Make your own free website on Tripod.com

Kinga na matibabu ya utapiamlo

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini na mahali ambapo si rahisi kumpata mtaalamu wa afya kwa haraka

Unyafuzi pamoja na upojazo vinaweza kuzuiwa au kutibiwa kwa kula chakula bora na kula vyakula vya kutosha. Kwa watoto wachanga, maziwa ya mama yanatosha kabisa.

Kunyonyesha ni lazima kuendelezwa kwa muda mrefu iwezekanavyo. Akina mama wengine wanawanyonyesha watoto wao kwa muda wa miaka 2 au zaidi. Baada ya miezi 4 mpaka 6 mtoto lazima apewe vyakula vingine vya kufaa hali akiwa anaendelea kunyonya.

Watoto wenye upojazo wanahitaji protini zaidi maziwa ya unga yasiyo na mafuta yanasaidia sana ikiwa yapo ni lazima yachanganywe na asali au sukari pamoja na mafuta ya kupikia ikiwa mtoto hapato vyakula vya kutia nguvu mwilini vya kutosha.

Mayai, kuku, nyama na samaki ni vyakula vyenye protini kwa wingi lakini ni ghali, maharagwe, njegere, kunde na karanga pia vina protini na ni rahisi maharagwe kuyeyushwa na tumbo vizuri.

Maharagwe ya soya yana protini kwa wingi na unga wake unaweza kucanganywa na vyakula vingine kama mchele, ngano, karanga, ufuta ili kuongeza protini.

Aina zingine za utapiamlo.

Kwa watu fukara aina kuu za uapiamlo zinasababishwa na njaa (unyafuzi) au ukosefu wa protini (upajazo) vila vile aina zingine za utapiamlo zinaweza kutokea wakati baadhi ya vitamini au madini vimekosekana kwenye chakula watu wanachokula.

- Watoto wadogo wasiokula matunda au mboga za majan au vyakula vingine ambayo vina vitamini A kwa wingi wanaweza kuwa vipofu, wakati wa usiku macho yao huwa makavu na mwishowe kupofuka kabisa.

- Watoto wasiopata maziwa au mwanga wa jua kabisa hupindika miguu au kupata vilema vingine vya mifupa. Ingawaje ugonjwa huu unaweza kutibiwa kwa kumpa mtoto maziwa pamoja na vitamini D (inayopatikana kwenye mafuta ya samaki) njia rahisi zaidi ni kuhakikisha kuwa mtoto anapata mwanga wa jua.

- Watu wasiokula chakula cha kutosha chenye chuma kama vile mayai, mboga za majani au nyama wanaweza wakapata upungufu wa damu.

- Matatizo mengi ya ngozi au kutokwa na damu kwenye fizi vinaweza kuletwa na ukosefu wa kula matunda mboga za majani, na vyakula vingine na vitamini.

Njia ya kula vizuri wakati huna fedha nyingi au kadri ya kutosha.

Kuna sababu nyingi za njaa na ukosefu wa chakula bora. Sababu moja ni umaskini. Katika sehemu nyingi za dunia ni watu wachache tu walio na utajiri na ardhi. Hulima mazao kupata fedha tu lakini hayana faida kwa chakula. wanalima mazao kama :-kahawa au tumbaku, ambayo huuza ili kupata fedha. Au maskini wanaweza wakawa Wanalima vishamba vidogo vilivyoazimwa, hali matajiri wenye mashamba hayo wakawa wanachukua sehemu kubwa ya mavuno. ‘tatizo la njaa na ukosefu wa chakula haliwezi kuisha mpaka hapo watakapojifunza kushirikiana na wengine sawa sawa.

Lakini kuna vitu vingi watu maskini wanavyoweza kufanya ili kula vizuri na kwa bei nafuu - na kwa kula vizuri-wapate nguvu ya kupigania haki zao. Katika "Maneno kwa waganga vijijini" utapata mapendekezo mengi ya kukuwezesha kupata chakula bora. Haya ni pamoja na matumizi mazuri ya ardhi, kubadilisha mazao, kuzuia mmomonyoko wa ardhi; na umwagiliaji maji pamoja na ufugaji wa samaki, nyuki, hifadhi nzuri ya nafaka na kulima bustani kwa kila familia. Kama kijiji kizima au kikundi cha familia kadhaa kinafanya baadhi ya vitu hivi kwa pamoja, itawezekana kufika mbali katika kukuza chakula.

Wakati tukifikiria suala la chakula na ardhi, ni lazima ikumbukwe kuwa sehemu fulani ya ardhi inaweza kulisha idadi fulani tu ya watu. lkiwa ardhi na njia zingine ambazo familia yako hujipatia riziki ni kidogo, ni busara kupanga mapema na kuwa idadi ya watoto wale tu ambao unaweza kuwalisha vizuri. Kuwa na watoto wengi zaidi kuna maana kuwa kuna watu wengi zaidi wa kulisha, lakini si lazima kuwa kuna ardhi kubwa zaidi ya kulima.

Watoto wanye njaa hawawezi kufanya kazi vizuri, na wengi wao hufa.

Kuwa na familia ndogo kunazidi kuwa njia muhimu ya kujipatia chakula bora Fikiria jambo hilo na anza kupanga mapema. Mara nyingi baba mwenye familia ndogo hutumia kilo kidogo alicho nacho kununulia pombe na sigara badala ya kununua chakula kilicho kizuri, kuku wa mayai au kitu kingine ili kuongeza afya ya familia yake. lngekuwa vizuri sana kama akina baba wanaolewa pamoja wangekutana na kukaa pamoja wakati ambao hawakulewa ili kuzungumzia matatizo haya na kutafuta suluhisho linalofaa.

