Make your own free website on Tripod.com

Ijue Afya yako

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini na mahali ambapo si rahisi kumpata mtaalamu wa afya kwa haraka

vyakula vya kujenga mwili au protini

Protini ni chakula cha kujenga mwili ni cha lazima kwa kumfanya mtu akue vizuri kwa misuli na sehemu zingine nyingi za mwili ziwe na afya. Ili kukua na kuwa na nguvu kila mtu lazima ale protini za kutosha kila siku.

Vyakula vyenye protini kwa wingi ni nyama, maziwa, kuku, jibini, mayai, maharagwe ya soya, Samaki, wadudu, vyakula vya maji ya baharini.

Vyakula vyenye protini kidogo ni maharagwe, karanga, mboga za majani, dengu, nafaka (ngano, shayiri, kokwa (nuts) mtama n.k.

Vyakula vya kutia nguvu mwilini vyakula vya sukari na wanga.

Vyakula vya sukari na vya wanga hutia nguvu mwilini. Viko kama kuni zilivyo kwa moto. Kwa jinsi mtu anavyofanya kazi kwa nguvu ndivyo anavyohitaji nguvu zaidi lakini kula vyakula hivi peke yake bila protini hufanya miili yetu idhoofike.

Vyakula vya wanga nafaka, (ngano, mpunga, mahindi, shayiri, mtama, ulezi) viazi mviringo, viazi vitamu viazi vikuu mihogo ndizi za kupika, magimbi.

Vyakula vya sukari ni:- matunda, sukari ndizi mbivu, asali, maziwa.

Vyakula vya kuweka akiba mwilini mafuta

Mafuta ni aina nzito ya akiba ya nguvu mwilini. Miili yetu huyabadilisha mafuta kuwa sukari. Wakati nguvu zinapohitajika kula mafuta mengi kunawezesha kumdhuru mtu, lakini mafuta ya kiasi katika mlo huleta afya bora.

Vyakula vyenye mafuta kwa wingi kama vile:-Mafuta ya kupikia mafuta ya mimea ni afadhali kuliko ya nguruwe.

Mafuta ya salad mafuta ya nguruwe, mafuta ya ng’ombe, siagi, margarine (tanbond, blue band n.k)

Vyakula vyenye mafuta kidogo kidogo

Karanga, kokwa (nuts) ufuta, embe mafuta (avocado) nazi, maziwa, maharage ya soya.

Vyakula vya kulinda mwilini vile vyenye vitamini na madini kwa wingi.

Vitamin hulinda mwili husaidia miili yetu ifanye kazi barabara.

Tunaugua ikiwa hatuli vyakula vyenye vitamin zinazohitajiwa.

Madini yanahitajika kwa kutengenezea damu mifupa na meno yaliyo bora.

Vyakula vyenye vitamini na madini kwa wingi:

Nyama, hasa maini, mayai, samaki na mafuta ya maini ya samaki kwa vitamini A, jibini, mboga za majani hasa zenye rangi ya kijani kibichi na ya njano, matunda, nafaka zisizokobolewa, maganda majani ya baharini (see weed, kwa iodine).

Kula vizuri kwa maana gani

Kula vizuri kuna maana ya kula vya kutosha lakini pia kuna maana ya kula mlo kamili wa aina mbalimbali za vyakula vinavyohitajiwa na mwili. Ili kuwa na afya bora mtu anahitaji kula chakula cha kutosha kutoka kila mojawapo ya mafungu yaliyotajwa. Watu wengi hupata vyakula vya kujenga au kulinda mwili kama maharagwe, nyama, samaki, mboga za majani, na matunda ya kutosha.

Watu hawa wanaweza kuugua ugonjwa wa ukosefu wa chakula bora ingawaje wanakula vyakula vyenye wanga kwa wingi.

Mara nyingi utapiamlo ni mkali zaidi kwa watoto ambao wanahitaji chakula bora kwa wingi ili waweze kukua vizuri na kuwa na afya bora. Aina mbili kuu za utapiamlo mkali ni zifuatazo:

Utapiamlo mkavu au unyafuzi kutokana na kutokula vyakula vyakutosha.

