Make your own free website on Tripod.com

Ijue Afya yako

Maelezo kwa Akina Mama na Wakunga (10)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini

Tiba:

Iwapo jipu limekwisha tokea

- Endelea kunyonyesha au likamue ziwa hilo wakati wowote linapokuwa haliumi sana.

- Likande na maji ya baridi ili kupunguza maumivu na pia tumia vidonge vya aspirini.

- Tumia dawa inayoua vijidudu kama ulivyoagizwa katika ‘homa baada ya kujifungua’

Aina mbalimbali za uvimbe katika ziwa

Mzazi ambaye ana uvimbe katika ziwa ambalo lina joto na maumivu linaweza kuwa ni jipu iwapo haliumi inaweza kuwa ni kansa.

Kansa ya Ziwa

Kansa ya ziwa ni ugonjwa mbaya sana ambao huwatokea baadhi ya wanawake, kama dalili ya kwanza ya kansa ni ikitumbuliwa ni rahisi sana kumponya mgonjwa kwa kumfanyia operesheni.

Dalili za kansa ya ziwa ni:

- Uvimbe hasa katika sehemu ya pembeni ya ziwa au ziwa linaweza kuwa linapoteza umbile lake la kawaida au lina kisehemu kimeingia ndani na mara nyingine lina vishimo vingi vidogovidogo kama vile ganda la chungwa.

- Mara nyingi kuna mitoki mikubwa kwapani lakini haiumi.

- Uvimbe wenyewe unakuwa taratibu.

- Mwanzoni uvimbe huo haumi wala kuwa na joto lakini baadaye huuma sana.

Kujipima ziwa mwenyewe

Kila mwanamke inambidi ajifunze namna ya kujipima ziwa lake mara moja kwa mwezi ili kugundua dalili ya kansa.

-Tazama maziwa yako kwa uangalifu na kuona kama kunatofauti ya umbile na usawa na pia hasa kwa dalili zilizokwishatajwa hapo juu.

- Ukiwa umelala chali juu ya mto mgongoni jaribu kupapasa ziwa kwa vidole vyako na kulitomasa ukianzia penye chuchu na kuendelea mpaka katika kwapa.

- Kamua chuchu na tazama kama linatoa damu au uchafu wowote.

Iwapo kuna kiuvimbe au dalili yoyote ya ajabu nenda ukamwone Daktari. vivimbe vingi sio kansa lakini ni bora kuondoa wasiwasi mapema.

Uvimbe katika kinena

- Uvimbe mkubwa wa kawaida ni ule unaosababishwa na mimba lakini kama ni wa ajabu unaweza kusababishwa na:

- Uvimbe wenye maji ndani katika kokwa ya vijiyai vya mwanamke.

- Mimba iliyotunga nje ya nyumba ya uzazi au Kansa.

Sababu zote hizi tatu huwa hazina maumivu mpaka hapo baadaye na hutibiwa kwa operesheni. Uonapo uvimbe wowote usio wa kawaida tafadhali kamuone daktari.

Kansa ya nyumba ya Uzazi

Kansa ya sehemu za uke mara nyingi hutokea kwa akina mama walio na umri zaidi ya miaka 40. Dalili ya kwanza kuwa ni upungufu wa damu mwilini au kutumia hedhi isiyo ya kawaida na hapo baadaye kujisikia uzito au kuona uvimbe wenye maumivu katika kinena. Kamuone Daktari mara tu unaposhuku una kansa.

Uganga wa kienyeji hautaponyesha chochote.

Mimba zilizotunga nje yakizazi .

Mara nyingine mimba huanza kutunga nje ya nyumba ya uzazi hasa katika mrija wa kupitisha mayai.

Kuharibu Mimba

Kuharibu Mimba hutokea mara nyingi katika miezi mitatu ya kwanza na mara nyingi kitoto chenyewe kimeumbwa vibaya na hii inakuwa ni njia moja wapo ya kuhifadhi tatizo lenyewe.

Wanawake wengi huwa wanaharibu mimba moja au zaidi katika maisha yao.

Mimba ya namna hii haiwezi kudumu muda mrefu na itahitaji matibabu kwa operesheni.

Iwapo unadhani una tatizo la namna hii muone daktari upesi sana kwa sababu unaweza kutokwa damu wakati wowote na ikahatarisha maisha yako.

Mara nyingi hawaelewi kuwa wameharibu mimba ila wanafikiri kuwa hedhi yao imechelewa na inaporudi huwa ya ajabu, ikitota mabonge bonge ya damu.

Katika kuharibu mimba kiini cha mimba (embryo) huwa si kirefu zaidi ya sentimita 1au2

Mwanamke ambaye anatumia sana baada ya kupitisha hedhi yake moja au zaidi huenda ikiwa anaharibu mimba.

Kuharibu mimba ni kama kujifungua mtoto kwani kiumbe pamoja na kondo lake ni lazima vitoke na damu huendelea kutoka mpaka vyote viwili vimetoka kabisa.

Tiba:

Kwa kawaida hakuna matatizo iwapo hakuna damu nyingi itokayo.

Hivyo mama mtoto huyo yambidi apumzike kitandani ili mimba yenyewe itoke kwa kuhudumiwa kama vile utaratibu unavyoelekezwa kwa mjamzito anayejifungua.

Iwapo kuna damu nyingi inayotoka au imeendelea kutoka kwa muda wa siku nyingi:

- Nenda kwa daktari. Operesheni ndogo itahitajika kusafisha nyumba ya uzazi

- Pumzika kitandani mpaka damu hiyo itoweke na uendelee kwa muda siku mbili au tatu baada ya kuharibu mimba.

- Fuata masharti kama yalivyoelekezwa awali jinsi ya kufanya wakati damu inapotoka kwa wingi sana.

- Ikiwa ana homa au dalili za ugonjwa wa kuambukiza jaribu kutibu kama vile ilivyoelekezwa kwa ugonjwa wa homa baada ya kujifungua.

Wazazi na watoto wanaotegemewa kuwa na hali ya hatari baadaye.

Tanabahi kwa wakunga mabwana mganga na yeyote yule anayehusika.

Baadhi ya wanawake huwa wanategemewa kuwa na matatizo wakati wa kujifungua, hali kadhalika baada ya kujifungua watoto wao huzaliwa na uzito pungufu licha ya kuugua. Mara nyingi hawa ni akina mama ambao hawajaolewa, hawana makao maalumu wamekonda, wana umri mdogo, akili zao si timamu au tayari wana watoto ambao ni wanyonge au wana utapiamlo.