Pia akina mama mara nyingine huwanunulia watoto wao pipi au soda wakati ambao wangetumia fedha hizo kununua mayai, maziwa, au chakula kingine cha kulisha mwili. Kwa njia hii watoto wao wangeweza kuwa na afya zaidi kwa kiasi cha fedha zile zile.

Ukiwa una fedha kidogo na unataka kumsaidia mtoto wako akue na awe na nguvu usimnunulie pipi au soda mnunulie mayai.

 

Chakula Bora kwa Bei Nafuu

Wengi wa watu duniani hula vyakula vya wanga kwa wingi, lakini hawali vyakula vya kutosha vilivyo na protini, vitamini, na madini. Hii ni kwa sababu ya vyakula hivi vizuri huuzwa ghali sana.

Protini za wanyama kama vile maziwa na nyama ni nzuri sana kulisha mwili, lakini pia ni ghali. Pia wanyama huhitaji ardhi zaidi kwa protini wanayotoa.

Watu wengi hawawezi kununua vyakula vinavyotokana na wanyama kwa wingi. Kusema kweli, familia maskini inaweza kujipatia protini zaidi kama wanalima au wananunua vyakula vinavyotokana na mimea ambayo ina protini, kama vile maharagwe, njegere, dengu, karanga, na mboga za majani badala ya vyakula vinavyotokana na wanyama kama nyama na samaki ambavyo ni ghali,

Watu wanaweza kuwa na nguvu na wenye afya ingawaje protini zao zote zinatoka kwenye mimea.

Hata hivyo ni busara kula protini kidogo za wanyama katika kila mlo. Hii ni kwa sababu mimea haina protini zote zinazohitajiwa na mwili, ingawaje ina wingi wa protini.

Jaribu kula mchanganyiko wa vyakula vya majani kuliko kung’ang’ania aina moja tu au mbili, mimea tofauti huupa mwili aina mbalimbali ya protini, vitamini, na madini. Kwa mfano kutumia maharagwe na mahindi kwa pamoja huusaidia mwili vizuri zaidi kuliko kula kimoja tu peke yake. Na ikiwa mboga zingine na matunda yakiongezeka, hivi ni bora zaidi.

Kanisa Katoliki na Umungu wa Yesu

KATIKA toleo lililopita ukurasa wa kwanza, tuliandika habari inayofafanua ukweli na uhalisi juu ya Umungu wa Yesu Kristo. Katika toleo hili, tutaendelea kuchambua mafundisho hayo sahihi juu ya uhalisi na Umungu wa Yesu. Sasa, endelea,

Kristo - Kiini cha Katekesi

"Kiini cha Katekesi, kimsingi, tunakipata katika Nafsi ya Yesu wa Nazareti, mzaliwa wa pekee wa Baba ... aliyeteswa na kufa kwa ajili yetu, na sasa amefufuka, anaishi milele pamoja nasi (Yohane Paulo II, CT 5).

Kufundisha Katekesi ni "kufafanua mpango wote wa Mungu ndani ya Nafsi ya Kristo. Ni kutafuta kujua maana ya matendo na maneno ya Kristo na ya ishara alizozifanya." (Yohane Paulo II, CT 5).

Kusudi la Katekesi ni "kuwaweka watu katika ushirika na Yesu: Yeye peke yake anaweza kutuingiza katika mapendo ya Baba ndani ya Roho Mtakatifu, na kutufanya tushiriki Uzima wa Utatu Mtakatifu" (Yohane Paulo II, CT 5).

Ndani ya Katekesi ni "Kristo, Neno aliyemwilishwa na Mwana wa Mungu, anayefundishwa, yote mengine yanasema juu yake.... Ni Kristo peke yake anayefundisha; mwingine yeyote anafanya hivyo kama msemaji wake, akimwezesha Kristo kufundisha kwa kinywa chake.... Kila Katekista anatakiwa alifanye neno la Yesu lenye fumbo kuwa lake mwenyewe: "Mafundisho yangu si yangu Mimi, ila yake Yeye aliyenipeleka." (Rej Yoh 7:16;CT 6 )

Yule ambaye ameitwa "kumhubiri Kristo" hana budi, awali ya yote, kutafuta "thamani hii kubwa ya kumjua Kristo Yesu"; akubali kupoteza kila kitu." ili ampate Kristo na yeye mwenyewe awe ndani yake."

Aidha, amjue yeye na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, akifananishwa na kufa kwake ili apate kwa njia yoyote kuifikia kiyama ya wafu." (Fip 3:8-11).

Kutokana na elimu hii ya upendo wa Kristo inazaliwa tamaa ya kutangaza, "kueneza Injili," kuwaongoza wengine, "kukubali" imani katika Yesu Kristo. Wakati huo huo anaonja hitaji la kujua siku zote vizuri zaidi imani hii.

Kwa lengo hili, tukifuata mpango wa Kanuni ya Imani, kwanza yatawekwa majina ya msingi yanayomhusu Yesu: "Kristo," "Mwana wa Mungu na "Bwana" (Kipengee 2). Kanuni itaendelea kuungama mafumbo ya msingi ya maisha ya Yesu: yale ya Umwilisho wake (kipengee 3), yale ya Pasaka yake (kipengee 4 na 5), hatimaye yale ya Utukufu wake (kipengee 6 na 7).

