Make your own free website on Tripod.com

Ijue Afya yako

Maelezo kwa akina mama wa Wakunga (6)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini

Iwapo miguu ya mtoto itatokeza na wala si mkono basi osha mikono yako vizuri sana, ipake spiriti au vaa maglovu na kisha ingiza mikono yako ndani na sukuma nyuma mabega ya mtoto au gandamiza mikono ya mtoto katika mwili wake.

Kichwa kimekwama, mlaze mama chali, Ingiza kidole chako ndani ya mdomo wa mtoto na gandamiza kichwa katika kifua chake.

Katika muda huo huo awepo msaidizi mwingine ambaye atakisukuma kichwa cha mtoto chini na kugandamiza tumbo la mama.Inambidi mama asukume kwa nguvu chini lakini asiuvute mwili wa mtoto.

Kutanguliza mkono

Iwapo mkono wa mtoto umetokeza kwanza haraka mpeleke hospitali.

Mama anaweza kuhitaji operesheni ili mtoto aweze kutolewa.

Choo ya mtoto mdomoni na puani:

Wakati chupa inapovunjika na umeona maji yana choo cheusi cha kwanza mtoto huyo anaweza kuwa katika hatari.

Mtoto anaweza kufa iwapo choo hicho kitaingia katika mapafu yake mara tu kichwa chake kinapotokeza, mweleze mama asukume tena ila apumue haraka haraka. Mfyonze na kupangusa choo chote puani na mdomoni kabla ya mtoto hajaanza kupumua. Iwapo ameanza kupumua endelea kufyonza na kutoa huo uchafu wote

- Mapacha.

Mara nyingi kujifungua mapacha kunaleta matatizo na hatari kwa mama na watoto kuliko kujifungua mtoto mmoja.

Kwa usalama yambidi mama ajifungulie mapacha wake hospitalini.

Baada ya mwezi wa saba wa ujauzito yambidi mama awepo karibu na hospitali kwa sababu uchungu wa mapacha huanza mapema sana.

Dalili za mama anayeweza kuwa na mapacha

-Tumbo linakuwa haraka na nyumba ya uzazi inakuwa pana kuliko kawaida hasa katika miezi ya mwisho.

-Kama uzito wa mama unaongezeka haraka kuliko kawaida au matatizo ya kawaida ya ujauzito (kutapika alfajiri, kuumwa mgongo, kuvimba mishipa ya vena, kuvimba miguu, n.k) yanazidi kuliko kawaida, hakikisha unatazama kama kuna mapacha.

- Kama unaweza kupapasa vitu vikubwa (vichwa na matako) vitatu au zaidi katika nyumba ya uzazi ambayo ni pana kuliko kawaida ni wazi kuwa kuna mapacha.

- Mara nyingine unaweza kusikia midundo ya moyo katika sehemu mbili tofauti (ukiacha ile ya mama) lakini hii ni ngumu sana.

- Iwapo mama atapumzika vya kutosha na ataepuka kazi ngumu katika miezi ya mwisho ni wazi kuwa hatapata uchungu na mapacha watazaliwa mapema.

- Mara nyingi mapacha wanazaliwa wakiwa na uzito mdogo na wanahitaji matunzo maalumu. Hakuna ukweli wowote kuwa mapacha wana miujiza.

Kupasuka Msamba

Mlango wa uzazi (msamba) unabidi utanuke sana ili mtoto aweze kutoka, mara nyingine huchanika au kupasuka hasa kama ni uzazi wa kwanza wa mama. Kupasuka msamba kunaweza kuzuiwa iwapo kutakuwa na uangalifu.

Inambidi mama asisukume ikiwa kichwa cha mtoto kimeanza kutokeza.

Huku kunawezesha msamba kutanuka. Ili asisukume inambidi mama apumue haraka haraka. Wakati msamba unapotanuka, mkunga anaweza kuupa nguvu kwa mkono mmoja na mwingine ukizuia kichwa kisitoke haraka,namna hii:

Inasaidia pia kukanda kitambaa cha maji ya mtoto katika ngozi iliyopo chini ya msamba mara tu inapoanza kutanuka.

Iwapo msamba utakuwa umepasuka, mtaalamu ambaye anafahamu namna ya kuushona inambidi afanye hivyo mara tu kondo la nyuma likisha toka.

Utunzaji wa watoto wachanga

Kitovu

Ili kuzuia kitovu kipya kisiambukizwe ni lazima kitunzwe na kuwekwa katika hali ya usafi na ukavu. Jinsi kitakavyokuwa katika hali ya ukame, ndivyo uzi utakavyochukua muda mrefu kudondoka na kitovu kupona. Kwa sababu hii ni bora kutokifunga bandeji na kama itatumika hakikisha imelegea.

Macho:

Kuepusha macho ya mtoto yasipate ugonjwa wa hatari, yaweke matone ya silver nitrate 1% au tetracycline eye ointment mara tu anapozaliwa. Hii ni muhimu sana iwapo mmoja wa wazazi alikuwa na dalili ya kisonono.

Namna ya kumpa mtoto joto lakini lisizidi

Mkinge mtoto asipate baridi na wala joto jingi. Mvike au mfunike nguo ambazo hata wewe ungependa zifunike mwili wako.

Wakati wa baridi mfunike mtoto vizuri lakini wakati wa joto au akiwa ana homa mwache uchi

Ili kumfanya mtoto apate joto la kutosha mama yake anaweza kumkumbatia

Usafi

Ni muhimu kufuata kanuni za usafi kama ilivyokwisha elezwa, hasa zingatia yafuatayo

-Mbadilishe nepi au matandiko yake mara anapojikojolea au anapozichafua, ikiwa ngozi inakuwa nyekundu, badilisha nepi mara nyingi zaidi lakini ni bora usimvike chochote.

Baada ya uzi wa kitovu kudondoka,mwogeshe mtoto kila siku ukitumia sabuni ya watoto na maji ya uvuguuvugu.

