IJUE AFYA YAKO

Maelezo kwa akina mama na Wakunga (4)

Ili kuielimisha jamii juu ya magonjwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, bado tunaendelea kuwaletea makala mbalimbali kwa msaada wa kitabu cha MAHALI PASIPO NA DAKTARI ambacho kinalenga kusaidia kutoa mafunzo ya afya vijijini.

- Mkunga asisugue, asigandamize tumbo la mzazi wala asimruhusu asukume katika hatua hii.

- Ikiwa mama ni muoga au ana maumivu makali sana, mueleze apumue taratibu kupunguza maumivu na atatulia vizuri.

Hatua ya pili ya uchungu wa kujifungua

- ambapo ni wakati mtoto anapozaliwa:

Wakati mwingine huanza wakati chupa ya maji inapovunjika. Kwa kawaida, ni hatua rahisi na fupi kuliko ya mwanzo. Uchungu unaporudi, inambidi mama asukume chini kwa nguvu zake zote.

Uchungu utowekapo ataonekana amechoka na amelegea kama mtu mwenye usingizi. Hii ni jambo la kawaida tu.

Ili kusukuma chini, inambidi asukume kwa nguvu akitumia misuli ya tumbo kama vile anapokwenda haja kubwa.

Ikiwa mtoto anateremka taratibu baada ya chupa ya maji kuvunjika, basi yambidi mama akunje magoti akiwa amechutama, ameegemea nyuma au amelala chali.

Wakati mlango wa nyumba ya uzazi umefunguka na kichwa cha mtoto kinatokeza, inambidi mkunga awe tayari na vifaa vyake vyote vya kumpokelea. Wakati kama huu, mama asijaribu kusukuma ili kichwa cha mtoto kitoke taratibu. Hii inasaidia mama asipasuke msamba.

Hii ni njia moja kubwa ya kuambukiza magonjwa baada ya kujifungua. Kichwa kitokapo, inambidi mkunga kukihifadhi na si kukivuta.

Kwa kawaida mtoto anazaliwa kichwa kikiwa kimetangulia, Sasa sukuma kwa nguvu, pumua upesi upesi. Hii inasaidia kuzuia kupasuka msamba, kichwa kinatokeza na uso ukiwa unatazama chini. Kisha, kiwiliwili cha mtoto kinajigeuza upande mmoja ili mabega yatoke.

Ikiwa mabega yanakwama baada ya kichwa kutoka:

Mkunga anaweza kukikamata kichwa cha mtoto na kukiteremsha chini taratibu ili bega litokeze na kisha, anakiinua juu kidogo ili bega lingine litoke.

Nguvu zote sharti zitoke kwa mama. Mkunga asijaribu hata kidogo kuvuta kichwa cha mtoto kwa sababu akikivuta mtoto ataumia sana.

Hatua ya tatu ya uchungu wa kujifungua -

inaanza baada ya mtoto kuzaliwa mpaka kondo la nyuma litakapotoka. Kwa kawaida, kondo linatoka lenyewe dakika 5 hadi saa moja baada ya mtoto kuzaliwa. Wakati unaposubiri hatua hii kutendeka mtazame, msaidie na mlee mtoto.

Utunzaji wa mtoto mara anapozaliwa

Mara baada ya mtoto kuzaliwa:

Kielekeze kichwa chake chini ili ute umtoke kinywani. Kiache namna hii mpaka atakapoanza kupumua.

Mweke mtoto chini ya usawa wa mama yake mpaka kitovu kimefungwa (kwa njia ya namna hii, kunamfanya mtoto apate damu zaidi na kukamilisha afya yake)

Ikiwa mtoto hajapumua, msugue mgongoni kwa taulo au kitambaa.

Kama bado hapumui, muondoe ute wote puani na kinywani kwa kutumia "suction catheter" au kitambaa kilichozungushiwa katika kidole chako.

Ikiwa mtoto hajaweza kupumua dakika moja baada ya kuzaliwa, ni bora kuanzisha pumzi ya mdomo kwa mdomo mara moja.

Mviringishe ndani ya nguo safi. Ni jambo la muhimu kuwa, mtoto asipate ubaridi hasa kama ni njiti; yaani amezaliwa kabla ya siku zake.

Jinsi ya kukata uzi wa kitovu:

Mtoto anapozaliwa, uzi wa kitovu una mapigo ya damu na ni wenye rangi ya kibluu, Subiri baada ya muda uzi huo unakuwa mwembamba na mweupe. Mapigo ya damu inatoweka sasa ufunge sehemu mbili ukitumia mshipi wa nguo safi ambao umepigwa pasi au kuokwa kwa muda mfupi uliopita. Kata katikati ya sehemu hizo mbili ulizofunga namna hii

Muhimu:

Kata uzi wa kitovu kwa kutumia wembe safi ambao haujatumika.

