UKIMWI unaua, kwa nini tucheze na hatari?

MAANDIKO Matakatifu yanatuambia kuwa umri wetu sisi binadamu wa kuishi hapa duniani ni miaka sabini (70) na tukiwa na nguvu zaidi ni miaka themanini (80). Lakini mambo yanavyokuwa siku za leo na hasa katika nchi yetu ni tofauti mno. Tunaona watu wengi na hasa vijana ambao hawajafikia miaka arobaini wanakufa kwa wingi sana.

Kuondoka kwa kundi hili la watu wenye umri mdogo kunapoteza ile tunayoiita "nguvu kazi".

Maisha ya binadamu hutoweka kwa njia nyingi kama vile maradhi, ajali na ile ya kawaida ya uzee. Tunatambua kuwa magonjwa kama vile malaria, kipindupindu, kifua kikuu, na maradhi mengine ya tumbo yamekuwa ni ya kawaida na yana tiba zake. Lakini kuna huu ugonjwa mbaya uliojitokeza miaka ya hivi karibuni, unaojulikana kama UKIMWI, ni wa hatari sana kwa vile hauna kinga wala tiba. Wataalamu wamejitahidi sana kutuletea dawa za kupambana na magonjwa hayo mbalimbali,lakini kwa bahati mbaya gonjwa hilo la UKIMWI halina tiba yoyote mpaka hivi sasa.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona watu wengi ambao hawajatoa mchango wowote wa maendeleo katika taifa letu wanakufa katika umri mdogo sana. Serikali na vyombo vingine katika taifa letu imejitahidi sana kuwaelimisha wananchi kuhusu ubaya wa ugonjwa huo.

Kumekuwa na mashirika ya kimataifa ambayo yamejitolea kwa hali na mali katika kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huo wa UKIMWI. Viogozi wetu sasa hivi wanaimba wimbo huo kila mahali katika kuwaangalisha wananchi na hasa vijana kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.

Hivyo pia hata mashirika ya kidini hufanya kila jitihada ya kuwaangalisha wananchi katika kujiepusha na ugonjwa huo wa kutisha. Mbinu mbalimbali zinabuniwa katika kujikinga na ugonjwa huo, kwa vile hauna tiba bado. Kwa vile ugonjwa unaoua siyo siri ya watu wachache au wa rika fulani tu, basi kila mahali hata huko mashuleni wanafunzi wanafundisha kuhusu maana ya ugonjwa huo na tahadhari zake.

Kumetangazwa njia nyingi na mbinu mbalimbali za kuepukana na ugonjwa huo. Kwa vile imebainishwa kwamba njia kuu kabisa ambayo watu wengi huupata ugonjwa huo ni ile ya kukutana kimwili au kujamiiana, basi mkazo mkubwa sana umetiliwa katika kuwa waangalifu katika vitendo vya mapenzi.

Kuna methali isemayo kuwa ukiona mwenzako ananyolewa, basi ujue kuwa itafika nawe zamu yako, kwa hiyo tia maji nywele zako. Maana ya methali hiyo ni kwamba unapaswa kujikinga na kujitetea unapoona ndugu yako yuko katika shida. Ni jambo la kusikitisha sana kuona wananchi wengi sana hawashituki kabisa na hawataki kabisa kubadilisha mienendo na tabia zao mbovu za kufanya mapenzi ovyo ovyo. Hakuna asiyetambua kuwa karibu kila familia siku ya leo ina marehemu ambao wamekufa kutokana na ugonjwa huu wa UKIMWI. Na kwa asili mia kubwa ni kutokana na kufanya matendo ya mapenzi ovyo ovyo.

Inashangaza kuona jinsi binadamu alivyo shupavu katika jambo hilo licha ya kushuhudia vifo kila siku. Takwimu kuhusu ugonjwa huo wa UKIMWI ni kubwa mno na zinatisha sana.

Ni kweli kuwa tendo la kufanya mapenzi limo katika sirika la binadamu, lakini papo hapo tunatambua kuwa matendo yote ya binadamu huongozwa na akili pamoja na utashi. Kwa hiyo binadamu lazima aulinde uhai wake kwa kutumia akili yake na utashi wake. Inapotokea kuwa binadamu anatawaliwa tu na tamaa zake za mwili na hivyo kufuata vionjo vyake bila kutumia akili na utashi wake hapo huwa ni vigumu sana kumtofautisha na kiumbe mwingine.

Binadamu kila tunapoona kuwa mbele yetu kuna hatari kubwa, basi hapo inatupasa kuchukua tahadhari kubwa zaidi. Lakini tunaposikia kuwa jambo hilo linachukuliwa kuwa ni bahati mbaya au "ajali kazini", hapo tunakatishwa tamaa kweli kweli.