Iwapo matatizo kama hayo yataweza kueleweka mapema na watu wenye kuhusika na kujaribu kuchukua hatua ya kikamilifu ya kutoa huduma zipasazo tofauti kubwa inaweza kutokea kwa afya bora ya akinamama hao na watoto wao.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza - Tanzania Bara (7)

KATIKA toleo lililopita, tuliishia juu ya malalamiko. Tuliona zipo ngazi kadhaa za malalamiko zinazoweza kutumika ikiwa ni pamoja na Rais. Endelea na Kitabu hiki kilichoandikwa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA - TANZANIA BARA, ambacho kimesambazwa katika magereza mbalimbali ili kuwafanya wanajamii na wafungwa wenyewe, kuzifahamu haki zao na kujua namna ya kujirudi.

Tofauti na kizuizi mtu aliyehamishwa si lazima akawa mfungwa katika eneo lake jipya la makazi.

Anakuwa huru kufanya lolote analotaka kufanya na kwa kweli kundelea na shughuli zake za kawaida kulingana na ujuzi wake. Masharti wanayopewa ni kuripoti katika mamlaka watakazoagiziwa na kwa muda waliopangiwa.

Mara nyingine uhamisho huwa ni wa kundi kubwa na hivyo kuongeza msongamano jela na mbaya zaidi kundi hilo huwa haieleweki lini wanaweza kusafirishwa Hali hii husababisha matatizo hasa kwa mamlaka ya gereza.

4:4 Kuwekwa ndani kwa kuhisiwa kutenda kosa na polisi.

Hali hii hutokea pale polisi wanapomhisi mtu kuhusika au kutenda kosa fulani baada ya uchunguzi wa awali kuelekea kuthibitisha hivyo.

Kiutaratibu na kisheria polisi hawaruhusiwi kumweka mtu anayedhaniwa kutenda kosa chini ya mamlaka yao kwa muda mrefu. Sheria ya makosa ya jinai (crimanal procedure Act, 1985) inaeleza bayana kuwa polisi hurusiwa kumweka mtuhumiwa kwa muda wa siku moja tu yaani saa 24. Kwa muda huo polisi hutakiwa kufanya maandalizi ya kumpeleka mtuhumiwa mbele ya mahakama ili aweze kuwekewa dhamana kama kesi yake inaruhusu wakati maandalizi ya kusikilizwa kesi yake yanafanyika.

4.5 Wafungwa walio Mahabusu

Takriban 40% ya walio jela ni mahabusu na huwa ni wale ambao wanasubiri kesi zao kusikilizwa na mahakama. Mara nyingi watu hawa ni wale wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa na wengine ni wale watuhumiwa walioshindwa kutoa dhamana iliyotakiwa. Kwa hawa njia pekee na iliyo ya hakika kuwa watafika Mahakamani pindi watapohitajika ni kuwaweka mahabusu chini ya ulinzi wa Magereza.

Kama ilivyo kwa walio kizuizini mahabusu huwa hawafanyishwi kazi na hivyo hawachangii chochote kwa mahitaji yao. Zaidi ya hayo mahabusu hawavai sare za wafungwa, na hili huwa ni tatizo kubwa hasa kwa wale wanaokaa muda mrefu na hawana ndugu wala rafiki wa kuwapatia nguo mara kwa mara.

4.6 Wafungwa waliokwisha hukumiwa

Hawa ni wale ambao wamepitia taratibu zote kulingana na sheria za nchi yaani kupitia hatua ya kukamatwa na polisi kesi zao kusikilizwa Mahakamani na kupatikana ushahidi kuthibitisha kuwa mtuhumiwa ametenda kosa analotuhumiwa. Baada ya hapo gereza ndio hatua inayofuata kumwezesha kutumikia hukumu yake na kwa kawaida hatua hii hutekelezeka pale ambapo jitihada za kukata rufaa kwa kutumia mikondo yote iliyowekwa na sheria zimetumika.

Wafungwa waliohukumiwa ni kama 60% ya wafungwa wote nchini. Kundi hili ndilo linalitumikisha kazi na wanapatiwa huduma kwa kiwango cha kuwawezesha kuishi.

Fikra za zamani kuwa jela ni mahala pa adhabu zinaanza kufifia japo kwa taratibu sana. Sasa watu wananza kupaelewa kama mahala pa mafunzo panapowasaidia wafungwa kubadilika na kuwa raia bora ambao baada ya kifungo wataweza kuchangia maendeleo ya nchi ili kuficha fikra hizo za zamani, jitihada za makusudi za kuelimisha umma zinapaswa kufanyika.

5 Hali halisi ya magereza Tanzania

Magereza kwa ujumla katika Tanzania yanakabiliwa na tatizo kubwa la msongamano, kulingana na taarifa iliyotolewa na Dk. L.S.Mmbaga, Naibu Kamishna wa Magereza (Deputy Commissioner of Prisons) nafasi iliyopo kisheria inaweza kuweka wafungwa 21, 188, lakini hali ilivyo kuna wafungwa zaidi ya 43,000 magerezani kila wakati ambapo ni ongezeko la zaidi ya 100%.

Hata hivyo msongamano magerezani ni mkubwa zaidi kwa magereza ya mijini kuliko yale ya vijijini.

Tuangalie takwimu zifuatazo zinazoonyesha hali ya msongamano magerezani ilivyokuwa tarehe 1.4.1999.

Na. Gereza Idadi ya Idadi ya Asilimia ya

Wafungwa Wafungwa Msongamano

Kisheria Kufikia 1/4/99

1. Kahama 70 424 606

2. Ruanda 400 2025 506

3. Morogoro 90 380 422

4. Keko 340 1154 339

5. Bukoba 360 837 233

Source: Mmbaga L.s (Dk) "Over crowiding in prisons in Tanzania: A Statistical Analysis, "A paper presented at the Seminar on Prisons and Alternative Sentencing as a Human Rights Issue, Arusha 6th - 10th April, 1999.

Takwimu hizo sio kwamba zinabaki hivyo hivyo kila mara kwa mfano kati ya 1960 na 1965 magereza hayakuwa na msongamano kabisa. Takwimu zilizopo zinaonyesha kulikuwa na wafungwa 12,495. Hali ilianza kubadilika katika miaka ya 1970. Mfano kati ya 1975 uwezo wa Magereza ulikuwa nafasi 18,332 wakati wafungwa walikuwa 23,505. Kufikia 1985 wafungwa walikuwa 36,233 wakati nafasi ni 19,433.

Tangu hapo tumekuwa tukitoka katika hali mbaya kuelekea hali mbaya zaidi kwa sababu idadi ya wafungwa imekuwa ikiongezeka bila ongezeko wianifu la mahitaji na nafasi ya kuweweka.

