IJUE AFYA YAKO

Jinsi ya kumhudumia mtu aliyeungua kwa moto, kuvunjika mguu, shingo n.k

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini.

Kinga:

Karibu kuungua kote kwa mto kunaweza kuzuiwa. Chukua tahadhari kwa watoto.

Usiwaache watoto wadogo waende karibu ya moto.

Weka taa na njiti za vibiriti sehemu ambayo watoto hawataweza kuzifikia.

Hakikisha kuwa, mikono ya sufuria zilizoko jikoni zimegeuzwa katika sehemu ambayo watoto hawataweza kuzifikia.

Mwunguzo mdogo usiotoa malengelenge (daraja la kwanza):

Ili kupunguza maumivu na madhara yaliyosababishwa na mwunguzo mdogo, tumbukiza haraka sehemu hiyo iliyoungua kwenye maji baridi. Hakuna matibabu mengine yanayohitajika. Kunywa aspirini kutuliza maumivu.

Mwungozo unaoleta malengelenge (daraja la pili)

Usipasue malengelenge

Kama yakipasuka, safisha taratibu na sabuni na maji ya moto yaliyokwisha kupoa. Chukua vaseline, ichemshe kisha ipake kwenye kitambaa kisafi, halafu kiweke kwenye jeraha.

Kama hakuna vaseline, kiache kidonda wazi, usipake grisi au siagi.

Ni lazima kuweka sehemu iliyoungua katika hali ya usafi na hakikisha unazuia sehemu hiyo isiingie uchafu, vumbi wala mainzi.

Kama dalili ya kuambukizwa imeanza kama vile usaha, harufu mbaya, homa au uvimbe wa mtoki kanda jeraha kwa maji ya chumvi yaliyo vuguvugu(kijiko kimoja cha chai kwa chupa 2 za maji).

Fanya hivyo mara tatu kutwa na kisha, ondoa ngozi na nyama iliyoharibika kwa uangalifu. Unaweza kupaka mafuta ya kuua vijidudu kama vile "neosporin". Kama amezidiwa, mpe penicilini au ampisilini.

Kina kirefu cha kuungua (daraja la tatu):

Hiki huunguza na kuharibu ngozi na nyama. Kuungua namna hii ni hatari sana hivyo mpeleke mapema katika kituo cha afya baada ya kufunika sehemu iliyoungua kwa kitambaa safi.

Kama ni vigumu kupata msaada wa mganga, anza kutibu kwa kufuata maagizo yaliyotolewa hapo juu.

Iwapo huna vaseline, basi usifunge jereha hilo ila, lifunike kwa pamba au nguo yoyote safi kuzuia vumbi na nzi. Hakikisha kuwa kitambaa unachokitumia kufunika jereha hilo, ni kisafi na kinabadilishwa mara kipatapo uchafu wa maji au damu. Mpe penisilini.

Ni mwiko kuweka grisi, mafuta, kingozi, mitishamba au kinyesi katika sehemu iliyoungua.

 

Ni wajibu kumfariji na kumpa moyo kuwa kila kitu kitakuwa sawa. Mpe aspirini ya kutuliza maumivu pamoja na "codeine" kama inapatikana. Pia, maumivu yatatulia ikiwa utasafisha majeraha na maji yaliyo na chumvi kidogo.

Mpe maji mengi ya kunywa. Kama sehemu iliyoungua ni kubwa, (mara mbili ya mkono wake), basi mtengenezee kinywaji kifuatacho:

Katika chupa mbili za maji: Ongeza nusu kijiko cha chai cha chumvi, na nusu kijiko cha chai cha "sodium bicarbonate."

Kisha, ongeza vijiko vikubwa viwili au vitatu vya sukari au asali pamoja na maji ya machungwa au limau.

Ni lazima aendelee kunywa kinywaji hiki kila wakati mpaka aanze kwenda haja ndogo mara kwa mara. Hali kadhalika, inambidi ale vyakula vilivyo na protini kwa wingi japokuwa hakuna mwiko wa aina yoyote ya vyakula.

Kuungua sehemu ya vikonyo

Kama mtu ameungua vibaya katikati ya vidole, kwapani au katika vikonyo vingine vyovyote, chukua vitambaa vidogo vilivyo safi na vaseline na viwekwe katikati ya sehemu iliyoungua ili kuzuia kuungana wakati inapopona. Pia, vidole, mikono na miguu lazima vifanyiwe mazoezi kila siku.

Kutakuwa na maumivu lakini, itamsaidia kukinga kovu gumu ambalo litazuia kufanya vitendo mbalimbali

Mifupa iliyovunjika

Mfupa unapovunjika jambo muhimu unaloweza kufanya ni kuweka mfupa huo katika hali imara. Hii itazuia hatari nyingine zaidi kuufanya uunge vizuri.

Kabla hujamwondoa au kumnyanyua mtu aliyevunjika mfupa, imarisha vipande hivyo vya mifupa visicheze cheze kwa kutumia "Splint" au magome ya mti kisha, mpeleke katika kituo cha afya na kuiweka sawa mifupa iliyovunjika.

