IJUE AFYA YAKO

Namna ya kuzuia kidonda kisitoke damu

1. inua sehemu iliyoumia juu.

2. Chukua kitambaa safi au mkono wako mwenyewe kama hakuna kitambaa. Gandamiza penye jeraha.

Shikilia hivyo hivyo mpaka damu iache kutoka tena. Hii inaweza kukuchukua dakika 15 hata saa moja au zaidi.

3. Kama damu inaendelea kutoka na unadhani mgonjwa amepoteza damu nyingi, basi msaidie kama ifuatavyo:-

-Endelea kugandamiza.

- Inua sehemu iliyoumia.

- Funga mkono au mguu karibu ya jereha katikati ya mwili na jeraha, kaza vya kutosha mpaka damu isitoke.

- Funga kwa kutumia nguo au mkanda, ni mwiko kutumia kamba nyembamba, uzi au waya.

Tahadhari:-

- Ufunge mguu kwa kitambaa ikiwa kama damu inatoka kwa wingi na haizuiliki kwa kukibana kidonda kwa mkono.

- Legeza hilo fundo la kitambaa kwa muda kidogo kila baada ya nusu saa kuona kama kufunga bado kunahitajika na pia, kuifanya damu itembee.

Kuliacha fundo hilo kwa muda mrefu bila kulilegeza kunaweza kukauharibu mkono au mguu kiasi ambacho itabidi mkono huo au mguu huo ukatwe.

- Kamwe usitumie takataka, mafuta ya taa, lime (yaani ndimu, chokaa, ulimbo) na kahawa katika kuzuia damu isitoke.

- Ikiwa damu inatoka kwa wingi au kidonda ni kikubwa, inyanyue miguu iwe juu na kichwa kiwe chini kuzuia mshituko.

Jinsi ya kuzuia kutoka damu puani

1. Kaa kimya

2. Minya pua kwa muda wa dakika kama 10 au zaidi mpaka damu isitoke.

 

 

Kama hii haizuii...

Tumbukiza pande la pamba puani ukiachia sehemu kidogo ining’inie nje.

Kama ikiwezekana, lowanisha pande hilo la pamba penye hydrogen peroxide vaseline au lidocaine with epinephrine’(adrenalin).

Kisha minya pua tena kwa muda wa dakika 10 au zaidi.

 

 

 

 

Kama damu haitoki, acha pande hilo la pamba ndani ya pua kwa muda wa saa chache kisha iondoe kwa uangalifu sana. Kama pua yake inavuja mara kwa mara basi ipake vaseline mara mbili kutwa.

Matunda kama machungwa, nyanya na mengineyo husaidia kuipa nguvu mishipa ya damu na kuzuia kutoka damu kwa wingi.

Kwa watu wazee, damu inaweza kuwa inatokea sehemu ya nyuma ya pua na kuminya pua hakutasaidia.

Hivyo akae kimya, mpe gunzi aume na ainame mbele na asijaribu kumeza mpaka damu igande (kuuama gunzi kunasaidia) asimeze kitu na inaipa damu nafasi ya kuganda)

Kujikata(kato) kwaruzo na majeraha madogo

Usafi ni jambo la kwanza muhimu kuzuia uenezaji wa ugonjwa na kuwezesha jeraha kupona

Kutibu jereha

Osha kwanza mikono yako vizuri sana ukitumia sabuni na maji safi.

Kisha osha jeraha vizuri ukitumia sabuni na maji ya moto.

Unaposafisha jeraha hakikisha uchafu wote umeondoka. Hakikisha kuwa chini ya ngozi iliyojeruhiwa kumesafishwa pia.

Kama inawezekana mwagie maji ya moto penye jeraha kwa kutumia sindano.

Uchafu wowote utakaobakia utasababisha ugonjwa.

Usitie kinyesi chochote au tope kwenye jeraha.

Hii, inaweza kuleta ugonjwa mbaya sana kama vile pepopunda (tetenus)

Usitie spiriti au dawa nyingine yoyote moja kwa moja penye jeraha.

Hii inaweza kudhuru na kuchelewesha kupona. Tumia maji na sabuni.

Majeraha makubwa: namna ya kukifunga.

