Make your own free website on Tripod.com

IJUE AFYA YAKO

TB ya ngozi au Tezi na magonjwa mengine

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini.

Mwekee mito alalie ili sehemu ya mifupa iliyochomoza isigote na kujisugua mara kwa mara.

Mlishe chakula bora kadiri iwezekanavyo. Kama hali vizuri, mpe dawa ya vitamini ambayo itaweza kumfanya ale zaidi.

Mtoto aliye mgonjwa kwa muda mrefu, ni afadhali akumbatiwe na mama yake.

Tiba:

Fanya vitu vyote vilivyotajwa hapo juu.

Osha vidonda kwa maji ya moto yaliyochanganywa na chumvi kidogo na Hydrogen- peroxide na kisha, yahifadhi kwa kuvifunika kwa bandeji zilizo safi.

Matatizo ya ngozi za watoto wachanga

Vipele vya Nepi

Hivi ni vipele vyekundu vinavyowasha vilivyo katikati ya mapaja au matakoni mwa mtoto mchanga na husababishwa na mkojo.

Tiba:

Mwogeshe mtoto kila siku kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini.

Epuka au kuponyesha vipele hivi, ni lazima kumwacha bila nguo na awekwe kwenye mwanga wa jua.

Kama unatumia nepi, basi ibadilishe mara kwa mara. Umalizapo kuzifua, zisuuze ndani ya maji yenye vinegar kidogo.

Tumia poda ya watoto baada ya upele kutoweka.

Mba ya kichwani (Cradle Cap - Sebornhoea Dandruff)

Huu ni ugonjwa wa ngozi ya kichwa cha mtoto mdogo yenye tabaka la njano na linalotokeza. Ngozi inayozunguka tabaka hili, ni nyekundu na huwasha.

Hutokana na kutoosha kichwa cha mtoto vizuri au kukifunika mara kwa mara.

Tiba:

Osha kichwa cha mtoto kila siku. Ikiwezekana, tumia sabuni ya hexachlorophene.

Safisha vizuri ili kuondoa mba yote pamoja na tabaka lake.

Kwa kurahisisha kazi, ni afadhali kwanza kukifunga kichwa kwa taulo iliyolowekwa ndani ya maji ya uvuguvugu ili iweze kulainisha tabaka pamoja na vigamba vyote vilivyoko kichwani.

Baada ya kukiosha, kiache wazi kipate hewa na mwanga wa jua.

Usifunike kichwa cha mtoto kwa kofia au kitambaa; kiache wazi

Kama kuna dalili za kuambukiza, basi mtibu kama vile ulivyotibu Impetigo.

 

Vibaka vibaka vyekundu vyenye vilengelenge vidogo (Eczema)

Dalili:

Kwa watoto wadogo, hivi ni vibaka au vipele vyekundu katika mashavu au mara nyingine, katika mikono. Huwa kama vijeraha vidogo vidogo ambavyo hutoa majimaji.

Kwa watoto wakubwa au vijana, vibaka hivyo hivyo huwa vikavu na mara kwa mara, huwa katika sehemu ya nyuma ya magoti au katika viko vya mikono.

Havianzi kama vile ugonjwa wa kuambukiza ila, huanza kama mzio.

Tiba:

Kanda mahali penye vipele kwa maji baridi.

Kama dalili za ugonjwa wa kuambukiza zinatokea, tibu kama Impetigo.

Acha mwanga wa jua uchome kwenye vibaka.

Kama ugonjwa umezidi sana na hauponi kwa tiba iliyokwisha shauriwa, tumia dawa ya mafuta ya cortisone au cortisosteroid.

 

Psoriasis

Dalili

Mabaka manene ya rangi ya kijivu ambayo ukiyakuna hutoa vigamba vyeupe hutokea hasa katika sehemu za mwili.

Kigonjwa chenyewe hukaa kwa muda mrefu sana kisha kikatoweka na kurudia tena. Hakiambukizi wala haidhuru.

Tiba

Achia sehemu hizo zipate mwanga wa jua ambao husaidia sana.

Kuogelea ndani ya maji ya chumvi(baharini), pia husaidia.

Dawa za mafuta zilizo na corticosteroids au coaltar, zinaweza kusaidia.

Kama umezidi sana, ni heri kumwona daktari.

Kuwatenganisha wanandoa hali ndoa ingalipo (2)

Katika toleo lililopita, tulifikia katika kipengele kinachosisitiza wajibu wa mawasilianondoa katika jamii.

Sasa tunaendelea na ufafanuzi juu ya kipengele hiki kama mwandishi wetu anavyoeleza kwa msaada wa jarida la kanisa Katoliki Jimbo la Moshi.

Wanandoa wakishafunga ndoa yao kwa mujibu wa sheria, hiyo ndoa yao haiwahusu wao tu, bali inalihusu pia Kanisa lililo mwili wa Kristo na "sisi ni viungo vya mwili wake’ (Efe 5:23,30). Kwa vile ndoa ni ya "uimara" (indissoluble) na inakataa kila aina ya talaka na kisakramenti, ina uhusiano wa kiundani na Kanisa.

Wakuu wa Kanisa wanawataka kila wanandoa wanapopania kutengana, walete mashauri yao mbele ya Kanisa kwanza ili yapate kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwani ndoa zenye mzozo na migogoro zilianzishwa kwa mujibu wa sheria (MSK, K 1060).

Hata hivyo lakini, ijapokuwa Mama Kanisa anaona kuwa ni vema mashauri hayo yakatwe kiutawala au kimahakama, wakati huohuo Mama Kanisa huyohuyo anashauri kwamba wanandoa watumie kwanza mapendo ya Kikristo na hata shauri nyingine za kujaribu kupatana kabla ya kuwaendea Wakuu wa Kanisa au mahakama za kikanisa kwa suluhu (MSK, k 1446, 1676).

Wakati wa mzozo na migogoro, ni vema wanandoa wafanywe kuona hasara wanayojiletea wao wenyewe pamoja na watoto wao ambao wanapaswa kuwalea "katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo"(Efe 6:4) wasije "wakakata tamaa" (Kol 3:21).

