Make your own free website on Tripod.com

Ijue Afya yako

Mitishamba na imani za uchawi (3)

UTOSI ULIODIDIMIA

UTOSI ni sehemu laini ya kichwa cha mtoto mchanga.Ni sehemu ambayo fuvu la kichwa halijaimarika sawasawa.

Kwa kawaida, huchukua takriban mwaka mmoja hadi mmoja na nusu kuimarika kabisa. Akina mama wa sehemu nyingi duniani, wanaamini kwamba utosi ukididimia chini, watoto wao wapo hatarini na wana imani nyingi za kuelezea sababu zake.

Huko Amerika ya Kusini, wazazi husema eti ubongo wa mtoto umeshuka.

Watatafuta hila ya kurudisha kama vile kuunyonya utosi, kuinamisha kichwa chini au miguu juu na kupigapiga nyao za miguu ya mtoto.

Hii haisaidii kwa sababu utosi uliodidimia umesababishwa na ukosefu wa maji mwilini.

Ndiyo kusema mtoto anapoteza maji mengi mwilini kuliko anayokunywa. Amekauka sana aghalabu kwa sababu anaharisha ama anaharisha na kutapika.

Tiba:

- Mpe mtoto maji mengi, maziwa ya mama au maji yaliyochemshwa.

Ikibidi, tibu kinachosababisha kuharisha na kutapika. Kwa kawaida, hakuna dawa inayotakiwa.

Namna ya kutambua kama tiba za kiasili zinafanya kazi au la

Kwa sababu watu wengi wanatumia dawa za kienyeji, haimaanishi kuwa dawa hizo zinafaa sana na kwamba hazina kasoro.

Ni vigumu kuelewa ni zipi zinafaa na zipi zitaleta madhara. Uchunguzi maalumu unahitajika kufanyika ili kupata uhakika.

Ifuatayo ni miongozi minne ionyeshayo kuwa matumizi ya dawa kama hizo hayaponyeshi ugonjwa na si ajabu zikadhuru . (mifano hii imetokea Amerika ya Kati).

1. IWAPO KUNA AINA NYINGI ZA TIBA ZA KIASILI KWA AJILI YA KUTIBU UGONJWA WA AINA MOJA, NI WAZI KWAMBA HATA MOJA HAINA NGUVU YA KUPONYESHA.

Kwa mfano huko Amerika ya Kati, kuna namna nyingi za kutibu tezi la shingoni na zote hazisaidii baadhi yao ni:

- Kufunga kaa wa majini penye tezi.

- Kulisugua tezi kwa mkono wa mtoto aliyekufa.

- Kupaka ubongo wa tai penye tezi.

- Kupaka kinyesi cha mtu penye tezi.

Usijaribu kabisa; hakuna hata moja miongoni mwa tiba hizi inayofaa.

Kama mojawapo ingaliponyesha nyingine hazingehitajika.

Kama ugonjwa unatibika kwa aina moja tu ya tiba ni dhahiri kwamba tiba hiyo ni nzuri. Kwa kinga na tiba ya tezi la shingoni, tumia chumvi iliyotiwa joto.

2. DAWA CHAFU AU ZINAZOTIA KINYAA NI DHAHIRI KUWA HAZIPONYESHI NA KWA KAWAIDA HUDHURU, mfano:

- Wazo kuwa ukoma unaweza kuponyesha na dawa ya kunywa iliyotengenezwa kutokana na nyoka aliyeoza.

- Wazo kuwa kaswende, inaweza kuponyeshwa kwa kula tai.

Mifano hii miwili ya tiba, haiponyeshi ugonjwa wowote mfano wa kwanza unaweza kuambukiza ugonjwa mbaya.

Imani za uganga wa namna hii aghalabu hupoteza muda wa kupata tiba zenye manufaa za hospitali.

3. TIBA ZA KUTUMIA KINYESI CHA WANYAMA AU CHA BINADAMU HAZISAIDII ILA ZINAWEZA KUAMBUKIZA UGONJWA MBAYA SANA TAFADHALI USIZITUMIE.

