Make your own free website on Tripod.com

Ijue Afya yako

Mitishamba na imani za uchawi (2)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa Kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini

Mfano wa imani zinazoweza kumfanya mtu augue, ni mama mmoja aliyeharibu mimba na sasa damu ilikuwa bado inavuja kidogo.

Kulikuwa na glasi ya maji ya machungwa ambayo alishauriwa ayanywe.( machungwa yana vitamini C inayoimarisha mishipa ya damu).

Alikunywa glasi hiyo ijapokuwa alikuwa na woga kuwa maji hayo yangemdhuru.

Kwa jinsi woga wake ulivyopita kiasi, mara bada ya kunywa, ugonjwa wake ukazidi.

Akapimwa lakini, hakikuonekana kitu chochote. Alitulizwa na kuelezwa kuwa, hakuwa hatarini.

Lakini hata hivyo, mwanamke huyo, alijibu kuwa angekufa.

Mwishowe, ikabidi achomwe sindano ya maji maalumu.

Maji hayo hayakuwa na dawa yoyote lakini kwa kuwa alikuwa na imani ya sindano, alijisikia vizuri mara tu.

Kwa kweli yale maji ya machungwa hayakumdhuru ila, imani yake ndiyo iliyomzidishia ugonjwa.

Na kilichomfanya ajisikie vizuri ni imani yake kwa sindano.

Labda kwa upande fulani, mwanamama huyu alikuwa amesaidiwa sana lakini, hata hivyo, hakuwa ametendewa wema isipokuwa, alikuwa amefanywa kuamini vitu ambavyo si kweli.

Mwandishi wa kitabu hiki anasema, "Hii iliniuma. Kwa hiyo, nikaona ni afadhali kurekebisha mambo. Hivyo siku chache baada ya yule mama kupona nilikwenda nyumbani kwake na kumtaka radhi kwa yote niliyomtendea alipokuwa mgonjwa. Nikijaribu kumweleza kuwa siyo yale maji ya machungwa yaliyomfanya azidiwe ugonjwa wake ila, ni uoga.

Na kwamba siyo ile sindano iliyomponyesha bali ni uhuru alioupata kutokana na kandamizo la uoga."

Kuelewa ukweli wa chungwa, sindano na fikra kichwani mwake, labda huyu mwanamama na jamii yake watakuwa huru kutokana na uoga na wataweza kutunza afya zao vizuri hapo baadaye.

Kwani afya njema huambatana sana na kuelewa na kutokuwa mwoga.

Vitu vingi vinaumiza kwa sababu watu wanaamini hivyo.

Uchawi ulozo, ulozi na kijicho

Kama mtu anaamini sana kuwa mtu fulani ana nguvu za kumdhuru, basi anaweza kuugua.

Kama mtu anaamini kuwa kalogwa au kutupiwa jicho baya, yeye ni mhanga wa woga wake.

Mchawi hana nguvu juu ya watu wengine ila ana uwezo wa kuwafanya waamini kuwa ana uwezo wa kuloga.

Kwa sababu hiyo, ni vigumu kumloga mtu ambaye haamini kuwa kuna uchawi.

Watu wengine hufikiri kuwa wamelogwa ikiwa wana magonjwa ya ajabu kama vile donda ndugu hasa la mguuni au la uumeni.

Magonjwa kama hayo hayasababishwi na uchawi au kulogwa. Sababu zake ni mambo ya kawaida.

Usipoteze fedha yako kwa waganga wanaodai kuwa wanaweza kutibu ulozi, pia usijaribu kulipiza kisasi dhidi ya mchawi, kwani hakutatatua tatizo.

Endapo u mgonjwa sana, nenda hospitali ukasaidiwe.

Kama una ugonjwa :

- Usimlaumu mchawi ila nenda ukamwone daktari

- Usiende makafarani

bali nenda ukamwone daktari

Maswali na majibu juu ya imani za kale na tiba za kienyeji

Mifano hii ni ya sehemu za milimani huko Amerika ya Kati ambapo napafahamu sana.

Labda baadhi ya imani za watu wako ni sawa na hizi.

Fikiria njia za kujifunza imani zipi katika sehemu yako... weka fikra zako zote katika imani yako uishipo ambapo unatekeleza uzima wa afya yako nzuri.

Swali: Watu wakiamini kuwa mwenzao kalogwa ni kweli kuwa atapona ikiwa ndugu zake watamtendea mabaya mchawi huyo au kumwua?

Jibu: Si kweli. Hakuna mtu anayesaidiwa kwa kumumiza mwenziwe.

Swali: Je, ni kweli kwamba ikiwa utosi wa mtoto umedidimia, atakufa kwa ugonjwa wa kuharisha kama hakupata matibabu ya kufaa?

Jibu: Aghalabu hii huwa kweli utosi unadidimia kwa sababu mtoto amepungukiwa na maji mwilini. Kama hatarudishiwa hayo maji atakufa haraka.

Swali: Je, ni kweli kwamba mionzi ya mwanga wa mwezi uliopatwa ikiwa ikimfikia mama mjamzito mtoto atakayezaliwa atakuwa kilema au mwenye kasoro?

Jibu: Hii si kweli, bali watoto wanaweza kuzaliwa vilema viziwi, viwete, au wenye kasoro ikiwa mama hakutumia chumvichumvi zilizotiwa joto au inaweza kuwa kwa sababu nyinginezo.

Swali: Je, ni kweli kuwa wazazi wajifungue watoto wao gizani?

Jibu: Ni kweli mwanga mdogo ni mzuri kwa mama na mtoto lakini ni lazima kuwe na mwanga wa kutosha kwa mkunga ili aone anachofanya.

Swali: Je, ni kweli kuwa mtoto mchanga asiogeshwe mpaka kitovu kimeanguka?

Jibu: Kweli, kitovu sharti kiwe kikavu mpaka kianguke.

Lakini, mtoto anaweza kusafishwa kwa kutumia kitambaa kisafi, laini na chenye unyevu.

Swali: Ni muda gani mzazi angoje tangu ajifungue mpaka kuoga.

Jibu: Mzazi anaweza kuoga siku ile ile alijifunguayo akitumia maji moto.

Tabia ya kukaa siku nyingi bila ya kuoga kunaweza kuleta maradhi.