Hatima ya yote ni msongamano mkubwa humo magerezani.

Yafaa sasa tuangalie sababu za msongamano magerezani.

5:1 uchache wa Magereza na kutojengwa mapya.

Ni kwa nadra sana kuona wanasiasa wanfungua rasmi magereza mapya, wakati mambo ni tofauti kwa Mahakama. Pengine kuna usahihi fulani kwa sababu mtekelezaji mkuu wa Sheria ni mahakama na zaidi ya hilo tatizo la uhaba wa fedha kwa Taifa letu ni wazi kwa kila mmoja.

Kwa ujumla kwa miaka mingi sasa ni kiasi kidogo cha fedha hutengwa kwa ajili ya Magereza hasa kwa ujenzi wa Magereza mapya.

Jedwali lifuatalo linatupa taarifa ya Magereza Makongwe Tanzania.

Na. Mkoa Gereza Kundi la Mwaka Uwezo

Gereza lilipojengwa

1. Kigoma Bangwe Gereza la 1914 66

Wilaya

2. Arusha Loliondo " 1922 20

3. Mwanza Ngudu " 1929 48

4. Rukwa K/Sumbawanga " 1929 137

5. Arusha Mbulu " 1935 53

6. Kigoma Kasulu " 1936 105

7. Mara Musoma " 1938 195

8. Mtwara Masasi " 1940 75

9. Mara Tarime " 1942 148

10. Tanga Maweni " 1943 896

11. Mwanza Geita " 1944 147

12. Kilimanjaro Karanga " 1949 840

Source: Law Reform Commission of Tanzania - Report of the Commission on the Congestion in Prisons, Dar-Es-Salaam, Government Printer, 1994, PP. 22-24.

 

5:2 Ongezeko la idadi ya Watu

Idadi ya Watu katika Tanzania inaongezeka kwa kasi kubwa sana. Katika Sensa ya 1978 watu walikuwa 17,512,610 na Sensa ya 1998 idadi ikawa imefikia 23,057,922. Ongezeko hili ni sawa na 2.8% kwa mwaka.

Wakati huo huo kumekuwa na hali ya watu kuhama kutoka vijijini kwenda mijini kutafuta ajira.

Kwa ujumla nafasi za ajira ni chache mno na kukosa ajira ikiwemo isiyo rasmi ama ya binafsi au kuwa na ajira isiyolipa vizuri yote huchangia hali duni kiuchumi na kimaisha kwa ujumla.

Hii yaweza kuwa sababu kubwa ya watu kujihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali.

5.3 Kutungwa kwa Sheria ya kiwango cha chini cha hukumu kwa makosa maalum

Kumekuwa na mitizamo tofauti kati ya Serikali na Mahakama katika suala zima la utoaji wa adhabu kwa wahalifu.

Wakati Mahakama inataka kutenda haki kulingana na Sheria, Serikali kwa upande mwingine inataka kukamilisha malengo yake yakiwemo ya kisiasa na mengineyo haraka iwezekanavyo wakati mwingine bila kujali ufundi wa sheria na mambo mengine muhimu.

Kuwa makini kuijua Biblia(3)

Hapo walichanganyika na wale waliobakia. Mchanganyiko huo ndio watu walioitwa miaka ya baadaye Wasamaria.

Utawala wa Yuda uliendelea kujikokota peke yake hadi mwaka 587Kk. Mwaka huo taifa la Wababeli waliuvamia utawala wa Yuda, wakalibomoa hekalu la Yerusalemu, Wakawachukua watu maarufu uhamishoni Babeli.

Awamu ya pili ilidumu kuanzia mwaka 587 K.K. hadi mwaka 538K.K. Katika kipindi hicho, Ukoo wa Kifalme na Utawala wa Yuda, pamoja na watu wengine maarufu, waliishi uhamishoni huko Babeli. Hao ndio walioendeleza historia ya Taifa la Mungu. Kuanzia kipindi hicho waliitwa mara nyingi Wayahudi japokuwa neno la Israeli lilitumika bado mara moja moja.

Maisha yao kiuchumi hayakuwa mabaya sana lakini walipata pigo kubwa la kiimani.

Walikuwa wamepoteza nchi waliyoahidiwa, hekalu lao tukufu na ukoo wa kifalme haukuwa na madaraka tena.

Baada ya miaka arobaini hivi mambo yakabadilika.

Dola jipya lilikusanya nguvu likawa tishio kwa dola la Wababeli.

Hao wapya walikuwa Waajemi waliowashinda vita Wababeli, wakawaruhusu Wayahudi (Waisraeli) kurudi kwao nchi ya Yuda.

Tukio hili lilifungua awamu ya tatu katika historia ya Taifa la Mungu kuanzia mwaka 538K. K hadi 142K.K.

Katika awamu hiyo ya mwisho, watu wa Yuda walijenga vipya hekalu lao mjini Yerusalemu. wakarejesha utaratibu wa kutolea sadaka. makuhani na wataalamu wa sheria za Musa walikuwa watu muhimu sana katika kipindi hicho.

Hata hivyo kipindi hicho hakikuwa na uhuru kamili kwa Wayahudi. Walitawaliwa kwa mfululizo na Waajemi na Wagiriki. Hali ilikuwa ngumu zaidi wakati wa utawala wa Wagiriki ambao walijaribu kupiga vita dini ya Wayahudi lakini Wayahudi walijaribu kutetea uhuru wa dini yao hadi wakawashinda Wagiriki mnamo mwaka 142KK.

Kuanzia mwaka huo Wayahudi waliweza kujitawala hadi Waroma walipoitwaa nchi ya Yuda mwaka 63KK.

Historia ya Agano la Kale ni historia ya kiimani maana yake waandishi wanaonesha jinsi Mungu alivyoongoza mtiririko wa matukio yaliyowapata Waisraeli.

9. Vitabu 7 vya hekima vyahusu nini?

Wakati huo Manabii walipiga vita imani potovu ya Waisraeli walipoigeukia miungu mingine na kumwacha Mungu wao. makosa mengine yalikuwa haya: kuwakosea haki wanyonge, kutoa rushwa mahakamani, kutegemea nguvu za kijeshi toka mataifa mengine na hivyo kuikaribisha miungu ya mataifa hayo. Manabii wa awamu hiyo walikuwa hawa:Amosi, Hosea, Isaya, Mika, Zefania,Nahumu, Habakuki, Yeremea.

Vitabu vya Hekima vimeandikwa katika mtindo tofauti tofauti.