- Kupaka kinyesi cha binadamu ukingoni mwa macho, hakuponyeshi kiwi cha macho(blurred vission) ila kunaambukiza ugonjwa.

- Kupaka kinyesi cha ng’ombe kichwani ili kuponyesha mapunye kunaweza kuleta pepopunda na mangonjwa mengineyo.

Halikadhalika vinyesi vya sungura na wanyama wengine haviponyeshi vidonda vilivyosababishwa na moto.

Ikiwa dawa inafanana na ugonjwa utibiwao, ni dhahiri kuwa faida yake inatokana na nguvu za imani ya mgonjwa.

Mfano:-

- Damu ikitoka puani zibia kwa uyoga mwekundu.

- Kiziwi mwekee sikioni unga wa mkia wa rattle snake. (Nyoka aina ya rattle)

- Donda la mbwa litibiwe kwa kunywa dawa iliyotengenezwa kutokana na mkia wa mbwa.- Aumwaye na nge akafungiwe nge huyo mahali alipomuuma

- Kukinga ugonjwa wa kuharisha kwa mtoto anayeota meno, mvike shingoni meno ya nyoka.

- Ili sumu itoke mwilini, kunywa maji yaliyochemshwa na magome ya msufi .

Uganga wa namna hii pamoja na mwingineo mwingi hauponyeshi. Labda unaweza kuwa na faida ikiwa mtu mwenyewe ni mshirikina.

Lakini jihadhari na ugonjwa unaoweza kuwa mbaya sana na kupoteza wakati bure katika ushirikina kama huo kuchelewa kupata dawa yenye kufaa.

Mitishamba

Mimea mingi ina nguvu za kuponyesha.

Dawa nyingi za kisasa zinatengenezwa kutokana na mimea ya porini.

Hata hivyo, mitishamba mingi itumiayo na wenyeji ina dawa ya kuponyesha...na ambazo zilizonayo zinatumiwa vibaya.

Jaribu kuelewa mimea gani katika mazingira yako ambayo inafaa.

Hapa kuna baadhi ya mimea iliyo na faida kama itatumiwa vizuri.

Angel’ s Trumpet, Datura Arborea

Majani ya mmea huu na mengine ya jamii ya night shade, ina dawa yenye kutuliza tumbo la kunyonga au kuuma.

Chukua gudulia lenye maji kiasi cha vijiko vya mezani saba kisha, saga majani mawili ya (angel’s trumpet) na changanya na maji hayo.

- Acha yatulie kwa muda wa siku moja.

Kipimo kama matone kumi hadi kumi na tano kila baada ya saa nne kwa mtu mzima.

ONYO: Angel’s trumpet ina sumu kali kama unazidisha kipimo chake.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza - Tanzania Bara (9)

Hapa serikali inapaswa kuangalia kwa makini sera zake na mipango ya utekelezaji ili iwe inawasaidia watu kutojihusisha na uhalifu.

Serikali na jamii kwa jumla inapaswa kuondokana na fikra potofu juu ya Magereza ya kwamba adhabu kali magarezani hupunguza uhalifu.

6:1 Adhabu nje ya kifungo gerezani

Kwa sasa jitihada zinatakiwa zilenge kuelekeza Mahakama kutumia hukumu zisizo za kifungo.

Hizi ni pamoja na:

- Kuachiwa huru watuhumiwa bila masharti au kwa masharti.

- Mtuhumiwa kumlipa fidia anayetuhumu.

- Kuweka faini inayolingana na muda wa kifungo.

- Kumweka mtuhumiwa chini ya uchunguzi.

- Kuhimiza usuluhishi kati ya mtuhumiwa na mtuhumu (to encourage reconciliation).

- Kumwachia mtuhumiwa kwa ‘bond’.

- Watuhumiwa kuamriwa watumikie vifungo vyao nje ya Magereza kwa kufanya kazi katika jamii k.m kukarabati barabara za vijijini, kujenga shule n.k.