Hakika, kuwatenganisha wanandoa siyo jambo rahisi vile na lenye matunda yanayoeleweka! Kuwatenganisha wanandoa huwaletea wanandoa wenyewe na watoto; athari mbalimbli kwa sababu hatua kama hii ni upeo wamlolongo wa matatizo mengi ya kindoa ambayo yalikuwa yakikua na kuibuka wakati mwingine kinyerenyere. (kwa pole pole)

Kwa kweli, hatua ya kuwatenganisha wanandoa mara nyingine inaweza kuwa chanzo cha kutibua matatizo kuliko suluhisho lenyewe.

Kama kweli wanandoa wanotenganishwa wanaipeda ndoa yao kufa na kupona, basi hatua ya kuwatenganisha inaweza kuwa chanzo cha kuimarisha ndoa yao zaidi kutokana na tafakuri za kunufaisha watakazokuwa wakifanya wakati wa kutengana kwao.

Lakini, kama wanandoa wanachukiana na kwa vyovyote hawaipendi ndoa yao, hatua ya kujaribu kuwatenganisha inaweza ikawa ndio mwisho wa ndoa yenyewe pamoja na athari zake.

Liwe liwalo lakini katika kuwatenganisha wanandoa, watoto wanaweza kuathirika sana.

Kwa maneno mengine, hatua nzima ya kuwatenganisha wanandoa inaweza kuleta athari za kijamii za kifamilia za kimaadili za kimalezi na hata kiuchumi. Kwa vyovyote, ingefaa sana wanandoa waishi daima pamoja bila mtengano wa aina yoyote kwa sababu ‘ mali isiyolindwa kwa ukuta, itaporwa’ (Sira 36:30a).

Kutengana kutokana na uzinzi

Ijapokuwa inashauriwa sana kwamba mwanandoa, kutokana na mapendo ya Kikristo na mahangaiko ya kifamilia waliyonayo, hapaswi kukataa kumsamehe mwanandoa mwenza aliyezini na hivi kusitisha mawasilianondoa, hata hivyo ikiwa mwanandoa huyo hajapenda kumsamehe moja kwa moja au kimya kimya mwanandoa aliyezini, yeye huyo ana haki ya kusitisha mawasilianondoa isipokuwa yeye mwenyewe awe amekubaliana na uzinzi wenyewe, au aliusababisha uzinzi huo, au yeye mwenyewe alizini.

Endapo mwanandoa mwenza hakuzini ataendelea kuwa na mawasilianondoa na mwanandoa mwenza aliyezini licha ya kujua ukweli wenyewe basi yeye huyo atachukuliwa kana kwamba amemsamehe kimya kimya yeye huyo aliyezini.

Tena, endapo mwanandoa ambaye hakuzini ataendelea kuwa na mawasilianondoa na mwanandoa aliyezini kwa muda wa miezi sita bila kuliarifu Kanisa, wala Serikali, basi yeye huyo atahisiwa kuwa amekubaliana kimyakimya na mwanandoa aliyezini.

Mwanandoa ambaye hakuzini akisitisha mwenyewe mawasilianondoa ni lazima alete malalamiko yake kwa wakuu wa Kanisa wenye mamlaka kuomba aruhusiwe kutengana rasmi na mwanandoa mwenza.

Afanye hivyo katika kipindi cha miezi sita baada ya kujitenga mwenyewe na mwanandoa mwenza. Akisha kuyapokea malalamiko, mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka husika baada ya kuchunguza makandokando yote inavyopaswa kuona kama mwanandoa ambaye hakuzini, anaweza kumsamehe mwanandoa mwenza aliyezini na hivi kuweka kando suala la mtengano unaokusudiwa (MSK, k 1152).

Kihistoria, katika mapokeo ya Kikristo na yasiyo ya Kikristo, uzinzi ni kosa kubwa sana ambalo huharibu mawasilianondoa na wakati mwingine hata kuyaficha.

Katika Sheria za Kiroma na za wengine waliotangulia, uzinzi ulikuwa kosa kubwa hasa kwa upande wa mke kwa mume.

Katika mapokeo ya Kikristo, uzinzi ni kosa kubwa la kukosa uaminifu katika ndoa ijapokuwa kosa lenyewe kama kosa, halitaliki ndoa (Mat 19:9b).

Kosa hili la kutokuwa na uaminifu linahusu pande zote mbili bila kubagua na bila kujali mhusika ni mume au mke.

"Mungu anataka nyinyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. Kila mwanaume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, na sio kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu.

Basi mtu yeyote asimkosee wala kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. tilikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo.

Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa bali tuishi katika utakatifu (1Tes 4:4-7).

"Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu (kwani) Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi"(Ebr 13:4).

Ijapokuwa uzinzi ni kashifa na kosa kubwa katika mawasilianondoa, sheria bado inataka mapendondoa ambayo ni msingi wa ndoa yenyewe yatawale.

Sheria inawataka wanandoa wawasamehe wanandoa wanaofanya uzinzi ili mapendondoa na maslahi ya watoto yapate kulindwa kweli. Mawasilianondoa yasije yakasambaratishwa na ndoa yenyewe aliyoiunganisha Mungu, isije ikafa kifo ambacho si cha kweli. Kwa kweli kabla, kabla mwanandoa hajaomba kutengana na mwanandoa mwenza kwa mujibu wa sheria, ni lazima apime sana athari za mtengano kama huo kwake mwenyewe, kwa mwanandoa mwenza, kwa watoto, kwa familia, kwa Kanisa na kwa jamii kwa jumla.

Itaendelea toleo lijalo

Utandawazi dhidi ya Utamaduni wa Afrika (4)

Utandawazi umeifanya dunia iwe kama ni kijiji kimoja. Hali hii imeifanya dunia iwe ni mkusanyiko wa kila aina ya mila na desturi. Mkusanyiko huo ni sawa na mtanziko uliomo baharini: samaki wakubwa huwameza samaki wadogo.

Vivi hivi, mila na desturi za mataifa makubwa humeza mila na desturi za mataifa madogo.

Utandawazi waweza kutazamwa katika sura zake zote mbili: chanya na hasi. Kwa upande wa sura chanya, tunaweza kunufaika kwa maendeleo makubwa ya mawasiliano duniani.

