IJUE AFYA YAKO

Je, unaweza kupona bila dawa?

MAGONJWA mengi hayahitaji tiba. Miili ina njia mbalimbali za kukinga maradhi. Njia hizi ni bora zaidi kuliko kutumia dawa.

Magonjwa mengi, kama vile mafua na fluu hupona bila ya dawa.

Ili kusaidia kukinga na kishinda maradhi ni lazima kujimudu katika hali hizi;

- kujiweka katika hali ya usafi.

- Kula chakula bora.

- Kupumzika vya kutosha

- Kufanya kazi na mazoezi

Hata kama ugonjwa ni wa kutisha na unahitaji dawa, mwili unaopambana na ugonjwa, dawa huwa zinasaidia tu. Jambo la muhimu ni usafi, kupumzika na kula chakula bora.

Huduma za kiafya hazitegemei dawa.

Hata kama unaishi sehemu ambazo hazina dawa za kigeni, kuna mengi unayoweza kufanya ili ukinge na kutibu magonjwa mengi mradi tu, uelewe namna ya kufanya.

Magonjwa mengi yanaweza kukingwa na kutibiwa bila ya kutumia dawa.

Kama watu wanaelewa namna ya kutumia maji vizuri, itakuwa njia nzuri ya kinga na kuponyesha magonjwa bila ya kutumia dawa.

Kuponya kwa maji

Wengi tunaishi bila ya kutumia dawa lakini, hakuna hata mmoja anayeweza kuishi bila maji. Ukweli ni kwamba, zaidi ya asilimia 57 ya mwili wa mwanadamu, ni maji.

Kama kila aishiye vijijini angeweza kutumia maji vizuri, basi magonjwa na vifo hasa kwa watoto wadogo yangepungua sana.

Kwa mfano, matumizi mazuri ya maji ni msingi wa kuzuia na kutibu ugonjwa wa kuharisha. Kuharisha ni ugonjwa mkubwa na wenye kuleta vifo kwa watoto wadogo katika sehemu nyingi ulimwengu. Maji machafu husababisha ugonjwa huu pia.

Njia mojawapo muhimu ya kuepuka ugonjwa huu wa kuharisha ni kuchemsha maji ya kunywa na kupikia hasa kwa ajili ya watoto wachanga.

Chupa ya maziwa na vyombo vingine vya mtoto mchanga, vinabidi pia vichemshwe kabla na baada ya kutumiwa.

Mikono lazima ioshwe kwa sabuni baada ya kutoka msalani, kabla ya kula chakula.

Ukosefu wa maji mwilini ni sababu kubwa ya vifo kwa watoto wenye ugonjwa wa kuharisha.

Kama mtoto anapewa maji mengi yenye chumvi na sukari na asali kidogo, hii itakinga na hata kutibu upungufu wa maji mwilini.

Kumpa mtoto mwenye kuharisha maji mengi, itamfaa zaidi kuliko dawa. Ukweli ni kuwa umpapo maji ya kutosha hutahitaji kumpa dawa yoyote ya kutibu kuharisha.

Nyakati ambazo matumizi mazuri ya maji yanasaidia zaidi kuliko dawa.

Kuhara, minyoo, ugonjwa wa tumbo namna ya kukinga, tumia maji, chemsha maji ya kunywa, osha mikono.

- Ugonjwa wa ngozi

- Oga kila siku

- Vidonda vyenye usaha, pepopunda; osha vidonda kwa maji na sabuni

Kutibu:

Kuharisha na upungufu wa maji mwilini, tumia maji, kunywa maji mengi.

-Homa; Osha kiwiliwili na maji baridi

-Homa kali

-Ogesha kiwiliwili kwa maji baridi

-Mkojo mchafu (hasa kwa akinamama)

-Kunywa maji mengi

-Kukohoa, pumu, nimonia, kifaduro - kunywa maji mengi na fukiza mvuke wa maji ya moto.

-Vidonda, baka la ngozi au kichwa na chunusi

-Sugua kwa maji ya sabuni.

-Madonda ya vijidudu yanayochonota - kanda kwa maji ya moto.

-Maumivu ya misuli na viungo

-Kanda kwa maji moto

-Kuwashwa na malengelenge ya ngozi

-Kanda kwa maji baridi.

Kuungua moto kidogo

- Paweke ndani ya maji baridi.

- Magogore au mafindofindo(sore throat au tonsillitis)

- Sukutua maji moto ya chumvi.

- Esidi au takataka iliyoingia jichoni - osha upesi kwa maji baridi.

Mafua - vuta maji ya chumvi

-Kuvimbiwa na kupata choo kigumu

-Kunywa maji mengi, pia kuinika ni bora kuliko dawa za kulainisha choo. Usitumie mara kwa mara).

Kwa kila mfano uliotolewa awali,(isipokuwa nimonia), inaonesha kwamba kama maji yatatumiwa vizuri mara nyingi, dawa hazitahitajika.

Somo hili litapanua mawazo mbalimbali ya kuweza kuponyesa bila kutumia dawa. Tumia dawa tu, kama zinahitajika kweli.

Matumizi mazuri na mabaya ya madawa ya kisasa

Baadhi ya madawa yanayouzwa na mkemia au maduka ya vijijini, husaidia sana.

Watu wengine wana tabia ya kutumia dawa nzuri vibaya na hii humuumiza mgonjwa ili dawa iweze kufanya kazi yake ni lazima itumiwe vizuri.

Watu wengi wakiwemo madaktari na waganga, hutoa dawa nyingi kuliko inavyotakiwa na kufanya hivyo, huzidisha magonjwa na vifo.

Kuna hatari katika matumizi ya madawa.

