Krismasi, Mwaka Mpya sawa lakini tumemtumikiaje Mungu?

DESEMBA 25 Wakristo nchini wataungana na wenzao kote duniani katika kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu na Mfalme wa Amani duniani.

Ni bahati wanayoipata wachache kusherehekea Sikukuu hii na hata kusherehekea maadhimisho ya sherehe za Mwaka Mpya ambazo huadhimishwa kila ifikapo Januari Mosi.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kumshukuru kwa dhati Mwenyezi Mungu kwani ni bahati ya pekee aliyomjalia hata kuumaliza mwaka na kuuona mwaka unaofuata.

Ni kwa mantiki hiyo, ndiyo maana kila mmoja wetu anapaswa kujua kuwa wakati huu ni wakati ambao watu hutoa sala mbalimbali wakishukuru kwa baraka za wakati uliopita na kumuomba Mungu awajalie tena baraka katika siku zijazo.

Kipindi kama hiki, pia hutumika kwa jamii kufurahi kwa kula, kunywa na kucheza pamoja wakiwa watoto wa familia moja ya Mungu.

Wakati tunamshukuru Mungu kwa kutujalia neema ya kushangilia Siku hii ya kuzaliwa Masiha kwa sala, nyimbo, chakula, vinywaji na burudani mbalimbali, ni vema pia tukatumia fursa hii kujipima tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi kimwili na kiroho.

Tunaanza kwa kuwapongeza wale wote waliobahatika kushiriki kwa uaminifu katika kumtumikia Mungu kwa kufuata maelekezo yake na kuyapinga vikali maongozi potofu ya shetani.

Tunawapongeza waliofanikiwa kujenga nyumba na kubariki ndoa zao katika Kanisa na zaidi, Mungu akawajalia hata zawadi ya watoto. Hao waifurahie hio na wawajibike viapasavyo kuzilea familia zao.

Bado kwa jumla tunawapongeza wote waliojiwekea malengo yasiyokiuka mapenzi ya Mungu na hatimaye wakafanikiwa kuyafikia au wakayakaribia na tunaamini Mungu atazidi kuwajalia ili wayakamilishe katika kipindi kijacho.

Hata hivyo, wakati tunasherehekea Sikukuu ya Kuzaliwa Yesu Kristo (Noeli) na hii ya Mwaka Mpya, tukianzia kwa Wakristo, Waislamu, Wahindu, Wapagani na Waamini wa dini na madhehebu mengine, kila mtu kwa nafasi yake ajiulize kuwa ni kwa kiasi gani amemtumikia Mungu kwa uaminifu.

Kila mmoja ajiulize amempenda jirani yake kwa kiasi gani, ni upendo wa ki-Mungu au ni ule wa kinafiki na wa kishetai? Kila mmoja ajiulize ni kwa kiasi gani yeye mwenyewe hakutenda yale anayotaka wengine wasiyatende.

Bado tunasema kila mmoja ajiulize kuwa ni kwa kiasi gani amemtendea mwenzake yale anayotaka atendewe yeye na hakumtendea mwenzake mabaya asiyotaka yeye mwenyewe atendewe.

Mfano, kama ni mwandishi wa habari ajiulize ni mara ngapi labda ameandika habari na makala za kupinga uzinzi na uasherati na yeye kweli akaishi kiaminifiu kama alivyoandika. Ajiulize kama hali hiyo inampendeza Mungu.

Kama ni kiongozi wa Serikali, ajiulilize kuwa ni mara ngapi amesimama jukwaani na kutoa hotuba zinazojenga chuki na utengano miongoni mwa jamiii na hivyo kuwa chanzo cha mapigano, vita na mateso katika jamii? Huyo naye, ajiulize kama hali hio inampendeza Mungu.

Tunasema, kama ni kiongozi wa dini, ajiulize kuwa ni mara ngapi amefanya anayohubiri katika utumishi wake.

Ajiulize ni mara gapi hakuhubiri uongo na uchochezi, mara ngapi hakuwa mbadhirifu, msengenyaji wala mwenye wivu na chuki kwa wengine ama wakubwa, au wadogo zake kikazi, kimwili na hata kiroho.

Ajiulize ni mara ngapi hakuwa kikwazo kwa wengine katika kumfuata Yesu Kristo kutokana na matendo na maneno yake.

Sisi tunasema, kila mmoja ajiulize kuwa tunaposherehekea Krismasi na mwaka Mpya, mbegu yake imezaa matunda mangapi mema au imezaa matunda machungu na yanaathiri vipi utukufu wa Mungu.

Ajiulize kuwa kwa nafasi yake, ametumwa na Mungu kufanya hivyo au anamsaliti Muumba wake.

Basi kwa kuwa tunaamini kuwa Mungu alimtuma Mwanaye wa Pekee Yesu Kristo kuja kuukomboa ulimwengu, kipindi hiki sasa kisiwe kipindi cha kuhesabiana makosa bali kiwe kipindi cha kusameheana kwa kuzaliwa na Yesu na kutembea naye katika masiha. Njia zote zinazokuwa na muelekeo wa kugawa uhusiano baina ya wanadamu na Mungu, ni vema jamii ikaziepuka.

Tunasisitiza kuwa ni vizuri kila mmoja akajua vema maana ya sikukuu hizi na namna ya kuzisherehekea. Ajue kuwa Yesu hakuja duniani kuchochea vitendo viovu bali kuwakomboa walio utumwani mwa dhambi.

Hivyo Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya hazipaswi kamwe kutumika kama siku za kuchochea uovu na vitendo vya uhalifu kwa jamii.