Kabla ya kufungua wembe huo, osha mikono yako vizuri. Iwapo huna wembe mpya, tumia mkasi unaotoka kuchemshwa.

Kila mara kata uzi huo karibu na mwili wa mtoto. Achia sentimeta 2 za kuning’inia.

Hii, inasaidia kuepuka kupata ugonjwa wa pepopunda.

Utunzaji wa kitovu

Jambo kubwa la muhimu ambalo linamsaidia kuepusha kitovu kipya kisiambukizwe na kukiweka katika hali ya ukavu. Ili kusaidia kikauke ni kukiachia hewa ipenyeze. Kama mazingira ya nyumbani ni mazuri na hakuna nzi, usikifunike kitovu, kiachie hewa ikiingie.

Kama kuna vumbi na nzi, basi kifunike vizuri. ni vizuri kutumia ngozi safi ambayo umeikata kwa mkasi uliochemshwa na kukifunika namna hii.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza -Tanzania Bara (4)

KATIKA gazeti hili matoleo yaliyopita, tuliandika habari juu ya kitabu kilichoandikwa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) kiitwacho, HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA-TANZANIA BARA, ambacho kimesambazwa katika magereza mbalimbali ili kuwafanya wanajamii na wafungwa wenyewe, kuzifahamu haki zao na kujua namna ya kujirudi. Katika toleo hili, tunaendelea kukichapisha kitabu hicho kama kilivyo baada ya kuanza na dibaji na kisha utangulizi.

Lengo la kuwatenganisha ni kuepuka mchanganyiko ambao huweza kusababisha maambukizo yakiwamo ya tabia na hivyo kupoteza thamani nzima ya mipango ya mafunzo. Hata hivyo tatizo la msongamano magerezani huathiri utaratibu huu wa kuwatenganisha.

(ii) Haki ya kupatiwa chakula, malazi na mahitaji mengine

Kulingana na sheria, mfungwa anapaswa kupewa chakula kama ilivyoidhinishwa na sheria ya magereza. Pamoja na sheria kuweka viwango maalumu vya vyakula kwa aina zote za wafungwa, mganga wa gereza anao uwezo wa kuelekeza mfungwa apewe aina tofauti ya chakula kulingana na afya ya mfungwa anayehusika.

Wafungwa wenye miiko ya kutokula vyakula fulani, nao wana haki ya kupewa vile vyakula wanavyohitaji kulingana na mila na desturi zao k.m Vegeterians(wala mboga).

Kila mfungwa anapaswa kupatiwa mahitaji yote ya msingi kama vile vifaa vya malazi, nafasi ya kutosha kwa malazi, isiyo na majimaji, yenye kuingiza hewa ya kutosha na inayozuia baridi wakati wa usiku.

Pia kuwe na magodoro na mablanketi kulingana na mapendekezo ya afisa wa afya/ mganga wa gereza.

Vifaa vya kutunzia usafi navyo ni muhimu mfano usafi wa maji, ndoo za uchafu, vifaa vya kufanyia usafi, dawa zake sabuni, mifagio n.k.

Hata hivyo utendaji wakati mwingine huenda tofauti na sheria inavyotaka kutokana na msongamano mkubwa wa wafungwa katika magereza.

(iii) Haki ya kufanya kazi inavyostahili -

wafungwa wale waliokwisha kuhukumiwa wanatakiwa kufanya kazi zenye kuwapa mafunzo.

Kwa wanawake sheria imeweka bayana kuwa watumike katika kazi zinazofaa kulingana na maumbile yao. Wafungwa wazee vilema na wenye afya mbaya hupewa kazi nyepesi kwa kuzingatia maelekezo ya waganga.

Mahabusu hawawajibiki kufanya kazi magerezani isipokuwa usafi maeneo wanayotumia.

Kwa ujumla katika suala la kazi afisa afya wa gereza ana jukumu la pekee.

Katika mazingira fulani huweza kuagiza mfungwa fulani kutofanya kazi kabisa au kupewa kazi nyepesi.

Pia inahimizwa wafungwa kupewa kazi zenye manufaa kwa lengo la kuwapatia mafunzo ili wakitoka kifungoni, wafanye kazi zitakazowasaidia kumudu maisha yao kwa kujitegemea.

(iv) Uhuru wa Mawasiliano na kuwatembelea Wafungwa.

Wafungwa wanaweza kuwasiliana na watu walio nje kwa njia ya barua ama kupokea wageni wanaowatembelea.

Kwa wafungwa ambao ni wageni toka nchi nyingine wanafanya mawasiliano yao kwa msaada wa wawakilishi wa kidiplomasia wa nchi zao waliomo Tanzania. Pia kwa kusaidiwa na Taasisi za kimataifa ambazo zinahusiana nao mfano wafungwa wakimbizi na walio kizuizini huhusishwa katika mawasiliano na taasisi zinazowajibika nao.