Dawa fulani zina hatari zaidi kuliko nyingine. Lakini, watu wengine hutumia dawa zenye hatari kwa magonjwa madogo madogo tu.

Watoto wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa sababu mama yake alimpa dawa ya hatari "Chlorophenical" eti kutibu mafua tu. Usitumie dawa yenye hatari kwa ugonjwa mdogo.

Mwongozo wa kutumia dawa:

- Tumia dawa tu, ikiwa ni lazima.

- Kila dawa uitumiayo, ni lazima ufahamu matumizi yake barabara na namna ya kujihadhari.

- Hakikisha unatumia kipimo kamili.

- Kama dawa haisaidii au inaleta matatizo, usiitumie tena

- Kama huna hakika, muone mganga.

Hatari za kutumia dawa vibaya

Hii ni orodha ya makosa ya kawaida tunayofanya tunapotumia madawa ya kisasa. Matumizi mabaya ya madawa yafuatayo yanaleta vifo kila mwaka, kuwa mwangalifu Chloramphenical (chloromycetin) - Kwa bahati mbaya, dawa hii hupendelewa sana kutumiwa kwa magonjwa madogo madogo kama vile kuharisha. Hii, ni hatari sana.

- Dawa hii inatumika kutibu magonjwa kama vile homa ya matumbo. Isitolewe kwa watoto wachanga.

- Oxtocin(pitocin) pituitrin na Ergonovine (Ergotrate) - kwa bahati mbaya wakunga hutumia dawa hizo kuharakisha kuzaliwa kwa mtoto au kumpa nguvu mzazi wakati akiwa na uchungu wa kujifungua.

Matumizi ya namna hii yana hatari sana. Unaweza kumwua mama au mtoto. Zitumie tu, kwa kuzuia kutoka damu baada ya mtoto kuzaliwa.

- Sindano za dawa: Imani kuwa sindano ni bora kuliko vidonge si ya kweli. Mara nyingi dawa za kunywa zinafanya kazi vizuri zaidi kupita sindano. Pia, dawa nyingi zitolewazo kwa sindano huhatarisha maisha kuliko za kunywa. Matumizi ya sindano lazima yapunguzwe.

- Penisilini: Penisilini hufanya kazi kwa magonjwa fulani ya kuambukiza. Ni makosa kutumia dawa hii kwa shida za kustuka misuli, kujiponda, aina yoyote ya maumivu au homa.

Kwa kawaida, majeraha yoyote ambayo hayakuchubua ngozi, ijapokuwa kuna uvimbe mkubwa ni vigumu vijidudu kuingia kwa hivyo hakuna haja ya kutumia penisilini au dawa nyingine yoyote ya kuua wadudu.

Penisilini ina hatari kwa watu wengine. Kabla ya kuitumia lazima ufahamu hatari zake na namna ya kuzizuia.

- Sindano za Penisilini na Streptomisini (zina majina mengine mengi)- Dawa hizi hutumika sana na mara nyingi kwa magonjwa yasiyohusika. Dawa hizi zisitumiwe kwa mtu aliye na mafua kwa sababu haziponyeshi ugonjwa wa mafua au fluu, zinaweza kusababisha matiti makubwa wakati mwingine, kuzimia au kifo, zikizidi kutumiwa ovyo ovyo, zitafanya magonjwa kama kifua kikuu na magonjwa mengine ya hatari yasiyoweza kuponyeka.

Vitamini B12; Dawa hii haisaidii kutibu ukosefu wa damu au udhaifu isipokuwa kwa wagonjwa wachache tu. Inaweza kutumika tu, kama mganga ndiye karuhusu baada ya vipimo vya damu. Karibu magonjwa mengi ya damu yanatibiwa kwa kutumia vidonge vya madini ya chuma (Ferrous Sulphate).

Vitamini Nyinginezo: Kwa kawaida, usidunge sindano za vitamini. Sindano hizo zina hatari, ni ghali na hazifanyi kazi yake vizuri kama vidonge.

Bahati mbaya, watu wengi hupoteza fedha zao kwa kununua dawa za maji ambazo zinasemekana zina vitamini. Ukweli ni kwamba nyingi kati ya dawa hizo hazina vitamini. Hata kama zingekuwa navyo ni afadhali kununua chakula kingi na kilicho bora.

Kujenga na kuhifadhi mwili kunahitaji vyakula kama mayai, nyama, matunda, mboga za majani na nafaka; ambavyo vyote vina vitamini na nguvu za kukuza mwili. Mtu mwembamba na aliyedhoofika akipewa chakula bora mara kwa mara, kitamsaidia sana kuliko kumpa vitamini na chumvi chumvi.

Mtu anayekula vizuri hahitaji nyongeza ya vitamini.

Njia bora ya kupata vitamini.

Kumbuka:

Waganga na madaktari wengine, hutoa dawa wakati hazihitajiki mara kwa mara ni kwa sababu wanafikiri kuwa, wagonjwa wanatazamia kupata dawa na hawataridhika kama hawatapewa.

Ni vizuri kuwaomba daktari au mganga wako dawa wakati unapohitaji tu, la sivyo, unaweza kuharibu afya yako.

Tumia dawa ukiwa na hakika kuwa inahitajika na ukiwa na huku ikiwa na uhakika namna ya kuitumia.

Kalsium

Kuna hatari kubwa sana kumpiga mgonjwa sindano ya Kalsium kwa kutumia mshipa wa damu. Kama njia hii inatumika, ni lazima dawa inyunyizwe taratibu sana. La sivyo, itaua mara moja. Ukipiga matakoni, inaweza kusababisha jipu.

