Make your own free website on Tripod.com

Mipakani: ukarimu wa kuwagawia ardhi wageni unatoka wapi?

KATIKA suala zima la usalama wa taifa; mipaka, kambi za kijeshi, viwanda, masoko, hospitali na madaraja ni miongoni mwa vitu vilivyo muhimu kuzingatia.

Tunasema hivi kwa kuwa ni kwa hayo, usalama wa taifa unaweza kupotea au kuimarishwa kupitia katika sekta za uchumi, mawasiliano na hata ulinzi.

Hii italeta mafanikio pale tu, wananchi wenyewe; wa ngazi zote, watakapokuwa makini na wenye uchungu kabisa kuepuka kutawaliwa kwa misingi yoyote ile, iwe ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiulinzi.

Katika suala zima la ulinzi na usalama wa taifa, mipaka ni kitu muhimu kinachostahili wakati wote kukaa katika misingi ya udhibiti ili kila aingiae au kutoka nchini, ajulikane ni nani, anakwenda au kutoka wapi, kwa lengo gani na tayari ajulikane dhahiri amefanya nini huko atokako.

Endapo kila mwananchi atakuwa na uchungu wa kutaka kujua hayo katika misingi ya usahihi kwa anayetoka na kuingia nchini, kwa kiasi kikubwa atakuwa ameshiriki katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yake.

Tunasema hivyo kwa kuwa yaliyosemwa hivi karibuni mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime; na walinzi na mabaraza ya jadi katika tarafa ya Inchugu wilayani humo, yalisikitisha.

Katika semina hiyo ya siku moja iliyofanyika katika shule ya msingi Sirari, washiriki wa semina walionesha wasiwasi kuwa kwa miaka takriban ishirini ijayo, huenda eneo la mpaka wa Sirari kwa upande wa Tarime nchini Tanzania, likafurika Wakenya wanaojisogezasogeza na kupata maeneo ya kujenga kinyemela.

Ingawa hali hii ni hatari, haitoshi kuiona ni hatari tu kwa usalama wa taifa halafu tukanyamaza, lazima atafutwe mchawi ili ajulikane ni nani.

Ni kweli kuwa mchawi hatoki mbali bali ni wananchi haohao wakazi wa eneo hilo la mpakani ambao wamekuwa wakifanya ukarimu wa kugawa viwanja vya Watanzania kwa Wakenya eti kwa vigezo vya huyu alioa kwa shangazi au huyu ni mtoto wa bibi.

Tunapenda kuwajulisha wahusika wa zoezi hilo kuwa kama hawakujua, basi tangu sasa wajue wanaua nchi na kuwaweka Watanzania katika uwezekano wa kutawaliwa tena na pengine kuigeuza nchi kuwa mithili ya Rwanda na Burundi.

Tunasema hivyo kwani kama walivyo Wahutu na Watutsi, utafika wakati Wakenya watakaokuwa wametanda na kuzaliana katika eneo hilo na mengine ya mipakani, wakataka kumiliki ardhi ya Tanzania wakiamini na kung’ang’ania kuwa ni mali yao.

Kinachosikitisha zaidi, ni baada ya Afisa mmoja wa Uhamiaji katika kituo cha Sirari, Bw. E. Mwanguku, kusema kuwa askari wa Idara ya Uhamiaji wanapohitaji ushirikiano wa raia ili kuwafichua wahamiaji wa kinyemela, baadhi ya Watanzania huchangia kuwaficha kwa kutoa taarifa batili hadi wanapokosana nao ndipo hurudi kuwatolea taarifa.

Sisi tunapinga vikali hali hii kwani isipodhibitiwa, itakuja kuliliza taifa zima na kuvikosesha vizazi vijavyo mahali pa kuishi na pengine kukosa usalama na hii, ni hali ambayo hakuna hata Mtanzania mmoja anayetaka itokee.