Kwa upande wa wageni wanaoruhusiwa kutembelea wafungwa ni ndugu, familia, jamaa na marafiki, washauri wa kisheria na viongozi wa dini pamoja na wengine kwa ruhusa maalumu toka mamlaka ya magereza.

Inashauriwa wananchi kujenga tabia ya kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki waliomo gerezani kwani zipo faida kadhaa katika kufanya hivyo.

Mfano kuwatumainisha kuwa huru baadaye, kuwafanya wajisikie kuwa nao bado ni sehemu ya jamii na kwa upande mwingine wananchi hupata fursa ya kuelewa hali halisi ya magereza yetu.

Wengine wanaoruhusiwa kuwatembelea wafungwa ni wakaguzi wa magereza (Visiting Justices). Hawa huyatembelea magereza mara kwa mara kuangalia hali za wafungwa na maofisa wa magereza.

Baadhi ya wakaguzi wa magereza huteuliwa na wakuu wa mikoa husika baada ya kushauriana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wengine ni mahakimu wa ngazi zote, wakuu wa mikoa, majaji wa mahakama ya Rufaa na wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mawaziri.

Wabunge pia ni wakaguzi wa magereza katika magereza ambayo yamo ndani ya majimbo yao ya uchaguzi na wakuu wa majimbo yao ya uchaguzi na wakuu wa wilaya hali kadhalika. Hawa ni wawakilishi wa wananchi na taasisi wanazozisimamia hivyo wanapaswa kutembelea magereza ili kufahamu hali halisi ya magereza kwa jumla.

Lengo la wakaguzi wa magereza kutembelea magereza ni kutoa maoni yao katika utatuzi wa matatizo yanayoyakabili magereza yetu na kuona kama wafungwa wanatendewa haki.

Wakaguzi wa magereza wanaweza kutembelea magereza kwa pamoja ama mmoja mmoja. Baada ya ziara yao wanawajibika kuandika maoni au na mapendekezo yao katika daftari ambalo kila gereza linatakiwa kuwa nalo.

Ni jukumu la Mkuu wa Gereza kuwasilisha ,maoni au mapendekezo hayo kwa Kamishna Mkuu wa magereza ili yafanyiwe kazi.

(v) Haki ya kuandika barua, kusoma magazeti na kusikiliza taarifa mbalimbali.

Kwa sababu za usalama barua zote zinatoka na kuingia gerezani hukaguliwa na Afisa Magereza, kama ikionekana barua ina lugha chafu, inaelekea kusababisha vurugu au kama inazungumzia masuala ya uhalifu na mbinu zake ina malalamiko dhidi ya mahakama au na polisi, barua hizo zitarudishwa kwa wahusika na kuombwa wazirekebishe. Barua zote kutoka gerezani husafirishwa kwa gharama ya serikali.

Kiutaratibu wafungwa wanaruhusiwa kuandika barua mara mbili kwa mwezi lakini pia wanaruhusiwa kuandika barua wanapoingia gerezani kwa mara ya kwanza na wanapohamishwa toka gereza moja kwenda jingine.

Hata hivyo Afisa Magereza huruhusu mawasiliano hayo katika matukio muhimu mfano ugonjwa au kifo cha ndugu wa wafungwa kufanya mipango ya ajira au kutafuta msaada wa kuweza kutolewa gerezani.

K.m kuwaomba ndugu zake wamlipie faini n.k na pia wakati mwingine wowote mkuu wa gereza atakapoona inafaa anaweza kumruhu mfungwa kuandika barua.

Mbali na njia hizo pale inapowezekana wafungwa hupata mawasiliano na mazingira ya nje kwa njia ya kusikiliza redio, kusoma magazeti yaliyoruhusiwa na hata kwa kuangalia televisheni.

Kuponya ndoa halali Batili kwa njia ya kawaida ~(MSK,k1156-1160)

NI ipi ndoa halali na ndoa batili?

ILI kukidhi haja za wasomaji, gazeti hili linafanya juhudi za kuwatafuta wataalamu wa mambo ya ndoa ili uwepo muendelezo wa moja kwa moja wa makala zetu mbalimbali za kiroho ikiwa ni pamoja na zihususuzo uchumba na ndoa kama zinavyoelekezwa na Kanisa.

Kwa sasa, bado tunaendelea kuwaletea makala mahususi za ndoa kwa msaada wa jarida la Jimbo Katoliki la Moshi kama ilivyoandikwa na Wakili Hakimu, Padre Augustine Mringi.