Kama kuna inzi au mbu inabidi kitanda chake kiwe na chandaruwa au kitambaa chochote kilicho chepesi.

Watu walio na ugonjwa wowote wa kuambukiza kama mafua, mafindofindo, kifua kikuu, n.k wasimshike wala kumjongelea mtoto.

Mlaze mtoto mahala pasafi pasipo na moshi wala vumbi.

Chakula

Maziwa ya mama ni chakula bora sana kwa watoto wachanga.watoto wanaolelewa kwa maziwa ya mama wana afya bora, wana nguvu na hawafi kwa urahisi hii ni kwa sababu:-

- Maziwa ya mama yana kila kitu ambacho mtoto anahitaji kuliko maziwa ya aina nyingine.

- Ni safi mtoto alishwapo vyakula vingine hasa kwa chupa ni muhimu sana kuviweka vyombo atakavyovitumia katika hali ya usafi na kuweza kukinga mtoto asipatwe na magonjwa kama vile kuhara na kutapika.

- Joto la mama ni lile hasa linalohitajika.

- Maziwa ya mama yana vitu (antibodies) vya kukinga mwili wa mtoto mchanga asipatwe na magonjwa ya surua kupooza n.k

- Mama anaweza kumnyonyesha mara tu mtoto akishazaliwa Katika siku chache za mwanzo maziwa yatakayokuwa yanatoka ni ya kiasi tu.

Hili ni jambo la kawaida na hailazimu mumwanzishe maziwa mengine kwa chupa ila itabidi kumnyonyesha mara kwa mara na hii itasaidia maziwa kujaa na kutoka kwa wingi.

- Mama aliye na maziwa mengi itambidi anyonyeshe tu kwa muda wa miezi 4 au 6 na baada ya hapo itambidi aendelee kunyonyesha lakini amwanzishie mtoto aina nyingine ya vyakula vinavyowafaa watoto:

Jinsi mama anavyoweza kutoa maziwa kwa wingi.

- Ni lazima atumie vinywaji kwa wingi.

- Ale vyakula bora hasa maziwa na vyakula vya kujenga mwili.

- Apate usingizi wa kutosha na aepuke uchovu na kuudhika, anyonyeshe mtoto wake mara kwa mara

- Watoto wenye kunyonya maziwa ya chupa huugua mara kwa mara na hufa.

- Watoto wenye kunyonya maziwa ya mama huwa na afya bora.

Uangalifu wakati wa kutoa dawa kwa watoto wachanga

Dawa nyingi huwadhuru watoto wachanga.

Hivyo ni wajibu kutumia zile dawa ambazo una hakika zimependekezwa kwa watoto wachanga na zitumiwe tu ikiwa kuna umuhimu na hakikisha kuwa unatumia kipimo kinachostahili dawa kama chloramphenical ni ya hatari sana kwa watoto wachanga na hasa kama mtoto amezaliwa kabla ya siku zake (njiti) au uzito wake ni haba (chini ya kilo 2).

Magonjwa ya watoto wachanga

Kuna umuhimu wa kutambua haraka tatizo lolote au ugonjwa na kutoa huduma mapema.

Magonjwa yachukuayo siku au majuma kuuma mtu mzima yanaweza kuua mtoto kwa muda wa saa chache.

Matatizo anayozaliwa nayo mtoto.

Matatizo hayo hutokana na kasoro fulani wakati mtoto anapokuwa ndani ya nyumba ya uzazi au hitilafu inaweza kutokea wakati anapozaliwa. kwa hiyo kuna umuhimu wa kumpima mtoto kwa uangalifu sana mara tu anapozaliwa ikiwa ana dalili yoyote kati ya hizi zifuatazo basi labda mtoto ana shida ambayo inahitaji huduma ya haraka.

Kama hapumui mara anapozaliwa

Kama mapigo ya mishipa ya damu au moyo haisikiki au kama mpigo hiyo inasikika lakini inazidi 100 kwa dakika.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza - Tanzania Bara (7)

KATIKA gazeti hili matoleo yaliyopita tuliandika habari juu ya Kitabu kilichoandikwaa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA - TANZANIA BARA, ambacho kimesambazwa katika magereza mbalimbali ili kuwafanya wanajamii na wafungwa wenyewe, kuzifahamu haki zao na kujua namna ya kujirudi.

Tume ikishaundwa na ikabaini kuwa jaji mhusika ana hatia basi Rais anaweza kumwachisha kazi ya ujaji, kwa hiyo kwa yeyote aliye na malalamiko au tuhuma dhidi ya jaji au kiongozi yeyote mwandamizi wa mahakama anaweza kuwasilisha tuhuma hizo mbele ya Rais.

3:2:2 Jaji Mkuu: Kikatiba huyu ndiye Mkuu wa Idara ya Mahakama na Kiongozi wa mahakama ya Rufaa. Kwa sababu hiyo basi jaji Mkuu anawajibika kuhakikisha kwamba mahakama ya Rifaa ya idara ya Mahakama zinafanya kazi kwa utaratibu unaoeleweka na kwa fanisi unahitajika kwa mujinu wa sheria. Kunapokuwa na lalamiko lolote kuhusu Mahakama ya Rufaa ama Idara ya Mahakama lalamiko hilo linaweza kupelekwa kwake kwa ufumbuzi.

3:2:3 Jaji Kiongozi.

Huyu ndiye msaidizi maalumu wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama kuu na Mahakama nyingine zilizo chini ya Mahakama Kuu. Kikatibu yeye ndiye pia Mkuu wa Mahakama Kuu. Hivyo kama kuna mahakama yoyote katika idara ya mahakama ukiondoa Mahakama ya Rufaa malalamiko hayo yanaweza kupelekwa kwa Jaji Kiongozi na yakapatiwa ufumbuzi.

