Make your own free website on Tripod.com

Daktari wa Kiongozi

Kinga na matibabu ya utapiamlo (9)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini na mahali ambapo si rahisi kumpata mtaalamu wa afya kwa haraka

Ili watoto wa umri huu waweze kuwa na afya ni lazima:

Kuwapa maziwa ya mama, kuwapa vyakula vingine vya kufaa pia kuchemsha maji wanayokunywa na kuweka watoto na mazingira yao katika hali ya usafi.

Mwaka 1 na kuendelea

Mtoto akishafikisha umri wa mwaka mmoja anaweza kula chakula sawa na watu wazima lakini apewe maziwa pia kila inapowezekana.

Kila siku jaribu kumpa mtoto chakula chenye protini vitamini, chuma, na madini kwa wingi (kama ilivyooneshwa hapo mwanzo ili akue vizuri akiwa na nguvu na afya).

Watoto na vitu vitamu vyenye sukari

Usiwazoeshe watoto kula vitu vitamuvitamu vyenye sukari au soda. wakati ambao wamekula pipi kwa wingi hawapendi tena vyakula vingine ambayo ni vya manufaa zaidi kwao.

Pipi ni mbaya kwa meno yao pia.

Walakini wakati ambao chakula ni kidogo kuongeza sukari na mafuta kidogo kwenye maziwa au chakula kingine humwezesha mtoto kutumia protini iliyoko kwenye chakula anachopata kabisa.

Vyakula vizuri kwa watoto

Miezi 4-6 ya kwanza maziwa ya mama bila kitu kingine chochote ni mazuri na si ya chupa.

Kutoka miezi 6-miaka 2 Maziwa ya mama na pia ya ng'ombe, mbuzi au maziwa ya unga na vyakula bora vingine vilivyo pikwa vizuri.

Mawazo mabaya kuhusu Chakula

1. Vyakula vya akinamama baada ya kujifungua: katika sehemu nyingi duniani kuna imani kuwa mwanamke ambaye amejifungua hivi karibuni asile baadhi ya vyakua.

Imani ya namna hii isiyomruhusu mama kula chakula kizuri bali kumruhusu ale vitu kama uji, maji ya mchele ni ya hatari sana. Mama anayekula chakula cha aina hii hudhoofisha na hupatwa na upungufu wa damu. inaweza hata kusababisha kifo kwa kufanya mtu apate mara kwa mara au kutokwa na damu.

Baada ya kujifungua mama anahitaji chakula kizuri kama inavyowezekana.

Mama ambaye amejifungua anahitaji vyakula vya kujenga mwili kama vile maharagwe, mayai, kuku, maziwa na bidhaa zake, nyama, samaki, matunda na mboga za majani.

Hakuna hata chakula kimoja kati ya hivi ambacho kitamdhuru; vyote vitamletea afya bora.

2. Si kweli pia kuwa machungwa, mapera au matunda mengine ni mabaya kwa mtu ambaye ana mafua, fluu au kikohozi, Ukweli ni kwamba matunda kama machungwa na nyanya yana vitamin C kwa wingi ambayo inaweza kuisaidia kupigana na mafua au maradhhi mengine.

3. Si kweli kwamba baadhi ya vyakula kama vile nguruwe, viungo, mapera haviwezi kuliwa wakati tunatumia dawa.

Matatizo ya afya yanahusiana na kiliwacho na watu

Vyakula maalumu ni kinga na matibabu kwa baadhi ya magonjwa mengine. Hapa kuna baadhi ya magonjwa hayo:

Upungufu wa damu (ANEMIA)

Mtu mwenye upungufu wa damu ana damu nyembamba.

Hii hutokea wakati damu inapopotea au kuharibika kwa kazi kuliko inavyotengenezwa. Damu inayopotea kutokana na vidonda vikubwa , vindonda vya tumboni au kuhara damu, inaweza kusababisha upungufuu wa damu hata kwenda mwezi kunaweza kusababisha upungufu wa damu kwa wanawake kama hawali vyakula vinavyohitajiwa na mwili.

