Make your own free website on Tripod.com

Shule za kimataifa: Ubora wa elimu si kujua Kiingereza pekee,

HIVI sasa nchini, kumeanzishwa shule nyingi tangu za awali, msingi na hata sekondari. Miongoni mwa hizo, nyingine zimepata hadhi ya kusajiliwa na kuitwa na kujulikana kama shule za kimataifa (international schools).

Mfumuko wa shule nyingi bila kutegemea zile za serikali pekee, sisi tunauita ni maendeleo kwa taifa hasa katika sekta hii muhimu ya elimu.

Hata hivyo, haitoshi kusema tu, kwamba taifa limepiga hatua kielimu kwa kuwa na shule nyingi pekee, bali kama shule hizo zitakuwa zinatoa elimu kwa kiwango cha ubora kinachotarajiwa.

Tunasema hivi kwani tunajua dhahiri kuwa licha ya wingi wa shule hizi zinazojiita za kimataifa, bado baadhi yake zinatoa elimu isiyokidhi kiwango cha mahitaji ya ubora unaokusidiwa kutolewa kwa wanafunzi wa shule hizo.

Ukweli huu unajidhihirisha katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi ambapo wengi wa wanafunzi wanaofaulu kuendelea na masomo ya sekondari wanatoka katika shule za kawaida na hizo zinazojiita za kimataifa huku zikitoza ada ya juu, zikitoa wanafunzi wachache.

Tunaamini kabisa kuwa wakati wa usajili, shule hizi hukubaliana na Serikali kuwa zitatumia mitaala ya kimataifa katika utoaji wake wa elimu.

Inasikitisha mno kuwa bado baadhi ya shule za kimataifa, licha ya usajili wake, zinatumia mitaala inayotumiwa na shule za kawaida na hali hii ni wizi ambao hauna budi kukemewa na kila mwanajamii .

Kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwamba baadhi ya shule hizo zinaweka mbele maslahi ya pesa bila kujali kiwango cha elimu, ni ya kweli kabisa na haiwezi kupita bila kuungwa mkono.

Kinachotushangaza zaidi na hata kutusikitisha, ni hali ya wamiliki, wakuu wa shule, walimu wakuu na walimu wengine katika baadhi ya shule za kimataifa, kudhani na hata kutaka kuwaamrisha wazazi na wageni wanaozitembelea kuwa ubora wa shule au kiwango cha ubora wa elimu, ni kujua kuongea Kiingereza.

Dhana hii ya kupima ubora wa elimu kwa kigezo cha kuongea Kiingereza, ni batili na isiyostahili kutiliwa maanani na ni kwayo, hata wazazi wengine wameshawishika kupoteza maelfu ya pesa kuwapeleka watoto wao nje ya nchi wakidhani huko watapata elimu bora.

Matokeo ya hali hiyo ni vijana kurudi katika shule za kawaida hapa nchini wakifanya vibaya katika mitihani yao ingawa wanakuwa na uwezo wa kuongea Kiingereza ambacho sasa hukigeuza kuwa mradi wa "kusumbulia mitaani."

Hatujui kwanini walimu wa shule kama hizo na wazazi wa namna hii, wanatumia kigezo hicho cha kuongea Kiingereza, hawaangalii pia masomo mengine.

Ndiyo maana sasa katika international schools hizo,kinachofanyika ni wafanyakazi wa shule hizo kuweka matangazo na mabango mbalimbali na mchoro kwenye kuta za madarasa ili kuwaonesha wazazi ama wageni wanaozitembelea huku wakiwashawishi kuamini kuwa, yaliyochorwa kwenye kuta na mabango hayo, ndiyo yanayofundishwa.

Ni kutokana na dhana hiyo duni ya kuamini Kiingereza kama kipimo cha ubora wa elimu, ndiyo maana wanapotembelewa na wageni walimu huwachukua wanafunzi wanaojiweza kwa lugha hiyo ya kigeni kama mfano kwa wageni.

Sisi tunasema kuwa ni vema kama shule hizo zinataka kuthibitisha ubora wake, zitumie masomo yote na kuwaachia nafasi wageni kuchagua ama kuteua wanafunzi wa kuzungumza nao bila kuwapa wanafunzi nafasi ya kujiandaa kujibu maswali ya kukariri waliyoandaliwa na walimu.

Tunajua shule zote zina masomo zaidi ya moja; sasa, iweje Kiingereza pekee ndicho kitumike kupima ubora wa elimu.

Sisi tunaamini kuwa wanaofanya hivyo, wanafanya kwa lengo la kujizolea sifa wasizostahili na hivyo kuvutia biashara katika shule zao.

Kwa vile serikali kupitia Wizara ya Elimu na Utamaduni ndiyo mtoaji wa vibali vya usajili kwa shule hizo, basi haina budi kufuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa shule husika.

Zitakazobainika kwenda kinyume na makubaliano na matarajio, zichukuliwe hatua za kisheria bila kujali dini, jinsia, kabila, cheo wala kundi la wamiliki wake kwani zinachafua majina ya shule nyingine zinazofanya vizuri.

Vijana tuwajibike

Ndugu Mhariri,

NAPENDA kuchukua nafasi hii kutoa maoni yangu machache kuhusu vijana wenzangu .

Kama inavyoeleweka taifa lolote lile, huwategemea vijana kwa shughuli zake za maendeleo.

Kutokana na hilo, vijana hatuna budi kujitahidi kutumia ujana wetu kulijenga, kuliimarisha na kulilinda taifa letu.

Ukiachilia mbali taifa kututegemea, pia Kanisa linatutegemea sisi vijana katika kukuza, kuendeleza na kueneza Habari Njema mahali kote tunakoishi.