3:2:4 Jaji Mfawidhi wa Kanda:

Pamoja na kwamba Mahakama Kuu ni moja lakini kwa ajili ya ufanisi wa kazi imeawanyika katika Kanda mbalimbali. Kila kanda ina kiongozi wake anayeitwa Jaji Mfawidhi wa kanda ambaye anachaguliwa na Jaji Mkuu kwa Mamlaka aliyopewa na Sheria. Huyu ndiye msaidizi wa Jaji Kiongozi katika utendaji wake wa kazi na kiongozi wa shughuli zote za idara ya Mahakama katika kanda yake isipokuwa Mahakama ya Rufaa.

Hivyo kama kuna malalamiko katika Kanda inayohusika ambayo yako ndani ya uwezo wa Jaji Mfawidhi wa kanda, basi malalamiko hayo yanaweza kupelekwa kwake kwa hatua zinazostahili.

3:2:5 Jaji Mfawidhi na Mahakama Kuu:

kuna sehemu ambapo Mahakama kuu imekuwa na masijala mbili moja kwa ajili ya kanda na nyingine kwa ajili ya eneo kama Dar es Salaam, Arusha n,k katika mazingira haya kumekuwa pia na majaji Wafawidhi wa Mahakama kuukwa ajili ya maeneo hayo na siyo kanda. Mfano masijala ya Dar es Salaam imegawanyika shehemu mbili moja inaitwa Masijala Kuu na nyingine Masijala ya Wilaya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu katika eneo fulani ndiye anayekuwa msadizi wa jaji Mfawidhi wa kanda katika masijala inayohusika na anashughulikia malalamiko na matatizo yatayakayojitokeza katika masijala hiyo.

3:2:6 Wasajili wa mahakama:

Hawa wako katika Mahakama Kuu na wanataraiwa na kudhibitiwa na Rais kwa mujibu wa Katiba.

Hawa kazi zao ni kusiamia Watendaji wa mahakama (makarani na wengineo) na kuhakikisha kwamba shughuli za mahakama zinakwenda kama inavyostahili. Kukiwa na lalamiko dhidi ya karani au ofisa mwingine wa Mahakama basi mtu wa kumjulisha ni msajili ili alishughulikie akishindwa atalipeleka kwa jaji Mfawidi wake kwa hatua zaidi.

3:2:7 Hakimu Mfawidhi:

Sheria ya mahakama za mahakimu ya 1984 inamruhusu Jaji Mkuu kuteua hakimu mfawidhi wa mahakama au hakimu Mkazi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya ufawidhi wa mkoa unaohusika. Pia sheria hiyo inampa Jaji mkuu mamlaka ya kuchagua mahakimu Wafawidhi wa mahakama za Wilaya na Mahakama za mwanzo.

Kwa sasa mahakimu wafawidhi wako katika kila mahakama ya Mahakimu. Hawa ndio viongozi wa mahakama hizo wakisaidiana na viongozi waliokwishatajwa hapo juu.

Kama kuna lalamiko katika mahakama ya Hakimu Mkazi basi lalamiko litakwenda kwa hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo.

Yafaa ieleweke kuwa hatakwa ngazi zilizotajwa hapo juu kama kiongozi ndiye anayelalamikiwa basi lalamiko dhidi yake litakwenda kwa kiongozi aliyeko juu yake, kwa mfano kama anayelalamikiwa ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya basi suala hilo linaweza kupelekwa kwa hakimu Mkazi kwa kadiri ya Sheria ya Mahakama za Mahakimu ya 1984.

3:3Vyombo vingine husika

Baada ya kuangilia ngazi za kiutawala zinazoweza kushughulikia utendaji wa mahakama tuangalie vyombo vingine ambavyo navyo pia vina wajibu huo huo.

(a) Tume ya idara ya Mahakama.

Hii imeundwa kakatiba na inaongozwa na sheria ya Tume ya Ajira ya Mahakama ya 1962. Kazi zakeni kuajiri na kudhibiti nidhamu ya Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama isipokuwa Wasajili wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu ambao masuala yao yamewekwa mikononi mwa Rais kwa mujibu wa Katiba. Tume hii ina uwezo wa kuwaondoa kazini hakimu au mtumishi mwingine wa idara ya mahakama na uwezo huo ni wa kikatiba.

(b) Bodi ya mahakama ya mkoa

Bodi hizi ziko chini ya Tume ya Idara ya Mahakama na zilianzishwa 1964. Majukumu ya bodi hizo ni kushughulikia malalamiko dhidi ya Maafisa wa mahakama zilizomo katika mkoa husika isipokuwa mahakama ya mwanzo.

Wajumbe wanaounda Tume hiyo ni:-

-Mkuu wa Mkoa (Mwenyekiti)

- Hakimu mkazi (Makamu mwenyekiti)

- Hakimu wa Wilaya (Katibu)

(c) Bodi ya mahakama za wilaya

Hizi zilianzishwa 1971 na kazi zake ni kushughulikia masuala yanayohusu ajira na malalamiko dhidi ya mahakimu wa mahakama za mwanzo, wajumbe wake ni:-

- Mkuu wa wilaya

- Afisa wa wilaya (katibu)

- Wajumbe wawili wanaochaguliwa na halmashauri ya Wilaya.

- Hakimu mmoja wa Wilaya.

Bodi hii inapopokea malalamiko dhidi ya hakimu wa mahakama ya mwanzo huanza kufanya uchunguzi ambao unapokamilika taarifa yake hutumwa kwa waziri wa Sheria na mambo ya katiba kwa hatua zaidi.

(d) Makatibu Tawala

Hawa wanaweza kupokeza malalamiko dhidi ya Mahakimu na Watumishi wa mahakama na kuyapeleka kwenye bodi ya mahakama ya mkoa au wilaya kwa ajili ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria.

(e) Mwakilishi wa mwanasheria Mkuu wa Serikali

Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali (Attorney General) inazo ofisi za kanda katika mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza, Dodoma,Mbeya, Tabora na Mtwara. Malalamiko dhidi ya mahakama yanaweza kufikishwa pia katika ofisi hizo kwa ajili ya kufikishwa pia katika ofisi hizo kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi kufuatana na taratibu zilizowekwa.