Chakula kilichopungua nyama, mboga za majani na vyakula vilivyo na chuma kwa wingi kunaweza kusababisha upungufu wa damu au kuufanya uzidi.

Kwa watoto upungufu wa damu unaweza kutokea kwa sababu ya kua vyakula ambavyo havina chuma kwa wingi unaweza pia kuletwa na kumnyonyesha mtoto au kumpa maziwa ya chupa baada ya miezi 6 bila kumpa vyakula vingine sababu Kuu za upungufu wa damu kwa watoto ni safura na kuharisha kwa muda mrefu na kuhara damu.

Malaria ambayo inaharibu damu, inaweza kusababisha upungufu wa damu pia.

Dalili za Anaemia.

-Ngozi nyeupe inayopenyeka na nuru

- Ufizi mweupe

-Kucha nyeupe

- Kulegea pamoja na kuchoka

-Kama upungufu wa damu ni mkali sana, uso pamoja na miguu vinaweza kuvimba, moyo hupiga na kasi sana, na mtu hupata shida ya pumzi.

-Kwa kawaida watoto pamoja na akinamama ambao hupenda kula uchafu wana upungufu wa damu.

Matibabu na Kinga za upungufu wa damu

-Kula vyakula vyenye chuma kwa wingi, nyama, samaki, kuku na mayai vina chuma kwa wingi.

Maini hasa ndiyo yenye chuma kwa wingi zaidi. Mboga za majani, maharagwe, njegere na dengu zina chuma kidogo pia.

-Kama vyakula vyenye chuma kwa wingi ni taabu kuvipata au upungufu wa damu ni mkali mgonjwa ni lazima ameze chuma (vidonge vya sulfate ya chuma jambo hili ni la muhimu sana hasa kwa akinamama wajawazito ambao wana upungufu wa damu.

Karibu wagonjwa wote wa upungufu wanaweza kutibiwa kwa vidonge vya sulfate ya chuma vizuri zaidi kuliko maji ya ini (liver extract) au Vitamin b12. kwa kawaida chuma ni lazima kitolewe kwa njia ya kumeza kwa mdomo siyo kwa sindano kwa sababu ni za hatari zaidi.

Wanawake wengine wana upungufu wa damu mara nyingi hii ni kwa sababu hawali vyakula vya kutosha vilivyo na chuma kwa wingi ili kuridhisha ile inayopotea wakati wa kwenda mwezini au wakati wa kujifungua kwa sababu hii ni muhimu sana kwa akinamama kula maharagwe kwa wingi iwezekanavyo hasa wakati wakiwa na mimba.

Kitabu cha kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (21)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Tunaendelea na chapisho la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyovyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC). Tulianza na dibaji iliyooandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na sura za ndani.

Hivyo basi uamuzi wowote kitika Mahakama ya Mwanzo utakuwa batili endapo hautahusisha maamuzi ya Wazee wa Baraza.

Ifahamike kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa Mzee wa Baraza.

Sheria imebainisha orodha ya watu ambao hawastahili kuwa wazee wa Baraza kama ifuatavyo:

a). Mawaziri na Wabunge,

b). Mahakimu na Majaji,

c). Viongozi wa dini,

d). Madaktari

e). Mawakili

f). Wanajeshi

g). Wasiokuwa na akili timamu

h) Askari Polisi na Askari Magereza

i) Maafisa wengine wa Serikali kama itakavyotangazwa na Jaji Mkuu.

Huu ni ushahidi kuwa Mahakama za Mwanzo zililenga katika kumaliza migogoro kwa haraka na hasa kwa kuzingatia sheria za mila; na ndiyo maana watu wenye taaluma wamezuiliwa kushiriki katika kundi la Wazee wa Baraza kwani wangeweza kuingiza ya kitaaluma na ubishi katika kushughulikia migogoro kuchelewesha uamuzi.