Kuiweka sawa mifupa

Kama mifupa ipo sawa sawa, ni afadhali isiguswe tena la sivyo inaweza kuleta matatizo zaidi.

Ikiwa kama mifupa hiyo imeachana na ajali imetokea hivi karibuni, unaweza kujaribu kuinyosha au kuiweka sawa kabla hujafungia splint au kuzungusha cast inakuwa rahisi zaidi ikiwa mifupa inawekwa sawa mara tu inapovunjika.

Jinsi ya kuweka sawa kiganja cha mkono kilichovunjika.

Vuta mkono kwa nguvu na bila kupinda kwa muda wa dakika 5 au 10 ili kutenga mifupa iliyovunjika.

Mtu mmoja akiwa bado anavuta mkono mwingine, aanze kurekebisha na kuuweka sawa mifupa

Ilani:

Inawezekana kuleta madhara zaidi wakati unapojaribu kuweka sawa mifupa. Ni afadhali kufanya kazi na mtu mwenye ujuzi. Usitumie mabavu.

Inachukua muda gani kwa mifupa iliyovunjika kuungua?

Mfupa unachukua muda mrefu zaidi kuungana ikiwa imevunjika vibaya au aliyepata ajali hiyo, ni wa makamo.

Mifupa ya watoto inaunga upesi zaidi kuliko ya watu wa makamo ambayo wakati mwingine inaweza isiunge.

Mkono uliovunjika inabidi ukae ndani ya cast kwa muda wa mwezi mmoja hivi na usinyanyue vitu vizito kwa muda wa mwezi tena. Mguu utachukua miezi miwili hivi katika cast.

Kuvunjika mfupa wa paja

Mfupa wa paja ukivunjika, utahitaji huduma maalumu. Ni vizuri kama mwili wote unawekewa splinti kama ilivyonyeshwa hapo chini na kumpeleka mgonjwa katika kituo cha afya mara moja.

Kuvunjika shingo na uti wa mgongo:

Ikiwa unashuku mtu kavunjika uti wa mgongo au shingo, jihadhari sana wakati unapomsafirisha. Jitahidi kabisa usimgeuze.

Ikiwezekana, mwite mganga kabla ya kumsafirisha. Ikiwa ni lazima umsafirishe, fanya hivyo bila kukunja uti wake au shingo.

Kuvunjika mbavu:

Hizi zinauma sana lakini, mara kwa mara hujiunga zenyewe.

Ni afadhali usirekebishe kifua. Dawa nzuri ni aspirini na kumshauri apumzike. Inaweza kuchukua miezi kabla maumivu hayajatoweka kabisa.

Si kawaida ya mbavu iliyovunjika kutoboa pafu. Lakini, kama mtu anakohoa damu au anapata tabu ya pumzi, mpe penisilini au ampisilini na mpeleke katika kituo cha afya.

Mfupa uliovunjika vibaya na kufanya jeraha (compound fracture):

Kwa kuwa hatari ya kuingiwa na vijidudu ni kubwa, ni afadhali kutafuta msaada wa mganga au daktari mapema baada ya kusafisha vizuri sana jeraha na mfupa uliojitokeza kwa maji ya mto.

Usirudishe mfupa huo ndani ya jeraha mpaka mfupa na jeraha hilo imekuwa safi kabisa.

Iweke sehemu hiyo ni ya mwili katika splint kuzuia madhara zaidi.

Ikiwa mfupa umechana ngozi, mpe penisilini au ampisilini kuzuia vijidudu.

Jihadhari:

Usichue sehemu ya mwili iliyovunjika au unayoshuku kuwa imevunjika.

Kuwatenganisha wanandoa hali ndoa ingalipo (3)

Katika toleo lililopita, tulifikia kipengele kinachojadili juu ya kutengana wanandoa, kutokana na uzinzi. Bado tunaendelea na ufafanuzi juu ya kipengele hiki kama MWANDISHI WETU, anavyofafanua kwa msaada wa makala iliyoandikwa katika jarida la Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na Wakili Hakimu, Padre Augustine Mringi.

Mwanandoa ambaye hakuzini, hawezi kisheria kuomba atenganishwe na mwanandoa mwenza aliyezini endapo yeye mwenyewe alifumbia macho uzinzi husika au alisababisha uzinzi wenyewe, au yeye mwenyewe alizini.

Tunaposema mwanandoa ambaye hakuzini amefumbia macho au amekubali kimyakimya uzinzi wa mwanandoa mwenza, tuna maana hii kwamba mwanandoa huyo, alipata habari juu ya uzinzi huo, alindelea kuishi na mwanandoa mwenza na kumpa denindoa (debitum) kama kawaida.

Tena, ufumbiaji macho huu wa uzinzi husika, utahisiwa na mwanandoa mwenza aliyezini kwa kipindi cha miezi sita au zaidi tangu tukio lenyewe bila ya kutoa malalamiko yoyote kwa wakuu wa Kanisa au wa Serikali wanaohusika.

Kama mwanandoa ambaye hakuzini alizuilika kisheria na kikweli kutoa malalamiko kama hayo wakati wake basi kwa vyovyote hatakuwa anabanwa na utaratibu sheria huu na hivi ataweza bado kutoa malalamiko hayo kihalali baadaye.

