Make your own free website on Tripod.com

Masomo ya twisheni sio dawa ya kufaulu

HIVI sasa tunashuhudia matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne iliyofanyika mwaka jana. Matokeo hayo kwa jumla siyo mazuri hasa kwa shule nyingi za Serikali na za binafsi.

Kwa shule za seminari, matokeo yanafurahisha sana. Wazazi na wahusika wengine ikiwamo Wizara ya Elimu wanapaswa kujiuliza, ni kwa nini seminari na baadhi ya shule za Serikali zimekuwa na matokeo mazuri.

Umekuwapo mtindo wa kuwapatia wanafunzi elimu kwa njia ya "tuition" yaani masomo ya ziada nje ya ratiba ya shule huko mitaani.

Tunasema moja kwa moja kuwa njia hiyo ya utoaji elimu kwa njia ya bishara, haifai kwani seminari zenye kufaulisha wanafunzi kwa kiwango cha juu, hazina kitu hicho.

Kinachofanyika ni kwamba walimu hutumia muda wa vipindi, kuwafundisha wanafunzi kwa kadiri ya uwezo na ujuzi wao katika masomo mbalimbali. Hivyo, walimu hujitoa mhanga kuwafundisha wanafunzi madarasani bila kutegeshea biashara ya twisheni.

La msingi kujiuliza ni kuwa, mbona walimu wanaofundisha katika seminari na nyingine chache za Serikali wanafundisha kwa moyo na juhudi hadi watoto wanafaulu vizuri?

Jibu lake sio siri na linaeleweka. Kwanza, walimu wanalipwa mishahara kwa wakati muafaka bila kucheleweshwa. Pia, kuna mazingira mazuri ya kufanyia kazi kama nyumba nzuri, huduma za maji, umeme na huduma nyingine muhimu.

Pia, uhusiano wa kidugu kati ya mwalimu na wakubwa wake wa kazi unazingatiwa katika taasisi hizo. Daima walimu wanapokuwa na matatizo, wakubwa wao huwa tayari kuwasikiliza na hata kuwasaidia.

Lingine linalosaidia kufaulisha wanafunzi katika seminari, ni upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada.

Shule nyingi za serikali na za watu binafsi hazina vitabu hivyo na wanafunzi wanabaki kuhangaika. Kumbe mambo ni tofauti katika seminari.

Mambo ni kinyume zaidi kwani hata mishahara ya walimu wa shule za serikali, hupatikana kwa shida na hucheleweshwa sana bila mtu wa kuwasikiliza wala kuwasaidia.

Hali hiyo inawafanya walimu wengi kuwa wazembe na wavivu katika kufundisha darasani na hivyo, kujenga mazingira na tabia ya kugonjea kwenda kwenye "tuition" ambako nako elimu hutolewa kwa nmna fulani ya upendeleo.

Pia, hali hiyo huufanya uhusiano baina ya walimu, wanafunzi, wazazi na shule kwa jumla, sio imara kijamii na kitaaluma.

Sisi tunasema kuwa masomo ya ziada (tuition), si suluhisho la watoto kufanya vizuri kitaaluma kwa kuwa ni ya ubaguzi na yanatolewa kwa watoto wa wazazi wenye uwezo wa kumudu gharama na pia, nayo yana mchngo mkubwa kwa watoto kubomoa maadili hasa wanapokwenda katika masomo hayo hata nyakati za usiku.

Masomo ya twisheni ni mabaya kwa kuwa yamewafanya walimu wengine hata kwa makusudi, kuzembea darasani ili wapate wateja katika twisheni zao. Hatukatai kama mwalimu kwa nia nzuri ameamua kuwasaidia watoto kwa pamoja, afanye hivyo kwa mahali na wakati muafaka yaani, masomo ya kujirekebisha(remedial classes)

Sisis tunasema, tuwisheni sio dawa ya watoto kufaulu katika mitihani, dawa ni walimu kuwekwa katika mazingira mazuri ya kufundisha ikiwa ni pamoja na kupewa mishara ya kutosha na kwa wakati mufaka, nyumba, na vitendea kazi vingine muhimu vinavyohitajika.

Kingine kinachohajika kutumika kama dawa la mafanikio kitaalauma katika shulecmbalimbali, ni moyo wa kila mwalimu kujisikia sifa kuwafundisha watoto wakaelewa na kufaulu na hapa pia, uongozi bora na utawala safi katika shule, unahitajika.

Ni muhimu wazazi wakashirikina na walimu kuwafanya watoto wawe na lengo moja la kupenda masomo na hivyo, kila mmoja kulenga kufaulu kwa alama za juu.