Jeraha la muda huu ambalo ni safi litapona haraka ikiwa pembe zake zitakutanishwa na kufanya jeraha liwe limefunikwa. Funga jeraha lililoingia ndani tu ikiwa masharti yafuatayo yamezingatiwa:

- Jeraha limetokea muda wa saa zisiozidi 12

- Jeraha ni safi na ni vigumu kumpata mganga kukifunga siku hiyo hiyo.

- Kabla ya kukifunga hakikisha umekisafisha vizuri sana ukitumia maji ya moto na sabuni. Hakikisha kuwa hakuna uchafu wowote ulioachwa ndani ya jeraha, bandeji au plasta.

Kushona kwa nyuzi maalumu

Tazama kama pembe za jeraha zinaweza kukutana bila ya kuvutwa. Kama zinaweza, basi hakuna haja ya kushona hilo jeraha.

Ili kushona:

- Chemsha sindano na uzi mnene (nailoni au silki ni zuri zaidi) kwa muda wa dakika 10.

- Osha jereha kwa maji ya moto na sabuni kama ilivyokishwa elezwa.

- Osha mikono yako vizuri sana kwa maji ya moto na sabuni

- Osha kidonda namna hii

- Shona kwanza katikati ya jeraha na lifunge kabisa. Shona sehemu nyingine ili jeraha lifunikwe kabisa na kisha uziache nyuzi hizo hapo hapo kwa muda wa siku 6 hadi 12.(usoni siku 6, mwilini siku 8, viganja au nyayoni, siku 12) kisha, ziondoe kwa kuzikata pembeni mwa mafundo na kuvuta mpaka nyuzi zitoke.

Ilani

Shona majeraha ambayo ni safi sana na hayana umri usiozidi saa 12.

Majeraha ambayo ni ya zamani, machafu au yenye kutoa usaha, ni lazima yaachwe wazi.

Jeraha la kuumwa na mtu, mbwa, nguruwe au mnyama yeyote, ni lazima liachwe wazi. Maana yakifungwa, yatatunga usaha.

Kama jeraha lililofungwa linaonesha dalili ya kutunga usaha, ondoa nyuzi haraka na liache wazi.

Bandeji:

Bandeji hutumika kusaidia kuweka jeraha katika hali ya usafi. Kwa sababu hii, bandeji au vipande vya nguo vinavyotumiwa kufungia majeraha, ni lazima viwe safi kila mara.

Vitambaa hivi ni lazima vifuliwe na kukaushwa kwa pasi au juani mradi pasiwe na vumbi.

Tumetekelezaje malengo ya Jubilei Kuu?

Na John Mbonde

KATIKA semina iliyofanyika kwenye Chuo cha Don Bosco mjini Moshi mapema mwezi Desemba 2000, Padre Paul Uria, wa Jimbo Katoliki la Moshi, alitoa changamoto kwa waamini Wakatoliki jimboni kujiuliza jinsi walivyotekeleza malengo ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000.

Alianza kwa kuwakumbusha wanasemina jinsi Kanisa zima duniani lilivyofanya maandalizi kwa kuzingatia barua ya kitume ya Papa Yohane Paul wa Pili, "Tertio Millenio Adveniente,"(ujio wa milenia ya tatu) ambayo ilitafsiriwa na Mhashamu Askofu Amedeus Msarikie wa Moshi na kuchapishwa Peramiho Printing Press.

Hali kadhalika, alidokeza ile milolongo ya dhamira kwa kila mwaka kabla ya kilele cha maadhimisho ya Jubilei Kuu yaliyotakiwa kuzingatiwa na waamini wa dunia nzima.

Vijitabu, majarida, magazeti na makala mbalimbali katika kipindi chote cha maandalizi vililenga katika kuhamasisha waamini duniani kote wajiandae kusherehekea Jubilei Kuu.

Je, Jimboni Moshi waamini walipania kufanya nini? Matokeo yake yamekuwaje?

Katika kutathimini suala hili, Padre Paul Uria, alianza kwa kuorodhesha mipango mingi, mbinu na mikakati ya utekelezaji wake.