Maendeleo hayo yamepatikana kutokana na kwenda kasi kwa mafanikio katika sayansi na teknolojia. Vyombo vya mawasiliano vimerahisisha sana upelekaji na upokeaji habari kutoka upande mmoja wa dunia hadi upande mwingine.

Kwa njia ya luninga, watu wanaweza kutazama matukio mbalimbali duniani; simu za mkononi; internet; fax; e-mail na njia nyingine nyingi zimemjengea binadamu uwezekano wa kuwasiliana na binadamu wa upande wa pili wa dunia haraka na kwa uhakika.

Kwa upande hasi, maendeleo hayo huongozana na aina fulani ya sumu inayoua kwa kasi sana tamaduni za nchi za dunia ya tatu. Kwa mfano, katika programu na vipindi vioneshwavyo katika luninga nchini Tanzania, baadhi huelezea zaidi kukomaa kwa tamaduni za Ulaya, Marekani na Asia.

Haupo msisitizo wa kuendeleza utamaduni wetu. Vivyo hivyo, kwa upande wa maonesho ya sanaa, muziki, mavazi, aina ya vyakula, na aina mbalimbali za vitendeakazi. Vijana hutazama jinsi majambazi yanavyowavamia na kuwapora watu mali zao na hata kuwaua kwa silaha.

Wanawaona maninja wanavyoonesha ubabe wao. Bila kuchuja, vijana wa Kitanzania nao wanaiga na kujijengea uhalali wa utamaduni wa kifo.

Utamaduni wa kifo

Kwa kuiga kimbumbumbu tamaduni za mataifa makubwa, Waafrika wanapoteza tunu za maadili mema; na huzikana kuwa zimepitwa na wakati. Kwa jinsi hiyo, huwa wanaua misingi ya asili yao.

Wanawake walio wengi nao hupenda kuua misingi ya aina zao za nywele kwa mikorogo na kuzifanya zionekane na kukaribiana na zile za watu wa mataifa makubwa. Wanaua asili ya rangi ya ngozi zao na kuzichubua ili mradi tu, kupoteza weusi!

Wako tayari kuua mbegu na mayai ya uzazi ili waonekane ni kizazi kipya cha kileo! Aghalabu, chochote wakiangaliacho kwenye luninga kikioneshwa na Wazungu, huona ni halali.

Waafrika wako mstari wa mbele kuiga jambo lolote hata ikiwa ni kutembea uchi wa nyama mbele ya kadamnasi ya watu mradi tu, Wazungu wanafanya hivyo! Huku ni kujiua kijinsia dhidi ya maadili mema.

Utamaduni wa kifo huongozwa pia na baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa, na hivyo kuleta hofu kwa jamii. Utamaduni wa kifo, huleta gharama kubwa kwa jamii. Nani ataliokoa jahazi hili liendalo kombo?

Ulimbwende

Maonesho ya warembo ni utamaduni unaoshika nafasi ya pekee katika utandawazi. Mathalani, maonesho ya mitindo mbalimbali za mavazi hasa yale ya kike ambayo baadhi yake huonesha hadi sehemu nyeti na hivyo huwashawishi na kuwakwaza watoto waangaliapo luninga.

Imebainika pia kwamba baadhi ya picha huonesha vitendo vya ufuksa na hivyo watoto hulelewa wakiwa hawana soni. Sioni vigumu kukiri kwamba ni kutokana na ulimbwende huo, vijana wanathubutu kuwatamkia wazazi wao kwa kiburi: "Ungechelewa, ningekuzaa!" Uko wapi ule Uafrika halisi na utamaduni wake? Labda Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) litaweza kuitanabaisha jamii mwelekeo na sera endelevu kuhusu suala hilo.

Aidha, wizara inayoshughulikia utamaduni itafafanua kwa vitendo changamoto dhidi ya tamaduni za kigeni.

Kikulacho, ki nguoni mwako

Pengine ni kweli kwamba ni sisi Waafrika wenyewe tunaosababisha kudumaa kwa utamaduni wetu na badala yake kutia mwanya wa kuuenzi utamaduni mgeni. Tumeshuhudia wenyewe katika Tanzania jinsi tunavyoshabikia muziki wa wasanii wa Kongo.

Hakuna juhudi za makusudi za kuendeleza muziki kama alivyodhamiria Salum Abdallah; Mbaraka Mwinshehe; Mohamed Maneti; Marijani Rajabu; Moshi William; Muhidin Ngurumo na Saidi Mabela.

Sambamba nao hao, ni waratibu katika taarab kama vile akina Hadija Kopa; Shakila; Dick Dude; Nasma Khamisi na wengine.

Lakini, kwa nini Watanzania tunajimaliza wenyewe katika uwanja huu wa muziki? Ni kitu gani Watanzania tunashindwa kukifanya hata kuweza kuvuka hadi nje ya mipaka yetu na tukavuma kama walivyofanya akina Rwambo Makiadi; Miriam Makeba; Pepe Kalle; Awilo Longomba; Kofi Olomide; Brenda Fassie na wengie?

Ama hakika changamoto tunalopata kutoka utandawazi likitumika vizuri, tutaweza kuboresha si tu utamaduni wetu, bali pia kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Mmomonyoko wa Maadili

Ni nani wa kulaumiwa mintarafu mmomonyoko wa maadili katika familia zetu? Wakazi takriban milioni tatu na kitu waishio jijini Dar-Es-Salaam, wanafahamu jinsi ilivyo vigumu kuwaadabisha vijana katika familia zao kwa vile hupotoshwa na hali halisi ya maisha ya jiji.

Wazazi hawana tena fursa ya kukaa na kuongea na watoto wao na ile tabia ya kuwasimulia hadithi imeshinikizwa mno hata pengine imeuawa na utazamaji wa luninga, video, au usikilizaji wa redio na muziki za kileo.

Hata hivyo, Kamati ya Kuhamashisha Roho ya Umisionari inajitahidi sana katika kuwa na programu endelevu za utamadunisho wa Kiafrika kwa kushirikiana na Radio mbalimbali za Kanisa kama vile RADIO TUMAINI iliyopo Dar-Es-Salaam, RADIO MARIA iliyoko Songea, RADIO KWIZERA iliyoko Ngara katika Jimbo la Rulenge, RADIO UKWELI iliyoko Morogoro, RADIO FARAJA iliyoko Shinyanga na RADIO CHEMCHEMI iliyoko Sumbawanga.

