Utamaduni wa kujisomea uimarishwe

WAINGEREZA wanao msemo, "Readers are leaders and leaders are readers", yaani "Wasomaji ni viongozi, na viongozi ni wasomaji".

Ili mtu awe kiongozi katika jamii yoyote, hana budi kuwa na maarifa katika mambo mbalimbali ya maisha na mazingira yanayomzunguka. Maarifa hayo hupatikana hasa kwa njia ya kusoma vitabu, majarida, magazeti na kadhalika.

Ni dhahiri kuwa, watu wote wakiwamo watoto, hujifunza kusoma na kuandika tangu wakiwa wadogo. Hii, hufanyika tangu nyumbani, katika shule za awali na kwingineko.

Taifa la Tanzania lilishatangaza vita dhidi ya maadui, ujinga, maradhi na umaskini. Ni ukweli ulio bayana kuwa adui mkubwa na mzazi wa adui wengine kati ya hao watatu, ni ujinga.

Ndiyo maana kumekuwa na jitihada kubwa katika kupambana na ujinga. Kwa kifupi ujinga ni ukosefu wa maarifa ya kusoma na kuandika. Pia, ukosefu wa maamuzi sahihi.

Katika kufanikisha vita dhidi ya ujinga, ulianzishwa mpango maalumu wa Elimu kwa Wote UPE- (Universal Primary School Education).

Mipango kamambe ya kueneza elimu hadi vijijini ikafanyika. Lengo lilikuwa kuwapa fursa watoto wote wenye umri wa kwenda shule, ili waende shuleni na hivyo, kuondokana na ujinga.

Siyo watoto pekee yao walioshughulilkiwa kielimu, bali pia watu wazima ambao hawakufanikiwa kupata elimu ya darasani ya kujua kusoma na kuandika walipelekwa kwenye madarasa ya watu wazima, yaani shule za "ngumbaro".

Kwa jumla mipango hiyo ilifanikiwa na ndiyo maana tunaipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Kwanza kwa mpango huo.

Licha ya kuwafundisha hao watu wazima kusoma na kuandika, Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu, ilisambaza vitabu katika maktaba za vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa na za kitaifa. Wananchi walipata vitabu vingi vya kusoma katika maktaba hizo.

Ni jambo la kusikitisha mno kuona ari na mwamko juu ya kisomo, imefifia na hata pengine kufa kabisa. Tunasema ni aibu kubwa kufikia hatua hiyo ya kupiga hatua nyuma badala ya kuendelea kielimu.

Ukweli wa jambo hilo umedhihirishwa wazi wazi na Meya wa Jiji la Dar-es-Salaam Mheshimiwa Kleist Sykes wakati alipofungua Maonesho ya Kumi ya Wiki ya Vitabu Tanzania Jijini Dar-es-Salaam, hivi karibuni.

Meya Sykes alisema kuwa, Tanzania imeondokana na utamaduni wa kusoma vitabu na hivyo kusababisha maduka yanayouza vitabu kuwa machache sana. Ingawaje kuna maduka mengi siku hizi yanayouza magazeti na majarida mbali mbali, lakini yana umuhimu finyu katika kuelimisha, kupanua mawazo na hivyo, kushindwa kuendeleza jamii kiakili.

Meya huyo alisema ipo haja ya kuihamasisha zaidi jamii katika kujisomea vitabu mbalimbali. Jambo hilo lisifanyike kwa wazee kuwahimiza watoto kusoma vitabu pekee, bali na wazee wenyewe wawe mstari wa mbele katika kuvisoma.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona watu wengi, na hata wale wanaojiita wasomi, hawasomi kabisa vitabu. Wengi kama wanasoma, basi ni ule usomaji rahisi rahisi wa magazeti na vijarida vya kipuuzi.

Ingawaje katika magazeti mbalimbali kuna makala nzito zinazoelimisha na kutoa maarifa katika fani mbalimbali, lakini wananchi wengi hawana muda wa kusoma vitu hivyo kwa sababu ule moyo wa kusoma umekufa na wengi wamejijengea moyo na tabia ya kutosoma kabisa.

Ni kweli kwa upande mwingine kwamba bei za vitabu ni kubwa mno siku hizi kutokana na malighafi ya kuchapishia vitabu, pamoja na kodi kwa wachapishaji lakini, mbona kuna vitabu vingi vinavyozagaa hapa na pale na vikikosa wasomaji?

Ni tabia mbaya kuona kuwa watu wengi wakiwamo wasomi ambao ni mfano bora wa kuigwa, wanasoma kwa shinikizo la kupata cha kujibu katika mitihani lakini, wakimaliza mitihani yao, wanavipa kisogo vitabu vyote.

Ni wazi kuwa aliyefuzu jana na kupata shahada katika fani fulani asipoendelea kusoma, baada ya kesho atarudi kuwa mjinga marudufu. Watu wa namna hiyo ni hatari kwani watadhani kuwa bado wana elimu kumbe wana vyeti pekee. Mengine wanasahau kadiri siku zinavyopita.