Yesu kwa Kiebrania maana yake ni "Mungu anaokoa." Wakati wakutangaza kuzaliwa kwa Bwana, Malaika Gabrieli anasema kwamba jina lake ataitwa Yesu, ambalo kwa upande mmoja linaeleza nafsi yake na kwa upande mwingine Utume wake. (Rej Lk. 1:31).

Kwa vile "Mungu peke" yake anaweza kuondolea dhambi, ni Yeye katika Yesu Mwanawe wa milele aliyefanyika Mtu "atakayewaokoa watu wake na dhambi zao (Rej. Mt. 1:21 ;2:7). Hivyo katika Yesu, kwa faida ya wanadamu, Mungu anajumlisha historia yote.

Katika historia ya wokovu, Mungu hakuridhika kumwokoa lsraeli" kutoka

nyumba ya utumwa tu" Kum 5:6 akimfanya atoke Misri; bali anamwokoa pia katika dhambi yake.

Kwa kuwa dhambi ni kumkosea Mungu, Mungu peke yake anaweza kuifuta. (Zab 51:11) Kwa sababu hiyo, Israeli, akifahamu zaidi na zaidi kuenea kwa dhambi ulimwenguni, hataendelea kutafuta wokovu isipokuwa kwa kuliita jina la Mungu Mkombozi. Yoh 3:18; Mdo 2:21; 5:41;3Yoh 7;Rom 10:6-13.

Jina la "Yesu" lina maana kwamba jina lenyewe la Mungu limo katika nafsi ya Mwanawe aliyefanyika Mtu kwa ajili ya Ukombozi halisi wa dhambi za wote.

Ni jina la Mungu ambalo peke yake linaleta wokovu, na linaweza kutajwa karibu na wote, kwa sababu kwa njia ya Umwilisho ameunganika na watu wote hivi kwamba "hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo (Mdo 4:12; Rej 9:14; Jak 2:7).

Jina la Mungu Mwokozi lilitajwa mara moja tu kwa mwaka, kwa ajili ya malipo ya dhambi ya Israeli na kuhani mkuu, baada ya kunyunyizia damu ya sadaka kiti cha rehema cha Patakatifu - Takatifu.

Kiti cha rehema pakawa ni mahali pa uwapo wa Mungu.

Mtakatifu Paulo anaposema juu ya Yesu kwamba, "Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake: ‘anataka kusema kwamba katika ubinadamu wake, "Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake." (Rom:3:25; 2Kor 5:19).

Ufufuko wa Yesu unalitukuza jina la Mungu Mwokozi kwa sababu ni Jina la Yesu linalodhihirisha kwa utimilifu uwezo mkuu wa "Jina lile lipitalo kila jina:" Pepo wabaya wanaliogopa jina lake, na ni kwa jina lake wafuasi wa Yesu wanafanya miujiza.

Kwa kweli chochote wamwombacho Baba kwa jina lake anawapa (Rej Mdo 16:16-18; 19:13-16; Mk 16:17; Yoh 15:16.)

Jina la Yesu ni kitovu cha sala ya Kikristo, sala zote za Kiltrujia huhitimishwa kwa maneno "Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo", Salamu ya Malaika - Salamu Maria" huhitimishwa na "Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa."

Sala ya Moyo na Makanisa ya Mashariki inayoitwa "Sala ya Yesu" husema: "Bwana Yesu Kristo Mwana wa Mungu unihurumie mimi mkosefu," Wakristo wengi kama Mt. Yona wa ARC wamekufa wakiwa na neno moja tu midomoni mwao "Yesu"

Kitabu cha kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (15)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Sasa, tunaongezea chapisho jingine la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyovyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC), tulianza na dibaji iliyooandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na sura za ndani.

2.8 Mahakama ya Mwanzo.

Hii ikiwa ni mahakama ya chini kabisa katika mfumo wa mahakama nchini imeundwa na kifungu cha 3 cha Sheria ya Mahakama ya Hakimu 32 (Angalia kifungu cha 3 cha sheria Namba 2/1984) kusikiliza mashauri yatokayo kwenye Wilaya ambayo mahakama hiyo iko. Ina uwezo wa awali kusikiliza kesi za ndoa, 33 (Kifungu cha 18 (1) b cha Sheria Namba 2/1984) Mirathi na madai ambayo yanaongozwa na sheria za Kimila au Kiislamu 34(Kifungu cha 18 (1) (a) (i) cha Sheria Namba 2/1984) Mhakama za Mwanzo zina uwezo wa kusikiliza kesi za jinai35 Zile ambazo zimeorodheshwa kwenye Jedwali la Kwanza la Magistrates Court Act, 1984.) na za Madai.

Kesi za jinai katika Mahakama za Mwanzo hufunguliwa kwa mlalamikaji mwenyewe kwenda mahakamani moja kwa moja au kwa kupitia polisi.

Pia Mahakama hizi zina uwezo wa kushughulikia kesi za madai ambazo zinatawaliwa na sheria za kimila au za kiislamu isipokuwa kama madai yanahusu umilikaji wa ardhi iliyosajiliwa chini ya sheria ya ardhi 36(Itakumbukwa kwamba Mahakama ya Mwazo itakuwa na uwezo wa kusikiliza shauri la mirathi ambalo linahusika na sheria ya kimila hata kama mali husika imesajiliwa chini ya sheria ya ardhi).