Utangulizi

NDOA HALALI (Licit Marriage); ni ile ndoa ambayo imeshuhudiwa kwa mujibu wa sheria. Neno sheria hapa linamaanisha desturi, kawaida, kanuni au utaratibu wa jamii au jumuiya fulani wa kuishi na kuendesha mambo yao.

Ndoa yoyote inayoshuhudiwa na kufungwa kwa kufuata desturi, kawaida, kanuni au utaratibu wa aina hiyo mintarafu ndoa huitwa NDOA HALALI.

Kwa hiyo, mtu anaposema au anapodai ndoa yake ni halali, anataka tu kusema kwamba ndoa yake hiyo ilishuhudiwa na kufungwa kulingana na taratibu za kisheria kuhusu ndoa.

NDOA BATILI (Invalid Marriage): ni ile ndoa ambayo KWELI imeshuhudiwa kwa mujibu wa sheria lakini, KIKWELI, HAIKO wala HAIPO kwa sababu, Mungu mwanzilishi wa ndoa zote (Mwa 1:27-28), hakuishuhudia ndoa kama hiyo ijapokuwa machoni pa wanadamu na sheria, ilionekana imeshuhudiwa na kufungwa (Marko 10:9). Ndoa yoyote inayoshuhudiwa na kuunganishwa na Mungu huitwa NDOA KWELI (Valid Marriage).

Kwa hiyo, kutokana na ukweli huu, ndoa inaweza kuwa HALALI na KWELI (Licit and Valid Marriage) au HALALI lakini SI KWELI (Licit but Invalid) au, ikawa SI HALALI lakini KWELI (Illicit but Valid) au SI HALALI WALA SI KWELI (Illicit and Invalid).

Ndoa kweli hutokea wafungandoa wenyewe wanapopeana na kupokea ukubalindoa (MSK,k, 1057). Hata hivyo lakini, endapo mmojawapo wa wafungandoa ni Mkatoliki, ukubalindoa ni lazima utolewe kwa mujibu wa utaratibu kanuni(MSK,k 1108) haukuzingatiwa vilivyo, basi ndoa husika ikishuhudiwa na kufungwa itakuwa ndoa batili.

Endapo ukabalindoa utakuwa batili na bado wahusika wakaendelea kuwa na mawasilianondoa (convictum conjungalem) (MSK, k 1151), basi kwa kawaida sheria hutumia mbinu au mizungu ya kufanya ukubalindoa husika kuwa wa kweli na wenye nguvu. Hatua kama hii huitwa kitaaluma,"Kuponya Ndoa Halali Batili".

Kuponya ndoa halali batili ni kitendo cha kisheria ambacho kwacho, ukubalindoa wa awali ambao ni batili hufanywa kuwa kweli kuponywa (convalidate) ndoa halali batili daima kunaashiria kwamba ukubalindoa wa wanandoa husika ijapokuwa hauna nguvu, unaendelea kuweko.

NDOA HALALI BATILI, huweza kuponywa kwa namna kadhaa ijapokuwa kuna njia kuu mbili. Huweza kuponywa kwa njia ya kawaida ambayo kwayo ukubalindoa hurudiwa faraghani au hadharani kwa mujibu wa utaratibu kanuni au, huweza kuponywa "kutoka shinani" katika hali ambayo wahusika hawalazimiki kurudia ukubalindoa wala kutumia utaratibu kanuni pale panapopasa.

Njia ya kawaida ya kuponya ndoa halali batili ni kurudia ukabalindoa kwa kutumia utaratibu kanuni. Hata hivyo, yafaa ieleweke wazi bila utata na hisia huria kwamba daima, ndoa inayoweza kuponywa ni ile tu; iliyo halali batili ambayo ukubalindoa wake, unatambuliwa kikanisa au kiserikali na siyo hali ambayo wahusika wameamua kwa ridhaa yao wenyewe kuishi "pamoja na kujamiiana" bila kufuata utaratibu wa jamii au jumuiya mintarafu ndoa.

Ndoa halali batii inaweza kuponywa mwanandoa au wanandoa wote wawili wanaporudia upya ukubalindoa wao ama faraghani au kwa kuzingatia utaratibu kanuni.

Katika kuponya ndoa halali batili kwa njia ya kawaida kama ilivyoelezwa awali, mwanandoa au wanandoa wahusika hutakiwa kurudia upya ukabalindoa.

Hatua hii ikisha kutelekezwa, agano ndoa huzuka na mapasa ya ndoa huzalika.

Kwa kweli, uponyaji wa ndoa halali batili husababishwa na wanandoa wenyewe au na mwanandoa mhusika mradi tu, ukabalindoa wa mwanandoa mwenza uwe unaendelea kwa sababu kinachoifanya ndoa kuwa ndoa, ni ukubalindoa wa wafungandoa wenyewe unaooneshwa na kutolewa kwa mujibu wa sheria na watu ambao wana uwezo wa kufanya hivyo na hawana kizuizi chochote (MSK, k 1057).