Hongera Monsinyori Kangalawe kwa kutuweka wazi

Ndugu Mhariri,

NAOMBA uniweke walau pembeni mwa gazeti lako tukufu la KIONGOZI ili niweze kumshukuru na kumpongeza sana Katibu wa Idara ya Liturujia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Monsinyori Julian Kangalawe, kwa kututoa wasiwasi na kutueleza kinagaubaga mintarafu msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Nyaraka hizo za vitisho.

Msimamo huo alioutoa katika Gazeti la KIONGOZI, Toleo la Aprili 7-13, 2001 katika habari yenye kichwa cha habari, "HATUTAMBUI NYARAKA ZA VITISHO", umetusaidia kutokana na hofu iliyotukumba baadahi ya Wakristo baada ya kupokea barua hizo na kushindwa kutekeleza masharti yake.

Kwa kweli nyaraka hizo zimeenea kote nchini mwetu na hata karibu mataifa mengi nyaraka hizi zimesambazwa.

Ni kweli kwamba nyaraka zenye kichwa cha habari, "BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA" zimekuwa tishio kubwa kwa waamini na zimewapa wasiwasi mkubwa mioyoni mwa watu ikiwa ni pamoja na kukatisha tamaa kabisa dhidi ya maisha yao; na hasa pale zinapotoa vitisho vya hatari kwa maisha ambayo vingeweza kumpata mtu asipoto asipotekeleza maagizo hayo ya kusambaza barua 28 ndani ya siku 10.

Tunamshukuru sana Monsinyori J. Kangalawe hasa pale anaposema nyaraka hizo ni za kitapeli kwani hazijatolewa tangazo lolote toka kwa Mamlaka ya Kanisa na kwamba, hatujui mwandishi wa nyaraka hizi kwani huenda ni mpinzani mkubwa sana na upendo wa Mungu anayewataka watoto wake waokolewe na wala si kinyume cha hayo.

Pia, mwanzilishi huyu amemshirikisha Mtume Yuda Thadei ashiriki na mambo hayo ya kitapeli kinyume cha matakwa ya Kanisa kwani Yesu mwenyewe aliyekuja kwa ajili ya wakosefu.

Kwa kweli tunamshukuru sana Monsinyori Kangalawe kututoa wasiwasi huo.

Nadhani tulikuwa wengi ambao wasiwasi huo ulitukumba dhidi ya nyaraka hizo.

Hivyo, sasa ni jukumu letu waamini hasa Wakatoliki kuwa na msimamo thabiti juu ya nyaraka hizo za kitapeli, tukizipata tujue namna ya kudhibiti na kupeleka pale panapohusika.

Xaver Mssillu,

P.O.Box 510,

Kihesa-Iringa.

Shairi

Shairi hili lilikuwa mahususi kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka

Leo Chereko Chereko

1. Amefufuka Mwokozi, Mauti amepitia

Ndiye hasa Mkombozi, Mbinguni na wa dunia,

Ameleta ukombozi, Dunia twashangilia,

Leo Chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

2. Mkombozi kafufuka, Chereko hizi Chereko,

Kaburini Kafufuka, Mapema mapambazuko,

Msiwe nayo mashaka, Galilaya ndiko yuko,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

3. Amepewa mamlaka, Ya mbingu na ya dunia,

Ameagiza kushika, Yote alotuambia,

Amri walioshika, Batizeni nawaambia,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

4. Tukampambe twendeni, Tubebe zetu zawadi,

Hima twende Kanisani, na maua ya waridi,

Twendeni hadi Chumbani, na manukato ya udi,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

5. Nguo nyeupe na njano, Tuzivae na heleni,

Tufanye maandamano, twendeni Kanisani,

Tubebe zawadi nono, tutoe altareni,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

6. Tukitoka kanisani, nyumbani tukishafika,

Tukaribishe wageni, Pasaka kujumuika,

Tuwe nao sebuleni, tule tunywe nao koka,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

7. Chakula tule kiasi, Pombe tunywe kwa kipimo,

Tusilipize kisasi, Shangwe ziwe za nderemo,

Tusifanane na fisi, asiyejua kipimo,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

8. Ugomvi pia matusi, Tuepuke ni hatari,

Tusiyafanye maasi, tusijeleta dosari,

Tutashikwa na polisi, Kama tutafanya shari,

Leo chreko chereko, Mkombozi Kafufuka.

9. Tuziepuke ajali, njiani tukitembea,

Magari tupishe mbali, upande yakisogea,

Nyumba tufunge kufuli, wezi wasijeikomba,

Leo chereko chereko, Mkombozi Kafufuka.

10. Nawaombea amani, Pasaka shangilieni,

Kujipamba jipambeni, hata muziki chezeni,

Mialiko peaneni, kumbukeni na nyumbani,

Kila la heri kwa wote, leo ninawatakia.

Mwana UVIKASO,

Joseph Kalimba Chicago (Simba Mtoto)

C/O Fr. Xavery Kazimoto Komba

Box 147- Mwenge Mshindo,

SONGEA