Dhamira zake ni tofauti pia. kitabu cha Yobu kinasimulia jinsi mtu mcha Mungu alivyopata mateso mengi yaliyotikisa imani yake kwa Mungu lakini aliondolewa mateso yake baada ya kudumu imara katika imani.

Zaburi ni mkusanyiko wa sala mbalimbali zilizoandikwa katika mtindo wa mashairi.

Vitabu vinavyobaki katika kundi hili vimeandikwa kwa kutumia semi fupifupi za kishairi, nyimbo na methali zenye kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali za maisha.

Licha ya kutumia mitindo tofauti tofauti pamoja na mchanganyiko wa mada vitabu vya hekima kimsingi vinatoa nasaha zilizomsaidia mtu katika masula haya: kuhusiana vema na Mungu, kuhusiana vema kati ya mtu na mwenzie, kufanikiwa katika kazi na namna ya kuyachukua mateso. Msingi wa mawaidha hayo yote ni huu: kumcha Mwenyezi mungu ni mwanzo wa maaarifa (Methali 1:7). Maarifa hayo ndiyo humletea mtu ufanisi maishani mwake.

10. Manabii ni nani na vitabu 18 vya Manabii vyahusu nini?

Nabii ni mtu anayeongea kwa niaba ya mwingine, kwa neno jingine ni mjumbe. Manabii ni watu waliojitokeza miongoni mwa Waisraeli na kutoa ujumbe. Walijielewa wenyewe kuwa walitumwa na Mungu kuwaonya Waisraeli walipopotoka katika mambo ya imani na maadili. Nyakati za utovu huo manabii waliwakemea watu walitoa tahadhari, waliwasihi wabadilishe mienendo yao na waliwaahidi msamaha wa Mungu endapo wangetubu. Biblia inawataja Manabii wengi sana. Baadhi yao hutajwa katika vitabu vya historia na mafundisho yao yamehifadhiwa katika vitabu hivyo vya historia. miongoni mwa manabii wa kundi hilo ni Samweli, Nathani, Eliya na Elisha.Manabii wengine walihubiri, na ujumbe wao umehifadhiwa katika vitabu vyenye majina yao. hao walijitokeza kuanzia karne ya 8 KK.

Vitabu 18 vya Manabii vinajumuisha ujumbe uliotolewa katika awamu tatu za historia ya Waisraeli.

Awamu ya kwanza ilianza mnano mwaka 750 KK hadi 587 Kk. Aliyefungua kipindi hicho ni Nabii Amosi.

Awamu ya pili yaani kile kipindi cha uhamisho kati ya mwaka 587 KK hadi 538KK, manabii waliwaeleza watu kwamba taifa lao liliangamizwa kwa sababu ya dhambi zao. Aidha manabii waliwatuliza watu wakisema kwamba Mungu hajawaacha watu wake kabisa, bali amewaadhibu kwa muda mfupi. Manabii waliendelea kusema kuwa baada ya muda Mungu atawasamehe watu wake na kuwarudisha nchini kwao. Waliohubiri kipindi hicho ni nabii Ezekieli na nabii anayeitwa Isaya wa pili ambaye mahubiri yake yamo katika sura ya 40 hadi 55 ya kitabu cha Isaya.

Awamu ya Tatu na ya mwisho ilianza mwaka 538 KK hadi karne ya 2KK. manabii wa awamu hiyo walihimiza ujenzi wa hekalu jipya, wajibu wa kutolea sadaka safi kwa Mungu, wajibu wa kuzingatia ibada kwa makini, kuvumilia mateso katika mazingira ya mchanganyiko na watu wa mataifa mengine na kumwona Mungu kuwa ndiye Bwana wa mataifa yote Manabii wa awamu hiyo walikuwa hawa: Hagai, Zekaria, Isaya (Sura 56-66) Obadia,Malaki,Yoeli, Baruku, Yona na Danieli.

Yaliyomo katika Agano Jipya

11. Sasa tujupatie maarifa juu ya Agano Jipya.

Kuna vitabu vingapi na ni vipi katika Agano Jipya?

Waumini wa makanisa yote ya kikristo Wakatoliki na Waprotestanti - wanavitambua vitabu 27 vya Agano Jipya.

Kama tulivyovigawa vitabu ya Agano la Kale katika makundi manne tunaweza kuvigawa vitabu vya Agano Jipya katika makundi manne pia kama ifuatavyo:

(1). Vitabu 4 vya Injili navyo ni Mathayo, Marko, Luka na Yohane.

(2.) Kitabu kimoja cha Matendo ya Mitume.

(3) Vitabu 21 vya barua za Mitume, navyo ni : Waroma, 1Wakorintho, 2 Wakorintho, Wagalatia, Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, 1Wathesalonike, 2Wathesalonike, 1Timotheo, 2Timotheo, Tito, Filemoni Waebrania, Yakobo,1Petro, 2Petro, 1Yohane, 2Yohane na Yuda.

(4). Kitabu cha Ufunuo.

Baada ya jibu hili tunaweza kuelewa kwa nini kuna tofauti ya idadi ya vitabu vya Biblia kati ya makundi mbalimbali ya waumini.

Waisraeli wanavitambua vitabu 39 tu vya Agano la Kale kwa hoja tulizotoa katika jibu kwa swali la sita.

Waprotestanti wanavitambua pia vitabu 39 vya Agano la Kale pamoja na vitabu 27 vya Agano Jipya, jumla vitabu 66. Wakatoliki wanavitambua vitabu 46 katika Agano la Kale na vitabu 27 vya Agano Jipya jumla vitabu 73.

12. Injili ni nini na vitabu 4 vya injili vinahusu nini?

Neno Injili latokana na neno la Kigiriki ‘euangelion’ tafsiri yake ni habari njema. Ingawa kila kitabu katika Biblia kinatoa habari iliyo njema.

hata hivyo neno Injili lahusu kwa namna ya pekee vitabu vinne vya kwanza katika Agano jipya.

Je Wakatoliki wanaelewa imani yao kwa kina?

Na Francis W. Rutaiwa, Ph.D

WAPO baadhi ya Wakatoliki ambao hata kama wanaelewa angalau misingi ya imani yao inawezekana hawajawahi kuongeza kina cha kuelewa imani hiyo, licha ya ibada nyingi tu. Hivyo wakikabiliwa na swali dogo tu, wanababaika hata kushindwa kutetea imani yao.

