Make your own free website on Tripod.com

Daktari wa Kiongozi

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini na mahali ambapo si rahisi kumpata mtaalamu wa afya kwa haraka

Chakula Bora kwa Bei Nafuu

Wengi wa watu duniani hula vyakula vya wanga kwa wingi, lakini hawali vyakula vya kutosha vilivyo na protini, vitamini, na madini. Hii ni kwa sababu ya vyakula hivi vizuri huuzwa ghali sana.

Protini za wanyama kama vile maziwa na nyama ni nzuri sana kulisha mwili, lakini pia ni ghali. Pia wanyama huhitaji ardhi zaidi kwa protini wanayotoa.

Watu wengi hawawezi kununua vyakula vinavyotokana na wanyama kwa wingi. Kusema kweli, familia maskini inaweza kujipatia protini zaidi kama wanalima au wananunua vyakula vinavyotokana na mimea ambayo ina protini, kama vile maharagwe, njegere, dengu, karanga, na mboga za majani badala ya vyakula vinavyotokana na wanyama kama nyama na samaki ambavyo ni ghali,

Watu wanaweza kuwa na nguvu na wenye afya ingawaje protini zao zote zinatoka kwenye mimea.

Hata hivyo ni busara kula protini kidogo za wanyama katika kila mlo. Hii ni kwa sababu mimea haina protini zote zinazohitajiwa na mwili, ingawaje ina wingi wa protini.

Jaribu kula mchanganyiko wa vyakula vya majani kuliko kung’ang’ania aina moja tu au mbili, mimea tofauti huupa mwili aina mbalimbali ya protini, vitamini, na madini. Kwa mfano kutumia maharagwe na mahindi kwa pamoja huusaidia mwili vizuri zaidi kuliko kula kimoja tu peke yake. Na ikiwa mboga zingine na matunda yakiongezeka, hivi ni bora zaidi.

Jaribu kula aina mbalimbali za vyakula vinavyotokana na madini zaidi kwa bei nafuu.

1. Maziwa ya mama. Haya ni rahisi zaidi, yanaleta afya zaidi, na ni chakula kilichokamilika kwa watoto wachanga. Mama anaweza kula protini nyingi kutoka kwenye mimea na kuzigeuza kuwa chakula kikamilifu kwa mtoto - maziwa. Kumnyonyesha mtoto si kitu kizuri kwa mtoto tu, Kunaokoa fedha pia.

2. Mayai na kuku. Mayai ndiyo protini inayo- tokana na wanyama iliyo rahisi na nzuri zaidi mahali pengi. Yanaweza kuchanganywa na vyakula vingine na kupewa watoto ambao hawapati maziwa ya mama. Au yanaweza kutolewa pamoja na maziwa ya mama kwa jinsi mtoto anavyozidi kukua. zinaweza kutwangwa na kuchanganywa na chakula ili kutoa calcium ambayo inahitajiwa na akina mama waja wazito, ambao hupatwa na vidonda, kupotea kwa meno au mishituko ya misuli.

Kuku ni aina nzuri, na mara nyingi, rahisi, ya protini inayotokana na wanyama - hasa ikiwa familia inafuga kuku wake wenyewe.

3. Maini, moyo, figo, na damu.

Hivi vina protini, vitamini na Chuma (kwa upungufu wa damu) kwa wingi kabisa, na mara nyingi huuzwa kwa bei nafuu kuliko nyama zingine.

Pia Samaki ni nafuu kuliko nyama nyingi ingawa thamani yake ya chakula ni ile ile.

4. Maharagwe na aina zingine za jamii ya kunde, (njegere, dengu n.k.) zina protini hasa maharage ya soya. Kama yakiachwa yachipuke kabla ya kupikwa na kuliwa, yana vitamini kwa wingi zaidi.

Chakula cha mtoto kinaweza kutayarishwa kutoka katika maharagwe kwa kuyapika vizuri, kuyaondoa maganda na kuyapondaponda.

Maharagwe, njegere, na aina zingine za kunde siyo aina rahisi tu ya protini, Kama yakipandwa kwenye shamba huongeza rotuba katika udongo. Kwa hiyo mazao mengine yanayopandwa baadaye huzaa vizuri zaidi. Kwa sababu hii, ni wazo zuri kutumia mabadiliko ya mazao.

