Make your own free website on Tripod.com

Twawapongeza Waislamu kumaliza Mfungo wa Ramadhani

KATIKA siku zisizozidi tatu kuanzia Jumamosi ii, ndugu zetu Waislamu wanahitimisha Mfungo wao Mtukufu wa Ramadhani. Kwa muda wa takriban mwezi mmoja, ndugu zetu Waislamu wamekuwa katika Mfungo wa kila mwaka.

Mfungo huo, ni moja kati ya nguzo tano katika Dini ya Kiislamu.

Sote tunatambua kuwa kazi ya kufunga na kujinyima ni tendo gumu sana, lakini hupewa nguvu ya mtu katika dini au kwa Mwenyezi Mungu.

Mtu akiwa na imani thabiti ni dhahiri atafanya mambo mengi hata yale ambayo ni magumu. Mtu anapofunga au kujinyima chochote ama kinachoshikika au kisichoshikika, kikiwamo chakula na kinywaji, huwa kwa namna fulani anajitesa mno.

Lakini kwa vile mtu hufanya tendo hilo la kufunga kwa nia ya kumpendeza Muumba wake, basi hujipatia mastahili kutoka kwa huyo Mwenyezi Mungu.

Kwa kawaida tendo la kufunga kwa kila dini huenda pamoja na sala,toba ya kweli na kutoa sadaka ama zaka.

Sisi tunatumaini kuwa ndivyo walivyofanya hawa ndugu zetu Waislamu katika Mfungo wa mwaka huu na hata kwa miaka mingine.

Hayo yote huenda pamoja, kwani kufunga tu haitoshi, bila kuongeza saa za kusali pamoja na kuwa na wema na ukarimu kwa wanyonge na maskini.

Tunaweza kusema kuwa wakati wa Mfungo Mtukufu ni muda wa muumini kufanya mabadiliko ya kiroho yaani kuachana na dhambi na kumgeukia Mwenyezi Mungu.

Wakati wa Mfungo huo muumini hufanya tafakuri juu ya mwenendo wake wa kiroho mbele ya Mwenyezi Mungu.

Licha ya kuyaangalia maisha yake yalivyo mbele ya Mwenyezi Mungu, pia huyaangalia mahusiano yake na jirani yake pamoja na binadamu wote anaoishi na kukutana nao kila siku. Hapo neno kubwa ni hasa upendo na huruma kwa binadamu wenzake.

Neno kubwa katika kila mfungo ni kufanya mabadiliko ya ndani, mabadiliko ya kiroho ambayo hujionesha hata kwa nje. Hii inamaana kuwa kipindi cha mfungo, ni kipindi kinachoanzisha rasmi mabadiliko ya kimawazo, kimaneno na kimatendo na kikubwa zaidi, kumuelekea Mungu.

Kwa hiyo tunataraji kwamba hawa ndugu zetu Waislamu licha ya kuwapongeza kwa kumaliza huo Mfungo Mtukufu, tunapenda pia kuwakumbusha kwamba huo mfungo unapaswa kuwa na faida kwao binafsi, lakini pia kwa binadamu wenzao, Waislamu na wasio Waislamu.

Tungeweza kusema hao ndugu zetu Waislamu baada ya huo Mfungo Mtukufu watakuwa watu wapya kiimani, kifikra na hata kimaadili.

Tunaamini kuwa wema, upole na ukarimu waliouonesha katika kipindi hiki, hautakuwa wa mpito bali utakuwa mwanzo unaohitaji kutunzwa na kuboreshwa zaidi.

Kwa Mfungo huo Mtukufu tunaamini kwamba watakuwa wameachana na mambo mbalimbali ya giza yaani dhambi. Kwa mfungo huo tunatumaini kuwa watakuwa ni vyombo vya amani katika nchi yetu kuanzia kwenye familia na jumuiya zao za Kiislamu na hata kwa taifa zima.

Tunatumaini kuwa Mfungo Mtukufu wa Ramadhani utazidi kudumisha uhusiano mzuri baina ya waumini wa Dini ya Kiislamu na waumini wa dini na madhehebu mengine.

Tunaomba udugu uliokuweko kati ya Waislamu na waumini wa dini na madhehebu mengine, uzidi kudumu na kuimarishwa licha ya tofauti ndogo ndogo zilizopo za kibinadamu.

