Makala Maalum

Homilia ya siku ya kuiombea amani Tanzania

Imetokea nini Tanzania ?

Nanyi watu wote wenye kuitakia mema nchi yetu ya Tanzania na Bara zima la Afrika kwa jumla.

Ibada yetu hii ni kwa ajili 1. Kuomboleza machoni pa Mwenyezi Mungu juu ya maafa yaliyolisibu Taifa letu hapo Januari 26 na 27, na hali nzima kisiasa na kijamii iliyotokana na maafa hayo; na 2. Kumwomba Mwenyezi Mungu atukirimie siku njema zaidi nyakati zijazo.

Tangu maafa ya tarehhe 26-27 Januari yalipotokea, mimi binafsi na pia kwa niaba ya viongozi wenzangu wote wa dini zote nchini Tanzania, nimeendelea kujiuliza kama haya hayakutupata kwa sababu labda sikutekeleza ipasavyo wajibu wangu na unabii niliokabidhiwa na Mungu?

Je, kwa dhamiri safi kabisa naweza nikasema kuwa mimi pamoja na viongozi wenzangu wote wa dini tulikuwa kama Nabii Yeremia tukaweza kusema:

"Bwana ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nchi hii na watu wake maneno hayo yote mliyosikia. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu mkaisikilize sauti ya Bwana Mungu Wenu." (26, 12-13).

Huenda ikawa pia kwamba tulishindwa kukemea maovu yaliyopelekea maafaa haya. Kwa sababu moja au nyingine, huenda tulihofia kulazimika kusema:

"Lakini kwangu mimi, natazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu, nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia. kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia."

(26:14-16)

Kwa vyovyote vile, kutokana na rehema za Mwenyezi Mungu, naamini kwamba Mwenyezi Mungu bado anatoa wasaa kwa manabii wake kuufikisha ujumbe wake wa kuinusuru Tanzania bila kuzuilika na hofu ya aina yoyote "Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima," (Yoh. 11,50).

Imetokea nini Tanzania hata tukafikia hali hii?

Kwa kifupi, mimi naamini kwa dhati kuwa hali hii imetupata kwa sababu tumeruhusu kuvunjika kwa umoja wetu; tukakuza ubinafsi unaojengwa juu ya misingi ya udini, tamaa ya mali na upupiaji wa madaraka.

Hayo mambo matatu: udini, tamaa ya mali na upupiaji wa madaraka tumeyaruhusu kukua pole pole mpaka kufikia hali tuliyonayo sasa kwa vile tuliukosa ujasiri wa nabii Yeremia katika jumuiya ya Watanzania.

a). Udini:

Minong’ono ya Watanzania kuhusu udini katika siasa unaotaka kuvunja umoja wa Taifa letu imekuwa ikikisakama zaidi chama cha CUF.

Kabla ya yote, sharti niseme kwamba huenda siyo halali kukipakizia chama cha CUF peke yake lawama hizo za udini! Kuendesha mijadala ya kisiasa ndani ya misikiti kama vile hata makanisani ni udini usiokubalika katika Taifa la Tanzania.

Lakini, vile vile viongozi wa dini kuruhusu watumike kwenye mihadhara ya kisiasa kama vile kwenye majukwaa ya kampeni za uchaguzi ni udini wenye madhara yale yale ya kuchanganya dini na siasa.

Tuanze kwa kujiuliza: ni nini hasa ubaya wa udini katika siasa? Siasa (politics) ni shughuli ya binadamu inahusu mipangilio ya mji au makao(polis) ya wanadamu. Kwa maneno mengine, siasa ni himaya ya binadamu aliye na mazuri yake lakini pia, na mapungufu yake katika mipango yake yote aifanyayo.

Dini kwa upande mwingine, ni himaya ya Mwenyezi Mungu katika ukamilifu wake wa kuwapangia wanadamu njia ya wokovu.

Kwa hiyo, ubaya wa udini katika siasa ni ile hatari ya kuweza kufanya kufuru ya kuhalalisha mapungufu na hata maovu ya kibinadamu kwa kutumia neno na mamlaka ya Mwenyezi Mungu.

Matokeo ya kufuru ya namna hiyo yamedhihirika mara nyingi katika historia ya binadamu ambapo watu wameuawa kwa jina la Mwenyezi Mungu kumbe kinachotetewa ni maslahi ya wanadamu; mara nyingi hasa katika uovu wao.