Nakala hii imetayarishwa kimsingi kwakutegemea "Katekisimu ya Kanisa Katoliki", yenye mpangilio wa mambo makuu katika ufafanuzi wa mafundisho ya imani, kuchochea Wakristo kufanyika wanafunzi waaminifu zaidi wa Yesu. Tunaanza na hatua hii ya kusaidia kuongeza kina cha kuelewa imani kwa manufaa ya waamini wote Wakristo.

"YESU KRISTO, MWANA WA MUNGU".

Nakala iliyotangulia tulijadiri kwamba "Yesu ni Mungu Kweli na Mtu Kweli". Mada ya leo inahusiana na imani hii katika umuhimu wa kuungama Injili ya Kristo.

Wakatoliki tunasadiki na kuungama kwamba Yesu wa Nazareti ni mwana wa milele wa Mungu aliyefanyika mwanadamu ambaye "alitoka kwa Mungu" (Yoh 13:3).

"Alishuka toka mbinguni" (Yoh 3:13;6:33) "amekuja katika mwili" (Yoh 4:2). Kwa kweli "Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba ... amejaa neema na kweli" "Kwa kuwa katika ukamilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema" (Yoh 1:14,16).

Tunasadiki, na kumwungama Yesu Kristo, tukisukumwa na neema ya Roho Mtakatifu na kuvutwa na Baba: "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai" (Mt. 16:6). Kristo amelijenga kanisa lake juu ya mwamba wa imani hii iliyoungamwa na Mtakatifu Petro (Rej. Mt 16:18).

Kuendeleza imani ya Kikristo kwanza ni kumtangaza Yesu Kristo, ili kuwaongoza wengine wamwamini. Tangu mwanzo, wakristo wa kwanza walikuwa moto moto kumtangaza Kristo: "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasadiki" (Rej. Mdo 4:20;1Yoh 1:1-4).

Katika kufundisha imani tunayoungama, kanisa halichoki kutafuta kujua maana ya matendo na maneno ya Kristo na ishara alizozifanya.Kusudi ni kuwaweka watu katika ushirika na Yesu:

Yesu peke yake anaweza kutuingiza katika mapendo ya Baba ndani ya Roho Mtakatifu na kutufanya tushiriki uzima wa Utatu Mtakatifu. (Katekisimu para 426).

Ndani ya Kanisa ni Kristo peke yake anayefundisha; mwingine yeyote anafanya hivyo kama msemaji wake kupitia nyayo za Yesu mwenyewe (Rej. Yoh 7:16).

Yule ambaye ameitwa kumfundisha Kristo hana budi akubali kupoteza kila kitu, ili ampate Kristo ,na yeye mwenyewe awe ndani yake, akifananishwa na kufa kwake ili apate kwa njia yoyote kuifikia kiyama ya wafu (Flp 3:8-11).

Kutokana na elimu hii ya upendo wa Kristo, inazaliwa tamaa ya kutangaza "Kueneza injili", na hapo muumini anataka watu wote waokoke, na wajue yaliyo kweli (1Tim 2:4,Yoh 14:6).

"YESU", kwa Kiebrania maana yake ni " Mungu anaokoa", ni jina ambalo kwa upande mmoja linaeleza nafsi yake na kwa upande mwingine Utume wake (LK1:31). Kwa vile Mungu peke yake anaweza kuondolea dhambi ni yeye katika Yesu Mwanawe wa milele aliyefanyika Mtu "atakayewaokoa watu wake na dhambi zao’ (Mt 1:21;2:7).Hivyo katika Yesu kwa faida ya wanadamu Mungu anajumlisha historia yote.

Kwa kuwa dhambi ni kumkosea Mungu peke yake anaweza kuifuata. (Zab 51:10-11). Israel hataendelea kutafuta wokovu isipokuwa kwa kuliita jina la Mungu Mkombozi (Rej Zab 79:9).

Jina la "Yesu" lina maana kwamba jina lenyewe la Mungu limo katika nafsi ya Mwanawe aliyefanyika Mtu kwa ajili ya ukombozi halisi wa dhambi zao" (Mt 1:21;2:7).

Kwa kuwa dhambi ni kumkosea Mungu, Mungu peke yake anaweza kuifuta (Zab 51:10-11). Israel hataendelea kutafuta wokovu isipokuwa kwa kuliita jina la Mungu Mkombozi (Rej Zab 79:9).

Jina la "Yesu" lina maana kwamba jina lenyewe la Mungu limo katika nafasi ya Mwanawe aliyefanyika Mtu kwa ajili ya Ukombozi halisi wa dhambi za wote. Ni jina la Mungu ambalo peke yake linaleta wokovu, na linaweza kutajwa karibu na wote kwa sababu kwa njia ya Umwilisho umeunganika na watu wote (Yoh 3:18; Mdo 2:21;5:41;3 Yoh7;Rum 10:6-7), hivi kwamba "hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu lutupasalo sisi kuokolewa nalo’ (Mdo 4:12; Rej9:14; Yak 2:7).

Mtakatifu Paulo anaposema juu ya Yesu kwamba "Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake", anataka kusema kwamba katika ubinadamu wake "Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake" (Rom 3:25; 2Kor5:19).

Ufufuko wa Yesu unalitukuza jina la Mungu Mwokozi kwa sababu ni jina la Yesu linalodhihirisha kwa utimilifu uwezo mkuu wa "Jina lile lipitalo kila jina" (Flp 2:9-10; Yoh 12:28). Pepo wabaya wanaliogopa jina lake, na ni kwa jina lake wafuasi wake Yesu wanafanya miujiza. Kwa kweli chochote wamwombapo Baba kwa jina lake anawapa. (Rej Mod 16:16-18; 19:13-16; Mk 16:17; Yoh15 :16).

Jina la Yesu ni kitovu cha sala ya kikristo sala zote za liturujia huhitimishwa kwa maneno "Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo".

"KRISTO" ni tafsiri ya neno la Kigiriki "Kristos" nalo ni tafsiri ya neno la Kiaramayo "Messiah" maana yake "Mpakwa". Masiha ilitakiwa apakwe mafuta na Roho wa Bwana kwa moja kama Mfalme na Kuhani, na pia kama nabii. (Isa 11:2;61:1;Zek 4:14;6:13;Lk4:16-21).

Yesu ametekeleza matumaini ya kimasiha ya Israeli katika kazi zake tatu za kuhani ,nabii na mfalme. Malaika aliwatangazia kuzaliwa kwa Yesu, kama Masiha waliyeahidiwa Waisraeli: "Leo katika Mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana" (Lk 2:11).

Tangu mwanzo yeye ni " yule ambaye Bwana alimtakasa na kumtuma ulimwenguni" aliyetungwa mimba kwa "Mtakatifu" katika tumbo la Bikira Maria. (Yoh 10:36, Rej. Lk 1:35).