Japokuwa wazee wa Baraza siyo maofisa wa Mahakama na wala hawachaguliwi na Mahakama bado wanalipwa na Mahakama posho zao za vikao. Malipo haya hufanywa kwa kutegemea kupatikama kwa fedha toka Hazina kama Idara ya Mahakama inavyooomba kwenye makisio ya matumizi yake ya Mwaka (Annual Budget).

Hii ina maana kwamba fedha ikichelewa au isipotolewa na Hazina, kama ilivyo kawaida hakutakuwepo malipo kwa wazee wa Baraza kipindi hicho wakati mwingine hupita hata miaka miwili au mitatu bila kutolewa posho kwa wazee wa Baraza. Pamoja na hali hii ngumu wazee wa Baraza huendelea kuhudhuria vikao vya Mahakama bila kukosa kwa kujitolea.

Kwa kuwa uamuzi wa Mahakama za Mwanzo unafanyika kwa kura kati ya Hakimu na Wazee aliokaa nao kusikiliza kesi hakuna shaka kwamba nafasi ya Wazee ni kubwa na muhimu kwenye Mahakama za Mwanzo. Mahakama isipozingatia haya itasababisha uamuzi mzima wa Mahakama ya Mwanzo ubatilishwe na Mahakama iliyo juu.

Itakumbukwa kwamba Wazee wa Baraza wanapaswa siyo tu kutolea uamuzi mambo yatokanayona maelezo (facts) na ushahidi (evidence) ila ni jukumu lao pia kuingilia suala la tafsiri ya sheria japokuwa wao hawakupata mafunzo hayo. Kimsingi lazima wazee wa Baraza wahusishwe katika mahakama ya mwanzo wakati wa vikao kushughulikia yafuatayo:-

(a) Kuahirishwa kesi

(b) Kutoa dhamana kwa mshitakiwa

(c) Kutoa hukumu na adhabu

(d) Ulipaji fidia

(e) Suala lingine lolote linalohusiana na mashauri

Kwa kadiri ya msimamo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kutowashirikisha kikamilifu wazee wa baraza katika mashauri yaliyo mbele ya mahakama ni sababu nzito na ya kutosha kubatilisha uamuzi wowote utakaofikiwa na mahakama hiyo.

3.4 Nafasi ya Hakimu

Katika kusikiliza kesi kwenye Mahakama za Mwanzo, Hakimu anayo nafasi kama ilivyo kwa Wazee wa Baraza. Hata hivyo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni Afisa wa Mahakama (Judical Oficer). lazima awe amepata mafunzo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo na kabla ya kuanza kazi anatakiwa kula kiapo kutenda haki bila woga, upendeleo wala huba. Hulipwa mshahara kila mwezi kama watumishi wengine wa umma/serikali (Civil Servant) kwa ajili ya kazi anayofanya.

Kwa kuwa Hakimu ana ujuzi na upeo wa uelewa katika sheria zinazotumika kwenye Mahakama za Mwanzo, basi ni jukumu lake kuu kuwafafanulia/kuwaelekeza wazee wa Baraza msimamo wa sheria kuhusu suala linalokuwa mbele yao kabla hawajafikia uamuzi wa kesi. Siyo sahihi kwa Hakimu kuwaachia Wazee wa Baraza kufanya wanavyotaka kwa kutumia kisingizio cha wingi wa kura zao wakati wa kuamua kesi. hivyo basi endapo itatokea Wazee wa Baraza wakapuuza ufafanuzi wake na kfuanya uamzui ambao sio wa haki, Hakimu bado anayo nafasi kuwasilisha taarifa kwenye Mahakama iliyoko juu (Mahakama ya Wilaya) ili itumie madaraka iliyokuwa nayo kufanya masahihisho (revision) na kunyoosha kile kinachokuwa kimepindwa. Hakimu anafanya kosa kubwa kunyamazia kitendo cha mtu kunyimwa haki kutokana na upindaji wa sheria.

