Make your own free website on Tripod.com

Watanzania: Umoja utufikishe katika kilele cha maendeleo

KATIKA makabila mengi hapo zamani na hata siku ya leo kuna ule utaratibu wa kufanya kazi kwa kushirikiana na kusaidiana.

Kuna maneno mengi yanayotumika katika kuelezea mtindo huo wa utendaji kazi. Kuna makabila kwa mfano huuita ushirikiano wa namna hiyo kama ‘mgowe’ au "mkwila’; wengine husema ni ‘harambee’, wengine huita ni "umoja" nk.

Hivyo, mara baada ya uhuru wa nchi yetu tulikuwa na ile Siasa ya Ujamaa, yaani watu kufanya kazi kwa kujitolea na kusaidiana.

Ni ukweli usiofichika kuwa nchi yetu ni maskini na licha ya pesa kidogo iliyonayo serikali, tunapaswa kufanya kazi kubwa na nyingi za kujitolea na kusaidiana.

Licha ya wafadhili kutusaidia kwa namna kadha zikiwamo kusamehewa madeni, ni wajibu wetu kutoa mchango wetu wa hali na mali katika juhudi za kuelekea maendeleo halisi.

Yapo majukumu na mambo mengi tunayopaswa kufanya kwa njia ya kushirikiana pamoja. Lakini, ni jambo la kusikitisha sana kuona watu wengine wengi, hawataki kabisa kuthamini wala kutilia maanani suala hili muhimu katika kupigania maendeleo ya jamii.

Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema hadharani akiwaaasa Watanzania kujua kuwa taifa letu hili litajenga na wenye moyo.

Lakini inashangaza na kusikitisha kuona kadiri siku zinavyopita, ndivyo wananchi wengi wanavyoonesha dhahiri kufa moyo wa kujitolea na kufanya kazi za maendeleo kwa njia ya kushirikiana na kujitolea.

Sisi tunasema hali hii ni hatari kwa maendeleo ya uchumi wa jamii yoyote tangu ngazi ya familia hadi taifa kwa jumla. Hivi ni nani asiyejua kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu? Au nani asiyejua kuwa kidole kimoja hakivunji chawa?

Kuna shughuli nyingi zisizohitaji pesa za kigeni na hata za nchini Tanzania. Kwa mfano, kuna majengo mengi katika shule ambayo yako katika hali mbaya. Kama wananchi wangeshirikiana kwa pamoja kutengeneza majengo hayo, hali isingekuwa mbaya kiasi hicho

. Ni jambo la aibu kuona leo watoto wetu wanasoma katika madarasa yasiyoeleweka kabisa au katika vibanda na hata pengine, chini ya miti. Mifano ni mingi.

Sehemu kubwa ya wananchi hawana mwamko wa kimaendeleo kabisa na ndiyo maana tunashuhudia jinsi nchi inavyozidi kuwa maskini.

Zipo sehemu nyingine zinazotia moyo sana kutokana na namna wananchi wanavyojitahidi kufanya kazi kwa kujitolea. hao tunawapongeza.

Tunasema hivyo kwani kuna baadhi ya vijiji ambako wananchi wapo mstari wa mbele katika kushirikiana kufanya kazi za kuwaletea maendeleo.

Wamekuwa mstari wa mbele kufanya kazi za pamoja kama kujenga shule, nyumba za walimu, zahanati, na hata kufanya kazi za kilimo kwa pamoja.

Kwao mtindo wa kila mmoja peke yake haupo, bali ni kwa kushirikiana kwani wanatambua kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kama wasemavyo fimbo ya mnyonge ni nguvu zake mwenyewe.

Watu wengi na hasa wageni husema kuwa Watanzania walio wengi ni wavivu na hasa wanaridhika na hali duni waliyo nayo.

Wako wengi wasiotaka kushiriki katika changamoto la maendeleo; iwe ya kibinafsi au ya kijamii. Kwa mfano, wapo wanaoridhika kuwa na vitu vichache kabisa na hata kuwa na mahali duni pa kulala sambamba na lishe duni waipatayo.

Sisi tunasema kuwa waliodumaa na wasio na tamaa ya maendeleo hawana budi kuamka na kuyasaka maendeleo kwa juhudi za makusudi wakizingatia kuwa njia muafaka ya kuwafikisha kileleleni, ni ushirikiano, juhudi na maarifa.

Tutafanya hivyo kwa njia ya kufanya kazi kwa bidii na kutumia maarifa tuliyonayo.

Hatupaswi kuridhika na maisha haya duni tuliyonayo. lazima tuige mfano wa wenzetu wa mataifa ya nje wenye kiu ya kuboresha hali zao kadiri kunavyokucha.

Linapaswa kuwa jambo la aibu na lakusikitisha kwa vijana kukimbilia mijini ambako hawafanyi lolote la maendeleo badala yake, wanajihusisha na vitendo vya uhalifu ambavyo ni kero na mzigo kwa jamii na taifa.Taifa linahitaji sana nguvu zao zitumike kuleta maenndeleo badala ya kutumika kupiga zogo vijiweni.