Pamoja na jitihada hizo, zipo sheria ambazo kama zingetumika, zingesaidia.

Mfano, Sheria ya Bodi ya Parole 1994.

Sheria hii inatoa fursa kwa mfungwa kuachiwa huru kabla ya kumaliza muda wake wa kifungo kama akiwa anatimiza masharti na kuiridhisha, Bodi ya Parole.

Inategemewa kama rekodi za mfungwa zingetunzwa vizuri na Bodi kufanya kazi yake ipasavyo, basi hii ingesaidia kwani wengi kati ya wafungwa waliotenda makosa madogo madogo wangeachiwa huru.

Njia nyingine ambayo ingesaidia sana, ni ile ya kuanza kutoa hukumu za kutumikia adhabu katika jamii badala ya kifungo kwa wale wenye makosa madogo.

Hii ingesaidia sana wafungwa kwani wangepewa mahala pa kuhudumia ambapo panalingana na vipaji na karama zao kwa faida ya jamii.

Utekelezaji wake unahitaji ushirikiano baina ya Mahakama na Mamlaka za Serikali ngazi za chini (Local Government Authorities).

6:2 Msamaha wa Rais kwa wafungwa

Kwa mujibu wa Katiba, Rais anaweza kutoa msamaha kwa wafungwa wa aina yoyote.

Mbali na mamlaka aliyo nayo Rais chini ya Katiba, Kamishna Mkuu wa Magereza kwa mujibu wa kifungu cha 50 cha Sheria ya Magereza ya 1969 (Act No. 34/1967), amepewa madaraka ya kumshauri Rais kutoa msamaha kwa wafungwa:-

(i) Watakaoonesha tabia nzuri ya kuigwa (Exceptional Merit)

(ii) Wagonjwa wataakaoonekana kuwa magonjwa yao ni ya kudumu na ya hatari kwa maisha yao iwapo wataendelea kubaki gerezani (on Medical Grounds).

(iii) Kwa sababu nyingine yoyote ya msingi, Kamishna Mkuu ataona kuwa kuna haja ya kumshauri Rais atoe msamaha

Kuwa makini kuijua Biblia(6)

16. Je, kuna uhusiano wowote kati ya Agano la Kale na Jipya?

Kuna namna mbili za kueleza uhusiano kati ya vitabu vya Agano la Kale na Jipya.

Namna ya kwanza ni kuona kwamba Agano la Kale lilitabiri mambo yaliyoelekezwa katika Agano Jipya.

Kwa mtazamo huu, waamini wa Yesu walisoma na kulielewa Agano la Kale.

Kwa mfano: Injili ya Mathayo katika Agano Jipya yasema mara nyingi kwamba jambo fulani lilitukia katika maisha ya Yesu ili utabiri wa manabii katika Agano la Kale utekelezwe. (Mathayo 1: 22; 2:5; 3:5; 4: 14; 26:31).

Barua kwa Waebrania katika Agano Jipya ina nukulu nyingi toka Agano la Kale zinazobainisha kwamba Yesu Kristo ni Mkuu zaidi kuliko watu maarufu na taasisi zote za Agano la Kale.

Kwa namna hiyo, mambo ya Agano Jipya yalidokezwa tayari katika Agano la Kale, lakini pia ni kilele cha Ufunuo wa Mungu ulioanza katika Agano la Kale.

Namna ya pili ya kuona uhusiano kati ya maagano hayo mawili ni kuchunguza uhusiano uliopo kati ya kundi moja la Vitabu vya Agano la Kale na jingine la Agano Jipya.

Upo mlandano wa mada na mtazamo kati ya maagano hayo. Tunaweza kuviainisha vitabu hivyo katika jozi nne. Tukifanya hivyo tunapata mwafaka wa vitabu vyote, kama kitu kimoja. Kila jozi ikifananishwa na sehenu fulani ya jengo jozi zote hufanya jengo nzima.

Uhusiano wa mtindo huu uko kama ifuatavyo: Vitabu 5 vya Torati vinahusiana na vitabu 4 vya Injili kama msingi wa Biblia.