Kuna ushahidi majadiliano kwamba Kanisa lilianza kuponya ndoa halali batili karibu kuanzia Karne Sita baada ya kuzaliwa Kristo. Mikutano fulani ya mwanzo katika Kanisa ilijaribu kuponya ndoa za walioongokea Imani Ukristo, ndoa ambazo zilikuwa batili kwa sababu hii au ile lakini, zilikuwa zimefungwa kwa nia njema.

Mkutano wa Orleansi III (538), ulitamka kwamba ndoa kama hizo zilipaswa kuchukuliwa kuwa kweli na zenye nguvu kwa sababu, zilikuwa zimefungwa kwa nia njema. Kuanzia karne 10 hadi 13, mapapa mara kwa mara walikuwa wakiruhusisha vizuizi batilindoa vilivyokuweko ukubalindoa ulipotolewa kwa mara ya kwanza ili kuponya ndoa husika.

Hata hivyo, hapakuwepo mfumo unaoeleweka na ulio wa wazi mpaka Mtaguso wa Trento ulipotoa mwongozo hapo karne ya 16.

Kuponya ndoa halali batili kwa njia ya kawaida huwezekana tu, kama ukubalindoa uliotolewa hapo mwanzo ulikuwa batili kutokana na mojawapo ya sababu tatu zifuatazo; kama palikuwapo kizuizi batili ndoa ambacho hakikuruhusishwa kwa mujibu wa sheria, kama ukubalindoa uliotolewa ulikuwa na kasoro msingi, na kama utaratibu kanuni haukutumika bila uruhusisho.

Makala haya yatajadili kuponya ndoa halali batili kwa njia ya kawaida kwa kuzingatiaa mtiririko huu uliotajwa hapa

Itaendelea

Dini Muhimu Kuliko Zote ni Ipi?

Na Padre Joseph G. Healey, M.M.

SIKU moja viongozi wa dini zote duniani walikutana kujadiliana na kuamua swali hili: "Dini muhimu kuliko zote ni ipi?" Kila kiongozi alitaja dini yake na hawa wakuu walianza kubishana. Mwishowe walisema, "Sisi tumeshindwa kuamua. Sasa tufanyeje?

Kiongozi mmoja alisema, "Mimi napendekeza hivi; Tungechagua mtu mwenye busara kuliko wote.

Halafu yeye ataamua kuhusu jambo hili." Viongozi walisikia kwamba yuko nabii mmoja aishiye katika mlima mrefu wa Afrika Mashariki (nchi za Kenya, Tanzania na Uganda) aliyekuwa na ujuzi mwingi na mang’amuzi juu ya dini na maisha yote.

Kwa hiyo, walikwenda kwake kumwuliza swali hilohilo; "Dini muhimu kuliko zote ni ipi?" Huyu Mzee Nabii hakujibu lolote. Mara aliingia pangoni mwake kusali na kufunga kwa siku tatu. Hawa viongozi walimsubiri nje.

Halafu alienda kwa umati wa viongozi wa dini zote na kusema, "Kwa sasa sitaki kushauri swali lenu. Lakini, naomba kila kiongozi arudi kwake kuzungumza na washauri wake.

Halafu, baada ya wiki moja, njooni hapa tena mbele yangu na ninyi viongozi mtatangaza neno moja kueleza msingi au kiini cha dini zenu."

"Halafu nitalinganisha majibu haya na kutokana na maneno mliyotaja, nitaamua dini gani ni muhimu kuliko zote."

Mara viongozi hawa duniani kote wakarudi makwao kujadiliana na washauri wao ili kuamua kiini cha dini yao.

Kisha walipanda tena katika mlima mrefu wa Afrika Mashariki. Kulikuwa na viongozi wa dini za jadi za Kiafrika, Kibudha, Kichina, Kihindi, Kiislamu, Kikristo, Kisikhi, Kiyahudi, na nyingine mbalimbali. Mbele ya Mzee Nabii walitangaza maneno ambayo yanaeleza dini zao.

Wakati walipomaliza, Mzee Nabii alisema, "Vizuri. Ninyi mumejibu vema.

Dini zenu zina maana na ni muhimu. Mumetangaza maneno ya maana kubwa sana. Tumesikia kiini cha dini za ulimwengu huu kwa maneno haya yafuatayo; Amani, Furaha, Haki, Huduma, Huruma, Imani na Jumuiya.

Mengine ni Kujinyima, Kujitoa, Kutokuwepo kitu, Mababu, Mizimu, Msamaha, Sala na Sifu.

Aksema kuwa mengine ni Tafakari, Ufufuko, Uhai, Uhusiano, Ukimya, Umoja, Upendo na Usawa.