Kuna kanda za redio takriban 55 za vipindi vya redio juu ya Sisi Sote ni Wasimisionari ambazo hupatikana kwa bei "poa" sana kutoka kwa Padre Joseph Healey MM. ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuhamasisha Roho ya Umisionari: Mission Awareness Committee( MAC) RSAT S.L.P. 5124 Dar-Es-Salaam, Tanzania. Hali kadhalika, kuna kanda za video zenye programu juu ya Amani Kwenu ambayo imekuwa ikirekodiwa na Video Tumaini chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Radio & Video Tumaini Padre Jean-Francois Galter, M. Afr. mara nne kwa mwaka (kipindi kimoja kila baada ya miezi mitatu) na kurushwa hewani na Televisheni ya CTN (Coastal Television Network). Aidha, unaweza kuulizia kutoka Radio Tumaini S.L.P. 9916 Dar-Es-Salaam.

Pia Wana-MAC kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa ngazi za kitaifa na za kijimbo, huandaa na kuendesha semina, warsha, na makongomano kwa shabaha ya kuhamasisha roho ya umisionari miongoni mwa jamii kwa kupitia taasisi mbalimbali.

Ni wazi kwamba lengo kuu la programu hizi ni kujaribu kuziba pengo linaloikabili jamii katika nchi maskini duniani kwa vile nguvu za mataifa makubwa zimefaulu kuzisambaratisha tamaduni zao na kuziacha katika simanzi isiyo kifani.

Ni sera ya Wana-MAC daima kutoa kipaumbele katika kujenga badala ya kukataza au kulaumu tu kwamba hili halifai, lile ni marufuku, au jambo hili ni potofu. MAC huwapatia jambo jingine lenye kuvutia badala ya kukataza na kuwaacha kwenye mataa.

Waamini wote wanakaribishwa kuisaidia MAC kwa hali na mali ili waweze kuliokoa jahazi hili ili, lisigonge mwamba.

Je, adui yetu ni nani? Huenda kuna adui mkubwa sana na pengine hasa, ni sisi wenyewe; nafsi zetu wenyewe; na wauaji wa maadili mema, ni sisi wenyewe.

Je, kuna uwezekano wa kufanya ukarabati dhidi ya mmomonyoko huo wa maadili? Je, kila aina ya mmomonyoko husababishwa na utandawazi?

Na huyo shetani utandawazi hawezi kudhibitiwa? Kila mmoja wetu anaweza kutafuta majibu kulingana na matatizo katika familia na jamii yake.

Viongozi kuanzia ngazi ya familia hatuna budi kuonesha mifano mizuri ili kuweza kujenga maadili mema na kukarabati mahali pale palipopata ufa au mmomonyoko na wala TUSIKATE TAMAA.

Hakika Maria Mwafrika anaelewa sala zangu kwa Kiswahili

Na. Mwandishi Wetu

Ilikuwa wiki moja kabla ya Krismasi wakati mama alipomkumbusha binti yake, Bahati, juu ya hadithi ya kuzaliwa Mwokozi. Mama huyo alichukua kadi ya Krismasi yenye mchoro wa Kizungu kutoka juu ya meza pale sebuleni iliyohusu kuzaliwa Yesu Kristo. Akasema:

"Bahati, hapa unaweza kuwaona Maria, Yosefu na mtoto mchanga Yesu. Na pia, kuna wachungaji na wanyama katika hori. Bahati anainamishainamisha kichwa kwa furaha. Hapo mama yake nae, akaendelea: "Iwapo unasali kwa Maria, Mama wa Yesu, daima atakusaidia."

Ghafla Bahati akakunja uso na kusema kwa sauti ya masikitiko: "Lakini, sidhani kama Maria mgeni huyo- Maria Mzungu huyu ataelewa sala zangu za Kiswahili!"

Mama yake Bahati akashangazwa na kusema: "Lo!" Hapo ndipo mama yake Bahati akaenda tena kwenye ile meza, akachukua kadi nyingine ya Krismasi na kumweleza: "Labda utaipenda zaidi kadi hii. Ilikuwa imechorwa na msanii mashuhuri wa Tanzania na iliyotamadunishwa kwa mazingira ya Kiafrika kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Pango la Bethlehemu lilidhihirisha kibanda cha Kiafrika kilichoezekwa kwa nyasi.

Kondoo kadha wa kadha wakigusagusa kwa pua majani makavu ambayo alilalia mtoto mchanga Yesu.

Maria Mwafrika alikaa kimya huku akipokea zawadi ya unga wa mahindi, maziwa, mafuta ya kumpaka mwanawe na kuni kutoka kwa majirani.

Naye Yosefu alikaa pembeni huku akiangalia kwa makini.

Kuku moja alikuwa anazunguka peke yake kando. Mamake Bahati akakaa akisubiri.

Ghafla, uso wa Bahati ukang’ara kwa tabasamu kubwa na akasema kwa sauti ya juu: "Ahaa! Sasa ndiyo! Nina uhakika kuwa Maria huyu Mwafrika anaelewa sala zangu za Kiswahili."

Wafiadini wa shirika la Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu watanganzwa wenyeheri

Na John Mbonde

Wafiadini watatu Jumapili hii(Machi 11,2001), wanatangazwa na Baba Mtakatifu, Yohane Paulo II, kuwa Wenyeheri. Masista hao wafiadini wote watatu ni wazawa wa Hispania, na walikuwa ni mashahidi hodari hata wakawa tayari kufa kwa kumtangaza Kristo.

Ilikuwa Julai 18,1936, wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe ilipozuka nchini Hispania na kuendelea hadi mwezi Aprili mwaka 1939. Vita hiyo, ilijihusisha na kuwatesa watawa na kuidhalilisha imani ya Kikristo.

Kutokana na vita hiyo makanisa mengi yalibomolewa na mengine kuchomwa moto na hata kuteketezwa kabisa. Maaskofu, mapadre; watawa wa kike na wa kiume, na waamini wengi, waliuawa kwa sababu moja tu, eti kwa kuwa walikuwa waamini wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya Kikristo.