Wakuu wa Kanisa husika baada ya kupokea shauri husika, itabidi waamue hima kama wataruhusu wanandoa watengane kwa mujibu wa sheria au watashauri kuendeleza mawasilianondoa ambayo yamekwisha kusambaratika au yamo njiani kusambaratika.

Ni jukumu la wakuu wa Kanisa husika kumsadikisha mwanandoa ambaye hakuzini, kumsamehe mwanandoa mwenza aliyezini na kujaribu njia zote kuwapatanisha.

Hata hivyo lakini, ni wazi kwamba endapo msamaha utapatikana, itabidi wanandoa wote wawili wapimwe kitaalamu kuona kama hawana magonjwa ya hatari ya kuambukiza kabla hawajarudishiana mawasilanondoa.

Kwa vyovyote, busara ya kichungaji inadai kwamba wakuu wa Kanisa wenye mamlaka wasiwalazimishe wanandoa ambao kikweli hawawezi kurudiana, warudiane bila ridhaa yao wenyewe.

Kutengana kutokana na sababu nyingine:

Endapo mmoja wa wanandoa atakuwa tishio na hatari kubwa ya kiroho au ya kimwili kwa mwanandoa mwenza au kwa watoto au kwa namna fulani, atafanya mawasilianondoa kuwa magumu mno kutekeleza, basi mwanandoa huyo atakuwa amempa mwanandoa mwenza sababu za kisheria za kujitenga naye.

Katika hali kama hii mtawala mahalia husika atatoa rasmi hati ya kumwangiza mwanandoa mlalamkaji aondoke na kama kuzidi kuchelewa kutahatarisha mambo zaidi, hata mwanandoa mlalamikaji huyo angeweza kujiondekea kwa mamlaka yake mwenyewe. Lakini, katika shauri zote sababu za kutengana zikisha kukoma, mawasilanondoa ni lazima yarejeshwe isipokuwa wakuu wa Kanisa husika waamue vingine tofauti (MSK, k1153).

Ni vigumu sana kutoa orodha kamili ya vitu vyote vinavyoweza kuwa sababu zinazoweza kuleta hatari kubwa za kiroho au za kimwili kwa mwanandoa na kusababisha mtengano kisheria.

Sheria inagusia tu; hapa matatizo makubwa ambayo hayawezi kutanzuliwa kwa urahisi na siyo shida zinazoweza kutatuliwa katika ndoa. Ijapokuwa sheria inaonekana kujadili masuala ya kukosa zaidi kama chanzo cha kutaka mtengano, hata hivyo matatizo ya kisaikolojia au mengineyo yasiyohusika na makosa yanaweza pia kutumika kama sababu ya kuomba mtengano.

Ni kweli kwamba sababu za kutengana zikishatoweka, ni vema wanandoa waliotengana warudishiane mawasilianondoa mara moja.

Lakini, kama sababu za kutengana zilikuwa nzito na kubwa, itakuwa vigumu sana kwa wanandoa kurudiana bila kusaidiwa na mtu wa kati.

Licha ya mtengano, wazazi wote wawili bado wanapaswa kuwalea watoto wao "Katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo" (Efe 6:4) na kuhakikisha kuwa, hawawachukizi watoto wao ili wasije wakakata tamaa (Kol 3:21).

Hakika hapa wakuu wa Kanisa husika, watahitaji sana kwa msaada ushauri, na utiajimoyo. Bila shaka wakuu wa Kanisa ambao tumekuwa tukiwataja katika makala haya, ni askofu jimbo ambaye anaweza kuruhusu mtengano wa kutoa hukumu ya kutengana kwa njia ya mahakama (MSK k 1692).

Yafaa daima ieleweke wazi kwamba, ijapokuwa mwanandoa anaweza kwa niaba yake mwenyewe kutengana kwa muda na mwanandoa mwenza (MSK, k 1152-1153) hata hivyo akitaka mtengano wa kudumu ni lazima auombe kutoka kwa wakuu wa Kanisa wenye mamlaka.

Matunzo na Malezi ya watoto wakati wa mtengano:

Baada ya wanandoa kutengana kisheria, ni lazima mpango ufanyike kuona kwamba watoto wanatunzwa vya kutosha na malezi yao yanazingatiwa inavyotakiwa (MSK,k1154). Kwa kweli mpango kuhusu utaratibu wa matunzo na malezi ya watoto baada ya mtengan, ulipaswa ufanywe na wanandoa husika wenyewe.

Sasa, kama watu hawa wamegombana na ikabidi mwisho wa yote watenganishwe kwa mujibu wa sheria, basi yule aliyewatenganisha anapaswa kutoa mpango kuonesha jinsi watoto watakavyotunzwa na kulelewa. Kiukweli, watoto walitakiwa wakae na walelewe na mzazi yule asiye na hatia lakini, matunzo yatokane na wazazi wote wawili licha ya kuwepo mtengano huo wa wazazi wote wawili.