(f) Polisi/ kikosi cha kuzuia rushwa

Iwapo suala linalolalamikiwa ni rushwa mwananchi anashauriwa kupeleka malalamiko yake katika idara ya polisi au kikosi cha kuzuia Rushwa kwa ufumbuzi.

(g) Tume ya kudumu ya Uchunguzi (Permanent Commission of Enquiry).

Kwa mujibu wa sheria iliyaanzisha Tume ya kudumu ya Uchaguzi, mwananchi yeyote mwenye malalamiko dhidi ya vyombo vya serikali anayo haki ya kupeleka malalamiko hayo kwenye Tume ya kudumu ili yafanyiwe kazi na kutafutiwa ufumbuzi.

Kimsingi inaonekana vyombo vya kudhibiti utendaji wa mahakama ni vingi lakini hiyo haitoshi. Kilicho cha msingi zaidi ni kwamba yawapasa watendaji katika vyombo hivyo wafanye kazi zao kwa nidhamu, uadilifu haki na kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. Kwa upande mwingine raia nao wanapaswa kushirikiana na mahakama ili ufanisi uweze kuwepo.

4. Taratibu za kumwingiza mtu mahabusu au jela

kwanza kabisa yafaa tuangalie mamlaka zenye nguvu kisheria kuagiza mtu fulani awekwe ndani. Mamlaka hizo ni pana kuanzia Polisi, mahakama mpaka Wanasiasa. Muda na mahali pa kuweka mhusika hutegemea aina ya kosa mhusika analotuhumiwa kulitenda na kwa maelekezo yaliyowekwa na Sheria.

Kwa waliokabidhiwa madaraka hayo mara kadhaa kumetokea hali ya kuyatumia vibaya mamlaka hayo, mfano mara kadhaa imetokea kuzidisha muda ulioelezwa na sheria au mtu kuwekwa kizuizini au kupelekwa uhamishoni kwa sababu ambazo sio zile zilizoelezwa katika sheria ya kuweka watu kizuizini au ya kuhamisha katika Sheria ya kuweka watu kizuizni au kuwahamisha watu. Wengine wamebambikizwa kosa la ‘kutishia usalama’ wakati kosa walilotenda ni uhalifu wa kawaida.

Hali hii imedhihirika baada ya vyombo husika vya kiserikali kushindwa kuithibitisha mahakama makosa ambayo baadhi ya watu wametuhumiwa kuyatenda.

Ikumbukwe kwamba mambo hayo hupelekea watu wengi kuishia jela na hivyo kuzidi kuongeza tatizo la msongamano ambalo tayari ni tatizo kubwa kwa magereza yetu nchini.

Tukirudi katika mamlaka husika zenyewe ni kama ifuatavyo:-

4:1 Kuwe kwa Gerezani na mamlaka ya umma (Civilian Authorities)

viongozi hawa wanao uwezo wa kumweka mtu kizuizini.

Kihistoria kuwapa watu hao mamlaka hayo kumeanzia wakati wa mwanzo wa uhuru ambapo sheria maalumu zilitungwa kuhimiza utekelezaji wa mamlaka hayo.

Waliokabidhiwa madaraka hayo ni wengi nao ni kuanzia rais Wakuu wa mikoa na Wakuu wa Wilaya kwenda chini mpaka Afisa Watendaji wa Kata.

Sheria ya mikoa na Wakuu wa Mikoa ya 1962 inamruhusu mkuu wa mkoa kumweka mtu kizuiani muda wa saa 28. Mkuu wa mkoa hutumia uwezo huu pale anapoona kuwa mhusika anaelekeza kuvuruga amani au kutishia utulivu katika uuma.

Mamlaka hayo hayo amepewa Mkuu wa Wilaya kuitekeleza Sheria hiyo katika eneo la Wilaya yake.

Baadhi ya wenye mamlaka hao wametokea kuyatumia vibaya lakini pale ambapo Mahakama imebaini hivyo haikusita kuchukua hatua mara moja na kulaani vitendo hivyo vya kukiuka haki za msingi za binadamu.

Hii imetokea katika kesi ya Hamisi Masisi na wengine sita ambapo walikuwa wanaituhumu Jamhuri kwa kosa la Mkuu wa Mkoa wa Mara kutoa agizo la kumweka kizuizini mtu aliyeruhusiwa na mahakama kuwekewa dhamana.

4:2 Kuwekwa kizuizini

Kufuatana na Sheria ya kuweka watu kizuizini ya 1962, mwenye mamlaka ya kumweka mtu kizuizini bila kuhojiwa na mahakam ni Rais mwenyewe. Sheria hiyo inatumika pale ambapo usalama wa nchi unaonekana upo hatarini lakini ushindi wa kutosha kuanzisha shauri la jinai haujakamilika.

Ijue Imani Yako

Katekisimu ya Biblia

1. Awali ya yote neno Biblia maana yake nini?

Neno "Biblia" latokana na neno la kigiriki ‘ta Biblia’ likiwa ni uwingi wa bilioni maana yake vitabu. Kwetu sisi Biblia ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vilivyoandikwa kuanzia mnao mwaka 1000 kabla ya ujio wa Yesu Kristo.

Vitabu hivyo vyahusu mambo ya uhusiano kati ya Mungu na wanadamu Mungu akiwa mwumbaji na mfadhili wanadamu wakiwa viumbe vyake na wafadhiliwa.

Uhusiano huo unawadai wandamua wamwamini na kumtumikia Mungu na papo hapo wanadamu wapendane na kuhudumiana wao kwa wao.

Wahusika asilia wa Biblia kama waandishi na walengwa wa maandishi hayo walikuwa watu wa taifa la Israeli. Walakini wahusika wa vitabu vya mwisho mwisho vya Biblia walikuwa watu wa mataifa mengine pia.