Vitabu 16 vya Historia vinahusiana na kitabu 1 cha Matendo ya Mitume kama ukuta wa Biblia.

Vitabu 18 vya manabii vinahusiana na vitabu 21 vya barua za mitume kama paa la Biblia.

Vitabu 7 vya Hekima vinahusiana na kitabu 1 cha Ufunuo kama ukamilisho wa Biblia katika majibu kwa maswali yafuatayo tutaona uhusiano uliopo kati ya jozi hizo.

Tutaona pia kwa nini jozi hizo zinafananishwa na sehemu za jengo: Msingi, Ukuta, Paa na Ukamilisho.

17. Uhusiano gani upo kati ya Vitabu vya Torati na Vitabu vya Injili?

Vitabu vya makundi hayo mawili wanahusiana katika vipengele vifuatavyo: kwanza Vyote vinasimulia mambo ya mwanzo katika kila Agano. Katika Vitabu vya Torati husimuliwa habari za mwanzo wa ulimwengu, mwanzo wa wanadamu, mwanzo wa Taifa la Israeli, mwanzo wa Ukombozi wa Waisraeli na mwanzo wa Agano kati ya Mungu na wanadamu.

Injili nazo husimulia mambo yalivyoanza katika Agano Jipya: mwanzo wa kipindi kipya, mwanzo wa maisha ya Yesu hapa duniani, mwanzo wa waamini wa Yesu na mwanzo wa Taifa Jipya la Mungu.

Pili, makundi yote mawili yanatoa mafundisho makuu ya imani inayoungamwa na waamini wa Maagano yote mawili.

Aidha, vitabu vya makundi hayo mawili vilipewa nafasi ya kwanza katika orodha ya Biblia kutokana na umuhimu wao. Waisraeli huvithamini na kuviheshimu sana vitabu vya Torati humo hupatikana misingi ya imani yao.

Hali kadhalika waamini wa Yesu Kristo hivithamini na kuviheshimu kwa namna ya pekee vitabu vya Injili, kwani humo hupatikana habari za maisha na mafundisho ya muasisi wa imani na taasisi zao, Yesu Kristo.

Kumbukumbu ya kuvuka milenia ya 2 kuingia ya 3

MOJA ya mambo ya kukumbuka katika historia ya TOLEO LA KIZAZI CHETU HIKI ni siku ya Desemba 31, 1999, ambayo kutwa nzima watu wote duniani walikaa chonjo na usiku kucha walikesha ili washuhudie namna mwaka 1999 utakavyokwisha na hivyo, kuifungulia dunia lango la kuingia milenia ya 3.

Hili kwa hakika halikuwa tukio la kawaida hata kidogo hasa ukizingatia kwamba uvumi ulikuwa umetapakaa kila pembe ya dunia kwamba sayari yetu hii ya Dunia ifikapo Desemba 31.1999 INAKWISHA!!!

Hilo kama halikutosha, ilisemekana kuwa hata mashine mbalimbali zinazowasaidia binadamu katika maisha yao ya kila siku kama vile computer baada ya hapo, zingesimama kufanya kazi.

Lakini basi tu ajabu na kweli ni kwamba usiku huo wa Desemba 31, 1999 ulikucha mtindo ule ule ‘na makucha yake’ kama ilivyo desturi yake tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Moja muhimu tunalojivunia kizazi chetu hiki ni kule kushuhudia mabadiliko ya karne na Milenia maana babu zetu walioifunga millenia ya kwanza na kuanzia ya pili mimi na wewe hatujui ni kizazi chao cha ngapi!

Kati yetu, hakuna ajuaye ni mjukuu wake wa ngapi atakayeiona na kuishuhudia tarehe ya mwisho ya Milenia hii yaani Desemba 31, 2999. Kumbe, kule kujipongeza na kusherehekea kwetu siku hiyo tukufu ya kufunga Milienia ya pili na kuanza milenia mpya ya tatu haikuwa kazi bure!