Mzee Nabii aliendelea: "Kati yenu viongozi mbalimbali wa dini wamesema UPENDO ni kiini cha dini zao. Mumejibu vizuri zaidi. Kufuatana na majibu yenu, dini muhimu kuliko zote ni Ukristo. Hii, ni kwa sababu kiini cha dini ya Kikristo siyo upendo tu, ni UPENDO WENYE HURUMA. Upendo msamehevu ni bora zaidi."

Mzee Nabii akaendelea kusema: "Yesu Kristo, mwanzilishi wa Ukristo, alifanya jambo la ajabu msalabani. Wayahudi walimkamata, walimsulibisha, lakini kabla ya kifo chake alisema, "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya." (Luka 23:34).

Mfano huu ni upendo wa pekee.

Pia Yesu alisema: "Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi" (Yohane 13:34). Alifundisha umuhimu wa upendo, huruma na msamaha. Katika sala ya Baba Yetu, Wakristo wanasali, "Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea."

Mwishowe, Mzee Nabii juu ya mlima mrefu, akawaambia viongozi hao waliokusanyika pamoja, "Sasa mlijua ya kwamba, dini muhimu ni Ukristo. Nendeni mfanyeni matendo ya upendo wenye huruma au upendo msamehevu."

Yajue yaliyojitokeza wakati wa siku ya Pasaka (2)

JUMAPILI hii ya Aprili 15, ni Siku ambayo Wakristo kote nchini wanaungana na wenzao popote walipo duniani, kusherehekea kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Sikukuu hii kwa kawaida, huja baada ya Mfungo wa Siku 40 ambazo Yesu alikuwa nyikani. Katika kusherehekea sikukuu hii, Mwandishi Wetu anatuelezea historia ya Pasaka ikiwa imesheheni vikorombwezo mbalimbali vikiwamo kupeana mayai, sungura kutaga mayai na hata mke kumwagia mume maji akiwa usingizini. Endelea na makala haya yaliyoanza katika toleo lililopita...

Pia, waamini wengi walitumia kitoweo cha mnyama huyo siku hiyo.

Barani Ulaya, masanamu madogo madogo ya kondoo yalitengenezwa kutokana na siagi, samli, ngano na sukari maalumu kwa ajili ya Siku ya Pasaka.

Katika Biblia Takatifu, Yesu hufananishwa na kondoo aliyetolewa kafara na kuchinjwa ili damu yake iweze kuosha dhambi za wanadamu.

Kipepeo pia ni alama ya pasaka. Iliaminika kuwa kama vile kipepeo atokavyo katika kiwavi akiwa mpya vivyo hivyo Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu akiwa mpya mwenye kujaa utukufu.

Pia kuna maji ambayo hujuliakana kama maji ya pasaka ambayo hubarikiwa siku ya mkesha wa Pasaka. Watu hushauriwa kuwa na maji hayo nyumbani kwao kwa ajili ya matumizi ya kuwabarikia watu, nyumba na kadhalika.

Familia zingine husafisha majiko yao siku ya Ijumaa kuu na kuepukana na moto mpaka wanapoleta mkaa uliobarikiwa katika mkesha wa pasaka. Pia katika maeneo mbalimbali duniani watu wana mikate maalumu kwa ajili ya Pasaka. Nchini Urusi mkate wa pasaka hujulikana kama ‘Paska’, nchini Ujerumani kama ‘Osterstollen’ nchini Poland ‘baba wielancona’ mara nyingi mikate hii pamoja na nyama na mayai hubarikiwa siku ya jumamosi kuu.

Nchini Italia mikate hiyo hubarikiwa siku ya mkesha wa Pasaka (Jumamosi usiku) na kutolewa kama zawadi siku ya Jumapili kwa ndugu jamaa na marafiki.

Wakristo wa zamani walisherehekea wiki nzima ya pasaka kama wiki ya furaha na vicheko. Walichekeshana kufanyiana mizaha, kula nyama ya kondoo kucheza, kuimba na kufurahia kushindwa kwa shetani mauti na dhambi.

Siku ya jumanne ya pasaka wanawake waliwaamsha wanaume kwa mtindo huo huo.

Jua linapokuchwa siku ya jumamosi kuu jioni wakristo hukusanyika gizani na kuwasha moto wa Pasaka kutokana na moto huo pia huwashwa mshumaa wa kristu ambaye ndiye mwanga wa ulimwengu.

Katika mwanga huo wa mshumaa ambao ni ishara ya mwanga wa Yesu miongoni mwa watu wake, wakristo walikuwa wakikaa na kusimuliana habari mbalimbali kutoka katika maandiko matakatifu ambazo huwakumbusha mambo mengi mazuri aliyowafanyia Mungu, ikiwemo suala la kumtuma Yesu kuwakomboa.

