Make your own free website on Tripod.com

Wizara ya Afya; mbona vifo vya wajawazito vinazidi?

KATIKA masikio ya Watanzania, sasa limekuwa jambo la kawaida kusikia kuwa wajawazito wametelekezwa, wakanyimwa huduma wakati wa kujifungua na hata kufariki dunia.

Tunaamini kuwa licha ya kuwa vifo hivyo vinavyotokana na uzembe na utovu wa maadili wa wahudumu katika taaluma hiyo wakiwamo wauguzi, waganga na madaktari, ni aibu kwa Serikali na ni dhambi inayotupwa kwa taifa zima kwa ajili ya watu wachache.Tunasema kuwa ni dhambi na aibu kwa kuzingatia ukweli kuwa unapozembea, kupuuza na hata kusababisha kifo cha mjamzito, ni ukweli usiofichika na ulio bayana kuwa unakuwa umewaua watu wawili au zaidi kwa wakati mmoja.; tena wasio na hatia.Mifano ya mauaji ya namna hii hapa nchini, ni mingi ikiwa ni pamoja na tukio la Mei 26, mwaka huu katika Hospitali ya Mount Meru, iliyopo mkoani Arusha, ambapo mjamzito Asia Hamis, alifariki dunia baada ya kutelekezwa na wahudumu wa hospitali hiyo wakati akijifungua.

Habari zilizotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari mwishoni mwa juma kuwa uongozi wa hospitali hiyo umeanza uchunguzi mkali mintarafu kifo hicho kwa kuwahoji baadhi ya wahudumu wanaodhaniwa kuhusika na tukio hilo, zilianza kutia matumaini kwamba huenda ukawa ni mfano wa kuigwa na hospitali nyingine.

Hii ilitarajiwa kuwa moja ya mifano ya maonyo kwa watu wanaochekea mauaji ya watu wasio na hatia na wanaojidai mahakimu wa uhai wa wenzao hasa wajawazito pamoja na viumbe wao wa tumboni.

Tunasema hivi kwa kuwa tunaamini kuwa, watumishi hao huku wanalipwa kwa ajili ya jukumu la kuwasaidia jamii kwa matazamio kuwa wanatumia taaluma na vipaji vyao kama yalivyo maadili.

Hata hivyo, habari zaidi kuwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Omary Chande, amekanusha vikali juu ya kuhojiwa kwa wauguzi hao kwa madai kuwa ofisi yake haijapokea malalamiko rasmi toka kwa wafiwa, zimezidi kutuchoma mshale wa maumivu katika mioyo yetu.

Tunasema hivyo kwa kuwa katu, hatukutarajia kuwa Mganga Mkuu anasubiri malalamiko ya wafiwa, ndipo achunguze sababu za wajawazito kutelekezwa na kufia katika hospitali yake na hali hiyo sisi tunaiita kuwa ni kituko.

Tunasema ni kituko huku tukijiuliza kuwa endapo wafiwa wataamua kulilia tumboni, wakazika na kuomboleza; kisha wakakaa kimya, Dk. Chande anawaambia nini Watanzania; kwamba kamwe hatafanya uchunguzi na hivyo mauaji kama hayo yawe ruksa katika hospitali hiyo?

Sisi tunaamini kuwa Dk. Chande si muadilifu katika kazi yake na labda hajui kuwa anawajibika kwa jamii maana kama angejua hilo, asingediriki kusema hivyo.

Mtumishi muadilifu katika kazi hangojei kupelekewa taarifa ofisini bali anapoona au kupata taarifa juu ya tatizo au hali inayotishia ubora wa utendaji wa majukumu, hunyanyuka na kuyafuatilia kwani asiyeziba ufa, hujenga ukuta.

Tunasema matukio ya kutelekezwa wajawazito si kitu cha kushangaza na kwamba labda Serikali imekuwa kimya na haichukui hatua kali au la, kwa sababu licha ya tukio hilo, lipo lingine la Aprili 24, mwaka huu, katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, mjamzito Mogosi Ogwit(24), alifia njiani akielekea katika hospitali ya kibinafsi ya Dk. H. Winani Health Center baada ya kuambiwa aondoke katika Hospitali ya Wilaya kwa kuwa mtoto alikwishafia tumboni.

Hata hivyo, tukio hilo la kumtelekeza, lilidaiwa kufanyika huku ndugu wa mjamzito huyo wakiwa tayari wameombwa na mganga wa zamu na wauguzi shilingi 15,000 na shilingi 5300 kwa nyakati tofauti.Kwa historia ya Hospitali hiyo ya Wilaya ya Tarime, tukio hilo lilikuwa marudio kwa historia ya kuwatelekeza na kuwasababishia vifo wajawazito. Agosti 2, mwaka juzi, mjamzito Mariamu Nyangarya(21), alitelekezwa na kufia sakafuni baada ya kuzungushwa hadi hospitali ile lile ya binafsi huku ndugu wakiwa tayari wametoa kiasi fulani cha pesa kwa wahudumu, kuweka radio na kamera rehani ili ndugu yao atibiwe na hivyo, kumnusuru lakini, wapi.

Hatujui ni kwanini watumishi wa hospitali hiyo wanajiamini kiasi hicho kwani licha ya kumtelekeza tangu asubuhi hadi usiku wakati wa mauti, bado waliutoa mwili wa marehemu usiku huo wa saa tano bila hata kumpasua na kutoa kiumbe wa tumboni.