Miongoni mwa kundi kubwa hilo la mashahidi, walikuwepo masista Rosaria, Serafina na Fransiska (Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu) ambao kwa wakati huo, walikuwa wakiongoza shirika lao na kamwe, hawakuogopa kukiri imani yao.

Walilazimika kuhama nyumba yao na kukimbilia nyumba nyingine ili kusalimisha maisha yao.

Mnamo Agosti 21, 1936, walikamatwa na kutumikishwa katika kazi ngumu, kupigwa na kudhalilishwa kijinsia. Siku iliyofuata, Sista Rosaria na Serafina walipigwa risasi hadharani huko Puzol (Valencia, Hispania).

Sista Rosaria hadi akiwa anakufa kishahidi, alitangaza msamaha wake kwa ushupavu. Sista Serafina kabla ya kufa; akavua pete yake mkononi na akampa mtesi wake na kumwambia, "Chukua nakupa kama ishara ya msamaha wangu kwako."

Na yule askari mtesi akaipokea akarudi nyuma kwa masikitiko akisema, "Tumemwua mtakatifu, tumemuua mtakatifu."

Naye Sista Fransiska Javier, aliuawa kwa kupigwa risasi Septemba 27, 1936, katika makaburi ya Gilet (Valencia Hispania). Bila hofu, Sista Fransiska alimwambia yule askari kabla ya kumwua kwa risasi, "Subiri kidogo nikuambie; Mungu akusamehe kama ninavyo kusamehe" halafu, akalia kwa sauti, "Salamu Kristo Mfalme", ndipo akaanguka na kukata roho.

Kwa jumla, masista wafiadini hao walionesha ushupavu katika kuitetea imani yao kwa moyo wa ukakamavu. Sista Rosaria alizaliwa Mei 13,1866 huko Soano (Santander Hispania), na alijiunga na shirika Mei 8, 1889 huko Montiel (Valencia). Aliweka nadhiri za kwanza Mei 14, 1891 kwenye Konventi ya Masamagrell na Mei 14, 1896, aliweka nadhiri za daima. Alikuwa na fadhila za upendo, upole, unyenyekevu, ukarimu na moyo wa ibada kwa Ekaristi Takatifu.

Sista Serafina, alizaliwa Agosti 6, 1872 huko Ochovi (Navarra Hispania) na alijiunga na shirika Mei 8, 1887.

Aliweka nadhiri za kwanza Mei 14, 1891 na nadhiri za daima mwaka 1896. Alikuwa mkarimu kwa wote alijaa upole na unyenyekevu, alikuwa mchapakazi hodari. Alikuwa hodari wa kusali hasa mbele ya Ekaristi Takatifu.

Sista Fransiska Javier, alizaliwa Mei 24, 1901 huko Rafelbunol (Valencia Hispania) na alijiunga na shirika Novemba 5, 1921, aliweka nadhiri za kwanza Mei 11, 1922 na za daima, Agosti 30, 1928.

Alikuwa mwangalifu, asiye na hasira na mpole. Alimheshimu kila mtu na alikuwa na utulivu na mwenye upendo mkubwa wa Ekaristi Takatifu. Alipendelea kuwakusanya vijana na kusali rozali pamoja.

Shirika la Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu lilianzishwa Hispania mwaka 1885 na Padre Mkapuchini, Mons Luis Amigo’y Ferrer (1854-1934).

"Nchini Tanzania, shirika hili lilianza kazi yake ya umisionari kule Mlali, Dodoma kwa kuendesha kituo cha watoto walemavu," alielezea Sista Mkuu Leticia wa Kihonda Morogoro.

"Pia tumefungua shule ya sekondari kidato cha I-VI kule Msolwa Mikumi, ni shule nzuri sana ambayo ina walimu hodari, na katika nyumba yetu hapa Kihonda, Morogoro, tunawalea wasichana walemavu waliomaliza darasa la saba na tunawafundisha fani mbalimbali za ufundi kwa mfano ushonaji, usukaji vitambaa, ufumaji, upishi!"

"Aidha, tunawafunza pia maadili mema yote hayo kwa miaka miwili".

Naye Sista Marihut Mosguera, alielezea kwamba baada ya muda, wanatarajia kufungua shule eneo la Kigamboni, jijini Dar-Es-Salaam.

Sista Lucina Escudelo ambaye ni Msimamizi wa Kituo cha Mazoezi ya Viungo (Rehabilitation Center) hapo hapo Kihonda, alielezea umuhimu wa kituo hicho.

Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu wako katika nchi 27 duniani wakiishi Injili kwa njia ya pekee wakimfuata Kristo fukara na mnyenyekevu na wakimtambua hasa katika neno lake msalaba na taabu.

Wanashiriki kazi ya kueneza Injili na utume wao una msingi katika maisha thabiti ya tafakari na sala ya moyo wanayotolea maisha yao kwa jamii ya watu wasiopendwa na wanaodharauliwa, masikini na vijana walio na mmomonyoko wa maadili mema kwa wagonjwa wazee na wasiojiweza, yatima na watoto wa mitaani.

Funga funga: Kituo cha wazee wasiojiweza

l Ni kielelezo cha kupotea kwa amali za utamaduni wa Mwafrika

Na Wenceslaus Bamugasheki, Morogoro

HIVI karibuni, wanafunzi wa chuo cha Mtakatifu Gaspar, kilichopo Kola Morogoro, pamoja na walezi wao, walipata fursa ya kukitembelea kituo cha kuwahudumia wazee wasiojiweza cha Fungafunga kilichopo katika manispaa ya Morogoro.

Wakiwa huko wanachuo hao walijionea jinsi wazee wanavyojiona katika hali halisi ya maisha siku hizi.

"Serikali ya zamani sio ya kisasa, maana mambo yamebadilika sana,’ alisema mzee Abubakari ambaye anatunzwa na kupata huduma katika kituo hicho.

Akiendelea kusisitiza usemi wake, alisema, "Huyu ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika hapa" alisema hayo akimwonesha mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Mponji.

"Hawa bwana walikula vizuri; walilala vizuri lakini siku hizi, mtu unakula mara moja kwa siku!" alisema kwa hasira.

