Make your own free website on Tripod.com

Mwaka 2001, tuuanze upya

JUMATATU hii, ulimwengu mzima unaingia katika ukurasa mpya wa maisha kwa kuingia mwaka mpya wa 2001.

Hii ni bahati kubwa kwa kila aliyefanikiwa kuushuhudia akiwa hai. Hatuna shaka kuwa hakuna atakayepinga ukweli kwamba, ni heshima na upendeleo wa pekee toka kwa Mungu kuumaliza Mwaka Mtakatifu wa 2000 na kuushuhudia unavyoyoyoma.

Ingawa huu ulikuwa ni mwaka 2000 ulikuwa ni Mwaka Mtakatifu, bado tangu awali kulikuwa na mizengwe ya kila aina toka kwa watu mbalimbali ukiwamo uzushi kuwa huu, ndio mwaka wa MWISHO WA DUNIA.

Si hilo tu, pia kumekuwa na matukio mengi ya hapa na pale yaliyosababisha vifo vya makusudi na hata vile vya bahati mbaya, kwa tafsiri ya kibinadamu lakini kumbe, ni kwa mapenzi mema ya Mungu.

Tunasema hivyo kwa kuwa ukiachia waliokufa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wote tunajua yaliyofanywa na manabii wa uongo huko Kanungu nchini Uganda wakiongozwa na Joseph Kibwetere baada ya kuamua kuangamiza mamia ya roho za watu wasio na hatia eti kwa imani za kidini, unyama mkubwa.

Si hilo tu, hata hapa Tanzania Mungu ametunusuru kushuhudia ambayo hatukuomba na hatuombi kamwe, yatokee hasa baada ya polisi kutumia nguvu za ziada kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na Novemba mwaka huu.

Sisi tunasema, mwaka 2001, kila mwenye akili timamu, hana budi kuutumia vema kwa kutafakari na kujisahihisha. Ajitazame kwa makini, ambapo nafsi yake inakiri kuwa ni safi, aendeleze lakini anapojua kuwa hata yeye akitendewa hatafurahi, aache mara moja.

Mwaka 2001, usiwe tena mwaka wa kuendeleza majaribio ya kuhatarisha amani kutokana na tofauti za kisiasa, bali uwe ni mwaka unaoeleweka kuwa, upinzani ni njia ya kujenga na kuchochea maendeleo katika jamii.

Mwaka Mpya uwe mwaka wa kila mmoja kwa nafasi yake, kujikosoa; awe msukuma mkokoteni, au afisa; mwajiri au mwajiriwa. Uwe ni mwaka wa kujenga mahusiano mema baina ya watu wa makundi hayo na mengine yote ambayo si rahisi kuyataja pasipo kunyanyasana kimadaraka.

Mwaka 2001, uwe ni mwaka ambao kila mmoja sasa ataona ni aibu kumpora mwenzie uhai eti kutokana na imani za kishirikina na pia, uwe ni mwaka ambao vijana wa kike na wa kiume wataona aibu kufanya mauaji kwa njia ya utoaji mimba kwa kuwa uwezo wa kujizuia wanao na sababu ya kufanya hivyo, wanazo.

Huu, uwe ni mwaka ambao ulevi wa kupindukia utalaaniwa na kila mtu na hata kila mwenye mapenzi mema kuhakikisha analinda haki zote za mwenzake kama anavyozilinda na kuzitetea za kwake maana huo ndio upendo halisi.

Mwaka Mpya wa 2001, uwe ni mwaka ambao kila mmoja atafanya kazi kwa moyo wa ufanisi, ili aendelee kula kidogo anachopata na hivyo, jamii nzima kushirikiana kuupiga vita umaskini.

Bado tunasema, mwaka huu mpya, uwe mwaka ambao wenye vyeo, hawapaswi tena kuendelea kuwatesa na kunyonya jasho la wasio na vyeo lakini kumbe, ni wazalishaji wakubwa. Uwepo uwiano sahihi na wa haki wa mapato na matumizi.

Huu uwe ndio mwaka ambao kila mmoja anajitahidi kupambana zaidi ili kuziba mianya yote inayotoa nafasi ya maambukizi ya UKIMWI na pia, uwe ni mwaka ambao hata ajali za barabarani hazina budi kuonewa aibu na kila mmoja.

Mwaka 2001, uwe mwaka ambao serikali haitasinzia ikisubiri mauaji kama yale ya Kilosa yatokee kwanza, na kisha kukurupuka kusimamisha kazi wakati watu wamekwisha kufa kwani hiyo ni sawa na kumuongeza damu maiti.