Swali: Je,ni kweli kuwa tabia ya kumnyonyesha mtoto ziwa la mama ni bora kuliko kutumia mitindo ya kisasa ya maziwa ya chupa?

Jibu: Kweli, maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto na humsaidia katika kumkinga kutokana na maradhi mbalimbali.

Swali: Ni vyakula gani mzazi inambidi aepuke katika wiki chache za mwanzoni baada ya kujifungua?

Jibu: Mara tu baada ya kujifungua wazazi wasiepuke vyakula vyovyote bora.

Badala yake wale matunda, nyama, mboga za majani, maziwa, mayai na maharage kwa wingi.

Swali: Je, ni vizuri kumuogesha mgonjwa, haitaleta madhara?

Jibu: Ni jambo zuri wagonjwa waogeshwe maji ya uvuguvugu kila siku.

Swali: Je, ni kweli kuwa machungwa, mapera na matunda mengine yanadhuru ikiwa mtu ana mafua ama homa?

Jibu: La! Matunda na maji yake yanasaidia ikiwa ana mafua au homa. Hayaleti madhara yoyote.

Swali: Je, ni kweli kuwa mtu mwenye homa kali hana budi afunikwe kwa nguo nyingi ili baridi isimuumize?

Jibu: La! Mtu akiwa na homa kali mwache apate ubaridi. Hii itamsaidia kupunguza homa.

Swali: Ni kweli kwamba chai iliyotengenezwa na magome ya mti uitwayo Willow husaidia kupunguza homa na kukomesha maumivu.

Jibu: Kweli, husaidia. Goma la Willow lina dawa ya asili ndani yake inayofanana na aspirini.

Utosi uliodidimia

Utosi ni sehemu laini ya kichwa cha mtoto mchanga.

Ni sehemu ambayo fuu la kichwa halijaimarika sawa sawa. Kwa kawaida, huchukua kiasi cha mwaka hadi mmoja na nusu kuimarika kabisa.

Kina mama wa sehemu nyingi duniani wanafahamu kuwa utosi ukididimia chini watoto wao wapo hatarini na wana imani nyingi za kuelezea sababu yake. Huko Amerika ya Kusini wazazi husema ati ubongo wa mtoto umeshuka.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza - Tanzania Bara (8)

Muda ulivyozidi kusonga mbele Serikali pia imeona mapungufu ya Sheria na hivyo msisitizo ukawekwa kwa makosa ambayo kwayo, dhamana hairuhusiwi mauaji na uhaini.

Kwa makosa mengine yote dhamana inaruhusiwa isipokuwa makosa ya kipigo kikali kilichosababisha madhara mwilini, tishio la kumuumiza mtu mwingine kwa kutumia nguvu, kushikwa na silaha na makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya. Pia mtuhumiwa ambaye alishawahi kutuhumiwa na kuwekewa dhamana na hakufuata masharti ya dhamana ya hapo awali hawezi kuwekewa dhamana.

Utekelezaji wa Sheria hiyo umeleta matatizo makubwa kwa Idara ya Magereza. Kwa ujumla wengi wanaotuhumiwa kwa makosa madogo huwekwa mahabusu kutokana na masharti ya dhamana kuwa magumu au kwa sababu ya kukosa wadhamini wanaoaminika. Matokeo ya yote haya ni kuendelea kujaza Magereza.

5.5 Kutegemea mno hukumu ya kifungo

Watu wengi huamini kuwa adhabu ya kifungo jela husaidia kupunguza uhalifu.

Na hii si katika Tanzania tu. Sheria za nchi nyingi humweka mtuhumiwa kifungoni muda mrefu na nyingine huzuia dhamana kwa watuhumiwa. Hizi ni pamoja na sheria za zamani, zilizorekebishwa na hizi mpya - mfano sheria ya unyanyasaji wa kijinsia 1998 inayolenga kulinda haki za wanawake na watoto. Mikakati ya kubadili fikra hizo ni muhimu kwani kujaza wahalifu jela sio njia pekee ya kupunguza uhalifu nchini. Kama ukali wa adhabu ndio suluhisho la uhalifu, hakuna mtu ambaye angetenda kosa la mauaji kwani adhabu ya kifo, adhabu ambayo ni kali kuliko adhabu nyingine yoyote.

Lakini uzoefu duniani pote unaonyesha mauaji yanaongezeka kwa kasi katika nchi nyingi Tanzania ikiwa mojawapo licha ya kuwepo kwa adhabu ya kifo.

5.6 Upungufu wa watendaji, wajuzi katika ngazi za chini za Mahakama

Kesi nyingi nchini mwetu huanzia Mahakama ya Mwanzo ambayo ni ngazi ya chini kabisa ya Mahakama nchini.

Mahakama za mwanzo zimo katika karibu kila Kata. Kiutendaji hapa pana upungufu mkubwa ambao inabidi kuushughulikia kwani zaidi ya robo tatu ya wafungwa waliomo jela leo wanatoka Mahakama za Mwanzo.

Mahakimu wa Mahakama za mwanzo ndio wenye elimu ya chini kuliko wote walio katika Idara ya Mahakama.

Wengine wamepandishwa tu toka ukarani wa mahakama au wachunguzi kufikia kuwa Mahakimu.

Wanahudhiria kozi fupi tu kisha wanategemewa kwenda kuwatendea watu haki. Kwa hali hiyo haishangazi kuona wanatoa hukumu zinazokandamiza watu.

Kutokana na uhaba wa mahakimu kujaza pengo la anayekwenda likizo ama shughuli za nje ya eneo lake la kazi hutokea wakati mwingine mahakama ikafunga shughuli zote kwa mwezi mzima au hata zaidi.

5:7 Kuchelewesha rufaa za wafungwa waliohukumiwa

Hapa ni pale ambapo mfungwa hakuridhika na hukumu hivyo anataka kuihoji mahakama. Katika utekelezaji wa rufaa uzoefu unaonyesha kuwa;

Hapa tena raia mhusika hulazimika kununua karatasi ili hukumu ichapwe. Hata baada ya kuipata anahitaji msaada wa kisheria katika kuandaa rufaa yake kwa kuwa huduma hiyo haipatikani katika magereza yote au mikoa yote nchini.