Usipige sindano ya kalsium kabla hujapata ushauri kutoka kwa mganga.

Kumbuka:

Huko Mexico na katika nchi nyingine ambako watu hutumia sana mahindi au vyakula vilivyotayarishwa na kuchanganywa na chokaa, haifai kutumia sindano, au vidonge vya kalsium (kwani mara nyingi hutolewa ili kurejesha nguvu ya mwili au kusaidia kukua kwa mtoto).

Mwili hupata kalsium inayohitajika kutokana na chokaa.

Kulisha kwa kutumia mishipa ya damu

Katika sehemu nyingine, watu walio na ukosefu wa damu au wadhaifu sana, hutumia fedha zao hadi senti ya mwisho kwa ajili ya kuwekewa dawa za maji katika mishipa yao ya damu.

Wanaamini kuwa kufanyiwa hivyo, kutawafanya wawe na nguvu za kuwa na damu safi. Lakini, wanajidanganya.

Hakuna kitu chochote katika dawa hii inayotolewa kupitia katika mshipa wa damu isipokuwa, ni maji matupu pamoja na chumvi chumvi au sukari. Haiongezi nguvu kuliko kipande kikubwa cha pipi na inafanya damu iwe nyepesi na sio nzito kama vile wanavyofikiria.

Haiponyeshi upungufu wa damu wala kumfanya mnyonge kuwa mwenye nguvu.

Na kama inatolewa na mtu asiye na ujuzi, kuna hatari ya kuingia vijidudu vibaya katika damu, na hii inaweza kumwua mgonjwa.

Dawa hii itumike tu, kwa mtu ambaye hawezi au haruhusiwi kula au ana ukosefu mkubwa wa maji mwilini.

Kama mgonjwa anaweza kumeza, mpe maji yaliyochanganywa na sukari pamoja na chumvi kiasi kipatacho painti mbili(tazama vinywaji vya kurudisha maji) - Dehydration drink, itamsaidia sana kuliko ukimpa kwa kupitisha katika mshipa wa damu.

Kwa wale ambao wanaweza kula, wanaweza kupata nguvu za kutosha kwa kula chakula bora kuliko kutumia aina yoyote ya dawa za maji zinazolishiwa kwa njia ya mishipa ya damu.

Kama mgonjwa anaweza kumeza na kuyahifadhi maji tumboni

Dawa za kuharisha na kulainisha tumbo

Wakati wowote kuna hatari ikiwa utampa mtoto au mtu mzima aliye mdhaifu mwenye ukosefu wa maji mwilini au mwenye tumbo la kusokota, dawa ya kuharisha au kulainisha tumbo.

Kwa bahati mbaya, watu wengi wana imani kuwa dawa ya kuharisha inamrudishia mtu afya nzuri au inasafisha vitu vyote mwilini. Sura ya kwanza imeelezea kuwa dawa za kuharisha au dawa za kulainisha tumbo, zinaleta matatizo zaidi kuliko inavyotegemewa.

Ni Wakati gani dawa zisitumike?

Watu wengi wanaamini kuwa kuna vitu ambavyo hawawezi kufanya au kula wakati wanapotumia dawa.

Kwa sababu hii, wanaweza kuacha kutumia dawa ambazo inabidi watumie.

Ukweli ni kwamba hakuna dawa ambayo inaweza kuleta madhara eti kwa sababu imenywewa wakati wa kula chakula fulani- hata kama iwe ni nyama ya nguruwe, pilipili, mapera, machungwa au chakula cha aina yeyote.

Lakini, vyakula vyenye mafuta au viungo, vinaweza kukuletea tatizo la tumbo hata kama hukumeza dawa. Kuna dawa nyingine zinaweza kudhuru iwapo mtu atakunywa pombe.

Kuna nyakati ambapo si vizuri kutumia dawa, kwa mfano:

- Mjamzito au mama mwenye kunyonyesha, hana budi kuepuka dawa ambazo si lazima atumie (lakini anaweza kutumia vitamini na vidonge vya damu bila kudhuru chochote).

- Kwa upande wa watoto wachanga ni vizuri kuwa mwangalifu sana kwa kuwapa dawa.

Ikiwezekana na afadhali upate ushauri wa waganga kabla ya kuwapa dawa yoyote.

Hakikisha huzidishi kipimo.

- Mtu yeyote ambaye amekwisha pata matatizo kama kuvimba, kuwashwa, na kadhalika, baada ya kutumia penisilini, Ampisilini, Sulfonamide au dawa nyingine zozote, inambidi aache kabisa kutumia dawa hiyo kwa muda wa maisha yake yote kwa sababu inaweza kumletea hatari kubwa.

- Kuna dawa maalumu ambazo ukizitumia, zinadhuru wakati ukiwa na ugonjwa fulani kwa mfano mtu mwenye ugonjwa wa ini, hatibiwi na dawa za kuua vijidudu au dawa zozote kali, kwa sababu ini halifanyi kazi hivyo, dawa hizo zinaweza kudhuru mwili.

- Watu ambao wamepungukiwa maji ya mwili au wana ugonjwa wa figo, ni lazima wawe waangalifu wa dawa wanazotumia.

Usitoe zaidi ya kipimo kimoja cha dawa ambayo inaweza kudhuru mwili mpaka uwe na uhakika kama mgonjwa anakwenda haja ndogo kama kawaida.

Ubinafsi katika jamii ni nini?

l Lakini kwanini upo

Na Erasto Duwe, Songea

UBINAFSI ni neno linalofahamika na kutumiwa na watu wengi katika maisha ya kila siku.