Yosefu aliitwa na Mungu "umchukue Maria mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu" ili Yesu aitwaye Kristo azaliwe na mchumba wa Yosefu katika ukoo wa kimasiha wa Daudi (Mt 1:20; Rej Mt. 1:16; Rom 1: 2, Tim 2:8; Ufu 22:16).

Huu ulikuwa uchumba maalumu wa kujitolea kwa Mungu bila nia ya kubatilisha ubikira wa Maria na inaelekea wa Yosefu pia. Vinginevyo Maria asingalitamka pingamizi la kumjua mume ili kuzaa mtoto kama ndoa iliyotarajiwa na Yosefu iliimanisha kungekuwepo tendo la ndoa pia. (Lk 1:34). Kanisa Katoliki linasadiki Maria ni daima bikira.

Kuwekwa wakfu kwa Yesu kama masiha kunafunua utume wake wa kimungu. "Kila kinachomaanishwa na jina lake lenyewe, kinadhihirika kwa sababu katika jina la Kristo anatajwa yule aliyempaka mafuta, yule aliyempaka na mpako wenyewe ambao kwao amepakwa nao: Aliyempaka mafuta ni Baba, Yule aliyepakwa ni Mwana na mpako wenyewe ambao kwao amepakwa ni Roho Mtakatifu. " (Katekisimu Para 438).

Wakfu wake wa kimasiha ulio wa milele umefunuliwa wakati wa uhai wake hapa duniani pale alipobatizwa na Yohani wakati Mungu ‘alipomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu", Ili adhihirishwe katika Israeli (Mdo 10:35;Yoh 1:31) kama Masiha wake. Kazi zake na maneno yake yatamfunua kama "Mtakatifu wa Mungu" (Mk 1:24; Yoh6:69; Mdo 3:14).

Yesu alilipokea jina la Masiha ambalo lilikuwa haki yake lakini siyo bila tahadhari Fulani, kwa sababu baadhi ya watu walioishi wakati ule walimwelewa masiha kibinadamu mno na hasa kisiasa (Yoh.4:25-26,6:15;11:27; Mt.22:41;Lk. 24:21).

Yesu alipokea ungamo la imani la Petro aliyemkiri kuwa ni masiha kwa kutangaza mateso ya Mwana wa mtu yaliyokuwa yamekaribia (Rej. Mt. 16:16-23). Alifunua maana halisi ya utawala wake wa kimaisha upande mmoja uthibitisho wa juu wa Mwana wa mtu aliyeshuka toka mbinguni na upande mwingine katika utume wa ukombozi kama mtumishi anayeteswa:

"Mwana wa Adamu asiyekuja kutumikiwa bali kumtumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi (Yoh 3.13; Mt. 20: 28; Yoh 6:62; Dn 7:13;Isa 53:10 -12).

Kwa sababu hiyo maana ya utawala wake itaonekana wazi tu atakapoinuliwa msalabani (Rej Yoh 19:19 -22; Lk 23:39- 43). Baada tu ya Ufufuko wake utawala wake wa kimaisha utaweza kutangazwa na Petro mbele ya Taifa la Mungu: "Basi nyumba yote ya Israel na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo" (Mdo 2:36).

Katika maandiko Matakatifu ‘MWANA WA MUNGU’ ni jina lililomaanisha kufanywa wana kunakoanzisha uhusiano wenye undani wa pekee kati ya Mungu na kiumbe chake (Mfalme - Masiha aliyeahidiwa alipoitwa " Mwana wa Mungu" si lazima imaanishe neno kwa neno kwamba yeye alikuwa zaidi ya binadamu. Wale waliomtaja Yesu hivyo kama Masiha wa Israel huenda hawakunuia kusema zaidi ya haya (Rej 1 Nya 17:13; Zab 2:7; Mt 27:54; Lk 23:47).

Hii siyo sawa na vile Petro alivyomwungama Yesu kama ‘Kristo Mwana wa Mungu aliye hai" kwani Yesu anamjibu rasmi kuwa " mwili na damu havikukufunulia hili bali baba yangu aliye mbinguni’ (Mt. 16:16).

Sawa sawa Paulo, kuhusu uongofu wake katika barabara ya Damesko, atasema: " Yeye aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kunidhihirishia Mwanawe ndani yangu ili niwahubiri mataifa..." (Gal 1:15-16). "Mara akamhubiri Yesu katika Masinagogi kwamba yeye ni Mwana wa Mungu (Mdo 9:20).

Toka mwanzo hiki kitakuwa ndicho kitovu cha imani ya kitume iliyoungamwa kabla ya wote na Petro ambaye ndiye msingi wa Kanisa (Rej 1Thes 1:10;Yoh20:31; Mt 16:18).

Makala ya Jamii

Modeko - Parokia inayotekeleza kwa uhodari ujumbe wa Sinodi ya Afrika

lUtoto Mtakatifu - mfumo bora wa kuigwa

Na John P. Mbonde, Morogoro

SI kitu kigeni katika masikio ya waliowengi kusikia Shirika la Utoto Mtakatifu ambalo kwa jina lililozoelekea na walio wengi ni Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu.

SISTA Marihut Mosguera T.C (Shirika la Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu) chini ya uongozi wa paroko wa Parokia ya Santa Maria Modeko jimboni Morogoro

,Padre Avodius Shao C.S.Sp wamehamasisha kwa nadharia na vitendo wajibu wa watoto wadogo wa kati ya miaka minne na kuminambili kuwa mstari wa mbele katika kazi ya umisionari.

Viongozi hao wa kiroho katika parokia hiyo wanasema kuwa ,watoto wengi katika parokia yao wamehamasishwa sana na shirika hili la Utoto Mtakatifu kutokana na kuvutiwa kwao na mbinu mbalimbali za utekelezaji wa ujumbe wao wa kimisionari.

Wanasema kilichowafurahisha zaidi ni mbinu mbalimbali zinazotumika kufikisha ujumbe huo kwa kupitia michezo mbalimbali ikiwemo ngoma, gwaride na sare nzuri za rangi ya bendera ya Vatikano ambayo ni njano na nyeupe.

Ujumbe wanaoutoa kwa kupitia maonyesho ya sanaa huwaingia haraka sana watoto wenzao.

Kwa kutumia vitu hivyo,watoto wadogo wanakuwa wepesi sana kuzijua sala ,umuhimu wa matendo mema kwa wahitaji na mafundisho na kuwa tayari kufikisha ujumbe wa injili hata kwa wenzao wadogo kwa wakubwa.