Kanisa linapaswa kuwa na utaratibu wa kuwatunza na kuwalea watoto wakati wanapotenganishwa na wazazi kwa mujibu wa sheria. Pia, ni vema Kanisa liungane na Serikali katika masuala ya kuwatunza na kuwalea watoto wakati wazazi wanapopewa mtengano wa kisheria mradi tu, mipango kama hiyo isiwe kinyume na mafundisho msingi ya Mungu na ya Kanisa (MSK,k 1672,SNT, Na. 110-111, 125-137).

Kurudisha mawasilianondoa:

Mwanandoa ambaye hakusababisha mtengano atasifika kwa kumsamehe mwanandoa mwenza aliyekosa na kumrudishia mawasilianondoa. Mwanandoa huyo hufutilia mbali ile haki yake ya mwanzo ya kujitenga na mwanandoa mwenza (MSK,k 1155).

Mwanandoa aliyeruhusiwa kutengana na mwanandoa mwenza kwa kudumu, halazimiki kurudisha mawasilianondoa.

Lakini, endapo mwanandoa huyohuyo ataamua mwenyewe kubadili nia na kurudisha mawasilianondoa, haki yake ya kutengana na mwanandoa mwenza itasitishwa mara moja.

Mwanandoa yeyote anayesitisha mawasilianondoa bila idhini ya Kanisa habanwi na adhabu yoyote ya kikanisa kama vile kunyimwa kupokea Komunyo isipokuwa, yeye huyu awe amejinyima mwenyewe huduma kama hizo (MSK,k13211) au dhamiri yake inamuuma na kumshitaki:

"Basi mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi." (Yak 4:17). Yafaa sana ieleweke wazi kwamba sheria kanuni mintarafu kuwatenganisha wanandoa kwa mujibu wa sheria, zinahusu tu, ndoa baina na Mkatoliki na Mkatoliki. Baina ya Mkatoliki na mbatizwa asiyemkatoliki na baina ya Mkatoliki na mpagani.

Tangu mwanzo Mungu alikataa talaka (Mwa 2:24) Kristo Bwana alikataa talaka (Mat19:6;9 Marko 10:9, 11-12; Luka 16:18), mitume walikataa talaka (1Kor 7:10-11;Rom 7:2-3), na hadi sasa Kanisa limekuwa likikataa talaka (MSK,k1055,1085). Kutokana na ukweli huu, Wakatoliki wote wanakatazwa kabisa kuomba talaka kutoka mahakama yoyote ya nchi au ya Kiserikali bila kupata ruhusa kwanza kutoka kwa Kanisa.

Kwa kawaida, Wakatoliki ambao ndoa zao hutangazwa kuwa batili au zimefutwa kwa mujibu wa sheria kwa sababu hii au ile (MSK,k 1056,1083-11-50), huagizwa na wakuu wa Kania wenye mamlaka kwenda kwenye mahakama ya kiserikali kuomba talaka au zaidi kile kinachoitwa "talaka".

Wakisha kupata talaka hiyo, ndoa mpya hushuhudiwa tena kwa mujibu wa sheria.

Lakini, hali halisi ni kwamba leo hii Wakatoliki wengi huenda kwenye mahakama za kiserikali kwa niaba yao wenyewe kuomba talaka bila idhini ya Kanisa na wengi, wao, hata hujiweka nje ya Kanisa moja kwa moja kwa kufunga ndoa nyingine wakati ile ya kwanza bado iko.

Hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulifumbia macho ijapokuwa msimamo wa Kanisa kuhusu umoja (unity) na uimara (indissolubility) wa ndoa ni ule ule. La maana, ni kwetu sisi wachungaji kuzidi kuwafundisha vema na vya kutosha, wote wanaotaka kufunga ndoa na kuwapa waliokwisha funga ndoa maleziendelea kuhusu ndoa na mengineyo.

Hatima:

Katika makala haya tumekuwa tukijifunza kwa mapana na marefu suala zima la mwanandoa kutengana na mwanandoa mwenza kisheria kutokana na sababu nzito zinazostahili.

Tumeona kwamba uzinzi pamoja na hatari kubwa za kiroho na za kimwili kwa mmojawapo wa wanandoa au kwa watoto, ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kusababisha mtengano wa kisheria miongoni mwa wanandoa.

Tumeona pia kwamba, kuna uwezekano kabisa kwa wanandoa wanaozozana vibaya sana na hata kufikia mauaji, kutenganishwa kwa muda ili wanandoa hao wapate kuyafikiria tena upya maishandoa yao kwa jumla.

Kwa kujifunza mada hii polepole, tumeona kwamba kuna njia ya kisheria ya kuwanusuru wanandoa ambao wako njiani kukata tamaa kutokana na matatizo makubwa wanayobeba na hawajui wamtupie nani.

Sheria inatutaka sisi wachungaji tuachane na majibu ya mkatomkato kwa wanandoa wenye matatizo kama vile "Vumilia tu kwani alichokiunganisha Mungu binadamu hawezi kukitenganisha", "Kama umeshindwa kabisa kuishi na mwanandoa mwenza, omba kifo kiwatenganishe" na "Kwa kweli hatuwezi kufanya lolote"; na mengine mengi ya namna hiyo.

