Ijue Afya yako

Mitishamba na imani za uchawi (4)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini na mahali ambapo si rahisi kumpata mtaalamu wa afya kwa haraka

Angel’ s Trumpet, Datura Arborea

Majani ya mmea huu na mengine ya jamii ya night shade, ina dawa yenye kutuliza tumbo la kunyonga au kuuma.

Chukua gudulia lenye maji kiasi cha vijiko vya mezani saba kisha, saga majani mawili ya (angel’s trumpet) na changanya na maji hayo.

- Acha yatulie kwa muda wa siku moja.

Kipimo kama matone kumi hadi kumi na tano kila baada ya saa nne kwa mtu mzima.

ONYO: Angel’s trumpet ina sumu kali kama unazidisha kipimo chake.

Afadhali kutumia vidonge kama inawezekana.

- Ndevu za Mahindi

Wakati mwingine, mtu akinywa maji yaliyochemshwa pamoja na ndevu za mahindi yanasaidia kupunguza uvimbe wa miguu hasa kwa akina mama wajawazito.

Chemsha mkono mzima wa ndevu za mahindi kisha, tumia kama glasi moja au mbili.

Haina hatari yoyote.

- Cardon Cactus (Pachicerins pectin - Orborginium)

Maji vya (cactus) hutumika kusafishia vidonda hasa kama maji yaliyochemshwa hayapatikani.

Kipande chake pia husaidia kufunga kumiminika kwa damu.

Kata kipande cha mti huo kwa kisu safi na kifunge vizuri penye donda livujalo damu.

Baada ya saa kama mbili au tatu, kiondoe kipande hicho cha mti na safisha donda hilo kwa sabuni na maji yaliyochemshwa.

- Papai

mapapai yaliyoiva yana vitamini nyingi sana na pia yanasaidia kuyeyusha chakula tumboni.

Hivyo, yanasaidia watu wanyonge na wazee walio na matatizo ya tumbo hasa baada ya kula nyama na mayai.

Mapapai husaidia vyakula hivi kulainishwa vizuri.

yanasaidia pia kuondoa minyoo, ijapokuwa dawa za kisasa ni bora zaidi.

Kusanya utomvu, pata vijiko vya chai vitatu au vinne.

Ichanganye na asali ndani ya kikombe chenye maji ya moto.

Ikiwezekana, inywe pamoja na dawa ya kuharisha.

Mitishamba ya kubandika ili kushikiliza mifupa iliyovunjika

Huko Amerika ya Kati, kuna mimea ya aina nyingi kama vile 'Tepeguaje' (mmea wa jamii ya maharagwe) na solda con solda' (aina ya mmea mkubwa ambao hutambaa katika miti) ambayo utomvu wake hutumiwa kwa kutengenezea vibandikizo vya miguu au mikono ili kushikiliza mifupa ilivyovunjika.

Hali kadhalika, unaweza kuganda vizuri na kutumika namna hiyo mradi tu, usichubue ngozi.

Jaribisha mimea ya namna hiyo katika mazingiria yako.

Kwa kibandiko cha kutumia 'tepefuaje',

chukua kilo moja ya maganda na ichanganye kwenye maji kiasi cha lita tano na chemsha mpaka imebakia kiasi cha lita mbili.

Chuja na chemsha tena mpaka utomvu utoke.

Tumbukiza kitambaa safi kama vile bandeji kisha, kitumie kama ifuatavyo:

-Rekebisha mifupa ili ikae sawa.

-Usiweke kibandiko kigusane na ngozi ila zungushia kwanza kitambaa chembamba katika mkono au mguu.

 

Kisha juu yake, zungushia pamba au sufi. Juu yake sasa zungushia bandeji iliyo na huo utomvu. hakikisha kuwa hakukaza sana. Acha ikauke.

Ni lazima kibandiko hicho kifunike mkono au mguu ili sehemu ya mfupa uliovunjika isiweze kuchezacheza na hakikisha kuwa, kiungo cha juu na cha chini ya mkono uliovunjika. havichezi. Kwa mfano:

Kama kiwiko cha mkono kimevunjika, hakikisha kuwa bandiko limezungushiwa karibu na mkono mzima kama vile inavyoonekana

Hakikisha vidole havikufunikwa vyote ili uweze kuona kwamba vina rangu nzuri ya kawaida.

