IJUE AFYA YAKO

Magonjwa mbalimbali ya ngozi (3)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini.

Katika toleo lililopita, tuliishia katika kipengele kinachozungumzia juu ya namna ya kujikinga na mba.

Katika toleo hili, tutajadili zaidi magonjwa mbalimbali ya ngozi ikwa ni pamoja na madoa meupe usoni na katika mwili, Mbaraga, sugu na chunusi.

Madoa meupe usoni na katika mwili

Madoadoa madogo ya kijivu yenye ukingo maalumu wa kujipindapinda katika shingo, kifua na mgongo huenda ikawa ni mba. Hata hivyo, mba ni ugonjwa usiowasha.

Tiba:

- Paka mafuta yenye salfa kila siku mpaka upone.

- Sodium thiosulfate husaidia zaidi. Yeyusha kijiko cha mezani kimoja cha sodium thiosulfate katika bilauri ya maji. Ipake kwenye ngozi na isugue kwa pamba iliyolowekwa ndani ya vinegar.

- Ili kuzuia isitokee tena, ni bora kurudia matibabu haya kila baada ya wiki mbili.

*Kuna aina nyingine ya madoa madogo meupe ambayo mara nyingi hutokea katika mashavu ya watoto wanaocheza juani. Kingo zake, hazionekani vizuri kama zile za mba. Haya, hayaambukizi wala kudhuru.

Hutoweka yenyewe bila tiba, si dalili ya ukosefu wa damu kama vile watu wengi wanavyofikiri.

Utumiaji wa toniki au vitamini hausaidii chochote. Madoa ambayo yapo mashavuni tu, hayahitaji tiba.

Mbaraga (Vitiligo):

Sehemu fulani za ngozi za watu za baadhi ya watu hubabuka na kupoteza rangi yao ya kawaida na kisha, pengine kuacha madoa meupe.

Mara nyingi huonekana katika mikono, miguu, uso na sehemu za juu za mwili.

Upotevu huu wa rangi ya ngozi uitwao MBARAGA, si ugonjwa na unaweza kufananishwa na mvi za watu wa makamo.

Hakuna dawa inayosaidia au inayohitajika ili kutibu hali hiyo ila, sehemu hizo ni lazima zikingwe zisiunguzwe na jua au zipakwe mafuta ya zinc oxide.

Sababu nyingine za kuwa na ngozi yenye madoa meupe:

Kuna magonjwa fulani yanayoweza kusababisha kuwa na madoa meupe kama mbaraga. Inaelezwa kuwa, huko Amerika ya Kati, kuna ugonjwa mmoja wa kuambukiza unaoitwa PINTA, ambao huanza kama chunusi ya kibluu au nyekundu na baadaye, kuacha kovu jeupe.

Hutibiwa kama vile ugonjwa wa kaswende ila, pinta si ugonjwa wa zinaa.

Doa lolote jeupe ambalo halina maumivu linapodungwa sindano, huenda likawa ni ukoma.

Aina nyingine za mba husababisha madoa meupe.

Alama za mimba

Hizi ni alama wanazopata baadhi ya akina mama wanapobeba mimba. Hupata alama hizi katika ngozi za uso, matiti na chini katikati ya tumbo. Huwa ni alama nyeusi. Alama hizi, nyingi hutoweka baada ya mimba.

Hutokea pia kwa akina mama wanaoutumia vidonge vya uzazi wa majira. Alama hizi ni za kawaida na si dalili ya uchovu au ugonjwa. Hakuna haja ya kutumia dawa.

PELLAGRA NA MATATIZO MENGINE YA NGOZI YANAYOSABABISHWA NA UTAPIAMLO.

Pellagra, ni aina ya utapiamlo inayosababishwa na kubadilika kwa ngozi na wakati mwingine, kuharisha na kuuguliwa akili.

Ni ugonjwa wa kawaida katika nchi ambazo chakula kikuu ni mahindi na aina nyingine za wanga na watu hawapati vyakula vya kutosha vya kujenga na kuhifadhi mwili kama vile maharagwe, nyama, mayai na mboga za majani.

Dalili za ngozi kukiwa na utapiamlo:

Mtu mzima mwenye pellagra, ngozi yake huwa kavu na yenye kupasuka na kutoa magamba hasa katika sehemu zile zinazochomwa na jua kama

Watoto walio na utapiamlo, ngozi zao za miguu na hata mara nyingine ngozi za mikono, zinaweza kuwa na madoadoa meusi ambayo huchubuka na kuacha madonda.