Hivi ombi langu kwa wanasiasa nchini Tanzania, jiepusheni na udini wowote ule katika harakati zenu za kisiasa. Na hapa napenda kusisitiza kwamba ninavyosema hayahusu chama cha CUF peke yake bali ni vyama vyote vya siasa nchini.

Mara ngapi nimesikia minong’ono ya migawanyiko kidini hata ndani ya chama kimoja cha siasa kama vile CCM? Minong’ono siyo tu ya mgawanyiko kati ya Waislamu na Wakristo, lakini pia kati ya Wakatoliki, Walutheri, Waanglikana n.k migawanyiko ya aina hiyo haiashirii amani.

Wapendwa Watanzania, kwangu binafsi ni vigumu sana kuweza kuthibitisha ukweli au la! wa minong’ono ya udini katika siasa ya nchi yetu. Ni katika ushirikiano wa ujumla wetu kwamba tunaweza kuthibitisha au kukanusha neno hilo.

Ni katika ujumla wetu kwamba tunakwenda makanisani, misikitini, mahekaluni na hata katika vikao vya siri vya siasa zenye udini.

Kwa upande wangu peke yangu, naweza kukemea udini katika siasa kwa misingi tu, ya minong’ono. Lakini, kwa pamoja tunaweza kujenga misingi ya uhakika ya kukabili tatizo hilo.

Tunao jukumu la kushikamana katika ukweli ili tumshinde ibilisi aliyeleta maafa katika nchi mbalimbali kwa kutumia silaha ya udini; na hivi sasa anataka kuitumia silaha hiyo hiyo dhidi ya amani ya Taifa letu.

b). Upupiaji wa Madaraka:

Ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi katika siasa ya nchi yetu, tulishuhudia mfumuko wa vyama vingi ambavyo ilikuwa siyo rahisi kubainisha tofauti ya malengo na misimamo yao kisiasa au kiuchumi.

Lengo moja lilionekana dhahiri kwa vyama vyote: kufanya kila njia kuingia Ikulu, hivi tuliweza kuona uhamiaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda chama kingine kadiri ya ukubwa wa uwezekano wa kuingia Ikulu.

Sasa, kwa bahati mbaya Tanzania kama Jamhuri ya Muungano, inayo Ikulu moja tu yenye mlango mmoja tu wa kuingilia. Nayo Zanzibar pia inayo ikulu moja bila mlango wa uani au wa jikoni wa kuingilia.

Vyama kumi na vitatu vikawania kuingia vyote kwa wakati mmoja kwenye milango hiyo mmoja mmoja, ni hakika kutakuwa na ushindani mkubwa wa mbio tena wenye faulo nyingi za kutiana mieleka.

Na yule aliyefaulu kupenyeza kwenye mlango wa kuingia ndani si budi atapigiwa kelele za faulo na hata kujaribu kulazimishwa atoke nje kwa mashindano mapya.

Sasa tofauti na nchi zilizokwisha imarika kiuchumi na kimaendeleo kama Italia inayoweza kubadilisha serikali ya nchi kila miezi michache, nchi zinazoendelea kama Tanzania yetu, haziwezi wala kujimudu bila serikali kwa muda mrefu wala kukabili gharama za kubadilisha serikali kila baada ya miezi michache.

Kwa hiyo: Tujitahidi sana kubainisha malengo ya vyama vyetu kiuchumi na kimandeleo kusudi wananchi wanapopiga kura kuwachagua viongozi, wawe na mwanga zaidi kuhusu nini wanachokichagua.

Kwa maneno mengine, malengo wazi ya vyama vya siasa yawe ndiyo misingi uchaguzi. Haitalazimika tena mieleka katika kimbilio la kuingia Ikulu.

Hapa ningependa kuongezea neno moja hususani hali ya kisiasa nchini mwetu wakati huu; wazo la kurudia Uchaguzi Visiwani Zanzibar.

Katika lugha ya Kiswahili tunao msemo wa busara sana usemao, "Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo." Katika madai ya sasa ya kurudia uchaguzi inadhihirika kwamba hekima ya msemo huo ni mdomo tu; wala siyo sehemu halisi ya utamaduni wetu.