Ilani:

Hata kama bandiko (cast) halikukaza sawasawa, palipovunjika panaweza kuvimba baadaye na kulifanya likaze. Kama mgonjwa analalamika kuwa bandiko hili limekaza sana, au vidole vimekuwa baridi, vyeupe au vyeusi, haraka ondoa bandiko hilo na kuweka jingine lililolegea.

Ni mwiko kuweka bandiko juu ya bandiko jingine au juu ya kidonda.

Dawa za kuinika, kuharisha na kulainisha choo

matumizi na miiko yake.

Watu wengi wanatumia dawa ya kuinika na kulainisha choo kupita kiasi.

Nia ya mtu kupata choo, inafahamika ulimwengu mzima.

Dawa za kuinika na kuharisha, zinatumika sana majumbani na mara kwa mara zinaleta madhara.

Watu wengi wana imani kuwa, homa na kuharisha vinawezaa kuondolewa kwa kutumia dawa za kuinika au kuharisha lakini, matumizi ya dawa za namna hiyo huongeza madhara zaidi katika utumbo ulio na ugonjwa.

Mara chache sana dawa za kuinika na kulainisha tumbo zinasaidia. Mara nyingi zinaleta madhara hasa kama dawa hizo ni kazli

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza - Tanzania Bara (10)

6:3 Wajibu wa Jamii kwa jumla:

Kwa upande mwingine, jamii nzima kwa jumla inapaswa kuangalia suala hili katika ngazi mbili kwa kulenga kupunguza msongamano magerezani na pili, kulenga kupunguza matatizo yanayokabili Magereza na wafungwa hivi sasa.

Kama hatua ya kwanza, raia wote tunapaswa kujiepusha na uhalifu ili tusiyajaze Magereza kwa wale walio gerezani wawe tayari kubadilika na kurudi uraiani wakiwa raia wema badala ya kurudi kifungoni mara kwa mara. Hapa, vyombo vya Mahakama, Polisi na Magereza vinatakiwa kushirikiana na kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa vile ushirikiano huo unaweza kuchangia kuondoa mapungufu yaliyopo.

Katika kukabiliana na hali iliyopo sasa tunapaswa kuelimishana na kuhamasishana ili sehemu kubwa ya jamii ilielewe vema suala hili.

Kisha, tuwe tayari kutoa huduma hasa za ushauri nasaha na wa kiroho kwa wafungwa na kusaidia kupatikana vitu mbalimbali vinavyokuwa na upungufu mkubwa magerezani mfano; sabuni, dawa za mswaki na miswaki pamoja na viatu.

Ndugu, jamaa au marafiki na mashirika ya kujitolea, wanaweza kusaidiana na serikali kuhakikisha vifaa hivi vya msingi wanapatiwa wafungwa bila kusubiri serikali ifanye kila kitu wakati tunaelewa majukumu ya serikali ni mengi na uwezo wa kuyatekeleza yote kwa wakati mmoja ni mdogo.

Jitihada za pamoja za jinsia hii zinaweza kuwasadiia wafungwa kujisikia kuwa wananchi wenzao wanawajali na kuwathamini, na hii inaweza kuchangia kubadilisha tabia na mienendo ya kihalifu miongoni mwao.

Mwisho, jamii inapaswa kuchukua hatua za makusudi kuanzisha NGOs zitakazoelekeza nguvu zake katika kuwasaidia wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo vyao au waliomaliza vifungo ili waweze kuanza maisha mapya yenye matumaini.

Kama hatua za awali, inawezekana kabisa kuanza kuandaa mahali pa kufikia wafungwa wale waliokaa magerezani kwa muda mrefu na ambao wanahitaji ‘orientation’ ya maisha ya nje ya Gereza kabla ya kurejea moja kwa moja kwenye jamii.