5. Mboga za majani. zina kiasi kidogo cha protini, chuma kidogo na vitamini A kwa wingi sana. Majani ya viazi vitamu, maharagwe na njegere, maboga, na mbuyu ni mazuri sana kwa chakula. Yanaweza kukaushwa na kufanywa kuwa unga ambao huchanganywa kwenye uji wa mtoto ili kuongeza protini na

Itaendelea toleo lijalo

Kanisa Katoliki na Umungu wa Yesu(3)

KATIKA toleo lililopita, makala hii ilifafanua ukweli na uhalisi juu ya Umungu wa Yesu Kristo. Katika toleo hili, tutaendelea kuchambua mafundisho hayo sahihi juu ya uhalisi na Umungu wa Yesu ikiwa ni pamoja na kujua maana ya jina KRISTO. Sasa, endelea,

Jina la Yesu ni kitovu cha sala ya Kikristo, sala zote za Kilitrujia huhitimishwa kwa maneno "Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo", Salamu ya Malaika - Salamu Maria" huhitimishwa na "Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa."

Sala ya Moyo na Makanisa ya Mashariki inayoitwa "Sala ya Yesu" husema: "Bwana Yesu Kristo Mwana wa Mungu unihurumie mimi mkosefu," Wakristo wengi kama Mt. Yona wa ARC wamekufa wakiwa na neno moja tu midomoni mwao "Yesu"

II. Kristo

"Kristo" ni tafsiri ya neno la Kigriki "Kristos," nalo ni tafsiri ya neno la Kiaramayo "Messiah," maana yake "Mpakwa." Limekuwa jina lake Yesu kwa sababu alitimiza kikamilifu utume wa kimungu ulio kadiri ya maana ya jina lenyewe.

Katika Israeli, wale waliokuwa wamewekwa wakfu kwa Mungu kwa ajili ya utume aliowakabidhi, walipakwa mafuta kwa jina lake; kama vile wafalme, makuhani,( Kut 29:7; Law 8:12;1 Sam 9:16;10:1;16:1,12-13;1Fal 19:16) na mara chache manabii.

Mtu wa aina hii alitakiwa awe bora hivi kama alivyokuwa Masiha ambaye Mungu angemtuma kuanzisha kikamilifu utawala wake.( Zab 2:2; Mdo 4:26-27) Masiha alitakiwa apakwe mafuta na Roho wa Bwana kwa mara moja kama Mfalme na Kuhani, na pia kama nabii. (Isa 11:2;61:1;Zek 4;14;6:13;Lk4:16-21) Yesu ametekeleza matumaini ya kimasiha ya Israeli katika kazi zake tatu za kuhani, nabii na mfalme.

Malaika aliwatangazia wachungaji kuzaliwa kwa Yesu, kama Masiha waliyeahidiwa Waisraeli: "Leo katika Mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana" (Lk. 2:11). Tangu mwanzo, Yeye ni "Yule ambaye Bwana alimtakasa na kumtuma ulimwenguni," aliyetungwa mimba kama "Mtakatifu" katika tumbo la Bikira Maria.(Yoh 10:36; Lk 1:35) .Yosefu aliitwa na Mungu "umchukue Maria mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu," ili Yesu aitwaye "Kristo" azaliwe na mchumba wa Yosefu katika ukoo wa kimasiha wa Daudi.(Mt. 1:20; Mt 1:16; Rom 1:1;2 Tim 2:8;Ufu 22:16).

Kuwekwa wakfu kwa Yesu kama Masiha kunafunua utume wake wa kimungu. "Kuanzia sasa kila kinachomaanishwa na jina lake lenyewe kinadhihirika kwa sababu katika jina la Kristo anatajwa yule aliyempaka mafuta, Yule aliyepakwa na mpako wenyewe ambao kwao amepakwa nao: aliyempaka rnafuta ni Baba, Yule aliyepakwa ni Mwana, na mpako wenyewe ambao kwao alipakwa ni Roho Mtakatifu.