Majibu ya harakaharaka na ya mkato kama hayo, yanatoa tu; hisia za kiongozi na mchungaji anayesambasamba katika uwanja wake wa kazi na hayuko makini sana kuhusu masuala nyeti kama ya ndoa.

Katika parokia, vigango, na taasisi zetu, wako wanandoa wanaohangaika na kuteseka hasahasa akinamama ambao hupigwa kiholela na hata kuambiwa bila aibu: "Uliletwa hapa kwetu kwa kikapu na kwa kuposwa; na kwa hiyo utafuata moja kwa moja masharti yangu kwani hata Mtume Paulo anasema, "Wake wawatii waume zao katika mambo yote," "(Efe 5:24b). lakini, wanaume hao hao wanaowapiga wake zao kiholela, wanasahau mafundisho mengine ya Mtume Paulo yanayosisitiza: (Mume atimize wajibu alionao kwa mkewe naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe) (1Kor 7:3).

"Basi waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. (Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia huulisha na kuuvika....)" Wanawake kama hao ambao hawajui mafundisho sahihi ya dini kuhusu uhusiano unaopaswa kuweko baina ya mume na mke, hukata tamaa na kwa vile hata sheria kanuni kuhusu hili nazo hawazijui, hubaki wakihaha hasa wakipewa majibu ya kukatisha tamaa.

Sasa Mkusanyo Sheria Kanuni unaambiwa; akinamama hao kwamba waume zao wakiwa wazinzi, wao hawa wanaweza kuletwa mbele ya sheria na mtengano ukapatikana kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo lakini, yafaa ieleweke wazi kwamba vitendo vya uzinzi au vya ukatli vinavyosababisha mtengano wa kisheria miongoni mwa wanandoa, vinawahusu pia wake watuhumiwa na walalamikiwa.

Ni matumaini yetu kwamba wachungaji wa roho za watu wakizingatia kwa dhati utekelezaji wa sheria kanuni kuhusu "Kuwatenganisha wanandoa ndoa ikingali bado iko", (MSK,k 1151-1155), watazishughulikia bila kuchelewa zaidi ndoa ambazo ziko hatarini kusambaratika siku kwa siku kwa sababu mmojawapo wa wanandoa ni mzinzi sugu au ni hatari kwa maisha ya mwanandoa mwenza au ya watoto.

Inaonekana mazoea yetu hadi sasa yamekuwa kuwasilisha tu, kwenye Mahakama ya Kikanisa mashauri ya ndoa yanayohusu ndoa zinazohisiwa kuwa batili (MSK,k 1056,1084-1129) au zinazotakiwa zifutwe ili kufaidi imani (MSK,k 1142-1150). Hatuleti kwenye mahakama hiyo, mashauri yanayohusu kuwatenganisha wanandoa ikingali bado iko (MSK,k 1151-1155).

Mashauri ya aina hii yamo mengi katika parokia zetu, vigango vyetu na taasisi zetu. Mara nyingi wachungaji huwaambia wanandoa walalamikaji watengane na wanandoa wenza bila kufuata sheria au utaratibu wowote wa kisheria.

"Kwa wale waliooa ninayo amri tena si yangu ila ni ya Bwana: Mke asiachane na mumewe; lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa ama la apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe" (1Kor. 7:10-11).

Na tena hata wanandoa wengine wenye matatizo huamua kutengana na wanandoa wenza bila hata kulishirikisha Kanisa wala Serikali.

Huvijia tu vyombo hivi mambo yanapowachachia. Daima, wanandoa wanaaswa na kufundishwa waishi pamoja bila kutengana; na endapo kwa sababu hii au ile watatengana, basi kila mmoja abaki bila kuoa au kuolewa.

Kwa hiyo, tafadhali sana wanandoa wanaotengana au wanaotenganishwa katika parokia zetu, katika vigango vyetu, na hata katika taasisi zetu; tuhakikishe wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria kwa sababu mkusanyo Sheria Kanuni, unadai kwamba ndoa yoyote iliyoshuhudiwa kwa mujibu wa sheria kulindwa na sheria mpaka hapo sheria itakapoagiza vingine kutokana na sababu zinazodhihirika kisheria (MSK,k 1060).

Kwa kweli wanandoa wanatakiwa waishi pamoja ili kutokumpa shetani nafasi: "Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mmeafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha, rudianeni tena mara ili shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu" (1Kor. 7:5) na hasahasa wanandoa wanatakiwa waishi pamoja kwa sababu "Mali isiyolindwa kwa ukuta, itaporwa" (Sira 36:30a).

TTCL yafungua ukurasa mwingine wa Mawasiliano

l Njia za simu kufikia 800,000 badala ya 162,000 za sasa

l Kumwaga simu za mkononi nchi nzima kwa bei poa

l Ni mradi wa zaidi ya shilingi bilioni 96

MIONGONI mwa mashirika nyeti ambayo hisa zake zimeuzwa hivi karibuni, ni Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Katika makala haya, Mwandishi Wetu anaeleza mikakati ya wawekezaji hao wapya na matarajio ya Watanzania katika sekta ya mawasiliano.

KUTANGAZWA kwa mbia wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Juni 26, mwaka huu, kulizua maswali mengi miongoni mwa wananchi ambao walikuwa wanataka kujua hatma ya shirika hilo.