Kuna mambo mengi sana ambayo husababisha watu wafanye mapenzi ovyo ovyo. Mojawapo ni ‘ULEVI’ wa pombe. Tunavyofahamu ni kwamba mtu akishalewa hupoteza nguvu zake ya kujitawala na kujishinda katika mambo ya kijinsia. Kwa mtu aliyelewa tamaa za mwili huamka upesi na hasa ikiwa mtu wa jinsia nyingine yuko karibu naye na pengine kwa hali ya kuvuta tamaa. Watu wengi hufanya mapenzi katika hali ya ulevi. Kwa hiyo ni sharti kujiangalia kwani ni lazima kabisa kukwepa mazingira yenye kumwingiza mtu katika kutenda mambo mabaya. Kuna watu wengi wanaosujudu ulevi wa kupindukiwa na hivyo wanafanya mambo ya mapenzi bila aibu, na mapato yake ni kupatwa na magonjwa, hasa ugonjwa huu wa UKIMWIi.

Licha ya ulevi wa pombe, lakini pia kuwa jambo jingine linalowafanya watu wengi wafanye mapenzi kutokana na utajiri pia umaskini. Wengi wanasema kuwa kuna watu maskini na watu matajiri ambao wanakufa kutokana na mali walizo nazo na pia wengine kutokana na umaskini walio nao. Kumbe wanaokufa kutokana na ugonjwa huu wa UKIMWI ni wale wenye utajiri kwa sababu utajiri huo unawavuta na kuwadanganya akina mama wengi na hasa wasichana. Pia hao akina mama au wasichana hudanganyika kutoka na umaskini wao na kuwa tayari kupata misaada yenye masharti kutoka kwa hao matajari na watu wenye uwezo.

Hapo jambo linalotakiwa ni kutumia busara kwa yule mwenye mali na vile vile kwa yule ambaye hali yake ni mbaya kifedha.

Tunaambiwa kuwa siyo kila kinachong’aa ni dhahabu, yaani siyo kila mtu anayependeza machoni au mwanaume au mwanamke, basi ni safi pia ndani ya mwili wake. Kumbe inafaa kabisa kujihadhari ni urafiki wowote ule siku hizi. Tutumie ile kanuni ya wanausalama kuwa tusimwamini mtu ye yote na tumtilie mashaka mtu ye yote katika jambo hili la mapenzi, kwani hakuna uhakika wa usalama. Ni kweli kuwa kila dini inakataza kabisa mambo ya kufanya mapenzi nje ya ndoa na kushika hilo tutakuwa salama kabisa. Tusicheze na hatari, kwani UKIMWI unaua. Kila siku tunashuhudia vifo kutokana na ugonjwa huu, tujiepushe na hatari hizo kwani miaka yetu ya kuishi ni sabini na hata themanini. Hapo tutakuwa tumetoa kweli mchango wetu wa maendeleo katika taifa letu.

Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Rais

MHESHIMIWA Rais, nakusifu sana kwa sababu umekuwa msomaji mzuri wa magazeti na nadhani nitumie njia hii kuongea nawe ili ujue kwanini watendaji wa vijiji na Kata tunakula rushwa.

Ni aibu, unafiki na kasoro kubwa nikisema kuwa, watendaji hatuli rushwa, lakini pia, ni dhambi tukifikiri na kuwashtumu watendaji "Eti" wote wanakula rushwa.

Mheshimiwa Rais, ninayekuandikia barua hii ni Afisa Mtendaji halisi wa KATA katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Na bila woga, ninataka nikujulishe ni kwa nini sisi watendaji wa kata na vijiji na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, tunakula Rushwa.

Kwanza kabisa, ni kutokana na kutolipwa mishahara yetu. Sijui kama una taarifa kwamba sisi watendaji wa kata 41 na VEOS yaani maafisa watendaji wa vijiji 150, hatujalipwa mishahara toka mwaka 1999 Desemba hadi Machi 2001.

Pili, kuhamishwa bila malipo. Tangu niajiriwe mwaka 1992, nimehamishwa zaidi ya mara nne, katika vituo mbalimbali bila kulipwa gharama zozote husika katika zoezi hili la kuhamishwa.

Mheshimiwa Rais, hivi unafikiria nini mtumishi wa raia anayetakiwa awaongoze watu akiwa ametulia akili awe hana fedha, ana njaa, anayo familia kubwa na anasomesha watoto, anayetakiwa awe mfano bora na mtawala; halafu hana hata kiatu.

Akili yangu yote ni njaa tupu; kodi ninakusanya, maendeleo ya wananachi nasimamia; kulipwa, silipwi.

Nikienda kudai, naambiwa ukiona Halmashauri haikulipi, acha kazi!.

Nahamishwa silipwi kama mtumishi wa serikali, je, wewe unafikiri katika mazingira magumu kama hayo, nitaacha kula Rushwa?