Pamoja na shamrashamra na sherehe za kila aina zilizofanyika karibu kila pembe ya nchi hii na duniani kote siku hiyo ya Desemba 31, 1999, katika makala yangu hii napenda kusisitiza nikiwaombeni watu wote wa mahali pote kwamba tuzidi kuenzi, kutunza na kuendeleza vitu vyote tulivyoweka kama kumbukumbu ya siku hiyo yaDesemba 31, 1999 ili vibaki kama kumbukumbu kweli na halisi ya vizazi vilivyopo, na vizazi vijavyo.

Ninasema hivyo maana nina hakika kwamba siku hiyo kila binadamu aliyekuwa na hali pamoja na afya njema, alikula na kunywa vizuri.

lakini jambo la msingi kujiuliza ni kuwa je, chakula hicho na kinywaji bado kimo tumboni mpaka leo?

Watu wengine tulisikia walikwea milima yenye sifa za pekee ulimwenguni kama kumbukumbu yao ya kuvuka karne na millenia lakini, baada ya kukwea huo mlima na kuteremka si basi......!?

Hapa pamoja na Dibaji ndefu hiyo nia yangu ilikuwa ni kuwashukuru na pia kuwapongeza sana Jumuiya ya Wakristo wa Kigango cha Kayungu Parokia ya Bushangaro Jimbo Katoliki la Rulenge kwa kazi nzuri waliyoifanya kutengeneza na kusimika MSALABA kama kumbukumbu yao pekee ya Milenia.

Msalaba huo ulizinduliwa rasmi na kutambuliwa kama kumbukumbu ya parokia nzima ya Bushangaro hapo Janiari 5, 2001 na Baba Paroko Mheshimiwa Sana Padre Francis Kagabiro kwa na adhimisho la Ekaristi Takatifu.

Tukio hilo lilihudhuriwa na mamia kwa mamia ya waamini toka kila pembe ya Parokia ya Bushangaro. Dhumuni la kuchagua msalaba uwe kumbukumbu ya Milenia kama ilivyoelezwa ndani ya Risala iliyosomwa siku hiyo ni kwamba, Msalaba kama Bendera ya Wakristo, ndicho chombo alichokitumia Bwana Wetu Yesu Kristo kuwakomboa wanadamu karibu miaka 2000 iliyopita na kusimikwa pale kwenye kilele cha mlima (Omukinengo) ni mahali penye mandhari inayofanana fanana na Mlima Golgotha mahali aliposulubibwa Mwokozi Wetu Yesu Kristo.

Na tangu siku hiyo uliposimikwa msalaba, wenyeji wa sehemu hii wamebadilisha jina la kilima hicho na kupaita CALVARI.

Siku hiyo ya Ijumaa Januari 5,2001 ni siku iliyotangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Yohane Paul wa Pili, kuwa ndiyo siku ya kufunga rasmi Yubilei Kuu.

Wenyeji na hasa waamini wa Parokia nzima ya Bushangaro waliobahatika kuhudhuria misa takatifu siku hiyo kwenye kilele cha mlima huo, hawatasahau na ni kumbukumbu tosha maana kilima chote kilifunikwa na mamia ya watu kama si maelfu, licha ya kwamba siku hiyo hali ya hewa ilibadilika ghafla kukawa kumenyesha mvua nzito na hivyo kusababisha ibada ya misa ichelewe na kuanza baada ya saa 11:00 jioni.

Katikati ya Misa, Kiongozi Mkuu wa Parokia (Paroko) Mheshimiwa Padre Francis Kagabiroa akifuatana na wahudumu wa Misa, masista na waamini, walikwenda mahali paliposimikwa msalaba na kutoa baraka huku Padre akiunyunyuzia maji ya baraka Msalaba na kuufukuzia ubani kama ishara ya kuweka wakfu, msalaba ule wa eneo lile na kwa maneno yake mwenyewe katika moja ya sala na maombi aliyotoa pale wakati wa baraka hizo alisema ,"...Kwa baraka hii msalaba huu na mahali hapa tangu sasa patakuwa ni mahali pa sala na ibada. Yeyote atakayekuja hapa akiomba kwa imani, ajaliwe kupata kile anachohitaji kwa njia ya Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi Wetu....Amina ".