Kwa bahati mbaya, hii inajidhirisha siyo kwa Tanzania peke yake, bali kwa nchi nyingi barani Afrika. Nafikiri mwanafalsafa aliyesema Waafrika tuna zamani ndefu ambako tunajaribu kurudi daima kuliko kutafakari vipi tuboreshe siku zijazo, alikuwa na ukweli mkubwa.

Badala ya wanasiasa wetu kujiandaa vema zaidi kwa siku zijazo, wanang’ang’ania, kurekebisha yaliyopita. Na katika kufanya hivyo, wanajikuta wanafanya uhakika wa usalama kwa hali ya kesho kuwa ngumu zaidi na zaidi.

Kuliko kudai kurudia uchaguzi ningewaomba wanasiasa wetu watafakari zaidi juu ya namna gani uchaguzi ujao unaweza kuwa bora zaidi. Angalau katika neno hili, wanasiasa wa Tanzania wanayo makubwa ya kujifunza kutoka kwa wenzao wa Marekani ambao pamoja na kutoridhika na mwenendo wa uchaguzi uliopita, wanasonga mbele kwa utulivu wakijiandaa vema zaidi kwa siku za mbele wakitilia maanani zaidi manufaa ya maendeleo ya nchi yao kwa ujumla kuliko heshima ya kukaa katika Ikulu ya Washington.

c). Tamaa ya mali:

Ni jambo la kusikitisha sana kusikia kwamba maafa ya Januari 26 na 27 yalikwenda sambamba na ukodishaji wa vijana wetu kwa kutumia fedha za nje ili kuwafanya watende ambayo yalitendeka.

Hii inakumbusha historia ya kuhuzunisha ya biashara ya utumwa ambapo wafanyabiashara hiyo haramu, waliwatumia viongozi wa Kiafrika wawatoe watu wao kupelekwa utumwani kwa faida ya vitu duni kama bangili na shanga.

Nawaomba wanasiasa wetu waepuke kwa kila hali kuwarudisha Watanzania katika kipindi kipya cha kuwa watumwa wa watu wa nje.

Kwamba duniani bado wako watu wenye hamu ya kuwafanya binadamu wenzao kuwa watumwa ni ukweli ulio dhahiri kabisa.

Inatosha kutembea katika miji mingi mikubwa ya Ulaya kujionea ukweli huo kwa kuwaangalia wasichana na wanawake wengi wa nchi maskini wanavyolazimishwa kuitoa miili yao itumike kwa uchumi wa matajiri wao.

Jambo la muhimu kwa wanasiasa wetu kulifanya, ni kupanga mikakati kuujenga uchumi wetu jinsi watu wetu wasijisikie kulazimika kuchagua kati ya kupata unafuu wa maisha kwa kuwasaliti ndugu zao au kubaki pamoja na ndugu zao na kuendesha maisha duni.

Na mbinu hizo hazitazaa matunda yoyote iwapo zitaruhusu hata kwa muda mfupi kuwaweka Watanzania rehani kwa matajiri wa dunia hii.

Tamati:

Naomba nimalizie homilia yangu kwa kusema kwamba yote niliyoyasema, nimeyasema kwa moyo mnyoofu kabisa machoni pa Mungu wangu kwa manufaa ya ndugu zangu Watanzania wote.

Yawezekana yakakubalika au yasikubalike kwa mtu yeyote.

Ombi langu ni kwamba kwa yeyote kuchukua msimamo wa kuyapokea au kuyapuuza niliyoyasema, ni vizuri kwanza kuyatafakari pia kwa dhati mbele ya Mungu wake. Ikiwa Mungu wake anadai tafakari hiyo iendane na kuchinja Mbuzi au kuku mweusi, asisite kufanya hivyo.

Jambo la maana ni kwamba hiyo tafakari isifanywe mbele ya ibilisi. Kama tulivyosikia katika Enjili tuliyoisoma katika ibada hii, "Ibilisi asemapo uwongo, husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo.’ Hivi ukifanya tafakari yoyote mbele ya ibilisi yeye hatashindwa kukuhadaa.

Mwisho wa kudaiwa na ibilisi daima ni mauaji; kwani "yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo".