Tusitumie muda wetu katika kupenda anasa na kujiingiza katika vitendo viovu vikiwemo vile vya utumiaji wa dawa za kulevya.

Matatizo mengi yanayowakumba vijana yanatokana na matumizi ya dawa hizi na kupenda anasa.

Ni lazima vijana tukumbuke kuwa dawa za kulevya na starehe sio njia sahihi na iliyobora kwa vijina.

Tujitahidi kufanya kazi kwa bidii na kujinyima starehe zisizokuwa na lazima.

Katika Maandiko Matakatifu tunasoma kuwa Bwana Yesu alisema "Msiwe na wasiwasi juu ya maisha yenu, mle nini, mvae nini, Baba Yenu wa Mbinguni anajua yote kabla ninyi hamjamwomba."(Mt.6.25) Kumbe basi vijana wenzangu tusishughulikie sana mambo ya mwili kama vile mavazi, chakula, starehe na mengine kama hayo kwani Baba Yetu wa Mbinguni anajua mahitaji yetu.

"Ombeni mtapewa, tafuteni mtapata, bisheni hodi nanyi mtafunguliwa (Mt. 7:7)" .

Jambo la msingi kwa vijana wenzangu ni kumwomba Mungu atupatie nguvu ili tufanye kazi za kuleta maendeleo ya taifa badala ya kutumia nafasi na muda wetu katika masuala ya utumiaji wa "madawa" ya kulevya na starehe za kupita.

Perpetua Damas

P.O. Box 6202

Dar Es Salaam

Jamani!Heshimuni Ibada,Misa Takatifu

Mhariri KIONGOZI

NAOMBA unipatie nafasi katika gazeti lako ili niweze kutoa maoni na masikitiko yangu ambayo yamekuwa yakinikera kwa muda mrefu.

Inasikitisha sana baadhi ya waamini kupageuza kanisani kama mahali pa kupigia porojo.

Nasema hivyo kwa vile nimeshuhudia kwa macho yangu katika makanisa mbalimbali watu wazima na akili zao,wanashindwa kusikiliza mahubiri yanayotolewa na Padre ama Mchungaji wakati wa Ibada ya Misa Takatifu.

Utakuta wao wanachofanya ni kupiga stori tu (sana sana huwa ni kakikundi kadogo ka watu wawili hadi wanne) na kibaya zaidi wakati mwingine hata hujisahau na kuanza kugongeana mikono.

Kundi linalohusika zaidi ni la vijana sana sana wasichana ambao hata wakati mwingine huchukua vioo vyao na kuanza kujiangalia.

Inapotokea msimamizi wa kanisa pengine alionye kundi hilo,bila aibu hujibiwa maneno ya kutisha na kukatisha tamaa.

"Wewe fuatilia lililokuleta hapa kanisani, achana na sisi kwani hatujui tumekuja kufanya nini",wanasema kwa kebehi.

Nachukua fursa hii kuwataka wale wote wenye tabia kama hii wajirekebishe mara moja na badala yake wamrudie Mungu.

Kama umeenda kanisani kuomba na kusali, basi hakikisha unafanya hivyo na siyo vingine.

Muumini Mtiifu

J.Katikilo

Dar-Es-Salaam.

Wapiga debe mjirekebishe

Ndugu Mhariri,

Tunaomba utupe nafasi katika gazeti lako la KIONGOZI linalongooza kwa habari zake za kweli.

Tunaomba nafasi hii tuitumie kutoa yetu machache katika mengi tuliyonayo. kwa leo tungependa malalamiko yetu yafike kwa vyombo husika na vichukue hatua kali zaidi kwa hawa watu wanaoitwa "wapiga debe" katika vituo vya daladala hapa jijini Dar-Es-Salaam.

Watu hawa pamoja na kupata "kula" yao kwa kazi hii ya kupiga debe katika vituo vya daladala, wamekuwa kero kubwa kwani wakati mwingine hufikia hatua ya kuwakanyaga na kuwasukuma abiria.

Kana kwamba hiyo haitoshi, ,wapiga debe hao wapo tayari hata kutoa lugha chafu ya matusi kwa abiria hao.

Mara nyingi hali kama hii inatokea pale abiria anapokataa kutii amri ama matakwa yao kwani wakati mwingine bila kujali kama gari limejaa,wapiga debe hao huwalazimisha abiria kujazana kwa kuwaambia maneno kama "ingia ndani chombo kiondoke; bado watu wanne".

Achia mbali hilo,tatizo lingine ni pale wapiga debe hao wanapowakataza wanafunzi kutopanda kwenye gari. Watu hawa ni waajabu katika jamii yetu ya Kitanzania ambayo imejengwa katika misingi ya umoja na upendo wa kuthamini utu wa mtu.

Kwa nini ninawaita watu wa ajabu, sababu ipo. Kwanza sijui kama wao walitokea wapi kwa safari ya kuja hapa katika sayari tunayoishi maana kama walizaliwa kwa njia ya kawaida inayotambuliwa na kila binadamu, ni lazima walipitia katika hatua za utoto zinazohitaji kutunzwa na kusaidiwa, ila kwa sababu zao wanazozijua inawezekana wamesahau walikotokea. Kama ndivyo basi tunaomba vyombo husika viwakumbushe si kwa maneno tu ila sheria ishike mkondo wake kwa kuwafunza na kuwapa adhabu hadharani kwa kuzingatia kwamba hawa watoto ndio taifa la kesho.

Tudhibiti hali hii mapema maana hata wahenga walisema asiyefunzwa na mamae (wazazi) hufunzwa na ulimwengu pia wakasema samaki mkunje angali mbichi

Ni wazazi wenye kukereketwa,

Ubungo Kiswani,

Dar-Es-Saalam.