Hao ni watekelezaji hodari wa Sinodi ya Afrika.

"Sinodi ilitoa ombi kwa kila familia ya kiafrika ya Kikristo kuwa mahali pema pa uenezaji wa Injili na ushahidi’ wa "Kanisa la kweli la kinyumbani" Jumuiya inayoamini na kueneza injili. Kwa maneno mengine suala la umisionari halina budi kuanza katika ngazi ya familia kwa watoto wakiwa wangali wachanga ili waweze kukua, kulelewa na kuimarishwa katika mazingira ya kumhubiri Kristo.

Wakati wa ziara yake Papa Yohane Paulo wa II hapa nchini Tanzania mwaka 1990 alisisitiza ukweli kwamba familia ni kikanisa kidogo yaani wazazi huwa ni mfano katika kauli na matendo yao wakiwa pia ni walinzi wa imani kwa upande wa watoto wao.

Utoto Mtakatifu katika parokia ya Mtakatifu Maria Modeko ni watekelezaji hodari wa ujumbe wa sinodi ya Afrika kwa misaada ya maongozi ya Mungu mwenyewe kwa kupitia uongozi wa Sista Marihut T.C na paroko wake Evodius Shao, C.S Sp.

Kanisa katika Afrika linajua kwamba vijana sio tu wa sasa bali juu ya yote ndiyo jamii ya baadaye. Kwa hiyo ni muhimu kuwasaidia vijana kushinda vizuizi vinavyopinga maendeleo yao kutojua kusoma na kuandika, uzembe, njaa, madawa ya kulevya.

Ili kutimiza barabara changamoto hizi vijana wenyewe kwa wenyewe lazima wahimizane, na wapatiwe kila aina ya msaada uwawezeshao kuwa waenezaji hodari wa injili kwa wenzao. Hakuna yeyote awezaye kufanya hivi vema ila wao.

Uchungaji wa vijana lazima uwe sehemu ya utaratibu wa uchungaji wa majimbo na maparokia, ili kwamba vijana wawezeshwe kugundua mapema thamaniya kipaji cha mtu binafsi, njia bora ya kuufikia upevu.

Wahamasishaji mahiri katika Uinjilishaji.

Kila parokia iwajibike kuwajengea watoto mazingira ambayo yatawawezesha kuwatendea wenzao matendo ya huruma: kuwatembelea watoto wagonjwa na kwenye mahabusu ili kuwafariji; kuwapatia misaada mbalimbali ya hali na mali watoto wenye kuteseka kwa vile ni yatima au waliotengwa na wazazi wao kwa sababu ya vita na maafa mengine n.k kwa njia ya nyimbo watoto wa Utoto Mtakatifu wa Parokia ya Modeko wamejidhihirisha kuwa ni wahamishaji mahiri katika uinjilishaji. Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kutekelezeka mradi tu yanaandaliwa muda muafaka kwa malezi na makuzi ya watoto wa parokia za mjini na vijijini.

Ni changamoto kwa Wabatizwa wote kuwa Wamisionari.

"Kwa sasa, ninyi Waafrika ni wamisionari kwenu ninyi kwa ninyi" maneno ya Baba Mtakatifu Paulo VI katika ufunguzi wa ukumbi wa SECAM huko Kampala,Uganda Julai 31,1969.

Tamko hili linatoa mwaliko kwa kila mbatizwa kuutambua na kuutekeleza wajibu wake wa kuushuhudia na kuuishi utume wa Kristo kwa sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara wakristo wote wameitwa kushiriki katika umisionari wa Kanisa.

Kwa maneno mengine Utoto Mtakatifu unatoa changamoto kwa kila mbatizwa kuihubiri injili kwa kauli na matendo. Hata katika maisha ya kila siku .Wahenga hutukumbusha kwa msemo Samaki mkunje angali mbichi, ukiwa na maana kuwa hapana budi kuwalea watoto kuwa wawajibikaji katika kuihubiri injili tangu wakiwa wadogo. Kwa jinsi hiyo wazazi wana wajibu wa kuwaandaa watoto wao kuutambua wajibu wa wabatizwa wote kuwa wamisionari.

Utoto Mtakatifu hutoa pia fursa nzuri ya kuwa kila mtoto kugundua mustakabali wake katika miito mitakatifu. baada ya miaka 2000 ya Ukristo na Umisionari duniani, hatuna budi kuitika na kukubali "Mimi hapa Bwana. Unitume mimi Bwana!" Sisi sote tumeitwa na kutumwa kuwa wamisionari kutokana na sakramenti za ubatizo na Kipaimara.

Lijue Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing

KATIKA matoleo yalipopita tulisoma jinsi wamisionari hao walivyofika Zanzibar na Masista wanne walibaki kwa muda huko Zanzibar ambapo Padri na mabruda waliendelea na safari hadi Pugu wakaweka makao yao. Sasa endelea...

Wamisionari huko Pugu walifuata mfano wa mapadre wa Bagamoyo na kuwakomboa watumwa na kuwalea katika shule ya Misioni. Mtoto wa kwanza aliletwa hapo Mei Mosi 1888. Mtoto huyo alikabidhiwa kwa Masista nao wakamfundisha dini akabatizwa akaitwa jina la Andrea.

Huyu alikuwa Mkristo Mkatoliki wa kwanza katika eneo hilo.

Padre Bonifas aliwakomboa watoto wengi watumwa na kuwakabidhi kwa Masista wawalee na kuwafundisha maarifa na dini. Serikali kila mara ilipokamata meli ya Waarabu yenye watoto watumwa, iliwapeleka watoto hao huko Pugu. Kwa nafasi moja moja jamaa walioshindwa kulea watoto wao walipelekwa huko Pugu kulelewa. Huko zilijengwa nyumba kubwa kwa ajili ya watoto hao.

Pugu inavamiwa.

Serikali ya Uingereza ilikuwa imekataza biashara ya utumwa. Wajerumani waliokuwa wameshika nchi hii walijitahidi sana kuona biashara ya utumwa inakomeshwa. Hivi kila walipoona Waarabu wamewakamata watumwa waliwanyang’anya watumwa hao na kuwaacha huru. Kule kukatisha na kupiga marufuku biashara hii kuliwaudhi sana Waarabu na wote waliokuwa wakishughulikia biashara hiyo kwani ilikuwa ni kuharibu uchumi wao. Hivyo walijenga hali ya chuki dhidi ya shirika la DOAG na dhidi ya watu weupe kwa ujumla.

