya kweli, basi ni lazima kila mmoja afuate sheria, kanuni na taratibu za kimungu na kiserikali.

Papo hapo tunapaswa kumwomba Mungu ili atuondolee kiburi, tamaa ya mali na madaraka, na upumbavu ambavyo husababisha mtu ajifanyie atakavyo bila kuzingatia matokeo ya analotaka kufanya.

Tambiko Letu la Sasa, Ni Yesu Altareni

1. Jukwaani twajikita, Wasanii wa shairi,

Ujumbe tunauleta, Mahiri na marimari,

Wapambe tunawaita, Sikieni ya johari,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

2. Kupokea yetu rai, Vilivyo jiandaeni,

Dondoo iliyo hai, Dhamira ya Vatikani,

Mambo ni sawa sawia, Ujumbe wetu makini,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

3. Tambiko la kizamani, Wanyama kuteketeza,

Sadaka hiyo ni duni, Imani inalemaza,

Mungu Baba wa mbinguni, Bayana katueleza,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

4. Bwana Yesu alikuja, Kukamilisha Torati,

Hiyo ndiyo yetu hoja, Ambayo tumezatiti,

Biblia kweli hija, Tena kitu hasanati,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

5. Tusiabudu mizimu, Na kufanya makafara,

Tutaipata hukumu, Ni kweli si hambarara,

Tutakuwa mahasimu, Muumba tutamkera,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

6. Tunaanza kueleza, Dhamira kuu tambiko,

Siyo vema kutubeza, Tunawapeni mwaliko,

Tena tunasisitiza, Tufanye mabadiliko,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

7. Tuabudu Mungu moja, Ni katika kila misa,

Siyo kwamba twabwabwaja, Au tunajimamasa,

Sisi tunatoa hoja, Yesu sadaka ya sasa,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

8. Sadaka zote za jadi, Zimepitwa na wakati,

Yesu ndiye ni shahidi, Ukombozi kazatiti,

Na sisi tutabaradi, Maisha ni hatihati,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

9. Kula nyama kaburini, Hilo si jema tambiko,

Ni dawa za kishetani, Kwa moyo ni hangaiko,

Kuweka roho rehani, Ni kuleta machafuko,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

10. Baba Desideri Rwoma, Endeleza mapambano,

Vijana sisi tunasema, Dumisha mshikamano,

Cheo chako muadhama, Tuna kuunga mkono,

Tambiko letu la sasa, ni Yesu Altareni.

11. Beti hizi edashara, Tumefikia tamati,

Tumesema ya tijara, Kuwa mchango mathubuti,

Shairi la tia for a, Lugha yake bai dhati,

Tambiko letu la sasa, Ni Yesu Altareni.

 

Vijana wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA),

Parokia ya Ntuntu,

Jimbo Katoliki la Singida.

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni Mtumishi

1. Katika jina la Bwana, Twawasalimu sawia,

Mlo wapenzi wa Bwana, Roho alowavevia,

Msidhani twawabana, Sisi tunawahusia,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

2. Daima ni mtumishi, Kiongozi wa kiroho,

Huyu asiwe mbishi, Na aongozwe na Roho,

Na awe mpatanishi, Akiongozwa na Roho,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

3. Ili adumu amani, Kwa Kristo na awe wazi,

Roho amtumaini, Yeye kama kiongozi,

Atakuwa matatani, Ye kipofu kiongozi,

Kiongozi wa Kiroho, daima ni mtumishi.

4. Anatakiwa kutenda, Kwa mfano wa matendo,

Kwake wachume matunda, Siyo awapige nyundo,

Tamjua kwa matunda, Kiongozi wa matendo,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

5. Awe mtu wa maono, Hata upendo kwa wote,

Kamwe asipende ngono, Husambaratisha wote,

Matendo yawe mfano, Muda na mahali pote,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

6. Aaminiwe na Mungu, Na anaowaongoza,

Ayapeleke kwa Mungu, Yote yanayowakwaza,

Kwa magumu na machungu, Ndipo atawaliwaza,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

7. Atumiaye karama, Alizopewa na Mungu,

Azibebaye lawama, Hata kama ni majungu,

Kwa hiari na huruma, Hata yajapo machungu,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

8. Yu tayari kujifunza, Kulingana na wakati,

Kwake mwiko kujikweza, Anakwenda na wakati,

Yote anayoyawaza, Ni kuweka mikakati,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

9. Ni mgumu uongozi, Kwa ulimwengu wa leo,

Vema uwe mkufunzi, Uyajuaye ya leo,

Na kwa hekima azizi, Ulete maendeleo,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

10. Asiwe mwenye kinyongo, Hasira hata kisasi,

Asiyesema uongo, Asiyelipa kisasi,

Mwenye kuchemsha bongo, Aukwepae uasi,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

11. Pole na asante kwake, Huitoa kwa upole,

Japo umpige teke, Ataipokea pole,

Yeye hataki makeke, Kuenenda kwa upole,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

12. Asiyekata tamaa, Na kutojihurumia,

Maoni kutokataa, Japobidi yatumia,

Ajapokataa tamaa, Mipango imetimia,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

13. Mwovu japo gonganisha, Na mumpinge kwa sala,

Huko ni kumaanisha, Hadi shetani talala,

Hapa tunahairisha, Twawaahidia sala,

Kiongozi wa Kiroho, Daima ni mtumishi.

Emmnauel Anthony Mmbando

St. Gabriel Parish

Parokia ya Bwika

Box 75,

Arusha.