Ubinafsi ni ile hali ya mtu mmoja au kundi la watu fulani kumiliki, au kuhodhi kitu au mali ya jumuiya kwa manufaa yao binafsi.

Kwa mali ya jumuiya, inabidi itumike kwa manufaa na maendeleo ya jumuiya nzima inayohusika ikiwa kinyume chake, basi huo ndio tunaoita, UBINAFSI au UMIMI.

Ladha ya ubinafsi

Ubinafsi kwake afanyaye mali ya jumuiya kuwa ni yake, ni mtamu sana kushinda utamu wa sukari, kwani ubinafsi huo humletea mbinafsi manufaa katika nafsi yake kadiri ya matakwa yake.

Kwa upande mwingine, ubinafsi huo huo, ni jambo linalosababisha maumivu makali kwake au kwao wanaotendewa hivyo na hivyo, kukosewa haki zao. Tena si kwao tu, bali hata kwa wakereketwa wa haki na usawa wa binadamu.

Ubinafsi na hali halisi ya maisha

Ubinafsi kwa wenyewe, sio jambo zuri kwani unakosea haki za binadamu. Matatizo mengi yaliyopo katika jamii na yanayoendelea kutokea, chanzo chake kikubwa ni ubinafsi.

Mathalani, mafarakano na msambaratiko wa watu katika jamii hutokana na ubinafsi wa pande fulani za watu. Tatizo sugu la rushwa linalozidi kushamiri na kukita mizizi yake katika jamii, sababu yake kubwa ni ubinafsi.

Watu huzifikiria kwanza nafsi zao badala ya kutoa misaada kwa wahitaji, bila "kitu kidogo", huduma haipatikani.

Jamii zetu zinakosa maendeleo na kuzidi kudidimia tu, kwa sababu ya "umimi.

Tatizo sugu la vita vinavyotokea kati ya mataifa, ukichunguza kwa undani na kufuatilia, utagundua kuwa, chanzo kikubwa ni ubinafsi.

Hakuna anayetaka kujishusha mbele ya mwenziye kila mmoja anataka aoneshe "ubabe" wake mbele ya mwenzake.

Matokeo yake, ndiyo migongano kadha wa kadha katika jamii.

 

Ubinafsi na Maandiko Matakatifu.

Maandiko Matakatifu yanapinga ubinafsi na hata kuonesha wazi adhabu yake.

Yanatudai, kutusihi na hata kutuomba kuwa na amani, upendano na ushirikiano kati yetu.

Katika kitabu cha MATENDO YA MITUME tunasoma hivi, "Jumuiya yote ya waamini ilikuwa na moyo na roho moja. Hakuna mmoja aliyekuwa na kitu chochote akikiweka kuwa mali yake binafsi ila, waligawana vyote walivyokuwa navyo..." (Mdo 4:32-36).

Katika fasuli ya tano ya kitabu hichohicho, tunaona kuwa, waliotenda dhambi ya ubinafsi na kumdanganya Roho Mtakatifu, wanapata adhabu ya kifo.

Hao ndio anania na Safira.

Twamsikia Petro akiuliza, "Anania, mbona shetani ameuingia moyo wako na kukufanya udanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba?... Anania aliposikia hayo alianguka chini akafa..." ndiyo mambo yalivyokuwa kwa Safira mkewe.

Soma(Mdo 5:1-11). Zipo sura nyingi za Maandiko Matakatifu zinazoelezea kosa hili la ubinafsi na mapato yake ambayo daima ni mahangaiko.

Hali halisi na ushauri nasaha.

Ubinafsi sio jambo zuri, ni kinyume kabisa na haki za binadamu. Tena, ni kinyume kabisa na Amri Kuu ya Mapendo, inayotusihi kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda sisi wenyewe au kama tunavyozipenda nafsi zetu.

Ubinafsi unarudisha nyuma maendeleo ya kimwili na kiroho(rejea Anania na Safira) Tena, ubinafsi huo hatima yake ni mahangaiko makubwa. Ubinafsi huzua mitafaruku, mafarakano na misambaratiko.

Katika wenzetu, tuuone uso wa Mungu na hivi tuishi kwa mapendo kidogo kiwacho na kikubwa kitumike kwa ajili ya manufaa ya jumuiya nzima na sio kwa manufaa ya mmoja au wachache.

Changamoto la Utamadunisho Barani Afrika

Na John Mbonde

UTAMADUNI ni dhana pana ikiwa ni pamoja na kukua na kukomaa kwa akili na mwili wa binadamu kutokana na mafunzo au uzoefu wa kutenda kazi.

Utamaduni unaoanisha mfumo mzima wa maisha kwa kadiri ya mila, desturi na mapokeo ya mang’amuzi ya jamii.

Kwa hiyo, utamaduni unagusa nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku ya binadamu kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

Mathalani, utamaduni wa mavazi, chakula, kazi, malazi, ndoa, malezi ya watoto na urithishaji wa tunu mbalimbali za koo na makabila ya jamii. Tunu hizo ni pamoja na imani(dini) na miiko na mistakabali yao.

Suala la utamadunisho katika uenezai wa Habari Njema, lilipewa msukumo mpya na wa pekee wakati wa sinodi ya Afrika.

Papa Yohane Paulo wa II katika kuiwasilisha Sinodi nyumbani yaani barani Afrika, pamoja na mambo mengine, alitilia mkazo suala la umuhimu wa utamaduni.

"Utamadunisho ni mwendo wa kuelekea kwa uenezaji Injili kamili. Unatafuta kuandaa watu kupokea ujumbe wa Yesu Kristo kwa jumla. Unawagusa kibinafsi, kijamii, kitamaduni, kiuchumi na kisiasa; ndipo waishi maisha ya utakatifu kwa muungano na Mungu Baba kupitia tendo la Roho Mtakatifu." (Na. 62 Kanisa Barani Afrika uk. 47).