Dalili hizi zinapotokea, ni lazima dalili nyingine za utapiamlo ziwepo kama kuvimba tumbo, vidonda katika pembe za midomo, ulimi unakuwa mwekundu na una vidonda, udhaifu na kutotaka kula chakula sambamba na kukonda.

Tiba:

- Ugonjwa huu huponywa kwa kula chakula bora, kula kila siku maharage, karanga, kuku, samaki, mayai, nyama na jibini. Ikiwezekana, tumia unga wa ngano badala ya unga wa mahindi.

-Kama umezidiwa sana utaweza kusaidiwa kwa kutumia vitamini lakini chakula bora ni muhimu zaidi.

Hakikisha kuwa, vitamini unayotumia ina vitamini B ya kutosha hasa "niacin" chachu ya kutengenezea pombe. Hii ina vitamini B kwa wingi.

Uvimbe wa madoadoa meusi katika miguu ya mtoto ni sababu ya utapiamlo kwa mtoto ambaye alikuwa anakula zaidi chakula cha mahindi bila aina ya protini na vitamini kwa wingi.

Baada ya wiki moja ya kula maharagwe, mayai, nyama na mahindi, uvimbe huweza kunyong’onyea na madoa kuanza kutoweka.

Kuugua ngozi ya miguu, ni dalili ya pellagra inayotokana na kutokula vizuri.

Kumbuka kuwa madoa meupe katika miguu husababishwa na ugonjwa uitwao "Pinta".

Chunjua:

Chunjua nyingi hasa zile zinazowapamba watoto huendelea kwa muda wa miaka 3 hadi 5 na kisha hutoweka zenyewe.

Sugu zilizoko katika nyayo za miguu mara nyingi ni chunjua za nyayo au zinaweza kuwa kovu la sugu.

Tiba:

-Dawa za nyumbani mara nyingine zinaponyesha chunjua lakini, usitumie esidi iliyo na nguvu au mimea iliyo na sumu kwa sababu inaweza kuunguza au kusababisha jeraha ambalo ni hatari kuliko chunjua.

-Kama chunjua za nyayo zinauma, nenda kamwone mganga aziondoe.

Sugu (Corns):

Sugu ni sehemu ngumu na nene ya ngozi. Husababishwa na viatu vinavyobana au vidole vinavyobanana. Sugu zinaweza kuuma sana.

Tiba:

-Vaa viatu visivyobana

-Ili ziume, fanya hivi;

- Loweka miguu ndani ya maji ya moto kwa muda wa dakika 15

-Tumia tupa au msasa na usugue mpaka iwe nyembamba

Chunusi:

Chunusi ni vivimbe vidogo vyenye ncha nyeupe yenye usaha au ncha nyeusi ya uchafu. Mara nyingine zinaweza kuuma na kutanuka.

Mara nyingi vijana hupata chunusi katika nyuso, vifua na migongo hasa kama ngozi zao zina mafuta mengi.

Tiba

Osha uso mara mbili kwa siku ukitumia sabuni na maji ya moto.

- Mwanga wa jua unasaidia kuondoa chunusi.

Hivyo, achia sehemu hiyo ya mwili ipigwe na jua.

-Kula vizuri, kunywa maji mengi na kulala usingizi wa kutosha, pia husaidia kupambana na tatizo la chunusi.

-Kabla ya kwenda kulala, paka usoni spiriti iliyochanganywa na salfa (sehemu 10 za spiriti kwa sehemu moja ya salfa).

Ikiwa manundu na usaha vinatokea baada ya kutumia maagizo hayo hapo juu, basi meza tetracycline kidonge 1 mara 4 kutwa kwa muda wa siku 3 na baadaye, vidonge 2 kila siku.

Inaweza kukulazimu kutumia kidonge kimoja au viwili kila siku kwa muda wa mwezi au miezi mingi.

Kansa ya ngozi:

Kansa ya ngozi hutokea sana kwa watu weupe ambao makazi yao ni ya juani.

Kwa kawaida hutokea katika sehemu za mwili zinapopigwa sana na jua hasa.

Inawezekana kuchukua umbile la namna mbalimbali.

Kwa kawaida, huanza kama kiduara kidogo chenye rangi ya kumetameta ikiwa na kashimo juu katikati. Kinakuwa taratibu.