Wakfu wake wa kimasiha ulio wa milele umefunuliwa wakati wa uhai wake hapa duniani, pale alipobatizwa na Yohani, wakati Mungu "alipomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu" "ili adhihirishwe kwa Israel (Mdo 10:38;Yoh 1:31) kama Masiha wake.

Kazi zake na maneno yake yatamfunua kama "Mtakatifu wa Mungu".(Mk 1:24;Yoh 6:69; Mdo 3:14) Wayahudi wengi na hata wapagani walioshiriki tumaini moja walitambua katika Kristo tabia za ‘Mwana wa Daudi’, Masiha ambaye Mungu alimwahidia Israeli.(Mt. 2:2;9:27;12:23; 15:22;20:30;21:9,15) .

Yesu alipokea jina la Masiha ambalo lilikuwa haki yake lakini siyo bila tahadhari fulani, kwa sababu baadhi ya watu walioishi wakati ule walimwelewa Masiha kibinadamu mno na hasa kisiasa.(Yoh.4:25- 26; 6 :15;11:27; Mt . 22 : 41 ; Lk 24:21).

Yesu alipokea ungamo la imani la Petro aliyemkiri kuwa Masiha,kwa kutangaza mateso ya Mwana wa mtu yaliyokuwa yamekaribia (Mt. 16:16-23).

Alifunua maana halisi ya utawala wake wa kimasiha, upande mmoja uthibitisho wa juu wa Mwana wa mtu aliyeshuka toka mbinguni:" na upande mwingine katika utume wa ukombozi, kama mtumishi anayeteswa: "Mwana wa Adamu asiyekuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.(Yoh. 3:13; Mt 20:28;Yoh 6:62; Dan 7:13. Isa 53:10-12).

Kwa sababu hiyo maana ya utawala wake itaonekana wazi tu atakapoinuliwa msalabani (Yoh 19:19-22; Lk 23:39-43).

Kitabu cha kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (16)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Tunaendelea na chapisho la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyovyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC). Tulianza na dibaji iliyooandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na sura za ndani.

Pili, na muhimu zaidi ni kwamba mahakama za mwanzo zilianzishwa karibu zaidi na mwananchi ili kusaidia katika kusuluhisha migogoro na siyo chombo cha mashindano na malumbano marefu ya kisheria.

Mawakili kwa kawaida wanapenda sana mashindano ya kisheria na hawaridhiki hadi mmoja ashinde na mwingine ashindwe.

Hali hii siyo nzuri katika mahakama za mwanzo ambapo watu wengi wangependa kufikia muafaka baada ya mjadala.

Hali hii ya kutowaruhusu mawakili kuendesha shughuli zao za utetezi katika mahakama za mwanzo imetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni kitendo cha ukiukwaji wa haki za binadamu. Tukiangalia umuhimu wa mawakili katika kusaidia mahakama kutenda haki wengi wanahisi kuzuiliwa mawakili kwenda kwenye mahakarna hizi kumechangia katika kuzifanya Mahakarna za Mwanzo zishindwe kutoa haki jinsi ilivyotegemewa kwani hawaoni sababu za msingi kuwanyima msaada wa mawakiii mahakimu wa mahakama za Mwanzo.

Hakuna shaka kwamba hali hii inawalazimu mahakimu wa mahakama za mwanzo kuwa makini katika uamuzi wao wa mashauri na hata katika utendaji wao wa kazi kwa ujumla kwani hawana msaada wa mawakili ambao wenzao wa Mahakarna za Hakimu Mkazi na za Wilaya wanapata.

Aidha Mahakama za Mwanzo zina uwezo wa kusikiliza rufaa zitokazo kwenye Mabaraza ya Kata (Ward Tribunals)

Kisheria kesi zinapaswa kuendeshwa mahali pa wazi na ambapo watu wamepazoea ili mtu yeyote mwenye kupenda kusikiliza au kufuatilia kesi fulani aweze kupata nafasi ya kufanya hivyo.

Ni mara chache na katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida mahakama huruhusiwa kuendesha shughuli zake mahali pasipokuwa wazi na wakati mwingine kuzuia watu zaidi ya wahusika wasihudhurie (proceedings in camera).

