Make your own free website on Tripod.com

Tuthamini malezi ya watoto wadogo

KILA mzazi mwenye upendo na mwenye uchungu na mtoto wake hupenda kurithisha mambo mazuri kwa maisha yake ya baadaye.

Katika siku hizi za maendeleo makubwa ya elimu, wazazi wengi hupenda kuwapa watoto wao elimu ya juu kabisa yenye kulingana na wakati uliopo.

Wapo wazazi walio tayari kujinyima na kuwahangaikia watoto wao kadiri inavyowezekana ilimradi watoto hao wapate elimu ya kufaa.

Wazazi wengi siku hizi hufanya juu chini ili watoto wao kwanza wapate msingi unaofaa katika elimu.

Mapema kabisa, huwapeleka watoto wao katika shule za awali ili watoto wajengeke vilivyo kielimu. Watoto hao wadogo hujifunza mambo ya msingi kama vile kusoma, kuandika na michezo mbalimbali.

Hapo ni kwamba hawajifunzi tu maarifa bali pia hujifunza namna ya kuishi na kucheza pamoja na wenzao. Kwa maneno mengine, tunasema watoto hao wanajifunza namna ya kuishi na kutenda katika ushirikiano na wengine.

Hujifunza namna ya kuvumiliana na wenzao na kuwasaidia katika shughuli mbalimbali.

Tunapenda kuipongeza Wizara ya Elimu kwa kutamka kuwa kila shule ya msingi iwe na shule ya awali ili kuwajenga vilivyo watoto wetu ambao ni taifa la kesho.

Mpaka sasa kuna wafadhili wengi ambao hujitoa kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule za watoto wadogo. Tunawashukuru na kuwapongeza hao wenye moyo wa kuwalea watoto wetu na pia, tunatoa rai kwa wananchi kuzingatia umuhimu wa malezi bora ya watoto wetu wadogo katika shule hizo za awali.

Waswahili husema kuwa, samaki mkunje angali mbichi maana ukichelewa, utamvunjavunja tu. Hivyo, tunapaswa kuwalea watoto wetu tangu wanapokuwa wadogo hasa tukiangalia hali halisi ilivyo siku hizi.

Tukumbuke kuwa, kila mtu anayakumbuka mambo aliyokuwa akifundishwa na kujifunza wakati alipokuwa mdogo.

Wangapi ambao tu watu wazima tunakumbuka mafundisho na hata miiko tuliyoambiwa na wazee wetu na hasa wazazi wetu? Wengi tunakumbuka nyimbo ambazo walimu wetu walitufundisha wakati tukiwa wadogo.

Tungependa kuona katika shule hizo za awali kuna kuwa na mkazo katika mambo ya kidini pamoja na maadili mema ya kijamii kama yanavyofanyika katika shule zinazomilikiwa na makanisa au mashirika ya kidini.

Kuna watawa na walimu ambao hufundisha siyo tu jinsi ya kusoma na kuandika, bali pia huwafundisha watoto hao misingi ya maadili mema pamoja na dini.

Kwa kuwa kila binadamu ni mwenye mwili na roho, hivyo watoto wetu wanapaswa kuyafahamu mambo ya kimwili na pia mambo ya kiroho.

Sote tunatambua ni kwa jinsi gani vijana wetu wanakosa misingi hiyo ya kimaadili na kidini na kwa mantiki hiyo, tunasema kuwa ni vema watoto wetu, licha ya kufundishwa kule nyumbani na wazazi wao mambo ya kimaadili na kidini, pia wafundishwe mambo hayo wawapo shuleni.

Tunatumaini kuwa watoto hao watafundishwa mambo ya uraia pia kama vile heshima na adabu kwa wakubwa na hata miongoni mwao wenyewe.

Vijana wengi wanakosa heshima na adabu au kwa sababu ya kutofundishwa na wazazi wao, au ni kwa sababu ya kukosa bahati hiyo ya kuwa katika shule za awali.

Kwa hiyo, tunatamani kuona walimu na walezi katika shule hizo za watoto wadogo wanaandaliwa vilivyo. Maana siyo kila mmoja anaweza kufundisha watoto wadogo na kuwafikisha kwenye malengo yanayotakiwa.

Mpaka sasa kuna shirika la Montfort ambalo hushughulika sana na kuwaandaa walimu ambao hufundisha katika shule hizo za watoto wadogo.

