Wanadamu: Tusifikiri Mungu yupo mbinguni pekee

MIONGONI mwa mambo muhimu katika jamii yoyote ya binadamu, ni uhuru wa kuabudu katika imani yoyote bila kuvuruga taratibu na sheria za jamii husika.

Hilo, hatuna shaka juu ya ukweli wake, kwani hakuna kilicho chema duniani, kama ilivyo kwa mwanadamu kujitambua na kukiri kwa mawazo, maneno na vitendo kuwa, kuwapo na kuishi kwake katika dunia hii, si kwamba kunatokana na mapenzi ya wazazi wake au ujanja wake, bali kwa mapenzi ya Mungu; muumba mbingu na nchi na vyote vya duniani na mbinguni.

Kwa mantiki hiyo, tunashauri kila ajidhania amesimama, aangalie asianguke kiimani. Njia pekee ya kumudu kutunza imani, ni juhudi za makusudi katika kumuomba na kumtegemea Mungu.

Tunapenda kuwapongeza huku tukiwaombea Mungu awazidishie neema zake, wote wanaotumia uwezo wao wote, kulitumikia Kanisa kwa imani na uadilifu huku wakilenga kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Huku tukiisisitiza jamii izingatie kuwa Mungu yupo mahali pote mbinguni na duniani, tunawashauri wanaotumia nafasi zao kama watumishi wa Mungu, kwa ngazi zote tangu mtu binafsi, familia na kuendelea, kuhakikisha kuwa kweli wanakuwa waadilifu na waaminifu katika nafasi zao wanazomtumikia Mungu kwa nyakati zote.

Tunasema hivi kwani ni ukweli ulio bayana kuwa sasa baadhi ya watu wamegeuza JINA LA MUNGU kuwa vioski vya kuendeshea miradi yao na hivyo, kujinufaisha wenyewe tofauti na ulivyo mpango wa Kanisa.

Tunapenda kuwakumbusha wenye tabia na mawazo hayo kuwa, kama kweli wanaamini kuwa Mungu yupo na hata wakaamua kutumia jina lake, wasidhani Mungu huyo yupo mbinguni pekee, bali wajue hata hapo wanapokuwa, wanaye sambamba akishuhudia mawazo, maneno na matendo yao.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa wapo baadhi ya watumishi wa Mungu ambao si waaminifu katika imani, Kanisa na hata jamii kwa jumla.

Watu wa namna hiyo, wamegeuza maeneo na majukwaa ya ibada kama mti wenye matunda ya kuchuma na kujinufaisha wenyewe nje ya kazi ya Kanisa na mpango wa Mungu.Hali hii, inajidhihirisha wazi kwa mfumuko wa vikundi vidogovidogo vinavyojiita kanisa huku vikitoa mafundisho potofu.

Tunadhani wanaopenda kujitenga kiimani na wenzao waakaanzisha vikundi hivyo na huku wakikimbiakimbia barabarani, wana lengo lao binafsi lisilo ndani ya mafundisho ya Kanisa wala mapenzi ya Mungu.

Labda la msingi kujiuliza hapa ni kwamba, ni wangapi kati yetu tunaojiita watumishi wa Mungu; tunafanya kazi ya Mungu siyo kwa lengo la kujipatia sifa au kuonekana wema machoni pa watu?

Ni wangapi tunafanya kazi za Mungu huku tukilenga kupata elimu na fedha za kuendeshea maisha yetu binafsi na labda kwa lugha nyingine, tuulizane, ni wangapi hatuliibii Kanisa kwa hali na mali.

Katika kuthibitisha kuwa kweli labda wanadamu wengi tunadhani kuwa Mungu yupo mbinguni pekee, tujiulize, ni mara ngapi katika maeneo mbalimbali inapotokea ajali, badala ya kuwaokoa waathirika na hata kunusuru maisha yao kwa kuwasaidia, tunapora mali za majeruhi na mali za waliopoteza maisha katika ajali husika?

Ni wangapi baina yetu, tumediriki hata kuwaacha na kuwatelekeza wenye shida hadi kuwasababishia mateso mengi na pengine vifo, huku tukiwa na uwezo wa kuwasaidia, bila sisi wenyewe kuathirika?

Ni wagonjwa wangapi wamepoteza maisha kwa kuwa wamekosa pesa za kulipia matibabu, iwe kwa utaratibu wa jamii au kwa rushwa? Ni wangapi wamediriki kuchangia hata mauaji ya watu wasio na hatia ambao bado hawajazaliwa kwa mauaji wanayoyaita utoaji mimba, au ni wangapi wameshiriki mauaji ya wazee na wagonjwa wasio na hatia?

Ni mara ngapi watu wenye nyadhifa mbalimbali katika jamii wamehusika katika vitendo vilivyo kinyume na maadili ya jamii na ya Kimungu huku, wakidhani wamejificha na kuamini kuwa hawaonekani?

Tunapenda kumbushana kuwa yote hayo yafanywe, popote tujifiche, lololote tulifikiri na kulisema hata kwa sauti ndogo lakini, tusisahau kuwa ingawa tunajaribu kujificha, tunajificha machoni pa watu, lakini kwa Mungu, ni uongo maana, MUNGU HAYUPO MBINGUNI PEKEE BALI MAHALI POTE na ipo siku atatuonesha yote tuliyofanya hata tulipokuwa tumejificha.