Watanzania waishio mipakani hasa Sirari, hawana budi kujiuliza kuwa ni Mtanzania gani amekwenda Kenya akapewa kiwanja ajenge? Kama hayupo, ukarimu unaohatarisha maisha yetu unatoka wapi?

Tunaunga mkono agizo la Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Bw. Paschal Mabiti la kutaka wahamiaji wa kiholela wote waliojipatia viwanja nchini, wafichuliwe na hata washiriki wa kuwagawia mali hiyo ambayo ni hazina ya taifa, wafichuliwe ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Hatukatai kuwepo kwa ushirikiano baina ya Watanzania, Wakenya na majirani wengine, hapana huo hata sisi tungependa kuona unaimarishwa na hata kudumu zaidi lakini tusichokitaka, ni tabia ya baadhi ya wakazi wa maeneo ya mipakani kugawa ovyo viwanja kwa wageni wa nchi jirani.

Hivi miaka ijayo vizazi vyetu vitajenga au kulima wapi kama maeneo yatakuwa yamemilikiwa na Wakenya na watu wa nchi nyingine?

Watanzania tusipokuwa makini; tukajisahau kutunza mazuri, tutakumbushwa kwa maafa kama ya Rwanda na Burundi. Hivyo, ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mipaka, na mali zote za Tanzania ikiwamo ardhi.

Ukarimu wa kugawa ardhi kwa wageni wa nje ya nchi, ni kufuga vijidudu vya maradhi ambavyo kesho na kesho kutwa, vitatudhuru wenyewe na kutupeleka kaburini kwa kilio huku tukishuhudia. Kila mtu awe makini kwani ardhi ni mali na ardhi, ni chanzo cha maendeleo.

U- Wapi Uaminifu

Toka toleo la Feb 24-Machi 2,2001

 

1. Si nduguye si jamaa, Malize wavamia,

Ni kipofu watwambia, Kiziwi hatasikia,

Akija kuyatambua, Dhiki ishamuonea,

U-wapi uaminifu, dunia yateketea.

2. Ndipo shetani hujongea, Imani kuichafua,

Ibada kupuuzia, Ramri kumpigia,

Jamii yaangamia, Pesa zinateketea,

U-wapi uaminifu, Dunia yateketea.

3. Ujumbe unamwachia, Kweli wanampatia,

Bali wanaongezea, Maneno usiyoyajua,

Majibu kukupatia, Washangaa waduaa,

U-wapi uaminifu, Dunia yateketea.

4. Tahadhari kuchukua, Pema tutaelekea,

Kazini nyumbani pia, Kulima kupalilia,

Mengi tutayachambua, Waovu kuwafagia,

U-wapi uaminifu, Dunia yateketea.

Edmundus Mtes

S.L.P.25086

DAR-ES-SALAAM.

 

Kipaumbele Lipewe, Shairi Lililo Nyota

1. Wengi twaweza duwaa, Hili lile kulitoa,

Maana tumezoea, Ndani ulitutolea,

Kumbe hiyo si sheria, Bali ndiyo mazoea,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

2. Gazetilo twanunua, habari ikivutia,

Ni ile unapambia, kurasa uloanzia,

Maana waichambua, ni nyota ulochagua,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

3. Dar Leo, Nipashe pia, Mbinu walijibunia,

Shairi kujishindia, Ni nyota watuelezea,

Mtunzi wampatia, Kilo mbili za gunia,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

4. Nyota tunajisomea, Uchumi lauchambua,

Ukweli laelezea, Ushauri linatoa,

Ndani kulichimbia, gazeti hatanunua,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

5. Ya Shabani twayajua, Shuleni wayatamia,

Uaminifu, hofu pia, Ni nyota waelezea,

Kwani, ukutuwekea, Kurasa uloanzia,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

6. Wahariri naishia, Kazi kwenu kupimia,

Habari kutobagua, Zote ujumbe zatoa,

Elimu wanayoitoa, Kilimo siasa pia,

Kipaumbele lipewe, Shairi lililo nyota.

Edmundus Mtes,

S.L.P 25086

DAR-ES-SALAAM.