Hivi karibuni timu maalumu ya wataalamu wawili ya Kamati ya Kuhamasisha Roho ya Umisionari(MAC), iliendesha semina mbili moja mjini Moshi na nyingine mjini Arusha ambayo ilihudhuriwa na waseminari wanaojifunza falsafa na Mashirika ya Kitawa saba tofauti.

Awali semina iliyofanyika kwenye Chuo cha Don Bosco cha Wasalesiani huko Moshi. Washiriki wake walikuwa wakitoka katika nchi za Nigeria, Ghana, Siera Leone, Kenya, Uganda, Sudan na Tanzania.

Hapa palikuwa na mchanganyiko mkubwa wa tamaduni tofauti za Afrika Magharibi, Kati na Mashariki.

Kule Arusha, chini ya uongozi wa Seminari Kuu ya Spiritani, iliyopo Njiro, jumla ya washiriki 122 watawa wa kiume na wa kike, walihudhuria na kupata changamoto mintarafu mada zile zile.

-Fasihi Simulizi ya Kiafrika ni chemichemi tajiri ya Falsafa na Teolojia ya Kiafrika.

-Teolojia simulizi ya Kiafrika kutoka methali, misemo, hadithi na nyimbo.

-Tofauti na msingi juu ya mwito na haiba, ujumbe, kanisa la mahali utamadunisho na wajibu wake barani Afrika.

-Tathmini ya utekelezaji wa maadhimisho ya Jubilei Kuu ya mwaka 2000 jimboni Moshi.

-Athari ya vyombo vya kisasa vya habari katika suala la Uinjilishaji.

-Jubilei Kuu ya mwaka 2000 ujumbe wake na jinsi unavyoenda sambamba na mwanzo wa Karne ya 21.

-Misemo ya vijana wa mijini katika Afrika Mashariki

-Makongamano ya kimisionari na maadhimisho yaliyofanyika mjini Roma, Italia Okotba 2000.

Wanasemina kwa mvuvumko na mwamko wa pekee, walijadili maeneo muhimu ya utamaduni ambayo yangeweza kutamadunishwa hatua kwa hatua ili kuleta ari mpya ya kumpokea, kumfuasa, kumtangaza na kumuishi Yesu Kristo.

Walibaini kuwa katika fasihi simulizi ya Kiafrika, kulijaa hazina kubwa ya kuboresha na kuimarisha maisha ya Kikristo.

Hata hivyo, wanasemina walisisitiza kwamba, Kanisa la mahali lisifanye pupa au kutamadunisha kwa mitindo wa zimamoto, bali ufanyike utafiti wa kina na kwa makini zaidi, ili kuchuja na kupembua kabla ya kutekeleza.

Wakinukuu maelezo kutoka kitabu 'Kanisa Barani Afrika', bila ya kupuuza mapokeo halisi ya Kanisa la Mashariki au Magharibi, utamadunisho wa Liturujia, mradi tu haubadilishi vipengele maalumu, ufanywe ili waamini waweze kuelewa na kuishi maadhimisho ya liturujia.

Kwa kuyakumbuka haya, Sinodi ilionesha tumaini kwamba mabaraza ya maaskofu yatashirikiana na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Kikatoliki, wangebuni kamati za utafiti wa mambo yanayohusu ndoa, matambiko na ulimwengu wa mambo ya kiroho ili kuchunguza kwa undani sehemu zote za utamaduni na shida kulingana na maoni ya kiteolojia, kisakramenti, kiliturujia na Sheria za Kanisa’ (Uk 48-49).

Katika vikundi vya majadiliano wanasemina walizingatia kuwa suala la umisionari ni la wabatizwa wote. Je, upi ni wajibu wa wamisionari na mashirika ya kitawa iwapo suala la utamadunisho wajibu wa waamini wazawa (wahusika wakuu na wakala) wa kanisa la mahali?

Uchambuzi na uhakiki , fasihi ya Kiswahili(2)

Tamthiliya hii, USHUHUDA WA MIFUPA, ilipata ushindi wa kwanza miongoni mwa miswada 160 iliyoshindanishwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mwaka 1989 baada ya jopo maalumu kuzichambua kwa kina chake.

Mwandishi hana budi kupongezwa kwa ubunifu wake wa wahusika wa USHUHUDA WA MIFUPA maana wanasawiri barabara hali halisi kama ilivyo katika jamii. Wahusika ni hai siyo vivuli. Mathalani, Ngariba, Mtambaji, Meneja, Dokoa, Toza, Makalikiti, Korido-Dokta, n.k. yote yanatanabaisha kwa namna moja au nyingine jinsi kila mhusika anavyomhusu awaye katika nafasi yake katika jamii.

Hali kadhalika, uhai wa mchezo umeongezewa msisimko kwa matumizi ya ngoma na muziki kama kichocheo licha ya lugha ya picha aliyotumia.

Amekuwa hodari na makini katika kujenga taswira kwa ustadi wa aina ya pekee toka mwanzo wa tamthiliya hadi mwisho wake. Igizo la aina hii, lingekuwa gumu sana kuoneshwa katika mchanganyiko wa wazazi na watoto lakini, inawezakena kwa jinsi mtunzi alivyotumia mtungo wa kitasifida kwa kupunguza makali lakini bila ya kumficha ukweli.

DHAMIRA

Dhamira kuu hasa ni kuutanabaisha umma kuhusu tishio la ugonjwa huu sugu wa UKIMWI (AIDS).