Kesi za namna hii mara nyingi ni zile zinazohusu mashauri ya binafasi au zile ambazo usalama heshima/ hadhi za mashahidi vinaweza kuathirika endapo

Itaendelea toleo lijalo

Ijue thamani ya damu kwa mwanadamu (9)

lUnayajua makundi yake ikiwamo Damu Azizi?

Na Pd. Evaristo J. Lefiyo C.PP.S

Mwenye Heri Maria De Mattias akiongozwa na Mt. Gaspari, Mwasisi wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, baada ya maongozi ya Mt. Gaspari ya tafakari juu ya Damu Azizi ya Yesu, alianzisha Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Yesu ambalo msingi wake ni kushiriki katika kazi ya ukombozi kwa njia ya utumishi kati ya maskini na waliosahauliwa. Maria De Mattias alijituma katika kazi ya uongozi wa Shirika kwa nguvu zake zote kwa ajili ya Kanisa. Yeye mwenyewe kutokana na unyenyekevu wake, na Masista wake katika utakatifu, akifanya kazi ya kitume kati ya watu waliomhitaji. Masista Waabuduo Damu Takatifu wanashirikiana na Yesu katika kujenga mwili wake kwa njia mbalimbali wa uenezaji wa dini na maendeleo ya watu hutumikia katika mahitaji ya wale ambao hawajaonja upendo wa Damu ya Yesu kulingana na mahitaji ya mahali wakisoma alama za nyakati. Ni matumaini yetu kuwa Damu ya Kristo iliyomwagika haitamwagika bure kamwe bali ni bei ya ukombozi wa watu katika ukosefu wa haki, vita vya rejareja na jumla, mauaji ya kinyama, kufa kwa dhamiri, na mmomonyoko wa maadili.

SALA

Bwana Yesu, tumetafakari juu ya kumwagika kwa Damu yako.

Ulijinyenyekesha kwa ajili yetu, ili kuosha dhambi zetu na kutustahilisha utukufu wa kuitwa wana wa Mungu.

Sisi tunakushukuru na kukuomba utujalie tuweze, pamoja nawe, kutoa damu yetu na maisha yetu kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wa jirani zetu.

Tunapokuwa katika huzuni au katika furaha, utusaidie kutafakari juu ya thamani ya ukombozi wetu na kuitikia pendo lako kwa ukarimu zaidi.

K: Astahili baraka na shukrani Yesu

W: Aliyetukomboa kwa damu yake takatifu.

Salaamu mtukufu

Ee Damu ya Kristo

Salaamu Damu ya Yesu Damu ile iliyomwagika

Dhambi zote kuzifuta

Damu ilotuchimbia

Mto ule wa Rehema

Sisi tunakuabudu

Na ku’tukuza milele.

TAFAKARI YA DAMU: MITO YA MAJI YA UHAI

Kwamba Damu halisi Azizi ya Kristo na maji vilibubujika kutoka katika moyo wa Kristo, kunatukumbusha yale maneno yake aliyotuambia "aliye na kiu na aje kwangu anywe kama yasemayo maandiko matakatifu; anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake. (Yn. 7:37-38)

Mt. Yohane mwinjli anatufundisha kuwa Damu ya Kristo ni chombo cha upatanisho. (1Yn. 2:2) kwani kumwagika kwake kumeleta wokovu.

Anaunganisha maji na damu kwani ni vimiminika vya utakaso. Maji hutakasa ndiyo maana yalitumika katika ubatizo wetu.

Kazi ya maji ni kuosha, maji huosha vyombo. Kuna msemo usemao "maji ni uhai". Maji ni uhai kwa sababu hutumika kumwagilia mimea na mwanadamu kupata chakula ili aishi. Maji ni uhai kwani wanyama huweza kunywa wanapohisi kiu ili waweze kunona na kama ni ng’ombe au wanyama wafugwao tuweze kupata nyama au maziwa.

Tunaposikia kiu tunatuliza kiu yetu kwa kunywa maji. Tunapofanya kazi nzito na ya muda mrefu hata tunatoka jasho badala ya kukaa tumebakia tumegandamana jasho letu mpaka tunaanza kunuka jasho la ndafu, tunatumia maji kuoga. Kweli maji ni uhai.

Damu ni uhai. Damu ni maisha.