- Mtoto huyu hapati chakula cha kutosha cha aina yoyote hasa vile vinavyotia nguvu mwili.

- Husemekana kuwa na utapiamlo mkavu au unyafuzi kwa kifupi ana njaa. Mwili wake ni mdogo, mwembamba na umekondeana sana. Karibu amebakia ngozi na mifupa tu mtoto huyu anahitaji chakula zaidi hasa vile vinavyotia nguvu mwilini.

- Uso wa kizee kila mara ana njaa tumbo kubwa uzito mdogo sana amekondeana sana

Utapiamlo majimaji au upojazo kutokana na kutokula protini za kutosha

2. Mtoto huyu hakua anakula vyakula vya kujenga mwili au protini za kutosha, ingawaje anaweza akawa anapata vyakula vya kutia nguvu mwilini kiasi cha kutosha.

Anasemekana kuwa na upajazo.

Huu huitwa utapiamlo majimaji kwa sababu miguu, mikono na uso huvimba ingawaje anaweza kuonekana kama amenenepa. kuna misuli kidogo sana iliyobaki. Amebakia mifupa na ngozi tu. Mtoto huyu anahitaji vyakula vilivyo na protini kwa wingi.

- Uso uliovimba ambao uko kama mwezi.

- Vidonda na kubabuka kwa ngozi miguu na mikono iliyovimba.

- Ukosefu wa rangi halisi ya nywele na ngozi ya juu mkono ni nyembamba msuli imedhoofika. Lakini anaweza akawa na mafuta kidogo.

Mara nyingi upojazo hutokea kwa mara ya kwanza wakati mtoto anaharisha au ana maradhi mengine. Mara nyingi huonekana kwa watoto ambao wameacha kunyonya na ambao wanapewa vyakula vilivyotengenezwa kwenye mchele, mahind, sukari au aina zozote za kutia nguvu mwili bila ya maziwa au vyakula vingine vyenye protini.

Mtoto mweye upojazo anaweza kuonekana kama amenenepa badala ya kukonda kwa sababu ya kuvimba na pia kwa sababu mara nyingine anakuwa na mafuta kidogo.

Lakini misuli yake imedhoofika na kama ukiangalia sehemu za juu za mikono yake utaziona ni nyembamba ajabu.

Upajazo na unyafuzi huanza polepole. Mtoto anaweza akawa na ukosefu wa chakula bora lakini akaonyesha dalili chache tu. Njia nzuri ya kuhakikisha kuwa na ukosefu wa chakula bora ni kupima urefu wa kuzunguka sehemu ya juu ya mkono wake.

Hupima ili kuhakikisha kuwa utapiamlo upo au haupo..

Baada ya umri wa mwaka 1 mtoto yeyote ambaye urefu wa kuzunguka sehemu ya juu ya mkono wake uko chini ya cm 13 ana utapiamlo hata kama uso wake miguu na mikono imenenepa kiasi gani kama urefu wa kuzunguka mkono wake uko chini ya cm 12 basi ana utapiamlo mkali sana.

Njia nyingine nzuri ya kuonyesha kuwa mtoto ana afya nzuri au ana utapiamlo ni kumpima mara moja kila mwezi.

Mtoto wenye afya nzuri ambaye anakula chakula bora huongezeka vizuri.

Kupata chakula bora cha kutosha

Watoto wengine hudhoofika na uzito wao kuwa mdogo au huonyesha dalili zingine za utapiamlo majimaji ingawaje wanapata maziwa na vyakula vingine vya kujenga mwili. Hii ni kwa sababu hawapati vyakula vya kutia nguvu mwili kiasi cha kutosha na huchoma protini ambao wangezitumia kwa kukua na kufanya miili yao iwe na nguvu.