Wengi walikuwa na wasi wasi juu ya uwezo wa wawekezaji hao ambao ni makampuni mawili makubwa ya mawasiliano ya MSI la Uholanzi; na Detecon la Ujerumani.

Makampuni hayo washirika, yaliweza kushinda zabuni ya ununuzi wa hisa za kampuni hiyo baada ya kuyapiku mengine sita katika hatua za mwisho.

Makampuni ambayo hali zake hazikuwaridhisha Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) ni pamoja na Mahanagar, Nigam ya India na Mauritius Telcom.

Mengine ni MTN South Africa, Sascatel Canada na Vodacom of South Africa ambayo inashirikiana na WorldTel.

Wakati MSI na Detecon walitangaza ofa ya Dola milioni 120 na kuongeza njia za mawasiliano hadi kufikia 800,100, Vodacom waliahidi kitita cha Dola milioni 66 na kuongeza njia hadi 850,000.

Zabuni iliyokuwa na thamani ya chini, ni ile ya kampuni ya mawasiliano ya Sasktel ambao waliahidi kutoa shilingi milioni 60.5 na kufikisha njia 575,000 za mawasiliano.

Kampuni hiyo imenunua hisa hizo kwa zaidi ya shilingi bilioni 96 (sawa na Dola milioni 120). Nusu ya kiwango hicho, imetolewa kwa serikali na kilichobakia ni kwa ajili ya kurekebisha miundo mbinu na shughuli za uendeshaji.

Urekebishaji wa mtandao wa kampuni hiyo utagharimu Dola milioni 900 katika kipindi cha miaka minne na hali hiyo, italiimarisha shirika hilo kifedha na kujenga mahusiano mazuri na wateja wake.

Kampuni hiyo itakuwa ni ya nne nchini ya mawasiliano ya simu ikiwa imetanguliwa na TRITEL, MOBITEL, ZANTEL na VODACOM ambazo zote tayari zimeshaanza kazi.

Zabuni ya kuuzwa kwa kampuni ya TTCL ilitangazwa Juni mwaka 1999 na jumla ya makampuni 120 yaliomba kununua hisa hizo na zilitangazwa kupitia vyombo vya habari na mtandao wa Shirika la Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).

Zoezi hilo lilifanywa chini ya Sheria ya Kurekebisha Mashirika ya Umma iliyoanza kutumika nchini mwaka 1992 na shirika hilo ni la tatu kuuzwa kati ya yale ambayo ni nyeti kwa uchumi wa Taifa.

Mashirika yaliyotangulia ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Kitengo cha Makontena katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA).

Kabla ya kutangazwa kuuzwa shirika hilo, serikali ililivunja kutoka Shirika la Posta na Mawasiliano ya Simu (TPTC) na kuundwa kwa TTCL ambayo ipo chini ya Tume ya Mawasiliano mwaka 1994.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), John Rubambe anasema kuwa shirika hilo sasa limeuza hisa zake asilimia 35 kwa makampuni hayo ya Detecon na MSI kuanzia Februari 23 mwaka huu.

Anasema kuwa tayari serikali imeshakabidhiwa zaidi ya shilingi bilioni 48 (sawa na dola 60,000 milioni) na anatarajia kuwa kampuni hiyo itaongeza ufanisi kwa namna moja au nyingine.

Rubambe anasema matarajio hayo yanatokana na ujuzi na uzoefu walionao wanunuzi hao na anatarajia kuwa malengo ya wanunuzi hao yatafikiwa katika muda uliopangwa.

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Mark Mwandosya anasema uuzaji wa hisa za kampuni hiyo una umuhimu wa pekee katika kuleta maendeleo ya mawasiliano nchini na kuinua uchumi wa Taifa.

Anasema kuwa hatua ya serikali kuuza hisa zake ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ambayo inataka kuwepo kwa wastani wa simu sita katika kila watu 100 baada ya miaka 20 ijayo.

Anasema hivi sasa kuna wastani wa simu 1 katika kila watu 100 kiwango ambacho ni cha chini kulinganisha na nchi zilizoendelea ambapo ni wastani wa simu 35 kwa watu wanne.

Anasema zilizouzwa ni hisa sehemu tu, ya hisa za serikali katika kampuni na itaendelea kuwa katika jina lile lile la TTCL na lengo ni kuinua ushindani katika sekta ya mawasiliano na kuwaongezea wateja wigo wa uchaguzi.

Anafafanua kuwa, tume imetoa leseni kwa kampuni za simu za mkononi za Mobitel na Tritel katika maeneo fulani tu lakini, hivi sasa kampuni hizo zinatoa huduma karibu nchini nzima.

Waziri anasema hali kama hiyo ipo pia kwa kampuni ya VODACOM ambayo imepata leseni hivi karibuni na Zantel ambao kwa kuanzia, wanatoa huduma zao katika Visiwa vya Zanzibar.

Anasema kuwa hivi sasa muswada unaandaliwa ili kuwezesha kutolewa kwa leseni za huduma za mtandao (Internet).