Usikilizaji kesi katika Mahakama hii hufanywa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo akisaidiana na Wazee wa Baraza (Assessors) wasiopungua wawili 37 Kifungu cha 6(1) (a) na 7 (1) cha Sheria Namba 2/1984. Uamuzi wa kesi huwa wa wengi (majority Verdict). Hii ina maana kwamba katika kufikia uamuzi kwenye kesi kila mmoja kati ya hakimu na Wazee wa Baraza au na yeyote kati yao na kura zikawa zimelingana hakimu anakuwa na kura ya uamuzi (casting vote) 38 Kifungu cha 7 (2) cha sheria Namba 2/1984.

Tunaona kwamba sheria inawapa madaraka makubwa Wazee wa Baraza katika Mahakama ya Mwanzo kiasi cha kumfanya hata Hakimu ambaye japokuwa amesomea hii fani, amekula kiapo na ana ujuzi wa sheria kuchukuliwa sawasawa na Wazee ambao ni watu wa kawaida. Hali hii haipo kwenye Mahakama zingine inapotokea sheria

ikazitaka mahakarna hizo kukaa na wazee wa Baraza. Hakimu 39 Angalia Kifungu cha Saba (3) cha sheria Namba 2/1984. au Jaji 40 kwa mfano katika kesi za mauaji au za uhujumu uchumi Jaji wa Mahakama hukaa pamoja na Wazee wa Baraza lakini wakati wa kutoa uamuzi kwenye kesi halazimiki kufuata maoni yao. katika Mahakama hizo zingine halazimiki kufuata, maoni au ushauri wa Wazee wa Baraza. Mahakimu wengi wa Mahakama za Mwanzo wamenufaika na hali hii ambayo imewapa visingizio vizuri vya kuwanyima watu haki kwani wanakimbilia kusema kuwa wao wanakuwa na maoni tofauti lakini Wazee wa Baraza ambao idadi yao ni kubwa wanazidi kwa wingi wa kura na uamuzi wa Wazee hao unakuwa ndio uamuzi wa mahakama hata kama Hakimu anaona kuwa haki haikutendeka.

Lugha inayotuinika katika Mahakama za Mwanzo ni Kiswahili.41 Kifungu cha 13 (1) cha Sheria Namba 2/1984 Hii ni tofauti na mahakama zingine ambazo lugha rasmi ni Kiingereza au Kiswahili lakini lazima katika mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya hukumu iandikwe kwa Kiingereza.42 Kifungu cha 13 (2) cha Sheria namba 2/1984.

Wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inatambua bayana haki ya mtu kuwakilishwa mahakamani na mwanasheria katika kesi yoyote inayomkabili,43 Tazama Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1997). mawakili hawaruhusiwi kusimama katika Mahakama za Mwanzo.44 Kifungu 33 (1) cha sheria Namba 2/1984. Wengi wanaounga mkono msimamo huu wa sheria wanatoa sababu mbili. Kwanza, elimu ya kisheria ya mahakimu wa mahakama za mwanzo ni duni sana ukilinganisha na walionayo mawakili. Baada ya kumaliza shahada ya sheria ya.Chuo Kikuu mwanasheria (Lawyer) anatakiwa pia afanye mtihani mgumu unaotayarishwa na Baraza la Elimu ya Sheria (Council for Legal Education) na akifaulu ndipo anapotangazwa rasmi kuwa wakili (Advocate). Hivyo, huyu ni mtu aliyebobea sana katika taaluma yake. Hivyo, akipambana na hakimu ambaye elimu yake ya sheria ni hafifu basi hapa haki haiwezi kutendeka kwa sababu ya tofauti ya kielimu waliyo nayo. Hakimu, ambaye anatakiwa kufanya maamuzi ni lazima atajisikia mnyonge.

Pili, na muhimu zaidi ni kwamba mahakama za mwanzo zilianzishwa karibu zaidi na mwananchi ili kusaidia katika kusuluhisha migogoro na siyo chombo cha mashindano na malumbano marefu ya kisheria. Mawakili kwa kawaida wanapenda sana mashindano ya kisheria na hawaridhiki hadi mmoja ashinde na mwingine ashindwe. Hali hii siyo nzuri katika mahakama za mwanzo ambapo watu wengi wangependa kufikia muafaka baada ya mjadala.

Hali hii ya kutowaruhusu mawakili kuendesha shughuli zao za utetezi katika mahakama za mwanzo imetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni kitendo cha ukiukwaji wa haki za binadamu. Tukiangalia umuhimu wa mawakili katika kusaidia mahakama kutenda haki wengi wanahisi kuzuiliwa mawakili kwenda kwenye mahakarna hizi kumechangia katika kuzifanya Mahakarna za Mwanzo zishindwe kutoa haki jinsi ilivyotegemewa kwani hawaoni sababu za msingi kuwanyima msaada wa mawakiii mahakimu wa mahakama za Mwanzo. Hakuna shaka kwamba hali hii inawalazimu mahakimu wa mahakama za mwanzo kuwa makini katika uamuzi wao wa mashauri na hata katika utendaji wao wa kazi kwa ujumla kwani hawana msaada wa mawakili ambao wenzao wa Mahakarna za Hakimu Mkazi na za Wilaya wanapata.

Aidha Mahakama za Mwanzo zina uwezo wa kusikiliza rufaa zitokazo kwenye Mabaraza ya Kata (Ward Tribunals)

Kisheria kesi zinapaswa kuendeshwa mahali pa wazi na ambapo watu wamepazoea ili mtu yeyote mwenye kupenda kusikiliza au kufuatilia kesi fulani aweze kupata nafasi ya kufanya hivyo.