Katika usiku huo huo mtakatifu, wanaopenda kumpokea Yesu hubatizwa.

Baada ya hapo watu hula meza moja, washiriki kinywaji na mkate na kumtukuza Mungu. Kula mkate na kunywa divai huchukuliwa kama kula mwili wa Yesu na kunywa damu yake.

Katika historia ya binadamu yai limekuwa likipewa heshima fulani kulingana na mahali. Katika baadhi ya maeneo yai lilionekana kama alama ya fumbo (siri). pengine lilitumika katika masuala ya uganga na ushirikina,dawa , chakula n.k

Yai ni kielelezo cha sherehe za Pasaka duniani kote na limekuwa likipakwa rangi, likirembwa, likipambwa na kutiwa madoido ya kila aina katika sherehe hiyo.

Kabla yai haliajanza kuhusishwa na Pasaka ya Kikristo lilikuwa likutumika katika sherehe mbalimbali za kimila katika maeneo ya Roma, Ufaransa, China, misri na Uajemi.

Kwa hiyo tangu zamani mayai yalipambwa kuheshimiwa na watu walipeana kama zawadi siku ya Pasaka.

Yai liliwakilisha dhana ya kuzaliwa upya kwa dunia. Kipindi cha kipupwe kilipoisha dunia ilionekana kuzaliwa upya kama vile yai linavyohidhi uhai wa kiumbe aliyeko ndani yake. Yai lilionekana kama kitu chenye nguvu za ajabu na za kipekee.

Lilizikwa chini ya misingi ya nyumba kama kinga ya maovu.

Maji ya Pasaka yaliyobarikiwa yaliongezwa manukato na kutumika kubarikia vyakula,wanyama wa kufugwa, bustani, nyumba na kadhalika. Siku ya Jumatatu ya pasaka wanaume waliwaamsha wake zao kwa kuwamwagia maji ya pasaka huku wakiwanong’oneza ‘kwamwe usinyauke’.

Wanawake wa Kiroma wenye mimba walilitumia yai kwenda kwa mganga ili waambiwe watazaa watoto wa jinsia gani.

Mabibi harusi wa Kifaransa walipaswa kuliruka yai kabla ya kuingia kwenye familia zao mpya.

Baada ya kuja ukristo yai likabadilika matumizi yake badala ya kumaanisha kuhusishwa kwa dunia likaanza kumaanisha kufufuka kwa mwanadamu yaani Yesu.

Wakristo wakawa wanalifananisha na kaburi alimozikwa na baadaye kufufuka Yesu.

Pia simulizi za kale juu ya maisha ya Yesu zinasema kuwa Mariamu mama yake Yesu aliwapa mayai askari waliokuwa wakimlindaa Yesu msalabani ili kuwataka wapunguze ukatili kwa mwanawe baada ya hapo Mariamu alilia kwa uchungu na machozi yake yakayadondokea mayai na hivyo yakaonekana kama yametiwa madoido ya kupendeza.

Pia inasemekana mwanamke mwingine Mariamu Magdaleni rafikiye Mariamu mama yake Yesu alipokwenda kaburini kuupaka mafuta mwili wa Yesu alikuwa na kapu la mayai kwa ajili ya chakula. Alipofika kaburini akakuta kuwa mayai yale meupe yamewekwa madoido ya rangi mbalimbali kimiujiza.

Kupamba na kuremba mayai kwa ajili ya pasaka ilikuwa ni desturi nchini Uingereza katika karne ya 13. hata hivyo Peter Carl Faberge wa Russia ndiye aliyesifika zaidi kwa shughuli hiyo katika karne ya 19 ambapo mwaka 1883 mfalme wa Russia Alexander alimpelekea oda maalumu ya kumtengenezea mayai ya pasaka mkewe Empress Marie.

Itaendelea

Lijue Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing (5)

KATIKA toleo lililopita, tulimuona Padre Amrhein amekwenda Roma ili kumaliza matatizo kadhaa yaliyohusu safari ya wamisionari kwenda nchi ya misioni. Moja ya matatizo hayo ilikuwa kupata eneo la kazi. Baada ya kupata eneo la kufanyia kazi, yeye mwenyewe alipata cheo cha kuwa prifekti wa kitume. Endelea

Anatangaza shirika lake

Padre Amrhein baada ya kupata kila kitu alichokihitaji toka Roma na toka serikali ya Ujerumani, alikuwa tayari kuwatuma wamisionari kuja Tanganyika.

Ingawa safari haikuwa wazi, mwanzoni mwa mwaka 1887 lakini matayarisho yalikuwa yakifanyika pole pole.