Baadhi ya vyakula ambavyo huliwa kwa wingi kama vile ndizi za kupika na mizizi (viazi vikuu, mihogo, jimbi n.k) vina maji na nyuzinyuzi kwa wingi kiasi ambacho mtoto hujaza tumbo bila ya kupata nguvu ya chakula cha kutosheleza mahitaji yake.

Ingawaje tumbo lake haliwezi kuweka chakula zaidi bado angali ana njaa.

Ni muhimu sana kwa watoto kupata chakula si chini ya mara 3 kwa siku na vile vile kuwe na vitafunio katikati ya milo. Kuchanganya kidogo na chakula cha mtoto kunasaidia pia. Ikiwezekana ale vyakula ambavyo si vingi vilivyo bora ambavyo vina nguvu na protini.

Kinga na matibabu ya utapiamlo

Unyafuzi pamoja na upojazo vinaweza kuzuiwa au kutibiwa kwa kula chakula bora na kula vyakula vya kutosha. Kwa watoto wachanga, maziwa ya mama yanatosha kabisa.

Kunyonyesha ni lazima kuendelezwa kwa muda mrefu iwezekanavyo. Akina mama wengine wanawanyonyesha watoto wao kwa muda wa miaka 2 au zaidi. Baada ya miezi 4 mpaka 6 mtoto lazima apewe vyakula vingine vya kufaa hali akiwa anaendelea kunyonya.

Kitabu cha kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (14)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Sasa, tunaongezea chapisho jingine la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyovyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC), tulianza na dibaji iliyooandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na sura za ndani.

2.7 Mahakama ya Wilaya

Mahakama ya Wilaya huendeshwa na Hakimu wa Wilaya.

Hapo mwanzoni Hakimu wa Wilaya ifikia ngazi au wadhifa huo kwa kupanda cheo kutoka Mahakama ya Mwanzo.

Baadaye, Hakimu wa Wilaya alitakiwa awe na Diploma ya Sheria.

Hivi sasa, kwa mujibu wa sera mpya ya Idara ya Mahakama, kada hii inaondolewa pole pole na Mahakama za Wilaya zitakaliwa na Mahakimu Wakazi.

Mahakama hii imeundwa kusikiliza mashauri ya jinai na yale ya madai kutoka kwenye Wilaya ambayo Mahakama hiyo imo.28(28 Kifungu cha 4 na cha 40 Sheria Namba 2/1984) Inao uwezo wa awa1i sawa na Mahakama ya Hakimu Mkazi katika kusikiliza mashauri ya jinai .Hali hii hufanya watu wengi wajiulize kama kweli kuna umuhimu wa kuwa na mahakama mbili tofauti ambazo kwa kiasi kikubwa zina madaraka na uwezo sawa.

Kwa kawaida rufaa zote kutoka Mahakama ya Wilaya kama i1ivyo kwa zile zitokazo Mahakama ya Hakimu Mkazi huenda moja kwa moja Mahakama Kuu. Aidha Mahakama ya Wilaya husikiliza rufaa zinazotoka Mahakama ya Mwanzo29(29 Angalia kifungu cha 20 (1)cha Sheria Namba 2/1984) lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi haina nafasi hii. Uwezo wa Mahakarna ya Wilaya katika mashauri ya madai pia ni sawa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ila lazima Hakimu katika Mahakama ya Wilaya 30 (30 Itakumbukwa kwamba siyo kila Hakimu wa Wilaya ana uwezo wa kusiliza kesi za madai isipokuwa yule ambaye ameteuliwa rasmi na Jaji Mkuu kufanya shughuli hiyo. Tofauti hii itakwisha kutokana na sera mpya ya Idara ya Mahakama kwamba mahakama za Wilaya zote zikaliwe na Mahakimu Wakazi (Mahakimu wenye Shahada za Sheria) ambao moja kwa moja wanakuwa na madaraka ya kusikiliza kesi za madai).