3.5 Haki ya Dhamana

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru. hivyo basi ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini au kunyang'anywa uhuru wake isopikuwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au katika kutekeleza hukumu au amri halali iliyotolewa na mahakama. Ibara hii ya Katiba inaonyesha wazi jinsi uhuru wa mtu binafsi ulivyo muhimu katika nyakati mbalimbali mahaka nchini Tanzania (hususan Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa) zimejitahidi kulinda haki hii ya kikatiba mpaka kubatilisha sheria ambazo zilijaribu kuondoa haki hii, lakini serikali nayo imekuwa macho na kuhakikisha kuwa sheria za namna hiyo haizondolewi na mahakama kwa urahisi. Katiba pia inabainisha hai ambapo uhuru wa mtu binafsi unaweza kuondolewa. Itaendelea toleo lijalo

Kuwa makini kuijua Biblia (24)

KATIKA toleo hili, tunaendelea kuangalia maswali kama tulivyokusudia kuwaletea mfulululizo wa maswali muhimu juu ya Kitabu Kitakatifu cha Biblia. Mfululuzio wa maswali haya muhimu tunazidi kuuleta kwa msaada wa kitabu cha KATEKISIMU YA BIBLIA kilichondikwa na Padre Christian L. Mhagama.

 

Mpango wa masomo ya Misa Jumapili na Sikukuu ulikuwaje siku za nyuma kabla ya utaratibu tulionao sasa?

Utaratibu wa masomo ya Misa Jumapili na Sikukuu utumikao sasa ulipendekezwa na Mtaguso wa Vatikano II.

Huko nyuma kulikuwa na masomo mawili kila Jumapili: moja toka hasa barua za Mitume na mmoja toka Injili. Masomo hayo yalirudiwa kila mwaka kwa utaratibu ule ule.

Mtaguso wa Vatikano II ulitoa mapendekezo gani yaliyobadili mpango wa masomo wa siku za nyuma?

Mtaguso ulitoa mapendekezo katika vipengele vitatu kama ifuatavyo: kwanza, idadi ya masomo iongezwe; pili masomo yachukuliwe toka sehemu mbalimbali za Biblia;tatu masomo yapangwe kwa jinsi inayofaa zaidi.

Je, mapendekezo ya Mtaguso wa Vatikano II yalitekelezwa vipi kwa ujumla?

Baada ya mapendekezo kutolewa, mara moja ilianza kazi ya kurekebisha mpango wa masomo.

Katika ibada zote zilizofanywa katika Kanisa kuhusu ibada ya Misa utekelezaji ulifanyika ifuatavyo:-

(a) Ongezeko la masomo: toka mawili yakapangwa masomo matatu na hayo hayakurudiwa kila mwaka bali yalipangwa katika mzunguko wa miaka mitatu A,B,C.

(b) Masomo toka sehemu mbalimbali; somo la kwanza lilichukuliwa toka Agano la Kale na Matendo ya Mitume, la pili toka barua za Mitume la tatu toka Injili.

(c) Mpango unaofaa: masomo yameoanishwa vizuri kulingana na dhamira zao.

Mapendekezo ya Mtaguso yametekelezwa vipi kwa namna ya pekee kuhusu Injili?

Injili tatu za kwanza kila moja imepata mwaka wake: A - Mathayo, B-Marko, C- Luka. Injili ya Yohane inaingia katika kila mwaka wakati wa kipindi cha Pasaka. Masomo yaliyoteuliwa toka Injili moja ni yale yaliyo ya pekee katika Injili ile.

Kwa maneno mengine, kila injili mkazo wa pekee kuhusu maisha ya mafundisho ya Yesu na hayo ndiyo yaliyoteuliwa toka Injili inayosomwa katika mwaka wake.