Tunapenda kuwasikia watu wakisema, "Nimesoma katika kitabu fulani jambo hili" na siyo "Nimesikia toka kwa mtu fulani...nk".

Sisi tunadhani kuwa tabia ya Watanzania wengi imekuwa ya maneno na porojo nyingi na tabia hiyo, inawaondolea ari, na muda wa kujipatia elimu ya vitabuni.

Wazazi na walezi hawana budi kuwahimiza watoto kujiendeleza kwa kusoma vitabu mbalimbali. Kwa upande wa kidini vile vile tunapenda kuwahimiza waamini wajitahidi sana kusoma vitabu vilivyo msingi wa imani yao.

Kitabu ambacho ni cha msingi kabisa kwa upande wa Wakristu, ni Biblia Takatifu (na kwa upande wa Ndugu zetu Waislam ni Quran Tukufu). Ni jambo la aibu kuona kuna nyumba nyingi za Kikristo ambazo hazina kitabu hiki kikuu yaani Biblia Takatifu.

Ni vema kukisoma Kitabu hicho kila siku. Gharama ya upatikanaji wa Kitabu hicho Kitakatifu, siyo kubwa kama inavyoweza kuchukuliwa na wanajamii wasio na utamaduni wa kusoma Maandiko Matakatifu kwani kinadumu katika maisha yetu yote.

Tukisoma Maandiko Matakatifu tunapata faida siyo ya kiroho tu bali pia maarifa na hekima ya maisha yetu kwani tunaambiwa Biblia ni kama maktaba ambamo tunasoma mambo mengi mno.

Tukitaka kuongoza familia zetu hatuna budi kuwa wasomaji wa vitabu, tukitaka kuwa viongozi katika jumuia na jamii zetu hatuna budi kuwa wasomaji wa vitabu na makala mbalimbali.

Pamoja na kusikiliza radio, kuangalia televisheni na kusoma mambo ya kila siku katika mtandao wa kompyuta, bado tuna ulazima wa kusoma vitabu vinavyohusu mambo hayo.

Tukumbuke kuwa hatuwezi kufaidi mambo ya kileo na kisasa bila kusomasoma katika vitabu, vijarida, magazeti na mahala popote pale ambapo kuna mambo yameandikwa kwani ulimwengu wetu ni wa kisomo cha mambo mbalimbali.

Basi tuondokane na ujinga wa kutopenda kusoma, bali tujenge tabia na utamaduni wa kujisomea ili twende na wakati.

Kondomu Si Salama (Jibu)

1. Emma ninajitokeza, Kukujuza Mose Buja,

Yote uliyouliza, Kama kondomu huvuja,

Ni wengi limewaliza, Tangu Bara na Unguja,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

2. Sio tu zinavuja, Ila pia zimeoza,

Wewe ukiwa wa kuja, Kondomu takumaliza,

Wao hawataki hoja, Wamekuja kuziuza,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

3. Kondomu siyo salama, Ni pesa zinatafutwa,

Hizo kamwe si salama, Ni kinyume zinaitwa,

Yesu tu ndiyo salama, Wa heri walioitwa,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

4. Ni kichocheo cha ngono, Dhambi hata vingi vifo,

Kwa watu wenye maono, Hawakichezei kifo,

Huu bayana mufano, Kila mahali ni vifo,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

5. Hii ni sera ya siri, Ya ongezeko la watu,

Tena yafanywa kwa siri, Ili kupunguza watu,

Wamezalisha kwa siri, Kuzuia kondomu watu,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalilisha.

6. Serikali shinikizwa, Kafiki bila hiari,

Na tena ikahimizwa, Kutushawishi kwa hari,

Nanyi kama mnalizwa, Kutotumia ni shwari,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

7. Mwenye macho haambiwi, Tazame yalo bayana,

Nawe usiwe kiziwi, Si kwamba tunalumbana,

Ni dumisho la ukimwi, Virusi vinazaana,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

8. Nayo akili ni nywele, Kila mtu ana zake,

Yalopita siyo ndwele, Ila sasa tuamke,

Nyani haoni kundule, Acha ngono sikuzike,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

9. Ukitaka salimika, Buja acha uasherati,

Salama zimewazika, Hao wengi hati hati,

Nawe ukielimika, Wengine uwazatiti,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

10. Madili ya dini zetu, Yanaelekeza vema,

Tukijali ndoa zetu, Kondomu tutazitema,

Zaharibu wana wetu, Sasa wengi wana ngoma,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

11. Kanisa lapiga vita, Matumizi ya kondomu,

Salama mnayoita, Ni nyukilia ya bomu,

Ukimwi hautapita, Kwa sababu ya kondomu,

Siyo tu yausambaza, ni kinu cha kuzalilisha

12. Kwa kutumia mpira, Haiwezi kuwa kinga,

Kwa shetani ni kafara, Na Yesu tu ndiye kinga,

Mungu hapendi kafara, Za shetani ni ujinga,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