Hii inaonesha jinsi wazee wasiojiweza walivyogubikwa na lindi la kukata tamaa hasa kwa kukumbuka zile jamala walizozipata zamani.

Hizo, siku hizi zimeanza kupelea, hivyo kuufanya wakati kuwa mgumu.

Alipoulizwa juu ya hali hiyo,Kaimu Afisa Ustawi wa jamii wa Mkoa, Bw.Oswin Ngungamtitu alisema ni kweli hali hiyo ipo.

Alisema, "tangu mwaka 1995 mambo yamebadilika sana;magari kwa mfano yaliyotumika kusaidia kazi mbalimbali katika idara hii tuliambiwa yauzwe," alisema.

Kuhusu chakula wanachodai wazee hao kuwa wanapata mara moja, amethibitisha kuwa ni kweli lakini alisema kinatosha.

"Chakula hicho kinachoandaliwa kinatosha kabisa."

Naye Mama Euphrasia Simba, Mhudumu Mkuu wa kituo hicho alisema kuwa hali hiyo inatokana na mpishi kuwa mmoja hivyo, kumfanya ashindwe kuandaa chakula cha mchana na baadaye cha jioni na hivyo, kuandaa chote kwa pamoja. Inasemekana wapishi walikuwa wawili lakini mmoja alikufa na hivyo hawajapata mwingine wa kumsaidia.

"Hata hivyo matatizo ya chakula wakati huu sio makubwa sana" alisema Bw. Oswin licha ya kuwa na matatizo kama kuchakaa kwa nyumba na kuharibika kwa jiko, alisisitiza kuwa kwa kipindi kirefu tangu mwaka 1995, vituo vyake vya Fungafunga na Chazi, vimekuwa vikikabiliwa na upungufu wa huduma muhimu ya chakula kutokana na wazabuni kuchoshwa na kutolipwa na serikali.

Hapo hapo amewaomba watu wenye mapenzi mema na wananchi kwa ujumla kulitupia macho suala la kuwajali wananchi wenzao wenye shida mbalimbali kama hawa wazee wasiojiweza.

"Jamii ingeona umuhimu wa kuwatunza wazee badala ya kuwatupa ovyo ovyo mitaani,’ alisema afisa huyo wa ustawi wa jamii.

Hata hivyo, tangu zamani kabla ya kuingiliwa na mawazo ya Kimagharibi na usasa (modernity); kila mtu katika jamaii alihesabika kama tunda la jamii husika.

Hivyo, jamii ilipaswa kufurahi pamoja naye kusikitika pamoja naye na kuishi katika upendo.

Ndio maana misemo kama NIPO KWA SABABU UPO, ilitumika umoja ni nguvu ni msemo wa wahenga kuhusu kushirikiana.

Inashangaza kuona jamii inaziba masiko katika kusikiliza vilio vya wahitaji na matokeo yake kuwatelekeza mitaani.

Labda hali hii inatokana na kuvunjika polepole kwa familia pana (extended family) na matokeo yake ni kuongezeka kwa familia kiini (nuclear family) mabadiliko yaliyo mazuri daima hupongezwa lakini inakuwa vigumu kwa yeyote mwenye mapenzi mema kufurahia na kushangilia mabadiliko yenye walakini.

Vile vile kuacha mambo yapite bila kujiuliza swali msingi kuwa kwanini hali hii inatokea si jambo la busara na hekima. Tunaambiwa Wagiriki walikuwa na utamaduni wa kudodosa na ndio maana waliendelea katika falsafa.

Hivyo, hatuna budi kujiuliza chanzo cha hali hiyo. Je, ombaomba amekuwa hivyo kwa hiari yake au ameshinikizwa na hali halisi ya maisha katika jamii?.

Yawezekana mtu akasema kuwa labda mali imezidi utu kwa thamani ndio maana ubinafsi umezidi kuota mizizi. Sababu hizi za ubinafsi zinapelekea kuzaliwa kwa jamii ya watu ambayo inaitwa eti ni ‘watoto wa mitaani’, ‘wazee wa mitaani’,’vijana wa mitaani’, n.k .

Hawa wamezaliwa kama binadamu awaye yote, wana baba na mama ambao nahisi hawako mitaani. Je, huko walipo wanaposikia mtoto kijana au mzee wao fulani yuko mitaani wanafanya juhudi gani kumsaidia kumrudisha kwenye jamii yao halisi?

Je wanapata faida yoyote kwa wenzao kuwa mitaani?.

Imekuwepo kasumba ya kuilaumu serikali kwa kutowasaidia watu wenye matatizo mbalimbali lakini je si wajibu wa kila mtu kumtunza ndugu yake? Haiwezekani kusema mtu fulani unamthamini wakati unamwacha apotee mitaani. Itakuaje tuishinikize serikali iwajali wale watu tusio wajali? Wazee wasiojiweza wana haki ya kutunzwa na ndugu zao kama ilivyo kwa watoto na hivyo serikali itakuwa na wajibu kwa wale ambao labda kwa namna mmoja au nyingine wametelekezwa.

Watashindikana kupata mtu wa kuwatunza, na hii ndio amali pekee ambayo Waafrika tunayoweza kujivunia.

Alipoulizwa kuhusu juhudi zinazofanywa na idara yake kuhusu kuielimisha jamii juu ya thamani ya maisha za kujaliana katika jamii hasa kwa watu wenye matatizo mbalimbali, alisema kuwa wamejihusisha na kutoa semina na warsha mbalimbali vijijini.

Aliongeza kuwa hata hivyo kabla ya kumpokea mtu yeyote hapa kwanza tunawatumia mabalozi na viongozi mbalimbali wa vijiji na kata ili wathibitishe kweli kwamba mtu huyo hana mtu wa kumsaidia.

Alisema, tusipofanya hivyo tutaleta akina ombaomba kama Matonya.’

Aidha alisema kuwa hivi karibuni amekuwa akitangaza kwenye vyombo vya habari kama vile kipindi cha Harakati na Abood Televishion kuhusu matatizo mbalimbali yanayowakabili kituoni hapo ambayo ni pamoja na kunguni na kuharibika kwa jiko lao ya kupikia.