- Mfungwa anayetaka kukata rufaa anaiweka mamlaka ya Magereza njia panda kwani hata kama yumo katika gereza lenye msongamano hawezi kuhamishwa mpaka akamilishe taratibu za rufaa.

5:8 Kuwepo kwa wazee wa Mahakama ambao hawana ujuzi wa Sheria za Mahakama

Kwa kawaida wazee wa mahakama wanapaswa kuwa wawakilishi wa wananchi katika mahakama.

Hawatakiwi kuwa wataalamu wa sheria lakini wanatakiwa wawe na uwezo wa kufikiri mambo na kuyaangalia kwa mapana hivyo kuwashauri mahakimu ipasavyo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka kikamilifu.

Kihistoria wazee wa mahakama waliwekwa kwa lengo la kuwashauri mahakimu ambao wakati huo walikuwa wazungu tu juu ya masuala yaliyohusiana na sheria za kimila za wenyeji ilipotokea masuala hayo kuhitaji kupelekwa mahakamani. Kwa wakati huu wa kukuza demokrasia wazee hao wanapaswa kusimama mahakamani kuiwakilisha jamii. Hawa wanakuwepo katika kesi zote za mahakama ya mwanzo na katika kesi ngumu kama za mauaji na uhaini katika mahakama kuu.

Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi hazina wazee wa mahakama.

Kiutendaji katika Mahakama za Mwanzo wazee wawili wanaoketi na Hakimu huwa na Mamlaka sawa na hakimu, hivyo katika kufikia uamuzi wanaweza kuamua kinyume na mtizamo wa hakimu.

Hii ni mbaya kwani wazee hawa ujuzi wao kisheria ni wa chini zaidi kuliko mahakimu. Hivyo katika mazingira haya wengi wamehukumiwa kwenda jela bila kustahili na hii inazidi kuongeza msongamano usio wa lazima huko magerezani.

Inafaa kuangalia sifa, nafasi na haki ya wazee wa mahakama kwa kuoanisha na huduma yao.

Tofauti na mahakimu wazee hawa huwa hawalipwi mishahara bali hulipwa posho tu kufuatana na siku wanazofanya kazi.

Kwa kuelewa madaraka waliyonayo juu ya watuhumiwa na madaraka hayo kutoambatana na mshahara hali hiyo imestawisha sana mazingira ya rushwa ndogo ndogo katika mahakama hizo. Haki inabaki kuwa ya kununua pale sheria inapopindishwa kumnufaisha mzee mwenye madaraka katika mahakama.

5:9 Upelelezi wa taratibu unaofuatwa na Maofisa wasio na motisha.

Uchunguzi wa Polisi una nafasi ya pekee na muhimu katika kesi za jinai.

Polisi huchukua hatua kwa taarifa wanazopata toka kwa wanaowataarifu, malalamiko ya raia au kwa msukumo wao binafsi.

Wanaodhaniwa kuwa wahalifu hukamatwa na kuwekwa mahabusu kisha polisi hufanya uchunguzi juu ya tuhuma.

Wana uwezo pia wa kuwatoa wengine kama ikithibitika kumbukumbu ziliandikwa kimakosa.

Pamoja na majukumu yote hayo polisi hawapewi vitendea kazi muhimu ambavyo vingewasaidia kufanya kazi yao vizuri. Hakuna usafiri wa kufuatilia upelelezi wa kesi hivyo mwenye kutuhumu hupaswa kutafuta usafiri. Karatasi na majalada pia ni matatizo.

Zaidi ya hayo hata makazi wanayoishi ni shida tupu. Haya yotee kwa ujumla huathiri utendaji wa Jeshi la Polisi.

5:10 Athari za Msongamano katika Magereza

Matatizo kadhaa hujitokeza katika Magereza kwa sababu ya msongamano. Matatizo hayo ni:-

(i) Huduma muhimu magerezani kama chakula, malazi na dawa, kushindwa kukidhi mahitaji halisi kutokana na wingi wa wanaohitaji huduma hizo.

(ii) Mlipuko wa magonjwa kama kifua kikuu, kipindupindu, upele, kuhara na hata ukimwi na mengineyo. Katika baadhi ya Magereza matatizo ya magonjwa husababisha vifo vya wafungwa.

(iii) Kiutendaji suala zima la ulinzi na usalama linakuwa gumu kwa maofisa wa Magereza.

Ni vigumu kuwadhibiti wafungwa na pia inakuwa ngumu kuwatambua wale wenye makosa makubwa ili kuwatenganisha na kuweka mpango mzuri na urekebishaji kwa makundi yote ya wafungwa.

(iv) Kisaikolojia wafungwa huathirika na hupoteza imani katika utu wao hasa watoto na vijana. Tabia zao pia huharibiwa na wengine kiasi kwamba ni vigumu kuwarudisha kuwa raia wema.

6. Mapendekezo na mbadala wa kifungo

Katika hali iliyozungumziwa kwa ujumla kuna haja ya jamii nzima kujihusisha katika kutafuta ufumbuzi.

Jambo la msingi ni kuweka mazingira yanayoleta ugumu kwa yeyote kujikuta yumo gerezani na hii ni katika kuyafanya maisha ya wananchi yawe bora na ya kuvutia.

Kuwa makini kuijua Biblia(5)

Siyo wale mitume walioteuliwa na Yesu tu ndio waliohubiri na kubatiza, bali wengine pia walioteuliwa na wale Mitume asilia. Miongoni mwa Mitume wapya walikuwa Paulo. Huyo akisaidiwa na wenzake wengi wote ndiye aliyehubiri katika eneo kubwa zaidi kuliko mitume wengie wote.

Nusu ya pili ya kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea matendo ya Mtume Paulo na kinaishia kwa taarifa ya Mtume Paulo kuwekwa kizuizini mjini Roma akiongojea hukumu. Mchango mkubwa wa Mtume Paulo ulikuwa kuondoa vikwazo vilivyowazuia watu wa mataifa mengine kujiunga na jumuiya za waamini wa Yesu Kristo.

Sharti pekee alilodai Mtume Paulo toka kwa waamini watarajiwa lilikuwa kumwamini Yesu Kristo kuwa ndiye Mwokozi (Wagalatia 2:15-21)

14. Je, Vitabu 21 vya Barua za Mitume vina ujumbe gani?

Barua za Mitume zilitumwa kwa jumuiya za waumini au kwa viongozi wa jumuiya hizo. Mambo yalitokea hivi baada ya mwanzilishi wa jumuiya kuondoka mara nyingi mambo mazuri na mabaya yalitokea.