Kutokana na dhamira hii kuu, kumeibuika vijidhamira tata ambavyo vinahusisha UKWIMI :

- Uchawi na Ushirikina (Jujuoloji)

- Siasa kali (Marekani dhidi ya Cuba na Urusi)

- Suala la ndoa na mapenzi

- Mgongano wa fikra na sera potofu

- Ustaarabu wa mfumo mpya wa maisha baada ya kuingia UKIMWI.

Dhamira kuu na kuzungukwa na vijidhamira hivyo, hutoshelezana katika kuufikisha ujumbe kwa wahusika.

UCHAMBUZI

Tofauti na tamthiliya nyingine nyingi, tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA ina onesho moja la mfululizo ambalo lina vijisehemu fulani fulani kadiri wahusika wanavyoingia na kutoka jukwaani.

Muundo wake ni wa moja kwa moja unaozingatia dhamira moja. Mathalani, chanzo cha UKIMWI; Njia za kuambukiza; Hisia potofu dhidi ya chanzo na njia zinazosambaza ugonjwa huo; majina mbalimbali ya UKIMWI n.k.

WAHUSIKA

Wahusika katika tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA, wangeweza kuitwa kwa majina ya nchi wanayowakilisha. Kwa mfano, Marekani, Afrika, Cuba, Russia n.k.

Hata hivyo, wahusika wamepewa majina ya jumla kama vile: Mfupa, Mtambaji, Mtu, Mtu 1-5, Muuguzi, Daktari, Korido Dokta, Ngariba, Makalikiti, Toza, Meneja Dokoa, Mtani, wote n.k.

Baadhi ya majina ya jumla ya wahusika hao yanaelezea tabia yao. Kwa mfano, ngariba ni mtu mwenye ujuzi wa kutahiri katika jando: Korido - Dokta limetoholewa kutoka Kiingereza , "Corridor-Doctor" likimaanisha daktari wa mitaani au vichochoroni. Makalikiti limetokana na wanawake wanaotumia mikorogo ili kubadilisha nywele zao (Curlykit).

Meneja Dokoa ni sawasawa na Meneja mwizi. Aidha, wahusika Mtu 1-5 wanaweza kushika nafasi mbalimbali tofauti katika tamthiliya hii.

(I) Mfupa(mfu):

Wako wahusika watano (I-V) ambao wanatumia jina Mfupa. Wahusika hao wanashirikiana katika kujadili chanzo cha UKIMWI na njia za kuambukiza. Mgogoro huo wenye utata, ni tishio la angamizo la binadamu. Na wahusika wote hujulikana kwa jina, MFUPA.

(ii) Mtambaji:

Mhusika huyu anakuwa ndiye anayeongoza mdahalo baina ya Mmarekani, Mwafrika, Mkyuba na Mrusi. Baadaye, kuanzia uk. wa 11, anashiriki mazungumzo.

(iii) Mtu:

Kuna wahusika sita wenye kutumia jina mtu (I-VI). Bindamu hai tofauti na wahusika vivuli "Mfupa"

a) Mtu 2

Anawakilisha Marekani, ambaye anadai wamefanya utafiti na kugundua kile kiitwacho upungufu wa kinga mwilini (Acquired Immune Deficiency Syndorme =AIDS)

b) Mtu 3

Ni Mwafrika. Ana hasira. "Wewe Marekani msenge nini?" (uk 4). Pia Mtu 3 anaitwa Bwana Jujumani, na Mtu 2 (Marekani) "Wamezoea hawa Marekani, kila kitu kibaya ni cha Mwafrika. Maaluni hawa! Mabaradhuli wakubwa!" uk 4. Mt 3 (Mwafrika) anaonesha ujasiri wake bila woga, "Ninyi hamjui jujuoloji!" (uk.5)

c) Mtu 4

Ni Mkyuba. "Wamezoea. Wapashe! Sisi Wakyuba tumewachoka," (uk 4).

Mkyuba huyo ni Fidel Castro "Acha ubishi wa kijinga Madevu", uk 4 . (Rais Fidel Castro ana madevu).

d) Mtu 5

Ni Mrusi. Anadharau utafiti wa Marekani. Anawashuku Marekani kuwa ndio waliozalisha virusi katika maabara vimesambaa kutoka kwenye maabara.

Wauguzi wawili

e) Muuguzi I.

Ana utovu wa uwajibikaji, maana yampasa kujua mapema mahitaji yote ya matibabu badala ya kulaumu zahanati: "Ah! Hili stovu halina mafuta hata tone!" (uk. 6) Mpumbavu hana mpangilio wa kazi.

f) Daktari:

Mtaalamu na ana uzoefu, "Lo! Mgonjwa mwenyewe huyu anahitaji kuwekewa damu mara moja". Tofauti ya Daktari Vs Dokta.

g) Korido-Dokta:

Dokta wa vichochoroni, mitaani.

Hana maadili ya udaktari, ingawa amespeshelaizi ng’ambo. Ana uroho wa pesa. Anatembea na zana na dawa katika begi. "Basi kila mtu mahali pake. Na mimi mahali pangu ni kwenye begi hii. Begi hii ina kila kitu..."

h) Ngariba

Mhusika huyu huwakilisha waganga wanaofanya kazi ya kutahiri, kutoga masikio, pua, kukata vimeo.

I) Makalikiti

Mhusika Makalikiti ni mwanamke ambaye ametumia mikorogo kwa ajili ya kulainisha nywele zake. Ni malaya. Amejirembesha kwa mavazi na marembo ili kuwa chambo kwa wateja.