Sehemu za aina hiyo katika nchi nyingi duniani hujulikana kama Halfway houses’.

Serikali kwa upande wake, isaidie katika kuwahamasisha wananchi kujihusisha zaidi na urekebishaji wa wahalifu badala ya jukumu hilo kuonekana ni la Magereza pekee.

Kwa mtizamo huu huu, ni vema pia taasisi za elimu ya juu hapa nchini zifikirie kuanzisha programu za utafiti kuhusiana na masuala ya uhalifu na kuishauri serikali na jamii kwa jumla namna nzuri zaidi ya kukabiliana na ongezeko la uhalifu nchini bila kusahau kwamba wahalifu ni matokeo ya mfumo wetu wa uchumi na maisha kwa ujumla.

......Mwisho.....

KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA -TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufa zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hayakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zadi kiu yao. Sasa, tunaongezea chapisho jingine la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambaco tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania. nacho, tunakichapa kama kilivyovyotolewa na Tume ya haki na Amani(TEC), tukianza na dibaji iliyooandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta ikifuatiwa na utangulizi

Dibaji

KATIKA dola yoyote ile kuna vyombo vikuu vitatu ambavyo vinaihimili. Vyombo hivi ni Bunge, Mahakama na Utawala.

Kila chombo katika hivi vitatu kina majukumu yake maalumu.

Kwa upande wa Bunge kazi yake ni kutunga sheria kwa kuzingatia maoni ya wananchi wanaowawakilisha.

Kazi ya kuzitafsiri Sheria zinazotungwa na Bunge na kuamua migogoro inayojitokeza katika jami ni ya Mahakama.

Utawala kwa upande wake una jukumu kubwa la kutoa maamuzi na kusimamia utekelezaji wake.

Lililo la muhimu kwa vyombo vyote hivi vitatu ni kutambua kuwa vinapaswa kufanya kazi zake kwa lengo la kuhudumia watu.

Mbali na vyombo hivyo pia zipo taasisi nyingine na vikundi mbalimbali katika jamii ambavyo navyo, vina wajibu wao maalumu katika ujenzi wa jamii yetu.

Makundi na taaisisi hizi ni pamoja na Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Ushirika, Vyama vya Siasa na Jumuiya za Dini zote.

Vyombo hivi vikuu vitatu yaani utawala, Bunge na Mahakama pamoja na Taasisi mbalimbali na vikundi vilivyomo katika jamii vinapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana ili Taifa liweze kuwa na amani na kupiga hatua ya maendeleo.

Hii si nadharia tu bali imeingia katika hatua ya utekelezaji. Kwa miaka kadhaa sasa vikundi mbalimbali vimekuwa vikishirikiana katika utekelezaji wa programu zake.

Hapa nitapenda kuweka bayana kuwa kijitabu hiki KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO, kimeandaliwa kwa msaada wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ikiwa ni sehemu ya shughuli zake ambapo wameona ili waweze kutoa huduma iliyokusudiwa ni vema kushirikiana na Idara ya Mahakama.

Kijitabu hiki ninaamini kitakuwa ni msaada mkubwa katika kuboresha utendaji wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo Nachukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa jitihada hizi na pia natoa wito wa pekee kwa vikundi vingine katika jamii yetu kujitokeza kushirikiana na Idara ya Mahakama ili kusaidia katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kutetea haki za watu.

Moyo huu wa ushirikiano ni dalili njema ambayo inaonesha kuwa kila mmoja ana nia ya kushirikiana katika ujenzi wa Taifa letu, kulinda uhuru wetu na haki kwa kila Mtanzania.

Ni kwa njia hii ya kushirikiana ndipo tutaweza kufanya kazi kwa pamoja kudumisha haki na amani kati yetu na hii ndio njia pekee ya kutuwezesha kuishi kwa pamoja na kwa furaha.

 

Jaji Barnabas Samatta

Jaji Mkuu wa Tanzania

7 Februari, 2001.

Kuwa makini kuijua Biblia(7)

18. Vitabu vya Historia na Kitabu cha Matendo ya Mitume vyahusiana namna gani?

Kama vile ukuta unavyosimama juu ya msingi, ndivyo vitabu vya makundi haya mawili yanavyosimama juu ya Torati na Injili. Kwa vipi? Vitabu vya Historia huendeleza Historia ya Agano la Kale toka pale vilipoachia Vitabu vya Torati.