Mazuri yalikuwa kama yafuatayo: imani ya watu iliongezeka jumuiya ilipanuka watu walionesha ujasiri katika kuvumilia mateso na ari ya kuhubiri ujumbe wa Mungu ilizidi.

Lakini mara nyingi zaidi ni matatizo yaliyozuka katika jumuiya kama mtengano kati ya wanajumuiya kuzuka kwa wahubiri waliopinga msimamo wa mwanzilishi, utovu wa imani, utovu wa maadili na nidhamu na kadhalika.

Kwa namna moja au nyingine, habari za matukio hayo zilimfikia Mtume mwanzilishi wa jumuiya.

Basi, katika mazingira hayo Mtume Mwanzilishi wa jumuiya husika aliandika barua kujibia mambo yaliyotokea.

Barua hizo sasa tunazichukua kama vitabu katika Biblia vitabu ambavyo vinapongeza, vinakemea, vinasahihisha, vinafariji na vinatoa miongozo.

Maadamu Mtume Paulo ndiye aliyeanzisha jumuiya nyingi za waumini, ni yeye pia aliyeandika idadi kubwa ya barua. Baadhi ya barua katika Agano jipya zina majina ya wale walioandikiwa jumuiya au viongozi kwa mfano: Wakorintho, Wafilipi, Waroma, Timotheo,Tito. Barua nyingine zina majina ya Mitume walioziandika kwa mfano: Yakobo, Petro, Yohane,Yuda.

15. Kitabu cha Ufunuo kinafunua nini?

Kitabu cha ufunuo kinafunua mazingira ya mateso yaliyowapata waumini kwa sababu ya kumwamini Yesu Kristo.

Waumini walioishi chini ya dola la Roma walidhulumiwa vikali hasa chini ya Kaisari (mfalme) Domitiano kati ya mwaka 81-96 baada ya Kristo (BK). Mwandishi anatumia lugha ya mafumbo kuwaeleza wale wanaowatesa waumini.

Aidha kitabu cha Ufunuo kinawahimiza waumini wavumilie mateso yao kwa vile hata Yesu mwenyewe alipitia njia ya mateso.

Yesu Kristo anafananishwa na mwana kondoo anayezijua siri zote za mipango ya Mungu na ndiye mwenye uwezo wa kuzifunua siri hizo kwa wakati wake. Ujumbe wa kitabu hiki ni kwamba, Mungu atawaadhibu wale wanaowatesa waamini.

Aidha Mungu atawaweka mahali pema waamini wanaovumilia mateso hadi mwisho.

Uhusiano wa Agano la Kale na Agano Jipya

16. Je, kuna uhusiano wowote kati ya Agano la Kale na Jipya?

Kuna namna mbili za kueleza uhusiano kati ya vitabu vya Agano la Kale na Jipya. Namna ya kwanza ni kuona kwamba Agano la Kale lilitabiri mambo yaliyotekelezwa katika Agano Jipya.

Kwa mtazamo huo waamini wa Yesu Kristo walisoma na kulielewa Agano la Kale.

Kwa mfano: Injili ya Mathayo katika Agano Jipya yasema mara nyingi kwamba jambo fulani lilitukia katika maisha ya Yesu ili utabiri wa Manabii katika Agano la Kale utekelezwe (Mathayo 1:22;2:5; 4:14;26:31),.

Ndoa

Kuponya Ndoa halali Batili kutoka Shinani ( MSK, k 1161 -1165 )

1. ILI kuponya ndoa halali ambayo ni batili kutokana na kukosekana utaratibu kanuni au kwa kuweko kizuizi batili ndoa ambacho sasa kimetoweka au kimeruhusiwa au kwa vile ukubalindoa haukutolewa ndoa iliposhuhudiwa kwa mujibu wa sheria (MSK, k1160,1158,1159), ni lazima ndoa iliyosherehekewa hapo awali itambuliwe angalao na mwanandoa Mkatoliki kuwa ilikuwa batili na kwamba kurudia upya ukubalindoa ni muhimu ili ndoa halali batili husika ipate kuponywa na kufanywa halali na kweli.

Na tena, kurudia upya ukubalindoa huu, ni lazima ufanyike kulingana na utaratibu kanuni pale inapolazimu (MSK, k 1157; 1159,#3).

Kwa vile kurudia upya ukubalindoa kunatokana tu na sheria ya kikanisa (MSK, k 11), wanandoa wasio Wakatoliki hawalazimiki kutambua kuwa ukubalindoa wao wa mwanzo ulikuwa batili na wala hawahitajiki kurudia upya ukubalindoa ili ndoa zao halali batili zipate kuponywa.

Hata hivyo lakini, ni lazima wanandoa wasio Wakatoliki, wamtamkie mhudumu aliyetiwa wakfu ukweli kwamba ukubalindoa wao wa mwanzo bado unaendelea na haujasitishwa.

2. Lakini, inaweza kutokea hali ambayo mmojawapo wa wanandoa au wote wawili hawawezi kuponya ndoa halali batili yao kwa kurudia upya ukubalindoa na kutumia utaratibu kanuni pale panapopasa.

Kwa maneno mengine, mwenye ndoa au weye ndoa halali batili husika, hawawezi kuponya ndoa yao kwa njia ya kawaida (MSK,k1156-1160). Anamhitaji au wanamhitaji Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka afanye kazi hiyo ya kuponya ndoa husika.

Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka huyo ni Jimbo Takatifu au Askofu Jimbo, au yeyote aliyeagizwa kufanya hivyo na mmojawapo wa hawa wawili.

Kitaaluma, hatua hii ya Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka ya kuponya ndoa halali batili bila kumhusisha au kuwahusisha wanandoa husika huitwa "kuponya ndoa halali batili kutoka shinani" (Sanatio in Radice).

Hatua ya kuponya ndoa halali batili huufanya ukubalindoa wa mwanzo ambao ni batili, kuwa wa kweli na wenye nguvu tangu siku ile ulipotolewa kwa mujibu wa sheria lakini bado ukawa batili kutokana na sababu hii au ile.