Matatizo mengine yanayowakabili wazee hao ni pamoja na magonjwa ya viungo kama ukoma, pumu na maradhi mbalimbali ya wazee ambapo ni pamoja na upweke.

Akionesha kufurahishwa na jinsi watu mbalimbali wanavyojaribu kuitikia mwito huo, alisema, "Nashukuru chuo cha Mtakatifu Gaspar kwa msaada yao ya daima ambayo inatutia moyo" Ameitaja misaada hiyo kuwa ni nguo, sabuni, kufanya usafi kituoni hapo, chakula na kuwapa moyo wazee hao kwamba bado jamii inawakumbuka vilevile ameshukuru kandarasi mmoja ambaye hivi karibuni alitoa msaada wa dawa aina ya ‘diazone’ kwa ajili ya kuua kunguni watu wengine ambao wametoa msaada huo wa dawa ni wanafunzi wa chuo cha Mtakatifu Gaspar.

Watu wengine aliowataja ni padre aliyemtaja kwa jina moja tu la Peter kwa misaada ya dawa ya binadamu.

Aidha amewashukuru wengine ambao kwa namna moja au nyingine, wamekuwa wakijitosa kusaidia.

Ametoa ombi lake popote kuwa, wazee wasiojiweza wasisahaulike, wapatiwe mahitaji yao ya msingi kwani nao ni binadamu.

Mapema akitoa historia fupi ya kituo hicho alisema mwanzoni majengo hayo yalikuwa sehemu ya kupumzika askari walitoroka vitani (rest house) na baadaye, kwenye miaka ya 1970 kilitumika kwa ajili ya kuwatunza wazee vikongwe waliokuwa wakifanya kazi mikongeni.

Baadaye, ndipo kikafikiriwa upya na kuwa na kituo cha kuwatunzia wazee wasiojiweza na watoto yatima hasa wale waliofikia umri wa miaka kumi na kuendelea.

Hivyo kikawekwa chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii. Kituo kwa sasa kina wasiojiweza 18 ambapo wanawake ni 11 na wanaume ni 7.

Aidha, kina wahudumu 11, wauguzi 5, walinzi 2, mpishi 1, mwalimu wa kituo cha kulelea watoto 1, na dobi 2.

Kituo hiki kimejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba ambayo kwa ujumla kina ukubwa wa hekali 10.

Pamoja na hayo imebainishwa kwamba hushindwa kuitumia ardhi yao vizuri kutokana na kukosa mtaji wa kulimia.

"Hatuna mtaji wa kulimia hivyo mpaka sasa hatujapanda" alisema Bw. Oswin Ngungumtitu.

Hata hivyo, amesema kuwa juhudi zimefanywa ambapo ni pamoja na kumwandikia Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kumwomba mbegu za kupanda baada ya kutayarisha shamba hilo. Alilishukuru shirika la Red Cross Tanzania ambalo mwaka jana, lilitoa msaada wa kutayarisha shamba .

Naye Padre Reginald Mroso ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Falsafa na Theolojia cha Wasalvatoriani na Gombera Msaidizi katika chuo cha Mtakatifu Gaspar, alisema kuwa ujio wa vijana hao una lengo la kutaka kujifunza zaidi namna ya kusoma alama za nyakati na kupata changamoto ya maisha wanayoyaendea.

"Hii ni sehemu ya utume na umisionari’ alisisitiza Padre Reginald.

Pamoja na hayo, jamii ya watu wasiojiweza inazidi kuongezeka kila mwaka inaonekana kutotiliwa maanani na jamii na hivyo kusahauliwa kabisa.

Mzee Abubakari alipoulizwa kuhusu maisha alikuwa na haya ya kusema, "Sisi bwana; tumesahaulika na ndio maana tunasumbuka na kuteseka; fikiria mtu unakula mara moja tu’.

Aidha serikali kwa upande wake inatakiwa angalau kubuni mbinu za kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika vituo vya watu wasiojiweza hasa kwa kutenga bajeti inayowatosheleza mahitaji na kufuatilia kwa karibuni zaidi matumizi ya bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na kuwalipa wazabuni kwa muda unaotakiwa ili wasikate tamaa.

Hata hivyo yatubidi kujiuliza swali kuwa ni kweli kwamba jamii ya Watanzania haiwezi kuwasaidia wazee hawa mpaka iwatelekeze?

Je, omba omba na wazee hawa si wanatoka katika familia? Je watoto wa mitaani sio ni mazao ya jamii ya Watanzania? Je, ni busara kumtupa binadamu eti kwa sababu ni mgonjwa, hana nguvu au ni mzee?

Janeth: Msanii anayetamba katika kikundi cha CHEMCHEM

Na Neema Dawson

"Usanii ni mzuri sana kwa watazamaji lakini, kwa asilimia kubwa una matatizo makubwa. Ukiwa katika nafasi mbaya inayokufanya uonekana mwovu na mbaya kwa jamii kwani, wengine wanachukulia vingine. Lazima wajue kuwa msanii hapaswi kukataa sehemu anayopangiwa katika mchezo. Lazima amudu pote."

Anasema msanii muigizaji katika mchezo wa KIDEDEA unaooneshwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Msanii huyo maarufu kwa jina la JANETH, anaendelea kufafanua kuwa, awapo kanisani watu wengi humuuliza sababu ya yeye kuigiza kama kahaba.

Anadai huwajibu kuwa, hucheza sehemu hiyo ili kutoa fundisho kwa Wakristo na jamii nzima kuepuka kuishi maisha ya namna hiyo(ukahaba)bali kuishi katika usafi wa mwili na roho ukimtumainia Mungu kwa kila ulifanyalo.

MIONGONI mwa wasanii chipukizi wanaopanda chati kwa kasi hasa katika makanisa ya jijini Dar-Es-Salaam na hata kujizolea umaarufu, hutakosa kulisikia jina Janeth likitajwa.

Msanii huyu yupo katika kikundi cha sanaa cha "Chemchem Arts Promotion" chenye maskani yake jijini Dar-Es-Salaam.

Kikundi hiki ndicho kinachoonesha mchezo wa kuigiza wa "Kidedea" katika kituo cha televisheni cha ITV.