Mtu anapopungukiwa damu huongezewa damu na maisha yanaendelea. Tunapopungukiwa damu vilevile madakatari hutushauri kula vyakula vinavyoongeza damu kama vile mboga, samaki na maziwa.

Nakumbuka wimbo mmoja wa Taifa wa Tanzania katika mpango bora wa afya ya jamii ulitaja maneno haya "kuleni kuku, mayai, mboga, samaki, maziwa. Na kujenga nyumba safi ya kulala nawe bora.

Tobo la ubavu wa Kristo litaangaliwa na watu wote kama mlango wa kutupeleka kwa Mungu. Na Damu yake Kristo katika tobo la ubavu wake ni chemichemi ya uhai.

Kuchomwa kwake mkuki Yesu, ubavuni, mkuki ambao uliutoboa moyo wake, kulibashiriwa na nabii Zekaria tangu kale (Rej. Yoh 19:36-37). Itaendelea toleo lijalo.

Kuwa makini kuijua Biblia (17)

KATIKA toleo hili, tunaendelea kuangalia maswali kama tulivyokusudia kuwaletea mfulululizo wa maswali muhimu juu ya Kitabu Kitakatifu cha Biblia. Mfululuzio wa maswali haya muhimu tunazidi kuuleta kwa msaada wa kitabu cha KATEKISIMU YA BIBLIA kilichondikwa na Padre Christian L. Mhagama.

"Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa.

Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula cha mtu yeyote bila kumlipa.

Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu.

Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula".

Tunasema mambo haya kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine.

Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe." (2Wathesalonike 3:6-12).

Ujumbe huu huu unapatikana pia katika fasuli zifuatazo: Mwanzo 3:16-19, Kutoka20:8-11; 1Wakorintho 9:8-18).

(Usisahau kuiweka takatitu siku ya Sabato. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote.

Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mtumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako.

Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba.

Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa. Kutoka 20:8-1).

Mpango wa masomo ya Jumapili na sikukuu

31 Mpango wa masomo ya Misa siku za Jumapili na sikukuu ulikuwaje siku za nyuma kabla ya kutaratibu tulionao sasa?

Utaratibu wa masomo ya Misa siku za Jumapili na sikukuu utumikao sasa ni matokeo ya mabadiliko yaliyopendekezwa katika mtaguso Mkuu wa Vatikano II uliofanyika kati ya 1962-1965.

Kabla ya hapo mambo yalikuwa hivi: kulikuwa na masomo mawili yaliyorudiwa kila mwaka.

Somo la Kwanza lilichukuliwa mara nyingi toka barua za mtume Paulo. somo la pili lilichukuliwa toka Injili zote nne, mara nyingi zaidi toka Injili ya Mathayo na mara chache sana toka Injili ya Marko.

32 Mtaguso wa Vatiakano Ii uliotoa mapendekezo gani yaliyobadili mpango wa masomo wa siku za nyuma?

Kuhusu mpango wa masomo ya Misa Mtaguso ulitoa mapendekezo katika vipengele vitatu kama ifuatavyo: Pawe na ongezeko la masomo, masomo yachukuliwe toka sehemu mbalimbali za Biblia, masomo hayo yapangwe kwa jinsi inayofaa. mapendekezo hayo yamo katika hati ya Mtaguso inayohusu Litrugia namba 51. kwa ujumla mtaguso huo ulisisitiza sana juu ya umuhimu wa Biblia na matumizi yake katika maisha ya Wakristo.

33 Je, mapendekezo ya Mtaguso yalitekelezwa vipi kwa ujumla?

Baada ya mapendekezo ya Mtaguso kutolewa, kamati ziliundwa ili kutafuta njia za utekelezaji. masomo yaliteuliwa vipya katika maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali na matukio mengine. hapa tutaangalia jinsi mapendekezo yale yalivyotekelezwa kwa ujumla katika Misa Takatifu siku za Jumapili na Sikukuu. kwanza kuhusu ongezeko la masomo.