Hatua ya kuponya ndoa halali batili kutoka shinani inapochukuliwa na Mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka, agano ndoa linaloponywa linachukuliwa kisheria kana kwamba lilikuwepo tangu mwanzo na yanayotokana na ndoa kweli yanaanza tangu siku ile ukubalindoa wa mwanzo ulipotolewa angalao kwa mujibu wa sheria.

Hatua ya kuponya ndoa halali batili kutoka shinani ilichukuliwa kwanza na Papa Bonfasio Vlll (1294-1303).

3. Kwa kuponya ndoa halali batili kutoka shinani, mwanandoa au wanandoa husika huondolewa vizuizi batilindoa na utaratibu kanuni huruhusishwa. Ndoa halali batili huwa ndoa halali na kweli moja kwa moja.

Na tena buniko la sheria (by fiction of law), yote yanayotokana na ndoa kweli (MSK, k 1134-1140) hufanywa kuweko tangu siku ile ndoa halali batili iliposhuhudiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa mfano, uhalaliwa watoto waliozaliwa katika ndoa halali batili hiyo unachukuliwa kana kwamba ulikuwako tangu siku ile ukubali ndoa batili ulipotolewa .

Ijapokuwa tunatumia msemo "kuponya ndoa halali batili kutoka shinani"; kwa kweli kuweka mambo wazi, hakuna uponyaji wa ndoa halali batili unaorudi nyuma (restroactive healing) hadi siku ile ukubali ndoa batili ulipotolewa, kwa sababu ukweli kwamba ndoa halali batili husika iliyokuwa batili tangu mwanzo unabaki uleule na palepale hata Mungu mwenyewe hawezi kuubadilisha ukweli huo kwa sababu kwa maumbile yake Mungu hajipingi mwenyewe.

Kudhibiti hasira hujenga busara

Na Benjamin Mwakibinga

WATU wengi wenye busara toka kale wamekuwa wakizungumzia sana suala la hasira na kueleza kuwa ni kitu kibaya jambo hili la hasira kutawala ndani ya jamii.

Hasira ni moto unaomwashia adui yako ambao unaweza kukuunguza mwenyewe au kwa maneno mengine hasira inaweza kuelezwa kuwa ni sawa na kichaa cha muda ambacho humpata mwanadamu.

Tendo la kukasirika hutokea mara tu baada ya binadamu mmoja ama kundi la watu fulani kujihesabia haki na kwamba hakustahili kutendewa hivyo na hapo ndipo hutokea uadui baina ya mtendaji na mtendewa na kupelekea mtendewa kupatwa na kichaa cha muda hivyo kuwa na uadui na mtendaji.

Katika maisha ya mwanadamu kuna maadui wanaomzunguka nao hawa wanagawanywa katika makundi makuu mawili, la kwanza ni la wale walio nje ya mwili wa mtu na kundi la pili wale maadui walio ndani ya mwili wa mtu.

Kwenye hili kundi la maadui walio ndani ya mwili wa mtu tunakuta kwamba linajengwa na vitu vifuatavyo: wivu, uchoyo, wasiwasi, mashaka, kukosa subira na hasira.

Kwa kuangalia kwa mapana zaidi ni kweli kabisa kuwa maadui wa ndani ndio wa hatari zaidi ukilinganisha na wale wa nje na hii ndio iliyopelekea mpaka Wahenga husema’Kikulacho ki nguoni mwako’ wakimaanisha kwamba ubaya wote ama uharibifu wote unasababishwa na mambo yale yaliyo karibu sana na mtu.

Hivyo basi Hasira huhesabiwa kuwa ni miongoni mwa maadui wakubwa na wenye uwezo wa kupoteza maisha ya mtu kwa pande zote mbili kwa maana ya maisha ya kimwili (nyama na damu) na maisha ya kiroho (Utakatifu).

Maandiko Matakatifu yamelizungumzia swala la hasira kwa mapana zaidi kiroho na hata kimwili, Wagalatia 5:19-21 inaeleza kuwa hasira ni adui kwa maisha ya mtu kwa vile husababisha mwanadamu kutengana na MUNGU aliyemuumba.

Biblia inafafanua zaidi juu ya hasira kuwa hutokana na hali ya kujihesabu kuwa na haki fulani .Katika kitabu cha Luka 15:25-32, mfano wa mwana mpotevu aliporudi kwa babaye na kufanyiwa karamu lakini jambo hili lilimkasirisha nduguye na akaanza kutoa masikitiko kwamba kwanini mwana mpotevu aandaliwe karamu?

Alistahili yeye kuandaliwa kwani amekaa na babaye wakati wote.

Ni vigumu sana kushughulikia hasira kwa kusema ,"dhibiti hasira yako" kama vile ambavyo watu wengi wamekuwa wakisema kwa madhumuni ya kuwashusha hasira wengine wanapokuwa wamekasirika, lakini ni lazima tukubaliane kuwa Hasira ni Imara mno na kwamba inatabia ya kuzikwepa zile njia zinazotumika kushughulikia hali hiyo.

Katika kuondokana na tatizo hili la hasira,kwanza kabisa inakupasa kujiuliza kuwa:

- Wewe ni nani

- Upo kwenye mazingira gani

- Je, hapo ulipo kuna watu wa aina gani?

- Je, nini kitatokea kama utadhihirisha hasira yako hapo?

- Je, umewahi kujiuliza kiwango cha hasira ulichonacho?

- Je, umewahi kujiuliza juu ya hasara ambayo inaweza kusababishwa na hasira yako?

- Pengine hujawahi kujiuliza na unadhani hasira uliyonayo ni maumbile ya kawaida na huna uwezo wa kufanya chochote juu yake.

Kuna mfano mzuri zaidi katika jamii kwamba hapo wazazi wenye busara ambao mtoto akifanya kosa wakati nyumbani kuna wageni husubiri mpaka mgeni aondoke, husitisha hasira yake.

Mzazi wa jinsi hii ataheshimika na tena ataitwa mzazi mwenye busara.

Wengine wakiona hasira zimewafika basi huamua kunyamza kimya mpaka zitakapotulia na ndipo huanza kutafuta suluhisho la jambo hilo.

Lakini jambo kubwa na muhimu ni kufahamu kuwa unaweza kudhibiti hasira uliyonayo.