Hali kadhalika, kitabu cha Matendo ya Mitume kinaendeleza masimulizi toka pale zilipoachia Injili.

Licha ya kuendeleza masimulizi, vitabu hivyo vinategemea misingi ile ile ya imani iliyotamkwa katika vitabu vya Torati na Injili.

Watu walioishi katika kipindi cha Historia ya Agano la Kale walipongezwa au walilaumiwa kadiri walivyoshika au walivyovunja amri zilizotolewa katika Torati.

Watu waliohubiriwa na Mitume walielezwa habari za Yesu Kristo aliyekuwa kiini cha matukio yaliyosimuliwa katika Injili.

Kwa namna hiyo vitabu vya jozi hii ni kama Ukuta wa Biblia.

19. Je, Vitabu vya Manabii na Barua za Mitume vinahusiana kwa

namna gani?

Manabii waliishi na kufanya kazi zao katika kipindi cha historia iliyosimuliwa katika vitabu vya Historia. Hali kadhalika Mitume waliishi katika kipindi kilichosimuliwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Tumekwishaona katika swali la 8 na la 14 vitabu vya Manabii na Barua za Mitume vinahusu nini. Hebu turudie kwa mhutasari tu. Vitabu vya makundi haya mawili vinakosoa, vinaonya, vinafariji na vinazipongeza jamii za waamini walioishi sambamba na Manabii na Mitume.

Manabii waliwahubiria ana kwa ana waamini wa nyakati zao wakawakumbusha imani na maadili waliyopaswa kuyashika. walakini Mitume walitengwa kwa umbali toka jumuiya zao, hivyo walitumia barua kuwasiliana na jumuiya hizo ili kutatua migogoro na kuyaweka sawa masuala mengine.

Kwa hiyo, mahubiri ya Manabii na Barua za Mitume, yote yamekuwa vitabu vyenye ujumbe uliolinda na kuhifadhi jumuiya ili zisimomonyoke kiimani, kimaadili na kinidhamu.

Kwa uhusiano wa namna hiyo, vitabu vya jozi hii hii ni kama Paa la Biblia.

20. Katika jozi ya mwisho, vitabu vya Hekima na kitabu cha Ufunuo vinahusiana kwa vipi?

Kazi ya kulikamilisha jengo inarudiwa katika sehemu zilizojengwa tayari. Ukuta hupakwa rangi paa linawekewa dari, madirisha huwekewa mapazia na madoido mbalimbali hungizwa ndani ya jengo.

Vitabu vya Hekima na Ufunuo hurudia na kukazia mafundisho makuu yaleyale ya Torati na Injili ambayo yalirudiwa pia katika vitabu vya Historia na kukaziwa tena katika vitabu vya Manabii na Mitume.

Baada ya kukamilishwa kiimani, muumini anatafuta mbinu za kuendana vizuri na watu wa nyadhifa mbalimbali na mbinu za kufanikiwa maishani kwa jumla. Vitabu vya Hekima hutoa mbinu katika masuala hayo kitabu cha Ufunuo nacho kinatoa ushauri kwa waumini namna inavyowapasa kuyachukua mateso na kuyavumilia katika ulimwengu huu. Kwa namna hiyo vitabu vya Hekima na kitabu cha Ufunuo ni kama Ukamilisho wa Biblia.

Hapo zamani,Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii lakini siku hizi za mwisho amesema nasi kwa njia ya Mwanawe.

Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliuumba ulimwengu akamteua avimiliki vitu vyote

Ndoa

6. Yafaa ieleweke kwamba ndoa halali batili inayoponywa kutoka shinani haiponywi kutokana na fadhili inayotolewa na Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka.

Zaidi, inaponywa kwa njia ya ukubalindoa wa wanandoa wenyewe. Inachofanya fadhili uponyi hii ni kuondoa vizuizi na vizingiti vyote.