"Awali ya yote," alidai Padre Uria na kuendelea, "Waamini walikuwa na uchu wa kuona ongezeko la uhai wa maisha ya Kikristo. Aidha, kuimarika kwa upendo na amani miongoni mwa jamii."

Lengo kuu la Jubilei Kuu ni kumtangaza Kristo kwa watu wote na wa mahali pote kwa njia ya kila mbatizwa kuwaza kuiishi Injili ipasavyo ili kujenga imani na matumaini yenye ukomavu.

Katika jimbo la Moshi, waamini wamedhihirisha mwamko mkubwa kwa wengi waliokengeuka kwa jambo moja au jingine, kuweza kumrudi Kristo. Vijana wengi waliokaa uchumba, wamefunga ndoa na waamini wengi wameshiriki katika makongamano, hija na ibada za Sakramenti ya Upatanisho.

Wengi wametoa zaka zao ikiwa ni pamoja na viporo vya miaka mingi.

Kumekuwa na ongezeko la miito mitakatifu ya upadre na utawa. n.k.

Kwa ujumla, hayo yote yaliamsha ari mpya ya uwajibikaji katika roho ya umisionari katika kila kigango, parokia na jimbo zima.

Kumekuwa na mfululizo wa ibada za kuabudu Ekaristi Takatifu, Hija ya Msalaba na ongezeko la watu kuhudhuria Misa Takatifu za kila siku hasa zile za Jumapili na za sikukuu huku wakiwa katika kutoa sadaka, hata kufanya makusanyo kuongezeka kwa siku.

Kubwa kuliko yote, ni kuimarika kwa mahudhurio katika jumuiya ndogondogo za Kikristo.

"Ni jambo la kujivunia kwamba Jimbo la Moshi lenye jumla ya parokia 46, lina jumuiya ndogondogo za Kikristo zilizo hai 3280. Kila jumuiya huwa ni huru kuchagua viongozi wake kadiri wao wenyewe wanavyofahamiana hivyo, huweza kuandaa mipango yao na kutatua matatizo yao wenyewe," alisisitiza Padre Uria.

Katika mantiki hiyo, majimbo mengi nchini Tanzania yangeweza kufanya tathimini yao jinsi yalivyotekeleza majukumu ya Jubilei Kuu na jinsi yanavyotumia uzoefu huo ili kudumisha utume wa Umissionari endelevu katika jumuiya, vigango, parokia, jimbo na hatimaye Taifa la Tanzania.

Tunahimiza kutumia moto huo katika kumpokea na kumtangaza Kristo kwa mataifa yote.

Jicho langu katika Mwaka 2000

Na Erasto Duwe, Songea

SHASH! Kumekucha, Machweo yameanza mawio. Tu tayari ndani ya mwaka 2001. Mwaka 2000 uliokuwa mwaka wa Jubilei Kuu duniani, Jubilei ya miaka 2000 tangu kuzaliwa kwake Yesu Kristo huko Bethlehemu; na ndio uliokuwa mwaka wa Sayansi na Teknolojia, umepita na umekwenda zake.Alamsiki 2000 karibu kwetu mwaka 2001.

Kabla ya kuingia mwaka 2000, anga lote lilikuwa limetanda hofu na harufu ya wasiwasi kutapakaa kila kona. Kisa kikiwa ni yale yaliyonenwa juu ya mwaka huu wa 2000.

Wapo walionena kuwa, Mwaka 2000, ndio mwaka wa kiyama. Kiyama chenyewe ndio mwisho wa dunia. Wengine walinena na kulonga kuwa, ifikapo mwaka 2000, kompyuta zote zitasimama na kufuta kumbukumbu zote yaani, (Y2K).

licha ya hayo yalinenwa mengine mengi pia.

Lakini, alhamndulilai; yote yana Mungu, mambo yakaenda shwari hali ya hofu na ikatoweka. Mwaka 2000 umepita salama na leo, ni mwaka wa 2001. Ni jambo la kumshukuru Mungu anayetuweka salama.