Watu walikusanyika wakamtema Bushiri Bin Salum kuwa mkubwa wa jeshi lao na hapo hapo wakaanza vita. Kwa muda wa miezi miwili hivi Pugu ilikuwa katika utulivu. Baada ya sikukuu ya Noeli Padri Bonifas aliamua kwenda Zanzibar ili kutafuta mahitaji kwa ajili jumuiya yake, akiwa njiani padri Bonifas akashikwa na homa kali sana akalazwa hospitalini.

Huko nyuma hali ya Pugu ilitisha sana watawa walisali novena ya siku tisa.Januari 10 asubuhi mwaka 1889 toka saa moja walisikia kishindo cha bomu kutoka huko Dar es Salaam. Wananchi walianza kuhangaika wakikimbilia misituni huko wakilia vita! Vita vinakuja. Siku ya pili na yatatu mambo yakionekana kutulia. Lakini siku ya nne yaani Januari 13 vita ilipamba moto .Baada ya chakula watawa walijipanga kwenda kanisani kusali. Kiongozi wao alianza zaburi "Unihurumie Ee Mungu...." Mara kishindo cha bunduki kikasikika kutoka kwenye kichaka na moja ya risasi ilimwangukia Bruda Perto Kifuani akafa pale pale. Katika muda wa nukta chache watu zaidi ya 150 waliwazunguka Wamisionari hao kote kote wakipiga risasi toka pande zote. Bruda Benedikti alikimbia kuelekea kanisani ili kuhifadhi Ekaristi Takatifu. Naye akapigwa risasi mbele ya tabernaklo. Kutoka nyumba ya masista iliyokuwa ng’ambo ya kanisa, Sr. Marta akikimbia pamoja na mtoto mkononi akaingia kanisani naye akauawa pamoja na mtoto. Namba ya washambuliaji iliongezeka waliingia nyumba ya masista wakamtoa Sista Benedikta aliyekuwa mgonjwa kitandani wakamleta nje ili kumpiga risasi. Lakini mkubwa wa kikosi alimzuia Sista huyo asipigwe risasi.

Wawili wanakimbia:

Katika mahangaiko hayo mabruda wawili waliruka kupitia dirashani wakapitia mstari wa maadui wakaelekea bustani ya migomba.

Bruda mmoja alipigwa risasi moja kwenye bega la kuume. Lakini risasi ilikamatwa na kanzu yake kwa kuwa kanzu yake ilikuwa nene kidogo. Adui zao wakawafukuza kwa kitambo kisha wakawaacha. Wao wakaendelea kukimbia kuelekea Kaskazini Magharibi hadi Dar es Salaam wakiwa njiani watu wema waliowatambua kuwa walikuwa wamisonari waliwapa chakula. Huko Dar Es Salaam walikutana na maofisa wa Kijerumani ambao waliwasaidia kuwasafirisha hadi Zanzibar kupitia Bagamoyo. Walifika huko Zanzibar siku ya nane baada ya uvamizi wa nyumba yao huko Pugu.

Washikiliwa mateka:

Wavamizi waliwakamata Sista Benedikta na Mabruda watatu kama mateka. Pamoja nao walikamatwa wasichana na wavulana waliokuwa wakilelewa hapo Pugu. Mabruda walifungwa minyororo shingoni na kufunguliwa pamoja wakiwa chini ya ulinzi. Sista Benedikta aliachwa kutembea bila kufungwa mnyororo. Walitembea kwa miguu hadi Kunduchi. Safari yao iliwachukua siku tatu. Walipofika huko Kunduchi mabruda walifunguliwa minyororo. Hapo mabruda ,sista pamoja na watoto waliotanguzana nao walifungiwa katika chumba kimoja mara kwa mara waarabu waliingia chumbani humo kuwahesabu mahabusu hao. Kila walipohesabiwa walihofu sana maana walijua kuwa wakati wowote ule wangeuzwa kwa wafanyabiashara wa biashara ya watumwa.....................

Wakati huo huo Padri Etienne Baur alikuwa akiwasiliana na kiongozi wa wavamizi Bw. Bushiri. Alimweleza Bushiri kwamba wamisionari hao walikuwa ‘Mapadri’ kama wale wa Bagamoyo.

Bushiri alijibu kuwa yeye hakujua kuwa Wamisionari hilo hawakuhusiana na Wajerumani ambao walikuwa wakipigana vita nao.

Lakini shauri hio lilikuwa mikononi mwa machifu wengine wadogo. Bushiri mwenyewe aliahidi kutuma ujumbe kwa machifu wadogo hao.

Bomoa bomoa yamsababishia upofu wa maisha

lAiomba serikali impatie matibabu ndani,nje ya nchi

Na Neema Dawson

KITENDO cha serikali kubomoa nyumba za wakazi wa eneo la Ubungo jijini Dar-es-Salaam kwaajili ya kuruhusu upanuzi wa barabara ya Morogoro, kumemsababishia upofu wa maisha mmoja wa watu waliokumbwa na zoezi hilo, Bi. Amina Muhamad (45).

Akielezea hali yake hiyo kwa Mwandishi wa habari hizi, Bi. Amina alisema kuwa ilikuwa ni mwaka 1997 nyumba yake iliyokuwa imejengwa katika eneo la Ubungo Kibo,ilipovunjwa na serikali.

Anasema kutokana na mshtuko walioupata mishipa yake ya fahamu iliathirika hivyo kumsababishia upofu wa macho.

Bi. Amina ambaye ukimwangalia kwa haraka utadhani anaona vizuri kutokana na macho yake yakiwa wazi bila kufumba alisema kuwa pamoja na hali aliyonayo,msaada pekee anaotegemea katika maisha yake ni ule unaotoka kwa watoto wake wa kuzaa.

"Mimi kwetu kabisa ninakozaliwa ni Ankole nchini Uganda na mume wangu ambaye ni Mtanzania alifariki mwaka 1987 ambapo kwa bahati nzuri tulikuwa tumeisha pata watoto saba,nashukuru pamoja na kufiwa na mume wangu lakini watoto wananijali sana "alisema.

Hata hivyo Bi.Amina alisema kuwa pamoja na kwamba watoto wake wakiwemo wasichana sita na mvuala mmoja,kujitahidi kumsaidia bado anahitaji msaada zaidi wa serikali kutafuta uwezekano wa kumpatia matibabu zaidi ndani ya nchi na hata ikiwezekana iwe nje ya nchi.

"Mimi ni mdogo bado,umri wangu wa miaka 45 unaniwezesha kufanyakazi za kilimo na biashara,lakini kutokana na upofu wangu,nashindwa kufanya jambo lolote la maana na pengine nisingekuwa nimezaa,hivi sasa ningekuwa ombaomba wa barabarani"alisema.