Japo kuwa wanadamu ndio walioshika kalamu na kunadika Biblia, hata hivyo Biblia ina ujumbe wa Mungu. Kwa maneno mengine, Biblia ni ujumbe wa Mungu ulioandikwa katika maneno mengine ya wanadamu na kwa mitindo yao ya uandishi. Hii ndiyo sababu Biblia huitwa ‘maandiko matakatifu’ neno la Mungu na neno la Bwana (2Timotheo 3:16;Waefeso 6:17; 2Wathesalonike 3:1).

2. Je, katika mkusanyiko huo kuna jumla ya vitabu vingapi?

Idadi ya vitabu katika Biblia ni tofauti kadiri ya makundi ya waamini walioipokea Biblia kama kitabu chao rasmi katika masuala ya imani na maadili. Kuna makundi makubwa matatu yenye biblia, lakini hutofautiana katika idadi ya vitabu katika biblia zao.

Waisraeli wanaitambua biblia yenye vitabu 39 waamini wa yesu wa makanisa ya Kiprotestatni wanaitambua biblia yenye vitabu 66 Waumini wa Yesu Kristo wa kanisa Katoliki wanaitambua Biblia yenye vitabu 73 katika majubu kwa maswali yafuatayo tutaeleweshw kwa nini kuna tofauti hizo.

3. Je vitabu hivyo twaweza kuvigawa katika sehemu zake kuu?

Ndiyo. Biblia inayotambuliwa na waumini wa Yesu Kristo iwe na makanisa ya Kiprotestanti au kanisa Katoliki inagawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inaitwa Agano la Kale na sehemu ya pili inaitwa Agano Jipya. Waisraeli wanayo sehemu moja tu ya biblia katika mgawanyiko huo wa sehemu mbili nayo ni ile ya Agano la Kale yenye vitabu 39 kwa Waisraeli vitabu hivi haviiitwi vitabu vya agano la Kale kwani wao wanalo Agano moja tu nalo siyo la Kale wala sio Jipya. Kwa hiyo hicho kinachoitwa Agano ndicho kigezo kilichotumika katika kuigawa Biblia katika sehemu kuu mbili.

4. Basi neno Agano maana yake nini katika Biblia?

Neno Agano maana yake mapatano makubaliano au mktaba. Mapatano hayo yaweza kufanywa kati ya pande mbili za watu walio na hadhi sawa au kati ya mkubwa na mdogo. Biblia inasimulia juu ya maagano yaliyofanywa kati ya Mungu na wanadamu katika maagano yaliyofanywa katika Mungu na wanadamu.

Katika maagano hayo Mungu aliahidi kuwalinda na kuwafadhili wahusika kwa kuwapa mali, watoto na ustawi maishani mwao. Wanadamu waliwajibika kuzitii amri za Mungu pamoja na kumwabudu peke yake Agano maarufu katika Biblia ni lile lililofanywa kati ya Mungu na Waisraeli chini ya mlima Sinai (Kutoka 20:1-21). Hapo Mungu aliahidi kuwapa Waisraeli nchi ya Kanaani na kwualinda safarini na katika nchi yao mpya.

Waisraeli walitakuwa kuachana na miungu mingine na waliwajibika kumtumkia Mungu huyo mmoja tu aliyewaondoa toka utumwani Misri. Mara nyingi Waisraeli walivunja masharti yao Agano hlo.

Alitokea mjumbe mmoja wa Mungu aliyeitwa nabii Yeremia.

Huyo nabii alitabiri kwamba Mungu anangefanya Agano Jipya na Waisraeli (Yeremia 31:31-34). Yesu Kristo alipokuja duniani alitangaza kuwa kipindi kipya katika historia kimeanza (Marko 1:14-15).

Alipokula karamu ya mwisho pamoja na wanafunzi wake, Yesu alitwaa kikombe akasema ‘Kikombe hiki ni Agano Jipya litakalothibitishwa kwa damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu’ (Luka 22:20) Baada ya kifo na ufufuko wa yesu, wanafunzi wake waliamini kwamba Yesu Kristo alizinduliwa kipindi cha Agano Jipya kama alivyotabiri nabii Yeremia (Waebrania 8:9-13;9:13-230.

Kwa hiyo waamini wa Yesu Kristo walijielwaa kuwa ni wana wa Agano jipya.

5. Kwa maana hiyo Agano sasa je vitabu vya agano la kale na Agano jipya vyamaanisha nini?

Ujio wa Yesu Kristo ambao ulizindua kipindi cha Agano jipya uliigawa historia ya Biblia katika vipindi viwili. Kipindi kilichokuwa kabla ya ujio wa Yesu Kristo kiliitwa kipindi cha Agano la Kale. Kipindi kilichofuata baada ya ujio wa Yesu Kristo kiliitwa kipindi cha Agano Jipya. Mgawanyo huo wa historia ya Biblia katika sehemu mbili.

Vitabu vilivyoandikwa juu ya Yesu Kristo na juu ya waumini wa Yesu kristo vilitambuliwa kuwa vitabu vya Agano jipya kwanza mtazamo huo waumini wa Yesu Kristo walivitambua vitabu vilivyoandikwa kabla ya ujio wa Yesu Kristo kuwa ni vitabu vya Agano la Kale.

Yaliyomo katika agano la Kale

6. Tuingie katika Agano la kale. Je katika Agano hilo kuna vitabu vingapi na ni vipi?

Waumini Wakatoliki wanavitambua vitabu 46 katika Agano la Kale Tunaweza kuvigawa tena vitabu hivyo katika makundi madogo madogo manne kama ifuatavyo:

(1) Vitabu 5 vya Torati au kwa jina jingine vitabu vya Musa,navyo ni Mwanzo, Kutoka, Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Sheria.

(2) Vitabu 16 vya Historia, navyo ni Yoshua, Waamuzi, Ruthu, 1Samweli,2 Samweli, 1Wafalme,2Wafalme,1Mambo ya Nyakati, 2Mambo ya Nyakati,Ezra, Nehemia, Tobith,Yudithi, Esta, 1Wamakabayo, 2Wamakabayo.