Mahakama ya Wilaya pia inao uwezo wa kuyafanyia masahihisho/mapitio (revision) maamuzi yoyote yaliyofanywa na Mahakama ya Mwanzo mara igunduapo kosa/makosa katika mwenendo wa kesi husika.31 (31 Kifungu cha 22 cha Sheria Namba 2/1984 Angalia pia Vifungu vya 30 na 31 Sheria Namba 2/1984.) Inaweza kugundua makosa katika mwenendo wa kesi baada ya kufanya ukaguzi mara kwa mara kwa kupitia mafaili ya kesi ambazo zimesikilizwa na Mahakarna ya Mwanzo Ukaguzi huu wa mara kwa mara ni jukumu la Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya kwa kutumia madaraka aliyonayo ya kusimamia mahakama zilizo chini yake (supervisory powers) Njia nyingine ambayo yaweza kuifanya Mahakarna ya Wilaya igundue makosa katika mwenendo wa kesi iliyo/inayosikilizwa na Mahakama ya Mwanzo ni kwa kupokea malalamiko toka kwa mhusika katika kesi Labda swali la kujiuliza ni je mara ngapi Mahakama za Wilaya , zimetekeleza jukumu lake la kiusimamizi kwa Mahakama za , Mwanzo.

Ukweli ni kwamba ukaguzi haufanyiki kama inavyopasa na ziko sababu mbalimbali, kama uhaba wa mahakimu wa Wilaya, ukosefu wa nyenzo kama usafiri, ukosefu wa fedha nk. Hali hii imepelekea Mahakama za Mwanzo kufanya shughuli zake bila kukaguliwa na matokeo yake ni Mahakimu husika kujisahahu na haki kuonekana kama bidhaa adimu kwa mtu wa kawaida.

2.8 Mahakama ya Mwanzo.

Hii ikiwa ni mahakama ya chini kabisa katika mfumo wa mahakama nchini imeundwa na kifungu cha 3 cha Sheria ya Mahakama ya Hakimu 32 (Angalia kifungu cha 3 cha sheria Namba 2/1984) kusikiliza mashauri yatokayo kwenye Wilaya ambayo mahakama hiyo iko. Ina uwezo wa awali kusikiliza kesi za ndoa, 33 (Kifungu cha 18 (1) b cha Sheria Namba 2/1984) Mirathi na madai ambayo yanaongozwa na sheria za Kimila au Kiislamu 34(Kifungu cha 18 (1) (a) (i) cha Sheria Namba 2/1984) Mhakama za Mwanzo zina uwezo wa kusikiliza kesi za jinai35 Zile ambazo zimeorodheshwa kwenye Jedwali la Kwanza la Magistrates Court Act, 1984.) na za Madai.

Kesi za jinai katika Mahakama za Mwanzo hufunguliwa kwa mlalamikaji mwenyewe kwenda mahakamani moja kwa moja au kwa kupitia polisi.

Pia Mahakama hizi zina uwezo wa kushughulikia kesi za madai ambazo zinatawaliwa na sheria za kimila au za kiislamu isipokuwa kama madai yanahusu umilikaji wa ardhi iliyosajiliwa chini ya sheria ya ardhi 36(Itakumbukwa kwamba Mahakama ya Mwazo itakuwa na uwezo wa kusikiliza shauri la mirathi ambalo linahusika na sheria ya kimila hata kama mali husika imesajiliwa chini y a sheria ya ardhi).

Ijue thamani ya damu kwa mwanadamu (7)

lUnayajua makundi yake ikiwamo Damu Azizi?

Na Pd. Evaristo J. Lefiyo C.PP.S

Sadaka ya Kondoo wa Pasaka.

Mungu alitaka kuwatoa wana wateule wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri alimwamuru Musa anyunyuzie/apake Damu ya mwanakondoo katika milango ya nyumba zao kwa njia ya malaika. Damu ilitumika kama nembo "Signal" au ishara ya kuwanusuru. Damu ilitumika hapa kama kitambulisho cha kubaini wana wa Mungu, wateule na wale waliojitenga naye. Wazawa wa kwanza walisalimika kwa ishara ya Damu kama kitambulisho.

