Maduka ya dawa yajirekebishe

HIVI karibuni kumetolewa taarifa ya kufungiwa maduka na sehemu mbalimbali ambapo hutolewa huduma mbalimbaliYa dawa yaani "Famasi".

Tulisikia na kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa zaidi ya maduka 100, yamefungwa jijini Dar-Es-Salaam baada ya kubainika yanakiuka taratibu za uuzaji wa dawa hizo.

Kwa mujibu wa Mkaguzi mkuu wa Bodi ya dawa nchini, Bibi. Olympia kowelo, maduka hayo yalifungwa kutokana na kubainika kuwa yalikuwa yakiuza dawa zenye sumu na kukiuka taratibu za kuuza dawa za binadamu.

katika toleo lake lililopita Gazeti hili , liliripoti kuwa maduka kama hayo ya dawa wilayani Tarime, mengine yamediriki kujichukulia mamlaka ya kulaza wagonjwa na hata kuwaongeza maji na damu.

Huenda kukawa na idadi kubwa zaidi ya hiyo. Hatua hiyo imechukuliwa na wahusika na wasimamizi wa masuala ya usambazaji dawa katika nchi.

Kimsingi, tunapenda kuwapongeza wafanyabiashara wote waliojitahidi kusogeza huduma hiyo ya upatikanaji wa dawa karibu na wananchi kwani sasa hali iliyopo, siyo iliyokuwapo katika siku za nyuma. Uwepo wa maduka mengi ya dawa katika miji, unasidia kwa upatikanaji wa huduma ya kwanza kwa mgonjwa kabla hajaonana na daktari na pengine hata kuchangia punguzo la bei kutokana na ushindani wa kibiashara.

Kwa kuamini kwamba wengi wetu tunalijua hilo, tunaamini hatua hiyo haikuchukuliwa kwa nia mbaya aidha ya kuwadhulumu, au ya kuwaonea wenye maduka hayo. Sisi tunaamini kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchunguzi na utafiti wa kina juu ya usalama wa afya za Watanzania.

Tunasema hivyo kwa kuwa tunajua kuwa hata hospitali kubwa za serikali, zina upungufu mkubwa katika upatikanaji wa dawa.

Maduka hayo yamekuwa na manufaa kwa kuwa baada ya kuonana na mtaalamu katika hospitali, wagonjwa wamekuwa wakitakiwa kujitafutia dawa na kuzitumia kadiri ya ushauri wa wataalamu na hivyo, upatikanaji kwa kiasi kikubwa, bado umekuwa ni rahisi, na hatua hiyo, ya kuanzisha maduka mengi ya dawa, tunaipongeza.

Pamoja na umuhimu wote tulioutaja na hata ule uliosahaulika wa maduka hayo ya madawa, bado usemi kuwa kizuri hakikosi kasoro, unadhihirisha ukweli wake.

Tunasema hivyo kwa kuamini kuwa, ili famasia zetu zifanye kazi sawia kama inavyatarajiwa na jamii, na ili ziwe za manufaa badala ya kilio kwa jamii, ni sharti zitekeleze kanuni na miongozo iliyowekwa na taasisi husika hususan Wizara ya Afya na wahusika wengine.

Kwa kuwa suala la dawa na afya ya mwanadamu ni nyeti, Sheria na kanuni za uendeshaji wa huduma ya dawa hazina budi kutiliwa mkazo ili kuwanusuru wanajamii wasiangamie zaidi kiafya.

Ni kwa kuzingatia uhalisi huo, maduka hayo ya dawa hayawezi kuachiwa yaendeshwe katika mtindo ambao unakiuka taratibu hizo muhimu na hivyo, kuziweka afya za jamii mashakani.

Kwa mfano, haiwezekani na ni hatari duka la dawa hasa za binadamu, kuwekwa mahali popote kama jirani na kilabu cha pombe.

Tukumbuke kuwa duka la dawa ni kama nusu ya zahanati na hivyo huhitaji mazingira mazuri na ya kufaa. Hilo ni jambo mojawapo ambalo linatakiwa kuangaliwa sana.