Angalia kwa mapana zaidi hasara ulizozipata kutokana na hasira yako.

Hasira yaweza kusababisha:

- Kuondokewa na heshima

- Kuharibu mahusiano ya kimaisha katika jamii .Wengine wamepatwa na hasira kiasi cha kutoa uhai.

Kwa vile tumeshaona kuwa jambo hili ni adui maishani, basi ni vizuri tujiulize kwa nini hasira huja.

Kwa mtazamo uliowazi kabisa kwa maana ya kusema sababu kubwa zaidi iletayo hasira kwa maisha ya mwanadamu ni ile hali ambayo mtu anafikia hatua ya kupambana na mazingira ambayo hakutarajia hapo awali.Mifano ifuatayo inaweza kuonesha mazingira yaletayo hasira.

-Matarajio ya kupata fedha

-Matarajio ya kupatiwa Elimu

-Matarajio ya kuoa au kuolewa na yale yanayofanana na hayo.

Kwa kushindwa kutimizwa kwa malengo hayo yaliyotajwa hapo juu mtu anaweza kupatwa na hasira.

Ni jambo la ajabu kwamba hasira inaweza kutokea katika mazingira ambayo hatuna uwezo wa kuyakabili.

Mfano halisi ni pale fundi ujenzi anapokuwa tayari ameshachanganya zege na mara mvua kubwa inaanza kunyesha .

Hili linaweza kumfanya fundi asipatwe na hasira sana. Ni kweli kwamba swala hilo lipo juu ya uwezo wake (Swali je, Anamkasirikia nani?).

Ni ukweli usiofichika kwamba katika dunia tunayoishi bila kuzingatia uwezo wa kifedha au jinsia hakuna mtu asiye na Hasira isipokuwa ni lazima uwe makini na Hasira yako uliyonayo na kujiuliza kuwa inaanza lini.

Hasira ya mtu mmoja hadi mwingine hutofautiana lakini pamoja na hivyo inafaa sana kuzingatia hayo yafuatayo:

-Mbali ya kuangalia hasara pia jilinde sana na kujiona wewe tofauti na wenzako kwa hali zozote zile utashinda tatizo la hasira.

Jifunze kuwaona wenzako kuwa bora kuliko wewe. Ni vyema ukifahamu kuwa jamii ianayokuzunguka si malaika kwa kuzingatia haya kamwe haitatokea ukasirike na utaitwa mtu wa busara maisha yako yote.

Lijue Shirika la Masista wa Tutzing

Katika toleo la mwisho la safu hii, tuliona Misioni ya Pugu inavamiwa. Sista mmoja na mabruda wawili waliuawa; sista mmoja na mabruda watatu walikamatwa mateka; mabruda wawili wakakimbia. Katika makala haya Mwandishi Wetu PADRE SIMPLISIUS KAPINGA wa Songea, anaendelea

Padre Ettiene alikiuwa akiwasiliana na Bushiri. Bushiri alikuwa akiwasiliana na viongozi wa ngazi ya chini. Bahati mbaya, Wajerumani waliokuwa Dar-Es-Salaam, walianza mazungumzo na viongozi wa ngazi ya chini waliokuwa huko Dar-Es-Salaam.

Viongozi hao walikubali kuwatoa mateka hao kwa masharti matatu. Mosi, Waarabu waliokuwa wamekamatwa na Wajerumani wawaachie pili, Wajerumani walipe Rupia (Fedha za Kijerumani zilizotumika) na tatu, Wajerumani watoke katika maeneo ya Bagamoyo na Dar-Es-Salaam.

Pia, walitaka Manowari za Kijerumani zisikamate vyombo vya Waarabu majini vikiwa na watumwa katika maeneo ya Kunduchi. Uongozi wa Serikali ya Kijerumani ukiongozwa na Admiral Deinhart, ulikataa kutimiza masharti mawili ya mwisho.

Ulishauri Padre Ettienne, aendelee kufanya mazungumzo na wapiganaji. Wapiganaji walikuja juu sana. Walipata hisia kuwa, Wamisionari walikuwa kundi moja na Wajerumani wakoloni.

Padre Ettienne alijitahidi sana kumweleza Bushiri kuwa, ingawa mateka hao walikuwa Wazungu, lakini nia yao ya kufika Afrika ilitofautiana na Wazungu wengine.

Bushiri aliwaeleza wapiganaji wa ngazi ya chini tofauti iliyopo kati ya wamisionari hao na Wazungu wakoloni. Hapo, wapiganaji waliondoa madai mawili ya mwisho. Sasa, walitaka Wajerumani walipe Rupia 6,000 na wawaache huru Waarabu walioshikiliwa mateka pamoja na watu wengine.

Taarifa hiyo ilichelewa kumfikia Bwana Admiral Deinhard. Mbaya zaidi, Waarabu waliokuwa wamefika toka Muscat Arabia muda mfupi tu kabla ya uvamizi, waliongoza mazungumzo.

Waarabu hao walikuwa na siasa kali na hawakutaka kutofautisha kati ya Wamisionari na Wajerumani wengine.

Hata hivyo, Padre Ettienne, alifaulu kumshawishi Bushiri aende hadi Kunduchi walipokuwa wamisionari hao na Wajerumani wengine wakishikiliwa mateka. Akawatoa na kuwaleta kwenye kambi yake (Bushiri) iliyokuwa Kaole (kilometa tisa toka Bagamoyo).

Februari 28,1889, Wamisionari walihamishwa toka kambi ya Kaole na Bruda Rupert aliyeumizwa vibaya kule Pugu, alikuwa wa kwanza kuachiwa huru.

Alipelekwa Misioni ya Bagamoyo ambako alipokewa na mapadre wa Roho Mtakatifu na kupatiwa matibabu. Wakati huohuo, Padre Ettienne, aliendeleza mazungumzo na wapiganaji.

Bruda Romuald aliachiwa huru siku chache baadaye.

Machi 9, 1889. Mateka wote pamoja na Sista Benedikta, waliachiliwa huru wakaenda Bagamoyo. Toka Bagamoyo, walikwenda Zanzibar ambako walikutana na Padri Bonifas.

Aprili 4, 1889,Sista Benedikta pamoja na mabruda, walianza safari kurudi Ulaya.