Tumsifu Yesu Kristu

Polycarp Kardinali Pengo

BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA

TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA KUHUSU HALI YA SASA YA NCHI YETU

Ndugu Watanzania na Watu Wote Wenye Mapenzi Mema,

Sisi Maaskofu tuliokutana katika mkutano wetu wa kawaida wa Kamati Tendaji kuanzia tarehe 21 - 23 Februari, 2001 Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar es Salaam, tunatoa masikitiko yetu makubwa kwa yale ambayo yametokea tarehe 26 na 27 Januari mwaka 2001. Watu wasiopungua ishirini na watatu walipoteza maisha yao na wengi kujeruhiwa kutokana na ghasia zilizofuatia maandamano ya kisiasa yaliyokuwa yamezuiliwa na Serikali. Vile vile tunatoa pole kwa wafiwa, walioumia, wanaoendelea kuhangaika na waliogubikwa na giza la simanzi. Aidha, tunaunga mkono tamko lililotolewa na viongozi wa dini tarehe 8 Februari, 2001 kuhusu hali ya siasa nchini Tanzania.

Tuonavyo sisi, tukio hili limesababishwa na mambo mbalimbali ambayo ni pamoja na hisia za kihistoria, kukosekana kwa mazungumzo ya wale wote waliohusika, kutoaminiana, kutokubali kuwa wote ni watu wa nchi moja, kughiribiwa kwa urahisi kutokana na watu kutojua kwa undani mambo yanavyokwenda na umaskini.

Sababu nyingine ni kuwa Watanzania wengi hawajauelewa barabara mwenendo wa demokrasia ya vyama vingi. Hali hii inasababisha baadhi ya watu kuona kuwa kutokubaliana au kuhitilafiana katika jambo fulani la kisiasa ni uasi au uadui. Kwa hiyo sisi Maaskofu:

* Tunatoa wito kwa watu wote wanaohusika na wale wenye mapenzi mema na nchi yetu kutafuta mbinu na namna ya kurejesha hali ya maelewano. Tunasisitiza rai ya viongozi wa dini kwa serikali na viongozi wa vyama vya siasa kutumia njia ya kukaa na kufanya mazungumzo kwa pamoja mara kwa mara kwa lengo la kumaliza tofauti zao. Katika kutafuta maelewano, makundi mbalimbali ya jamii yahusishwe kwani yana haki na wajibu huo katika jamii. Swala la kujenga nchi yetu ya Tanzania kwa utulivu na amani linawahusu wananchi wote.

* Tunataka ukweli utafutwe na mambo yote yawekwe bayana. Wale wote au yeyote yule anayetaka au kusababisha machafuko kutoelewana, awajibishwe kwa mujibu wa sheria za nchi.

* Tunaomba itengenezwe mipango yenye mikakati ya kweli na thabiti ya kufuta umaskini na kuongeza nafasi za kazi kwa vijana.

* Tunaomba viongozi wa dini, serikali na makundi mbalimbali kuweka juhudi za dhati za kuunda Taifa moja, na kujenga uzalendo, mshikamano na upendo.

* Tunaomba elimu ya uraia iimarishwe na ipewe msukumo mpya.

* Tunawataka watu wanaotoka nje na vyombo vya habari watoe maoni na ushauri sahihi kulingana na ukweli juu ya matatizo yetu. Hii itaepusha kuwachanganya na kuwachochea watu. La sivyo, maoni ya juu juu kuhusu matatizo yetu yanaweza kuwa kama kumwaga mafuta ya petroli katika moto.

* Tunawataka viongozi wawe karibu na watu wakati wa raha na dhiki.

* Tunawaomba watu wasiongozwe na jazba bali busara itumike kwa wakati wote wanaposhughulikia masuala ambayo ni ya kisiasa na yale ambayo yanaweza kuhatarisha amani.

* Tunaomba vyombo vya dola vielimishwe vizuri na kufundishwa mbinu za kisasa za kushughulikia ghasia na machafuko wakizingatia utu na uungwana wa raia.

* Tunatoa wito kwa waamini wa madhehebu na dini zote kufunga na kusali kwa ajili ya amani na utulivu na tuwe na huruma ya kuwasaidia wale wote walio na shida.

* Tunawaomba watu na viongozi wote kusamehe na kusahau yale yote yaliyotokea na kuanza kulijenga Taifa letu pamoja ambalo limepata doa kubwa.

"Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu" Mt. 5:9.

Mungu Ibariki Tanzania.

Tamko hili limetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tarehe 23 Februari,

Askofu Severine NiweMugizi,

Rais wa TEC

As001.