NDOA

Utaratibu wa kusikiliza na kukata kesi za Ndoa katika Kanisa (MSK k 1671 - 1707) (4)

Kesi zinazohusika na Ndoa Batili (MSK k 1671-1688)

7. Kwa kawaida, ndoa huweza kuwa batili kutokana na kizuizi batilindoa (MSK, k 1083-1094), au kutokana na kuathiriwa mno ukubalindoa ambao huifanya ndoa kuwa ndoa (MSK, k 1095-1107, 1057), au kutokana na kutokutumika utaratibu kanuni bila uruhusisho na kama utaratibu huo ulitumika ulikuwa na kasoro muhimu na msingi (MSK, k 1108-1123, 1160).

Ni wazi kwamba panapokuweko kasoro kama hizi hata kama wanandoa wana habari au la, Mungu hawezi kushuhudia ndoa kama hizo kwa sababu yeye "hutenda kwa fadhili na uaminifu kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake" (Zab 25:10).

Kwa kweli, tunapotangaza ndoa iliyoshuhudiwa kwa mujibu wa sheria kuwa ni batili, tunataka tu kusema kuwa ndoa kama hiyo haikuwahi kuwako tangu mwanzo wake kwa sababu Mungu hakuishuhudia ijapokuwa machoni mwa wanadamu ilionekana ikishuhudiwa.

Na ndiyo maana Kristu Bwana aliwaambia Wafarisayo waliokuwa wamemwuliza kuhusu talaka:

"Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini" (Mat 19:9b). Kwa maneno haya "isipokuwa kwa sababu ya uzinzi", Kristu Bwana alimaanisha kuwa endapo mwanandoa atagundua kuwa ndoa yake i batili kwa sababu hii au ile, ni lazima ampe mwanandoa mwenza talaka kwa sababu "mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi" (Yak 4:17).

Wenye Uwezo wa Kutangaza Ndoa kuwa Batili (MSK k 1671-1673)

8. Ni haki binafsi ya jaji wa kikanisa kusikiliza na kukata kesi za ndoa za wabatizwa (MSK, k 1671).

Hizi kesi kati ya mengineyo, zinahusu kuamua kama ndoa ni batili au inaweza kufutwa kwa mamlaka ya Baba Mtakatifu, na pia kuhusu haki na wajibu msingi za ndoa.

Hata hivyo lakini, ijapokuwa Kanisa kutokana na Kanuni 1671 linaonekana kudai haki ya kusikiliza na kukata kesi za ndoa zinazohusu wabatizwa wasio wakatoliki wawili (yaani waprotestanti), Kanisa hilo hilo halitumii haki hiyo kimatendo isipokuwa tu patokee mwanandoa mprotestanti ambaye anataka ndoa yake itangazwe batili ili aweze kufunga ndoa na mkatoliki. Kadhalika, ijapokuwa Kanisa lilivyo halina haki ya kusikiliza na kuamua kesi ya ndoa ya wapagani wawili waliooana, hata hivyo kikweli linaweza kusikiliza na kukata kesi kama hiyo linapoombwa na mmojawapo wa wanandoa wapagani wawili husika ambaye anataka kufunga ndoa na Mkatoliki. Kuhusu hili, Mkusanyo Sheria Kanuni unatamka kuwa mtu yeyote awe amebatizwa au la, anaweza kushtaki au kushtakiwa (MSK, k 1476) na kuwa mwanandoa yeyote bila kujali ni nani, anaweza kushambulia ndoa yake kisheria kwa sababu hii au ile (MSK, k- 1674, 1o). ljapokuwa hapo juu tumesema kwamba ni haki pekee ya jaji wa kikanisa kusikiliza na kukata kesi za wabatizwa; hata hivyo, jaji wa kiserikali ana haki ya kusikiliza na kukata kesi za ndoa za wabatizwa kuhusu mambo yale ya ndoa ambayo yanahusika moja kwa moja na masilahi ya Nchi na hayana uhusiano wowote na Imani, kama vile madai ya mirathi, mikataba inayowahusu wengine, mahari, na kadhalika.

Lakini endapo sheria faridi au mahalia fulani itaamua kwamba katika mazingira fulani kesi za aina hiyo zisikilizwe na kukatwa na jaji wa kikanisa kwa vile zenyewe zinatumika kama makandokando na msaada kwa kesi husika, basi jaji husika anaweza kusikiliza na kukata kesi kama hizo (MSK, k 1672).