Ijue thamani ya damu kwa mwanadamu (8)

Na Pd. Evaristo J. Lefiyo C.PP.S

Twaeni mnywe wote:

Yesu alipoiweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu alitualika sote tushiriki kula na kunywa Damu ya Yesu ( Mk 14:22-26) , alituachia agizo kwamba tuendeleze karamu hiyo na kuwalisha wengine, kuwajali maskini, watoto wa mtaani, walemavu, waliokumbwa na balaa la madawa ya kulevya, wakimbizi wa kisiasa, yatima, wenye taahira ya akili na wale wanaokosa amani kwa sababu ya vita vya mara kwa mara. Yesu anapotuambia "... fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi" (Lk 22:19) anatualika kuendeleza huo ukarimu, kugawiana chakula chetu kwa wale wahitaji na mahitaji mengine hata kama ni ushauri. Hii "Twaeni mle "(Mt 26:26) na "...kunyweni nyote" ni lugha ya ujamaa na upendo. Yesu hasemi "Twaa ule wewe" bali "Twaeni". Hii inaonyesha kuwa Damu ya Yesu ni kinywaji kwa wote wanaoamini. Yesu mkarimu hana ubiinafsi bali ni Pelikani wa Agano Jipya ushirika wa Kanisa ni kinyume kabisa na umimi hasa katika Ekaristi Takatifu. Bwna anatup a agizo kwamba tu le na tunywe damu yake tusije tukapata utapiamlo wa kiroho (Yoh 5:53-587) Ni mwaliko kwetu kuwa uwima tunaopata katika Mwili na Damu ya Kristo tuupeleke kwa wengine.

Ushirika wa Kanisa unajikita katika Damu ya Yesu ambayo inalifanya Kanisa katoliki kuwa na kubaki moja duniani kote, (Efe 4:4-6).

Katika Kanuni ya Imani tunaungama ‘Nasadiki kwa Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki, la Mitume.

Naungama Ubatizo mmoja, nangojea na ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo. Amina.

Kwa kushiriki mwili mmoja na kalisi moja tunakiri ushirika mtakatifu unaoletwa na ile Damu Azizi ya Yesu (1 Kor 10:16).

Mtakatifu Agostino anatuambia kuwa ile Damu tunayoishiriki ni kifungo cha ushirika wetu na bei iliyolipwa kwa ajili yetu (1Pt 1:18-19) kwa vile bei aliyolipa Kristo ni ya juuna ya thamani, basi hata sisi tulionunuliwa kwa bei hiyo ni ghali (1Kor 6: 20, Efe 1:7).

Kama Damu hiyo imeweza kutununua sisi tulioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa 1:26) na ambao tulifanywa wadogo kidogo tu kuliko malaika ( Zab 8:5-8) na kupewa mamlaka juu ya viumbe vyote.

Upendo

Upendo wa Kristo uliomfanya amwage Damu yake kwa ajili yetu wadhambi unafanana na ule wa yule ndege aitwaye Pelikani. Pelikani, wakati wa njaa, hujitoboa damu yake kidogokidogo na kumnywesha kinda wake hadi anajimaliza mwenyewe kwa kumlisha kinda wake (Yoh 15:13).

Sisi nasi katika upendo wetu tuwe kama yule ndege, Pelikani katika kuwahudumia wahitaji wetu hasa pale tunapojisahau kwa ajili ya wengine.

Sala ya mapendo inatukumbusha jambo hilo inaposema "... nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu, Amina. (Mt 22:32-34). Kumbe kuwa na upendo kama wa Pelikani ni zaidi ya kumpenda tu jirani kwa kuwa upendo wa Pelikani unazidi hata kujipenda wenyewe katika hali yake ya kujisahau kwa ajili ya mwingine hata kufa kwa ajili yake. Huo ndio upendo wa Kristo ( Yoh 15:13-15).

Damu ya Kristo inatualika kuwa mashahidi kupitia kazi zetu katika kujitoa bila kujihurumiahurumia kama alivyofanya Mt. Gaspari.

Mtakatifu Gaspari Del Bufalo Mwasisi wa Shirika la Damu Azizi alifanya kazi mpaka akaisha kama mshumaa. Aliposhauriwa kupumzika kidogo alijibu akionesha moto uliokuwa unawaka ndani mwake akisema: "Kwa Mungu ni lazima tufanye mengi, upesi na vema; mengi kwa sababu anastahili hivyo, upesi kwa sababu maisha ni mafupi, na vema kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kumtumikia Mungu". Mt. Gaspari alitumia vipaji vyake vyote kwa manufaa ya wengine. na kuonesha mfano wa mtumishi mwema na mwaminifu kwa Mungu ambaye alitolea kwa uwezo wake wote vyote alivyomjalia (Mt 10:8-10).

Mwenye Heri Maria De Mattias akiongozwa na Mt. Gaspari, Mwasisi wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, baada ya maongozi ya Mt. Gaspari ya tafakari juu ya Damu Azizi ya Yesu, alianzisha Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Yesu ambalo msingi wake ni kushiriki katika kazi ya ukombozi kwa njia ya utumishi kati ya maskini na waliosahauliwa.