Profesa Mwandosya anasema katika kipindi cha miezi sita hadi tisa, kampuni hiyo itakuwa imekamilisha utoaji wa huduma za simu za mikononi kwa mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Arusha.

Mikoa mingine ni Morogoro, Dodoma, Visiwa vya Zanzibar na Dar-Es-Salaam na huduma hizo zitasambazwa nchi nzima kwa gharama nafuu ambazo zitachochea ushindani na makampuni mengine ya mawasiliano.

Waziri ambaye anakiri huduma za shirika hilo kwa sasa haziridhishi, anasema kuwa kampuni hiyo imelenga kupunguza malalamiko ya wateja hususan juu ya lugha isiyo ya kiistaarabu ya maopareta wa simu.

Hali kama hiyo inakikabili pia kitengo cha mauzo na huduma na kwamba, marekebisho yatafanywa ili kujenga sura nyingine ya mahusiano baina ya wateja na kampuni.

Kupunguza gharama za huduma na kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa urahisi, kuongeza pato la shirika na kuwezesha serikali kunufaika kutokana na kodi mbalimbali zitakazotozwa ni lengo jingine la uuzaji wa hisa za kampuni hiyo.

Mwenyekiti wa MSI, Dk. Mohamed Ibrahim anasema kuwa kampuni hiyo ina miradi mingine kama hiyo katika nchi za Amerika ya Kaskazini, Ulaya na katika nchi zingine zilizo katika Bara la Afrika.

Anataja miradi mingine ya mawasiliano katika Afrika ya mashirika hayo kuwa ipo katika nchi za Misri, Uganda, Zambia, Malawi, Kongo Brazaville, Gabon, Siera Leone, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na Burkinafaso na Guinea na Niger.

Anasema mkakati wa kampuni hiyo kutengeneza mtandao wa kisasa wa mawasiliano wa GSM Cellutar na kupanua njia za mawasiliano hadi kufikia 810,000 na anawataja washirika wengine katika kampuni hizo.

Wana hisa wengine katika kampuni ya MSI na ambao watakuwa pia sehemu ya mradi huo ni pamoja na Citibank, CDC, IFC, AIG na kampuni ya vyombo vya elektroniki ya Mitsui.

Upande wa Detecon wanahisa ni pamoja na kampuni ya Deutsche Telecom, The German PTT, Deutsche Bank, Dresdner Bank na Bau-un Handelsbank.

Mwenyekiti huyo kutokana na ushirikiano huo anaamini kuwa TTCL itakuwa moja ya kampuni kubwa ya mawasiliano katika Afrika.

Detecon ina hisa katika makampuni yaliyopo katika nchini 18 duniani na mengine yanafanyakazi katika nchi za Uganda, Msumbiji, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Urusi.

Ni matumaini ya Watanzania walio wengi kuwa, kuuzwa kwa hisa za kampuni hiyo kutachochea ushindani wa kibiashara ambao utashusha maradufu gharama si za huduma tu bali hata simu zenyewe (hand set).

Pamoja na yote serikali inapaswa kuwa karibu na kufuatilia kwa makini utendaji wa wawekezaji hao kwa kuwa TTCL ni kampuni ambayo ina mtandao nchi nzima tofauti na kampuni nyingine yoyote ya mawasiliano nchini.

Lijue Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing

Utangulizi:

Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing lenye makao yake huko Tutzing Ujerumani, lilianzishwa na Padre Andreas Amrhein.

Masista wa shirika hilo wanafanya kazi hapa Tanzania katika majimbo ya Njombe, Songea, Mtwara na Lindi. Julai Mosi, 1901, masista wa shirika hilo waliwasili huko Peramiho ili kuanza kazi yao ya umisionari.

Julai, mwaka huu, masista wanaofanya kazi huko Peramiho wataadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Kazi ya Umisionari katika majimbo ya Njombe, Mbinga na Songea.

Katika makala haya, tutaeleza mwanzo wa shiririka hilo, ujio wake hapa nchini, kazi zao na maendeleo ya shirika katika kipindi cha miaka 100.

Mwanzilishi wa Shirika:

Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing, lilianzishwa na Padre Amrhein aliyezaliwa huko Uswisi Februari 4, 1844 katika kijiji cha Gunzwil.

Akiwa na umri wa miaka 18, Amrhein alikwenda Italia ambako alitumia muda wake kujifunza uchoraji. Baada ya kukaa huko miaka 20, alirudi Uswisi. Muda si muda, alienda Munich na Paris ambako alijufunza Falsafa ya Maadili.

Baada ya kupita kitambo alikwenda Tubingen, Ujerumani kuendelea na masomo yake. Akiwa huko, aliamua kukatisha masomo yake akajiunga na monasteri ya Beuron. Alipadrishwa mwaka 1872.

Akiwa safarini, Padre Amrhein alikutana na Arnolda Janssen, aliyeanzisha Shirika la Watawa Wamisionari ambao watafufua Roho ya Watawa Wabenediktini wa zamani kama akina Agustini wa Cantebury.

Yeye alitaka zianzishwe monasteri ambazo zitakuwa vituo vya Kikristo vitakavyofundisha dini, ufundi, kusoma na mbinu za kilimo kama ilivyokuwa wakati wa miaka ya kati.