Hatua ya kuponya ndoa halali batili kutoka shinani ni fadhili inayotolewa na mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka na hakuna anayeweza kuidai kama haki inayompasa.

Kwamba katika kuponya ndoa halali batili kutoka shinani, yatokanayo na ndoa kweli huchukuliwa kana kwamba yalikuwako tangu siku ile ndoa halali batili hiyo iliposhuhudiwa.

Hili ni suala la uwanja wa kisheria ambamo hisia na mabuniko huzingatiwa ili haki na huruma ya Kikristo vipate kutendeka.

Katika kuponya ndoa halali batili kutoka shinani, Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka ni lazima awe mwangalifu sana na mwenye busara kila anapotoa fadhili hii kwa hisani yake.

Jitihada zinazopita kipimo katika kujaribu ‘kuweka sawa’ ndoa halali batili kwa kuziponya kutoka shinani, zinaweza wakati mwingine kusababisha zaidi maombi ya kutaka ndoa kama hizo zibatilishwe.

7. Wakati wa kuponya ndoa halali batili kutoka shinani, siyo lazima wanandoa husika wawepo.

Na kwa kweli wanandoa kama hao mara nyingi hawapo! Katika hali zisizo za kawaida, kuponya ndoa halali batili kutoka shinani kunaweza kukawa si kamili- yaani, yatokanayo na ndoa kweli hayarudi nyuma hadi siku ile ukubalindoa halali batili ulipotolewa.

Hali kama hii hutokea ukubalindoa wa ndoa halali batili unapotolewa baadaye na siyo siku ile ndoa halali batili iliposhuhudiwa.

Katika hali kama hii, ni vema Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka anayeponya ndoa halali batili husika, aseme uponyi ndoa huo unaanza lini hasa.

Kinadharia kuponya ndoa halali batili kutoka shinani, kunaweza pia kufanyika baada ya mmojawapo wa wanandoa husika kufariki.

Lakini, ijapokuwa katika hali kama hii ndoa halali batili husika haiponywi kwa vile mwanandoa jozi mmoja amekwisha kufa; hata hivyo, yatokanayo na ndoa kweli kama vile uhalalishaji wa watoto, husababishwa.

Kuponya Ndoa Halali Batili kutoka Shinani kutokana na ukubalindoa Kasoro

8. Kuponya ndoa halali batili kutoka shinani hakuwezekani endapo ukubalindoa wa mwanandoa au wanandoa husika haukuwepo. Ukubalindoa kama huo inawezekana haukuweko tangu ndoa halali batili iliposhuhudiwa au, ulitolewa tangu mwanzo lakini baadaye, ukasitishwa.

Lakini hata hivyo, kama ukubalindoa ulikuwa hauko tangu mwanzo lakini baadaye ukatolewa, basi ndoa halali batili hiyo inaweza kuponywa kutoka shinani tangu wakati ule ukubalindoa ulipotolewa (MSK, k 1162)

9. Endapo ukubalindoa wa awali ulikuwa batili kutokana na vitu kama vile kujisingizia(MSK, k 1101), shinikizo na hofu nzito (MSK, k 1103), au sharti batilindoa (MSK, k 1102), ndoa halali batili haiwezi kuponywa kutoka shinani mpaka hapo vitu kama hivyo vitakapoondolewa.

Ili ndoa kama hiyo ipate kuponywa kutoka shinani, ni lazima ukubalindoa uliotolewa uwe uko.

Ukubalindoa ambao ni kasoro kutokana na mmojawapo ya sababu zilizotajwa hapo juu, hauwezi kuponywa kutoka shinani na kufanywa kuwa kweli kwa sababu kuponya ndoa halali batili kutoka shinani kwenyewe hakuchukui nafasi ya ukubali ndoa husika wala hakuondoi kasoro.

Kasoro hiyo inaweza tu kuondolewa na mwanandoa au wanandoa husika.

Kwa hiyo, kasoro inapaswa kuondolewa kwanza kabla ya ukubalindoa halali batili haujaponywa katoka shinani.