Ambao hawakuwa na kile kitambulisho yaani Damu walipoteza maisha yao.Vivyo hivyo katika Agano Jipya Kristu, kwa Damu yake ametuweka alama kama mchungaji awajuavyo kondoo wake (Yoh 10:4-6).Kristo ametutambulisha kwa Baba kwa zawadi hii ya kitambulisho yaani Damu ya mwanaye, kitambulisho ambacho ndicho bei ya wokovu wetu. Katika nchi zetu ili utambulike kuwa wewe ni raia halali na kupata mafao ya raia ni lazima kuonyesha kitambulisho la sivyo utakamatwa kama jambazi, mzururaji,watumwa, mzamiaji na pengine kama mkimbizi.

Sisi sote tuliobatizwa tukanyweshwa Damu ya Kristu si Wazururaji tena, wala wakimbizi, wala watumwa tena wala wazamiaji bali ni Taifa Takatifu la Mungu (1Pt 2: 8-10). Sisi ni rafiki zake Yesu (Yoh 15:14-15) iwapo tutafanya aliyotufundisha. Ndiyo kusema kwamba hakuna haja ya kuhangaika na kukata tamaa tukijua kwamba bei ya wokovu wetu ni Damu Azizi ya Kristo.

"Wakaimba wimbo huu mpya: "Wewe wastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechijwa na kwa Damu yako umemnunulia Mungu wetu watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa (Ufu 5:9)

Damu kama sadaka ya kuondolea dhambi:

Katika Misa Takatifu kila siku "Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia ...", ndiye ambaye kwa Damu yake tu twaweza kuondolewa hila na dhambi zote (Yoh 19:36; 1Pt 1:19). Ndiye ambaye hata Yohane alimkiri kuwa kweli kafara iondoayo dhambi ya dunia (Yoh 1:29-31);

KALISI YA AGANO LA KALE NDANI WATU

KALISI YA AGANO JIPYA

Damu ya Kristu iliyomwagika na inayoashiria kifo cha huzuni inaonyesha pia, lakini, wokovu, maisha, amani na utukufu. Sadaka ya maondoleo ya dhambi ifanyike kwa njia ya Damu ya Yesu (Ebr 9:11-14).

Ni sadaka ya maondoleo ya dhambi kama ile ya Agano la kale ya "YoM KiPPur" yaani siku ya maondoleo "The day of atonent" inapoombwa dua kwa ajili ya maondoleo ya dhambi wa kuhani anatoa sadaka na dhambi za watu wa Mungu.

SADAKA ya maondoleo ya dhambi:

Sadaka ya maondoleo ya dhambi iliyokamilishwa katika kunyunyizia Damu Sanduku la Agano katika Agano la Kale iliendeleza muungano; marudiano/mapatano, na undugu kati ya Taifa na Mungu (Rej. Law 16).

Marudiano hayo, upatanisho huo haukuishia katika Agano la Kale bali unaendelezwa na ile damu ya Abeli, kuliko ile damu ya Agano la Kale iwapo tunaona mwandishi kwa Waebrania anaendelea kutualika walimwengu wa leo akisema,

"Lakini kwa Damu ya Kristo mambo makuu zaidi hufanyika! kwa nguvu ya Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tuupate kumtumikia Mungu aliye hai " (Ebr 9: 14).

Watakatifu wataosha mavazi yao katika Damu ya huyo mwanakondoo (Ebr 7: 9 ,14) na kuyafanya meupe katika Damu Azizi, kwa sababu wameteseka na Yesu, wamevumilia na kustahimili kifodini chao na Kristo na wakakingwa na Damu ya Kristo kama vile ile Damu ya Agano la kale ilivyowakinga Waisraeli na hatimaye kupata kibali cha utukufu pamoja na Kristo.