Aprili 9, 1887 gazeti la "Muncherner Allgemeine Zeitung" lilitoa taarifa kuwa shirika changa la watawa wa Mt. Benediktini, lingetuma Afrika si tu watawa wa kiume(monks), lakini pia masista ambao watawafundisha watu na kufanya kazi za hospitali.

Padre Amrhein aliona ingefaa kutangaza na kueneza mashirika yote mawili ya kiume na masista kwa pamoja na wakati mmoja katika magazeti kama "Germania", "Augsburger Postzeitung" "Die Katholischen Missionen".

Mapato ya matangazo hayo yalikuwa makubwa. Wasichana wengi waliuliza kwa njia ya barua juu ya shirika la masista.

Ilimpasa Sista Katharina kutafuta wasaidizi waliomsaidia kujibu barua zilizotaka maelelzo zaidi juu ya shirika hilo.

Anaomba msaada

Padre Amrhein alipoona kuwa watu wanachuchumia kujua zaidi juu ya shirika lake, aliomba msaada toka Wakristo Wakatoliki wa Ujerumani. Kwa nafasi hii, alitumia mara ya kwanza, jina jipya la shirika lake, "St. Benedict Mission Society" badala ya jina la awali la "Missionary Society of Reichenbach" ambalo ndilo lililotambuliwa na serikali ya Ujerumani wakati ule.

Alieleza kuwa ili kazi ya kuwaongoza watu katika nchi ya misioni ikamilike, walihitajika watawa wa kiume na kike.

Padre Amrhein alieleza kuwa shirika la masista lilikuwa limeanzishwa na kukubaliwa na serikali na Askofu wa Augsburg, shirika hilo litashughulikia elimu ya wasichana(education of girls) na kuwatunza wagonjwa(nursing).

Padre Amrhein alianzisha uabudu (adoratton) mbele ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa watawa wote katika Kanisa la Mt. Ottilia.

Sala hiyo ilianza Septemba 25, 1887. Yeye aliamini kuwa sala zitawapa nguvu wale watakaokwenda kufanya kazi katika nchi za misioni kama vile sala ya Musa ilivyowasaidia Waisraeli kuwashinda maadui zao (Taz. Kuk. 17:11-13). Wanachaguliwa kwenda misioni

Kama ilivyokuwa kawaida ya Padre Amrhein kabla ya tukio kubwa la kidini, alitanguliza sala ya Novena kwa Roho Mtakatifu kwa nafasi ya kuwachagua wamisionari kwenda Afrika.

Sala ya Novena ilikwisha Agosti 15, 1887. Siku hiyo majina ya watawa wanaume wa kwenda misioni yalitangazwa. Hapakuwa na uamuzi juu ya majina ya masista. Siku chache baadaye, Askofu Pankratius Von Dinkel alitembelea St. Ottilia akasikia habari za wamisionari waliokuwa wakijiandaa kwenda Afrika.

Askofu huyu alifurahi kusikia kuwa waliokuwa pia masista.

Kadiri siku za kuondoka zilivyokaribia, wamisionari hao walikuwa wakijiandaa kwa safari yao. Kwa kuwa hawakujua nchi waliyotarajia kwenda, walijitahidi kuchukua chochote walichoweza kuchukua kwa ajili yao wenyewe kwa ajili ya Liturugia na kwa ajili ya kazi nyingine ya misioni.

Mahitaji hayo yote yawaligharimu sana. Walipata msaada toka chama kimoja kilichoitwa "St. Louis Mission Society" Bw. Von Gravenrenth naye pia alichangia kwa vikubwa.

Ndipo ulipofika wakati wa kuwatangaza masista wa kwenda Afrika. Mpaka kipindi hicho haikujulikana kwa uhakika ni sista gani atakwenda Afrika.

Padre Amrhein alikusudia kutangaza majina hayo Oktoba 18, siku ya Sikukuu ya Mtakatifu Luka. Wakati wa misa takatifu, masista wafuatao walitangazwa; Sista Benedikta, Sivering, Sista Raphaela Kamphaela Kamphaus, Sista Lioba Allwanger na Sista Martha Wansing.

Masista wote walishangilia kwa furaha. Masista wengine waliwatakiwa heri waliochaguliwa.

Wanakwenda Roma

Novemba 11, 1887, masista wanne na mabruda tisa wakiongozwa na Padre Bonifas Fleschutz, waliondoka St. Ottilia Ujerumani kuelekea Roma. Padre Amrhein alikuwa ametangulia huko ili kushughulikia tatizo la kuweka nadhiri kwa watawa hao.

Yote yalipokuwa tayari, watawa wa kiume waliweka nadhiri zao Novemba 20, katika kanisa la Maria (German Comp Santo) na siku iliyofuata, sikukuu ya kutolewa Hekaluni Bikira Maria, masista waliweka nadhiri zao katika kanisa lile lile.

Itaendelea…