Hazipawi kuwa ndizo siku za ulevi, uzinzi, uasherati, ugomvi, vita, usengenyaji, chuki za chini chini na majigambo yasiyo na maana.

Sisi tunasema kuwa, itakuwa aibu ya kimwili na kiroho kama wakati Yesu anazaliwa Desemba 25, wewe utakuwa katika mdomo wa mamba tayari kwa kufariki kwa UKIMWI kwa kuwa eti umesherehekea Krismasi bila mpango na hatimaye, ukajitumbukiza kwenye janga la maambukizi ya ugonjwa huo.

Sikukuu ya Krismasi itujenge upya kiroho, isherehekewe kwa amani, utulivu, umoja, upendo na mshikamano vyote vikiwa chini ya sala na ulinzi wa mikono ya Mungu iwe katika kula, kunywa na kuburudika kwa namna yoyote. Mungu atangulizwe.

Mwisho tunawatakia sikukuu njema ya Krismasi na heri ya Mwaka Mpya.

Zimamoto mnafanya kazi gani?

Ndugu Mhariri,

Naomba unipatie nafasi kidogo katika gazeti lako la KIONGOZI ili nitoe yanayonikera na kunisikitisha dhidi ya hawa wenzetu wanaofanyakazi katika Kikosi cha Zimamoto hapa jijini Dar es Salaam.

Kwa kweli inasikitisha sana kuona wanashindwa kufanya kazi ipasavyo likiwamo jukumu la kuzuia ajali za moto zisilete madhara makubwa zinapotokea.

Mara nyingi tunashuhudia nyumba na vitu mbalimbali vikiteketea mbele ya watumishi hawa wa Kikosi cha Zimamoto ambao ni maarufu kwa jina la FAYA.Hii Yote inatokana na uzembe na pengine unaosababishwa na labda kutokuwa na sheria ya kazi inayowabana na kuwawajibisha wanaohusika na uzembe kama huo.

Ninauita ni uzembe kwa sababu karibu kila matukio ya moto yanayotokea, wao huwa wa mwisho kufika na huku wakiwa wamesheheni visingizio wanavyotumia kulinda uzembe wao.

Ni dhahiri katika kazi yoyote, wakati mwingine hujitokeza matatizo ya kiufundi yanayokuwa nje ya uwezo wa kawaida kuepuka kwa wakati huo lakini, ni vema na sahihi kuwa visingizio hivyo viwepo kwa kila siku na kila tukio badala ya kukaa katika hali ya tahadhahari kama ilivyo asili ya kazi yao? Kama ni hivyo maana na faida ya kuwapo Kikosi hicho iko wapi?

Limekuwa jambo la kawaida kusikia kuwa magari ya kikosi cha Zimamoto yamefika kwenye eneo la tukio huku yamechelewa, haya, pole sana labda kutokana na msululu wa magari na muda wa kupatikana kwa taarifa hiyo.

Lakini, iweje magari ya Zimamoto licha ya kufika yamechelewa, yafike na "robo lita" ya maji au bila maji kabisa? Huwa yanafuata nini pale au ni njia ya kuhujumu mafuta na labda kuna kingine kinachotafutwa?

Mfano mzuri, ni hivi karibuni kulipotokea moto mkubwa katika jengo la Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Wafanyakazi wa Kikosi cha Zimamoto na magari yao walifika karibu kabisa na mwisho wa tukio.

Kama hiyo haitoshi, walikuja na "maji nusu chupa" kwa ajili ya kuzima moto mkubwa kwenye jengo kubwa namna ile.

Hali hiyo inanifanya niamini kuwa hawa watu hawako makini na kazi yao bali wapo tu kubabaisha na pengine hawajui maana na umuhimu wa wao kuwapo katika kitengo hicho.

Malalamiko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitolewa na watu mbalimbali yalikuwa ya kutosha kutufanya tuamini kuwa watumishi wa kikosi hiki muhimu watajirekebisha, lakini juzi tena kumezuka moto mkubwa katika kituo cha Umeme Ubungo jijini Dar es Salaam, waliosaidia wa kwanza ni NIGHT SUPPORT ambao tunawapongeza sana.

Sasa nyie watu wa FAYA kama mlivyozoeleka, jiulizeni kuwa kama Knight Support wasingekuwapo kama zamani, hali ingekuwaje pale Ubungo? Hivi nyie huwa mnalala wapi na aina gani ya usingizi hadi kila tukio mnakuwa wa mwisho kufika?

Cha kushangaza na kuchekesha mnakwenda bila maji mnapoulizwa, mnasema eti mlikwenda kuangalia moto una ukubwa gani ili mkachukue maji. Hivi kweli mpo makini na kazi au basi tu mnafika tu ili kutimiza wajibu wa kufika?

Kwa kweli ni jambo la kusikitisha sana mnaitwa muende mkazime moto, kisha mnakwenda kuangalia ukubwa wa moto hayo magari yenu ni mapambo?

Ni vema mkajua kuwa katika ajali na matukio ya moto, kinachohitajika sio kufika na kuonekana kwenu pale, bali ni huduma mnayoitoa ili kuokoa maisha ya watu na mali zisiangamie kwa moto.

Umefika wakati ambao mnapaswa kuchagua moja, ama kuacha kazi au kuendelea maradi tu, jamii nayo ijue moja. Hata wanaoamua kuendelea na kazi , sasa ni wakati wa kuipenda na kuithamini kazi yenu mkizingatia kuwa mliipokea mkijua majukumu yake na pasi na shaka, tunaamini watumishi wote mliomba kazi hizo bila kulazimishwa na mtu hivyo, pendeni kazi yenu ili iwafae katika maisha.

Agusta Fertgerald,

C/o P.O. Box 27014

Dar-es Salaam