Mei 1889, watu toka Pugu waliitarifu kampuni ya GEAS huko Dar-Es-Salaam kuwa, mifupa ya wamisionari waliouawa huko Pugu bado inalala huko.

Ndipo Bwana Heinrich Schimidt pamoja na kikosi cha askari walifika Pugu Juni 2,1889. waliona majengo yote yameharibiwa. Walifaulu kuona kirahisi mifupa ya Bruda Petro; na ya bruda Benediktini lakini, ilikuwa shida kuona mifupa ya Sista Martha.

Walitafuta mifupa yake huko na kule hadi kwenye bustani lakini hawakuuona mwili wake. Mara alifika Chifu wa eneo hilo, akaeleza kuwa mwili wake ulikuwa kanisani umeangukiwa na ukuta wa kanisa hilo.

Baada ya kutoa udongo waliuona mwili huo. Kisha kupata mifupa ya Wamisionari watatu, walitia katika masanduku matatu na kuzika karibu na makabauri ya wamisionari waliokuwa wamekufa kabla yao.

Makao mapya

Serikali ya Ujerumani ilifaulu kuzima nguvu za wapiganiaji huko Dar-Es-Salaam. Hali ilikuwa tulivu. Septemba 1889, Kiongozi wa mapadre wa Roho Mtakatifu aliyekuwa huko Zanzibar, aliandika barua kwa viongozi wa Shirika la Mtakatifu Ottilia wakimwomba Padre Bonifasi aende kuendelea na kazi yake.

Novemba 30,1889, Padre Bonifasi pamoja na mabruda wawili waliwasili Zanzibar. Walipata nafasi ya kuwasiliana na mapadre na masista ambao walimtunza wakati alipokuwa mgonjwa.

Desemba 1, 1889 walifika Dar-Es-Salaam. Kazi ya kwanza ilikuwa kutafuta nyumba ya kuishi. Walifaulu kupata nyumba na wakaanza kuitengeneza, Februari 28,1890 Padri Bonifasi aliandika barua kwenda St. Ottilia akiomba padre mmoja, mabruda sita na masista wengi inavyowezekana.

Alieleza kuwa hitaji la masista ni kubwa na kwamba zilikuwapo kazi nyingi. Wakati huo, jitihada zilifanyika kutengeneza nyumba. Mwishoni, zilipatikana nyumba mbili; moja kwa ajili ya watawa wanaume iliyojulikana kama "St. Joseph" na nyingine kwa ajili ya masista ambayo iliitwa "St.Maria".

Wamisionari wapya

June Mosi,1890, barua toka St. Ottolia ilileta ujumbe kuwa masista na mabruda wapya wangefika mapema. Mwezi mmoja baadaye, wamisionari wapya waliwasili Zanzibar. Padre Bonifasi, alikuwa pale kuwalaki.

Padre Franziskus Mayr, aliongoza kundi la masista saba na mabruda watano. Sr. Agnes alikuwa amechaguliwa kuwa mkubwa wao; wengine walikuwa Masista Scholastika, Juliana, Afra, Johanna, Pankratia na pia, palikuwa na manovisi wawili nao ni Helena na Tekla.

Julai 4,1890, wamisionari hao wapya waingia Dar-Es-Salaam na hapo wakapokewa na mabruda Joseph na Fridolin. Masista walianza kazi. Shida moja iliyowakabili ni kutokujua lugha waliyoongea wazalendo. Wamisionari hao walijitahadi kujifunza Kiswahili.

Maisha karibu na bahari

Wazungu waliotoka nchi ya baridi (Ulaya), waliona shida kuishi mahali penye joto kali kama Dar-Es-Salaam. Wakati mwingine wakiwa kanisani, ilimpasa Sista mmoja kutoka nje kwa muda ili avute hewa na kupata ubaridi kidogo. Walivumilia hayo yote.

Hata hivyo, walianza kuugua malaria katika ya mwezi mmoja tangu wafike. Karibu kila siku au bruda au sista alikuwa mgonjwa. Walitumia dawa ya "Quinine" kwa ajili ya kutibu malaria.

Wakati huo, hapa kwa daktari katikati ya mwezi Septemba Sista Johanna alianza kuugua. Septemba 20 mchana, akafariki.

Mazishi yake yalihudhuriwa na maafisa wa serikali pamoja na Wakristo wazalendo. Licha ya taabu na mahangaiko hayo, masista waliendelea na kazi za kuwashughulikia watoto waliogomkolewa, kuwatunza wagonjwa na kuwatembelea watu vijijini mwao . Pia, walishughulikia bustani iliyonunuliwa huko Kurasini.

Wakati huo huo Padre Bonifasi alizidiwa na homa; baada ya kupata Sakramenti ya Wagonjwa, alifariki Septemba 29, Januari 1891.

Taarifa ilipofika Pugu, watu wengi toka huko walifika kuuaga mwili wake mjini Dar-Es-Salaam. Wazungu, Wahindi na Wazalendo walifika. Xaver Baumanu pamojana mabruda wawili na masista Klara, Valeria, Monovisi Marcella, Raphaela na Winfrida waliwasili Dar-Es-Salaam.

Makala ya Jamii

Kijue kituo cha maendeleo ya kilimo cha Mogabiri

Na Christopher Gamaina,Tarime

KITUO cha Maendeleo ya Kilimo cha Mogabiri yaani MOGABIRI FARM EXTENSION CENTRE (MFEC), kipo umbali wa km.8 kutoka mjini Tarime. Pembeni kidogo mwa barabara iendayo kijiji cha Nyamwaga.

MFEC ni Shirika la Maendeleo Vijijini linalofanya kazi chini ya Kanisa la Kianglikana lililoko katika mkoa wa Mara.

MFEC ilianzishwa mwaka 1986 na lengo lake kuu, lilikuwa kuchangia katika kuboresha hali ya maisha ya wakulima walioko katika nyanda za juu, Tarime.

MFEC inajihusisha zaidi na programu za ushauri na mafunzo kwa wakulima katika shughuli mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa ardhi na kilimo cha mseto.

Pia, inajishughilisha na ufugaji wa ndani na ng’ombe wa maziwa na maendeleo ya jamii kwa jumla.