13. Huu ni mfano wa Musa, Lichonga nyoka wa shaba,

Kwa wa Ukimwi mkasa, Tazama nyoka wa shaba,

"Kondomukimwi" ni misa, Na wa shetani swahiba,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha

14. Kama bado hujaoa, Wewe mtazame Yesu,

Vionjo atavitoa, Ukiwa ndani ya Yesu,

Mzima ukijitoa, "Kinga- Salama" ni Yesu,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

15. Kweli taweka huru, Mtakuwa huru kweli,

Ndivyo Yesu kaamuru, Naye ni njia na kweli,

Yesu kawaweka huru, Mtaujua ukweli,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

16. Ndivyo ninavyoishia, Ijapo yamesalia,

Bado nakukumbushia, Yesu kumuangalia,

Siyo nimekutishia, Soma pia Biblia,

Siyo tu yausambaza, Ni kinu cha kuzalisha.

Emmanuel Anthony Mmbando,

St. Gabriel’s Parish-Burka

Box 7591

Arusha.

Mwenyezi Tumrejee, Apate kutuokoa

1. Wasi wasi umetanda, Vita pili kutokea,

Wasiwasi umetanda, Maradhi yatunyeshea,

Wasi wasi umetanda, Ubakaji umeenea,

Mwenyezi tumrejee, Apate kutuokoa.

2.OAU Iling’aa, Ukombozi tukatwaa,

Pinda pindua sheria, Wenyewe twagombania,

Upendo ukazimia, Tamaa njaa katua,

Sasa tu mwana mpotevu, Twapaswa kumrejea.

3. Ni nani alotugea, Hapa tulipofia,

Twatamba twajivunia, Sayansi Teknolojia,

Msomi kumzidia, Kompyuta aulizia.

Mwenyezi tumrejee, Apatye kutuokoa.

4. Shingoni yameishatua, Nani tunamlilia,

Kusali twapuuzia, Mitume twapuuzia,

Maradhi yametujaa, Twashindwa kuyatibia,

Sasa tu mwana mpotevu, Twapaswa kumrejea.

5. Kumi alitugawia, Amrize ndo sheria,

Tukacheza zichezea, Sasa zimetupindua,

Nani atayatatua, Haya yanayotunyeshea,

Mwenyezi tumrejee, Apate kutuokoa.

6. UN kutwanzishia, Ili amani kulea,

WHO tukaongezea, Maradhi kuyafukia,

FAO haikukawia, Njaa kiti kuondoa

Sasa tu mwana mpotevu, Twapaswa kumrejea.

7. Kumbe sote twamjua, Ni Mola alotugea,

Karama vipaji pia, Hivi tunavyotumia,

Leo kutomheshimu, Dhambini tumezamia,

MWENYEZI TUMREJEE, APATE KUTUOKOA.

Na Edmundus Mtes

Magomeni Parish,

Dar-es-Salaam

Utamadunisho wa Tambiko

1. Mungu Baba tupe jaha, Tuiunde fani yetu,

Iundwe kwa ufasaha, Afaidi kila mtu,

Njoni tuwape nasaha, Motomoto si fukutu,

Kristo tumaini letu, Salamu twawasalimu

2. Muhimu tutatungia, Nyote mpate faidi,

Ya kiroho kunenea, Hayo kwenu yawe udi,

Nyoyo zipate nukia, Maisha yawe na sudi,

Pande zote karibia, Uhondo pate faidi

3. Tambiko neno kunena, Linenwe na lineneke,

Lisije pata tatana, Kwa wote lieleweke,

Twalichambua kwa kina, Tuyaondoe makeke,

Tambiko neno tambiko, Si budi kulitambua.

4. La kipagani tambiko, Nia kusibu maisha,

Wengi kukosa mwamko, Wa kiroho kuboresha,

Miungu kwao tamko, imani kuififisha,

Tambiko la kipagani, Ni chukizo kwa Mwenyezi.

5. Ijue Ekaristia, Mwili na Damu ya Bwana,

Sadaka ilotimia, Ya Yesu wa Mungu Mwana,

Kila tunapotolea, Twaupata Uungwana,

Ekaristi Sakamenti, Futa tambiko pagani.

6. Lengo sadaka kutoa, Ni kumtukuza Mungu,

Pia kumshukuria, Kwa pendole la Kimungu,

Na nema kujipatia, Tupateiona mbingu,

Twaeni kuleni nyote, Twaeni kunyweni nyote.

 

7. Kweli ni tambiko jema, lile la Ukiristo,

Kutupatia Neema, Roho kupata mwamko,

Tambiko liso gharama, Kwa wote likawa fiko,

Inatosha ‘Karisiti, Acha kuchinja mbuzio.

 

8. Hapa twaitua nanga, Ufukoni tunatua,

Ya tambiko tumelonga, Mpate kuelimika,

Waliya-amba wahenga, Chenye kichwa kimkia,

Tambiko la kipagani, Kwa heri meza talaka.

 

Vijana Wafanyakazi Wakatoliki,

Parokia ya Itigi,

Jimbo Katoliki la Singida,

S.L.P.

SINGIDA