Kansa nyingi za ngozi, hazina hatari ikiwa zinatibiwa mapema kwa kupasua na kuondoa donda lote pamoja na ngozi inayoizunguka.

Kama una donda ndugu ambalo unadhani ni kansa ya ngozi, mwone mganga upesi.

Ili kukinga Kansa ya ngozi, wale wote walio weupe ni lazima wahifadhi ngozi zisipigwe na jua na wavae kofia mara kwa mara.

Wale ambao wamekwishapata ugonjwa huu na makazi yao yako juani, ni afadhali wanunue mafuta maalumu ya kukinga ngozi zao.

Mafuta ya Zinc oxide ni rahisi na hukinga vizuri.

Uchambuzi na uhakiki, Fasihi ya kiswahili

KIMBUNGA (Tungo za visiwani -3)

Mtunzi wa mashairi haya Bwana Haji Gora Haji alizaliwa katika kijiji cha Kokoni, Tumbatu Zanzibar mwaka 1933. Bwana Haji Gora Haji hakubahatika kwenda shule, bali alijifundisha mwenyewe hadi akawa mtunzi mahiri wa nyimbo na mashairi. Kazi alizopata kuzifanya ni uvuvi, ubaharia na ukuli. Hatimaye, akaamua kuishi Chumbuni wilaya ya mjini Zanzibar na kufanya kazi ya uchukuzi.

Mara nyingi hao wachache ni tabaka la viongozi vitimbakwira.

Mshairi anatoa taswira kuhusu maisha ya jamii. Falsafa yake ni kwamba kuna uonevu, dhuluma, na wasiwasi kwa wanyonge.

Msanii anawatetea wanyonge ili kudai haki zao. Maisha ni mapambano. Msanii anawataka wanyonge kuendelea katika harakati kwani mapambano ni sehemu ya maisha ya binadamu.

Kwa maneno mengine matatizo yanayowakabili binadamu hayana budi kutafutiwa ufumbuzi na wao wenyewe. Haitoshi kulia tu, kulaumu peke yake, bali jamii itafute ufumbuzi wa kudumu dhidi ya matatizo yawayo; kama vile lile shairi Kimbunga linavyopiga mbiu la mgambo kwa jamii.

Ubeti wa sita:

"Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika, Tukakatana miguu, kwa mapanga na mashoka,

Manufaa kwa wakuu, wadogo yetu mashaka,

Wezeni kutukumbuka, mjuwe nasi wenzenu."

Falsafa ya msanii ni kuielimisha jamii kwamba licha ya adha na shinikizo walipatalo kutoka kwa viongozi wao, "hapana marefu yasiyo na ncha." Msanii anatanabaisha kwamba hao wakuu wana uwezo wa kuwakumbuka wanyonge ambao ni wenzao.

Katika maisha kuna mfululizo wa mambo mengi. Katika maisha kuna vipindi vya furaha na vipindi vya majonzi.

Shairi jingine ambalo msanii anatoa falsafa ya maisha ni lile Na. 15 "Usafi" (uk. 13); Na. 21 "Hili mnatutakiya" (uk. 18); Na. 22 "Wazazi" (uk. 19); Na. 23 "Si vema" (uk. 20); Na 31 "Kitu Gani?" (uk. 26); Na. 33 "Ndiye Avumaye" Na. 37 "Dawa ya Deni Kulipa" (uk. 32) n.k.

Kwa jumla kitabu Kimbunga, kina dhamira nyingi zaidi kuliko hizo chache tulizozijadili. Mathalani, kuna dhamira ya ujenzi wa jamii mpya. Yaani wasanii wanapoelezea umuhimu wa kwenda na wakati, kwa kuyakubali mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande mwingine, ile falsafa ya mabadiliko makubwa katika jamii hususan mvutano baina ya ukale na usasa (vijana dhidi ya wazee), maisha ya mijini dhidi ya vijijini n.k.

Fani

Mashairi yaliyomo katika Kimbunga ni ya aina zote (mapokeo na ya kisasa - masivina). Baadhi yake yanazingatia kanuni za urari wa vina na mizani, na mengine hayafungamani na vipengele hivyo vya fani.

(i) Matumizi ya Lugha

Malenga wa diwani Kimbunga ametumia lugha ya kishairi vizuri hata kuwashinda wale ambao walikwenda shule. Katika diwani hii kuna nahau, misemo na tamathali za semi.