Anasoma kidato cha sita. Hujinadi haraka kwa wateja. Anaposifiwa na Meneja "Hupendelea dogodogo za shule kama wewe," Makalikiti hujibu "Uwongo tu".

j) Toza:

Mhusika mwanamume anayegeuza sauti ya kike. Ni kuhadi, malaya.

k) Meneja: Meneja anajulikana kwa jina, Dokoa.

Dokoa, jina hili linahusiana na tabia yake ya udokozi (wizi, hujuma). Ni meneja wa Kampuni ya Kondomu. ana majivuno. "Ha! Ha! Ha! Ni mtu mkubwa kidogo, anajisifia" uk. 12.

Ana majivuno na mpenda sifa. Kwa mfano, anapoongea na Mtamkaji, Meneja Dokoa anajitamba, "Oh! Kumbe unanifahamu... er Ndiyo. Jina langu ni Meneja Dokoa... Lakini siku hizi nimepata uwaziri mdogo kwenye Wizara mpya ya Kondomu. Kwani bado hujasikia...? (uk. 14)

l) Mtani: Mhusika ambaye katika mila na desturi za makabila mengi, ni kiungo katika tambiko, ugonjwa, sherehe na hasa kifo (msiba).

Wahusika wengine huingia kama vitu, sauti, ngoma, Sokwe, n.k.

Matumizi ya Lugha

Lugha iliyotumika ni nyepesi, fasaha na sanifu. Kwa matumizi ya lugha ya kawaida, inaiwezesha tamthiliya hii kueleweka moja kwa moja na watu wa kawaida mijini na vijijini.

Matumizi ya Lugha na Fani:

Ana hakika, msanii Ibrahim Ngozi, amefaulu sana katika kuuelimisha umma mintarafu chanzo na athari za UKIMWI kwa lugha nyepesi lakini iliyojaa ufasaha, hekima na busara.

Kwa kutumia misemo, misimu na lugha ya mitaani inapatikana. Tamthiliya hii ina umuhimu wa pekee na kwa wakati muafaka ambapo usugu wa UKIMWI unaangamiza maelfu ya watu kila siku itokayo kwa Mungu na iendayo kwa Mungu.

Fauko ya umuhimu huo, kasi ya uambukizaji UKIMWI yadai mbinu na mikakati madhubuti zaidi. Lugha ya mitaani(kifo kazini; Acha Iniue Dawa Sina (AIDS); simufiti; eidesi; Acha Iniue Dogodogo Siachi uk. 15).

Majina hayo ya UKIMWI ingawa yanatolewa katika lugha ya mitaani kama kichekesho, yanaashiria juu ya ugumu wa kuwaelimisha watu kuchukua tahadhari.

Pia lugha ya Kiingereza imetumika hapa na pale ili kusisitizia maana ya kina kwa kutumia lugha ya kisayansi. (Acquired Immune Defeciency Syndrome (AIDS) uk 4); Shit! uk 5; emergency cases uk 7; Oh! No! My God uk 14).

Pia matumizi ya Kiingereza ni kuwajengea uhalali wahusika wasomi wenye kuweza kuelezea jambo kwa kuchanganya lugha mbili au zaidi.

Kwa upande mwingine kuna maneno mengi sana yaliyotoholewa ilivyo na isivyo: (kuspeshalaizi uk 7; manesi uk 7; grupu uk 7; Korido-Dokta uk 7; jujuoloji uk 5; shenzi taipu uk 5; konfyusheni uk 19).

Matumizi ya Mbinu za Kisanaa

Mtunzi Ibrahim Ngoji amefauli sana katika kuiwekea tamthiliya hii mawanda ya kisanaa na kuifanya kuwa iliyojaa drama na kuweza kuigizwa barabara kwa uhakika hata bila ya kuwa na jukwaa wala ulazima wa pazia. Kwa maneno mengine, USHUHDA WA MIFUPA ni tamthiliya iliyofika kwa wakati mwafaka.

Tamthiliya hii imetumia mbinu ya kuielimisha jamii na kuipatia taswira sahihi kuhusu mustakabali wa maisha hasa kwa vijana.

Kwa kuwapambanisha wahusika wenye msimamo tofauti, kama vile Marekani dhidi ya Waafrika (masokwe), Mkyuba dhidi ya Marekani, Mrusi dhidi ya Marekani; ("Sisi Marekani tumefanya utafiti... Tumeridhika kabisa viini (Virus) visivyokuwa na dawa. Tunakijua changzo cha Virusi - HIV. Kutoka Masokwe. Masokwe yapo Afrika uk 4).

Kwa mbinu ya kujitetea na kukataa kuonelewa Mwafrika anakana dai hilo (Wewe Marekani msenge nini...? Sisi tuliingiliana na hao masokwe ndiyo tukaupata?

... Wamezoea hawa Marekani kila kitu kibaya ni cha Mwafrika. Maaluni hawa! hata huko kwenye mwezi watakakokwenda siku wakikuta mavi watasema sisi ndiyo tuliokunya huko. Mabaradhuli wakubwa!"

Mdahalo wenye mvuvumko na wa kusisimua uliyojaa drama huipatia tamthiliya uhai hata kumfanya mtu aendelee kusoma, kutazama na kusikiliza toka mwanzo hadi mwisho.

Mbinu nyingine aliyoifumua ni kuwa na sentensi fupi fupi kwa kila mhusika. Sentensi zilizojaa kejeli, dhihaka na kusababisha watu kupasuka vicheko, ("Viini hivi vilisambaa kutoka maabara moja huko Marekani" uk 5).

Ndipo mhusika anayetetea Marekani anajibu kwa ghadhabu, ("Shenzi taipu. Majungu matupu! uk 5).