Twaeni mnywe wote:

Yesu alipoiweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu alitualika sote tushiriki kula na kunywa Damu ya Yesu ( Mk 14:22-26) , alituachia agizo kwamba tuendeleze karamu hiyo na kuwalisha wengine, kuwajali maskini, watoto wa mtaani, walemavu, waliokumbwa na balaa la madawa ya kulevya, wakimbizi wa kisiasa, yatima, wenye taahira ya akili na wale wanaokosa amani kwa sababu ya vita vya mara kwa mara. Yesu anapotuambia "

Itaendelea

Kuwa makini kuijua Biblia (16)

KATIKA toleo hili, tunaendelea kuangalia maswali kama tulivyokusudia kuwaletea mfulululizo wa maswali muhimu juu ya Kitabu Kitakatifu cha Biblia. Mfululuzio wa maswali haya muhimu tunazidi kuuleta kwa msaada wa kitabu cha KATEKISIMU YA BIBLIA kilichondikwa na Padre Christian L. Mhagama.

Lakini kwenu isiwe hivyo ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu sharti awe mtumishi wenu; anayetaka kuwa wa kwanza sharti awe mtumishi wa wote. Maana Mwana wa mtu hakuja kutumikiwa ila kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi (Marko 10:40-45).

Ujumbe huu wapatikana pia katika fasuli zifuatazo Ezekieli 34; Hekima ya Yoshua bin Sira 9:17-10:5; Mathayo 18:1-5,1Timotheo 3:1-13.

28. Biblia yatuambia nini kuhusu suala la matumizi ya miili yetu?

Biblia inawaonya watu wasitawaliwe na tamaa za mwili zinazoweza kuwatosa katika dhambi za uzinzi. Aidha Biblia hufundisha kuwa watu watumie miili yao kwa sifa ya Mungu. Tusikilize ujumbe:

"Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali kwa ajili ya kumtumikia Bwana naye Bwana ni kwa ajili ya mwili. Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake. Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo! Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye kama ilivyoandikwa ,nao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye. Jiepusheni kabisa na uzinzi.

Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili, lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, aliye ndani yenu, mliyempokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi si mali yenu wenyewe. Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu." (1Wakorintho 6:13-20). "Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda nyumbani; lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.

Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha. Basi, walimu wa sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.

Kisha wakamwuliza Yesu, ,"Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. Katika sheria yetu Musa alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe.

Basi, wewe wasemaje?’ Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, ‘mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.’ Kisha akainama tena, akaandika ardhini. Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmoja mmoja, wakitangulia wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. Yesu alipoinuka akamwuliza yule mwanamke, ‘Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?’ huyo mwanamke akamjibu, ‘Bwana hakuna hata mmoja!’ naye Yesu akamwambia, ‘Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena’ (Yohane 7:53-8:11 ). Ujumbe huu wapatikana pia katika fasuli zifuatazo: Methali 5: 1- 23; Hekima ya Yoshua bin Sira 23: 16-19; Wakolosai 3:5- 7).

29. Biblia yatuambia nini kuhusu suala la umoja na amani?

Biblia yatuambia kwamba japokuwa Mungu aliwateua Waisraeli kuwa Taifa lake kwa namna ya pekee, hata hivyo alikuwa na mpango wa kuwaunganisha watu wote chini ya mwanae Yesu Kristo. Katika Yesu Kristo hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru.

‘Vision Hotel and Tourism College’ Chuo kinachojali ubora wa taaluma kuliko pesa

lHuzingatia zaidi mafunzo ya vitendo kuliko nadharia

lWashauri Serikali isimamie mitaala kwa vyuo vya utalii

lAsilimia 70 ya wahitimu hupata kazi katika hoteli kubwa

Maryamu Salumu, DSJ, na Josephs Sabinus

"WAZAZI wengi wamezoea kulipa ada kwa malipo nafuu na kushindwa au wengine kukwepa kulipa kozi nzuri au za muda mrefu. Tungeweza kupunguza muda na programu zetu ili kupata wanafunzi wengi zaidi lakini, lengo letu sio kupata wanafunzi wengi, wala pesa nyingi bali, ni kutoa kiwango bora cha elimu."