Tufanyejeli waumini wauelewe na wafaidike na mpango huu wa masomo?

Tunawajibika kuwaeleza Waumini mantiki ya mpango wa masomo utumikao sasa. Waumini wapewe kozi ya msingi kuhusu Biblia kwa jumla na hasa kozi ya msingi kuhusu Injili.

Kuwaaga na kuwaasa wasomaji/wasikilizaji

Ndugu Wasomaji

Tumefikia mwisho wa kozi hii ya iliyotarajia kuwapeni maarifa ya msingi juu ya Biblia. Maarifa hayana mwisho. Maarifa mliyojipatia katika ‘Katekisimu ya Biblia’ ni hatua ndogo ya mwanzo. Ili kuifahamu biblia kwa undani, safari haina budi iendelee. Kwa hiyo katika kikao hiki cha kuagana nanyi tunapenda kuwapeni nasaha chache.

Jambo muhimu na la kwanza ni kujipatia Biblia yenye msaada. Tunapendekeza mjipatie ‘Biblia Takatifu’ iliyotayarishwa na Shirika la Familia ya Maamkio Jimbo la Iringa. Biblia hiyo ina misaada, yaani maelezo mafupi na fasaha kwa kila kundi la vitabu na kwa kila kitabu. Tena kuna maelezo juu ya maneno au semi ngumu katika Biblia.

Inasisitizwa kuwa Waziri anawajibika katika utengenezaji wa Sera ya Ardhi na kuhakikisha utekelezaji wa sera pamoja na Sheria ya Ardhi jukumu ambalo anakuwa anakabidhiwa na Rais.

 

haki za raia Kitabu cha Tatu

Sheria ya Ardhi Tanzania (4)

3.1 Kamati ya Ugawaji Ardhi

Waziri amepewa mamlaka na sheria hii kuunda kamati za ardhi kushughulikia maombi ya ardhi kwa lengo la kuhakikisha ushiriki wa raia, kurahisisha kazi na kuweka bayaana usimamizi wa ardhi.

Kwa mujibu wa sheria Waziri ataunda Kamati za kugawa ardhi katika ngazi ya Taifa na Wilaya kwa lengo la kusaidia ushauri katika maombi ya hati za haki miliki ya ardhi.

Kamati hizi huundwa kwa kushirikisha watu na maofisa wa serikali hata kutoka Wizara nyingine.

Majina ya wajumbe wa kamati hizo hutolewa katika gazeti la serikali na kutumwa Makao Makuu Wizarani na Wilayani.

3.2 Baraza la Ushauri wa Ardhi la Taifa

Mbali na kuwa na mamlaka ya kuunda kamati ya kugawa ardhi, Waziri anayo pia mamlaka ya kuunda Baraza la Ushauri wa ardhi la Taifa na kuweka kanuni za kuainisha wajumbe wanaounda Baraza hilo na kuweka taratibu za majukumu yao. Sheria imeweka msisitizo wa kuhakikisha kuwepo kwa uwiano wa jinsia katika uteuzi wa wajumbe wa Baraza hilo.

Baraza hili ni chombo cha ushauri kwa Waziri kuhusu kufanya marejeo na mabadiliko kwenye sera ya ardhi, lakini sio kwenye Sheria ya Ardhi.

Pia huweza kushauri juu ya muundo na mmalaka ya vyombo vinavyoshughulikia masuala ya ardhi.

Umuhimu wa Baraza hili ni kutoa ushauri ili kuepuka migongano ya madaraka na vyombo vingine halali vilivyopo ambavyo shughuli zake zinagusa masuala ya ardhi kwa njia au nyingine.