Mwaka unaoanza, uwe ni mwaka wa aibu kwa mabomu kuendelea kulipuka ovyo bila njia sahihi za kuyazuia na badala yake kuyakemea kwa kauli bila vitendo maana majeshi tunayo yenye utaalamu wa kutosha kutengua mbinu za magaidi au vinginevyo, labda basi tuseme "kuna mkono wa Mtu".

Tunasema mwaka huu, uwe mwaka wa vitendo hata kwa wanasiasa, watendaji wa serikali na majeshi yote kufanyakazi kwa misingi ya maadili na usahihi , usiwe mwaka wa maneno mengi matendo kidogo.

Tunasisitiza kuwa, kwa kuwa Mwaka Mtakatifu wa 2000, umekwisha, sasa tuonekane kweli kwamba tuliupokea na kuufanyia kazi na sio kusikiliza tu na kuacha.

Tunasema mwaka huu mpya uwakatae watumishi wa Mungu wasio na wito bali wanaoingia katika kazi hiyo kutafuta sehemu rahisi ya kuendeshea maisha huku yakiwapo mashindano ya kuanzisha makanisa.

Mwaka huu jamii nzima ibadilike kimaneno, kimawazo na kimatendo. Kila mmoja akusudie kutimiza mapenzi ya Mungu. KWA HERI MWAKA 2000, KARIBU MWAKA 2001.

Wana - nachingwea gongo itakufikisha wapi

Ndugu Mhariri,

Najitokeza tena gazetini nikiwa na machache yanayosibu.

Kadiri ya utafiti wangu pombe aina ya gongo au kama inavyojulikana na wenyeji kwa jina la Nipa, imeshamiri sana katika maeneo ya kusini wilayani Nachingwea hasa maeneo yajulikanayo kama Mnero.

Pombe hii hunyweka pasipo kificho chochote na kwa nyakati zote kana kwamba ni nzuri na ni halali.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa, hata wanafunzi na wanachuo wa vyuo mbalimbali wanaochukua mafunzo ya dini huko katika vyuo mbalimbali, hutoroka na kwenda kunywa pombe hiyo.

Hiki ni kinywaji ambacho hunyweka na watu wote akina baba kwa akina mama huku madhara yake yakiwa yanajulikana dhahiri.

Ndugu zangu wa maeneo hayo husika, pombe aina ya gongo ina madhara yake tena makubwa mwilini mwa mwanadamu ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa maini na kudhoofisha mwili wa binadamu.

Vyombo vya dola vya maeneo hayo yawezekana vinafahamu lakini vinafumbia macho jambo hilo.

Kutokana na unywaji huo wa pombe ya gongo, baadhi ya watu wamekuwa dhaifu, nguvu za uzalishaji nazo pia, zimepungua huku umaskini ukishamiri.

Ombi kwa kipindi hiki cha uongozi mpya, matendo kama hayo yakemewe kwa nguvu na kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watakaobainika kujihusisha nayo ili taifa liweze kupata wananchi imara wanaotumia muda wao katika kubuni mbinu za uzalishaji na hivyo, kufuta ombaomba isiyo na maana.

Wahusika fuatilieni jambo hili mazingira ya ulevi daima yanabaki kulalamika na kulaumu viongozi wao kwamba hawana maendeleo.

Maendeleo haya hutokana na nguvu za wananchi wote na siyo na viongozi peke yao.

Mkereketwa

Box 324

Nachingwea.

Shairi

MPENDWA BABA KYAMBO.

1. Habari tulipokea, kwa kusikitika sana,

Msiba umetokea, ni pigo lingine tena,

Kyambo katutangulia, rafiki yetu mwanana

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO

2. Idara ya Kichungaji, aliiongoza vema,

Alipoenda kuhiji, na wenzake kule Roma,

Mungu akamuhitaji, asingeweza kugoma,

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEEE BABA KYAMBO

3. Alikuwa ni rafiki, kwa wazee na vijana,

Mpole mpenda haki, na tunu za kila namna,

Mchapa kazi hachoki, asubuhi na mchana,

MWEYEZI TUNAKOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO.

4. Imetushika huzuni, hatuwezi kueleza,

Theobad hatumuoni, umefifia mwangaza,

Atayeliziba nani, pengo tunajiuliza,

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO.

5. Tunapaswa kuchukua, kwake Kyambo mtukuka,

Mengi yenye manufaa, na kujitoa sadaka,

Watu kuwahudumia, bila chochote kutaka,

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO.

6. Kyambo tumuombee, sisi sote waamini,

Mwenyezi ampokee, amfikishe mbinguni,

Mwingine atupatie, Kichungaji Idarani,

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO.

7. Tamati natiatama, nimefika ukingoni,

Kanisa la Tanzania, sasa lipo simanzini,

Nguzo tuliyozoea, imeshaanguka chini,

MWENYEZI TUNAKUOMBA, MPOKEE BABA KYAMBO

Imetungwa na David Mpangile