Mkurugenzi Mtendaji wa chuo cha Vision Hotel and Tourism College, kilichopo Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Mile S. Mbwile, aliliambia gazeti hili katika mazungumzo maalumu yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo mintarafu chuo hicho, Bw. Mbwile alisema uongozi mzima wa chuo hicho ulishaweka mkakati wa kutoa kipaumbele katika ubora wa taaluma kuliko idadi ya wanafunzi na pesa hivyo, hawapendi kupunguza malipo ya kozi za chuo kwa lengo la kupata wateja wengi.

Anasema kama lingekuwa suala pekee la kujaza wanafunzi ili kujipatia pesa nyingi, wangefanya hivyo lakini, hawawezi kwa kuwa watalazimika kupunguza vipindi na hali hiyo, italazimu kupunguza muda na ubora wa taaluma kitu alichosema, hawakitaki.

"Tunataka hata kama tutakuwa na wanafunzi wachache, lakini ubora wa taaluma watakaoupata, waende kuwa mabalozi wetu. Na lengo hili linatusaidia sana maana karibu zaidi ya asilimia zaidi ya 70 mpaka 80 ya wahitimu wetu, wanapata kazi katika hoteli nyingi kubwa kubwa hasa katika hoteli walizofanyia mafunzo kwa vitendo; wakaonekana walivyo bora."

Katika mazungumzo hayo, Bw. Mbwile alitoa mfano wa mhitimu wake anayeitwa Lilian Sanga, anayefanya kazi katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), yaliyopo Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Katika ufafanuzi wake, Bw. Mbwile alisema chuo hicho, kina taaluma ya uendeshaji wa mafunzo (kozi ) mbalimbali ya hoteli. Chuo hiki chenye Hoteli maarufu mbili; moja ikiwa ni ile ya Mision to Seamen na nyingine iliyopo katika Makao Makuu yake maeneo ya Kurasini, kinaaminika kwa kuwa na walimu wenye taaluma na uzoefu katika huduma za hoteli.

Chuo hiki kilichoanzishwa mwaka 1996, kimekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wahitimu wake wengi, wameajiriwa katika hoteli mbalimbali za kitalii na wengine kati yao, ni wakuu wa idara katika shughuli za uendeshaji wa hoteli.

Anasema kwa miaka mitano iliyopita, chuo kimejipatia umaarufu na hata kutembelewa mara kwa mara na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu za Serikali, vyama vya siasa, na taasisi mbalimbali, kimetoa kozi zake katika maeneo makuu mawili.

Anayataja maeneo hayo kuwa ni Idara ya Mapishi (Food Production), na Idara ya Mauzo na Huduma za Vyakula na Vinywaji (Food and Beverage Service & Sales).

Anaendelea kufafanua kuwa, kozi hizi ni za mwaka mmoja mmoja. Zimegawanywa kwa taratibu kuwa, miezi minne ya mwanzo, ni kwa ajili ya masomo ya nadharia yanayofanyika chuoni. Miezi mitatu inayofuatia, ni kwa ajili ya mafunzo ya nadharia na vitendo hapo hapo chuoni.

Bw. Mbile anaendelea, "Miezi mitatu mingine inayofuatia, hutumika kwa ajili ya Industrial Attachment (mafunzo kwa vitendo) katika hoteli mbalimbali za kitalii na kisha, miezi miwili ya mwisho, hutumika kwa marudio, mitihani na shughuli za mahafali."

Anasema, "Vipindi hivi vya kozi, vinawasaidia sana wanafunzi uelewa wa kutosha kuwawezesha kutafuta kazi kwa kuwa kivitendo, wanakuwa wameiva sana.

Anadokeza kuwa, kwa kuwa mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho yanakuwa na msisitizo mkubwa katika vitendo, wahitimu wake hukubalika kwa wingi na kwa urahisi kuajiriwa hasa katika hoteli walizofanya mafunzo kwa vitendo na kuonekana namna walivyoiva kitaaluma.