Tusimuasi Mungu; tunajiteketeza

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nafasi kidogo nieleze machache juu ya jinsi tunavyomwasi Mungu na namna madhara yake yanavyoturudi na kutuumiza wenyewe.

Kwa muda mrefu sasa kumetokea vurugu mapigano na kila aina ya mahangaiko na mateso katika baadhi ya mataifa hapa duniani.

Tukiacha niliyoyataja hapo juu mataifa yaliyojaliwa kiuchumi na kiulinzi, sasa ndiyo hayo badala ya kutumia maendeleo yao kuwasaidia wengine nao wanyanyuke ikiwa ni pamoja na mataifa ambayo wao ndio waliwakwaza kimaendeleo wakati wa ukoloni, wanayakandamiza na kuyasababisha mataifa hayo nyongeza ya matatizo makubwa.

Hii ni kwa sababu tu, ingawa hata haya mataifa yaliyoendelea kuna baadhi ya raia wake wako katika shida nyingi, bado uongozi wa mataifa na vikundi vya namna hiyo, wanatafuta sifa na heshima tu; za kidunia.

Mataifa hayo kila kukicha yanashindana kutengeneza silaha kubwa kubwa, si kwa ajili ya kujilindia dhidi ya maadui wa iana mbalimbali wakiwamo wanyama wakali, bali kwa ajili ya kuanzishia uchokozi na vita.

Je, hizo silaha ni za nini kiasi kwamba ssa zinatumika ovyo hata kwa uporaji na unyang’anyi wa mali za watu? Hivi kama kila mmoja ataichukia na kuitupa silaha, hivi zitafanya hayo yaliyo kinyume na mipango ya Mungu? kuuana!

Kwa mawazo yangu binafsi, kutengeneza silaha kwa ajili ya kumuuua mwenzio, ni kumkosea Mungu. Hebu labda kwa wewe utakayebahatika kusoma barua yangu hii, nisaidie hata kumuuliza mwenzio kuwa, hivi ni kweli Mwenyezi Mungu alituumba sisi wanadamu ili tuje kuuana sisi wenyewe kwa wenyewe?

Kama jibu sio, kwanini sasa tuuane?

Tukichunguza, hakuna sehemu yoyote hapa duniani ambayo ni salama. kila kona ya dunia, ina vita, njaa mabishano na mauaji ya kila siku. Mungu alituumba sisi wanadamu kwa sababu alitupenda. Baada ya kutuumba lengo kuu tumwabudu sasa, kwanini tumsaliti kwa mawazo, maneno na matendo yetu?

Yote haya, yanatokea kwa sababu ya ugumu wa mioyo yetu ya kutoweza kushika zile Amri zake Kumi ikiwamo ile kuu ya UPENDO.

Kuhusu hili, ni kweli kuwa hata migogoro mikubwa ya kitaifa na kimatafa, inasababishwa na viongozi wetu na sisi wenyewe kukosa UPENDO kwa wenzetu.

Hakuna jingine, na sio tu kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa hata katika familia zetu, kabila zetu, dini zetu na utaifa wetu; tunakosa upendo ndio maana kila siku ni vurugu na mateso hata kufikia mauaji kwa njia mbalimbali.

Basi, tumuombe Mungu atusaidie tupate nguvu za kuishinda mioyo hatari ya chuki baina yetu na badala yake, tustawishe upendo ili tupokelewe mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

 

Sinderellah Migel

B.O.X Msimbazi,

DAR-ES-SALAAM

Jiji leteni huduma ya vyoo

Ndugu Mhariri,

NAOMBA unipatie nafasi kwenye gazeti lako la KIONGOZI, niweze kutoa maoni yangu kwa wahusika.

Ni maoni ambayo siyo siri, ni siku nyingi yamekuwa yakinikera kwa muda mrefu hapa jijini, Dar-Es-Salaam.

Inasikitisha sana kuona Tume ya Jiji ikiweka sheria ya kuwapatia adhabu watu wanaojisaidia ovyo wakati wao wenyewe(jiji), wameshindwa kutengeneza mazingira ambayo yatamzuia mhusika kufanya hivyo.

Nasema hivyo kwa sababu ninasikitisha kuona jiji kama la Dar-Es-Salaam, halina vyoo vya kulipia kwenye katika sehemu mbalimbali kama ilivyo katika mikoa mingine kama Arusha na Moshi na mahali pengine?

Kwa nini maeneo yote ya jiji hili yasiwe na huduma hii ili kusaidia jamii na kuiepusha kujidhalilisha huku pia, hali hiyo ikichangia uharibifu na uchafuzi wa mazingira?

Nachukua fursa hii kuiomba Serikali na Tume yenyewe ya Jiji, walipe suala hili umuhimu wa pekee.

Yatengenezwe mazingira yatakayomwezesha mtu kuepuka vishawishi vya kujianika hadharani kwa kuwa wengine wana lazimika kufanya hivyo baada ya kuzidiwa.

Ninaposema hivyo sima maana kuwa hatua yao ya kujisaidia ovyo ninaipongeza, la hasha ! hata mimi ninajua madhara yake kiutu, kijamii na kiafya na kwamba yanaweza kuanzia hata kwangu mimi lkini ninachokifanya, nina jaribu kushauri njia za kuondoa adha hiyo.

Baada ya kuwepo huduma hii muhimu, ni vema sasa ikawekwa sheria madhubuti kumdhibiti yeyote atakayeonekana kujisaidia hadharani na afikishwe kwenye vyombo husika vya sheria.

Elvisi Wilbord

Dar-Es-Salaam.