Umuonapo msanii huyo katika Luninga akifanya vitu vyake, hutakosa kuwa na kiu ya kutaka kumuona uso kwa uso ili umsimulie kwa kinywa chako na kumbainishia namna anavyovutia.

Katika mchezo huo unaorushwa hewani na ITV kila Jumamosi msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Nuru Ipembe, anacheza kama mmoja wa wasichana katika jamii ambao wanadanganywa na wanaume kwa mambo mbalimbali.

Yeye, katika mchezo huo anaigiza kama msichana ambaye anadanganywa na mwanaume aitwaye Janguo, anayemueleza kuwa hana mke na licha ya ukweli kuwa janguo ana mke na familia yake, anajaribu kumpa mahitaji kadha huku akitimiza haja zake na kuiacha familia yake(Janguo) ikiteseka kwa kukosa mahitaji.

Hata hivyo wakati bado janeth "anakimbia kimbia" na Janguo, anakumbana tena na kijana mwingine . mambo yanakuwa "mkorogo"

Msanii huyu ambaye kipaji chake kinazidi kuonesha kukua na kuwa cha hali ya juu, ni mzaliwa wa mkoani Mbeya. Ana umri wa miaka 24 akiwa mtoto wa kwanza katika familia yao ya watoto watano. Anafuatiwa na wadogo zake wanne.

Anaishi na wazazi wake eneo la Mikocheni Dar-ES-Salaam na anafanya kazi katika saluni ya PUB Hair Dressing iliyopo mtaa wa Migombani

Akielezea historia yake katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, Janet anasema kuwa usanii ni fani iliyopo katika damu yake na ndiyo sababu, hata kanisani kwake hayuko nyuma kimichezo.

Katika kanisa lake la KKKT usharika wa Msasani jijini Dar-Es-Salaam, Janeth ni muimbaji wa sauti ya pili katika kikundi cha Kwaya ya Vijana.

Anasema ni huko huko alikoanzia kushiriki michezo ya kuigiza katika mashindano yaliyokuwa yakifanyika baina ya sharika za kanisa hilo na hali hiyo, ikamfanya ajizolee umaarufu mkubwa na kumpa moyo wa kushiriki zaidi.

Alipoulizwa sababu hasa ya kujihusisha na usanii katika michezo hiyo, Nuru Ipembe(Janeth), alisema, alijitumbukiza moja kwa moja katika usanii akiwa na umri mdogo tu(hautaji).

"Nilijikuta nafarijika sana hasa kwa kuwa wazazi wangu hawanikatazi kuimba kwaya kanisani ambapo ndipo palikuwa chanzo cha kukua kwa kipaji changu. Nikaendelea na uhuru katika usanii wangu, ukawa mpana zaidi," alisema Nuru.

Anadokeza kuwa kutokana na akili yake tangu zamani kumuelekeza katika fani ya usanii na kwamba labda ndiyo ingekuja kumuokoa katika mapambano dhidi ya maisha, Nuru(Janeth), alikuwa na tabia thabiti ya kuchunguza na kujifunza juu ya maisha na historia ya wasanii mbalimbali.

Msanii huyo alisema anaigiza mchezo huo ikiwa ni njia ya kuielimisha jamii hususan wasichana (wanawake) waelewe jinsi ya kudanganywa, kurubuniwa, kutapeliwa na hata kuharibiwa maisha yao na baadhi ya wanaume.

Alisema anajua kwa kufanya hivyo, watajifunza na kuepuka mbinu hizo ambazo jamii imekuwa ikishuhudia namna zinavyotumika kuwaathiri vibaya wanajamii.

Msanii huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Janeth, alisema kuwa watunzi wa mchezo wa KIDEDEA walipoutengeneza mchezo huo, walihitaji wachezaji na ndipo waliwasiliana na viongozi wa kikundi cha kwaya ya KKKT Msasani.

Anasimulia kuwa ili kuwapata wasanii, uongozi wa kwaya Ulikagua mchezo huo kabla ya kuruhusu wasanii wake kujiunga nao.

Lengo la kufanya hivyo, lilikuwa kuhakikisha kuwa mchezo huo hautapingana na maadili ya kanisa hilo na jamii kwa jumla. Ndipo walipogundua kuwa unaburudisha, unakosoa na unaonya jamii dhidi ya maovu bila kulidhalilisha kanisa..

Analalamika kuwa ingawa michezo yao ya maigizo inaelimisha jamii, wapo baadhi ya watu miongoni mwa jamii, wengine wamekuwa wakiwachukulia vibaya na kuwaona kama waovu katika jamii. "Hii siyo kweli. Huu ni mchezo tunaofundisha jamii iepuke mambo mengi mabaya. Si kwamba ukicheza hivyo na wewe ndivyo ulivyo," alisema Janeth na kuongeza,

"Usanii ni mzuri sana kwa watazamaji lakini, kwa asilimia kubwa una matatizo makubwa. Ukiwa katika nafasi mbaya inakufanya uonekana mwovu na mbaya kwa jamii kwani, wengine wanachukulia vingine. Lazima wajue kuwa msanii hupaswi kukataa sehemu unayopangiwa katika mchezo. Lazima umudu pote."

Anasema awapo kanisani watu wengi humuuliza sababu ya yeye kuigiza kama kahaba ambapo anadai huwajibu kuwa, hucheza sehemu hiyo ili kutoa fundisho kwa Wakristo na jamii nzima kuepuka kuishi maisha ya namna hiyo(ukahaba)bali kuishi katika usafi wa mwili na roho ukimtumainia Mungu kwa kila ulifanyalo.

Anaishauri jamii kuyapokea, kuyatafakari na kuyafanyia mafunzo yote wanayoyapata katika mchezo wa kuigiza badala ya kuuchukulia tu, kama burudani. Anasisitiza kuwa lengo la sanaa hii ni kuonya na kuonyeka, kukosoa na kukosolewa na pia kuburudisha.

Msanii huyo anawashauri wasichana kuwa watulivu, waaminifu na wasijiingize katika maisha ya papara yakiwamo ya ukahaba na tamaa kwani wote wanaokubali maisha hayo, hupotea na kamwe hawashindi na huishia katika vilio vya kimwili na kiroho visivyokoma..