Mawazo yake yalipokuwa yamekomaa, Padre Amrhein alikwenda kumweleza Katibu wa Propaganda Fide huko Roma, Monsinyori Jacobini. Katibu huyu baada ya kuyachunguza mawazo hayo, alikubali mawazo yake.

Ananunua Monasteri:

Wakati huo katika mji Regensburg huko Ujerumani, kulikuwa na monasteri ya zamani sana ambayo ilikuwa imeachwa na haikukaliwa na mtawa yeyote. Tena, ilikuwa inakaribia kubomoka.

Padri Amrhein aliamua kuinunua monasteri hiyo alipoanzisha shirika lake kisha, akatafuta vibali rasmi toka serikali ya Ujerumani, na upande wa Kanisa - Roma.

Kibali toka serikalini:

Padre Amrhein alianza kuomba kibali cha kuanzisha shirika lake toka Serikali ya Ujerumani mwaka 1883. Katika maombi yake, alitamka kuwa alitaka "kupandikiza utamaduni na Ukristo toka kwenye Seminari ya Kimisionari ya Kijerumani; kwenda kwenye nchi zisizostaarabika".

Mwaka huo, kibali hakikupatikana. Desemba 18, 1884, Padre Amrhein alipeleka tena maombi yake ya kupata kibali. Safari hii ombi lake la kupata kibali liliwekwa kiufundi hata Serikali ya Ujerumani ikakubali kutoa kibali cha kuanzisha shirika, Machi 15, 1885.

Kibali hicho kilisema kwamba, kuanzishwa na shirika la kimsionari na nyumba ya kimisonari kadiri ya ombi lake, hakuhitaji kibali toka serikalini. Jibu hilo lilimpa Padre Amrhein fursa ya kuanza kazi yake.

Aprili Mosi, 1885 katika maandishi, alianzisha rasmi Shirika la Watawa Wanaume wa Kimisionari ambao badaye waliitwa Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia.

Kibali cha Kanisa:

Baada ya kupata kibali toka serikalini, Padre Amrhein alitafuta kibali toka upande wa Kanisa.

Novemba 23, 1880 alinunua nyumba huko Emming, karibu na mji wa Munich. Mwezi Machi 1884, Amrhein akapeleka maombi huko Roma ili kupata kibali rasmi cha Kanisa ili kuanzisha shirika lake.

Juni 23, 1884 Propaganda Fide ilitoa kibali hicho naye Padre Amrhein, akataarifiwa rasmi Juni 29, 1884. Padre Amrhein, aliiona siku hiyo kama ni siku ya kuundwa kwa shirika lake.

Januari 10, 1887, mabruda wa kwanza watano toka Reichenbach, walihamia huko Emming na Januari 25, 1887, Padre Amrhein alitolea misa ya kwanza hapo Emming. Mwaka 1904 St. Ottilien, ikatambuliwa rasmi kama kijiji na jina Emming, likafa. Hapo ndipo yalipojengwa makao ya watawa na Amrhein na ndio wanajulikana hadi leo kama watawa wanaume Wabenediktini na Mtakatifu Ottilia.

Masista Wabenediktini wa Tutzing:

Padre Amrhein baada ya kuanzisha Shirika la Watawa Wanaume Wabenediktini, alitamani kuwa na watawa wa kike ambao wangesaidiana na watawa wa kiume katika kazi ya umisionari katika Afrika.

Mwanzoni, Padre Amrhein alipata wazo la kuomba masista toka shirika fulani ambalo lilikuwa limeanzishwa tayari lakini, wazo hilo halikutekelezwa.

Hii ilitokea kutokana na ukweli kwamba, wakati fulani alipokuwa katika mji wa Munich, Ujerumani, alikutana na mama mmoja kwa jina la Maria Jores, mwanzilishi wa "Marian Institute" Padre Amrhein akajaribu kumshawishi mama yule na kikundi cha wanawake wenzake, wajiunge na kazi ya umisionari katika Afrika kama Waoblati wa Mtakatifu Benediktini lakini, wazo hilo halikuzaa matunda.

Wasichana wa kwanza:

Mwezi Septemba, 1885, Padre Amrhein alipata nafasi ya kuhudhuria kongamano kubwa la Kikatoliki huko Munster, Ujerumani. Kongamano hilo lilijulikana kwa jina la "Katholikentag".

Padre Amrhein alipata nafasi ya kutoa hotuba hiyo. Alieleza juu ya nia yake ya kuanzisha shirika jipya la masista. Padre mmoja jina lake Ehring, aliposikia hotuba ya Amrhein, alimwendea akamtaarifu juu ya wasichana wanne ambao walikuwa na wito wa kwenda kwenye nchi za misioni.

Wasichana hao walikuwa na nia ya kwenda kufanya kazi ya umisonari huko India. Majina ya wasichana hao yalikuwa: Johanua Katharina, Elisabeth Siverung, Auguste Smessing na Getrud Reckers.

Amrhein alikutana na wasichana hao na akazungumza nao juu ya wazo hilo. Wasichana hao walikubali mwaliko wa kujiunga na nyumba ya kimisionari ya Amrhein huko Reichnbach.