Halafu mtu 4 mtetezi wa Mrusi anaingilia kati (utafiti wa Mrusi kiboko: Heko Bwana Vodka heko zako" uk 5).

naye mtetezi wa Afrika anafika juu, ("Msitutishe! Na sisi Waafrika tumetazamia. ... Ninyi hamjui jujuoloji... uk5).

Baada ya Mwafrika kutukanwa ‘Shenzi’ na Marekani anahamaki na kulipiza kisasi, ("Shenzi mwenyewe...! Nitakuroga, nikugeuze fisi, mahamri we! uk 5).

Mbinu nyingine aliyotumia mtunzi ni kuingiza sauti ya kilio (Vilio vinayidi).

(Mtambaji: Wakati wanabishana, watu wanaendelea kupukutika katika mji... (vilio) uk 5).

Mbinu nyingine inayofanya tamthiliya hii kuvutia ingawa ujumbe wenyewe ni tishio la vifo, ni matumizi ya lugha ya picha, ("Msinikodolee macho kama vyura! Waone macho! uk 5).

Anapofukuzwa Mtani hunatokea drama, ("Toka hapo afriti mkubwa. Sisi tunaumwa halafu wewe unatupigia makelele! Yala kichomi... Yalaa... Nani anisaidie nakufa mie jama ee," uk 19).

Matumizi ya Tamathali za Semi, Misemo, Methali n.k.

Kwa ufundi wa pekee mtunzi wa Tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA ametumia methali hapa na pale (Ama kweli kufa kufaana uk 18).

Takriri

Tamathli ambayo hutumia mbinu ya kurudiarudia maneno, sentensi au kauli imetawala tamthiliya mzima. (Tumia mipira, ni kinga bora! Tumia mipira, ni kinga bora! Tumia mipira ni kinga bora! uk 18).

Tanakali - Santi

Tamathali inayoiga sauti ya kitendo imejitokeza mara nyingi katika USHUHUDA WA MIFUPA. (Eh! uk 16; Sssh! uk 11; Mh! uk 11; Aaa! uk 9; Anhaa! uk 15).

Udamisi

Tamathali inayotilia chumvi jambo au vitu kuwa na uwezo imejitokeza hapa na pale. (... akina mama wao mikono yao hutetema, yangu mikavu inatulia na imara kuzidi chuma uk 9).

Tasifida

Tamathali hii hutumia mbinu ya kuficha makali ya jambo, tendo kwa kutumia maneno tofauti (Basi nikaona nipunge upepo kidogo. Unajua tena dereva lazi awe na spea taya uk 8).

Dhihaka

Ni aina ya kejeli, ni tamathali ambayo ina ubeuzi mkali, jahili unaopenya ukweli. Basi katika tamthiliya hii kejeli na dhihaka zimejitokeza toka mwanzo hadi mwisho.

(Wewe Marekani msenge nini? uk 4; Shenzi taipu, Shit! Nitakuroga nikugeuze fisi uk 5; Kila mtu ajichimbie kaburi lake. Kila mtu avae sanda yake uk 20).

Tashibiha

Hii ni tamathali inayolinganisha vitu, watu au jambo kwa kutumia viungo: kama, mithili, mfano wa n.k. (... Imekuwa ngumu kama mawe uk 10; Usinitolee ulimi kama kenge uk 10).

Sitiari

Tamathali hii hufanana na ile ya tashibiha ila haitumii viungo vya maneno. (... Makalikiti alibaki ufito mtupu uk 14).

MAZOEZI

1. Wahusika wa tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA wanawakilisha watu wa marika yote katika jamii, na hasa vijana. Jadili kauli hii kwa kuwahusisha wahusika wawili tofauti.

2. Ingawa dhamira kuu ya tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA inalenga katika kuutahadharisha umma kuhusu athari za UKIMWI, lakini pia limejitokeza suala la kisiasa na la ushirikina. Bainisha kauli hiyo kwa kutoa mifano halisi kutoka katika tamthiliya hii.

3. Nafasi ya Mtambaji katika USHUHUDA WA MIFUPA inaweza kulinganishwa na nini katika maisha ya kila siku ya binadamu?

4. Jadili kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kwa kuzingatia matumizi ya lugha na tamathali za usemi.

5. Maudhui ya USHUHUDA WA MIFUPA yana umuhimu wa pekee katika jamii ya Tanzania. Jadili ukweli wa tamko hili.

6. Tamthiliya USHUHUDA WA MIFUPA inaonyesha falsafa gani?

7. Jadili masuluhisho ya tamthiliya KWENYE UKINGO WA THIM na yale USHUHUDA WA MIFUPA:

8. Kwa kutumia MORANI; USHUHUDA WA MIFUPA; KWENYE UKINGO WA THIM na KIVULI KINAISHI eleza jinsi waandishi hao, kila mmoja peke yake, alivyofaulu kuzingatia maudhui yake kuwa kielelezo cha jamii ya Tanzania.

9. "Uibushaji migogoro/migongano katika tamthiliya ni nyenzo muhimu ambayo huleta drama na ufanikishaji kwa upeo mkubwa". Kwa kutumia vitabu viwili kati ya MORANI; KWENYE UKINGO WA THIM; KIVULI KINAISHI; na USHUHUDA WA MIFUPA chambua na kubainisha kauli hii.

10. Jadili nafasi ya mwanamke jinsi ilivyojitokeza kwa pande zote mbili, chanya na hasi, katika tamthiliya mbili kati ya USHUHUDA WA MIFUPA; MORANI; KWENYE UKINGO WA THIM; na KIVULI KINAISHI.

Copyright J.P. Mbonde 1997