3.3 Usimamizi wa Ardhi ya Kijiji

Halmashauri za serikali za vijiji ndizo zenye jukumu la kusimamia ardhi yote ya Vijiji katika utekelezaji wa jukumu hilo, halmashauri ya kijiji inapaswa:-

a). Kuzingatia kanuni za maendeleo endelevu na kuoanisha matumizi ya ardhi na suala zima la utunzaji wa mazingira.

b). Kushauriana na kupokea maoni ya mamlaka ya kisheria iliyomo katika eneo lao.

Kwa kurahisisha utendaji, Halmashauri ya kijiji inachukua nafasi ya udhamini na inaweza kuunda kamati maalumu za kushauri na kutoa mapendekezo katika shughuli za usimamizi wa ardhi kwa kuhakikisha hayo hayaendi kinyume na sheria ya Serikali za Mitaa.

Ieleweke wazi kuwa kamati maalum kazi yake ni kutoa ushauri tu na wala siyo kutoa maamuzi yoyote kuhusu usimamizi wa ardhi ya vijiji. Halmashauri ya Kijiji inaweza kugawa ardhi na kuwapatia wamiliki ‘Hati ya Haki ya kumiliki ardhi ya kimila’ baaa ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa kijiji.

Katika utendaji wake halmashauri ya kijiji inapaswa;

a). Katika kila Mkutano Mkuu wa kawaida wa kijiji kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya wanakijiji katika utendaji utawala na usimamizi wa ardhi.

Kuitaarifu kamati ya Maendeleo ya Kata na Halmashauri ya Wilaya ambamo ardhi ya kijiji imo kuhusu ugawaji ardhi ya kijijini.

Kamishna anaweza kutoa ushauri wowote kwa halmashauri za vijiji kijumla ama kwa vijiji au kwa kijiji maalumu kuhusiana na usimamizi na utawala wa ardhi na halmashauri hizo zinapaswa kuafiki ushauri huo.

Endapo inatokea malalamiko ya wanakijiji zaidi ya mia moja kufikishwa katika halmashauri ya Wilaya ya kwamba halmashauri ya kijiji haitekelezi majukumu yake kwa mujibu wa sheria Halmashauri ya Wilaya itamtaarifu kamishna wa ardhi na uamuzi unaweza kuwa:

i. Kuwapa fursa wahusika kumaliza mashauri hayo kwa makubaliano ya pamoja au,

ii. Kupitia Halmashauri ya Wilaya tatizo linaweza kutafutiwa ufumbuzi na kuionya halmashauri ya kijiji kuwa makini katika utendaji wake wa kazi ya usimamizi wa ardhi.

iii. Kumwomba kamishna kuagiza uchunguzi ufanyike juu ya malalamiko yaliyotolewa na kutoa maelekezo ya ufumbuzi ambayo lazima yafuatwe.

iv. Kutoa mapendekezo kwa kamishna ambayo yatatakiwa zaidi na hata kama ikiwezekana kulingana na hali ilivyo kumteua Jaji wa Mahakama Kuu kulingana na ushauri wa Jaji Mkuu kuchunguza malalamiko na kutoa ushauri.

Kama ushauri na mapendekezo vitaonyesha kuwa Halmashauri ya Kijiji haiwajibiki ipasavyo Kamati inaweza kupendekeza kwa Waziri kwamba usimamizi wa ardhi ya Kijiji husika uhamishwe kutoka mamlaka ya Halmashauri ya kijiji kwa muda muafaka na kukabidhiwa kwa

i. Halmashauri ya Wilaya yenye mamlaka juu ya Halmashauri hiyo ya kijiji au

ii. Kamishna.

Riwaya

Na Emmanuel Boniface

Sasa akili yangu ilirudi nyuma kwa takribani miaka kumi na mbili iliyopita. Ni wakati nilipokuwa ninasoma katika shule ya sekondari ya Mwembeni mjini Musoma. .. Endelea

Ni hapo nilipokutana kwa mara yakwanza na Massa; nikampenda, lakini penzi langu na Massa lilikuja kufa na kuniacha na majeraha yenye uchungu mkubwa moyoni. Yalikuwa majeraha yaliyonifanya nisiwe na haja tena hata ya kuonana na mwanamke yeyote.