Kutokana na matumizi ya vipengele hivi vizuri, kumefanya taswira mbalimbali zijengeke.

a) Tamathali za Semi

Sitiari

Sitiari ni tamathali inayolinganisha vitu viwili au zaidi vyenye sifa tofauti, ila haitumii maneno ya viungo. Katika Kimbunga shairi Na. 35 "Wasia" (uk. 31) ubeti wa 4 lina mfano:

"Dunia ni jiti kavu, mara hukuangukia."

Tashibiha

Tashibiha ni tamathali inayolinganisha vitu viwili au zaidi vyenye sifa tofauti kwa kutumia maneno: mithili ya, mfano wa, kama n.k.

Shairi Na. 15 "Usafi" uk. 13 ubeti wa 3 na 4; kile kibwagizo "Tusiwe kama Mapunda, tukenenda kwa michango."

Tashihisi

Tamathali inayoipa vitu uwezo/sifa za binadamu.

"Rushwa kajenga kambi, na kuondoka hataki,

Afanya kila vitimbi, mkaidi hashindiki,

Tumzushiye wimbi, isiwe kutuhiliki,

Tumchimbie handaki, rushwa tukamzikeni."

Tabaini

Hii ni tamathali ya usemi inayotumia maneno au mawazo yanayokingana katika sentensi ili kuleta msisitizo.

CARITAS inavyolilia maendeleo ya Wanawake Dar, Pwani

Na Getrude Madembwe

CARITAS ni shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, linaloshughulika na utoaji wa misaada katika jamii inayokumbwa na majanga mbalimbali yakiwamo ukame, mafuriko, njaa , magonjwa na hata vita kwa kutoa huduma muhimu kama chakula, dawa na mavazi.

Mbali na kusaidia watu walio katika majanga, shirika hili pia limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa akinamama wasio katika sekta maalumu, wanainua hali zao za maisha kwa kupewa mikopo yenye masharti nafuu ili kuendesha miradi mbalimbali.

"Mwaka 1995/96 utafiti wa matatizo na mahitaji ya maendeleo ya jamii ulifanywa katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam(mkoa wa Dar-Es-salaam na Pwani)na idara ya maendeleo yaani Caritas-DSM.

Sehemu kubwa ya jamii ilikuwa katika dimbwi la umaskini mkali. Ilidhihirisha pia kuwa kina mama ndio walikuwa nyuma kimaendeleo kwa hali na mali bila ya huduma muhimu za kuwawezesha kupambana na umaskini," alisema Simon Yohana, ambaye ni Afisa wa Miradi wa Caritas-DSM.

Alisema hayo katika taarifa fupi ya maendeleo ya mpango wa akiba na mikopo kwa maendeleo ya akina mama senta ya Kibaha na Mlandizi, aliyoitoa kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Wakati wa kufunga semina kwa akinamama wanaotarajiwa kukopeshwa na Caritas-DSM, ili kuwafundisha namna ya kutumia mikopo, Februari 15, 2001, taarifa iliendelea kusema,

"Mpango wetu wa maendeleo wa mwaka 1998-2000, uliamua kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya akinama maskini na wenye kipato kidogo hasa kwa walio katika sekta isiyo rasmi ili kupunguza kiwango cha umaskini katika familia.

Mikakati iliyowekwa na Caritas-DSM, ilikuwa pamoja na kuwapatia kina mama elimu ya maendeleo, elimu ya haki za kinamama, na elimu ya kusoma na kuandika.

Mingine ni mbinu za kuendesha miradi na kuongeza kipato cha familia na kuwawezesha kupata mitaji midogo kwa njia ya mikopo na kujiwekea akiba ili kukuza mitaji yao.

Mpango wa Akiba na Mikopo Midogo ya muda mfupi kwa ajili ya kuanzisha, kukuza na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali, ulianza mwaka 1998.

Mikopo ya mwanzo kabisa ilitolewa Mlandizi Februari 1999.

Ilifuatiwa na Kibaha mwaka 2000.

Mikopo inayotolewa na Caritas huanzia shilingi 10,000 hadi 175,000 kwa riba ya asilimia 15 kwa miezi sita. Na asilimia 25 kwa mwaka.

Katika taarifa fupi kwa Mhashamu Kilaini, Mwenyekiti wa Senta ya urafiki Mlandizi, Devota Mbatia, alisema kuwa mpango huo ulianza mwaka 1999 ukiwa na wanachama 58.