Kuwa makini kuijua Biblia (17)

29. Biblia yatuambia nini kuhusu suala la umoja na amani?

Biblia yatuambia kwamba japokuwa Mungu aliwateua Waisraeli kuwa Taifa lake kwa namna ya pekee, hata hivyo alikuwa na mpango wa kuwaunganisha watu wote chini ya mwanae Yesu Kristo. Katika Yesu Kristo hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Tusikilize ujumbe: "Mwenyezi Mungu asema: Watu wageni watakaonikiri mimi Mwenyezi-Mungu, watakaoniheshimu, wakapenda jina langu na kuwa watumishi wangu, wote watakaoshika sabato bila kuikufuru, watu watakaozingatia Agano langu, hao nitawaleta katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; dhabihu za sadaka zao zitakubaliwa madhabahuni pangu. Maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote.

Hili ni tamko langu mimi Bwana Mungu-Mwenyezi ninayewakusanya Waisraeli waliotawanyika.

Licha ya hao nitawakusanya watu wengine wajumuike nao" (Isaya 56:6-8).

Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine -mnaoitwa "Wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita "Waliotahiriwa" - kumbukeni mlivyokuwa zamani.

Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo, mlikuwa nje ya jamii ya Israeli, mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile Agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani.

Lakini sasa kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.

Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja.

Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. Aliionda ile sheria pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.

Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao, kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. Basi, Kristo alikuja akahubiri habari njema na amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.

Hivyo kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba kwa Roho mmoja (Waefeso 2:11-18).

Ujumbe huu unapatikana pia katika fasuli zifuatazo: Efeso 4: 1- 6; Wafilipi 2:5-11; Yohane 20: 19-23.

30. Biblia yatuambia nini kuhusu suala la kazi?

Biblia yatuambia kwamba mwanadamu ataishi kwa kufanya kazi.

Kuishi kwa njia ya kuombaomba ni aibu. Hata hivyo mwanadamu anahitaji kuupumzisha mwili wake kutokana na kazi mara moja katika siku saba. Tusikilize ujumbe:

 

 

 

 

 

"Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa.

Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula cha mtu yeyote bila kumlipa.

Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu.

Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula".

Tunasema mambo haya kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine.

Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe." (2Wathesalonike 3:6-12).

Ujumbe huu huu unapatikana pia katika fasuli zifuatazo: Mwanzo 3:16-19, Kutoka20:8-11; 1Wakorintho 9:8-18).

(Usisahau kuiweka takatitu siku ya Sabato. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote. Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mtumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako. Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba.

Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa. Kutoka 20:8-1).

Itaendelea toleo lijalo

Utaratibu wa kusikiliza na kukata kesi za Ndoa katika Kanisa (MSK k 1671 - 1707) (3)

5. Mkusanyo Sheria Kanuni Mwaka 1917 uliagiza kwamba kesi zote zinazoshambulia ndoa kuthibitisha zi batili ni lazima zisikilizwe na urika wa majaji watatu bila kujali desturi nyingine zilizokuweko ambazo zinasema kinyume na tofauti (MSK 1917, k 1576,#1)

Kama vile ilivyokuwa huko nyuma, Mkusanyo Sheria Kanuni huu uligusia pia uwezo wa mahakama haki ya kutuma rufaa, na mwisho kesi nyingine za ndoa zilizo wazi kama vile kizuizi ndoa awali halali, ambazo zingeweza kusikilizwa na kukatwa kwa kutumia ushahidi unaotokana na hati na kuhitimishwa bila kulazimika kutumia utaratibu wa kawaida kwa kusikiliza na kukata kesi (MSK 1917, k 1960-1992).

Mwaka 1936, Jimbo Takatifu liliandika bauramaelezo kujaribu kurahisisha utaratibu ule wa kawaida wa kusikiliza na kukata kesi za ndoa uliokuwa umetolewa na Mkusanyo Sheria Kanuni Mwaka 1917.

Baruamaelezo hiyo kwa jina Provida Mater (AAS 28 [1936), uk 313-361), baada ya kufafanua utaratibu husika, ilizidi kufanya mambo kuwa magumu zaidi na majaji mahali pengi walishindwa kufanya na kutekeleza majukumu yao na kesi nyingi za ndoa ziliachwa kusikilizwa au zilikatwa kinyume na matarajio.

Na Mwaka 1971, Papa Paulo wa Sita alitoa Barua yake ya Kitume kwa jina Causas Matrimoniales (L Wrenn, Annulments 3rd ed [Toledo CLSA 1978, uk 115-128) ambayo ilijaribu kuweka wazi zaidi utaratibu wa kusikiliza na kukata kesi za ndoa uliokuwa umetolewa na Mkusanyo Sheria Kanuni Mwaka 1917.

Barua kitume hiyo iligusia uwezo wa mahakama wa kupokea na kuamua kesi ya ndoa inayohusika, idadi ya majaji wanaotakiwa kwenye kesi inayohusu ubatili wa ndoa, kutumia huduma ya walei katika mahakama, na taratibu za kukata rufaa.

Karibu marekebisho na mabadiliko yote yaliyotolewa na Causas Matrimoniales yamo kwenye Mkusanyo Sheria Kanuni Mwaka 1983 ambao ndio msingi wa utafiti na mafunzo yetu katika Makala haya.

6. Madhumuni na lengo la Makala haya ni kutoa utaratibu mzima wa kusikiliza na kukata kesi za ndoa katika Kanisa kwa mujibu wa sheria kanuni (MSK, k- 1671-1707) kwa sababu kwa vile ndoa ni chombo cha kisheria kinachoanzishwa na kulindwa na sheria (MSK, k 1108-1123, 1060, 1150), kikikumbwa na matatizo yoyote kama ilivyo kawaida katika maisha ya binadamu (Yobu 7.-1, Efe 6:10-20, Ebr- 5:7-10) ni lazima kishughulikiwe kwa mujibu wa sheria (MSK, k 1060, 1150).