Kwa muda mrefu, nilijikuta bila kutazamia, nimejitenga nao na kuzamisha nguvu na akili yangu katika biashara na masuala mengine ya kutafuta pesa.

Niilifanikiwa sana katika biashara zangu na hata nikawa tajiri mkubwa.

Lakini hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, nilijihisi sina raha; nina kosa kitu.

Huo, ulikuwa wakati nilipomwona Caroline.

Caroline alikuwa mwanamke mwenye uzuri usiokadirika, mchawi wa mapenzi na anayejua kubembeleza, kuliwaza na kuteka hisia za watu.

Nilijikuta nagundua kitu kilichokuwa kinanikosesha raha.

Mke! Hata hivyo nyuma ya uzuri wa Caroline na utamu wa maneno yake kulijificha hila na uharibifu;

xxxxxxxxxxxxxxxxx

Massa, alikuwa binti mzuri wa haja ingawa uzuri wake kwa kusema kweli, haukaribii ule wa Caroline hata kidogo!

Alikuwa mfupi wa wastani, mnene kidogo, ngozi nyororo yenye weusi wa kung’aa, macho malegevu na maangavu, midomo minene yenye tabasamu pevu.

Akitabasamu au kucheka vishimo vidogo hujiumba mashavuni mwake.

Kwa kifupi, alikamilika kila idara isipokuwa miguu yake ilikuwa na matege kidogo.

Kwa haiba, alikuwa mtulivu mwenye maneno machache yaliyopimwa kwenye mizani barabara, sauti laini na maridadi katika mavazi na mapambo.

Kwa akili ya darasani, hakuwa zaidi ya kawaida.

Hali hiyo ilimfanya

mara kadhaa, aje kwangu kuomba msaada kitaaluma.

Wakati huo mimi Zitto niliyekuwa ‘kijogoo’ wa darasa wenyewe wakiniita "jiniasi".

Tangia tukiwa katika Kidato cha Kwanza, moyo wangu ulitokea kumpenda sana Massa lakini kwa sababu nilikuwa na aibu na hofu kwamba mimi nilikuwa mtoto wa maskini, niliona ilikuwa ni jambo lisilowezekana kumnasa msichana mlimbwende kama Massa.

Aibu hiyo ilikuwa na mizizi mirefu. Nasema hivyo kwani mpaka wakati huo nilikuwa bado "Msafi" na mazoea ya kuwa karibu kuliko mipaka ya kawaida na msichana, ilikuwa ni changamoto kubwa kwangu.

Hii pia ilitokana na ukweli kuwa, nilikuwa sijiamini sana katika kuzungumza na wasichana.

Nikiwa peke yangu nilipanga maneno fulani fulani jinsi ya "kumtokea" msichana fulani niliyetokea kumhusudu lakini, kila nilipokutana naye, yote yananitoka.

Kwa hiyo, hata Massa japo nilimpenda sana, iliniwia vigumu kumtokea. Hali hiyo iliufanya uhusiano wangu na wake uendelee kuwa wa kawaida; ubaki kuwa ni urafiki wa kaka na dada.

Nilikuwa nikimsaidia katika masomo huku hata utani tuliotaniana, ukiwa ni utani wa kawaida tu.

Hata hivyo, walikuwepo wasichana wengine wawili waliotokea kunitaka sana kimapenzi lakini hao, sikuwatilia maanani hata kidogo.

mmoja wao aliitwa Rozi na mwingine Dotto.

Walipenda sana kunipa kampani na kujichekeshachekesha kwangu. Hata hivyo, tulipofika kidato cha pili, Dotto aliacha shule. Hatukujua ni kwa sababu gani.