(3) Vitabu 7 vya hekima navyo ni: Yobu, Zauri, Methali,Mhubiri, Wimbo ulio bora, Hekima ya Solomoni na Hekima ya Yoshua bin Sira.

(4) Vitabu 18 vya manabii navyo ni: Isaya, Yeremia, Maombolezo,Baruku,Ezekieli, Danieli, Hosea, Yoeli, Amosi, Obadia,yona, Mika, Nahumu, Habakuki,Sefania,Hagai, Zekaria, Malaki.

Waisraeli na waumini wa makanisa ya kiprotestani wanavitambua vitabu 39 tu miongoni mwa hivyo 46 tulivyovitaja vitabu visivyotambuliwa na makundi hayo mawili ni hivi Yudithi, Tobithi,Baruku, hekima ya Yoshua bin Sira, Hekima ya Solomoni,1Wamakabayo na 2Wamakabayo.

Vitabu hivi viliandikwa katika kipindi cha Agano la Kal. Vilitoka vikiwa vimeandikwa katika lugha ya kigiriki au vilitolewa katiak tafsiri ya kigiriki, wakati vile vingine 39 viliandikwa toka mwanzo katika lugha ya kiebrania lugha iliyotumika na Waisraeli.

Manamo mwaka 95 baada ya kristo, Waisraeli waliamua kuthibitisha idadi na majina rasmi ya vitabu vya Biblia.

Katika maamuzi hayo waliviondoa vile vitabu 7 vilivyoandikwa katika lugha ya kigiriki.

Hali kadhalika makanisa ya Kiprotestani katiakkarniya 16 baada ya Yesu Kristo, yaliviondoa vitabu hivyo toka orodha yao ya vitabu vya Agano la Kale, muda huo huo kanisa katoliki lilithibitha rasmi orodha ya vitabu vya Biblia. Katika mkutano mkuu (mtaguso) uliofanyika katika mji wa Trento, nchini Italia, mwaka 1546 ilithibitishwa kwamba idadi ya vitabu vya Agano la Kale ni 46 .

Idadi hiyo ilijumlisha vile vitabu 7 vilivyoondolewa na waumini Waisraeli na makanisa ya kiprotestani.

7. Tuanze kuvichunguza vitabu vya kundi la kwanza vitabu hivyo vitano vya Torati vyahusu nini?

Awali ya yote inatupasa kuelewa maana ya neno Torati Torati ni neno la Kiebrania tafsiri yake ni fundisho mwongozo au sheria.

Vitabu vitano vya mwanzoni katika Biblia vinaitwa Torati kwa sababu vinatoa mwongozo au sheria zinazohusu maana ya kumtumikia Mungu na mwongozo kuhusu mahusiano mema kati ya mtu na mwenzie.

Kitabu cha Walawi,Kumbukumbu la sheria na sehemu fulani ya kitabu cha Hesabu vinafafanua sheria mbalimbali juu ya namna ya kutolea sadaka, kuadhimisha sherehe na uhusiano wa kijamii kati ya Waisraeli.

Msingi wa sheria hizo ni imani kuwa Mungu aliumba mbingu na dunia, aliwaumba wanadamu alimteua Abrahamu kuwa babu wa taifa la Waisraeli. Aidha Mungu aliwakomboa Waisraeli toka utumwani Misri na waliwaongoza katika safari hadi alipowaingiza katika nchi ya Kanaani.

Matukio haya ya mwanzo na yaliyo msingi wa sheria za kumtumikia Mungu yameelezwa katika vitabu vya Mwanzo, kutoka na sehemu fulani ya kitabu cha Hesabu.

Musa alikuwa kiongozi mkuu wa Waisraeli katika matukio ya kuondoka toka Misri na katika safari ngumu iliyopitia jangwani. Aidha Musa alikuwa pia mhusika mkuu katika tukio la kufanya Agano chini ya mlima Sinai.

Kwa sababu ya kuhusika kwake katika matukio hayo makubwa, Musa alifikiriwa kuwa mwandishi wa vitabu vya Torati katika vitabu vyenyewe vya Torati Musa ndiye anayepokea sheria toka kwa Mungu na kuwatangazia Waisraeli. Kwa hiyo vitabu vya Torati huitwa pia vitabu vya Musa. Hata katika kipindi cha Agano Jipya ilikuwa kawaida kuviita vitabu 5 vya mwanzo kuwa ni vitabu vya Musa , (Luka 16:29;24:44).

8. katika kundi la pili kuna vitabu 16 vya Historia. Vitabu hivyo vyahusu historia gani?

Vitabu 16 vya Historia vyasimulia matukio katika historia ya Waisraeli kuanzia kipindi walipoingia nchini Kanani mnamo mwaka 1250 KK hadi karne moja na nusu hivi kabla ya ujuo wa Yesu Kristo.

Vitabu hivyo tunaweza kuvigawa tena katika sehemu mbili. Viko vitabu vinavyosimulia matukio yaliyomshuhisa hasa Mwisraeli mmoja mmoja na mchango alioutoa katika kulilinda,kuliokoa na kuliendeleza taifa la israeli. Vitabu hivyo vina jina la mhusika wake mkuu navyo ni Yoshua, Ruthu, Ezra,Nehemia, Tobith, Yudithi na Esta. Vitabu vya kundi la pili ni vile vinavyosimulia mfululizo wa matukio makuu yaliyowahusisha Waisraeli wote kama tiafa moja. Twaweza kuigawa historia hiyo katika awamu tatu.

Awamu ya kwanza ilianza mwaka 1250 KK hadi mwaka 587 KK.

Kitabu cha Yoshua kinaanza historia hiyo tangu makabila 12 ya Waisraeli yaliyoingia nchini Kanani. Mwanzoni kila kabila lilijitawala lenyewe chini ya viongozi walioitwa Waaamuzi.

Wakati wa mapambano na maadui wao makablia kadhaa yalijiunga kusaidiana vitani.