"... hata taarifa tunazopata toka katika hoteli wanazofanya mazoezi, zinafurahisha sana kwa kuwa ni nzuri mno," alisema na kuongeza kuwa, Vision Hotel and Toutrism College, ni miongoni mwa vyuo vichache vya utalii nchini, vyenye walimu na wakufunzi waliobobea katika masuala ya hoteli. Wengi wao, wamepata mafunzo yao nje ya nchi na wana shahada mbalimbali.

Alizitaja baadhi ya hoteli ambazo chuo hicho hupeleka wanafunzi wao kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kuwa ni pamoja na iliyokuwa Sheraton (siku hizi Royal Palm), White Sands, Bahari Beach na Jangwani See Breeze za Dar-Es-Salaam.

Nyingine anasema ni Mapenzi Hoteli, Kiwenge Club, Motel Agip, New Africa, Mount Meru (Arusha), Impala Hotel (Arusha) na Serengeti Safari Lodge.

Hata hivyo licha ya kuzipongeza hoteli zote zinazotoa ushirikiano kwa kupokea wanafunzi wake katika mafunzo kwa vitendo na hata kuajiri wahitimu, anazilaumu nyingine zinazokataa kuwapokea wanafunzi kwa ajili ya mazoezi.

Mkurugenzi huyo Mtendaji anadokeza kuwa, katika kipindi cha mwaka ujao, chuo chake kitaendesha kozi za Food Production, Food and Bevarage Services & Sales na House Keeping (Utunzaji wa Nyumba). Wahusika ni wahitimu wa Kidato cha Nne na kuendelea, waliofaulu vizuri katika somo la Kiingereza.

Katika mwaka huo, pia chuo kitatoa Shahada katika Usimamizi wa Hoteli (Diploma in Hotel Manegement) na Shahada katika Usimamizi na Utoaji wa Huduma za Vyakula (Diploma in Catering Management). Wanaohusika ni wenye mafunzo ya awali katika mojawapo ya mafunzo ya taaluma za mambo ya hoteli.

Bw. Mbwille anasema mafaniko katika Hoteli hiyo, yanatokana na uvumilivu wao juu ya vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wazazi wengine kuchelewa kulipa ada, vyuo vingi kutoa elimu kwa mvuto wa bei nafuu na hivyo kuwakosesha wateja.

Ingawa hataji kiasi, Bw. Mbwile anadokeza kuwa, licha ya ubora wa taaluma inayotolewa na chuo chake, bado gharama ni nafuu mara nne kuliko ilivyo kwa baadhi ya vyuo nchini Kenya na anawashauri wazazi wasipoteze pesa nyingi kupeleka vijana nje ya nchi huku wakiacha taaluma bora nchini mwao.

Anawataja viongozi (Wakurugenzi) wengine wanaoshirikiana kuendesha chuo hicho kuwa ni pamoja na Adamu Nderumaki, ambaye pia inaiongoza Idara ya Vyakula na Vinywaji, wakati Deogras Sakibu, anaongoza Idara ya Chakula.

Kutokana na mlipuko wa vyuo vingi vinavyojali maslahi binafsi, Bw. Mbwile anaishauri Serikali kuunda mitaala na kuisimamia ili iwe na kiwango sawa cha taaluma ya mambo ya hoteli katika vyuo vyote kuliko hali ilivyo sasa ambapo kila chuo kinajiamualia mambo yake.

"Serikali iweke muhtasari katika vyuo vya utalii.

Hivi sasa kila chuo kina Mhtasari wake. Ni vema Muhtasari ikawa moja na Serikali iweke utaratibu madhubuti wa kusimamia mwenendo wa vyuo hivi vya utalii. Hii itasaidia kuwa na taaluma bora ya utalii nchini," alisema.

Anasema, anayetaka taaluma bora ya Utalii, asihangaike kutafuta unafuu wa gharama, bali atafute chuo kinacholenga kutoa taaluma hiyo bora. Anasema, "Chuo hicho ni Vision Hotel and Tourism College".

Anaongeza kuwa, chuo hicho huwatafutia hoteli za kufanyia mafunzo ya vitendo wanafunzi wake, na kuwasaidia wahitimu kutafuta kazi.