Mheshimiwa Rais, mtendaji mbele ya watu hana heshima kabisa, vaa yake ovyo, nyumba yake yote njaa tupu, mtawala asiye na Pesa! Kila leo ni omba omba.

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ni kati ya Halmashauri zinazoingiza pesa sana; lakini ndiyo Halmashauri mbaya kwa utumishi kuliko zote.

Mheshimiwa Rais, uliza ni kwa nini watumishi wa hapo Makao Makuu (Halmashauri) hata wafagiaji tu wanajenga nyumba nzuri tu na wengine wanayo magari lakini shangaa mimi mkusanyaji sina hata baiskeli.

- Hebu angalia nyumba anayoijenga Mkurugenzi na Afisa Utumishi wake ni ya mamilioni ya fedha.

- Angalia jengo la Halmashauri linalojengwa ni la mamilioni ya fedha, lakini sisi hatuna mishahara kwa nini hilo jengo lisingesubiri ili tulipwe mishahara kwanza.

- Hebu jiulize ni kwa nini Mkurugenzi anunue gari la milioni zaidi ya 40 wakati hatuna mishahara.

- Watendaji wa vijiji tu wanadai zaidi ya milioni 60. Mheshimiwa tunajuwa kuna rushwa inayoombwa kwa sababu ya tamaa tu; lakini kwetu sisi hatuna njia na tumeamua kuufufua ule msemo usemao kuwa Mbuzi hula alipofungwa.

- Vikao vya madiwani viko rundo na vinalipwa vyote na vikao vikianza tu, tunaanza kukoromewa kwa maagizo ya kukusanya malaki ya fedha na tuziwasilishe bila matumizi.

- Mheshimiwa Rais mimi kama mtendaji wa kata au kijiji kazi yangu si kukusanya kodi tu ! hii ni dhana potofu tuna kazi nyingi sana ambayo ni ulinzi na usalama na uratibu na usimamizi wa shughuli za maendeleo za kila siku ambazo zitawaletea tija wananchi. Lakini mwajiri wangu yeye anachokazania ni kodi tu na hata nikifikisha malengo bado mishahara silipwi.

- Mfano: Ni katika kijiji fulani ambacho VEO ana takiwa akusanye Tshs 3,700,000.00 (milioni tatu na laki saba), amekusanya shilingi (3,200,000(milioni tatu na laki mbili) lakini amelipwa shilingi 142,242 yaani mishahara mitatu tu!!.

- Kama hakuna haki bila wajibu vile vile hakuna wajibu bila haki na kuchelewesha haki ni kunyima haki.

- Mheshimiwa Rais chanzo cha rushwa kwa watendaji wa Halmashauri ya Tarime si watendaji au tamaa bali ni Halmashauri yako. Hebu wewe jiulize nitaishije na kila siku niko ofisini? Hivi nitaendelea kujihamisha kwa gharama zangu mpaka lini?

- Mheshimiwa Mkapa hili halina haja ya kufanya uchunguzi au kuwa ni majungu hata ukipiga simu kwa DC wako atakueleza kila kitu ingawa atakuficha mambo mengine mengi ya msingi.

- Tumevumilia tumeshindwa tulidhani mvumilivu hula mbivu kumbe hula mbichi na kuwa wizara ya serikali za mitaa iko ofisini kwako; tunatarajia mabadiliko makubwa sana na ya kutusaidia sana sisi WEOS na VEOS hasa wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Ni Mtiifu Na Mtumishi wa Halmashauri Wilaya ya Tarime

Ikoshimyo N’kebhondo

Halmashauri ya Wilaya

Tarime.

Shairi

Waamini tusali Rozari

1. U- wapi mama Maria, Wanao twakulilia,

Salamu zetu pokea, salamu mama maria,

Farajazo twanyatia, zidi kutuandalia,

Mwezi tano wa Rozari, waamini sali Rozari.

2. Sifa tunakutolea, pongezi twakutumia,

Salamu zetu pokea, Mkombozi kumzaa,

Kateswa kutukomboa, ya pili twamgojea.

Mwezi tano wa Rozari, waamini sali Rozari.

3. Ya pili alipokea, nasi akatugawia,

Rosari twajisalia,Neema twajichotea,

Utakatifu Maria, Twasali Twaulilia,

Mwezi tano wa Rozari, waamini sali Rozari.

4. Dukani- ko elekea, Rozari yako nunua,

Kasisi atapokea, Baraka kunyunyiza,

Shingoni utaivaa, sote tutafurahia

Mwezi tano wa Rozari, waamini sali Rozari.

5. Taratibu ni sheria, Kukwepa ndio udhia,

Maalumu nyakati pia, waweza kujisalia

Bikira Mama Maria, uzidi kutuombea ,

Mwezi tano wa Rozari, waamini sali Rozari.

 

Na Edmundus M.Mtes

S.L.B 25086

Dar-Es-Salaam