Jambo jingine ambalo kweli ni nzito ni kuhusu watoaji au wasimamizi wa hayo maduka ya dawa. Kutoa dawa ni tofauti kabisa na kutoa bidhaa nyingine za kawaida.

Mtoa dawa sharti atoe dawa ya uhakika kwa mteja au mgonjwa. Kwa hiyo, hutakiwa kabisa awe na ujuzi wa juu wa mambo ya dawa. Tumnaamini wahusika wanalifahamu hilo na kwamba ni kiwango gani cha elimu kinatakiwa.

Ilivyo kwa kadiri ya mang’amuzi yetu, wengi wenye kuanzisha mambo ya biashara mara kwa mara, hujitahidi kuepuka gharama za msingi, ili kupata faida.

Hivyo kwa kuogopa kuwalipa wale wenye ujuzi, basi huwatumia watu wenye ujuzi mdogo na wasio na elimu ya kutosha kulingana na kazi hiyo.

Kwa kuwa kila kazi au huduma siku ya leo tukitaka kweli iwasaidie wananchi kwa kiasi cha kutosha, sharti iendane na kisomo, watoa huduma ya dawa wote katika maduka ya dawa hawana budi kuwa na elimu ya kutosha katika fani ya dawa.

Mwenye kutoa dawa au kuuza dawa, pia ni mshauri katika mambo hayo ya afya. Ili mtu atoe ushauri bora, hana budi kuwa na elimu juu ya shughuli nzima ya utoaji dawa na pia kumshauri mwenye kutumia madawa.

Tunapenda kuwapongeza wote waliowaweka madaktari katika maduka yao ya madawa na kwa kuwa licha ya kutoa dawa, hutoa pia ushauri wa kitaalamu wenye kulingana na hitaji la mgonjwa.

Hilo tunapenda liwe ni hasa tarajio la wote wanaoanzisha au kuendesha maduka hayo. Tunaamini kuwa licha ya maduka hayo kufungwa, wamiliki watajitahidi kurekebisa pale ambapo kwa kadiri ya wataalamu na wahusika, wameona kumeonekana kasoro.

Ni wazi kuwa tunahitaji sana maduka ya madawa sehemu mbalimbali ya nchi yetu, lakini, lazima tuangalie viwango vya ubora. Tunaweza kuwa na maduka mengi ya dawa ambayo hutumika zaidi kibiashara kuliko kihuduma.

Kuna mwelekeo mkubwa sana kwa watu wengi hasa wale wenye pesa kuanzisha maduka kama hayo kwa ajili hasa ya kuchuma kuliko kutoa huduma kwa wananchi. Na kwa upande mwingine, hakuna mtu asiyeelewa kuwa huduma nzuri hudai gharama kubwa pia.

Ni dhahiri mtoa huduma anahitaji "kipangusa jasho" na hivyo, wenye maduka hayo ni haki yao kujipatia faida kidogo ili waendeshee miradi na familia zao.

Tunatoa wito kwa wamiliki wa maduka ya namna hiyo, wasitumie dhiki za wagonjwa, kujitajirisha haraka haraka. Wafanye biashara au huduma hiyo kwa moyo wa kizalendo na kiutu kweli.

Tunawasihi waliokumbwa na kimbunga cha kufungiwa maduka yao ,warekebishe kasoro zilizojitokeza katika maduka yao ili waendeleze huduma zao muhimu kwa jamii.

Kwa kuwa hiyo ni biashara, basi wakamilishe masharti ya kibiashara, kwa na kuwa ni huduma kwa binadamu, wakamilishe masharti yanayodaiwa na Idara ya Afya.

Hata hivyo tunaishauri Bodi ya dawa nchini, isimalize nguvu zake jijini Dar-Es-Salaam, itembelee katika mikoa na wilaya nyingine ione yaliyopo huko.