Tungependa kuona katika Siku ya Eid-El-Fitri, Waislamu na wasio Waislamu wanakaa, wanakula, wanakunywa na kuzungumza na kucheza pamoja kama ndugu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma katika nchi hii.

Inapendeza sana kuona waamini wa dini na madhehebu mbalimbali wakikaa pamoja kwa upendo wakifanyakazi kwa ushirikiano na kuvuna matunda ya umoja, upendo na amani.

Kwa upande mwingine, tunatumaini kwamba baada ya huo Mfungo Mtukufu, hawa ndugu zetu kwa pamoja watakuwa wamepata nguvu ya kupigana kikamilifu na ugonjwa huu wa UKIMWI.

Tunaamini pia kuwa, katika Mfungo huo, hawakukosa kuliombea Taifa letu liweze kuepukana na janga hilo.

Bado sisi tunaamini kwamba hata Waislamu hao wenyewe baada ya Mfungo huo Mtukufu wa Ramadhani, watakuwa imara kabisa katika kupigana na gonjwa hilo.

Tunazidi kuwatakia Sikukuu njema ya Eid-El-Fitri ndugu zetu Waislamu wote. Tunaomba hizo baraka walizozipata katika Mfungo huo Mtukufu, zidumu katika mioyo yao na katika familia zao na taifa kwa jumla.

Tunaamini pia kuwa, Sikukuu yoyote inapendeza ikiimarishwa na sala, upendo, na amani na matendo bora na hizo, ziwe ndizo nguzo zetu katika kumtumikia Mungu na kulitumikia Taifa.

Tunawapongeza Waislamu wote waliofunga kwa uaminifu wakilenga kumuonesha Mungu upendo na uaminifu wao. Mola awabariki Waislamu wote na awadumishe katika amani ya kweli.

Twaomba Kuzingatia, Baba uleye Mbinguni

1. Mathayo kaulizia, "Sala ipi omba vema,

Kristo akamwambia, Ogopeni ya kiama,

"Heri nane " wania, Na msifanye dhuluma,

Yesu hutuhurumia, wacha domo kuloloma.

2. "Kulia lia" kichizi, Viumbe chini ya mbingu,

Uchuro pia ulozi, Mna mkosea Mungu,

Ombeni rehema dozi, Kesho hupati uchungu,

Yesu alinena wazi, ibada zao mizungu.

3. Kuzurura mitaani, "Lia lia" kanisani,

Waenda mkutanoni, Huyu hoi kitandani,

Anaumwa taabani, Okoka kweli jamani?

Yesu ni ibada gani, Injili hiyo ya nani?

4. Mchungaji fafanua, Ni somo au maono?

"Kuokoka " ninajua, Kama tundu la sindano,

Mfumo kuubutua, Lokole lenye maneno,

Yesu aliyachambua, "kuanguka" ni mfano.

5. Ndoa aipa kisogo, Aende huko na zake,

"Kuokoka bure zogo, Kunaleta peke peke,

Aondoke kwa mikogo, Walimwengu wamcheke,

Yesu mtue mizigo, Kesho peponi afike.

6. Mapokeoye Mathayo, Mwanafunzi wakeYesu,

Tusali kimoyo moyo, Msalaba tuubusu,

"Mlokole " mwiko hayo, Asema hayamhusu,

Yesu hao ni vihiyo, Toba zao nusu nusu.

7. Tuombe Baba Mbinguni, Atupe riziki zetu,

Lifanyike duniani, Asamehe kila mtu,

Tuopoe maovuni, Kila somo lenye kutu,

Yesu penda waamini, Na wapagani vibutu,

8. Eti "haombei " wafu, Twawaona na sikia,

Zama zao kukashifu, Ajabu hiyo tabia,

Bishara zao potofu, Ndani ya hii dunia,

Yesu mwana timilifu, Mbona hukulia lia?

9. Mna payuka payuka, Kina wasibu ni kipi?

"Vilio" juu sikika, Teolojia ya wapi?

Swali nani "kaokoka," Yu hai hajafa yupi?

Yesu uliye tukuka, Wasamehe au vipi?

10. Hekima asili mali, Warithi wanangu peke,

Karama toka jalali, Mioyoni mziweke,

Busara zenu wakili, Tulieni mnizike,

Yesu wabariki hili, Vichwanimwao waweke.

Mhando, M. Makunga - Pindu - Sese yamoto

(Mzee) S. L. P 25311,

DAR ES SALAAM.