Kuanzia mwaka 1000 KK Waisraeli waliungana chini ya mfalm moja katika mfululizo huu: Mfalme Saulo alifuatiwa na mfalme Daudi na mwisho mfalme Solomoni. Mwaka wa kifo cha mfalme Solomoni 922 KK yale makabila 12 ya Waisraeli yalitengana.

Kumi kati yao yaliyokuwa upande wa Kaskazini yalianzisha utawala wao ulioitwa utawala wa Israeli au utawala wa Kaskazini baada ya kubadilisha makao yake makuu katika mji huu na ule, hatimaye makao makuu ya utawala wa Israeli (utawala wa kaskazini) yaliwekwa katika mji wa Samaria. Makabila mawili yaliyokuwa upande wa Kusini yalianzisha utawala wao ulioitwa utawala wa kusini au utawala wa Yuda.

Makao yake makuu yalikuwa katika mji wa Yerusalemu. Utawala wa Yuda uliendeleza ukoo wa mfalme Daudi aliyekuwa mfalme maarufu sana katika historia ya Waisraeli. Mwaka 722KK utawala wa Israeli (Kaskazini) ulivamiwa na taifa la waashuru. Mji wa Samaria ukaangamizwa.

Raia wake wengi walihamishiwa katika nchi nyingine na raia wa nchi hizo waliletwa katika utawala wa Israeli uliovunjwa.

Hapo walichanganyika na wale waliobakia. Mchanganyiko huo ndio watu walioitwa miaka ya baadaye Wasamaria. Utawala wa Yuda uliendelea kujikokota peke yake hadi mwaka 587KK. Mwaka huo taifa la Wababeli waliuvamia utawala wa Yuda wakalibomoa hekalu la Yerusalemu wakawachukua watu maarufu uhamishoni Babeli.

Awamu ya pili ilidumu kuanzia mwaka 587 KK hadi mwaka 538KK katika kipindi hicho ukoo wa kifalme na utawala wa Yuda pamojana watu wengine maarufu waliishi uhamishoni huko Babeli. Hao ndio walioendeleza historia ya taifa la Mungu. Kuanzia kipindi hicho waliitwa mara nyingi Wayahudi japokuwa neno la Israeli lilitumika bado mara moja moja.

Maisha yao kiuchumi hayakuwa mabaya sana lakini walipata pigo kubwa la kiimani walikuwa wamepoteza nchi waliyoahidiwa, hekalu lao tukufu na ukoo wa kifalme haukuwa na madaraka tena baada ya miaka arobaini hivi mambo yakabadilika. Dola jipya lilikusanya nguvu likawa tishio kwa dola laWababeli hao wapya walikuwa waajemi waliowashinda vita wababeli wakawaruhusu Wayahudi (Waisraeli) kurudi kwao nchi ya Yuda.

Tukio hili lilifungua awamu ya tatu katika historia ya taifa la Mungu kuanzia mwaka 538Kkhdi 142KK.

Katika awam hiyo ya mwisho watu wa Yuda walijenga tena vipya hekalu lao mjini Yerusalemu wakarejesha utaratibu wa kutolewa sadaka makuhani na wataalamu wa sheria za Musa walikuwa watu muhimu sana katika kipindi hicho.

Hata hivyo kipindi hicho hakikuwa na uhuru kamili kwa Wayahudi. Walitawaliwa kwa mfululizo na Waajemi na Wagiriki. Hali ilikuwa ngumu zaidi wakati wa utawala wa Wagiriki ambao walijaribu kupiga vita dini ya Wayahudi lakini Wayahudi walijaribu kutetea uhuru wa dini yao hadi wakawashinda Wagiriki mnamo mwaka 142KK.

Kuanzia mwaka huo Wayahudi waliweza kujitawala hadi Waroma walipoitwaa nchi ya Yuda mwaka 63KK.

Ijue Tume ya Mawasiliano na huduma za posta na simu

Na Mwandishi Wetu

Kama nchi nyingine duniani, nchini Tanzania urekebishaji na uundaji mpya wa mawasiliano ulianza kwa kutenganisha shughuli za udhibiti toka uendeshaji kwa upande mmoja na kutenganisha huduma za posta kutoka katika huduma za uendeshaji simu, redio au televisheni kwa upande mwingine.

Hatua hii ilifikiwa mwaka 1993 kwa kuvunja iliyokuwa mdhibiti na mwendeshaji yaani, Shirika la Posta na Simu(TP & TC), na kuanzisha taasisi tatu tofauti ambazo ni Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC), Shirika la Posta tanzania(TPC) na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Tume ya Mawasiliano tanzania (TCC), ilianzishwa chini ya kifungu cha Sheria za Mawasiliano namba 18, cha mwaka 1993 kama mdhibitii wa huduma za posta na simu na mwendeshaji wa mpangilio wa masafa ya redio katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni Tume huru ya serikali yenye wajibu wa urekebishaji na uboreshaji wa huduma za posta na simu.

TPC na TTCL vilianzishwa kama vyombo vya kibiashara chini ya Shirika la Posta. Kifungu cha Sheria Namba 19/ 1993 TPC na Kampuni ya Simu Tanzania (Tanzania Telecommunications Company Incoperation), Kifungu Na. 20/1993.

Tume hii inaundwa na wajumbe watano, yaani Mwenyekiti ambaye huteuliwa na Rais.

Kwa sasa, Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Balozi Ahmed Hassan Diria.

Pia, Tume inapaswa kuwa na makamishna wasiopungua wanne na wasiozidi sita wanaoteuliwa na Waziri anayehusika na mawasiliano nchini.

Kwa sasa makamishina waliopo ni sita ambao ni Hashim Saggaf, Dk. Suleman J. Omar, Peter Nyamhokya, Timoth Shindika, Profesa Mark Mwandosya na August B. Kowero.

Tume pia inayo Sekretarieti inayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu naye pia, anateuliwa na Rais. Kwa sasa ni Kanali Abihudi N. Nalingigwa.

Wajumbe wengine wanaounda Sekretarieti ni Ephraim Madeje ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Posta, John A. Mpapalika ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Simu.