Kesi makandokando (incidental Case) ni ile kesi ambayo inazuka baada ya kesi husika kuanza kusikilizwa rasmi na ni muhimu ikatwe kwanza kabla ya kesi.

Itaendelea toleo lijalo

Yesu anasema nini juu ya watu kuokoka? (2)

l Wote waokoke: lakini, kwa kuthibitisha imani yao

Na Francis W. Rutaiwa, Ph.D

Inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo wasioamini kwamba Roho Mtakatifu anaendelea tangu Pentekoste ya Kwanza hata leo kutoa nguvu za kumshuhudia Kristo kwa ujasiri (Rej. Mdo 1:8, 2:17-21), (Yn 15:26).

Ati hayo ni ya historia ya zamani yaliyowahusu wa kina Petro na mitume wenzake tu. Kwamba Wakristo wa sasa wameisha elimika ya kutosha kukabiri maswali yote ya kiroho kwa kujitegemea kiakili!

Wanasaahu kwamba maisha ya kiroho daima yanahitaji nguvu ya Mungu, na kwamba nguvu ya Mungu ni kazi ya Roho Mtakatifu (Efe 3:16).

Kwa hiyo, Pentekoste ni ya daima na ya kudumu, jinsi "Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele" (Ebr 13:18) Kristo ni Bwana! Tena "Bwana ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru" (2 Kor 3:17).

"Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu" (Rum 8:14). Zaidi ya hiyo, Roho pia ni Nafsi ya Mungu, sawa na Baba na Mwana, katika Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja.

Je, unatafuta nafasi za kuonesha na hata kuthibitisha imani yako? Je, unatafuta njia nyepesi au njia ya imani? (Mt 17:20).

Je, unatukuza imani ya wengine? Kwa vipi? Nao je, wanatukuza imani yako?

Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona (Ebr 11: 1).

Imani si tabia au desturi tuliyonayo, au kitu fulani tunachokifanya kwenye nafsi za pekee.

Imani ni kuwa na hakika ambayo ni matokeo ya uhusiano wa ndani sana, na wa upendo. Lengo letu kama Wakristo ni kufanya kila sehemu ya maisha yetu ioneshe imani. Paulo alitangaza: ‘Kristo yu hai ndani yangu, na uhai nilionao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu" (Gal 2:20).

Umpe Yesu maisha yako, uishi katika upendo wake (Yn 15:9), pokea imani ya ndani zaidi kataka yeye. Kila kitu ni kwa imani (Rum 4:16).

Kwa kweli nyakati hizi watu wengi wana njaa ya kiroho na wanahitaji mwanga wa Roho kutenda yanayompendeza Mungu.

Wengi kiroho wana njaa hata kufa.

Hatuwezi kuishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka kwa Mungu (Mt. 4:14). Hata hivyo, hatutumii muda mwingi katika kula na kulishwa Neno la Mungu. Wala hatuli chakula cha Kiroho Neno na Ekaristi Takatifu ni chakula bora cha roho.

Basi tumruhusu Baba kutupa "Mkate" wetu wa kila siku. (Mt 6:11).

Ni ahadi ya kiroho kuwa, "Walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza" (Mt 19:20).

Ukristo sio kubweteka tu, bali kutumia vizuri vipaji na Sakramenti Mungu alivyotujalia kupitia Kanisa, yaani mwili wake Yesu.

Mt. Paulo anatufandisha kuwa sisi sote tuliobatizwa tumemvaa Kristo (Gal 3:27), maana "Nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu" (Gal 3:26).

Kristo mwenyewe aliyezaliwa na Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na kufufuka kwa nguvu ya Roho, ndiye yeye anayetujaza Roho kutokana na imani (Rej. Gal 3:2-5).

Hivyo, "Kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani" (Gal 5:5).

Maana yeye apandaye kwa Roho atavuna tunda la Roho (Gal 5:22), na katika Roho atavuna uzima wa milele (Gal 6: 8).

Inabidi tuombe sana tupate kuyatengeneza mapungufu ya imani yetu (1The 3:10), tusije tukamzimisha Roho (1The 5:19), tukalemewa "na anasa na ulevi na masumbufu ya maisha haya" (Lk. 21:34).