Tunawahimiza wale wote wanaoshughulikia malezi na ufundishaji wa watoto wadogo, wajishirikishe na shirika hilo katika kuwaandaa walimu ambao watafundisha watoto wetu wadogo.

Ni kweli kuwa siyo kila mmoja mwenye wito wa kufundisha watoto wadogo anaweza kupata nafasi katika shule hizo, lakini inawezakana hasa katika kuhudhuria semina na warsha mbalimbali za ufundishaji watoto wadogo.

Malezi ya watoto wadogo katika hizo shule za awali ni muhimu sana kama vile ulivyo msingi wa nyumba. Taifa letu linahangaika sana kuhusu malezi ya vijana wenye tabia na mienendo mibaya.

Tunajiuliza ni kwa sababu gani mambo hayo yamekuwa hivyo. Jibu lake tukiangalia kwa undani ni ukosefu wa malezi bora ya mwanzo kabisa.

Tukitaka kulinusuru taifa lisiangamie kwa siku zijazo, hatuna budi kufanya kila tuwezalo, kuwapa watoto tulio nao sasa msingi bora wa malezi ya kimwili na kiroho .

Tunamalizia Kauli Yetu tukiwapongeza waliojiwekea lengo muhimu la kuendesha shule za watoto wadogo katika misingi ya taaluma na madili mema na tunawawaomba wenye uwezo wa kuzisaidia shule hizo kufikia malengo yao, wafanye hivyo kwa hali na mali.

Tunasema hivyo kwa sababu taifa letu linao watoto wengi, lakini hakuna shule za kutosha.

Kwa hiyo ni jukumu la kila mwananchi kusaidia kwa hali na mali katika kujenga na kuziendesha shule hizo hasa katika maeneo ya vijijini.

Barua ya malalamiko kwa Shirika la Bima la Taifa

Ndugu Mhariri,

Napenda kuchukua nafasi hii kutoa malalamiko yangu kupitia gazeti lako kuhusu malipo ya mke wangu Kuruthum Abdalla, aliyefariki kwa ajali ya basi dogo lenye namba za usajili TZG 2164 la Bw. Straton Peter wa Dar-Es-Salaam, ajali iliyotokea mwaka 1997. basi hilo likitokea Tarime kwenda Musoma.

Baada ya ajali hiyo, mimi Abdallah Ismail, ambaye ni mume wa mama huyo, nilimuandikia barua mwenye gari hilo Machi 17, 1998 ya kuomba fidia kutokana na ajali hiyo ya mke wangu.

Katika barua hiyo, niliomba fidia ya shilingi milioni 16 na mmiliki wa gari hilo Bw. Peter, aliijibu April 7, 1998 na akatoa pole kwa familia ya marehemu na akasema, gari lake lilikuwa na Bima hivyo, ni jukumu la shirika la Bima kulipa fidia hiyo.

Aliniomba niwasiliane na Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Bima jijini Dar-Es-Salaam.

Nilipowasiliana na shirika la Bima, Mkurugenzi aliniandikia barua ya Septemba 28,1999 kunitaka nipeleke vielelezo kama vile jina la marehemu, ajali hiyo ilitokea lini na vyeti vya ndoa pia, niliambatanisha hukumu ya mahakama ya mwanzo Tarime Mjini iliyonihalalisha kuwa msimamizi halali wa mirathi ya marehemu mke wangu; Kuruthumu Wanjara.

Licha ya viambatanisho hivyo vyote, pia niliambatanisha ripoti ya polisi juu ya ajali hiyo iliyokuwa na majina ya watu 17 waliokufa akiwamo mke wangu, na majina ya majeruhi waliokuwemo ndani ya gari hilo.

Mhariri, licha ya kuwa nimetimiza masharti yote na kutuma katika shirika la Bima mwaka 1999, shirika hilo limekaa kimya bila majibu yoyote ya malipo.

Hali ambayo ilinisababishia mimi kwenda Tawi la Bima la Musoma ili kuelewa hatima yake lakini, kuanzia Agosti 5,2000 hadi hivi sasa hakuna majibu yoyote.

Kulingana na usumbufu ninaoupata na majonzi makubwa kwa mke wangu mpendwa kunitoka na kuniachia watoto watatu, imekuwa ni fedheha tena kupata usumbufu kudai haki ya fidia hiyo kuanzia marehemu alipofariki mwaka 1997 hadi sasa.

Mimi binafsi ninapenda shirika la Bima kuelewa kuwa si vizuri kukaa kimya kana kwamba fidia hiyo ninaomba msaada.