Katika mwaka 2000, yalitendeka mambo mengi makubwa na madogo. Tena yenye furaha na yale ya uchungu kidini, kijiografia, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kidini:

Mwaka 2000 kidini ulikuwa ni mwaka wa Jubilei Kuu duniani. Ni Jubilei ya miaka 2000 ya Ukristo wetu yaani imetimia miaka 2000 tangu Kristo alipozaliwa. Ulikuwa ni mwaka wa mataifa kurudi nyumbani kwa Baba na kupata rehema kamili.

Ulikuwa kweli ni Mwaka Mtakatifu kutokana na yale yaliyotendeka ndani yake. Mathalani, hija mbalimbali zilifanywa na waamini. Pia, safari ya Msalaba wa Jubilei ambao kwa kiasi kikubwa kisichotarajiwa, umeamsha imani kubwa kwa waamini na hata wengine kuponywa magonjwa yao kutokana na kuugusa.

Tuzidi kumshukuru Mungu na kumwomba ili neema tulizozipata katika Mwaka wa Jubilei(2000), zidumu pamoja nasi siku zote.

Tukio jingine la furaha, ni lile lililotokea Oktoba Mosi, 2000. Yaani kufuatia aliyekuwa Mwenyeheri Mama Yosefina Bakhita, kutangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo wa II. Mtakatifu Bakhita, ni mzaliwa wa kijiji cha Olgossa karibu na Darfur Sudan.

Vile vile, kutangazwa Wenyeheri, Papa Pio wa IX (tisa) na Papa Yohane XXIII (23).

Papa Pio wa tisa atakumbukwa kwa kuitisha Mtaguso Mkuu wa Kwanza wa Vatikano na Papa Yohane 23 (XXIII), ndiye aliyezindua Mtaguso wa Pili wa Vatikano na kutoa mchango mkubwa katika hali ya Kanisa la kisasa.

Aidha, Abate Kolumba Marmion OSB wa Ireland, alitangazwa Mwenyeheri.

Hatuna budi wote kuyafanya mambo hayo ya kiimani, yatupe zaidi moyo wa kujitoa muhanga kwa Mungu na hivi kuuwania utakatifu.

Kijiografia:

Mwezi Februari 2000, huko Msumbiji kulitokea kimbunga kikali na mafuriko yaliyosababisha hasara kubwa. Watu walipoteza maisha yao, wengine kukosa makazi na mashamba yao kuharibiwa vibaya.

Huko Ufilipino, nako tetemeko la ardhi lilitokea mwezi Julai na likasababisha watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine, wakakosa makazi na kubaki katika hali ya mahangaiko.

Mwezi Agosti wa mwaka 2000, kulikuwa na mafuriko makubwa yaliyotokea huko India na vile vile, mlipuko wa Volkano ulitokea huko Japan. Mambo hayo yote yameharibu maisha ya watu na kuwacha wengine katika hali ngumu.

Kiuchumi.

Hali ya uchumi katika mwaka 2000 imezidi kuwa ngumu siku hadi siku. Wenyenacho walizidi kuwa nacho na makabwela walizidi kudidimizwa na kulala hoi zaidi kwa uchovu na njaa.

Haukuwepo uwiano sawia baina ya bei za bidhaa na bei za mazao ya wakulima. Bei za pembejeo za kilimo zimezidi kuwa juu kiasi kwamba, wakulima wanauliza ikiwa hali ndiyo hiyo, wao watajikwamua vipi na lini?

Vile vile, kulikuwa na matukio kadhaa wa kadha ya ujambazi wa kutumia silaha. Matukio hayo yote yana athari kubwa katika uchumi wa nchi na raia kwa ujumla.

Kijamii:

Ajali nyingi za ndege zilitokea, mathalan huko Kongo-Kinshasa, ajali ya ndege iliyotokea huko Ufilipino ambayo ilisababisha watu 131 kupoteza maisha yao, ndivyo hivyo hivyo, huko India kutokana na ajali ya ndege watu 58 walipoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa.

Ajali za vyombo vya usafiri majini hazikuwa nyuma, huko India kutokana na ajali ya meli watu 500 walipoteza maisha yao. Vilevile, ajali ya boti iliyotokea mwezi Julai huko Bukoba ilisababisha watu 15 kupoteza maisha yao.

