Make your own free website on Tripod.com

Hongera Rais Mkapa kwa mpango wako wa elimu lakini....

OKTOBA 31 mwaka huu, wakati akihutubia taifa kama ulivyo utaratibu aliojiwekea, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, alitoa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya msingi kwa miaka 2002 - 2006.

Katika hotuba hiyo, Rais alisema mambo mengi yanayohusu uboreshaji wa elimu ya Msingi na Sekondari nchini.

Alizungumzia vipengele mbalimbali vya uboreshaji wa elimu kama vile Serikali ili kuongeza bajeti ya sekta ya elimu, mchango wa wananchi kuhusu uboreshaji wa elimu, ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa, uandikishaji wa watoto kwa ajili ya elimu ya awali, msingi, sekondari ya kawaida na elimu ya juu ya Sekondari na vyuo.

Vile vile Rais Mkapa hakuacha kuzungumzia suala la uboreshaji wa mazingira ya kusomeshea watoto.

Tunapenda kumpongeza Rais wetu kwa Mpango huo mzuri na mzito katika kuboresha elimu katika taifa letu.

Siyo siri, elimu ya watoto na vijana wetu ilikuwa katika hali mbaya na karibu kila Mtanzania mwenye uchungu na nchi yake alikuwa katika masikitiko makubwa.

Lakini Kulikuwa na wakati fulani ambapo ulimwengu ulikuwa ukitusifia kwa sababu ya jitihada zetu za kuboresha elimu na hata kuondoa au kupunguza ujinga katika taifa letu. Lakini mambo yakaenda vibaya na hata tumekuwa na watu wengi katika taifa letu wasiojua kusoma wala kuandika licha ya watu hao kuwa matajiri wa maneno.

Kama walivyodokeza wananchi mbalimbali kuhusu mpango huo, ni kweli mpango mzuri, lakini ni mgumu kutosha kwani unahitaji sana utendaji na uwajibikaji wa hali ya juu.

Mpango huo utafanikiwa ikiwa kila mhusika anatimiza wajibu wake sawa sawa. Ni kutokana na uzoefu wa utekelezaji wetu, wananchi wengi wamekuwa na mashaka hasa na wenye kushika hatamu katika suala hilo la elimu.

Hata hivyo, tunaamini kwamba kutakuwa na mafanikio kwani Mkuu akitoa tamko ni sharti litekelezwe ipasavyo na kwa kadiri ilivyokusudiwa.

Watanzania tumeambiwa kwa miaka yote hii kwamba tunao maadui wale watatu: ujinga, maradhi na umaskini.

Tungeweza kusema kuwa mama wa maadui hao ni ujinga kwani ikiwa mtu ana elimu, basi ataweza kabisa kushindana na adui, maradhi pamoja na huyo adui umaskini.

Hali zetu Watanzania zimekuwa duni kutokana na ukosefu wa elimu, na hasa elimu bora.

Wako wananchi wengine ambao huthamini mambo ya mifugo kuliko elimu. Hali hii huwafanya kutokuwa tayari kuwapeleka watoto wao shuleni. Kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kuwasadikisha watu hao ili watambue kuwa na mifungo mingi bila kuwa na elimu bado ni umaskini mkubwa ungalipo.

Kuna watu wengi waliobahatika kupata mali kwa njia wanazozifahamu wenyewe, lakini hajui kusomo na kuandika bali hutumia tu akili ya kuzaliwa. Hivyo mara nyingi mali hizo hupotea na baadaye huwa maskini kutokana na kutokujua kusoma na kuandika.

Kuna vijana wengi waliokosa elimu hata ile ya msingi na hivyo hufanya biashara ambazo hazina hesabu yo yote. Kwa mfano, utamkuta kijana anashinda akikimbia na vifuko vya plastiki vya maji ambavyo kusema kweli haviwezi kumletea faida yoyote ile.

Lakini, kwa vile hana kisomo hata kile cha msingi anaona kuwa anafanya kazi ya maana, kumbe ni kupoteza muda tu.

Tunaambiwa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha kwa binadamu. Tunapozungumzia kuhusu ulimwengu wa sayansi na tekinolojia, linakuwa ni jambo la kichekesho ikiwa katika nchi yetu hii kuna vijana wengi ambao hawakwenda shule.

Rais Mkapa katika hotuba yake hiyo alisema kuwa kama kuna kitu kizuri ambacho tunaweza kuwarithisha watoto wetu ni elimu. Amesema kuwa unaweza kumrithisha mtoto wako mali,iwe ni fedha, mifugo , mashamba, nyumba au magari lakini kwa dunia ya leo, bila elimu anaweza kuishia kwa kufedhehesha jina lako anapokuwa mtu mzima.

Jambo hilo limeshatokea kwamba kuna watu wamewarithisha watoto wao mali nyingi, lakini kutokana na ukosefu wa elimu, mali yote imepotea na wamekuwa maskini kabisa. Ni kama ule msemo tuliokuwa tukiusikia hapo zamani: kosa mali pata akili. Ukiwa na akili utaweza kutafuta mali kwa kiwangu chochote kile.

Tungeweza kusema kuwa Rais Mkapa amepiga la mgambo kuhusu elimu yetu. Sisi wananchi wote imetupasa tuitikie kwa hali na mali. Ingawaje mzigo mzito wa kuwaelimisha watoto wetu umo mabegani mwa walimu wetu, lakini wanahitaji msaada wa wananchi wote na hasa zile kamati za shule. Tunasema kuwa huo ni mwito ambao umetolewa na Rais wetu na hivyo haitakiwi kabisa kuufanyia mzaha, bali tushirikiane ili tuboreshe elimu kwa watoto wetu kwani huo ndio urithi hai kwa taifa letu la kesho.