"Kiasi cha mkopo tulichoanza nacho ni shilingi milioni sita. Viwango vya mikopo tulivyoanzia kwa kukopeshana ni shilingi 30,000 kwa kima cha chini na shilingi 200,000 kwa kima cha juu."

Alisema kwa sasa kiasi kilicho katika mzunguko ni shilingi 42,535,000. Hii inadhihirisha kuwa kweli kupitia mpango huo wa Caritas-DSM, akinamama hao wananufaika na mashirika na taasisi nyingine na hazina budi kuiga mfano huo.

Mwenyekiti huyo alisema ni asilimia mbili tu, ya wanachama ambao hawajaweza kufanya vizuri katika marejesho ya mikopo hiyo. Anadokeza kuwa, mikopo inaweza kurejeshwa mapema na mwanachama akakopeshwa tena.

Shughuli zinazofanywa na akinamama hao, ni za aina mbalimbali zikiwamo maduka ya rejareja, maduka ya nafaka ya jumla na rejareja, maduka ya vifaa vya ujenzi, maduka ya kuuzia nyama, kununua na kuuza nafaka toka mikoani, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na ufugaji wa kuku wa nyama na mayai kuuza nguo za mitumba na za viwandani.

Nyingine ni magenge, grosari, kuuza mbao na mkaa na akinama wa senta hiyo katika taarifa yao, walibainisha dhahiri kuwa mikopo na mpango huo, unawanufaisha sana.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa akinama waliokuwa maskini, baada ya kujishirikisha katika mpango huo, siku hizi wanaonekana kama ndio waangalizi wakubwa kwa familia zao baada ya kupatiwa mikopo na shirika hilo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Naye Mratibu wa Caritas jimboni humo, Bw. Christian Shembili, alisema "Tuliamua kuanza kutoa elimu kwa akina mama hao ili wajue jinsi ya kuongea na mteja na pia, wajue mahali pa kutafuta masoko na kuwapa ushauri wa biashara gani wafanye ili wanufaike na kurudisha mikopo hiyo kwa wakati".

Caritas jimboni wanasema hawatoi mikopo hiyo wakiwalenga Wakristo au Wakatoliki pekee, bali akinamama wote bila kujali dini wala siasa.

Mikopo wanayotoa huanzia shilingi 10,000- 175,000 hadi 1,500,000 kwa riba ya asilimia 15 kwa kipindi cha miezi 6 na asilimia 25 kwa mwaka.

Hadi sasa Caritas-DSM, wameshatoa jumla ya mikopo 321 katika kipindi cha kuanzia Februari, 1999 hadi Februari, 2001 ambapo jumla ya shilingi 64,460,000 zimekwishatolewa ikiwa ni mikopo iliyotolewa na mashirika ya Misereor la Ujerumani, na Holy Union Sister’s la Roma.

Bw. Yohana alisema shilingi 42,535,000 zilitolewa katika tarafa ya Mlandizi kwa kipindi cha Februari, 1999 , ambapo shilingi 38,180,000 zilitolewa na shirika la Misereor na shilingi 4,355,000 zilitolewa na shirika la Holy Union Sisters.

Katika tarafa ya Kibaha, jumla ya shilingi 20,425,000, zilitolewa na shirika la Misereor lilisaidia shilingi 18,075,000, Holy Union Sister’s, shilingi 2,350,000.

Alisema kuwa kutokana na utoaji wa mikopo hiyo, shirika hilo jimboni limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani asilimia 98 ya wanaokopeshwa, hurudisha mikopo hiyo bila ya usumbufu wowote.

Hata hivyo, caritas Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wamefanikiwa katika malengo yao kwa kuwa licha ya kutarajia kutoa mikopo 300, ifikapo Februari mwaka huu, wamevunja rekodi na kutoa mikopo 321.

Pia wamefanikiwa kuwabadili akinamama wengi kiuchumi, na kifikra kutokana na semina na mikutano mbalimbali wanayopata na hii, imeongeza heshima kwa kina mama hao toka kwa ndugu, jamaa, na marafiki.

Caritas Jimboni dar-Es-Salaam, endelezeni moyo huo wa kuinua hali za maisha ya watanzania hasa akinamama na sisi tunatoa wito kwa taasisi na majimbo mengine kuiga mfano huo.

Hata walengwa wa mipango hiyo, wazingatie kutumia mikopo na kuirejesha kama ilivyokusudiwa ili wengine wanufaike nayo na hata kama inawezekana, wachukue mingine.