Dk. John Stephen ambaye ni Livestock Extrension Officer wa kituo hicho, katika mazungumzo yake na mwandishi wa makala hii hivi karibuni, alisema shughuli za MFEC zinafadhiliwa na wafadhili mbalimbali wakiwamo ICCO ya Uholanzi, Bread for the World ya Ujerumani, Serikali ya Tanzania na Kanisa la Kianglika Dayosisi ya Mara.

Alisema lengo lingine la kuanzishwa kwa MFEC wilayani Tarime, ni kuboresha uwezo wa wakulima wa nyanda za juu kutumia rasilimali walizonazo kujilelea maendeleo yao wenyewe.

Kwa mujibu wa Dk. John, kwa sasa shughuli za MFEC hufanywa katika vijiji 18 vilivyoko katika tarafa za Inchange, Inchungu na Ingwe wilayani hapa.

Aliongeza kuwa, walengwa wa maeneo ya kazi za MFEC ni wakulima wadogo wadogo; wanaume kwa wanawake wasio na mitaji mikubwa kwa ajili ya kuendeshea miradi mbalimbali.

Alisema kuwa, katika shughuli za hifadhi ya ardhi na kilimo mseto, mkazo unaelekezwa kwenye uzuiaji mmomonyoko wa ardhi katika Nyanda za Juu kwa kutengeneza na kutunza makingo, kupanda miti na mazao mchanganyiko.

Pia, MFEC, huhimiza na kufundisha matumizi madogo ya pembejeo za viwandani katika kilimo.

Katika shughuli za ufugaji wa ndani na ng’ombe wa maziwa, MFEC hushauri uundaji wa vikundi vya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa vinavyosaidia maendeleo ya shughuli za ufugaji katika vijiji vyao.

Vile vile, wanavikundi hupata ng'ombe mitamba wenye mimba au wasio na mimba kwa mkopo ili kuanzisha ufugaji wa ndani katika miji yao.

Vikundi hivyo vya ufugaji hujiendeleza kwa kutumia miradi ya uletaji pembejeo za kilimo vijijini mwao, kutafutiwa soko la maziwa, uboreshaji wa ng’ombe wa kienyeji (zebu) kwa kutumia madume bora.

MFEC ina programu ya maendeleo ya jamii inayohamasisha na kujenga moyo wa kujitegemea miongoni mwa wakulima wa nyanda za juu ili washiriki katika shughuli za kituo kwa hiari.

Kituo husaidia kuunganisha wakulima na taasisi mbalimbali kutatua matatizo yaliyo nje ya uwezo wa kituo.

Kituo huendesha shughuli za kilimo cha nafaka ili kuwahamasisha wakulima wadogo kuboresha uzalishaji wa ulezi kwa kutumia mbolea na kupanda kwa mistari.

Kilimo cha alizeti, ni moja ya programu za MFEC na lengo lake kubwa ni kuwawezesha wakulima kujipatia mafuta ya kula, kujiongezea kipato kutokana na ziada ya mafuta yanayopatikana baada ya kukamua alizeti, na kuboresha lishe ya mifugo kutokana na mashudu ya zao hilo.

Kituo kina programu ya kilimo cha migomba ili kuwaelimisha wakulima namna ya kuinua uzalishaji wa ndizi kwa kupanda migomba kwa nafasi, kutumia mbolea, utunzaji bora wa shamba la migomba na kupanda migomba yenye kutoa mavuno makubwa.

MFEC hushugulika pia na ufufuaji wa kahawa zao la biashara ambalo ni muhimu la katika Nyanda za Juu za Tarime.

Kituo hushauri wakulima kupanda mazao mengine katika shamba la kahawa ili kupunguza magugu na uzembe katika kuhudumia zao hilo.

Vile vile, wakulima hushauriwa kuungana katika vikundiili wawe na sauti moja katika kujadili bei ya zao hilo na utafiti wa soko.

Huwashauri wakulima kuendeleza ufugaji wa kuku wa kisasa ili kuinua lishe na kuongeza kipato kutokana na kuuza mayai ya ziada.

Shughuli za mashamba ya majaribio na maonesho hufanyika kituoni na vijijini ili kuwafundisha wakulima kwa vitendo mbinu bora za kilimo pamoja na kuthibitisha teknolojia kabla ya kutumiwa na wakulima.

Kituo cha MFEC hutoa mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa wakulima, wakulima wakufunzi, mabwana shamba na mabwana maendeleo.

Mafunzo haya hufanyika kituoni na vijijini. Vile vile, huduma na vifaa vya mafunzo vilivyoko kituoni kama madarasa na malazi , hukodishwa na taasisi mbalimbali zenye kuhitaji huduma hiyo.

Dk. John alisema MFEC inaendesha maduka mawili yaliyoko mjini Tarime na kituoni.

Katika ngazi ya vijiji, kituo kinahamasisha uanzishaji maduka kupitia vikundi vya wakulima.

Kwa upande wa shughuli za maendeleo ya vikundi vya akinamama, kituo kinashauri akina mama juu ya miradi mbalimbali ya kiuchumi inayowawezesha kujitegemea kupitia katika vikundi vyao.

Kipaumbele hutolewa kwa kilimo cha mazao ya nafaka.

Dk. John aliongeza kuwa MFEC iliyo chini ya uongozi wa Bw.Goodluck Kimaro ambaye ni Meneja, hushirikiana kwa karibu na mabwana shamba wa serikali walioko vijijini, maafisa wa maendeleo na wakulima wakufunzi katika kugundua matatizo na njia mbalimbali za kuyaondoa.

Pia, MFEC imeweka mkazo mkubwa kwenye uundaji wa vikundi imara vya wakulima katika ngazi za vijiji ambavyo vinaweza kujiimarisha na kusaidiana kuleta maendeleo ya wanavikundi na wananchi kwa jumla.

‘MFEC pia hutoa mkopo wa baiskeli kwa wakulima kwa mkataba wa miaka miwili bila riba na tunatarajia kuongeza vijiji 12 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu ili kituo kuendeshe shughuli katika vijiji 30 badala ya vijiji 18 vilivyopo kwa muda huu, " alisema Dk. John na kuongeza,

"Lengo kuu la kuongeza vijiji hivyo ni kuendelea kuinua hali ya maisha ya wakulima wadogo katika Nyanda za juu,’ alisema