Hadi tunafika kidato cha pili, wavulana wengi walikuwa wamemsarandia sana Massa.

walitumia njia nyingi zikiwamo pesa na vizawadi vya kila aina na bado wasiambulie lolote.

Hali hiyo ilizidi kuimarisha hofu na mashaka yangu kuwa nisingeweza kamwe kumtia Massa katika miliki yangu.

Massa alikuwa msichana shupavu asiyeingilika kwa vyovyote iwavyo; kwa hiyo nikazidi kuumia moyoni.

Sasa nikawa nimeanza kupevuka taratibu. Aibu zikanibanduka; nikijiamini na kuongea na msichana bila tabu kubwa, na wasichana wakazidi kunizoea na kunizengea kwa wingi.

Tamaa mbaya zikaniumuka; tamaa fulani yenye kutaka kuridhishwa na kupoozwa ikanikaa tele mwilini; kwanza nikajaribu kuipuuza nikijifanya kama vile haipo.

Pengine Rozi alitambua haja na uzito ulionikabili au kwa nasibu tu siku moja tukitoka shuleni kumwagilia bustani ya mboga akaniambia

"Zitto, leo nataka twende kwenu" "Hakuna taabu, karibu sana," nikamjibu kisha tukaendelea kutembea.

Kimya kilitanda baina yetu; hewa kati yetu ikiwa imepaliwa na harufu yenye hisia nzito zisizo na fasiri.

Tayari jua lilikuwa limezama na giza lilikuwa linatisha kuumeza mji wa Musoma.

Mara Rozi alisita kutembea na kuniita "Zitto!" "Unasemaje Rozi?"

"Kuna kitu nataka kukuambia," sauti yake ilikuwa ni yenye kitetemeshi.

Macho yake yaling’aa katika kiza kile; nilihisi kwamba alikuwa analengwalengwana machozi.

Nilimsogelea na kumshika begani "Niambie tu Rozi, ni kitu gani?"

"Nakupenda Zitto. Nakupenda sana sijui kwanini!" Alisema kwa sauti yenye kubembeleza karibu na hata kukaribia kulia.

Sauti iliashiria ana tashwishwi na ni mwenye wasiwasi mwingi.

Kwa hakika, hapo kabla nilikuwa sijawahi kumpenda msichana yeyote zaidi ya Massa. Nilijikuta katika mtahani mgumu pale Rozi aliponitamkia maneno hayo. Sasa sikuwa na hakika kama nilikuwa nampenda Rozi au la !

Lakini, kwa upande mwingine ndani kabisa ya moyo wangu, nilihisi mguso wa huruma na fukuto la mahaba.

Neno "nakupenda" liliendelea kuelea ubongoni mwangu na kuniletea rajua yenye kusisimua na kupumbaza.

Nilihisi kupoteza uhimili na udhibiti wa hisia na utashi; kwa sekunde kadhaa nilitembea katika dunia nisiyoijua bila hata ya kusogeza mguu;

"Zitto; niambie unanipenda kweli," Rozi alinigutua kwa sauti yake laini.

"Ndiyo Rozi nakupenda, nakupenda sana," aliniparamia kwa hamu na kunikumbatia kwa nguvu.

Nilifumba macho na kumkumbatia kwa uimara. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuwahi kumkumbatia msichana nilihisi raha; isiyomithilika ingawa nafsi ilinusuta kwa kukiuka maadili ya jamii na imani yangu ya Kanisa.

Alipotosheka alinyanyua macho yake na kunitazama sawia usoni huku akitabasamu huku vitone vidonge vya machozi vikimdondoka toka machoni.

Nami nilitabasamu nikamwinamia na kukutanisha midomo yake na yangu. Giza lilikuwa limefunika na kutasitiri.

Twende hatimaye nilimwambia tulihitaji mahali penye faragha na usalama zaidi.

Hatukwenda nyumbani kama tulivyokuwa tumepanga badala yake tulienda kwa rafiki yangu. Itaendelea toleo lijalo