Ijue Imani Yako

Shetani mwongo: lakini,chunga tamaa za mwili na nafsi yako

Na Francis Rutaiwa (PhD).

TANGU Mwanzo, Sisi wanadamu tuna matatizo kukubali kwamba sisi tumeumbwa, ni viumbe. Ingawa tumependelewa kuumbwa kwa mfano wa Mungu, lakini bado sisi tumeumbwa tu.

Yaani tumefanywa kuwepo kwa utashi na makusudi ya mwingine, na tunaendelea kuishi kadiri tu Mungu anavyoturuhusu.

Hii hali ya utegemezi na kuwekewa mipaka inatuudhi na inaamsha ndani mwetu upinzani mkali.

Hasa tamaa ya kujitawala bila mipaka ndiyo iliyovutia shetani toka mwanzoni kutunyanyasa sisi wanadamu.

"Mtakuwa kama Mungu"(Mwa 3:5). Nyoka (yaani shetani) alisema, Adamu na Eva wakapokea hiyo ahadi ya uongo na upuuzi, wakapinga Neno la Mungu, wakachagua kukubalia kishawishi, kitu kilichovuruga mpangilio mzuri na amani katika ulimwengu wote.

Yule nyoka (shetani) kwa kusema tu: "Mtakuwa kama Mungu" (Mwa 3:5) yaani kujitegemea na kutawala vyote, ilikuwa ahadi tosha ya kuvutia; lakini iliyopingana na ukweli wa mambo, ukweli kwamba sisi binadamu bado ni viumbe tu, tupende tusipende.

Licha ya kuambulia kifo na shida, tangu hapo, hiyo ahadi inajirudia kama kishawishi kikubwa kwa binadamu mpaka hivi leo. Jinsi Adamu alivyojificha baada ya kumkosea Mungu, na hata wale wanaompiga Mungu wanajaribu kujificha, ati Mungu asiwaone: "Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia uko wapi? Akasema, nalisikia sauti yako bustanini nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha" (Mwanzo 3:9-10).

Watu wangapi siku hizi wamezama katika ubinafsi, anasa, starehe, shughuli "nyingi", mali, kijiweni, TV hata na dini huria "kujificha" Mungu asiwaone na, labda pia, kwa nia ya kutajirisha binafsi au kujinufaisha au kujitengenezea hadhi na madaraka binafsi.

"Lakini pima mali ya mbinguni, utaona kwamba mambo hayo ya dunia si kitu kabisa; hayana imara, yana matata; huwezi kuwa nayo bila masumbuko na hofu’ (Rej. Kumfuasa Yesu Kristo).

Historia imeshuhudia roho nyingi na hata jamii nzima zikiangamizwa na kishawishi cha kuwa "Kama Mungu" bila kumtegemea mwingine au kushirikisha yeyote mwenye kuwazidi uwezo.

Inabidi tukubali sisi ni viumbe vya mwingine; tena isitoshe tumefanywa kutoka mavumbi ya udongo (Rej Mwa. 2:7;3:19;3:23)

Kukiri kuwa sisi si Mungu, ni kitambulisho chetu cha msingi kusudi tupate kukombolewa.

Matatizo yetu sisi binadamu yanatokana na kwamba utaratibu wote wa haki ya kwanza ambayo Mungu, katika mpango wake, alikuwa ameuweka kwa ajili ya mtu, ulipotea kwa dhambi ya wazazi wetu wa kwanza, (Katekisimu para 379).

Mwanzoni mtu alikuwa na heri kwa urafiki wake wa Mungu (Kkk. para 384).

Amani ambayo wazazi wetu walikuwa nayo kwa haki ya asili imevunjika kwa dhambi: utawala wa roho juu ya mwili unaotokana na vipawa vya kiroho umeharibika (Ibid. Para 400).

Mwishowe matokeo yanayotangazwa waziwazi katika dhana ya ukaidi yatatekelezwa mtu ‘atarudi mavumbini’ (Mwa 3:19; 2:17) mavumbi yale ambamo katika hayo alitwaliwa; mauti yanaingia katika historia ya mwanadamu (Rum 5:12).