AMECEA karibu Tanzania

1. Kuanzishwa AMECEA, furaha ya Tanzania,

Kuzaliwa AMECEA, wote tunafurahia,

Kwa kufika AMECEA, Shangwe ya Mtanzania,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

2. Baba yetu AMECEA,’welcome’ Tanzania,

Bendera inapepea, kukulaki Tanzania,

Jisikie u mlea, si tena ajinabia,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

3. Ewe baba AMECEA, mzazi wa JUMUIA,

Huka sasa chekechea, u mzazi twakwambia,

Umoja wapendelea, Ndogo Ndogo JUMUIA,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

4. Michango ya kuchochea, twaianza JUMUIA,

Ili upate pembea, kwetu hapa Tanzania,

Upate kuwa mbolea, kurutubu Tanzania,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA

5. Wamini twawachochea, watoe zao adia,

Na Watawa twanenea, Kanisa kulifalia,

Imani pate enea, popote payo dunia,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

6. Wamini wa ERITREA, karibuni Tanzania,

Wa KENYA ndugu walea, furahini Tanzania,

WAMALAWI mlo pea, mwimbe na WATANZANIA

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

7. Kwa nyuma nikirejea, nasalimu wa Zambia,

Nanyi ndungu wamecea, salamu ETHIOPIA,

Wote ndugu nasemea, karibuni Tanzania,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

8. SUDAN kamammea, karibia Tanzania,

Na UGANDA naongea, fika petu Tanzania,

Na TANZANIA hemea, ndugu zako andalia,

Wapokewa Tanzania baba yetu AMECEA,

9. Nchi zote AMECEA, hongera kutufalia,

Mema yenu yaenea, na ubaya kuzuia,

Magonjwa twayaombea, yapate yote fifia,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

10. Michezo ya kuhamasisha, ianze kujifunza,

Mashairi na Ngonjera, mwanze bila kuchelewa,

Wanyamwezi, Wasukuma, utamaduni watakiwa,

Wapokewa Tanzania baba yetu AMECEA.

11. Vyungu vya Ufipani, Wafipa tayarisheni,

Kitoto ngoma Kingoni, sasa hamasisheni,

Mwinamire msanii, leo jitupe hewani,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

12. Lipuoa Undendeule, zikazeni ngoma zenu,

Kamwe msilale lale, msimame penye kinu,

Muwe kama vile kwale, kwazo nyimbo hizo.

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA

13.Wasukuma fuga nyoka, onyesheni tamaduni,

Wagogo we Tanganyika, nyimbo zenu zitungeni,

Wamatengo msochoka, nyimbo zenu leteni,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

14. Msanii bwana Komba, mbwembwe zako tuletee,

Na Wakonongo wa Mpanda, nyimbo zenu mzilete,

Kila kabila twaomba, nyimbo zenu mzilate

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

15. Wasanii nyimbo za dini, tayarisheni miziki

Kwa vizuri zitungeni, kwa moyo uso wa chuki,

Wasanii sasa anzeni, kwa kuitunqa miziki

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA.

16. Asifiwe Yesu Kristu, AMECEA namaliza,

Na kwa ajili yao utu, sitaki kuleta giza,

Ninasimama kibantu, kwayo mimi kumaliza,

Wapokewa Tanzania, baba yetu AMECEA

 

 

Frt. Raymond N.S.K. Mlekwa OSS

(Masalakulangwa)

T.M.P, KIPALAPALA MATBAA

S.L.P, 314.

TABORA

Wimbo Niupendao, uambatane na Nota

Getruda ulitubunia, Chuo umeelekea,

Neema umemwachia, Wimbo anatuwekea

Apanda auchagua, Neno lausimulia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Utaja kuutambua, Pale ukijiimbia,

Maana hukujia, Na utafurahia,

Nota kutokuwekea, Huwezi kujiimbia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Shinani tungeanzia, Hili kulikumbushia,

Kwaya wanatuimbia, Bila nota kuzijua,

Ndipo kuiga igia, Kunapojitokeza,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Waweza kujionea, Wimbo mpya ukitoa,

Wale nota wasojua, Sauti waulizia,

Taaluma inadumaa, Bendi nota kutojua,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Mimi nawashangaa, Wana muziki wa Daa,

Muziki watutolea, Si wa Kimtanzania,

Enzi tulijitambia, Japan watutambua,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Mbaraka kumbukia, Volkano iling'aa,

Balisidya twamjua, Afro sabini ilifaa,

Na Tabora Jazz pia, Wakongo wamuulizia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Waweza tajirikia, Wimbo ukijiimbia,

Maiko twamtambua, Tajiri kwa kuimbia,

KIONGOZI watwekea, Tupate kujifunzia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Mbali na ya Biblia, Uchovu kuuondoa,

Changanya changanyizia, Nyimbo za bendi za Daa,

Tamaduni zingatia, TOT Muungano pia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Wino walega legea, Karatasi zaishia,

Machache hayo pokea, Mengine nayaandaa,

Mzidi kutubunia, Nasi tutakuchangia,

Wimbo huo upendao, Uambatane na nota.

Na Mtima Mtema Mtes,

Parokia ya Magomeni,

Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.