Hali hiyo ilifanya polisi washinikize na hivyo mganga wa hospitali hiyo, aende kufanyia upasuaji huo nyumbani kwa marehemu siku mbili baadaye.

Jijini Dar-Es-salaam, hilo lipo kwani hakuna asiyejua namna ambavyo hata Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam, Luteni Yusufu Makamba ambavyo amekuwa akikemea vitendo hivyo hususan katika Hospitali ya Mwananyamala.

Hatujui kwanini licha ya ubaya huu kujulikana wazi namna hii,, kwanini bado unaendelea.

Kinachoshangaza hasa mkoani Mara, uongozi wa hospitali mkoani humo, umewahi kuongopa kuwa ungetoa taarifa lakini, hiyo, imekuwa ndoto ya mchana.

Sisi tunadhani labda watumishi wa Idara ya Afya katika hospitali zetu, ni wazembe, watovu wa maadili, wasioogopa wakubwa wao ( Wizara) na wapenda rushwa ndiyo maana, siku hadi siku matukio hayo yanajitokeza zaidi.

Tunasema hivi tukiwashauri wahusika katika Wizara ya Afya, kutumia imani zao za kidini, na nafsi zao kama watumishi wa umma kuona kuwa, maisha ya watoto ambao hawajazaliwa, pamoja na mama zao, hayadhulumiwi kwa uzembe wa watumishi na wala, yasiwe mikononi mwa mapenzi ya wauguzi na madaktari bali yaachwe mikononi mwa Mungu.

Ingawa tunaishauri Serikali yetu tukufu kuvalia njuga suala hili, bado tunaiuliza Wizara ya Afya kuwa tatizo liko wapi na kama halijaonekana, vifo vya wajawazito na watoto wao, vitakwisha lini; mbona vinazidi?

 

 

Tusimuasi Mungu; tunajiteketeza

 

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nafasi kidogo nieleze machache juu ya jinsi tunavyomwasi Mungu na namna madhara yake yanavyoturudi na kutuumiza wenyewe.

Kwa muda mrefu sasa kumetokea vurugu mapigano na kila aina ya mahangaiko na mateso katika baadhi ya mataifa hapa duniani.

Tukiacha niliyoyataja hapo juu mataifa yaliyojaliwa kiuchumi na kiulinzi, sasa ndiyo hayo badala ya kutumia maendeleo yao kuwasaidia wengine nao wanyanyuke ikiwa ni pamoja na mataifa ambayo wao ndio waliwakwaza kimaendeleo wakati wa ukoloni, wanayakandamiza na kuyasababisha mataifa hayo nyongeza ya matatizo makubwa.

Hii ni kwa sababu tu, ingawa hata haya mataifa yaliyoendelea kuna baadhi ya raia wake wako katika shida nyingi, bado uongozi wa mataifa na vikundi vya namna hiyo, wanatafuta sifa na heshima tu; za kidunia.

Mataifa hayo kila kukicha yanashindana kutengeneza silaha kubwa kubwa, si kwa ajili ya kujilindia dhidi ya maadui wa iana mbalimbali wakiwamo wanyama wakali, bali kwa ajili ya kuanzishia uchokozi na vita.

Je, hizo silaha ni za nini kiasi kwamba ssa zinatumika ovyo hata kwa uporaji na unyang’anyi wa mali za watu? Hivi kama kila mmoja ataichukia na kuitupa silaha, hivi zitafanya hayo yaliyo kinyume na mipango ya Mungu? kuuana!

Kwa mawazo yangu binafsi, kutengeneza silaha kwa ajili ya kumuuua mwenzio, ni kumkosea Mungu. Hebu labda kwa wewe utakayebahatika kusoma barua yangu hii, nisaidie hata kumuuliza mwenzio kuwa, hivi ni kweli Mwenyezi Mungu alituumba sisi wanadamu ili tuje kuuana sisi wenyewe kwa wenyewe?

Kama jibu sio, kwanini sasa tuuane?

Tukichunguza, hakuna sehemu yoyote hapa duniani ambayo ni salama. kila kona ya dunia, ina vita, njaa mabishano na mauaji ya kila siku. Mungu alituumba sisi wanadamu kwa sababu alitupenda. Baada ya kutuumba lengo kuu tumwabudu sasa, kwanini tumsaliti kwa mawazo, maneno na matendo yetu?

Yote haya, yanatokea kwa sababu ya ugumu wa mioyo yetu ya kutoweza kushika zile Amri zake Kumi ikiwamo ile kuu ya UPENDO.

Kuhusu hili, ni kweli kuwa hata migogoro mikubwa ya kitaifa na kimatafa, inasababishwa na viongozi wetu na sisi wenyewe kukosa UPENDO kwa wenzetu.

Hakuna jingine, na sio tu kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa hata katika familia zetu, kabila zetu, dini zetu na utaifa wetu; tunakosa upendo ndio maana kila siku ni vurugu na mateso hata kufikia mauaji kwa njia mbalimbali.

Basi, tumuombe Mungu atusaidie tupate nguvu za kuishinda mioyo hatari ya chuki baina yetu na badala yake, tustawishe upendo ili tupokelewe mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Sinderellah Migel

B.O.X Msimbazi,

DAR-ES-SALAAM