Wengine ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Masafa, Emmanuel T.K. Mange na Mshauri wa Tume, Elizabeth Nzagi.

Kipindi cha uongozi cha Mwenyekiti na makamishna ni miaka mitatu; wakati Mkurugenzi Mkuu ni miaka mitano. Mwenyekiti, makamishna na Mkurugenzi Mkuu, wanaruhusiwa kuendelea kama watateuliwa tena na wanaweza kuondolewa katika nyadhifa zao kwa sababu maalumu.

Tangu kuanzishwa kwa TCC, idadi kubwa ya waendeshaji wa mawasiliano simu za umma na za binafsi zimekuwa zikisajiliwa.

Kwa kipindi hicho, TCC imepata uzoefu mwingi wa usajili uliopelekea kuongezeka kwa ubora na huduma mbalimbali za simu.

Kabla ya kuendelea kuitazama TCC, hebu tuangalie kazi zake.

Kazi ya Tume ya Mawasiliano Tanzania, ni pamoja na kutoa vibali kwa waendeshaji wa huduma za posta na simu, kustawisha na kudhibiti ushindani katika sekta ya mawasiliano na kudhibiti aina za vifaa na teknolojia za mawasiliano zinazotumika.

Shughuli nyingine ni kudhibiti na kupanga maeneo ya kurusha masafa, kurekebisha na kudhibiti mawasiliano ya ndani ya mifumo ya mawasiliano ya simu, kuiwakilisha Tanzania katika mashirika ya kimataifa ya posta na simu, kuishauri serikali juu ya masuala ya posta na simu na kudhibiti ushuru kwa huduma za posta na simu, Kusimamia na kuhakikisha kunakuwepo na huduma bora za posta na simu.

Tangu kuanzishwa kwake, TCC imekwisha toa vibali kwa waendeshaji wa huduma za simu kama Kampuni ya Simu Tanzania(TTCL) ili kuendesha huduma zake za simu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya Simu ya Zanzibar (ZANTEL) ili kuendesha huduma za Simu kwa Zanzibar (Unguja na Pemba).

Hadi sasa waendeshaji wa huduma za mawasiliano ya simu watano walikwishapewa kibali na wanne kati yao, wanatoa huduma kwa nchi nzima. Waendeshaji hao ni MIC, Tanzania Limited inayojulikana kama Mobitel, TRI Telecommunications Tanzania Ltd, inayoendesha shughuli zake ikijulikana kama Tritel, Tanzania Telecommunication Company Limited (TTCL) na VODACOM Tanzania Ltd.

ZANTEL imepewa kibali cha kutoa huduma za simu za mkononi kwa Zanzibar.

Huduma maalumu za Mawasiliano ya redio

Mwaka 1995, kampuni zifuatazo zilipewa kibali cha kutoa huduma maalumu za mawasiliano ya redio (Radio Paging Services) katika Tanzania. ACG Telesystems Ltd, Beep Me Ltd, Call Systems Ltd na TTCL.

Hata hivyo, biashara hii ya huduma maalumu za mawasiliano ya redio zilikuwa na marejesho hafifu yaliyopelekea waendeshaji kufilisika na hadi sasa, hakuna hata mwendeshaji mmoja anayeendelea na shughuli hiyo.

Pia, kampuni kadhaa zimepewa kibali cha kutoa huduma ya mawasiliano ya umma kwa njia ya taarifa (Public Data Communication) katika Tanzania. Kampuni hizo ni pamoja na SITA GROUP, Wilken Afsat Tanzania Ltd, DATEL Tanzania Ltd, EQUANT (T) LTD na SIMBANET (T) Ltd.

Nyingine ni SOFT TECH (T) Ltd, FASTCOM AFRICA Ltd na TANSAT (T) Ltd.

Pia kampuni kadhaa zimepewa kibali cha kutoa huduma za mtandao wa kompyuta (Internet Service Provider). Kampuni hizo ni pamoja na Tanzania Posts Corporation(TPC), Internet Africa, Computers & Telecoms Systems Ltd-(CATS), Yellow Pages Ltd, Africa Online na Star Telecom.

I Nyingine zilizopewa kibali cha kutoa huduma hiyo ni pamoja na COSBI Systems Ltd, Green Growth R & D Ltd, International Communications Systems (T) Ltd, Cyber Twiga Ltd, SIMUNET CO. Ltd na J.R. Electronics Ltd.

Nyingine ni Arusha Node Marie, Planetel Communications (T) Ltd na CRDB Ltd

Makandarasi wa mawasiliano

Zaidi ya vibali 80 vimetolewa kwa kampuni za kibinafsi kuingiza, kugawa, kuunganisha na kuendeleza njia za simu na vifaa vya mawasiliano kwa njia ya radio.

Uhakiki wa aina za mawasiliano ya redio na njia za mawasiliano ya simu umekuwa ukiendelea.

Vibali kwa huduma za Posta na utarishi

Vibali vifuatavyo vimekwisha tolewa kwa huduma za posta Mwendeshaji mkuu wa huduma za Posta na utarishi (Tanzania Posts na Courier Operator).

Hawa ni watano ambao ni Skynet Express Worlwide, TNT Wordwide Express, Sangare Limited, DHL Wordwide Express na East African Courier(T) Ltd.

Kampuni moja ya utarishi wa ndani; Ndondo Mwenda Mbio Limited (NMM) na makampuni mengine saba yanayoendesha huduma za utarishi, pia yamekwisha pata kibali.

Matarishi wa usafiri ambao pia hutoa huduma kimataifa ni Jet Travel Services, Ndeng’aro Agencies & Consultants, Scandinavia Bus Express, Akamba Bus Sevice, John Terry Establishment, Swift Express na A. Karim Limited.

.

TCC imefanikiwa kuweka miongozo ya huduma za mawasiliano ya simu na radio na kuanzishwa kwa na kupata gari maalumu la vifaa vya kudhibiti masafa na kuitisha mikutano ya Kitaifa juu ya mawasiliano ya simu.