Huko Pakistani nako, bomu lililipuka ndani ya treni na kuua watu 9. Aidha, huko Nigeria, mlipuko wa bomba la mafuta ulitokea mara kadhaa kusababisha vifo vya mamia ya watu na wengine kujeruhiwa vibaya. pia Nyambizi ya Urusi iliua watu 119.

Ajali za barabarani nazo zilikuwa tu, kama wimbo katika vyombo vya habari kwa asilimia kubwa. Asili ya jambo hili lililoangamiza uhai wa wengi na kuwaacha wengine wakihangaika na vilema vya kudumu, ni uzembe wa madereva. Madereva punguzeni mwendo na muwe makini mnapoendesha, mtachinja watu mpaka lini?

Rushwa nayo, usiseme. Bado ni tatizo sugu linalozidi kupenyeza mizizi yake siku hadi siku. Watoaji na wapokea rushwa wanazidi kushamiri katika sekta zote kijamii. Rushwa ipo ofisini shuleni, hospitalini, na hata barabarani; imezagaa bila mwangalizi wala mtu wa kuikemea kwa sauti inayosikika na kueleweka.

Kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola ambao hauna tiba wala kinga, pia kumeteketeza watu wengi hususan huko Uganda. Ugonjwa huo umekuwa tishio kubwa kwa jamii.

Kisiasa:

Kwa upande wa nchi yetu ya Tanzania, Mwaka 2000, umekuwa mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Jambo la kushukuru Mungu, ni kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika na kuisha kwa usalama ingawa mikwaruzo ya hapa na pale isingekosekana kama vilivyo vikombe ndani ya kabati. Hugongana ingawa havina chuki wala uhasama.

Ni makusudi mazima kusema hivyo kwa kuwa, kulikuwa na ghasia za hapa na pale hususan huko Zanzibar kulikokuwa na mchezo mbaya wa kulipua mabomu. Jambo hilo kwa lenyewe, si jema na linatia wasiwasi hasa ukizingatia sera za "Jino kwa jino" na "ngangari na ngunguri" zenye lengo la kulipizana visasi. Hizi ni sera zinatishia amani ya jamii.

Jambo hilo, ni dalili wazi ya kuwa chanzo cha fujo nchini. Yafaa jambo hilo liangaliwe na vyombo vya dola kwa namna ya pekee ili amani tuliyoachiwa na Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa), iendelee kudumu siku zote na kubwa zaidi, tuishi kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Tuanze mwaka mpya wa 2001 kwa amani na utulivu, tena tudumishe upendo, shime kwenu nyote! Hatujachelewa kufanya mabadiliko, bado tunao muda uliosalia na unatosha kulifanya jambo lolote baya, likawa lenye manufaa kwa Kanisa na nchi nzima.

Kwa kuwa ni juma lilopita tu, tulikuwa tunasherehekea kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu wakati wa Krismas, basi tutembee na tuishi naye huku tukifuata nyayo zake.

Uchambuzi na uhakiki , fasihi ya Kiswahili

l Tamthiliya kwa kidato cha 5 na 6: Kivuli kinaishi

Ushuhuda wa mifupa

Tamthiliya hii, USHUHUDA WA MIFUPA, ilipata ushindi wa kwanza miongoni mwa miswada 160 iliyoshindanishwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mwaka 1989 baada ya jopo maalumu kuzichambua kwa kina chake.

Awali ya yote, tumpongeze mtunzi Ibrahim Ngozi, kwani kama inavyofahamika msanii ni kioo cha jamii. Mtunzi huyu amesaidia sana kuifanya jamii kujiona na kujikosoa kwa kuangalia sanaa hii ya maonesho, hususan wale wanaokisoma kitabu hiki au kufanya igizo wanaguswa vya kutosha.

Katika kuitikia wito wa Mpango wa Taifa, wa kudhibiti UKIMWI, mtunzi Ibrahim Ngozi, kwa kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, pamoja na wasanii wenzake wa fani mbalimbali kote nchini, alishiriki kutoa mchango wake kwa kuandika mchezo huu wa kuigiza.

Hatimaye, alijijengea uhalali wa kuwa mshindi wa kwanza katika fani ya tamthiliya katika kampeni maalumu ya kuuelimisha umma mintarafu chanzo, athari na jinsi ugonjwa unavyoenea.