Kanisa limetufafanulia kwa usahihi kwamba "baada ya dhambi ya kwanza, dunia imejaa mafuriko ya uozo wa kila aina ambao ni matokeo ya dhambi"(Kkk. Para 401).

Mzigo wa tamaa mbaya na mazoea ya dhambi

Mtakatifu Paulo alishuhudia hali hii ya uozo kutokana na tamaa ya dhambi kuhusu nafsi yake yeye akisema "...lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapigana vita na ile sheria ya akili zangu na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu"(Rum. 7:23).

Hapa Mtume Paulo alikuwa akijilalamikia alipoona amesongwa na tamaa ya kutenda baya ambalo alilichukia sana. Kwa njia hiyo amedhihirisha pia athari ya dhambi tuliyorithi kwa Adamu na Eva inayotupa sisi wanadamu maelekeo mabaya ya kutenda dhambi.

Hivi mpaka sasa, watu sote tunavutwa mno na tamaa ya maovu, na inatubidi kuingia katika pambano kali na gumu dhidi ya dhambi.

Watakatifu mara nyingi walimwomba Mungu awajalie mwanga wasitende dhambi.

Kwa mwanga huo walitambua wazi hatari ya kutawaliwa na tamaa na vionjo vya mwili ambavyo ni uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasara, fitina, kafara, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo.(Gal 19-21).

Waliomba neema ya kushinda Tunda la Roho. "Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi" (Gal. 5:22-23)

Kila dhambi inatia giza akilini. Jinsi wengi wetu tumeisha tenda dhambi, mashahidi wa ukweli huu ni nafsi zetu sisi wenyewe.

Kadiri dhambi zinavyoongezeka, ndivyo giza linavyozidi kumtanda na kumtia upofu mkosaji.

Neema, ambayo ni mwanga wa Mungu, unashindwa kufikia rohoni mwa mdhambi.

Ndiyo maana, mtu akishajizoesha dhambi fulani, haachii hapo bali anaendelea kututika dhambi juu ya dhambi bila kufikiria kutubu hata kushindana na vishawishi hawezi. Anaangushwa navyo tena na tena.

Ukisha zama katika mazoea ya kutenda dhambi, huna tena uhuru wa kweli. Shetani naye anakuchezea. Mazoea ya dhambi yanageuka kuwa tabia ya ‘kiamumbile’

Saa shetani kwa kuchochea nafsi yako, anakufanya mtumwa asiyeweza kuishi bila kutenda dhambi ile uliyozoea.

Sasa unakuwa mtumwa wa kulazimishwa kufanya tendo hilo baya bila kutaka.

"Faida" yako ni ile ya kutenda dhambi tu; basi! Shetani anakudanganya kuiona dhambi kama faida.

Kweli "Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo" na "Yeye ni mwongo na baba wa uwongo’ (1Yoh 3:8;Yoh 8:44). Lakini Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili azivunje kazi za ibilisi" (1Yoh 3:8). Miongoni mwa kazi za Ibilisi, mbaya zaidi kulingana na matokeo yake, ni kishawishi cha udanganyifu kulichomfanya mtu amkaidi Mungu.

"Kila mara kama mtu anatamani kitu kwa namna isiyofaa, hupoteza amani moyoni" (Kumfuasa Yesu Kristo, Kit 1, Sura 6 ). Kumkaidi Mungu kunaleta vurugu zaidi na si ajabu, mtu kuathirika kwa njia nyingine, hasa maumivu na uchungu wa ndani kisaikolojia.

Inatupasa kulilia na kumwombea mtu aliyezama katika mazoea ya dhambi, kwa kuwa yeye haoni tena hatari ya kupotea milele.

Maana, amenaswa "chini ya kongwa la utumwa’ (Gal 5:1), na hawezi kujitetea kwa sababu si huru.

Yesu anatuonya kwamba "Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi" (Yoh 8:34). Lakini tukimwomba Yesu atatuweka huru na anaahidi tukimtegemea yeye tutakuwa huru kweli kweli (Rej Yoh 8:36).