Kwa mantiki hii, wanandoa wanakatazwa kujichukulia sheria mikononi na kutengana au kupeana talaka kiholela na kujiwekea wachumba wengine wanaowatafuta kwa njia zao wenyewe na hivi kuzidi kujilimbikizia matatizo yasiyo na idadi na ya kujitakia.

Kwa hiyo katika Makala haya, tutajadili kimtiririko mambo yafuatayo: kesi zinazohusu ndoa batili, kesi za kuwatenganisha wanandoa, ndoa ikingali bado ipo, utaratibu wa kupata uruhusisho dhidi ya ndoa kanuni zisizotumika bado, na utaratibu wa kuthibitisha kifo cha mwanandoa mwenza kinachohisiwa. Katika kesi zinazohusu ndoa batili, mambo yafuatayo yatajadiliwa: wenye uwezo wa kutangaza ndoa kuwa batili, wenye haki ya kushambulia ndoa, wajibuchungaji (office) wa majaji, shahidi zinazotakiwa, hukumu na kukata rufaa, na utaratibu wa kukata kesi batilindoa kwa uthibitisho hati.

Kesi zinazohusika na Ndoa Batili (MSK k 1671-1688)

7. Kwa kawaida, ndoa huweza kuwa batili kutokana na kizuizi batilindoa (MSK, k 1083-1094), au kutokana na kuathiriwa mno ukubalindoa ambao huifanya ndoa kuwa ndoa (MSK, k 1095-1107, 1057), au kutokana na kutokutumika utaratibu kanuni bila uruhusisho na kama utaratibu huo ulitumika ulikuwa na kasoro muhimu na msingi (MSK, k 1108-1123, 1160).

Ijue Imani Yako

Yesu anasema nini juu ya watu kuokoka ?

l Wote waokoke: lakini, kwa kuthibitisha imani yao

Na Francis W. Rutaiwa, Ph.D

Miaka mingi iliyopita, wakati tunaoweza kuuita wa kiberiti na moto wa Kanisa, kulikuwepo mawazo kwamba karibu hakuna mtu atakayekwenda mbinguni.

Matumaini yalikuwa kwamba labda wachache tu watapenya kwa siri kupitia mlango wa nyuma wa toharani. Wakati huu sasa tunasikia hoja kwamba kila mtu atakwenda mbinguni.

Watu wengine wanathubutu hata kufundisha kwamba hakuna moto wa milele, au kama upo basi hakuna yeyote humo ila tu Yuda Iscarioti, Adolf Hitler, na wengine wachache wauaji maarufu sana. Je, Yesu anasemaje?

Kwa kujibu swali ikiwa kweli watakao okoka ni wachache, Yesu alisema:

"Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba; kwa maana nawaambieni kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze" (Lk 13:24).

Yesu pia alisema: "Waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache" (Mt 22:14).

Inaonekana kwamba si Kibiblia, na ni ya kiburi, kufundisha kwamba karibu kila mtu anamkubali Yesu kama Bwana na atakwenda mbinguni tu, hata kama hakuna kithibitisho cha imani hiyo.

Kwa upande mwingine, sio sehemu ya mpango wa Baba yetu wa mbinguni kwamba, hata mtu mmnoja apotee (Mt 18:24), kwa maana Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokolewe (1Tim 2:4). Kama mapenzi ya Mungu yangetimizwa, wote wangeokoka na kwenda mbinguni.

Kwa hiyo, tuwe na matumaini, lakini inabidi pia tuwe na hekima, tusiwe na majivuno au kiburi kuhusu maisha yetu ya milele pamoja na Yesu. "Kwahiyo ndugu jitahidi zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu, maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele na Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo" (2 Pet 1:10-11).

Kwa hiyo, kaifanyieni "Miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe" (Ebr 12:13). Basi tumwombe Baba atupe moyo mnyenyekevu, wenye toba (Rej. Zab 51:17).

Kweli tunaweza kutubu dhambi zetu, kuufanya mtindo wa maisha yetu uwe wa kawaida zaidi, kuiosha miguu ya wengine (Yn 13:13), kuchukua nafasi ya mwisho (Lk 14: 10) na kujitia hatarini pakukataliwa na kudhulumiwa (Rej Mt 5: 10 -11). Ziko njia za Ki-biblia za kujinyenyekesha.

Karibu watu wote wanataka kupata mafanikio katika maisha. Tatizo ni kuwa wengi tunayataka mafanikio kwa nia ya kujitukuza. Lakini Mungu anaahidi kuwashusha watu wanaojitukuza.

Ni watu wachache sana wanaochagua wenyewe kujinyenyekesha. Mungu anaahidi kuwakweza. Basi tufanye kujishusha wenyewe, na tumwache Mungu afanye kule kutukuza. "Yeye amekuonesha....na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako" (Mika 6:8). "Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia yake" (Zaburi 128: 1).

Mt. Paulo anasema kwamba imani iliyothibitishwa inavuma na kuenea, jinsi alivyomshukuru Mungu, na kuwasifu Wakristo wa Thesalonike kwa ajili ya imani yao (Ref. 1The 1:8). Je, imani yetu sisi inaweza sawasawa kuitwa imani iliyothibitishwa kwa kusifiwa, kuvuma na kuenea? Je, tunajaribu kutembea kwa imani, wala sio kwa kuona? (2 Kor 5:7).

Inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo wasioamini kwamba Roho Mtakatifu anaendelea tangu Pentekoste ya Kwanza hata leo kutoa nguvu za kumshuhudia Kristo kwa ujasiri (Rej. Mdo 1:8, 2:17-21), (Yn 15:26).

Pitio la Kitabu

Jina la Kitabu: Tuingie Milenia Mpya

Mwandishi: Papa Yohane Paulo wa Pili

Mchapishaji: Pauline Publications Africa.

Kurasa: 54

Bei: Shilingi 900/=

TUINGIE MILENIAM MPYA (Novo Millenio Ineute), ni Barua ya Kitume na hati rasmi ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili ya kuwaongoza watu kuingia katika Milenia ya Tatu ya Ukristo na kuishi milenia hiyo kwa ari kubwa na uchangamfu wa kiimani kwa kumtafakari na kumtegemeza YESU KRISTO ambaye ni YULE YULE JANA, LEO NA HATA MILELE.

Kitabu kinaanza kwa dibaji iliyoandikwa na Mwenyekiti wa Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Amedeus Msarikie.

Barua hiyo inatoa mwaliko kwa maaskofu, mapadre na mashemasi, watawa; waume kwa wake na walei wote, kuungana na Baba Mtakatifu katika kumshukuru Mungu kwa baraka zake na kwa mema aliyowatendea mwaka 2000 na kuangalia siku zijazo hasa kwa kufanya maazimio na kujiwekea mikakati ya utekelezaji.

Kitabu hiki kimegawanyika katika sura nne zinazofuatiwa na hitimisho ambalo linajikita katika maeneo ya Yesu ambayo siku moja baada ya kuwahutubia watu wengi akiwa kwenye mashua ya Simon, alimwelekeza mtume huyo "atweke mpaka kilindini" akavue samaki (Duc in altum) (Lk. 5:4).

Katika sura ya kwanza yenye kichwa cha habari, KUKUTANA NA KRISTO URITHI KUTOKA JUBILEI KUU, Baba Mtakatifu anawaalika Wanakanisa wote kujitafiti na kuomba msamaha ili kupata rehema.

Anasema kuwa, yeye kwa niaba ya Kanisa zima, aliomba Machi 12,2000, huko Vatican, na anawaalika Wakristo wote kuendeleza moyo huo ili kuwa wanyenyekevu na waangalifu zaidi katika kuipokea Injili.

Anawaalika Wakristo kujali na kuwa mashahidi wa imani kwa kuimarisha roho ya Kanisa lililo safarini kwa kuhusisha vijana katika mipango ya Kanisa na pia, kuwa na mahujaji wa aina mbalimbali ili kulipa Kanisa sura mpya ya kiekumene.

Anadokeza mambo mengine yaliyofanyika wakati wa Jubilei Kuu kama hija yake katika Nchi Takatifu, kampeni ya kufutwa deni la nchi maskini, kulipa Kanisa sura na nguvu mpya ya kiekumene na kuonesha nafasi ya Kanisa katika maisha ya ulimwengu.

Katika sura ya pili, Baba Mtakatifu, anahimiza Jubilei Kuu iliyoadhimishwa na Kanisa iendelee kuwa chachu ya mabadiliko kuelekea utakatifu na kuwasaidia watu kufikia lengo la kuutazama uso wa Yesu katika nyakati zote ili macho yao daima yawe yamekazwa kwa dhati juu ya Bwana kuliko hapo zamani.

Anataka watu wadumu katika KUSOMA MAANDIKO MATAKATIFU, kuishi maisha ya imani na kudumu katika safari ya kwenda kumtangaza kristu ulimwenguni kote.

Katika sura ya tatu, Baba Mtakatifu anawaalika wanakanisa kwenye makanisa mahalia kuwa na mipango ainifu ambayo itawezesha tunu za Injili kuleta mabadiliko katika jamii na utamaduni.

Hii itasaidia watu kuishi maisha ya utakatifu, ya sala kupenda na kushiriki misa ya Jumapili kupokea sakramenti ya upatanisho na kusikiliza na kutangaza neno la Mungu.

Katika sura ya nne na ya mwisho Baba mtakatifu anakumbusha na kuwataka watu waishi amri kuu ya upendo kikamilifu kwa kudumisha roho ya muungano jambo linalofuma kiini halisi cha fumbo la kanisa kwa kuwa upendo ni moyo wa Kanisa (Wakristo).

Baba Mtakatifu anasisitiza watu kujiingiza katika mazungumzo baina ya dini nyingine yakitawaliwa na upendo.

Jambo hili litasaidia kuwa pamoja katika kukabiliana na changamoto za leo kama vile uharibifu wa mazingira amani ya dunia, kuwanyima watoto hali ya msingi ya kuishi (utoaji mimba) na mengine.

Pia, anakumbusha kuwa mwanga wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano ambao haujazimika basi uwashwe zaidi ili kupata mwelekeo mpya wa kuishi ukristo.

Anahitimsha barua yake kwa kuwaalika watu kuanza safari ya kwenda kutangaza Habari Njema ili kuwaleta watu kwa kristo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wakisindikizwa kwa maombezi ya mama Maria na Watakatifu.

Kila Jumuiya Ndogondogo ya Kikristo, naam kila familia inapswa kuwa na nakala ya barua hii ya Kitume ya baba Mtakatifu.

Kitabu hiki kinapatikana katika maduka yote ya vitabu ya majimbo yote ya Kanisa Katoliki