Lakini, pia litambue kuwa ni wajibu wa shirika hilo kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Hivyo, kunicheleweshea malipo hayo ni kutaka kunidhulumu haki yangu.

Ingawa kiasi hicho ni kidogo ambacho hakiwezi kulipa fidia ya uhai wa mtu, lakini kitaziba pengo fulani ambalo marehemu alikuwa akisimamia.

Hivyo, naiomba serikali ya Tanzania yenye uwazi na ukweli kutusaidia kutatua suala hilo ili wote walioathirika kufiwa na ndugu zetu katika ajali hiyo, tulipwe fidia zetu kwa vile masharti tuliyopewa na shirika hilo tayari tumemaliza kwani tutasubiri malipo hayo mpaka lini.

Pia, ninaiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina katika shirika hilo, na kuona ugonjwa uliomo ndani yake kwa vile kumekuwepo na usumbufu wa malipo ya fidia mara ajali zinapotokea na kufanya wadai kuwa watumwa hali ambayo inakatisha tamaa hasa kwa wale wasio na uwezo wa kutoa rushwa.

Haki za wanyonge hupotea kwa sababu ya Rushwa.

Abdallah Ismail,

Box 10,

Tarime.

Tuwe na imani kwa Yesu kwa njia ya sala, maneno na matendo mema

Ndugu Mhariri,

NAOMBA japo nafasi kidogo katika gazeti lako tukufu la KIONGOZI, ili nieleze au nikumbushe kidogo kuhusu imani yetu kwa Yesu Kristo ambaye ni Mungu Mwana.

Katika mazungumzo yangu, ninaposema imani, ninamaanisha kuifanya iwe na uhai.

Ndugu zangu katika Kristo, sina shaka kuwa kila mmoja wetu anajua kuwa alizaliwa siku moja na kwamba, ipo siku moja ambayo kwayo, atakufa na kumrudia Mungu wake.

Hivyo, hatuna budi kila tunapoishi, tujiulize maswali kadhaa juu ya uwepo wetu duniani. Kila Mtu anajua kuwa tuliumbwa na Mungu ili tumwabudu, kumsifu na kumtukuza Tukijihangaisha katika kujaribu kutafuta jibu jingine mbali na hilo, kamwe hatutalipata kwa kuwa Mungu hahitaji chochote zaidi, toka kwetu na badala yake, ni sisi tunaohitaji vitu vyote toka kwake ili tuishi.

Sina shaka kusema kuwa wengi wetu tunajua namna Yesu alivyokubali kuja duniani na kujifanya mtu, kuteswa na hatimaye kufa msalabani ili wanadamu wakombolewe toka katika utumwa wa dhambi.

Sasa cha kujiuliza ni kwamba, ni nani kati yetu wanadamu awezaye kutoa uhai ili awasaidie wengine?

Au ni nani aliye tayari kuuza mali yake ili hata atoe sehemu ya kipato na kumsaidia mwenye shida?Nikisema hivyo ninataka kusema kuwa kubwa zaidi analotaka Mungu toka kwetu ni kumpenda kwa dhati ili wakati wowote akituita, tuwe tayari.

Anataka tuwe watu wa kushirikiana kwa upendo hadi kufa kwetu kwani ni jambo lililo wazi kuwa siri moja ya mafanikio katika kumshinda adui yeyote akiwamo shetani, ni upendo na ushirikiano.

Hivyo, ninawaomba watu wote mjue kuwa; uwe tajiri au maskini; uwe na elimu au sio msomi, kama hauna ushirikiano na upendo kwa watu wengine, hata kama utasali na kuwa katika hali ya namna gani, ni bure maana hata Maandiko Matakatifu yanasema hata mkiwa na yote lakini bila upendo miongoni mwenu, ni bure.

Hakuna awezaye kusema na kudhani akilini mwake tu kuwa anampenda Mungu, huku wenzake wanataabika kwa njaa na yeye anasaza na kutupa.

Ningependa kukumbusha kuwa, kama kweli tunataka kuwa wafuasi na wanafunzi sahihi wa Yesu Kristo, basi mawazo, maneno na matendo yetu lazima yawe mema na sio kwa lengo la kuonekana machoni mwa watu au kutenda mema kwa kuogopa sheria za nchi, bali kwa lengo la kutimiza mapenzi ya Mungu.

Perpetua Thomas,

Box 77

Songea.