Mama Bikira Maria hachukui nafasi ya Yesu

Ndugu Mhariri,

Nitashukuru ukinipa nafasi ili nijibu barua ya Wales Mhina (Gazeti la Mwananchi toleo No. 00246, la 12/2/2001) kuhusu ombi la Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa Parokia kuombea amani kwa Mungu kupitia kwa Mama Bikira Maria.

Ninapenda kumfahamisha Mhina kwamba, tangu kuanzishwa kwake rasmi siku ile ya Pentekoste pale Yerusalemu, Kanisa Katoliki daima linafundisha kwamba hakuna mpatanishi mwingine kati ya Mungu Baba na sisi Wanadamu isipokuwa Yesu Kristo. Bikira Maria hachukui nafasi ya Yesu na hana mpango huo kwa sababu anaelewa vema mpango wa Mungu kuliko kiumbe yeyote na daima, hutekeleza mapenzi ya Mungu.

Hakuna sehemu yoyote katika ibada ya misa takatifu ambapo Padre anaomba kwa njia ya Bikira Maria.

Kila sehemu inayohusika Padre anaomba kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo anayeishi na kutawala pamoja na Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu Mungu daima na milele.

Huo ndio ukweli kuhusu kuomba kwetu na mwenye kudai kwamba tunaomba kwa njia ya Mama Maria kwa maana ya kumwekea kando mwanae, ni mwongo na mzushi na sote tunajua kwamba uwongo wote hutoka kwa yule mwovu, ibilisi.

Hakuna Mkatoliki anayeamini au kufundisha hivyo.

Ifahamike kwamba Wakatoliki tunapoomba kwa Mama Maria, lengo letu ni kwamba atufikishe kwa Mungu Mwana, Yesu Kristo ili atufundishe kwani Mungu Mwana na Roho Mtakatifu ni Mmoja (Yohana 17(22).

Maombi ya Mama Maria kwa mwanae yanaufikia Utatu Mtakatifu.

Hivyo, ndivyo tunavyoamini na tunawaomba wote wasioelewa, au kwa makusudi kabisa hawataki kuelewa jambo hili, watuelewe hivyo.

Kwa hilo, haturudi nyuma. Kristo kama alivyoahidi, Yohana 17(26), ametufumbulia mapenzi ya Baba yake ndani ya Kanisa lake aliloanzisha na kuliongoza kwa njia ya Roho wake.

Ili kusaidia kuelewa ukuu wa Bikira Maria katika Kanisa, tafadhali soma LK1(28);LK1(35) na LK1(41-43) na Yoh.2(3na 5).

Katika Lk.28, Mungu kupitia Malaika Gabriel, anasalimu Mwana Maria tena kwa unyenyekevu mkubwa kama ulivyooneshwa na Malaika Gabriel.

Maana ya tendo hili ni kwamba, sisi kama wafuasi wa Kristo, lazima tumsalimu huyo mama kama yeye mwenyewe alivyofanya. Ni Roho Mtakatifu kweli. Anayekuzuia kufanya kama Mungu alivyofafanya? Bila shaka ni Roho ile ya upinzani (mwa.3(15)

Na katika LK 1(35),Maria anazidi kupewa heshima toka kwa Mungu kwa kumteua kuwa Mama wa mwanae, kumfunika na nguvu zote za Mungu na kumjaza Roho Mtakatifu kwa kiwango cha juu.

Ikiwa Mungu mwenyewe ameamua kumkweza huyu Mama juu ya viumbe vyote, LK1(52b), sisi kama kweli tunamfuata Kristo, lazima tumpe Maria heshima ile anayopata kutoka kwa Mungu.

Kuhusu nguvu za maombezi ya Mama Maria kwa mwanae kwa ajili yetu, ninakuomba usome na kutafakari yaliotokea Kana ya Galilaya Yoh 2(3na 5).

Ili kuelewa vema ujumbe huu, chukua nafasi ya Bwana na Bibi harusi na wanafunzi wa Yesu.

Sasa, elekeza ujumbe huu kwako katika maisha yako au Kiroho.

Maana ya ujumbe huu ni kwamba kama Bwana na Bibi Harusi walivyofanya kule Kana. Hapa utaona pia kwamba, ingawa saa ya Bwana Wetu kuanzia kazi iliyomleta hapa duniani ilikuwa haijafika, Baba wa Mbinguni alimruhusu Mwanae kutekeleza ombi la Mama yake ili kuonesha anavyofurahia maombi ya Maria.

Hivi ndivyo Mama Maria anavyofanya daima kwa ajili yetu kutuombea kwa Baba wa Mbinguni kwa njia ya Mwanae na maombezi yake kwa mwanae kwani yana nguvu sana kuliko tunavyoweza kufikiria.

Maombezi kwa Mama Maria ni jambo la imani, jaribu uone. Hutapenda kuacha. Anachotaka Mama Maria kwanza, timiza mapenzi ya Mwanae halafu, nenda kwake.

Wako katika Kristo,

S.F.Kilato

Box 4011

Dar Es Salaam