Hongera Jeshi la Polisi

Ndugu Mhariri,

Naomba sehemu walau kidogo ya ukurasa katika gazeti lako la KIONGOZI ili nitoe dukuduku langu juu ya Jeshi letu linaloshughulikia usalama wa raia na mali zao.

Mhariri ni dhahiri nitakuwa mnafiki endapo nitakalia pongezi zangu nikizificha badala ya kuzitoa wazi kwa kuwa, anayefanya jema hana budi kupongezwa na pia, anayevurunda, hana budi kulaumiwa.

Pongezi zangu ningezitoa pengine sambamba na raia aliyewezesha Jeshi hili la Polisi nchini kugundua kilipo kiwanda cha kutengeza dawa haramu ya kulevya katika eneo la Kunduchi hapa jijini Dar-Es-Salaam.

Kugundulika kwa mitambo hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja, na kukamatwa kwa watuhumiwa wanaohusika na mitambo hiyo haramu, sio siri kwa kiasi kikubwa kumetoa mchango mkubwa kwa wananchi kujenga imani kwa jeshi hilo kwani ni wachache ambao wangetarajia hilo lifanyike.

Dhana hii inajengeka kwa kuamini kuwa jeshi hili ni miongoni mwa vyombo na taasisi ambazo zimekuwa zikilaumiwa sana kwa kuhusishwa na kashfa ya rushwa.

Ni kwa mantiki hiyo, ni wachache wangeamini kuwa mfanyabiashara kama huyo angeweza kukamatwa bila kutoa rushwa nayo ikapokewa na hivyo akafumbiwa macho kuendelea kuangamiza taifa la Tanzania.

Ninasema HONGERA JESHI LA POLISI kwa kufanya vizuri kazi hiyo kwa kuwa ni nani asiye jua madhara ya dawa za kulevya ? ni nani asiyejua dawa hizo zinavyoathiri afya za watumiaji na hata kuwavuruga akili?

Ni nani ambaye hajui hata wafanyabishara wa dawa hizo wanavyojisahau kimaadili na kujihusisha mno na ulevi, umalaya na kutumia vibaya fedha ambayo ni kitu cha thamani kwa taifa lolote likiwamo hili letu?

Napenda kuwashauri hawa askari wetu wa Jeshi la Polisi wa kitengo maalumu cha kuzuia dawa hizo za kulevya, na wale wa vitengo vingine kuendeleza uzi huo huo ili hao wanaoliangamiza taifa,wafichuliwe bila kuogopwa wala kuonewa aibu.

Hata hivyo ninaamini kabisa kwa upeo wangu binafsi,Polisi wenyewe hawawezi kufanikisha kazi hii ya kufichua maovu haya ikiwa raia hawatazidi kuwapa ushirikiano wa kutoa taarifa za watu na majengo wanayoyatilia mashaka kuhusika na uhalifu wa aina yoyote ukiwamo huu wa uzalishaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.

Licha pia ya kuishauri serikali kuongeza umakini wakati vitu kama hivyo vinaingia nchini, ningependa kulisihi jeshi hili kuhakikisha kuwa yeyote anayetoa taarifa za kuhofia au kushuku hujuma fulani, hatiwi kashikashi na yeyote, iwe taarifa zake zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa au la.

Jeshi lihakikishe linawahifadhi kwa usalama wao, watoa taarifa wote ili wasiwindwe na maadui na kuwafanya wengine waogope kutoa taarifa za namna hiyo.

Ninaliomba Jeshi hili chini ya Uongozi wa Mahita na Wizara husika ya Mambo ya Ndani ichunguze kwa makini wote wenye hisa katika mitambo hiyo. Kama kuna "Vigogo" au "vibosile" wanaovaa ngozi ya kondoo kumbe ni chui, wamulikwe na kusombwa.

Lakini licha ya kusema HONGERA JESHI LA POLISI, Watanzania tusingetegemea watuhumiwa waishie kula bure polisi, na kukanyaga mahakama kisha wakarudi. Hii haitakuwa tiba bali ni kichocheo cha maradhi.

Christina Damas,

Kinondoni,

Dar-Es-Salaam.