Ibada ya Misa Takatifu ilihitimishwa kwa maandamano, sala, nyimbo, vigelegele na vifijo vya aina aina hadi kwenye Kanisa la Kigango cha Kayungu ambako ndiko kulikofanyika mkesha wa kuabudu Ekaristi Takatifu .

Sala, nyimbo ngoma na michezo mbalimbali viliongozwa kwa ushirikiano wa vikundi vitatu maarufu vya kwaya.

Wakristo waliendelea mpaka asubuhi ya Jumamosi yaani Januari 6, 2001.

Kwaya zilizoshiriki ni pamoja na wenyeji yaani Kwaya ya Mt. Daudi Kayungu na kwaya maarufu kwa uimbaji kutoka Kigango cha Nyakabanga.

Nyingine zilizoimba ni kwaya safi yenye wasanii chipukizi wanaopepeta kikweli ngoma za utamaduni kutoka kigango cha Kandegesho.

Vikundi hivi kwa hakika viliufaya usiku ule uonekane mfupi mno kuliko ilivyo kawaida.

‘Omukinengo’ Kayungu mahali uliposimikwa msalaba huo wa kumbukumbu ya Milenia , kwa yeyote anayebahatika kufika eneo hilo si rahisi hata kidogo kufika na kutoka mara ile ile; lazima atakawia tu pasipo kulazimishwa na mtu ili ashuhudie maajabu ya Mwenyezi Mungu aliyoyafanya katika kilima hicho.

Kwanza, mandhari ya mahali hapa ni ya kuvutia sana. atasimama uangalie pande zote hadi upeo wa macho yako.

Upepo mwanana ulioko pale utakufanya ajihisi kana kwamba yuko SAYUNI.

Ama, mawazo yakimrudisha nyuma katika Maandiko Matakatifu, utapafananisha mahali hapa na mlima ule unaosimuliwa katika Injili ya Luka Mtakaitifu 9:28 -36 (Mahali ambako Bwana Wetu Yesu Kristo aliwatwaa Petro, Yohana na Yakobo akapanda nao mlimani ili aombe) . Kufika kule, Petro alipendezwa sana na aliyoyaona pale mlimani.

Akatamani sana kuwepo pale muda wote akimshawishi Yesu wajenge pale vibanda.

Ili kuitunza na kuiendeleza kumbukumbu hii, mipango inayofanywa ya kujenga vituo vya njia ya msalaba kuanzia chini ya mlima hadi juu mahali uliposimikwa msalaba na vile vile Banda dogo la kupumzikia.

Utakuwa ni mpango wa kila mwaka kukutana hapa mara mbili kwa ajili ya sala, ibada na hata pengine mafungo kila siku ya Ijumaa Kuu tunapokumbuka mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na pia, kila Desemba 31, tunapokuwa tunafunga mwaka ili tushukuru na kuomba baraka zake Mwenyezi Mungu kwa mwaka unaofuata.

Kwa kazi hii nzuri ya KIHISTORIA iliyokiwsha anzishwa, nina imani kubwa kwamba uongozi mzima wa Kigango cha Kayungu ukishirikiana kwa karibu sana na uongozi wa Parokia ya Bushangaro na waamini wote, watakitunza kituo hiki na kukiendeleza hadi kifikie sura inayofanana na karne yetu hii tuliyomo ambayo wanasema ni Karne ya Sayansi na Teknolojia, maana hata imani yetu Wakristo inakua na kwenda na nyakati.

Mungu Baba Mwenyezi apende kutubariki sisi sote tulioingia katika karne hii mpya ya MILLENIA mpya na azibariki pia kazi zetu zote njema tuzifanyazo ili zitufae sana na kutupatia RIZIKI ya kutosha na riziki hiyo itupatie nguvu, akili na hata uwezo wa kuendeleza ufalme wake hapa duniani.