Hii, ililenga kuubadili mwenendo wa maisha katika jamii ikiwa ni ndio njia ya kujikinga na UKIMWI kwani hauna tiba.

Mwandishi Ibrahim Ngozi, katika kuutumia ufundi wake katika sanaa za maonesho, anafafanua jinsi UKIMWI unavyolipuka na kusambaa na hata kusababisha vifo vya lukuki ya watu.

Anatanabaisha kuwa, baadhi ya sababu ni kile kitendo cha kutumia mabomba ya kudungia sindano bila ya kuyachemsha, kuongeza watu damu yenye viini vya UKIMWI kabla ya kuipima, utumiaji wa kuchangia vyombo vya kutogea masikio, pua, vyombo na vifaa vya kukalikiti.

Pia, vitendo vya usherati, umalaya na kukosekana uaminifu kwa watu wa ndoa wa kufanya mapenzi kiholela na watu wengine nje ya ndoa au kabla ya ndoa.

Msanii huyu pia anauasa umma kuacha dharau dhidi ya hatari ya maradhi hayo yanayotishia kufyeka uhai wa binadamu. Anawataka watu waache kuupuuza ukweli na kufanya UKIMWI kama jambo la mzaha kwa kuita ugonjwa huo majina "ACHA INIUE DAWA SINA! Acha Iniue Dogodogo siachi! Kidini-Feilia! n.k."

Msanii Ngozi, anawatahadharisha na kuwakanya wale wanaoleta tafsiri potofu kuhusu UKIMWI kwa kutia chumvi au kuendeleza uzushi wenye kuhofisha kama "Ukikanyaga mavi au matapishi ya mgonjwa wa UKIMWI, tayari umeshapata!"- ukimpa mkono; vinywaji; kumtunza mgonjwa wa UKIMWI, tayari umeambukizwa". uk 18"

Aidha, amewatoa wasiwasi kuwa siyo kila mwenye upele; nywele nyekundu; aliyedhoofu na kuwa mwembamba, basi eti ana UKIMWI!

Mwishoni, anawataka watu kuepukana na ulaghai na udanganyifu wa watu wenye uchu wa fedha wanaojidai kuwa wana dawa za kutibu UKIMWI. Wale wanaodanganya kuwa tiba ya UKIMWI, ni kuruka maji, MM II; Moro kuna mambo; Kemroni n.k.

Msanii anatoa suluhisho kwamba kila mtu anatakiwa kujitahidi kuzingatia masharti ya kinga dhidi ya UKIMWI.

Anasema mzizi mkuu na sugu, ni kuuacha uasherati.

Katika hitimisho hilo anamtaka kila jamaa, mzazi, mwalimu, kiongozi na jamii nzima, kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti mienendo na tabia zetu vinginevyo, ipo hatari ya kasi ya kuangamiza jamii ya taifa letu.

Kwa kutumia mchezo huu, amefaulu kujenga mazingira au mandhari halisi ambayo walengwa wa rika zote wanaweza kujipambanua jinsi wanavyohusika katika harakati dhidi ya UKIMWI.

Ujumbe wake unaugusa umma haraka bila ya kuacha nafasi ya mtu kubabaisha.

Kwa mantiki hiyo, aliyekuwa Naibu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Ndugu Salim Ahmed Salim (kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika - OAU), katika uzinduzi wa kampeni iliyoandaliwa na BASATA dhidi ya UKIMWI tarehe 2 Juni, 1989 alitamka,

"Kampeni hii ya wasanii dhidi ya UKIMWI isiwe ya mwaka mmoja tu, bali iwe ya kudumu kwani dawa haijapatikana na jamii yetu ya Tanzania na dunia nzima ikingali inatafuta dawa. Aidha, bado watu wengi hasa vijijini hawajaufahamu ugonjwa huu vema..."

Tishio la UKIMWI kuangamiza wanadamu duniani, linaongezeka kwa kasi sana. Juhudi za kutafuta dawa za kutibu UKIMWI, bado zinaendelea na hakuna matumaini ya uhakika kufaulu mapema kama ilivyotarajiwa mwanzoni ulipogunduliwa ugonjwa huu.